CHIMBUKO LA TAMTHILIYA NA HISTORIA FUPI YA TAMTHILIYA YA KISWAHILI
CHIMBUKO LA TAMTHILIYA NA HISTORIA FUPI YA TAMTHILIYA YA KISWAHILI
Kabla
ya mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki kuingiliwa na athari za kigeni
zilizotoka ng'ambo, fasihi ya Kiswahili, kama fasihi nyinginezo za kiafrika,
ilikuwa ni ya kusimuliwa tu (pasi na kuandikwa) na ilikuwa na tanzu kama vile
ngano, sanaa za maonyesho, vitendawili, methali na kadhalika. Utanzu wa
tamthiliya haukuwa na taswira kama iliyokuwanayo sasa, bali palikuwa na maigizo
ambayo yalitolewa mbele ya hadhira kwa minajili ya kuongoa na kufundisha
maadili au hata kutoa sifa kwa vitendo mwafaka vya wanajamii husika. Baada ya
majilio ya wageni (Waarabu na Wakoloni) maonyesho haya yalianza kubadilika kwa
kuingizwa katika maandishi na kuiga mitindo ya kimagharibi ili kuchukua mkondo
wa tamthilia kwa jumla.
Kihistoria,
tamthiliya ilianza kwa kutongoa maudhui ya kidini ambayo aghalabu yalikuwa ni
uteuzi wa visa fulani kutoka katika Bibilia Takatifu ili kutoa funzo fulani.
Pindi mabadiliko yalipoendelea kutokea katika maisha ya mwanadamu, hali hii
ilibadilika hadi kuingia katika tamthiliya zilizozingatia maudhui mengine kama
vile vichekesho na tanzia. Peck na Coyle (1984:75), wanashadidia maoni haya kwa
kusema kuwa katika drama ya Kigiriki, wahusika walikabiliana na matatizo
yaliyohusu uhusiano kati ya binadamu na miungu au Mungu. Katika karne ya kumi
na sita (16) hata hivyo msisitizo ulitoka katika dini na kuingiza masuala ya
kijamii, hivyo tamthiliya zikaanza kuzingatia maadili ya kijamii na kisiasa.
Katika Kiswahili,
tamthiliya ya kwanza kabisa kutungwa na mwafrikanakuchapishwani ile ya Henry
Kuria (1957) kwa kichwa cha Nakupenda
Lakini, ambayo ilitungwa katika enzi ya ukoloni, tamthiiya hii iliigizwa
kwa mara ya kwanza mwaka 1954 huko Kenya. Maudhui yake sawa na tungo nyingine
nyingi za wakati huo, yaliegemea zaidi upande wa kufurahisha. Huu ni mchezo wa
kuigiza unaotongoa maisha ya kijamii, lakini maudhui yake si mazito na
hayazingatii hali ya jamii kujisaka na kujitafiti.
Henry Kuria,
Kimani Nyoike, Gerishon Ngugi na B.M Karutu ni miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo
wa Graham Hyslop waliokuwa wakisoma katika shule ya Alliance High School.
Hyslop ni mwingereza aliyekuwa katika utumishi wa serikali ya kikoloni nchini
Kenya. Hyslop alianzisha kikundi cha maigizo kwa ajili ya askari waliopigana
katika vita ya pili ya dunia, miaka ya 1950 alianza kutunga michezo ambayo
iliigizwa na kikundi chake. Michezo yake ya mwanzo katika lugha ya Kiswahili ni
Afadhali Mchawi (1957), na Mgeni Karibu (1957). Inasemekana kuwa
Mwingereza huyu (Graham Hyslop) ndiye mtu wa kwanza kuleta tamthiliya kwa lugha
ya Kiswahili yenye kufuata kanuni zote za Ki-Arstotle. Mbali na Henry
Kuria, wanafunzi wengine wa Hyslop walioandika tamthiliya kwa Kiswahili ni
Kimani Nyoike aliyeandika tamthiliya ya Maisha
ni Nini mwaka 1955, B.M Karutu Atakiwa
Polisi mwaka 1957 na Gerishoni Ngugi Nimelogwa
Nisiwe na Mpenzi mwaka 1961.
Mulokozi (1996),
anadai kuwa kabla ya Graham Hyslop kuchapisha tamthiliya zake tayari kulikuwa
na tathiliya za Kiswahili zilizoandikwa kwanza kabla ya kuigizwa jukwaani.
Katika kutetea hoja yake Mulokozi anamtaja C. Frank na tamthiliya yake ya Imekwisha iliyochapishwa mwaka 1951,
vilevile anadai kuwa tamthiliya nyingi katika kipindi hiki zilizugumzia masuala
ya kidini, ziliandikwa na kuigizwa tu mashuleni na makanisani, lakini
hazikuchapishwa vitabuni. Mtaala huyu wa fasihi ya Kiswahili anahitimisha hoja
yake hii kwa kusema kuwa hadi tulipopata Uhuru, tamthiliya zote za Kiswahili
zilizochapishwa ilikuwa zimeandikwa na Wakenya. Madai haya yanaugwa mkono na
mtafiti wa utafiti huu.
Kipindi cha Uhuru,Coyle (1984), anadai kuwa, kabla ya miaka ya 1970,
tamthiliya za Kiswahili zilikuwa chache sana, na nyingi kati ya chache hizo
zilikuwa ni tamthiliya tafsiri, kwa mfano Mfalme
Edipode, Mabepari wa Venisi, Julias Kaizari na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Tamthiliya hizi zilitungwa kwa kufuata
kanuni za Ki-Aristotle na zilikuwa katika mtindo wa kishairi, nyingine
zilizotungwa katika hali ya mazungumzo.
Mulokozi (1996), anaeleza kuwa
tamthiliya ya Kizungu na zile za vichekesho ziliendelea kuandikwa na kuigizwa
majukwaani. Tamthiliyaandishi ya Kiswahili ilishika kasi sana kipindi hiki,
Ebrahim Hussein na Penina Muhando waliongoza katika uandishi wa Tamthiliya ya
Kiswahili kwa wakati huu. Tamthiliya za kipindi hiki zilikuwa zikizungumzia
masuala mbalimbali kama vile Migongano ya Kitamaduni ( mfano ‘Wakati Ukuta na
Kwenya Ukingo wa Thim’), Matatizo ya Kijamii (mfano ‘Lina Ubani, Mke Mwenza,
Hatia’), Dini (mfano ‘Aliyeonja Pepo, Maalim, Mukwava wa Uhehe), Ukombozi na
Utaifa (mfano ‘Mkwawa Mhinya, Johari Ndogo, Kinjekitile, Tone la Mwisho,
Harakati za Ukombozi’), Ujenzi wa jamii mpya (mfano, ‘Kijiji Chetu, Nuru Mpya,
Giza Limeingia, Mashetani, Mwanzo wa Tufani, Kilio cha Haki), Uake na matatizo
ya Kijamii (mfano, ‘Nguzo Mama, Ngozi, Machozi ya Mwanamke), Falsafa ya Maisha
(mfano, ‘Kinjeketile, Kwenya Ukingo wa Thim) na Uchawi, Uganga na Itikadi za
Jadi (mfano, ‘Njia panda (muhanika), Ngoma ya Ngw’anamalundi, Kinjeketile na
Mafarakano).NANI MUASISI WA KUTUMIA KANUNI ZA KI - AFRIKA KATIKA TAMTHIL;IYA YA KISWAHILI?
Hoja
hii ya nani mwanzilishi wa fasihi ya kiswahili ya kimajaribio katika uwanja wa
tamthiliya ilianza kujitokeza katika miaka ya 1980 ki mabishano. Wahakiki wa
mwanzo kabisa katika fasihi ya kiswahili kama wakina Nkwera walianza
kuizungumzia hoja hii mwishoni mwa miaka ya 1970 pasipo mabishano.
Miaka
ya 1980 na kuendelea ilikuwa ni miaka iliyowapambanisha mafahari wawili katika
uandishi wa tamthiliya ya kiswahili, Ebrahim Hussein na Penina Muhando walitawala
fikra, majukwaa, mijadala na makabrasha ya wahakiki wa kazi za kifasihi.
Baadhi ya mawazo ya wahakiki nguli juu ya“nani muasisi katika matumizi ya kanuni za
ki-afrika katika tamthiliya ya Kiswahili?”
Nkwera
(1977), anachambua kazi mbalimbali za Ebrahim Hussein na Penina Muhando. Katika
kujadili maendelao ya kazi za sanaa za Ebrahim Hussein, muhakiki huyu anamtaja
Bretch, mwandishi hodari na wa pekee wa michezo ya kuigiza ya kimashariki.
Nkwera anaanza kwa kusema:
“Hapo mwanzo
Ebrahim Hussein aliathiriwa sana na Bretch katika utunzi wake. Lakini kadri
alivyoendelea kustawi katika uandishi wake wa sanaa za maonyesho Ebrahim
Hussein alianza taratibu kuchanganya jadi za kiafrika kama vile masimulizi,
utambaji, mianzo pamoja na miisho ya kifomula katika uandishi wake. Hivyo
Hussein ndiye mwandishi wa mwanzo kabisa aliyeanza kuzikiuka taratibu za
kiuandishi katika tamthiliya zilizofuata kanuni za ki-aristotle kwa kuingiza
ujadi wa ki-afrika katika kazi zake”.
Mhakiki
huyu anahitimisha hoja yake hii kwa kujenga mazingira yanayoonyesha kuwa
mwanzilishi wa fasihi ya kiswahili ya kimajaribio katika tanzu ya tamthiliya ya
kiswahili ni Ebrahim Hussein, kwani ndiye mwandishi wa mwanzo kabisa aliyeanza
kuzikiuka taratibu za kiuandishi katika tamthiliya zilizofuata kanuni za
ki-aristotle. Nkwera ana hitimisha kwa kuchambua tamthiliya ya Mashetani
ya Ebrahimu Hussein na Pambo ya Penina Muhando. Nkwera anasema:
“Pambo ni
mchezo wa hali ya juu kimuundo. Hapana shaka yo yote kwamba Penina Mlama (hapo
awali alijulikana kwa jina la Penina Muhando) ameathiriwa na Ebrahim Hussein
kama Ebrahim Hussein alivyoathiriwa sana na Bretcht, mwandishi hodari na wa
pekee wa michezo ya kuigiza ya Kimashariki. Nkwera anasisitiza kuwa kwa mtu
aliyesoma Mashetani (OUP) hatasita kusema kuwa Mama Mlama kaathiriwa na
Ebrahim Hussein katika uandishi wake. Jambo hili liwe ni kweli ama sivyo, Si
jambo la msingi bali la maana zaidi nikufahamu tu kwamba waandishi hawa wawili
wamejitokeza kuwa mafundi na mabingwa wa kuandika michezo ya kuigiza katika
fasihi ya Kiswahili na ile ya kimajaribio”.
King’ei
(1987), anamtaja Ebrahim Hussein kama mwandishi wa sanaa ya maigizo
aliyefanikiwa katika kuchanganya mbinu za masimulizi ya mapokeo ya fasihi
simulizi kama vile ngano na vitendawili, na ufundi wa fasihi andishi ambao
ameutumia kutungia hadithi hizi kwa muundo wa maigizo jukwaani. King’ei
anaitaja tamthiliya ya Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi ya Ebrahim
Hussein kuwa mfano wa tamthiliya iliyoathiriwa sana na kumbo ya fasihi
simulizi.
Wafula
(1999), anautaja mwaka 1971 kuwa ni mwaka wa mabadiliko makubwa katika tasnia
ya tamthiliya ya Kiswahili. Mhakiki huyu anamtaja E. N. Hussein na tamthiliya
yake ya Mashetani, kuwa ni moja kati ya tamthiliya za mwanzo kabisa
katika harakati za utumiaji wa kanuni za kijadi ndani ya kazi za kifasihi.
Wafura anasema:
“Hussein alijitokeza
tena uwanjani, akathibitisha ameidhibiti bahari ya tamthiliya kwa kutoa Mashetani.
Tamthiliya ya Mashetani iliweka tarehe mpya katika utungaji wa mchezo wa
kuigiza katika lugha ya Kiswahili. Tamthiliya hii ilionyesha kwa mafanikio
makubwa, jinsi mapokeo ya kiafrika yanavyoweza kutumika pamoja na mbinu za
kisasa kufanikisha malengo ya kijukwaa”.
Katika
kutafuta udhibitisho kwa waandishi wenyewe wanaozungumziwa mvutano huu, utafiti
huu ulifanya mahojiano na mama Penina Muhando kutaka kujua mambo kadhaa juu ya
suala hili. Mwanafasihi huyu mashuhuri alilizungumzia suala hili kwa ufupi
sana. Mama Muhando alisema:
“Vuguvugu la
mabadiliko nchini Tanzania lilianza mwishoni mwa miaka ya 1970, katika kipindi
hiki wasomi wengi wa kiafrika walianza kupinga taratibu za kimaisha zenye
umagharibi (taratibu za watu wa Ulaya). Wasomi hawa waliutaja waziwazi ukoloni
kama sababu kubwa iliyopelekea kuharibika kwa utamaduni wa kiafrika. Baadhi ya
waafrika walianza kubadili majina yao yenye asili ya ukristo ama uislamu
kwenda. Kipindi hicho tukiwa wasomi na wanaharakati vijana tuliadhimia kuleta
mabadiliko kwenye sanaa ya kiafrika kwa kuzitumia kanuni za kiafrika hasa
katika sanaa za maonyesho, ndipo sasa kanuni za jadi ya ki-afrika kama
masimulizi, utambaji, mianzo na miisho ya kifomula zilianza kutumiwa na
waaandishi. Ukweli ni kwamba katika kipindi hiki cha vuguvugu la mabadiliko
Ebrahim Hussein alikuwa tayari ameanza kuugua maradhi yanayomsumbua hadi sasa,
hivyo hakushiriki sana katika vuguvugu la mabadiliko haya”.
Muhando (2013);
“Mimi na wasanii
wenzangu kipindi hicho tulitunga michezo mingi na kwenda kuicheza katika maeneo
mbalimbali “live”, tuliandika michezo mingi sana yenye kanuni za kijadi na
mingi kati ya michezo hiyo haijachapishwa na kwasababu kilikuwa ni kikundi
michezo mingine sijui hata ilipo. Na unapozungumzia mageuzi ama mabadiliko
katika tasnia hii ya sanaa za maonyesho usitazame kazi zilizoandikwa tu
vitabuni na kuwekwa ujadi ndani yake, lengo la mabadiliko yetu kipindi hicho ni
kuhakikisha kuwa sanaa za jukwaani zinaigizwa katika maeneo husika ya wanajamii
na kuleta mwamko wa kimaendeleo zinakuwa na nguvu kuliko zile zinazoandikwa na
kuishia kwenye vitabuni tu”.
Maelezo
ya Muhando yanaonyesha mwelekeo kuwa yeye pamoja na wasanii wenzake kipindi
hicho ndio walikuwa waanzilishi wa kutumia kanuni za jadi ya ki-afrika katika
tamthiliya za kiswahili.
(Williady, 2013) katika Utafiti wake, anaunga mkono mawazo ya Nkwera (1977),
King’ei (1987), Wafula (1999), Sengo (1977), yanayodai kuwa mwasisi wa kutumia
kanuni hizi katika tamthiliya za Kiswahili ni Ebrahim Hussein. Uungaji mkono
huu umetokana na sababu moja kubwa. Mwaka 1971, Ebrahim Hussein alichapisha
tamthiliya yake inayoitwa Mashetani, kama wasemavyo wahahiki kuwa Mchezo
huu wa Mashetani umekaa kishetani shetani ili msomaji au mtazamaji
auelewe vizuri inampasa ajigeuze shetani katika ulimwengu wa chukulizi za
kifasihi, ndipo atapata kuuelewa. Mwaka 1975, takribani miaka 4 baadaye tangu
kuchapishwa kwa mchezo wa Mashetani,
Penina Muhando alichapisha tamthiliya yake inayoitwa Pambo, ama
hakika Pambo ni mchezo wa kiwendawazimu wendawazimu, ili msomaji
auwelewe vizuri inampasa kujitia katika wendawazimu wa kifasihi. Hakuna tofauti
kubwa kati ya michezo hii miwili ya Mashetani na Pambo,
inaonekana Penina Muhando alichota baadhi ya misingi ya Hussein katika uandishi
wake. Haitoshi, mwaka 1976, Ebrahim Hussein alichapisha michezo yake miwili
aliyoiweka katika kijitabu kimoja, Jogoo kijijini na Ngao ya jadi.
Michezo hii imeandikwa kwa utaratibu wa fasihi simulizi, kuna ngano, watambaji,
hadhira na kuna kuanza na kukamilisha kazi ya fasihi kikanuni (mianzo na miisho
ya kifomula). Mwaka (1984), miaka takribani nane (8) baadaye Penina Muhando
alichapisha tamthiliya yake inayoitwa Lina Ubani, tamhiliya hii
inaonekana kuwa na sifa sawa na zile za Jogoo kijijini na Ngao ya
jadi. Kwa hoja hii utafiti huu unaunga mkono mawazo ya Nkwera na wenzake
kuwa mwasisi wa michezo yenye kukiuka taratibu za ki-aristotle na kufuata
taratibu za jadi ya ki-afrika ni Ebrahim Hussin. Kauli hii ya kumtaja Ebrahim
Hussein kuwa ndiye mwasisi wa tamthiliya hizi za kimajaribio haitoi ukweli kuwa
Penina Muhando naye anaumuhimu mkubwa sana katika tamthiliya ya Kiswahili.