Misingi ya Uhakiki katika Fasihi ya Kiswahili
Fasihi, Uandishi na Uchapishaji (Dar Es Salaam University Press, 1993, 260 p.)
SEHEMU YA TATU: UHAKIKI |
18. Mchango wa Waandishi wa Riwaya
R.S. Mabala
Kila mwandishi ni mwandishi mwanasiasa.
Swali la pekee la kujiuliza ni: siasa gani na ni siasa ya nani.
Ngugi wa Thiong'o
Lugha na Fasihi
Mjadala kuhusu lugha na fasihi hapa Tanzania una sura tofauti
sana tukilinganisha na nchi nyingine za Afrika kwa sababu ambazo sote
tunazifahamu. Ijapokuwa wapo bado waandishi wachache ambao wanapendelea kutumia
Kiingereza, kwa waandishi walio wengi hakuna mjadala tena kuhusu suala hili kama
linavyowatatiza waandishi wengi kama kina Ngugi wa Thiong'o.
Hali hii ni ya kimaendeleo kwa sababu waandishi na wahakiki
Watanzania wanaweza kuzama moja kwa moja katika uandishi wenyewe bila kupoteza
nguvu nyingi katika mijadala mirefu kuhusu lugha ipi itumike. Vilevile waandishi
hawana tatizo kuhusu wasomaji, maana lugha wanayoitumia ni ile ambayo wasomaji
wote wanaijua. Kwa hiyo wana nafasi nzuri ya kuweza kuifikia jamii nzima,
tofauti na Ngugi ambaye, bila kuwa na wafasiri, analazimika kuchagua ama
Kiingereza, ili aweze kuongea na watu wa kila taifa ndani ya Kenya, japo wasomi
wachache tu; ama Kikikuyu ili awafikie wakulima na wafanyakazi kama
anavyodhamiria, Japo Wakikuyu tu. Ndiyo maana Ngugi anasisitiza umuhimu wa kuwa
na wafasiri wawezao kufasiri kazi zake katika kila lugha ya Kenya.
Hata hivyo, nafasi hii ya kipekee aliyo nayo mwandishi Mtanzania
lazima itafakariwe vizuri maana ni rahisi kwa mwandishi kujiona yu mwandishi wa
umma kwa sababu tu anatumia lugha ya umma bila kutafakari yaokanayo na matumizi
ya lugha hiyo. Iko hatari ya mwandishi kuridhika kwamba iugha ndiyo kigezo pekee
cha mwandishi wa kimapinduzi. Hali hii hasa yahusu kizazi kipya cha waandishi
ambacho kimerithi mafanikio yanayotokana na mapambano ya 'vaandishi wakongwe
kukipa Kiswahili nafasi na hadhi yake kama lugha ya Watanzania. Katika
mapambano kama hayo mtu huelewa zaidi umuhimu wa lugha, pia matumizi na maudhui
yanayobebwa na kuwasilishwa na lugha hii. Kwa mfano, msimamo thabiti wa Ngugi
umetokana na mapambano hayo. Katika kitabu chake Decolonising the Mind
anasisitiza mambo mawili muhimu:
(a) Mwandishi Mwafrika anayedai kwamba hawezi kuandika bila kutumia lugha ya kigeni ni sawasawa na mwanasiasa ambaye anasema kwamba Afrika haiwezi kuendelea bila ubeberu. Tena mwandishi huyu yuko nyuma zaidi kuliko wamisionari na tabaka la vibepariuchwara ambao wote, kutokana na masilahi yao, wanatambua umuhimu wa kutumia lugha za watu ili waweze kufikisha ujumbe wao hata kama ujumbe wenyewe si wa kimaendeleo.
(b) Kutumia lugha za Afrika ni hatua ya kwanza ya lazima, lakini ni hatua ya kwanza tu. Kutumia lugha hii hakutachochea mabadiliko wala maendeleo ya maana iwapo haitatumika kuendeleza mapambano ya wafanyakazi na wakulima dhidi ya ubeberu.
Na anaendelea; "Kwa maneno mengine, waandishi wanaotumia lugha
za Kiafrika wanapaswa kujihusisha upya na mila za kimapinduzi za wakulima na
wafanyakazi wakijitayatisha katika mapambano yao ili washinde ubeberu na kujenga
mfumo madhubuti zaidi wa kidemokrasia na kijamaa."1
Hoja hii ya Ngugi ni nzito sana na sitegemei kwamba kila
mwandishi anaweza kulenga hivyo katika kila analoliandika. Lakini hoja hii,
katika muktadha wa dondoo letu la kwanza - kwamba kila mwandishi, akubali
asikubali, anahusika na siasa - ni msingi mzuri sana katika kuangalia na kupima
mafanikio ya waandishi wetu.
Mwandishi na Jwnii
Kutokana na maneno ya Ngugi hapo juu, yafaa vilevile kukumbuka
maneno ya wananadharia wawili wengine ambao waliandika katika mazingira tofauti.
Kwanza, Lenin alimwandikia Maxim Gorky baada ya Mapinduzi ya mwezi Oktoba 1917:
Ukitaka kuchunguza, sharti uchunguze kutoka chini, ambapo yawezekana kuangalia vizuri kazi ya kujenga maisha mapya katika makazi ya wafanyakazi, mikoani au vijijini.2
Hii inafanana na usemi wa Bertolt Brecht aliyesema kwamba
mwandishi sharti "atazame mdomo wa umma."3
Hapa tunaona kwamba Lenin na Brecht, kama wananadharia wote wa
kijamaa, waliona hatari ya mwandishi kujitenga na jamii. Lenin alimwandikia
Gorky kwa sababu wakati ule Gorky, ambaye daima huko nyuma alikuwa akiakisi
maisha ya wafanyakazi, alikuwa ameanza kulowea makao makuu akishirikiana na
waandishi na wasomi wenzake tu kiasi kwamba alianza kujitenga na umma. Brecht
kadhalika aliona umuhimu wa kuwakumbusha waandishi na waigizaji hatari hiihii.
Na hapa Tanzania hatari hii ipo vilevile kwa baadhi yetu. Uwezo wetu wa kuona,
kuelewa na kuakisi jamii barabara umeanza kufifia kutokana na kujitenga kwetu na
jamii au kushirikiana na aina au tabaka fulani tu ya watu, au kuchunguza kutoka
juu.
Lengo la Makala
Lengo la makala haya basi, ni kuangalia baadhi ya waandishi
ambao wameamua kuandika kuhusu matatizo, migongano, mapambano na maendeleo ya
Tanzania baada ya kupata uhuru. Hivyo sitaweza kuangalia wale ambao lengo lao ni
kustarehesha, wakiendeleza, kudekeza na kukuza fikra potofu katika jamii kama
anavyotahadharisha Ernest Fischer:
Kuigeuza sanaa kuwa biashara tu ili kuburudisha na kuridhisha nafsi ni hatari sana kwa sababu wakati vitabu vya aina hii vinajifanya kuwa vinamkomboa binadamu kumbe vinamdhalilisha.4
Hata baada ya kufinya uwanja wa makala haya, bado hatuwezi
kusema kwamba kutalii huku katika mada kunatosheleza, ila tu katika riwaya
ambazo napenda kuzingatia mielekeo fulanifulani inajitokeza. Unaweza kuzigawanya
riwaya hizi katika mafungu matatu:
(a) Riwaya zinazohusu Tanzania na suala la ukombozi kwa jumla nje na ndani ya Tanzania.
(b) Riwaya zinazoangalia hasa tabia ya watawala wa nchi.
(c) Zile zinazoangalia matatizo ya jamii ya tabaka la nchini, hususan katika vijiji.
Nimeamua kuangalia riwaya hizi kwa misingi mitatu mikubwa:
1. Haitoshi kusema kwamba fasihi inaakisi jamii. Kama anavyosema Ngugi:
Fasihi haiakisi hali halisi tu bali hujaribu kumshawishi msomaji kujenga msimamo fulani kuhusu hali halisi hii. Kwa hiyo suala siyo je, ameakisi Jamii? Bali je, ameakisi kutoka wapi na ana shabaha gani katika uakisi wake?5
Nikinukuu shairi moja fupi kabisa la mwandishi mashuhuri wa Afrika ya Kusini, Dennis Brutus, anasema:
Kioo kinahudumia
Mtazamaji anakielekeza.6
2. Yawezekana na yatokea mara kwa mara kwamba mwandishi anaweza, bila kujitambua mwenyewe,
(i) kuonyesha mambo ambayo hakudhamiria
(ii) kuonyesha mambo ambayo yanapingana na yale aliyodhamiria kuonyesha.
Kwa hiyo yawezekana kutokea mgongano kati ya ujumbe wa wazi aliodhamiria na ule uliofichika ambao pengine hakudhamiria au aliutambua kwa mbali.3. Ijapokuwa makala haya yanaangalia hasa maudhui ya riwaya hizi, ni wazi kwamba suala hili haliwezi kutengwa na fani anayoitumia mwandishi.
Mafanikio ya Riwaya
Mafanikio yanaonekana katika ule ujumbe wa wazi. Waandishi
wameongelea dhamira nyingi zenye maana na umuhimu sana hapa Tanzania.
Kwanza riwaya zimechochea na kuendeleza fikra za ukombozi wa
Tanzania na Afrika kwa ujumla. Kwa mfano, Pepo ya Mabwege na
Njama vimesaidia kuwapa Watanzania mwamko na urazini mkubwa zaidi. Katika
Njama mwandishi ametumia fani ya kina James Hadley Chase ambazo huhusu
uhalifu na upelelezi kupanua mawazo kuhusu ukombozi wa Afrika ya Kusini, uonevu
wa makaburu na mbinu zao.
Pili, zimefichua na kukosoa wapinga maendeleo ambao wamejivisha
ngozi ya kondoo na wanatumia nafasi zao kama viongozi kujinufaisha wenyewe na
kuihujumu Tanzania. Dhamira hii inaonekana katika riwaya karibu zote, k.m.
Pepo ya Mabwege, Sudiya Yohana, Nguzo Uhondo, Nyota ya Huzuni, na
kadhalika. Bila kuogopa, wameonyesha uozo mbalimbali ndani ya jamii, jinsi
viongozi walivyo na vyeo vingi, k.m., Sir Henry Mwapeker na Mzee James Katika
Pepo ya Mabwege; na mbinu wanazotumia ili kujijenga na kujiimarisha mpaka
wote wanawaogopa. Hata polisi wanaogopa kufungua kesi ya Kalenga dhidi ya
Waziri. Hali hii yaonekana hadi uongozi wa kijijini. Kwa mfano, katika Njozi
Iliyopotea wanakijiji wote wanaogopa mwanzoni kumpinga Jumbe Mpwite kwa kuwa
ni Mwenyekiti na anaye mganga wake.
Vilevile waandishi wamekazana kuonyesha ulaghai wa watu kama
hao. Mzee James anagombea ubunge kama mjamaa. Joseph katika Sudi ya
Yohana anahubiri kuhusu ukombozi wa Mwafrika na anapenda kusaidia ndugu zake
huku akiwa mstari wa mbele katika kuhujumu kijiji chake na kuharibu maisha ya
nduguze. Katika Njozi Iliyopotea Lupituko anatumia nguvu kujenga siasa ya
ujamaa ili kuridhisha silika yake ya ukatili na kuonyesha uwezo alio nao.
Kadhalika itikadi ya Mambosasa katika Gamba la Nyoka imejaa kujitetea
kwingi na visingizio vya kuridhisha nafsi yake.
Tatu, riwaya hizi zimeweza kuangalia kwa undani na kufundisha
juu ya matatizo yanayolikabili tabaka la wanyonge.
Mojawapo ni kuhusu uongozi mbaya. Viongozi wengi ni vidikteta
vidogo kama Lupituko au Katibu Tarafa Kagunda ambao wanaonea wananchi. Lupituko
anahamisha familia kikatili kwa sababu mtoto wa kike alimkataa na baadaye anaua
msichana mwingine katika kujaribu kumnajisi. Katika Sudi ya Yohana
Kagunda kadhalika alimfunga mwanamke aliyemkataa. Katika Gamba la Nyoka
Mambosasa anapokea hongo kutoka kwa wafanyabiashara.
Uongozi huu ulionekana hasa katika kipindi cha kuanzisha vijiji.
Mara nyingi vijiji vilijengwa mahali pabaya kwa sababu ya wivu wa pimapima au
hongo wanazopewa na makabaila au matajiri. Vilevile nguvu zimetumika kuhamisha
watu bila sababu yoyote.
Athari za udhanifu katika jamii, ukiwa uchawi au Ukristo,
unaonyeshwa pia. Katika Mirathi ya Hatari tunaona jinsi uchawi
unavyotishia jamii nzima hadi hapo wachawi wote wanapoteketea. Hali kadhalika
katika Gamba la Nyoka tunaona jinsi imani za wanakijiji zilivyoruhusu
Mmarekani asiye hata Padre kupenya, kuchokoza vita kati ya wanakijiji na
serikali, na kusababisha vifo vingi na baadaye kuua wengine kwa kutia sumu
kisimani.
Katika Sudi ya Yohana, Amina anamsifu na kumshukuru
Yohana kwa kusema:
Mwenyezi Bwana ndiye kakutuma uje uniokoe, hakunitupa mimi mja wake. Si haki kumlaumu bali kuomba kujaziwa mema zaidi.7
Nne, riwaya zimeonyesha vijana wengi wanavyokimbilia mjini, kwa
mfano, Matika na Chonya katika kitabu cha Shida. Hii yaweza kutokana na
mila (kwa mfano Matika alikimbia kuozwa kwa nguvu); au fikra finyu kuhusu maisha
ya mjini na nafasi za kupata kazi na kuishi kwa raha.
Tano, riwaya hizi zimefaulu kuonyesha matatizo ya wanawake
katika jamii. Mara kwa mara wanawake wanaonyeshwa kuwa chombo cha uchu na ulafi
wa wanaume. Familia ya Nyalindele inahamishwa kwa nguvu kwa sababu Nyalindele
anamkataa Katibu Kata. Tulilumwi anakufa kwa sababu hiyohiyo; Losia analeweshwa
na kudanganywa na kuachwa na mimba hadi anaamua kujiua. Agnes, mke wa Yohana,
ananajisiwa kwa nguvu na shemeji yake. Matika anapokimbilia mjini analazimika
kuwa malaya; Josina naye ananajisiwa baada ya kupewa dawa za kulevya. Mkewe
Zautwa nave anafungwa kwa sababu ya kumkataa Katibu. Wanawake wanaonyeshwa
wakidharauliwa kupita kiasi. Anavyosema Lukova katika Njozi Ilivopotea:
Mke ni kama ngalawa. Matumizi yake makubwa na faida yake kidogo daima imaji mkukuu; hufaa lakini haiaminiki.8
Hata wanapojitahidi kujitetea au kubaki na msimamo wao
wanaadhirika vibaya. Mara nyingi mwisho wanahesabiwa kuwa vyombo vya starehe tu.
Sita, waandishi nao wametoa ufumbuzi wa aina mbalimbali wa
matatizo wanayoyaonyesha. Kwa mfano, mwishoni mwa Njozi Iliyopotea
wanavijiji wameshagundua ubaya wa Jumbe Mpwite, na wanasimama imara kwa pamoja
dhidi yake na wenzake. Katika Gamba la Nyoka mwandishi anaonyesha vizuri
sana kwamba watakaoendeleza maisha ya wakulima ni wakulima wenyewe, si wahubiri
kutoka nje, wawe wa siasa au dini:
Wana mapinduzi halisi ni wale waishio vijijini wanaoathiriwa na upepo wa wakati unaowasukuma mbele kutoka walipokuwa. Kwao maisha ni maisha. Wanatazama kwa uangalifu kila badiliko linalohusu maisha yao kama watazamavyo kwa uangalifu na matumaini makubwa mimea yao ikikua9
Mara nyingi pia waandishi wanapenda kuonyesha maadui
wakifichuliwa au kuteketezwa kama katika Pepo ya Mabwege.
Kwa kweli maelezo haya ya mafanikio yamekuwa mafupi mno na ya
jumla, maana lengo la makala haya halikuwa kuangalia mafanikio haya ya wazi kwa
undani sana. Lakini isingefaa kuzama kwenye matatizo tu bila kutambua kwamba
waandishi hawa wamekwisha kutoa mchango mkubwa.
Matatizo ya Riwaya
Mafanikio ya dhamira za waandishi yameathiriwa mara nyingi na
mambo makuu manne:
(a) Kushindwa kuonyesha uhalisia kamili.
(b) Kuzama katika nadharia ya ubinafsi bila hata kujitambua.
(c) Falsafa na mtazamo wa kukata tamaa katika maisha - mtazamo kwamba maisha ni matatizo tu; mfululizo wa mateso usio na mantiki wala utatuzi.
(d) Waandishi kupenda kusisitiza hoja zao kwa kuhubiria watu.
Uhalisia
Katika riwaya zao waandishi kwa ujumla wamefuata mtindo wa
uhalisia, yaani wamedhamiria kuakisi jamii jinsi ilivyo, mara nyingi wakiwa na
lengo la kuikosoa jamii ili ijirekebishe. Katika hali hii, lazima matukio na
wahusika viwe vya kuaminiwa. Iwapo msomaji husita kupokea yanayotokea, riwaya
huanza kuchechemea.
Mtiririko wa Vituko
Udhaifu huu unaonekana mara a kwa mara katika riwaya. Kwanza
kuna matukio mengi ambayo yanapunguza uzito wa dhamira. Kwa mfano katika Pepo
ya Mabwege, Josina, Kalenga na Hamisi ambao walikuwa wameachana siku nyingi
wanakutana kwa bahati tu wakati mambo yameiva. Kalenga anapokwenda kumshitaki
Mzee James, asingefika popote bila kufika ghafla kwa Hamisi ambaye hajaonanana
Kalenga miaka kumi na nne lakini sasa amerudi na bahati nzuri amepandishwa cheo
sana kiasi cha kuweza kumsaidia Kalenga moja kwa moja. Vilevile katibu wa Mzee
James ni Blandina ambaye ndiye alikuwa mchumba wa Hamisi walipokutana Urusi, na
ni huyuhuyu ambaye mbele ya Josina na Kalenga "anaponda" mvulana wake kwenye
kituo cha basi kwa sababu ya kupewa lifti na mkwasi. Matukio kama haya labda
yaweza kukubalika lakini utatuzi wa matatizo yote katika riwaya unakuwa kana
kwamba ni wa juujuu tu na wa kulazimisha. Kalenga ameshachukiwa na wakubwa,
wakiwemo Mhariri Mkuu wa gazeti analofanyia kazi. Msimamo wake wakati huu
umekwishakua, na hata kufukuzwa amefukuzwa kazi, lakini katika siku chache
zilizobaki anaachiwa gazeti awe mhariri mkuu. Anatumia nafasi hii vizuri
kufichua njama kadha wa kadha na maadui wa taifa wanakamatwa. Basi ufumbuzi
mzima wa riwaya. wategemea kitu ambacho kiko nje ya uhalisia.
Kadhalika katika Njama, mtiririko wa vituko wategemea
Willy Gamba au wenzake wa Sierra Leone kuwepo, kwa bahati tu, mahali na wakati
unaofaa kila mara. Mfano ni Willy anavyomwokoa Zabibu nukta chache kabla ya
kuchinjwa. Kadhalika Willy anapokwenda Sierra Leone anatokea kukutana na mtu
atakayemfaa katika mapambano ya baadaye.
Mtiririko mzima wa Njama unamtaka msomaji afumbe macho
ili asione mambo yasiyoaminika. Kwa mfano, mauaji makubwa yanafanywa na kundi la
majasusi wasaliti lakini kila mara wanapomkaribia Willy wanamwonya tu na hivyo
kumpa nafasi ya kuwamaliza wote mwishoni. Vilevile shabaha yao ghafla inageuka
kuwa mbaya kila wakimlenga yeye. Hivyo umaarufu wote wa Willy Gamba unatokana na
mwandishi kwenda nje ya uhalisia.
Mtiririko wa Gamba laNyoka nao haufuati uhalisia katika
sehemu muhimu. Kwa mfano, maisha ya Mambosasa na Mamboleo hayaeleweki.
Wamerudishwa kijijini kwa sababu ya tabia zao mbaya na upinzani wao dhidi ya
serikali. Sasa yashangaza kwamba japo hawajaonyesha kuwa wamejirekebisha
wanaruhusiwa kugombea uongozi wa kijijini. Halafu baadaye ingawa bado matendo
yao hayakubaliki kwa watawala (k.m., wanampiga Padre Madevu, wanakula fedha za
kijiji, na wanahongwa na watu binafsi hadi kijiji chenyewe kinawakataa),
Mamboleo anachaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya. Kwa hiyo matukio
yanaonekana yanatukia tu kwa amri ya mwandishi ambaye yeye, kama Mungu, anaweza
kuamua afanye lolote lile na dunia aliyoiumba. Hata mwanzoni mwa riwaya watu wa
Kisole, katika kuamua kukataa kuhamia kijiji kipya wanaua wanamgambo karibu mia
moja lakini zaidi ya kukalishwa juani kwa muda wa saa chache na kuhamishwa kwa
nguvu siku inayofuata, hakuna hatua yoyote inayochukuliwa dhidi yao, au viongozi
wao. Hivyohivyo, Madevu anapoua watu ishirini kwa sumu hatuoni hatua yoyote ya
maana inayochukuliwa. Mikasa hii ya hatari katika jamii inapita sawasawa na
mkasa wowote mwingine kama vile mtu anavyowatembelea wakwe zake! Uzito wa mikasa
na vipi jamii inalichukulia jambo hili zito hatuonyeshwi. Badala yake tunaona tu
kwamba Tina anajuta kumwua Madevu bila hata kukumbuka wanakijiji wenzake
waliokufa.
Upande wa Njozi Iliyopotea yaelekea kwamba mwandishi
anataka kutuonyesha kwamba viongozi wanatumia vibaya madaraka yao lakini uzito
wa hoja hii unapungua kutokana na kwenda nje ya uhalisia. Hii inaonekana hasa
katika kesi ya Lukova baada ya kumpiga Katibu Lupituko.
Lupituko, akiwa ni kiongozi wa serikali, alikuwa na nafasi ya
kutosha kummaliza Lukova kwa kuonyesha jinsi Lukova, kama 'mpinga mapinduzi',
alivyomwingilia katika kazi yake na kumpiga akiwa kazini. Lupituko angeweza kula
njama na hakimu na kumwadhiri Lukova sawasawa. Mashtaka dhidi ya Lukova ni
makubwa: wizi wa kutumia nguvu, kuwa na meno ya tembo kumi na moja na ngozi tatu
za chui bila kibali, kuwa na bangi masanduku mawili, na kuwa na bunduki ya
serikali iliyoibiwa. Mashtaka kama hayo yanahitaji ushahidi wa kutosha na
yanaweza kubatilishwa kabisa na wakili mahakamani, lakini utetezi wake tu ni
kwamba ndugu na marafiki wanasema kwamba Lukova hana tabia ya namna hii. Hivyo:
(a) Mashtaka yenyewe yameongezwa kupita kiasi
(b) Utetezi upande wa mshtakiwa ni mdogo mno. Iwapo wakili kweli alimwonea huruma na kuamua kumtetea ipasavyo, anastahili kufukuzwa kazi kwa kushindwa kubatilisha mashtaka yasiyo na ushahidi.
(c) Ushahidi wa Kiligilo usingekuwa na maana yoyote hata kama angeweza kusema bila kuondoka kwa ghadhabu. Kwa hiyo dhana ya kwamba rafiki yake alihukumiwa kwa sababu Kiligilo alishindwa kumtetea haipo kabisa. Kutokana na hayo, uzito wa hoja ya mwandishi unapunguzwa.
Mifano kama hii inaonekana katika karibu kila riwaya. Katika
Sudiya Yohana Joseph anazidi kumdhulumu ndugu yake kuanzia kumwingilia
mke wake kwa nguvu, hadi kumkatalia nafasi yake ya kusoma ng'ambo, na mwisho
kumfukuzisha kazi. Licha ya yote haya bado anategemea kwamba Yohana atakubali
kumwendeshea kampuni yake. Vilevile migomo ya wafanyakazi inapachikwa tu kwa
kuwa mwandishi anataka kuonyesha mwamko wa wafanyakazi.
Uchoraji wa Wausika
Kukosa uhalisia upande wa wahusika nako kunaathiri sana dhamira
ya mwandishi. Tukianzia kwa Mambosasa na Mamboleo katika Gamba la Nyoka,
ni kweli kwamba hawa ndugu wawili wana migongano mikubwa ndani yao kutokana na
kulewa itikadi na ukatili wao, lakini mwandishi ameshindwa kuoanisha vipengele
mbalimbali katika tabia zao. Mara twaambiwa wamefanya mema mengi katika jamii,
kwa mfano, kufichua wenye maduka wanyonyaji na wapimaji wa pamba walaghai;
kujenga visima vizuri kwa kushirikiana bega kwa bega na serikali katika
operesheni vijiji, n.k.; mara twaambiwa kwamba ni wapinzani wakubwa ambao
walimpiga mwalimu wa siasa J.K.T. na kusambaza karatasi ya uchochezi kambini.
Upande wa mapenzi, Mambosasa anajiambia:
"Sina muda wa mapenzi. Mapenzi ni mojawapo kati ya mambo ambayo hayapasi kuambatana na tabia njema ya mwanamapinduzi halisi."10 Lakini hapohapo tunafahamishwa kwamba sababu nyingine ya kurudishwa kwao kijijini ni kwamba walimnajisi msichana. Hivyohivyo katikati ya mjadala mzito juu ya matatizo ya ujamaa Mambosasa anauliza: "Mamboleo umekwishashika maziwa ya msichana mdogo?"11
Ni kweli kwamba binadamu amejaa mikinzano ya kila aina, lakini
lazima kuwepo na uhusiano na mfungamano kamili wa wahusika hao ambao utafanya
tuyaamini mabadiliko haya ya tabia ya mara kwa mara. Hali hii inaathiri hata
wahusika wengine. Mara nyingi pia tabia za wahusika hazionekani kwa vitendo
kiasi kwamba kunakuwepo na mgongano. Kwa mfano, katika Njozi Iliyopolea
mwandishi anataka kujenga dhana ya kwamba Kiligilo ni mcbapakazi na mpenda haki
anayewafunulia wanakijiji haki zao na kujenga umoja thabiti katika kuendeleza
kijiji. Hayo yote tunaambiwa moja kwa moja na mwandishi mwenyewe, hatuyaoni sana
katika vitendo vya Kiligilo. Kinyume chake mara nyingi anachelewa kuamka na
kwenda kazini; mara tu baada ya kufika kijijini na kuanza kazi, anapata matatizo
na anapotea mwezi mzima. Hajaonyesha tabia yoyote inayotudhihirishia kwamba
maneno ya mwandishi ni kweli. Hivyo inaonekana kwamba mwandishi analazimisha
hoja zake.
Hata hivyo Kiligilo angalau ni binadamu, kinyume na Willy Gamba
ambaye kwa uwezo wake anafanana na miungu, na kama miungu walivyo anaabudiwa,
hasa na wanawake. Anatamba mwenyewe, "mimi huwa sielewi kwa nini binadamu hawa
hutokea kunipenda mara tu nionyeshapo uso wangu.13
Na kweli. Kwa mfano, Zabibu anaambiwa kwamba mpenzi wake
ameuawa. Wakati huohuo mara amekwishampenda Willy:
Niko tayari kukusaidia kwanza kwa sababu umeniokoa pia kwa sababu unapeleleza kifo cha mpenzi wangu na tatu nafikiri wewe ni kijana mwenye kupendeka.13
Ikifika usiku anakwenda kulala na Willy.
Mfano huu unaonyesha uhalisia hafifu katika uchoraji wa
wanawake. Nisingependa kusema mengi maana mada hii ina siku yake, lakini kwa
ujumla wanaonekana binadamu dhaifu kupita kiasi. Katika Njama, mapenzi
yao hubadilika mara moja. Mfano mwingine ni Margret. Mara atokeapo mwanamume
shujaa basi tunaona mara moja msichana huyo "ameshakwisha" japo wakati huo
anaomboleza kifo cha mpenzi wake. Hata kama wako wasichana ambao nao wana nguvu,
kama vile Veronica, bado haifuti wazo kwamba wanawake ni chombo cha starehe,
hasa kwa mtu kama Willy ambaye mwandishi anatuambia kwamba anastahili warembo
hao kwa sababu ya kazi ngumu anayoifanya.
Hata katika riwaya nyingine, wanawake huonyeshwa wadhaifu kupita
kiasi na rahisi kudanganywa au kulazimishwa. Hata jitihada za baadhi yao
kusimama imara zinaishia ukingoni tu. Josina anapewa dawa za kulevya na
kunajisiwa. Losia, msichana mwenye tabia nzuri ajabu, ambaye wakati wote akiwa
shuleni hakuteteleka hata kidogo, anadanganyika kirahisi na pombe ya siku moja
na kuamka kesho yake kitandani mwa mwanamume bila hata kujitambua alifikaje
pale. Tena hapohapo anabeba mimba na mwisho kuona njia ya pekee ni kujiua.
Ameshindwa. Mama Liganga naye anasimama imara kujitetea lakini matokeo yake
anafungwa miaka mitatu na kugeuka malaya anapofunguliwa. Mkewe Yohana naye
analazimishwa na Joseph. Kuna mifano mingine mingi. Ni kweli kwamba waandishi
wanataka kuonyeshajinsi wanawake wanavyoonewa, lakini mwishoni inaonekana kwamba
hata wale wanaotaka kusimama imara wanashindwa wote. Kwa hiyo watabald dhaifu
tu.
Mwisho, upande wa wanawake, mara nyingine tunalazimishwa
kujiuliza kama wanawake wasio na uzuri kupita kiasi wana nafasi kalika jamii.
Hali hii yajitokeza hasa katika Njama. Kila msichana ni mrembo kupita
kiasi, ambaye hajawahi kuonekana, na ni haohao wenye uwezo. Hii ni kurahisisha
mambo kupita kiasi na inadhalilisha uwezo na tabia za wanawake. Katika riwaya
nyingine hali hii siyo mbaya sana lakini hujitokeza hapa na pale.
Mauaji
Riwaya nyingi zimejaa mauaji. Katika Njama Willy anaua
karibu watu mia moja peke yake. Katika Pepo ya Mabwege, Josina na Master
Peter wanakufa. Katika Njozi Iliyopotea Losia Lukova, Tulilumwi, na
Lupituko wanafariki; na katika Mirathi ya Hatari wanakufa watu wengi
sana. Huenda hali hii inatokana na:
(a) kutaka kumshawishi msomaji kwa kutumia vituko visivyo vya kawaida
(b) haja ya kuipatia riwaya tamati yenye kuridhisha. Hata hivyo mauaji nayo yakizidi uhalisia hupungua.
Kutia Chumvi Nyingi
Mauaji ni mfano mmoja tu wa jinsi waandishi wanavyotia chumvi
kupita kiasi. Njama inatupa mfano halisi mwingine:
"Nilijiviringisha hewani namna ambayo wote walishangaa; risasi zao zote zikanikosa. Wakati uleule nikaachia za kwangu nikawapata wote nao wakaanguka chini.14 Au kwingine tunaambiwa kwamba Willy anaweza kuruka futi nane, ambayo ni zaidi ya rekodi ya dunia. Kutokana na chuku za namna hii, mhusika haaminiki.
Hali hii inaonekana mara nyingine mwandishi anapotaka kusisitiza
hoja yake. Kwa mfano hadithi nzima ya Amina anavyoachwa pale kwenye kituo cha
basi huku akitaka kujifungua. Mwandishi anataka kutuonyesha jinsi jamii
ilivyoharibika lakini lengo na msisimko wa sehemu hii unapotea.
Mwisho waandishi wengi wanapenda kutuinia tashititi, ucheshi,
n.k., ili kuwasilisha ujumbe wao. Kwa mfano, katika Pepo ya Mabwege
mwandishi anaonyesha jinsi watumishi wa hoteli wanavyowakimbilia Wazungu hadi
wanagonganisha vichwa na mmoja anapoteza jino. Vivyohivyo kanisani Josina
anapomkataa Peter, matendo ya watu kuhusu jambo hili yanatiwa chumvi sana.
Tashititi kwa kawaida hutegemea utiaji wa chumvi lakini ili ifanikiwe inapaswa
iwe sehemu kamili ya muundo na mtiririko wa hadithi kwa jumla.
Udhanifu
Udhanifu huonekana hasa katika tamati za riwaya. Mwandishi
anapenda kuonyesha hali ya maendeleo au kuondoa waovu, kwa hiyo anapachika
tamati nzuri ambayo mara nyingine inakwenda kinyume na yaliyotokea awali.
Pepo ya Mabwege ni mfano mzuri. Tumeshaonyesha kwamba kufichuliwa na
kuondolewa kwa uovu ndani ya jamii kunategemea Kalenga kuwa Mhariri Mkuu kinyume
cha hali halisi. Matokeo yake ni kwamba wema unashinda, jamii inasafishwa, na
Kalenga anapandishwa cheo kuwa Mhariri Mkuu. Kwa hiyo inavyoonekana uozo
haukutokana na mfumo hata kidogo, bali umetokana na watu wachache tu wenye nia
mbaya ambao wametumia nafasi zao kwa faida yao. Sasa kizazi kipya kimeshika
hatamu, kwa hiyo hakuna matatizo yoyote wala haja ya kufanya mabadiliko katika
jamii.
Katika Shida, Chonya na Matika wanarudi katika kijiji cha
Paradiso. Mapambano yamekwisha. Katika Gamba la Nyoka mwandishi anakwepa
udhanifu huu. Anaonyesha matatizo kadha wa kadha yanayokabili uanzishaji wa
vijiji vya ujamaa, lakini mwishoni mapambano yanakwisha hivyohivyo. Viongozi
wabaya vijijini na wilayani wanaondoka, trekta inafika, na mabomba ya maji -
mpaka tunaelezwa hata kazi za kila kamati kijijini. Kwa hiyo baada ya dhiki,
faraja yapatikana moja kwa moja. Katika Mirathi ya Hatari wachawi wote
wanateketea. Si kwamba tamati nzuri ya matatizo haiwezi kupatikana, ila tamati
hizi zinaishia katika ndoto kwa sababu:
(a) mara nyingine hazitokani na yaliyotangulia; na
(b) zinakuwa nje ya maisha ya kila siku ya jamii. Harakati zinatoweka.
Kwa kifupi, lengo la sehemu hii ya "udhanifu" ni kuonyesha jinsi
udhaifu wa uhalisia unavyoathiri sana dhamira za waandishi, maana mahali ambapo
msomaji anashindwa kukubali uakisi wa wahusika na hali halisi basi na dhamira ya
mwandishi nayo haitakubalika.
Ubinafsi
Ijapokuwa waandishi wanaonyesha jamii ikipambana na waovu,
mapambano haya daima hutegemea nguvu ya watu wachache sana. Umma haupo. Mfano
halisi ni Njama. Ijapokuwa mwandishi anasema kwamba riwaya ni: "Kwa ajili
ya wale wote ambao wamejitoa mhanga katika kupigania uhuru wa bara hili la
Afrika,"16 dhamira inayojitokeza ni kwamba bila Willy Gamba na uwezo
wake wa kujiviringisha kwa namna ya ajabu, ukombozi wote ungekwama. Wapigania
uhuru wenyewe wamepigwa butwaa pamoja na kamati ya ukombozi na polisi. Hawana
nguvu yoyote. Hata mwishoni mahali ambapo imeeleweka wazi mahaini wako wapi na
ni kiasi tu cha kuwazingira na kuwakamata bado ni Willy tu na Sherriff, Eddy na
Isaac ambao wanakwenda peke yao kuteketeza kundi zima la wahalifu. Hivyo dhana
inayopatikana hapa ni kwamba ukombozi wategemea nguvu ya binadamu wachache wenye
vipawa vya ajabu. Kazi ya umma ni kukaa na kushangilia na kushukuru hawa
wachache kwa kuwaokoa wao wasio na akili na uwezo wowote.
Huu ni mfano mmoja wa dhamira zilizojificha, dhamira zenye
kuhitilafiana na zile zilizo wazi. Mapema katika riwaya mwandishi anaeleza kwa
ufasaha umuhimu wa mapambano ya umma na jinsi vyama vya kupigania uhuru
vinavyojitahidi, lakini hadithi yenyewe inaonyesha kwamba mbele ya mbinu za hali
ya juu ya makaburu, umma hauwezi kitu.
Dhana nyingine inayotokana na hiyo ni kwamba hawa binadamu
wachache wa ajabu wanastahili maisha ya ukwasi wa hali ya juu kutokana na
mchango wao. Hivyo Wasichana warembo "wanawaangukia" kila dakika, wanaweza
kusafiri dunia nzima kupumzika kama Willy alivyokwenda Sierra Leone, maisha yao
ni.kula katika hoteli za kitalii na kunywa pegi nyingi za wiske. Hapo vilevile
twaambiwa kwamba lipo tabaka la juu linalostahili maisha haya mazuri lakini siyo
tabaka la umma.
Katika Pepo ya Mabwege hali hii haijitokezi kiasi hicho
lakini ipo. Mwapeker na James ni watu wakubwa katika jamii na nyadhifa zao ni
nyingi lakini wanaangushwa na jitihada za Kalenga peke yake akisaidiwa na Hamisi
na watu wengine wachache. Kwa hiyo hapa vilevile mapambano ni kati ya wale waovu
wakubwa na watu wachache wanaowaona. Ni vita vya mafahali, sisi wengine twabaki
ni watazamaji tu.
Kwa ujumla nguvu ya wafanyakazi haionekani kabisa. Hata wale
wasaidizi wa Kalenga waliosoma naye wana kazi nzuri katika jamii, k.m. mwandishi
wa habari, inspekta wa polisi, mwalimu - wote wamepata nafasi ya kusafiri nje.
Kwa hiyo karibu ni wa tabaka lilelile la kina Mwapeker. Labda tofauti ni kwamba
hiki ni kizazi kipya lakini nafsi zao ndani ya mfumo ni zilezile, na mfumo
unabaki palepale. Mwapeker na James wanajenga himaya yao kwa kutumia watu
binafsi wanaowafahamu, na Kalenga na wenzake wanawaangusha kwa kufanya
hivyohivyo. Tunaweza kujiuliza kama Hamisi angemsaidia Kalenga iwapo hawakusoma
pamoja. Vilevile ni jambo la ajabu kwamba wote wenye msimamo imara wanatoka nje
ya Tanzania au wamekwenda ng'ambo. Katika Njama Willy anasaidiwa hasa na
watu wa Sierra Leone. Ni vizuri sana kuonyesha umoja wa Afrika lakini Watanzania
nao hawana uwezo huu isipokuwa Willy na wenzake katika upelelezi? Katika Pepo
ya Mabwege kadhalika, Kalenga amesoma Nairobi na kufanya kazi Msumbiji,
Josina kasoma Cuba, na Hamisi Urusi. Waliosoma Tanzania wanaonekana hawawezi
kupata urazini huo mkubwa.
Ubinafsi unaonekana vilevile katika dhamira ya wahusika wengi ya
kulipiza kisasi. Willy anamfuata Shuta kumlipizia kisasi Veronica. Kalenga naye
anasukumwa na nia ya kumlipizia kisasi Josina. Vilevile katika Sudi ya
Yohana mwandishi anaona kwamba njia pekee ya kutatua matatizo
yanayojitokeza katika jamii ni Yohana kwenda kumchoma kisu Joseph. Zautwa
alikuwa hoi kwa sababu alishindwa kulipiza kjsasi. Mdogo wake Wakili Mwakipusi
naye aliishia kulipiza kisasi. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo waandishi wanaleta
dhana ya kwamba kila mtu binafsi akiamka namna hiyo basi hata kama jamii
haibadiliki angalau haki fulani itakuwa imetendeka; kilio cha wanyonge kitakuwa
kimesikika na mwovu atakuwa ameadhirika hata kama mfumo ulioruhusu uovu huu
umebaki palepale.
Kusema yote hayo hakuna maana kwamba mwandishi wa makala haya
anataka kuona wafanyakazi wakiamka na kupigana moja kwa moja wakiwa na urazini
mkubwa na mikakati ya hali ya juu. Hii itakuwa kinyume cha uhalisia tena. Lakini
yawezekana kwamba waandishi hao wameathiriwa na elimu yao na nafasi zao katika
jamii kiasi cha kuona mapambano upande wa tabaka la kati tu, na mapambano ya mtu
binafsi kutetea haki zake kazini, shuleni, na kadhalika, bila kuona na kushiriki
katika mapambano ya walio wengi ambayo yanaendelea siku hadi siku. Tukitumia
mfano mmoja wa tamthiliya, tunaona kuwa katika mchezo wa mafuta
wafanyakazi wanagoma lakini mara tu wanapofukuzwa kazi na kuona njaa ya siku
mbili wanarudi na kulamba miguu ya tajiri wao. Hii ni tofauti na waandishi
wengine mashuhuri wa Afrika, k.v., Sembene Ousmane, Ngugi wa Thiong'o na Alex la
Guma ambao daima wanatambua kwamba umma upo na nguvu unazo hata kama hawaamki
wote kwa pamoja na kupambana kila wakati. Kwa hiyo mapambano ya mtu binafsi
yanapewa nafasi yake katika mapambano mapana na mazito zaidi ya jamii nzima.
Kukata Thmaa
Waandishi wengine wanaonyesha vizuri sana matatizo ndani ya
jamii lakini yaelekea kwamba matatizo haya hayatokani na mfumo wa jamii
uliojengeka bali hulka za binadamu. Mambo yakiwa hivi, basi hakuna matumaini ya
kuleta mabadiliko ndani ya jamii. Dunia ni tambara bovu. Labda tungoje ya
mbinguni. Kwa mfano katika Gamba la Nyoka, maisha ya Mambosasa na
Mamboleo yanabadilika siku hadi siku bila kueleweka. Inavyoonekana maisha hayana
mantiki kabisa: Mamboleo ghafla anapandishwa kuwa Mkurugenzi bila kufanya lolote
la maana. Mwenzake anarudishwa kuwa Mwalimu vilevile bila sababu yoyote ya
kuonekana tofauti na mwenzake. Mkuu wa Wilaya anakalia barua ya Mambosasa tu
bila sababu wakati Mamboleo anapewa ya kwake.
Katika Njozi Iliyopotea kadhalika tunaona jamii na wema
katika jamii wakizidi kudidimizwa na mwandishi. Si kwamba tunatakiwa kuona
kwamba wema wanashinda kila mara, la hasha, lakini ni kama mwandishi amedhamiria
kutuonyesha kwamba maisha ya binadamu ni kuwa mpweke tu. Kiligilo na Mzee
Malongo wanaelewana mara moja kwa sababu ya upweke wao, lakini kila Kiligilo
akiwa na tegemeo la kuondoa upweke, tegemeo hili linavunjiliwa mbali. Mpenzi
wake Losia anadanganywa na mwisho anajiua. Lukova anaonewa kwa mashitaka ya
ajabu na baadaye anakufa ghafla kutokana na ugonjwa unaozuka jela. Matumaini ya
Kiligilo kwa Tulilumwi yanakatishwa na ukatili wa Katibu Lupituko mpaka Kiligilo
anaishia kupata kichaa. Mwandishi anatuonyesha kwamba kweli njozi imepotea
kabisa.
Mahubiri
Mara nyingi mwandishi anaamua kufikisha ujumbe wake kwa njia ya
mahubiri, ambayo mara nyingine yanapingana na uhalisia. Kwa mfano, katika
Mirathi ya Hatari mhusika mkuu anaamua kuwahubiria wachawi palepale ndani ya
pango lao. Katika Njama mwandishi anafikisha ujumbe wake sehemu ya mwanzo
ya kitabu kwa kutueleza historia yote ya nyuma ya Afrika ya Kusini na sababu ya
mapambano - Vero, Sherriff na Willy ambao wote wanajua mambo hayo fika inabidi
wahutubiane ili sisi wasomaji tupate ujumbe sawasawa. Hali hii inatokea vilevile
katika Pepo ya Mabwege kati ya Josina na Kalenga. Katika Gamba la
Nyoka mwishoni, mwandishi anaamua kuingilia kati kuhakikisha kwamba kweli
tunaelewa sawasawa. Hatari za hali hii ni kwamba:
(a) riwaya hugeuka hotuba na kupoteza nguvu yake ya kutufanya sisi kuona na kusikia kwa namna ya pekee yale yanayojitokeza katika jamii.
(b) Huu ujumbe wa hotuba huhitilafiana na ujumbe unaotokana na vitendo vilivyoelezwa awali.
Tamati
Kazi ya msanii, kwa kuwa inagusa hisia zetu zote, ina uwezo
mkubwa wa kuleta mabadiliko makubwa katika urazini na msimamo wa wasomaji. Hivyo
wajibu wa mwandishi ni mkubwa. Inafurahisha kuona jinsi baadhi ya waandishi wa
riwaya walivyobeba wajibu huu; wamekazana kuakisi na kuelimisha jamii, na kwa
kiasi kikubwa wamefanikiwa.
Hata hivyo, mara nyingi ujumbe na dhamira zao vinaonekana zaidi
katika maelezo yao ya wazi mwandishi anapoingilia mwenyewe au kwa kupitia kwa
mhusika mmojawapo. Lengo la makala haya limekuwa ni kuonyesha kwamba ili aweze
kufanikisha zaidi dhamira anayoikusudia, mwandishi wa riwaya anapaswa kuzingatia
zaidi jinsi muundo mzima wa riwaya unavyochangia kutoa ujumbe wake; na iwapo ana
nia ya kuwakilisha umma katika maandishi yake yafaa ajichunguze zaidi
anaiandikia jamii kwa mtazamo gani na wa nani ili pasiwe na mgongano kati ya
ujumbe ulio wazi na ule uliofichika.
Tanbihi
1. Ngugi wa Thiong'o, (1986) Decolonising the Mind.
Currey, London, uk. 29 - 30, tafsiri yangu.
2. V. Lenin, (1981) On Literature and Art. Progress
Publishers, Moscow, uk. 226, tafsiri yangu.
3. D. Craig (ed) (1975) Marxists on Literature. Penguin,
Harmondsworth, uk. 14, tafsiri yangu.
4. E. Fischer, (1969) Art Against Ideology. Braziller,
New York, tafsiri yangu.
5. Ngugi, (1981) m.y.k. uk. 6 - 7, tafsiri yangu.
6. D. Brutus, (1978) Stubborn Hope. Heinemann, London,
uk. 79, tafsiri yangu.
7. C.S.L. Chachage, (1981) Sudiya Yohana. DUP, Dar es
Salaam, uk. 18.
8. C.G. Mung'ong'o (1980) Njozi Iliyopotea. TPH, Dar es
Salaam, uk. 28.
9. E. Kezilahabi (1979) Gamba la Nyoka. Eastern African
Publications, Arusha, uk. 150.
10. Kezilahabi, (1979) uk. 46.
11. Kezilahabi, (1979) uk. 58.
12. A.E. Musiba, (1981) Njama Continental Publishers, Dar
es Salaam, uk.
13. Musiba, k.h.j., uk. 129.
14. Musiba, k.h.j. uk. 170.
15. Musiba, k.h.j. Kwenye jalada la nyuma.
Bibliografia
Balisidya, N. (1981) Shida. DUP, Dar es Salaam.
Brutus, D. (1978) Stubborn Hope. Heinemann, London.
Craig, D., ed. (1978) Marxists on Literature. Penguin,
Harmonds worth.
Femia, J.V., (1981) Gramsci's Political Thought. O.U.R,
Oxford.
Fischer, E., (1969) Art Against Ideology. Braziller, New
York.
Gugelberger, G., (Mh.) (1985) Marxism and African
Literature. Currey, London.
Kavanagh, R.M., (1985) Theatre and Cultural Struggle in South
Africa. Zed, London.
Kezilahabi, E., (1979) Gamba laNyoka. Eastern African
Publications, Arusha.
Lenin V., (1982) On Literature and Art. Progress, Moscow.
Mung'ong'o, C.G., (1977) Mirathi ya Hatari, TPH, Dar es
Salaam.
(1980) Njozi Iliyopotea. TPH, Dar es Salaam.
Musiba, A.E. (1981 Njama. Continental, Dar es Salaam.
Mruma I., (1980) Nguzo ya Uhondo. TPH, Dar es Salaam.
Mwakyembe, H., (1981) Pepo ya Mabwege. Longmans, London.
Ngugi wa Thiong'o (1981) Writers in Politics. Heinemann,
London.
(1986) Decolonising the Mind. Currey. London.