MAENDELEO YA KISWAHILI TANGU UKOLONI HADI SASA
Lugha
ya Kiswahili ni kiungo muhimu sana katika maendeleo ya nchi za Afrika
Mashariki hasa katika uchumi, elimu, siasa, maendeleo ya Kiswahili,
utamaduni, biashara, n.k. Hivi sasa ziko juhudi za ushirikiano na
maelewano kwa jamii nzima ya Afrika Mashariki kupitia lugha ya
Kiswahili.
Soma zaidi ili ujue juhudi za kuiendeleza lugha hii.
Nchi
wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki yaani Burundi, Kenya,
Tanzania, Rwanda na Uganda ziko katika harakati za kuboresha muundo wa
jumuia hii kwa kuangalia upya majukumu yake baada ya kuvunjika kwa
Jumuia ya Afrika Mashariki takriban miaka 20 iliyopita. Idadi ya
wanachama imeongezeka kutoka nchi tatu za Kenya, Tanzania na Uganda na
kuwa nchi tano baada ya nchi za Rwanda na Burundi kujiunga na Jumuia
hii.
Mojawapo
ya mambo muhimu yaliyokubaliwa na viongozi wa nchi hizi yalihusu
suala zima la lugha ambalo litasaidia kurahisisha mawasiliano baina ya
wananchi wa nchi hizi kuanzia ngazi za chini kwa wananchi wa kawaida
hadi ngazi ya juu kwa viongozi wakuu. Lugha ya Kiswahili ilipewa nafasi
kubwa ya kuweza kutumika kama lugha ya mawasiliano miongoni mwa nchi
zote za Jumuia hii.
Itakumbukwa
kuwa wakati wa enzi ya ukoloni wa Uingereza ilikuwapo kamati ya lugha
ya nchi za Afrika Mashariki iliyojulikana kama Kamati ya Lugha
(Kiswahili) ya Afrika Mashariki. Lugha ya Kiswahili ilipewa nafasi kubwa
tangu mwaka 1930 wakati kamati ilipoanzishwa hadi mwaka 1964 kamati
ilipovunjika. Kamati ilipovunjika mwaka 1964 baada ya kila nchi kupata
uhuru wake, Tanzania ndiyo iliyokuwa mwenyekiti wa mwisho wa kamati na
hivyo kuendelea kutekeleza baadhi ya majukumu ya Kamati hadi leo chini
ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ambayo iko Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) imefanyiwa mabadiliko
ya muundo wake kiutendaji na sasa inafahamika kama Taasisi ya Taaluma za
Kiswahili (TATAKI). Taasisi ya TATAKI sasa imekuwa ni muunganiko wa
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili na Idara ya Kiswahili zote cha Chuo
Kikuu cha UDSM. Idara ya Kiswahili iliyokuwa inajishughulisha na
ufundishaji wa Kiswahili kwa wanachuo wa digrii ya kwanza, ya uzamili na
uzamivu.
Kamati ya Lugha (Kiswahili) ya Afrika Mashariki ilikuwa na utaratibu wa kukutana kwa zamu katika nchi wanachama kama ifuatavyo:
Dar es Salaam: 1930 – 1942
Nairobi 1943: - 1952
Makerere: 1953 – 1961
Dar es Salaam: 1962 – 1964.
Tangu
mwaka 1964 baadhi ya shughuli za kamati ziliendelea kusimamiwa na
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI). Kutokana na kila nchi kupata
uhuru wake, mfumo wa sera ya lugha uliachwa nchi wanachama jukumu la
kuendeleza lugha ya Kiswahili. Mwaka 1967 Tanzania ilianzisha Baraza la
Kiswahili la Taifa (Bakita) kwa lengo la kukuza, kuendeleza na kuratibu
maendeleo ya Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majukumu
ya Bakita yalitekelezwa vilivyo hasa suala la kusanifu lugha ya
Kiswahili na kutayarisha istilahi za masomo mbalimbali kama Kemia,
Fizikia, Hisabati, Utawala, Siasa, Elimu, n.k. Hatua ya pili ni
kutayarisha kamusi za istilahi hizi kazi ambayo imekamilishwa na TUKI.
Mwaka
1970 TUKI iliwekwa chini ya mamlaka ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
wakati kilipoanzishwa rasmi. Hadi sasa taasisi hii iko chini ya chuo
hicho.
Mwaka
1999 viongozi wa Jumuia ya Afrika Mashariki walikutana na kuona umuhimu
wa kuwa na chombo kimoja rasmi ambacho kazi zake ni kukuza, kuendeleza
na kuratibu Kiswahili katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Afrika
kwa jumla. Chombo hiki kinajulikana kama Kamisheni ya Lugha ya
Kiswahili Afrika Mashariki chenye malengo ya kuwezesha kukuza siasa,
uchumi, maendeleo ya jamii, elimu, utamaduni, sayansi na teknolojia
katika eneo la Afrika Mashariki.
Dira
ya Kamisheni hii ni kuwa chombo mahususi cha kukuza, kuratibu na
kuendeleza Kiswahili kwa ajili ya maendeleo ya uchumi, siasa, utamaduni,
elimu kwa nchi wanachama.
Makao Makuu wa Kamisheni hii yatakuwa Zanzibar na mipango ya kuwapata viongozi wa Kamisheni inaendelea.
Shabaha za Kamisheni:
1. Kuimarisha mawasiliano kitaifa, kikanda na kimataifa katika kukitumia Kiswahili.
2. Kukikuza Kiswahili kama lugha ya kanda kwa kuzingatia tunu kama usawa, uwiano, haki za binadamu na demokrasia.
3. Kuanzisha, kusaidia na kuhimiza maendeleo ya Kiswahili katika Jumuia ya Afrika Mashariki.
4. Kuhimiza ushirikiano katika utafiti na vituo vya elimu ya juu kwa mafunzo ya Kiswahili na utafiti.
5. Kuzisaidia nchi wanachama kutoa elimu ya juu ya Kiswahili kwa walimu na mawasiliano kwa jamii kwa jumla.
6.
Kufanya marekebisho ya mitalaa na kuongeza ujuzi katika masomo ya
fasihi na isimu kulingana na mahitaji ya jamii ya Afrika Mashariki.
7.
Kuendeleza ubora wa Kiswahili katika kuhuisha lugha ya Kiswahili na
programu za elimu. Mitalaa ihakikishe kuwa ufundishaji na utafiti katika
Kiswahili unafikia kiwango kinachokubalika.
8. Kuzisaidia nchi wanachama kwa maendeleo ya watu binafsi na uendeshaji wa asasi za Kiswahili.
9.
Kuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya kimataifa kuhusu Kiswahili na
kuziarifu nchi wanachama. Kuhimiza ubadilishanaji wa wafanyakazi na
wanafunzi miongoni mwa asasi za Kiswahili.
10.
Kuchunguza, kufuatilia, kuhuisha na kuhimiza maendeleo ya Kiswahili kwa
ajili ya upashanaji habari, mawasiliano, shughuli za kiteknolojia na
matumizi ya lugha.
11. Kuwezesha na kuratibu tafsiri kwa Kiswahili kwa nchi wanachama na vyombo vingine vya kimataifa.
Usanifishaji wa Kiswahili
Mojawapo
ya shughuli za Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki ni kusanifu maneno
mapya pamoja na kuoanisha maneno ya zamani ili yatumike kwa ajili ya
kuimarisha maelewano baina ya nchi zote za Jumuia ya Afrika Mashariki.
Kikwazo kilichokuwapo hapo awali ni kutoikuza lugha ya Kiswahili kwa
kiwango cha kimataifa kwa upande wa taaluma ya sayansi na kiteknolojia.
Bingwa na mtaalamu aliyebobea katika Kiswahili Profesa Ali Mazrui
aliwahi kusema kuwa sera ya elimu na ya lugha ya Kiswahili havikupewa
kipaumbele katika ukuzaji wa sayansi na teknolojia. Ukosefu wa istilahi
za Kiswahili katika sayansi na teknolojia umesababisha walimu na
wahadhiri kupata matatizo katika kuandika vitini na vitabu vya sayansi
kwa lugha ya Kiswahili.
Kihistoria
nchi za Kenya na Uganda zimetegemea sana istilahi zilizotayarishwa na
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), Taasisi ya Ukuzaji Mitalaa
(TIE), Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (IAE) na Baraza la Kiswahili la
Taifa (Bakita).
Hata
hivyo, katika ngazi ya vyuo vikuu, wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na vyuo vikuu vya Kenya, wamekuwa na mawasiliano ya karibu ya
kitaaluma baina yao kwa kubadilishana taaluma mbalimbali. Mfano mzuri
ni wakati UNESCO/SIDA walipofadhili semina kuhusu masuala ya
usanifishaji wa istilahi za Kiswahili mwaka 1989. Wanataaluma wengi
kutoka Kenya walihudhuria semina hii na huu ukawa ni mwanzo nzuri wa
ushirikiano katika kukuza lugha ya Kiswahili kwa kiwango cha vyuo vikuu.
Utayarishaji wa Istilahi
Inasemekana
kuwa watumiaji wa istilahi za Kiswahili ni kwa ajili ya wanataaluma na
si kwa watu wa kawaida. Kwa hiyo wataalamu wanaotaka kuandika vitabu au
vitini vya kufundishia masomo ya sayansi wanazo istilahi za kuwawezesha
kukamilisha azma zao. Wataweza kutumia istilahi zilizotayarishwa na
Bakita na kuchapishwa katika kitabu cha Istilahi za Kiswahili cha mwaka
2005 na machapisho mengine yanayoweza kupatikana Bakita na Tuki. Iko
mifano michache ya wanataaluma wa masomo ya Kemia na Hisabati waliowahi
kuandika miswada ya masomo hayo kwa Kiswahili katika kiwango cha elimu
ya kidato cha tano na sita wakitumia istilahi ambazo zimetayarishwa na
Bakita. Kwa bahati mbaya wachapishaji wa vitabu walishindwa kuchapisha
miswada ya vitabu hivyo kutokana na kutokuwapo kwa sera kamili ya lugha
ya Kiswahili katika shule za sekondari.
Bakita walitayarisha istilahi za aina mbalimbali kwa kutumia njia zifuatazo:
- Upatikanaji wa maneno kutoka katika lugha za kigeni hasa Kiingereza ambayo ni kwa mtindo wa kutohoa. Hii ina maana kuwa maneno ya kigeni yanaandikwa kwa mfumo wa tahajia ya Kiswahili kwa kuzingatia matamshi ya Kiswahili. Kwa mfano katika utohozi tunapata maneno kama:
Kiingereza Kiswahili
Atom Atomi
Adapter Adapta
Battery Betri
Speaker Spika
Transformer Transfoma, n.k.
Istilahi
hizi huandikwa kwa kutumia misingi ya Kiswahili inayozingatia misingi
ya mofolojia ya Kiswahili. Mojawapo wa misingi hiyo ni kwa kumalizia
neno kwa kutumia irabu isipokuwa maneno machache yasiyoishia na irabu
kama mathalan, takriban na hususan.
- Njia nyingine inayotumika ili kuwa istilahi za Kiswahili ni kwa kupata maneno kutokana na visawe mbalimbali vya Kiswahili. Kwa mfano:
Ship Meli
Capital Mtaji
Plans Mpango
Usawa Equality, n.k.
- Njia ya tatu ni kwa kukopa maneno kutoka katika lugha za asili badala ya kutoka katika lugha za kigeni kama Kiingereza, Kiarabu, Kireno , Kihindi, n.k.
Kwa mfano yako maneno ya kikabila yaliyochangia kupata istilahi za Kiswahili kama:
Ikulu (Kinyamwezi) = State House
Kitivo (Kipare) = Faculty
Mbuti (Kimasai) = Duodenum
Kisabeho (Kipemba) = Breakfast dish
Uloto (Kizaramo), = Bone marrow
Msigano ( Kiyao/Kihaya) = Inequality
Upepo nyiri ( Kipare/Kihaya) = Jet-stream
Ubigiaji = )Kibondei) = Reafforestation, n.k.
- Kuunganisha maneno mawili na kuunda neno moja jipya, (Compouding of words).
Kwa mfano:
Prehistory Historiakale
Labour force Nguvukazi
Appendix Kidoletumbo
Triangle Pembetatu
Back sight Kipimonyuma
Fungicide Kiuakuvu
Boar Nguruwedume
Saw Nguruwejike, n.k.
Hii
ni mifano michache ambayo imetumika katika kuongeza istilahi za
Kiswahili katika juhudi za kupata maneno mapya ya sayansi. Inawezekana
ziko njia nyingine ambazo wataalamu wetu wa Kiswahili watabuni ambayo
yatasaidia kukifanya Kiswahili kiweze kumudu maendeleo ya sayansi na
teknolojia. Jambo la msingi ni kwa serikali kutoa fedha za kutosha kwa
watafiti wa lugha ya Kiswahili kuweza kufanya utafiti wa kina katika
lahaja za Kiswahili kama Kiamu, Kingazija, Kitumbatu, Kihadimu, Kimvita,
n.k. pamoja na lugha zetu za asili ambazo ni hazina kubwa katika
ukuzaji wa Kiswahili.
Kwa
mujibu wa Sera ya Elimu ambayo imetoka hivi karibuni, upo mpango wa
muda mfupi, wa kati na muda mrefu wa kukiwezesha Kiswahili kuwa ni lugha
ya kufundishia katika mfumo mzima wa elimu kuanzia elimu ya msingi hadi
vyuo vikuu. Lengo ni kuhakikisha kuwa masuala ya sayansi na teknolojia
yanapata nafasi yake katika maendeleo yetu kwa kutumia Kiswahili.
Maandalizi yanayotakiwa kufanywa ni kama kuandika vitabu na vifaa
vingine vya kujifunzia na kufundishia na pale inaposhindikana kutafsiri
kutoka lugha za kigeni. Pia kuwaandaa walimu hata wale wa kigeni
watakaokuja kufundisha hapa nchini . Suala la msingi ni kwa viongozi
wetu kubadilika kifikra na kuona kuwa kukitumia Kiswahili si
kujidhalilisha bali ni kupiga hatua kimaendeleo katika sayansi na
teknolojia kwa taifa letu. Matumizi ya lugha za asili katika elimu ni
dhana inayokubalika kwa nchi nyingi duniani kama vile Kenya. Je, ni nini
mwelekeo wa Tanzania?