MFANO WA SOGA
KIFENGE NA BARUA KWENDA KWA BWANA MUNGU
Mtu
mmoja aliyejulikana kwa jina la Kifenge alikuwa maskini sana. Yeye na
familia yake waliishi kwa kuombaomba chakula, mavazi na mahitaji
mengine.
Siku moja wazo la kuomba msaada kutoka kwa Bwana Mungu lilimjia. Kifenge alienda dukani akanunua karatasi,bahasha na stempu akaamua kumwandikia Bwana Mungu barua.
Barua ilipofika posta wafanyakazi wa posta wakashangaa kuona barua inatakiwa kutumwa kwa Bwana Mungu. Wakaifungua
wakaisoma,wakamhurumia sana Bwana Kifenge. Wakaamua kuchanga fedha hadi
zikafika laki tano,wakazituma katika anwani iliyokuwa kwenye barua.
Baada
ya wiki moja fedha zikafika kwa Kifenge. Alifurahi sana na akamwambia
mke wake, "Mke wangu sasa dhiki imeisha. Tununue mahitaji yote, tukae,
tustarehe."
Mke
wake alifurahi sana akamuuliza mume wake, "Hivi siku zote tulikuwa wapi
mume wangu? Kumbe ndiyo maana watu wanatajirika lakini hawasemi kama Bwana Mungu huwa anawatumia fedha?"
Wakanunua magunia ya mchele, sukari, unga, mafuta na nguo na mahitaji mengine mpaka fedha zote zikaisha.
Fedha zilipoisha na mahitaji yakaisha wakaandika barua ingine kwa Bwana Mungu kuomba
msaada. Wafanyakazi wa posta walipoiona wakajua mwandishi ni yuleyule.
Wakamjibu, fedha ulizopata kama hukuweka mtaji, hakuna fedha tena.
Bwana
Kifenge alipoipata akazunguka kila mahali akitangaza kuwa atawashitaki
wafanyakazi wa posta kwa sababu wameiba fedha zake alizotumiwa na Bwana Mungu.
Hata hivyo wenye akili wakasema kweli wajinga ndio waliwao. "Hivi
Kifenge hakujua kuwa ule ulikuwa ni msaada uliotoka kwa watu wema ambao
alitakiwa kuutumia vizuri?"
Kelele za Kifenge hazikuzaa matunda, akarudia umaskini wake kama zamani.
Kutokana na hadithi ya Kifenge tunaona kuwa Soga ni hadithi fupi za kuchekesha au kukejeli. Mara nyingi wahusika wake ni watu wa kubuni, na huwa na kisa kimoja tu.