Misingi ya Uhakiki katika Fasihi ya Kiswahili
Fasihi, Uandishi na Uchapishaji (Dar Es Salaam University Press, 1993, 260 p.)
SEHEMU YA TATU: UHAKIKI |
14. Mwanamke ni Ibilisi?
R.D.K. Mekacha
Katika kuchanganua jinsi mwanamke alivyosawiriwa Mbughuni (1982)
anaainisha picha mbili za mwanamke zinazojitokeza katika riwaya. Kwanza lu picha
ya mwanamke kama kiumbe mharibifu, na pili ni picha ya mwanamke kama kiumbe
mwongofu. Katika picha ya uharibifu usawiri wa mwanamke unashabihishwa na wasifu
wa Hawaa (au Eva) katika masimulizi ya kibiblia ya dhambi ya asili, na katika
picha ya uongofu usawiri wake unashabihishwa na wasifu wa Maryam (au Maria) mama
wa Nabii Issa (Yesu Kristu). Katika picha ya mwanzo mwanamke anaiponza jamii kwa
kuipoteza pepo (paradiso), na katika picha ya pili mwanamke ni kiumbe wa kufugwa
katika ndoa. Matteru (1982) anaainisha picha tatu za mwanamke zinazobainika
katika fasihi simulizi: mwanamke kama mzazi, mwanamke kama chombo cha anasa ya
mwanamume, na mwanamke kama chombo au mali ya kumilikiwa. Kama mzazi dhima ya
mwanamke ni kuzaa watoto, kama chombo cha anasa dhima yake ni kumburudisha
mwanamume, na kama mali uamilifu wake ni kumilikiwa na kuwa zana ya kuzalishia
mali. Wahakiki wote hawa wanaafikiana kuwa katika picha zote hizo mwanamke
anajitokeza akiwa mtu duni akilinganishwa na mwanamume.
Azma ya makala haya mafupi ni kushadidia hoja hiyo kwa
kuchanganua mwanamke alivyosawiriwa katika nyimbo za kisasa za muziki wa dansi.
Nyimbo za aina hii hutawala sana matangazo ya redio - vyombo vya mawasiliano
ambavyo kwa makisio yetu vina nguvu sana katika jamii hii. Mahususi tutajibana
katika kuchanganua namna wasanii wa nyimbo hizo wanavyouonyesha udhalili wa
mwanamke kwa kumsawiri kama kiumbe mwenye uovu unaozidi ule wa Hawaa hata
ukamithilishwa na ule wa ibilisi. Tunatazamia kuonyesha kuwa sambamba na usawiri
huo mwanamume anajitokeza akiwa mbabe na mwadilifu. Tumeteua na kutumia nyimbo
chache kwa sababu tu ya maudhui yake.
Kama ilivyo katika kazi nyingine za sanaa mwanamke amesawiriwa
kwa namna mbalimbali katika nyimbo za kisasa za muziki wa dansi. Mwanamke ni
mchapakazi,1 ni mwenye busara na mshauri wa mumewe,2 ni
mnyonge na mwenye kumtegemea mume kupata mradi wake wa maisha,3 ni
chombo cha anasa cha kumburudisha mwanamume,4 ni fasiki na mwovu sawa
na ibilisi.
Hakuna mipaka ya wazi na bayana kati ya picha hizo za wasifu wa
mwanamke, bali huingiliana kwa namna ya mwendeleo unaoanzia kwenye zile nyimbo
zenye mwelekeo chanya hadi zile zenye mwelekeo hasi. Kwa makadirio yetu idadi
kubwa ya nyimbo hizi inaegemea kwenye mwelekeo hasi, na hata zile zinazomsawiri
mwanamke kwa mwelekeo chanya hatimaye huzishawishi hadhira kuhitimisha kuwa
mwanamke ni kiumbe dhalili mbele ya mwanamume hasa kimaadili.
Motifu ya usawiri wa mwanamke kama ibilisi ni utendekaji wa kosa
au jambo lolote linalosababisha madhara kwa mtu mmoja au jamii kwa jumla. Ili
kuikamilisha motifu ya aina hii watunzi wa nyimbo hizo huumba chanzo
kinachosababisha tendo ambalo hatimaye hubainika kuwa kosa, huumba pia mbinu
zitumiwazo kukamilisha tendo hilo, malengo ambayo ndiyo huwa tendo limedhamiriwa
kuyakidhi na matokeo, taathira au madhara ya tendo hilo.
Mojawapo ya chanzo cha utendekaji wa kosa hilo ni udanganyifu.
Katika masimulizi ya kibiblia ya dhambi ya asili ambayo kwa kiasi hushabihiana
na picha hii, mwanamke (Hawaa) alishawishiwa na Ibilisi kuchuma na kula tunda
lililokuwa limekatazwa.5 Katika idadi kubwa ya nyimbo za kisasa za
muziki wa dansi pia mwanamke hushawishiwa. Lakini hapa vishawishi aghalabu huwa
tamaa ya maisha ya starehe. Katika kukidhi haja hiyo mwanamke anashawishika ama
kuacha masomo, au kumwacha mchumba wake, au kuwatelekeza wazazi wake huko
vijijini na kukimbilia mjini.6
Udanganyifu kama chanzo cha kosa hutuelekeza katika kuhitimisha
kuwa mwanamke anastahili sehemu tu ya lawama kwa kosa lililotendeka. Sehemu
nyingine ya lawama inabebwa na vile vishawishi ikiwa ni shetani (kama ilivyokuwa
kwa Hawaa), mali, starehe, au ulaghai wa mwanamume. Lakini pamoja na kugawana
lawama hizo, hatimaye nyimbo hizo hutuongoza katika kumwona mwanamke kama kiumbe
dhaifu, asiyeweza kuhimili vishawishi, na ambaye kwake yote yang'aayo ni
dhahabu. Kwa hiyo madhara yatokeayo hatimaye huwa ni kwa sababu ya udhaifu wake
(mwanamke).
Chanzo kingine cha tukio liletalo madhara ni dhiki. Dhiki
aliyonayo mwanamke humsukuma kutafuta njia za kukidhi mahitaji yake, na katika
kufanya hivyo husababisha madhara au kosa kutendeka.7 Katika chanzo
cha namna hii pia inawezekana kuhoji kuwa mwanamke ni mhasirika tu va mahitaji
na hivyo lawama anayostahili kubeba ni ndogo. Aidha hapa ile hali ya udhaifu
haijitokezi, bali tunamwona mwanamke kama jasiri na mwenye kuthubutu kuchukua
hatua za kujiondoa kwenye madhila ya unyonge na umaskini. Lakini si aghalabu
hali hiyo kusisitizwa katika nyimbo hizo. Badala yake linalosisitizwa na watunzi
ni mbinu aitumiayo (mwanamke) kukidhi haja hiyo na madhara ayasababishayo kwa
mwanamume, na hasa kwake mwenyewe.
Katika idadi kubwa ya nyimbo hizo, hata hivyo, chanzo cha
matendo au matukio yaletayo madhara si vishawishi vya Ibilisi au tamaa, wala si
msukumo wa kukidhi mahitaji ili kukabili dhiki inayomzinga, bali wivu
unaochochea nia ya kuharibu "maisha bora" ya ndoa za wenzake. Hapa ubaya wa
mwanamke hukiuka ule wa Hawaa katika masimulizi ya dhambi ya asili na
kushabihiana na ule wa Ibilisi. Mtunzi wa wimbo uitwao "Mwanameka" anahitimisha
kisa cha mwanamke huyo kwa kusema:
Hivi sasa nimeshaamini,
Ibilisi wa mtu ni mtu.
Yaani Ibilisi wa Musa (mwanamume) ni Mwanameka (mwanamke). Siyo
kwamba kisa hicho kimemfanya atambue hivyo, bali kimethibitisha jambo ambalo
alikwishahisi au kudokezwa. Ndiyo maana asema kuwa "sasa nimeshaamini."
Mbinu zitumiwazo na mwanamke kukidhi malengo yake, ikiwa ni
starehe, mali, au uharibifu wa ndoa, ni mbili. Kwanza ni ahadi ya ndoa; ahadi
ambayo aghalabu huwa haitimizwi. Msichana aitwaye Mwanaidi katika wimbo wenye
jina hilohilo aliahidi kuolewa na mtunzi. Naye mtunzi akatumia mali yake yote
ikiwa ni pamoja na kuuza shamba na nyumba ili kumridhisha "mchumba" wake huyo.
Lakini hatimaye mtunzi akafilisika na Mwanaidi akamgeuka na kumkataa.
Mbinu ya pili ni mapenzi na uzinzi. Mwanameka katika wimbo
tulioutaja ni msichana aliyetumia uzuri wake, vipodozi, na mbwembwe ambazo
zilimzuzua Musa hata zikamghilibu akili licha ya kujitahidi kuvumilia.
Alipopotea njia na kumtaka mapenzi Mwanameka, basi naye akayatumia hayo mapenzi
kumfanya Musa asahau kwake, jambo ambalo lilisababisha ndoa yake kuvunjika.
Mtunzi analieleza hilo ifuatavyo:
Ukajikuta mrembo
Ukazidisha na mapambo
Kipini wanja kwa poda
Na mwendo wako maringoMusa macho yake yameona
Na moyo ukaanza sononekaUkabadili na njia
Lazima upite kwa Musa
Ukenda sokoni kwa MusaMusa amevumilia
Mwisho kapotea njia
Kakusimamisha bila kutambua
Akazungumza neno la mapenziUkakubali bila kusita
Uliyotaka yamekuwa
Kazi ikawa ni moja
Ni mapenzi moto moto
Lakini mara tu baada ya ndoa ya Musa kuvunjika Mwanameka pia
akavunja mapenzi yake na Musa.
Mbinu hizi mbili, kwa kweli, ni sura mbili za sarafu moja. Zote
zinaelekea katika kuhitimisha kuwa mbinu aitumiayo mwanamke kuleta madhara ni
ile jinsi yake ya kike. Hii ni jinsi ambayo pia inahusika na dhima muhimu ya
kuiendeleza jamii. Kwani mwanamke ni mzazi na mlezi wa kizazi cha kesho, dhima
ambayo wasanii hawa huonyesha kuiheshimu sana.8 Lakini hapa
inashushwa hadhi na kuonekana kama silaha kuu au ya pekee ya mwanamke kufanyia
hila zake za kiovu. Pengine mtazamo huu unaakisi ukweli: (i) kuwa bado jamii
yetu inaiona dhima ya msingi ya mwanamke kuwa ni kuzaa watoto (Matteru
1982);9 (ii) kuwa bado jamii yetu inauona wajibu wa kuzaa na kulea
kama ni wajibu binafsi hasa kwa mwanamke na wala sio wajibu wa jamii
nzima;10 na (iii) kuwa mwanamke katika jamii yetu harithi wala
kumiliki chochote isipokuwa uwezo wake wa kuzaa - na kama akizaa - watoto wake.
Mbinu hizi hutumika kukidhi malengo tuliyoyadokeza hapo juu. -
Mojawapo ni kupata "maisha bora" hasa katika ndoa. Kwa kweli nyimbo nyingi
humwona mwanamke kama "mateka wa saikolojia ya unyonge wake" (Mohammed 1980).
Wasanii hudhani kuwa mwanamke mwenyewe huitazama ndoa kama mwokozi. Kwamba
anapokuwa ameolewa ndiyo anakuwa amekombolewa kutoka kwenye majanga na madhila
ya kilimwengu, na anapokuwa ameachika hujuta kwa kuwa anakuwa ameadhibiwa kwa
kutumbukizwa tena katika majanga ya "dunia hadaa ulimwengu shujaa." Hapa
itakumbukwa kuwa wahusika wanawake takriban wote wa nyimbo hizi ni wale
walioathiri au kuathiriwa na kuvunjika kwa ndoa, au wale ambao hawajaolewa. Si
aghalabu kukutana na mhusika ambaye ndoa yake ni imara au ni wa kijijini.
Hii ni kusema kuwa kuolewa, hasa na mume mwenye mali, ndiyo
tamaa ya mwanamke, kwani huko ataishi raha mustarehe. Hata hivyo, kadiri nyimbo
nyingi zinavyoonyesha mwanamke anapofanikiwa kuolewa na mume mwenye mali
hatimaye hugundua kuwa maisha ya ndoa hiyo siyo raha mustarehe. Ama mume
humsahau akamgeuza kuwa pambo au mlinzi wa nyumba akamwacha aghalabu akiteseka
na huku yeye (mume) akiendelea kutumbua raha,11 au ndoa huvunjika, au
mali kutoweka na mume akafilisika.
Lengo jingine ambalo mbinu hizo hutumika kulikidhi ni tamaa ya
mali au utajiri. Mwanamke humlaghai mwanamume, hasa mwenye utajiri, kwa mapenzi
"motomoto" au ahadi za kuolewa naye ili aweze kuchuma mali toka kwake. Aghalabu
mwanamke huwa hampendi mwanamume huyo, lakini mwanamume anakuwa anampenda
mwanamke. Naye mwanamke hutumia hali hiyo kujineemesha, na mara nyingi huwa hata
siyo kujitajirisha bali kujisheheneza mavazi na vipodozi tu.12
Anapokuwa amekidhi haja yake, au anapobaini kuwa hawezi tena kuambua chochote
kwa mwanamume huyo humpa kisogo akamsahau.
Lengo jingine huwa ni kutibua ndoa au uchumba wa watu wengine.
Wasanii hawa wala hawajali kutueleza mwanamke ananufaika vipi kwa kufanya hivyo.
Kinyume chake hujaribu kutuaminisha kuwa analolifanya mwanamke amelidhamiria.
Tazama maneno haya kutoka wimbo wa "Mwanameka"
Uliposikia ee ee
Kwamba Musa ameoa
Kaoa mke wa ndoa
Musa sasa katulia
Uhuni kaacha kando
Ukatumia kila uwezo,
Kuyabadili mawazo ya Musa
(Msisitizo umeongezwa)
Tumeelezwa katika beti tulizozidondoa mwanzoni jinsi Musa
alivyovumilia. Lakini hatimaye tunaambiwa akapotea njia akamsimamisha Mwanameka
"bila kutambua" na kuzungumza neno la mapenzi. Naye Mwanameka kusikia hivyo
"akakubali bila kusita" kwani alilolitaka ndiyo hilo nalo likawa.
Matokeo ya matendo hayo ya mwanamke ni madhara. Madhara hayo
huathiri mwanamume na mwanamke. Baadhi ya nyimbo huonyesha kuwa mwanamume
kahasirika na mwanamke kanufaika. Katika wimbo "Mwanaidi" kwa mfano, mwanamke
alinufaika akapata kujineemesha yeye na ukoo wake na mwanamume akahasirika kwani
alifilisika na hatimaye hakuwa na la kufanya. Tukichunguza zaidi tunabaini kuwa
kilio cha msanii ni kuwa mwanamume ni mwaminifu na mkweli wakati mwanamke ni
mwongo na mwenye kujinufaisha kwa hila. Hadhira inashawishiwa imhurumie
mwanamume na imbeze mwanamke.
Katika idadi kubwa zaidi ya nyimbo za aina hii wasanii hufanya
juhudi ya makusudi kabisa kuonyesha kuwa ingawa mwanamume amehasirika pia,
lakini mwanamke ndiye amehasirika zaidi. Mwanamke aitwaye Edita katika wimbo
uitwao "Kipenzi Edita", kwa mfano, anapewa talaka kwa kufanya "mapenzi ya
pembeni."13 Mwanamume anamkosa mke, lakini kinachosisitizwa ni kuwa
mwanamke ameadhibiwa kwa kupewa talaka (rejea maelezo hapo juu).
Katika baadhi ya nyimbo wasanii hujitahidi sana kuonyesha kuwa
ingawa mwanamume amehasirika, lakini pia amenufaika walau kwa kiasi kidogo.
Hivyo ndivyo inavyotubainikia katika wimbo wa "Mwanameka." Mwanamke
alimsababishia mwanamume hasara maradufu: "kakosa mwana" (msingi wa ndoa) na
"maji ya moto" (mapenzi). Uteuzi wa maneno katika sehemu ya mwisho ya wimbo huo,
hata hivyo, umefanywa makusudi kuonyesha kuwa mwanamume amenufaika au ana
liwazo. Nalo ni funzo. Tazama ubeti huu:
Bwana Musa hatakusahau mpaka kufa
Tena amekwisha apa
Mambo ya upuuzi hataki tena
Kishaumwa na nyoka
Akiona unyasi anastuka.
Lakini mwanamke hana funzo wala haliwazwi. Badala yake
anashutumiwa na kulaaniwa kwa kufanya mkasa, madhambi, na mambo ya kusikitisha.
Msanii asema:
Kweli Mwanameka
Umefanya madhambi makubwa
Mambo uliyomfanyia Bwana Musa
Yanasikitisha
Mwanameka mkasa uliofanya ni wa mwaka.
Kwa sababu ya mkasa aliofanya, tunaambiwa kuwa watu wanamdharau,
wanamkashifu na kumlaani:
Mwanameka umetuachia hadithi mtaani
Kila mmoja anashangazwa na vitendo vyako
Kila mtu anasimulia mambo yako
Ati watu wanasema... mgombanishi
Kweli watu wanasema... mhuni
Ati watu wanasema... mdanganyifu
Kwa jumla mwanamke amekuwa mhasirika mkuu wa maovu yake
mwenyewe. Kwa hiyo wakati hadhira inashawishiwa imsikitikie mwanamume, inatakiwa
pia imlaani na kumshutumu sana mwanamke.
Mambo mawili yanajitokeza katika uchanganuzi huu. Kwanza ni
kwamba mwanamke ni mwenye tamaa, mwenye wivu, dhaifu na mwanzilishi wa matatizo
katika jamii. Mwanamke hutumia jinsi yake ya kike, tena kwa hila, ili kutenda
mambo ambayo huleta madhara. Katika kufanya hivyo mwanamke humshawishi mwanamume
na hata hutokea akamshurutisha kwa kumghilibu akili, akamshirikisha katika
kutenda maovu. Mwanamke hupania ama kujinufaisha au kutibua maisha bora ya ndoa
za wenzie. Madhara yatokanayo na matendo ya mwanamke humdhuru pia mwanamume,
lakini mhasirika mkuu wa maovu hayo ni mwanamke mwenyewe.
Pili ni kwamba mwanamume hahusiani na msingi wa matendo hayo
maovu. Yeye hushawishiwa tu au wakati mwingine kwa hila akashurutishwa kushiriki
katika maovu hayo. Yeye hana hatia. Lakini hudhurika kwa madhara yaletelezwayo
na maovu ya mwanamke. Yeye, hata hivyo, aweza kuliwazwa kwa kunufaika walau
kidogo, hata kama liwazo lenyewe ni kuhurumiwa tu.
Kwa hiyo hatimaye inabainika kuwa mwanamke ni mwovu, mwanamume
ni mwongofu; mwanamke ni fasiki, mwanamume ni mwadilifu; mwanamke ni ibilisi,
mwanamume ni malaika!
Ni vigumu kuamini kuwa wasanii wa nyimbo hizi wanaamini kwa
dhati kuwa hii ni picha mojawapo ya mwanamke, Nyimbo hizi, kama kazi nyingine za
sanaa, hueleza tu jinsi uyakini wa maisha unavyoakisiwa akilini mwa msanii.
Lakini pia msanii huwa na uhuru wa kusawiri uakisi huo kisanaa, aweza ama
kulitia jambo chuku, au kulidhalilisha ili kukidhi malengo yake ya kisanaa.
Licha ya matakwa yake binafsi, msanii pia hudhaminiwa na nguvu mbalimbali za
kijamii ambazo zinamzinga. Mojawapo, au zaidi ya moja, ya mambo hayo yaweza
kusababisha usawiri wa aina fulani kwa kundi fulani la watu katika jamii.
Usawiri huu wa mwanamke, kwa maoni yetu, unatokana na nia ya
wasanii ya kumtaka mwanamke, hasa aishiye mjini na ambaye
hajaolewa,14 aendelee kukiri nguvu za mfumo wa mahusiano ya kijamii
unaotawala hivi sasa. Asiwe na tamaa ya maisha bora na ya starehe, aepuke au
ahimili vishawishi mbalimbali, na aheshimu pingu za maisha katika ndoa
yake na zile za wenzake. Au la atasababisha madhara sawa na asababishayo
Ibilisi, tena kwake yeye mwenyewe. Wasanii wanajaribu kumwadibu mwanamke kwa
kubeza tabia zinazokiuka mahusiano yaliyopo. Hivyo chimbuko la mtazamo huu wa
mwanamke ni hofu ya wasanii kuhusu madhara yatakayotokea endapo mwanamke
atakiuka mwenendo ambao wasanii hao wanadhani ndiyo murua katika jamii. Ikiwa
hofu yao yaweza kutetewa au la ni hoja inayodai mjadala ulio nje ya mipaka finyu
ya makala haya.
Tanbihi
1. Kwa mfano katika wimbo uitwao "Kwini Lusi" wa Kimulimuli
Jazzband.
2. Katika wimbo uitwao "Mabruki" wa Marquis Orchestra.
3. Kwa mfano katika nyimbo "Ndoa ya Mateso" wa Dar Intemational
Orchestra; "Mume Wangu" wa Makassy Orchestra, na nyingine.
4. Hii ndiyo picha inayobainika katika nyimbo nyingi sana ambapo
mwanamke kaltwa tausi, tunda, nyota, mwezi, ua, na mengine mengi. Mohammed
(1980) ameiita picha ya "sili - sikogi - silali".
5. Masimulizi haya yamejitokeza vizuri sana Katika Utenzi wa
Adamu na Hawa uliotungwa na AbdilatifAbdalla. Rejea pia makala ya Mbughuni
6. Msichana katika wimbo "Mume Wangu", kwa mfano, anashawishika
kupuuza ushauri wa wazazi na kukatisha masomo yake kwa kutamani raha za "nyumba
kubwa kama Kilimanjaro, pesa na gari" alizoahidiwa na mwanamume.
7. Mwanamke aitwae Mwanaidi katika wimbo wenye jina hilohilo wa
Or- chestra Toma Toma anasukumwa na mahitaji ya kupata mali "ili kuneemesha ukoo
wake", na msukumo huo ndio unaomwingiza katika kutenda kosa.
8. Wahusika takriban wote wa nyimbo hizo huwa ama wasichana wa
mjini ambao hawajaolewa au wale ambao ndoa zao zinayumba. Ni nadra sana
kusawiriwa mwanamke mzazi isipokuwa pale anapolalamika kuwa kalemewa na mzigo wa
kulea watoto. Aidha ni nadra sana kusawiriwa mwanamke anayeheshimu pingu
za ndoa yake na za mwenzake.
9. Kwa hiyo mwanamke asiyezaa huonekana kuwa duni zaidi au asiye
na thamani. Katika wimbo mmoja wa Juwata Jazz Band, mwanamke anamlalamikia
mumewe aliyemfukuza akisema yeye "mwanamke gani asiyezaa".
10. Katika wimbo uitwao "Ndoa ya Mateso", kwa mfano, mwanamke
analalamika hivi:
Niulizieni enyi walimwengu
Huyu mwanamume sijui mume gani
Ananipa mateso huku ugenini
Na mimi nina watoto sijui ni tabu gani
Na mimi nina watoto sijui ni tabu gani.
11. Katika wimbo uitwao "Mume Wangu", kwa mfano, mwanamke
analalamika kuwa hamwoni mume nyumbani, anapika "ubwabwa, chai, chapati" lakini
vinachacha. Wenzake wote wametulia na waume zao, naye alitaka mumewe atulie ili
wazae, lakini bahati imemtoka. Katika wimbo "Ndoa ya Mateso" inasemekana kuwa
mume anakula "makuku ya kukaanga" lakini yeye mwanamke ashindia "mkate mkavu".
12. Kwa mfano, mtunzi wa wimbo uitwao "Esta" wa Orchestra
Marquis du Zaire anadai kuwa msichana Esta "anaponzwa na ujana kwa tamaa ya
mavazi" kwani kila wanapokutana hudai fedha za matumizi.
13. Katika wimbo huo ulioimbwa na Mlimani Park Orchestra kitu
kinachomfanya mtunzi amtilie mashaka Edita awali ya yote ni kutokumkuta nyumbani
arudipo kazini. Kwani mahali pa mwanamke aliyeolewa ni nyumbani. Kuhusu hili
rejea Mbunguni (1982).
14. Kwani kama tulivyoeleza juu (tazama maelezo Na. 8) wahusika
takriban wote ni wale ambao hawajaolewa na waishio mijini.
Marejeo
Abdalla, A. (1971) Utenzi wa Maisha ya Nabii Adamu na
Hawaa. Oxford University Press, Nairobi.
Matteru, M.L.B. (1982) "The Image of the Woman in Tanzania Oral
Literature: A Survey" katika Kiswahili, TUKI, Dar es Salaam, Juzuu 49/2.
Mbughuni, P. (1982) "The Image ofWoman in Kiswahili Prose
Fiction" katika Kiswahili, TUKI, Dar es Salaam Juzuu 49/1.
Mohamed, S.A. (1980) "Mwanamke katika Ushairi wa Kiswahili"
makala yasiyochapishwa, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.