SWALI: Jadili mtazamo wa Massamba na wenzake kuhusiana na aina za virai ukilinganisha na mtazamno wa wanazuoni wengine.
SWALI:
Jadili mtazamo wa Massamba na wenzake kuhusiana na aina za
virai ukilinganisha na mtazamno
wa wanazuoni wengine.
UTANGULIZI
Kirai
ni dhana pana na yenye mkanganyiko mkubwa kiasi cha kuwaibua wanazuoni
mbalimbali ambao kila mmoja amejitahidi kwa uwezo na uelewa wake kufafanua
dhana hii. Kwa mahitaji ya swali hili tutatalii mitazamo ya wataalamu
mbalimbali akiwemo Massamba na wenzake katika kufasili dhana hii ya kirai na
aina za virai.
KIINI
FASILI
YA KIRAI
Kwa
kuanza na tuangalie fasili ya kirai kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali
Massamba
na wenzake (2009), wanasema kuwa kirai ni kipashio cha kimuundo chenye zaidi ya
neno moja na ambacho hakina muundo wa kiima kiarifu.
Fasili
hii ya Massamba na wenzake inaelekea kutuaminisha kuwa kirai ni lazima kiwe na
Zaidi ya neno moja. Swali la kujiuliza hapa ni je, neno kuu linalotambulisha
aina ya kirai likisimama peke yake haliwakilishi aina husika ya kirai? Ukweli
ni kwamba kila neno kuu la kirai lisimamapo pekee huwakilisha aina husika ya kirai
hata bila ya kuambatana na kijalizo chochote cha kirai.
Mfano:
Kirai Nomino
Kirai
hiki chaweza kuwa nomino pekee au nomino na kijalizo.
(a)
Mtoto mzuri
KN
(b)
Mtoto
KN
Kihore
na wenzake (2007), wanasema kuwa kirai ni kipashio cha kimuundo chenye neno
moja au zaidi lakini bila uhusiano wa kiima kiarifu. Kwao mahusiano ya kiima
kiarifu ni yale yanayoonesha anayetenda jambo na tendo linalotendwa, anayetenda
jambo ni kiima na tendo linalotendwa ni kiarifu.
Mfano:
mtu mnene/ anachoma nyama.
Kiima kiarifu
TUKI
(2011), wanadai kuwa kirai ni kipashio chenye zaidi ya neno moja lakini ambacho
hakina muundo wa kiima kiarifu.Maana hii ya TUKI inawiana na ile ya Massamba na
wenzake.
Mdee,
J.S (2007) anasema kuwa kirai ni neno au kifungu cha maneno chenye neno kuu
moja. Kwa mujibu wa Mdee kirai kinaweza kuwa neno moja au kifungu cha maneno.
Uhusiano kati ya neno kuu na maneno mengine (vijalizo) ndio hutambulisha na
kutofautisha aina ya kirai.
Fasili
zote hapo juu zinashadadia mambo ya msingi kuwa kwanza kirai sharti kijikite
katika mahusiano baina ya maneno ambapo huwa kuna neno kuu moja linalotawala
aina ya kirai, pili neno kuu la kirai huweza kusimama pekee au kuambatana na
kijalizo kimoja au zaidi. Hivyo basi kirai kinaweza kusimama kama neno moja au
zaidi iwapo tu kuna neno kuu linalotawala na kumiliki maneno mengine.
AINA
ZA VIRAI
Kuhusu
aina za virai wataalamu pia wametofautiana, tofauti zao zipo hasa katika aina
na idadi lakini pia matumizi ya istilahi zao.
Massamba
na wenzake (2009) wanatambua aina tano za virai ambazo ni:
· Virai – nomino
· Virai – vitenzi
· Virai –
vivumishi
· Virai – vielezi
· Virai –
viunganishi
Zabron,
T.P (2017) yeye anatambua na kutetea aina sita za virai ambazo ni:
· Kirai – nomino
· Kirai – kitenzi
· Kirai –
kivumishi
· Kirai – kielezi
· Kirai –
kihusishi
· Kirai –
kibainishi
Naye
Mdee, J.S (2007) anatambua aina tano za virai ambazo ni kama zifuatazo:
· Kirai – nomino
· Kirai – kitenzi
· Kirai –
kivumishi
· Kirai – kielezi
· Kirai –
kihusishi
Ukichunguza
kwa makini miongoni mwa wanazuoni waliorejelewa katika kazi hii utabaini kuwa
kuna mfanano juu ya idadi kati ya Massamba na Mdee isipokuwa Zabron ambaye
anatambua aina sita. Baada ya uainishaji huo hapa chini tutaonesha tofauti
baina yao kwa kurejelea aina wanazotofautiana na misingi ya utofauti huo.
TOFAUTI ZA AINA ZA VIRAI
Kwa kuanza na kundi la Massamba na wenzake, wao
hawatambui kirai kihusishi badala
yake wanatambua kirai kiunganishi. Kiunganishi
kinaelezwa kuwa ni neno linalounganisha pande mbili zenye hadhi sawa kisarufi. Msingi
wa tofauti hii ni kutokana na ukweli kwamba maneno yanayotumika kama kiunganishi ndiyo pia hutumika kama kihusishi.
Maneno hayo ni kama vile:
Ingawa, Na, Kwa kuwa, Bila, Pasipo, Sembuse, Lakini,
Mfano:
Baba alifika ingawa
mama hakumuona
Shule imejengwa na
mafundi wameondoka
Wanafunzi walifeli kwa kuwa walimu hawakuwafundisha ipasavyo
Kwa upande wa Mdee, J.S (2007) na Zabron, T.P (2017)
wanatambua kirai kihusishi kama aina moja wapo ya virai na
hawatambui kirai kiunganishi. Mdee,
(ametajwa) anasema kirai kihusishi ni
kirai ambacho neno kuu ni kihusishi na Kihusishi
ni neno linaloonesha uhusiano baina ya pande mbili zenye hadhi tofauti
kisarufi.
Mifano ya maneno yaundayo kirai kihusishi ni kama
vile:
Kwa, ya, na, au
katika
Mfano:
- Alienda kwa
miguu
- Atakuja kwa
amri yako
- Anasoma na
mama
- Amelala katika
chumba
Kwa
upande mwingine Zabron, T.P (2017) yeye pamoja na kutambua kirai kivumishi kama wengine pia ameongeza aina moja zaidi
ijulikanayo kama kirai kibainishi (KB).
Anafafanua zaidi kuwa KB ni kirai
ambacho neno kuu ni kibainishi.
Vivumishi vibainishi vinaundwa na maneno kama vile: wawili, changu, kile, wote, hawa au wangu.
Mfano:
- Wanafunzi wale
pale
- Kitabu
hiki
- Wachezaji wote
hawa
Wapo
wanaoona kuwa aina hiyo ya kirai ni sehemu tu ya kirai kivumishi na pengine ndio sababu ya kutoainisha kama aina ya
kirai inayojitegemea.
HITIMISHO
Kwa
ujumla dhana ya kirai ni pana na yenye utatanishi mkubwa usioweza kumalizwa kwa
urahisi. Ikumbukwe kuwa dhana hii inaukilia zaidi misingi ya kisarufi ya umiliki na utawala wa kategoria za
maneno ambapo maneno makuu humiliki na kutawala maneno mengine katika msululu
wa kategoria za maneno. Watangulizi katika taaluma hii walianza kwa kuainisha
aina tano za maneno makuu ambazo ndizo zilizotumika kama kigezo kikuu cha
kuamulia aina ya kirai. Hivi leo mitazamo inazidi kuibuka kutokana na mwamko wa
wanazuoni wa kisasa katika kushughulikia dhana hii. Hata kazi hii itabaki kuwa
kwego ya kuendelezea mpando wa kitaaluma katika kuifikia kweli ilipo.
MAREJELEO:
Massamba
D.P.B na wenzake (2009) Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA): Sekondari
na vyuo, TUKI, Dar es salaam.
Mdee,
J.S (2007) Sarufi ya Kiswahili: Sekondari na Vyuo, DUP, Dar es Salaam.
Kihore
Y.M na wenzake (2007) Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA): Sekondari na
Vyuo, TUKI, Dar es salaam.
TUKI
(2011) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI,
Dar es salaam.
Zabron,
T.P (2017) Miundo Msingi ya Sarufi ya Kiswahili. Karljamer Publishers Ltd, DSM.