WANAFASIHI MBALIMBALI
Wanafasihi
- PENINA MUHANDO
- EBRAHIM HUSSEIN
- MWALIMU J. K. NYERERE
- SAID AHMED MOHAMED
- MOHAMED SAID ABDULLA
- KALUTA AMRI ABEDI
1. PENINA MUHANDO
Penina
Muhando alizaliwa tarehe 3 mwezi wa machi mwaka 1948, katika wilaya ya Kilosa
mkoani Morogoro nchini Tanzania. Alisoma katika shule mbalimbali za Tanzania na
baadaye alijiunga na masomo ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
kusomea sanaa za maonesho. Baada ya kumaliza masomo aliajiriwa hapo hapo Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo alifanya kazi ya kusomesha masomo ya Sanaa za
maonyesho. Vile vile aliandika na kuigiza tamthiliya. Aidha mwandishi huyu
baada ya kuolewa na Bwana Mlama alibadili jina na kuitwa Penina Mlama. Hata
hivyo, katika kazi zake mbalimbali ameendelea kutumia jina la Penina Muhando.
Mwandishi
huyu ambaye kwa sasa amerudi tena Chuo Kikuu cha Dar es salam kusomesha baada
ya kuwa amepumzika kwa muda kutokana na kutingwa na majukumu ya ukurugenzi
katika asasi zinazojishughulisha na masuala ya wanawake. Baadhi ya asasi hizo
na mashirika hayo yasiyokuwa ya kiserikali aliyoyafanyia kazi ni Foundation for
African Women Educationalist (FAWE), shirika lenye makao makuu jijini Nairobi,
Kenya, na pia asasi isiyo ya kiserikali iitwayo CAMFED yenye makao yake makuu
jijini Dar es salaam, Tanzania.
Penina
Muhando ameandika kazi mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza zote zikiwa
na mchango mkubwa kwenye fasihi andishi hususani kwenye utanzu wa tamthiliya.
Baadhi ya kazi hizo ni;
1. Hatia
(EAPH 1972)
2. Tambueni
Haki Zetu (TPH 1973)
3. Heshima
yangu (EALB 1974)
4. Pambo
(Foundation Books 1975)
5. Modern
African Theatre with special Emphasis on East Africa
(1975)
6. Talaka
Si Mke Wangu (EAPH 1976)
7. Nguzo
Mama
(DUP 1982)
8. Lina
Ubani (DUP 1984)
9. The
Challenge to the African Writers Today (1990)
10. The
Popular Theatre In Africa (1991).
Penina Muhando na Sanaa (Thieta)
ya Umma
Sanaa
(thieta) ya Umma ni aina ya sanaa za maonyesho au maigizo yaliyofanywa moja kwa
moja na wanajamii wa eneo fulani wakishirikiana na wataalamu wa sanaa kwa lengo
la kuyaibua, kuyaeleza na kuyatolea suluhisho matatizo ya watu wa eneo husika.
Muhando
(1991), katika kitabu chake kiitwacho Culture and Develeopnment: The popular
Theatre Apprach in Africa, anaieleza vizuri dhana ya “Thieta ya Umma” au
sanaa kwa maendeleo ya jamii. Mhando anaitaja miaka ya 1970 kama nyakati za
mwanzo katika vuguvugu la “Theata ya Umma” kwa nchi nyingi za Afrika. Majaribio
kadhaa yalifanyika yaliyokuwa na lengo la kuitambuliisha dhana hii ya Thieta ya
Umma kwa wanajamii. Kwa mfano nchini Kenya dhana ya Thieta ya Umma ilijulikana
sana kwa jina la “Thieta ya Ukombozi”. Maigizo mengi ya namna hii yalizungumzia
sana harakati za ukombozi wa kifikra, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa kwa
mwafrika dhidi ya utawala wa kikoloni, kwa sababu hii ya msingi Wakenya wengi
walipenda kuiita aina hii ya sanaa ya maonyesho “Thieta ya Ukombozi”. Jaribio
mojawapo lililokuwa mashuhuri sana ni lile lililofanyika katika kijiji cha
Kamiriithu huko Limuru nchini Kenya. Hapo mwanzo maiigizo haya yalitumia lugha
za asili kama Gikuyu ya nchini Kenya na baadaye maigizo haya yalileta athari
kubwa ndani ya maigizo yaliyotumia lugha ya Kiswahili kwa mfano Thieta ya Umma
ya Penina Muhando na wenzake ilitumia lugha ya Kiswahili lakini ilifuata mfumo
sawa na ule wa maigizo ya Kamiriithu.
(Mulokozi
1996), anaendelea kufafanua dhana ya Thieta kwa Umma. Anasema:
“Ili kufanikisha
lengo la Thieta kwa Umma kiukamilifu, ilibidi igizo liwe katika lugha
inayozungumzwa na wananchi wenyewe, ambayo katika Kamiriithu ya Limuru nchini
Kenya ni Gikuyu. Mfano Ngugi wa Thiong’o na tamthiliya yake ya Nitaolewa
Nikipenda ambayo kwa mara ya kwanza iliandikwa kwa lugha ya Gikuyu na
kujulikana kwajina la Ngaahika Ndeenda kueleza mbinu za sanaa za
maonyesho za jadi zilizotumika. Baadhi ya mbinu hizo ni pamoja na nyimbo na
ngoma, lugha iliyosanifiwa kulingana na mzingira, maudhui yanayoakisi maisha na
matatizo ya watu wenyewe na yanayoendeleza maslahi yao, ushirikishwaji wa mtu
yeyote, badala ya wataalamu tu, katika sanaa, matumizi ya ishara na mbinu
nyingine za kijadi.”
Ushiriki
wa Penina Muhando katika kueneza dhana hii ya Thieta ya Umma ulikuwa ni wa
kiwango cha juu sana. Mwanamama huyu alijidhatiti na kukaza Kibwebwe ili
kuhakikisha kuwa sanaa za maonyesho zinaleta mantiki na kunufaisha jamii.
Mtaalamu huyu wa sanaa za maonyesho na wenzake ambao baadhi yao ni pamoja na
Amandina Lihamba, E. Chambulikazi, G. Marengo na baadhi ya walimu na wanafunzi
wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo na Chuo kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Sanaa za
maonyesho walitumika ndani na nje ya nchi. Nchni Tanzania juhudi hizo zilifanyika
katika maeneo kadhaa, baadhi ya maeneo hayo ni Bagamoyo Mjini (Pwani),
Mkambalani (Morogoro), Malya (Mwanza) na Msoga (Pwani). Nje ya mipaka ya nchi
Penina Muhando alishiriki pia katika uhamasishaji wa Thieta ya Umma, baadhi ya
nchi hizo ni Zimbambwe, Kameruni na Bangladesh.
Mulokozi
(1996) katika kitabu chake cha Fasihi ya Kiswahili, anasisiti kuwa
japokuwa Thieta ya Umma haikuanzia Tanzania lakini juhudi kubwa za kuendeleza
aina hii ya sanaa za maonyesho kwa lugha ya Kiswahili zilizofanikiwa zaidi ni
zile za Penina Muhando na wenzake.
Penina Muhando Mwasisi wa Mkakati wa TUSEME
Penina Muhando Mwasisi wa Mkakati wa TUSEME
Katika
kuhakikisha kuwa sanaa za maonyesho zinaleta tija katika maisha ya wanajamii,
mama Penina Mhando (ambaye katika maandiko yake mengi ya kitaaluma anatumia
jina la Penina Mlama na katika kazi zake za kisanaa anatuma jina la Penina
Mhando), alianzisha mkakati wa kuwafikia vijana hasa wasichana na kuwaelimisha
juu ya haki na wajibu wao ndani ya jamii kwa njia ya sanaa za maonyesho. Katika
mahojiano yaliyofanyika kati ya mwasisi huyu wa TUSEME na utafiti huu, Mama
Muhando alieleza mengi juu ya mkakati huu uliokuwa maarufu sana kuanzia miaka
ya 1990. Katika mahojiano haya Mama Mhando aliitaja hadhira yake kama chanzo
cha msukumo uliomshawishi yeye kuanzisha mkakati huu, alisema mwitikio mkubwa
wa hadhira yake katika tamthiliya ya Nguzo Mama ndio uliomshawishi
kubuni mkakati huu. Vilevile katika mahojiano haya Mama Mhando alionyesha
mapenzi yake ya dhati juu ya mkakati huu. Jambo hili liliibuka pale ambapo
mtafiti alipomuuliza swali lililouliza kuwa “Kazi zako zipi unazozipenda? Na ni
kwa nini”? Mama Mhando alisema kuwa kwa dhati ya moyo wake aliupenda mkakati wa
TUSEME zaidi ya tamthiliya zake andishi. Alisisitiza kauli yake hii kwa kusema
kuwa vijana wengi katika Dunia ya tatu wamekata tamaa, wengi hawajui hatima ya
maisha yao ya mbele. Lakini mabadiliko yaliyoletwa na mkakati wa TUSEME
waliyaona wazi wazi. Walipokuwa wanafanya aina hii ya sanaa ya maonyesho mbele
ya vijana na watoto waliopo vijijini kabisa waliona badiliko la ghafla,
badiliko hilo lilihashiriwa kwa kujitokeza tabasamu na uso wa kuchangamka
mwishoni mwa maonyesho hayo. Hivyo alifurahi sana kuyaona mabadiliko haya wazi
wazi. Kuhusu mbinu zilizotumika katika kuendeleza mkakati huu wa TUSEME Mama
Mhando alisema kuwa mbinu zilizotumika katika kuendeleza Thieta kwa Umma ndizo
zilitumika katika kuendeleza mkakati huu wa TUSEME. Katika mkakati huu Penina
Mhando na wenzake walitembelea mashule, vyuo na maeneo ya makazi ya watu kwa
lengo la kutoa elimu kwa njia ya sanaa ya maonesho. Baadaye wanafunzi kutoka
shule mbalimbali walikuwa wakikutana kila mwaka mkoani Dar es salaam kwa lengo
la kufanya sanaa za maonyesho kwa mtindo wa kushindana. Serikali ya Tanzania
chini ya Wizara ya elimu na utamaduni iliamua kudhamini mkakati huu. Jambo la
kusikisha ni kwamba mkakati huu unasuasua, mpaka sasa takribani muda wa miaka
kumi mpango huu hauja fanyika kikamilifu.
NA
MWL. MAJUMBENI
0745 - 101842
2. EBRAHIM HUSSEIN
Ebrahim
N. Hussein alizaliwa Mkoani Lindi, kwenye Pwani ya Kusini ya Tanzania, mnamo
mwaka 1943. Hussein anasadikiwa kuwa mwandishi wa maigizo anayeongoza Afrika ya
Mashariki. Ni mwanashahada wa sanaa za maigizo, na mhadhiri aliyewahi
kufundisha katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Pia Ebrahim Hussein ana shahada
ya juu (doctorate) kutoka Chuo Kikuu cha Humboldt, Ujerumani. Alifundisha sanaa
za maigizo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia mwaka 1975 hadi 1985
ambapo alistaafu mwaka 1988. Alishinda tuzo ya Umoja wa Waandishi wa Vitabu wa
Tanzania (UWAVITA) kama mwandishi bora wa maigizo ya Kiswahili.
Hussein
aliibuka na kazi zake mnamo miaka ya 1960, kwa michezo ya kuigiza ya Alikiona
uliotolewa mwaka 1967 na Wakati Ukuta uliotolewa mwaka 1969. Hii
ilikuwa michezo ya kuigiza ya kijamii, iliyokuwa na mada za migongano na
mabadiliko. Kazi zake za baadaye katika mfumo huohuo zilikuwa Sokomomo
ambao haujatolewa, na Kwenye Ukingo wa Thim iliyotolewa mwaka 1988.
Mchezo mwingine ni Kinjekitile, uliotolewa mwaka 1969, ambao ni mchezo
wa kuigiza unaohusiana na vita vya Maji Maji, ambao aliutafsiri kwenye lugha ya
Kiingereza mwaka 1971. Pia mchezo wa Mashetani ambao ulitolewa mwaka
1971 ni moja kati ya kazi zake bora kabisa, mchezo huu unahusiana na migogoro
katika jamii nchini Tanzania wakati wa awamu ya “Ujamaa”. Arusi, ni
mchezo ambao unajadili Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Jogoo
kijijini na Ngao ya Jadi, iliyotungwa mwaka 1976, nayo pia
ilihusisha mada za mgongano katika jamii pamoja na harakati za kuleta ukombozi
kwa baadhi ya mambo.
Hussein
anaweza kufananishwa na mwandishi wa Nigeria na mshindi wa Tuzo ya Nobel, Wole
Soyinka. Kama Soyinka, Hussein ni mwasisi wa sanaa ya maigizo ya kisasa ya
Kimajaribio. Kazi zake kama zile za Soyinka, daima huwa zinadadisi zinachemsha
akili na huwa zimetayarishwa kwa ustadi na ufundi mkubwa. Hata hivyo, Hussein
hajulikani sana nje ya ulimwengu wa lugha ya Kiswahili. Lakini kama Soyinka,
Hussein analenga katika masuala ya dunia nzima ya maisha na matatizo ya jamii
ya Kitanzania katika hali halisi ya Afrika Mashariki.
NA
MWL. MAJUMBENI
0745 - 101842 3. MWALIMU J. K. NYERERE
Samandito (2013) anasema, watu wanamfahamu Mwalimu J. K. Nyerere kama mwanasiasa na
kiongozi maarufu wa enzi zake. Anafahamika pia kama mwalimu na mwanafalsafa
maarufu aliyetetea haki na usawa wa watu wote bila kujali rangi, dini na hata
kabila. Mwalimu J.K. Nyerere anafahamika kwa kuasisi Falsafa ya Elimu ya Watu
Wazima iliyoonekana yenye manufaa makubwa na endelevu miongoni mwa jamii za
kimataifa zilizojihusisha na shughuli za maendeleo. Mwalimu Nyerere kama
binadamu wengine alikuwa nazo sifa nyingine kama vile Baba wa familia, baba wa
watoto saba, babu wa wajukuu ambaye alipenda kucheza nao. Joseph Warioba (2009)
anathibitisha haya, akisema:
“Mwalimu Nyerere alikuwa inadamu wa
kawaida. Maisha na chakula chake vilikuwa vya kawaida kabisa. Jumapili moja
nikiwa kijijini kwetu wakati wa likizo, mke wangu kwa kuwa yeye ni Mkatoliki,
aliamua kwenda kusali katika kanisa la Butiama. Niliongozana naye. Baada ya
ibada Mwalimu alitukaribisha kwa ajili ya kifungua kinywa ambapo alikuwa
amewakaribisha pia wajukuu zake. Chakula kilikuwa cha kawaida na watoto
walikuwa wakipiga kelele na kufanya fujo nyingi, wakimwaga chai na maziwa huku
wakimwita babu yao kwa sauti wakitaka hiki na kile. Mtu anaweza kuona ni jinsi
gani Mwalimu alifurahia kucheza na wajukuu kama mzee au babu mwingine wa
kawaida” (Tafsiri yangu).
Pamoja
na hayo, Mwalimu Nyerere alikuwa mtaalamu wa lugha ya Kiswahili. Akiwa mtaalamu
wa lugha, Mwalimu J.K. Nyerere alitafsiri kazi za tamthiliya za William
Shakespeare za Julias Kaizari na Mabepari wa Venisi kwa lugha ya
Kiswahili. Pia aliandika mashairi mengi kwa lugha ya kiswahili. Kupitia
mashairi hayo, alikuwa akijibizana na kujadiliana na washairi wenzake. Jambo la
msingi tu ni kwamba, Mwalimu Nyerere alikuwa mshairi, mpenzi wa ushairi, mpenzi
wa malumbano ya washairi na alipenda mashairi ya washairi wengine. Katika
utangulizi wa Mashairi ya hekima na
Malumbano ya Ushairi yaliyokusanywa na Mathias Mnyampala mwaka 1965,
anaonesha jinsi alivyopenda ushairi na hasa mashairi ya washairi wakongwe.
Barua yake kwa Mathias Mnyampala ya tarehe 14/08/1965 inaeleza jinsi
alivyopenda malumbano ya washairi. Inasemekana pia kwamba, akiwa madarakani, na
hisia zilipomshika kutaka kueleza jambo zito, alitumia mashairi.
Karsten Legere (1999) anasema kwamba Mwalimu Nyerere alitoa
mfano bora kwa kutafsiri tamthiliya mbili za William Shakespeare katika lugha
ya Kiswahili. Katika kuthibitisha hili anasema:
“Mwalimu anakumbukwa wakati wote
kama mwandishi na mtaalamu wa tafsiri za vitabu vyenye hadhi kubwa duniani kama
vile tamthiliya za mwandishi mashuhuri wa Kiingereza Shakespeare ambavyo ni Mabepari wa Venis na Julias Kaizari. Kwa kuongeza, kabla ya
uhuru, Julius Kambarage Nyerere alikuwa akiandika mashairi ambayo yalijumuishwa
katika kazi za washairi wengine kama vile Mathias Mnyampala au Abdul Kandoro”.
(Tafsiri yangu).
Legere
anaendelea kusema kuwa Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa mwandishi wa makala nyingi
katika lugha ya Kiswahili ambazo zilichapishwa katika Sauti ya TANU. Makala mojawapo ilimsababishia kulipishwa faini na
watawala wa serikali ya kikoloni kwa sababu walijisikia kukosewa heshima.
Naye
Laurent Magesa(2011)
katika makala yake (The Hidden Face of Mwalimu Nyerere) anaeleza kwamba Mwalimu
Nyerere alichapisha mashairi kwa lugha ya Kiswahili yenye kubeba maudhui
mchanganyiko: ya kisiasa, kijamii na kiidili. Nyerere pia alitafsiri tamthiliya
mbili za mwandishi mashuhuri wa Kiingereza, William Shakespeare zikiwa na
ujumbe wa kijamii na kimaadili. Pia alitafsiri sehemu ya Biblia Takatifu Agano
Jipya katika mtindo wa kishairi. Alikuwa na lengo la kutuonesha kwamba
Kiswahili kama lugha inao uwezo kama lugha nyingine kutumika katika kuelezea
ujumbe wa aina yoyote hata kama ni tata (Tafsiri yangu).
Wataalam wa fasihi ya Kiswahili wanakiri kuwa, Mwalimu
Nyerere alikuwa ni mahiri si wa lugha ya Kiswahili tu, bali pia wa Lugha ya
Kiingereza na Kizanaki, ambayo ni lugha yake mama na katika taaluma ya tafsiri.
Mwalimu Nyerere pia alikuwa hodari wa fasihi simulizi. Mara nyingi hotuba zake
zilisheheni vielelezo kutoka fasihi simulizi ya Kiswahili – visa na mikasa. Tunaweza kukumbuka hadithi ya Kijiji
kilichokumbwa na baa la njaa na wakamtuma kijana mmoja kwenda kutafuta chakula
na asirudi. Pia simulizi ya mke wa Kaisari aliyekuwa mzinzi. Harith
Ghassany (2010:259).
Legere
(1999) ni miongoni mwa wanataaluma walioandika juu ya uanafasihi wa Mwalimu J.
K. Nyerere. Amemwonesha Mwalimu Nyerere kuwa ametoa mchango mkubwa sana katika
kukuza na kuinua lugha ya Kiswahili. Anaeleza kuwa mwalimu Nyerere alikuwa
jasiri na alichukua hatua madhubuti za kukienzi na kukitukuza Kiswahili ili
kiweze kutumika katika nyanja mbalimbali za kijamii na kitaaluma. Anaendelea
kusema kwamba Mwalimu Nyerere alitoa mfano bora kwa kutafsiri tamthiliya mbili
za William Shakespeare katika lugha ya Kiswahili. Katika kuthibitisha hili
anasema:
“J. K. Nyerere ni mfano unaong’ara
kwa ubunifu na mchango wake mkubwa katika kukuza na kuinua hadhi ya lugha ya
kiswahili katika Tanzania. Akitambua upinzani na mtazamo hasi uliotamalaki
nchini Tanzania, alikuwa jasiri na alichukua hatua madhubuti zilizokikuza
Kiswahili katika nyanja mbalimbali za matumizi. Hivyo, mwalimu anakumbukwa
wakati wote kama mwandishi na mtaalamu wa tafsiri za vitabu vyenye hadhi kubwa
duniani kama vile tamthiliya za mwandishi mashuhuri wa Kiingereza Shakespeare
ambavyo ni Mabepari wa Venis na Julias Kaizari. Kwa kuongeza, kabla ya
uhuru, Julius Kambarage Nyerere aliendelea kuandika mashairi ambayo
yalijumuishwa katika kazi za washairi wengine kama vile Mathias Mnyampala au
Abdul Kandoro”.(tafsiri yangu).
Anaeleza
pia kwamba, J. K. Nyerere alikuwa mwandishi wa makala nyingi katika lugha ya
Kiswahili ambazo zilichapishwa katika Sauti
ya TANU. Makala mojawapo ilimsababishia kulipishwa faini na watawala wa
serikali ya kikoloni kwa sababu walijisikia kukosewa heshima. Aliandika pia
makala nyingine iliyokuwa na kichwa kilichosomeka, Mali ya Taifa. Anaeleza pia kwamba Mwalimu Nyerere aliandika
ushairi wa kidini ambao ni tafsiri ya Biblia Takatifu kutoka Agano Jipya.
Kassam
(2000) anamwelezea Julius Nyerere kuwa ni mwasisi na Rais mstaafu wa Jamuhuri
ya Muungano wa Tanzania, anayejulikana si tu miongoni mwa viongozi wa nchi
wanaoheshimika duniani na wasemaji wa ukombozi na utu wa Waafrika, bali pia
mwalimu na mwanafalsafa mashuhuri wa masuala ya elimu. Anaendelea kusema kuwa,
kabla Nyerere hajajiunga na siasa alikuwa mwalimu, na ndiyo matokeo ya
maandishi yake juu ya falsafa ya elimu na mahusiano baina ya uongozi wa kisiasa
na kitaaluma nchini, anapendwa na kuheshimiwa na Watanzania wote na hivyo
humwita kwa jina la mwalimu. Anaendelea kuelezea kuwa Julius Nyerere anasifika
pia kwa falsafa yake ya elimu ya watu wazima iliyoonekana ya kufaa na endelevu
miongoni mwa jamii za kimataifa za elimu ya watu wazima na taasisi zisizo za
kiserikali zilizojihusisha na shughuli za maendeleo. Kutokana na malengo yake
mazuri na kujitoa kwa ajili ya elimu ya watu wazima aliombwa kuwa mwasisi na
Rais wa heshima wa halmashauri ya kimataifa ya elimu ya watu wazima mwaka 1973.
Naye
Mwansoko (2000) anaeleza mchango wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika
fasihi ya kiswahili. Anatueleza kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mpenzi na shabiki
mkubwa wa ushairi wa kiswahili na ndiyo sababu huenda ilimsukuma kutafsiri kazi
za Shakespeare. Hivyo basi Mwansoko anasema:,
“Mwalimu Nyerere alitafsiri
tamthiliya za Shakespeare Julias kaizari na Mabepari wa Venisi kwa sababu
mbalimbali: kwanza ni kwa sababu tamthiliya za Shakespeare ni miongoni mwa
maandiko bora Ulimwenguni. Sababu ya pili ni ushabiki wake wa ushairi, alivutwa
kutafsiri tamthiliya za Shakespeare kwa vile ziliandikwa kwa mtindo wa mashairi
guni, yaani yale yasiyo na vina. Japo mashairi guni yametofautiana sana na
mashairi ya Kiswahili ya kawaida au ya kimapokeo, bado yalimpatia Mwalimu
Nyerere burudiko la kutosha baada ya kuchoshwa na kazi zake za kawaida”.
Mwansoko
anaendelea kueleza kuwa,
“Katika siku za mwisho za uhai wake,
Mwalimu Nyerere alijishughulisha sana na kazi ya kutafsiri. Alitafsiri Biblia
kwa ushairi na tayari vijitabu vinne vya tafsiri hiyo vimeshachapishwa. Aidha
Mwalimu keshasawidi tafsiri ya Plato ya “The
Republic” ambayo bado haijachapishwa.
Mwalimu Nyerere ameshachapisha mashairi yake katika magazeti, vitabu vya
washairi wenzake na hata kuchapisha tenzi zake binafsi, kama vile Utenzi wa Tanzania! Tanzania! (1993)”.
Malangwa
(2005) anaelezea matatizo yanayowapata wataalamu wanaojishughulisha na
kutafsiri kazi za fasihi kutoka lugha chanzi kwenda lugha nyingine. Ameeleza
uwezo wa Mwalimu Nyerere katika taaluma ya tafsiri na matatizo yaliyojitokeza.
Akishughulikia kazi ya tafsiri iliyofanywa na Mwalimu Nyerere ya Mabepari wa Venisi anasema:
“Matatizo yaliyompata mfasiri
(Mwalimu Julius Kambarage Nyerere) ni yale ya kiisimu na kifasihi. Matatizo
mengine ambayo yanaweza kufanyiwa utafiti ni tofauti za kiisimu baina ya lugha
ya Kiswahili na Kiingereza, tofauti za kijiografia baina ya jamii za watumiaji
wa lugha hizi na tofauti za kisanaa baina ya lugha chanzi na lugha ya tafsiri”.
(tafsiri yangu).
Rose
Shayo (2010/11) anamwelezea Julius Kambarage Nyerere kama mjasilia mali wa
kisiasa wa wakati wake. Anaeleza pia kuwa, alikuwa mpigania haki na usawa wa
waafrika wote. Licha ya kupingwa na baadhi ya wasomi, Shayo anaeleza kuwa
Mwalimu Nyerere aliendelea kuwathamini wasomi na mchango wao aliutegemea zaidi
katika ujenzi wa taifa la Tanzania. Anaeleza pia kwamba, licha ya Nyerere kuwa
mkristo Mkatoliki, hakuwa na ubaguzi wa kidini na wala hakupendelea upande
wowote wa imani wakati wa uongozi wake. Katika kuthibitisha haya, Shayo
anasema:
“Nyerere akiwa mfuasi mzuri wa dini
ya kikristo kwa dhehebu la Katoliki, hakuonesha kuathiriwa na uumini wake kwa
kupendelea dini fulani au dhehebu. Yeye alikuwa muumini mzuri wa dini yake,
akiwa Dar es Salaam hakukosa kuhudhuria misa za masifu kila siku asubuhi
kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa moja asubuhi katika kanisa kuu la
Mtakatifu Josefu. (Tafsiri yangu).
Nyerere,
licha ya kuwa mkristu Mkatoliki, aliwalazimisha wasimamizi wa shule za misheni
kudahili wanafunzi wa madhehebu na imani zote. Mwaka 1969, shule zote ambazo
hazikuwa za serikali zilitaifishwa na kuwa za serikali, isipokuwa zile za
seminari tu (The Guardian, September 28, 2006). Aliendelea kuwaambia viongozi
wa dini kwamba kanisa lazima limhudumie mtu kiakili, kiroho na kimwili. Anasema:
“Kanisa lazima liwahudumie watu nje ya mipaka ya kanisa”. Kwa mfano, shule,
hospitali na taasisi zake za kibiashara zisifaidishe kanisa na wakristu tu,
bali hata wasioamini.
Kutokana
na imani na mapenzi yake kwa watu wake wa Tanzania, Mwalimu Nyerere alisikitika
sana alipogundua kuwa anawaacha kwani aliona kifo chake kabla. Shayo anasema: “
Nyerere alikiona kifo chake kabla hakijatokea. Muda mfupi kabla ya kuondoka
kwenda kutibiwa ng’ambo, alijua kwamba hatarudi akiwa hai, na hivyo kama maneno
ya buriani kwa watanzania aliahidi kuwaombea kama alivyonukuliwa akisema:
“Najua sitapona toka ugonjwa huu. Nasikitika kuwaacha watanzania wangu. Najua
watalia sana. Lakini mimi nitawaombea mbele ya Mungu”.
Shayo
anataja pia kazi alizoandika Mwalimu Nyerere zikiwemo za kifalsafa na kifasihi
pia. Baadhi ya kazi anazozitaja ni: Uongozi
Wetu na Hatima ya Tanzania (1993), Biblia iliyotafsiriwa kwa Kizanaki.
Mwaka 1996 aliandika ushairi na nyimbo za kiroho zilizotokana na Enjili za
Matayo, Marko, Luka, Yohana na Matendo ya Mitume. Pia alitafsiri tamthiliya za
William Shakespeare ambazo ni Julias
Kaizari na Mabepari wa Venis kwa
lugha ya Kiswahili na zilichapwa na Oxford University Press mwaka 1969.
Magesa
(2011) anaandika kwamba, “Juhudi za mwalimu Nyerere katika kukiendeleza
Kiswahili kama chombo cha kujielezea na elimu nchini Tanzania, Afrika Mashariki
na Ulimwenguni kote zinajulikana vema. Alichapisha mashairi kwa lugha ya
kiswahili yenye kubeba maudhui mchanganyiko; ya kisiasa, kijamii na kiidili.
Kama haitoshi kueleza uzuri na uwezo wa lugha kuelezea mawazo mbalimbali,
Nyerere alitafsiri tamthiliya mbili za mwandishi mashuhuri wa Kiingereza,
William Shakespeare zikiwa na ujumbe wa kijamii na kimaadili. Pia alitafsiri
sehemu ya Biblia Takatifu Agano Jipya katika mtindo wa kishairi. Nini alitaka
kutueleza katika haya yote? Jibu jepesi ni kwamba kiswahili kama lugha inao
uwezo kama lugha nyingine kutumika katika kuelezea ujumbe wa aina yoyote hata
kama ni tata (Tafsiri yangu).
Mtaalamu
huyu anagusia tu kuwa, Mwalimu Nyerere aliandika mashairi kwa lugha ya
Kiswahili yenye maudhui tofauti, bila kuweka bayana maudhui ya mashairi hayo na
mchango wake katika fasihi ya Kiswahili. Hajaeleza pia kama kazi hizo za
kifasihi za Mwalimu Nyerere ziko wapi na zina mchango gani katika maendeleo ya
fasihi ya Kiswahili. NA
MWL. MAJUMBENI
0745 101842
4. SAID AHMED MOHAMED
Said
Ahmed Mohammed alizaliwa pemba huko Zanzibar, Mnamo tarehe 12 Desemba
1947. Haku bahatika kupata malezi ya baba na mama ipasavyo kwani wazazi
wake walitengana akiwa mdogo sana. Hivyo alilelewa na mama zake wakuu
(mama zake wakubwa), Bi. Jokhana Bi Rukia. Alisoma shule ya msingi Wete
Boys, Pemba baadaye alihamia Kiembe samaki, Unguja. Kisha akapelekwa
skuli ya Darajani (shule yenye watoto wenye vipaji) Unguja baadaye
akaendelea na masomo yake ya sekondari katika shule ya upili ya Gulioni
ambapo zamani iliitwa “King George The VI”. Mapinduzi ya Zanzibar
yalitokea akiwa kidato cha pili. Baada ya kuhitimu masomo yake ya
sekondari alijiunga na chuo cha ualimu cha Nkurumah TTC kilichopo mjini
Zanzibar mwaka 1966, ilishindikana kujiunga na kidato cha tano na sita
kwani wakati huo kiongozi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar hayati
Abeid Aman Karume alipiga marufuku masomo ya kidato cha tano na sita.
Baada
ya kuhitimu chuo alifundisha shule ya msingi Kizimbani kwa wiki mbili
tu, halafu akahitajika kwenda kufundisha shule ya sekondari Utaani,
kuanzia 1969 hadi 1974. Saidi Ahmed Mohamed alifundisha masomo ya
biologia, hesabu, kemia na pia Kiswahili. Baadaye alibahatika kusoma
katika skuli ya International Correspondence kiwango cha kidato cha tano
na sita. Baada ya kujiunga na kidato cha tano na sita alipanga
kujifunza masomo ya sayansi lakini palikosekana vifaa vya kufanya masomo
ya utekelezaji wa kisayansi yaani (practical) na hivyo alichagua
kufanya masomo ya kisanaa.
Mnamo
mwaka 1976 Said Ahmed Mohammed alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es
salaam kusomea shahada ya kwanza katika elimu akijikita katika kusoma
Isimu na Fasihi ya Kiswahili, baada ya kufuzu katika shahada hiyo
alirejea nyumbani Zanzibar na kuwa mwalimu mkuu wa shule za msingi na
upili za Hamamni kwa miaka mitatu. Na baadaye alirudi Chuo Kikuu cha
Dar es salaam na kujisajili kusomea shahada ya uzamili yaani (MA),
katika Isimu Telekezi . Alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Dar es salaam
kipawa chake kilimvutia mwalimu kutoka Ujerumani aliyefundisha Isimu
Linganishi na ya kihistoria bwana Sigmund Bruner. Hapo ndipo alipopata
fursa ya kuelekea Ujerumani kufanya shahada ya uzamifu yaani PhD,
alijiunga na Chuo Kikuu cha Karl Marx Leipzig Ujerumani mwisho wa mwaka
1981 na kukamilisha shahada ya uzamifu mwaka 1985 na kutunukiwa shahada
ya udaktari, kipindi hicho alikuwa pamoja na familia yake.
Baada
ya kumaliza shahada yake ya uzamifu huko Ujerumani aliteuliwa na raisi
wa Zanzibar wakati huo mzee Idris Abdul Wakil, kuwa mkurugenzi wa pili
wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI), ambayo baadaye
ilikuwa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), hivyo kurejea nyumbani
Zanzibar kwa miaka miwili na baadaye akaondoka kwa sababu za kisiasa na
fitina za watu ambao haku wafahamu, akaelekea Kenya mnamo mwaka 1987 na
kuwa mwenyekiti wa kwanza wa idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha
Moi mjini Eldoret na baadaye kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu
cha Nairobi hadi mwaka 1990.
Said
Ahmed Mohammed aliondoka Kenya kutokana na matatizo aliyokumbana
nayo Moi-Kenya. Tatizo kubwa ni mtoto wake ambaye alifanyiwa visa
mbalimbali kama vile kutafunwa meno na mtoto wa kikenya na suluhu ya
kisa hicho haikuwa sahihi kwa mujibu wake. Sababu ya kisa hicho ni
utundu wa watoto pamoja na kasumba ya utaifa ambayo iliwafanya kumuona
ni mgeni na kuanza kumnyanyasa. Hivyo kwa kuwa hakupenda wanawe wateseke
aliamua kuacha kazi kwani ilifikia hatua watoto wake hawakutakiwa
kupanda gari ya shule. Alipotoka Nairobi alielekea Japan katika Chuo
Kikuu cha Osaka, idara ya lugha za kigeni na hapo ndipo alipopata
uprofesa. Alipotoka Osaka ndipo akaenda Chuo Kikuu cha Bayreuth,
Ujerumani na kufundisha tangia mwaka 1997 mpaka 2012.
Said
Ahmed Mohammed alipenda kusoma, kutunga mashairi na hadithi fupi,
alipokuwa darasa la tano alitungama shairi yaliyotumiwa na walimu katika
madarasa ya juu. Kazi yake ya mwanzoni utunzi wa shairi ambalo
liliitwa “Nimfuge Ndege Gani Ili Nipate Salama” mwaka 1960. Shairi hili
lilifungua mdahalo mkubwa kwa wapenzi wa fasihi na wana fasihi. Baada
ya hapo alipata hamu kubwa ya kuendelea kuandika. Hivyo aliandika
mashairi na kupeleka redio ya Zanzibar. Alipata hamasa zaidi kutoka
kwa walimu wake ambao ni Mohamed Abdallah, na Kindi Abubakary ambao
waliona kipaji chake na kumsisitiza aandike.
Said
Ahmed Mohammed aliwahi kushiriki mashindano ya liyoanzishwa na
idara ya Kiswahili BBC. Mashndano hayo yalihusu uandishi wa hadithi
fupi za Kiswahili. Mara nyingi hadithi zake zilishinda lakini kati ya
vitabu hivi viwili, hadithiya “Sadiki Ukipenda” ndiyo iliyompa
umaarufu, katika hadithi hii mtunzi alionesha umakini wake katika
kutunga visa bunilizi ambavyo vilielezea maisha halisi ya kila siku
katika jamii.
Said
Ahmed Mohammed alirithi kipawa cha usanii kutoka kwa mama yake mkubwa
ambaye alikuwa nyakanga. Mama huyu alikuwa bingwa wa kuimba nyimbo za
unyago. Pia alikuwa mtunzi mzuri wa mashairi, na alipenda sana hadithi
za fasihi simulizi. Uandishi wa Said Ahmed Mohammed zaidi ya kurithi
kutoka kwa mama yake mkubwa, ulitokana pia na mafunzo ya elimu ya dini
ya kiislam, aliyoipata kutoka madrassa.
Said
Ahmed Mohammed alivutika na kuanza kusoma riwaya, riwaya ya mwanzo
kuisoma ilikuwa ni riwaya ya Kiu( 1972), ikifuatiwa na Nyota ya Rehemu
(1976), zilizotungwa na Mohamed M.S. Baada ya kusoma riwaya ya
Kiu ndipo alipopata hamu na shauku ya kuandika riwaya. Riwaya yake ya
mwanzo aliyoiandika ni Asali Chungu ( 1977), ikifuatiwa na Utengano
(1980), na Dunia Mti Mkavu ( 1980). Aliendelea na jitihada za uandishi
hadi kuwa muandishi maarufu na kupata tuzo mbalimbali ndani na nje ya
nchi. Vilevile amebobea katika ugawa ushairi ambapo ametunga diwani
mbalimbali, zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, mapenzi na utamaduni. Diwani
hizo ni kwa lengo la kuibua maudhui aliyokusudia muandishi huyu kama
waandishi wengine wa kazi za fasihi. Ametumia fani katika kazi zake za
fasihi mojawapo ya mitindo aliyotumia ni uhalisia mazingaombwe katika
kazi kama vile, “Babu alipofufuka, Kivuli Kinaishi, Amezidi na Sadiki
Ukipenda, pia alitumia bunilizi, utomeleaji na taswira katika kazi
zake nyingi.
Said
Ahmed Mohammed ametajwa kama muandishi mashuhuri zaidi Africa Mashariki
na hata Afrika nzima akiwa ameweza kuandika riwaya, Tamthilia,
Mashairi, kazi za watoto na hata vitabu vya shule na vyuo. Baadhi ya
kazi zake zimetafsiriwa kwa lugha za kigeni, pia kuna miswada ambayo
imechapishwa hivi karibuni ya riwaya ya Nkama dume, Mhanga Nafsi
yangu, na kitabu cha kusoma katika darasa la saba kiitwacho Gharama ya
Amani kinachozungumzia fujo za kisiasa zilizotokea Kenya. Mwandishi huyu
ni miongoni mwa waandishi wa riwa ya za kimapinduzi na kifalsafa.
Familiayake;
Profesa
Said Ahmed Mohammed ana mke mmoja anayeitwa Rahma, na watoto wawili
msichana na mvulana. Msichana anaitwa Najima jina linalo maanisha
nyota na ,wa kiume anaitwa Mahirna neno la kiarabu lenye maana ya
mwenye ujuzi na wote wamekamilisha shahada ya kwanza.
KAZI ZAKE;
Inasadikika ameandika zaidi ya vitabu hamsini na tano (55), vifuatavyo
ni baadhi ya vitabu alivyoandika, kuna vitabu vya:
USHAIRI
Kina cha Maisha.
Jicho la Ndani (2001), Nairob:Longhorn Publisher.
TAMTHILIYA
Kivuli kinaishi (1990), Oxford University Press .
Amezidi (1995), East African Educational Publishers.
KitumbuakimeingiaMchanga (2004)Nairob :Longhorn Publishers ltd
RIWAYA
Asali Chungu( 1989), East Afracan Publishers.
Babu Alipofufuka (2001), JomoKenyatta Foundation.
Utengano (1980), Longhorn Publishers.
Tata za Asumin i(1990), Longman Kenya.
Dunia Mti Mkavu (1980), Longman Kenya Ltd.
Kiza Katika Nuru (1988), Oxford University Press.
Dunia Yao (2006), Nairob:Oxford University Press.
NA
MWL. MAJUMBENI
0745 - 101842
5. MOHAMED SAID ABDULLA
Mohamed Said
Abdulla alizaliwa mnamo mwaka 1918 katika mtaa wa Malindi Zanzibar. Alipelekwa
chuoni ambako alijifunza kusoma Kurani. Mwaka 1928 alisoma masomo ya msingi
katika shule ya serikali. Alifanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari mwaka
1938 katika shule ya serikali pia. Baada ya kuhitimu aliajiriwa kuwa ofisa wa
afya ambako alifanya kazi hiyo mpaka mwaka 1958 wakati ajira yake
ilipokatishwa. Baada ya kuachishwa kazi katika idara ya afya alifanikiwa kupata
ajira nyingine katika gazeti la Mkulima
kama mhariri. Alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1968 pale alipoachishwa tena kazi
ya uhariri katika gazeti hilo. Baada ya kuachishwa kazi hiyo alipata kazi ya
utayarishaji kipindi cha redio kilichoitwa Sadiki
Ukipenda katika Sauti ya Unguja.
Katika uhai wake alioa na kupata watoto wanne.
Katika taaluma
ya fasihi mchango wake unaonekana sana katika taaluma ya riwaya kwani aliandika
na kuchapisha riwaya saba pamoja na hadithi fupi moja kama ifuatavyo;
Mzimu wa Watu wa Kale ,Kisima cha Giningi,
Duniani kuna watu, Siri ya Sifuri, Mke Mmoja Waume Watatu, Mwana wa Yungi
Hulewa, Kosa la Bwana Msa, Mke Wangu ambayo ni hadithi fupi. Mohamed Said Abdulla alifariki mnamo
mwaka 1992.
NA
MWL. MAJUMBENI
0745 -101842
Sheikh Kaluta Amri Abedi alizaliwa Ujiji
Kigoma mnamo mwaka 1924 Baba yake Kaluta Amri Abedi aliitwa Abedi bin Kaluta.
Kaluta Amri Abedi Alikuwa ni mtoto wa pili wa kiume katika familia ya watoto
kumi. Sheikh Kaluta Amri Abedi alipofika umri wa miaka 6 hivi alianza masomo ya
Kurani mwaka 1930. Baada ya miaka mitatu ya masomo ya kurani aliingia katika shule ya masomo ya Kizungu. Baada ya kumaliza
elimu ya awali mwaka 1937 alijiunga na Shule ya Sekondari Tabora.Baada ya
masomo yake ya sekondari Sheikh Kaluta Amri Abed alikwenda kusomea ukarani wa
posta Dar-es-salaam 1942—1943 .Kaluta Amri Abed alikwenda kusoma elimu ya dini
Rabwah Pakistan ambako aliweza kufaulu vizuri na kuweza kutunukiwa shahada ya
elimu ya dini (Teolojia).
Sheikh.Kaluta
Amri Abedi alioa mke wake wa kwanza 1941 ambaye aliitwa Zamda bint Sudi ambaye
alibahatika kuwa na mtoto mmoja aliye itwa Radhia kabla ya kumtaliki kutokana
na upinzani mkubwa uliotokana na mgogoro wa tofauti za kidhehebu yaani Kaluta
alipo hamia madhehebu la Ahamadiyya tofauti na mke ambaye alitoka katika
familia yenye imani ya madhehebu ya sunni. Sheikh Kaluta Amri Abedi alioa mke
mwingine mwaka 1956 ambaye aliitwa Amina bint Hamisi Mlenzi ambaye alibahatika
kuzaa naye watoto sita na kufanya jumla
ya watoto saba.
Sheikh
Kaluta katika maisha yake amekuwa mtumishi wa serikali kwa nyadhifa
mbalimbali,kama: aliwahi kuwa Mbunge wa kigoma, aliwahi kuwa meya wa kwanza
mwafrika wa jiji la kwanza Dar-es-salaam, aliwahi kuwa mkuu wa mkoa jimbo la Magharibi,aliwahi
kuwa waziri wa sheria,mpaka mauti yanamkuta alikuwa waziri wa maendeleo na
utamaduni.
Katika
dini Sheikh Kaluta alikuwa Sheikh na mbashiri
katika imani ya kiislam ya Ahamadiyya
alijishughulisha na kueneza dini
pamoja na kutafsiri kurani katika lugha
ya Kiswahili na lugha za kizungu.
Sheikh
Kaluta Amri Abedi alikuwa na kipaji cha usanii. Kipaji hiki cha usanii kilianza
kuonekana alipofika umri wa miaka 13, aliweza kutunga na kuimba mashairi kwa sauti nzuri na pia aliweza kudhibiti kanuni za
mizani. Aliweza kusoma mashairi ya lugha ya Kiingereza, Kiurdu, Kiarabu na
kiajemi.
Mchango wa Kaluta Amri
Abedi kwenye lugha ya kiswahili
Katika maandishi ya Mathias Eugen Mnyampala yanayotaja
historia ya maisha ya:
Sheikh Kaluta Amri Abedi, Mwandishi Mathias Eugen
Mnyampala amemtaja Kaluta kama mtu hodari wa kutumia Lugha ya Kiswahili
katika
fani ya kuimba Tajuwidi, Mashairi na Tenzi kwa mahadhi ya namna
mbalimbaali za Maghani. Hivyo Mnyampala anaweka bayana mchango mkubwa
wa Sheikh Kaluta Amri Abedi kwenye Lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo:
Kaluta Amri Abedi akiwa
na umri wa miaka sita
Kaluta Amri
Abedi alionyesha dhamira ya kupenda Lugha ya Kiswahili, alianza kupigania
matumizi ya Lugha ya Kiswahili tangu akiwa na umri mdogo kati ya miaka sita,
ambapo akiwa mwanafunzi wa masomo ya Kurani alionyesha kutoridhika kujifunza
Kurani kwa Lugha ya Kiarabu tu hata akadiriki kumuuliza mwalimu wake “Kwa
nini tunasoma kama kasuku hatuelewi yaliyomo katika aya za kurani tukufu?
Kwa nini kurani haitafisiriwi katika Lugha ya Kiswahili.” Hata waalimu wake walipomjibu juu ya maneno
ya Kiarabu kuonyesha ukamilifu wa aya na madai ya Masheikh wake kwamba kurani
ikitafsiriwa ingeharibiwa maana yake tofauti na zilivyoteremshwa na Mwenyezi
Mungu, Kaluta Amri Abedi hakuridhika na majibu hayo aliendeleza jitihada za kudai
matumizi ya Lugha ya Kiswahili zaidi kuliko lugha zingine. Mnyampala (Uk. 10)
Kaluta Amri Abedi kama mshairi
Sheikh Kaluta Amri Abedi alitumia kipaji
chake cha kuimba na kughani mashairi na tenzi kuenzi matumizi ya Lugha ya
Kiswahili akizidisha maneno yenye utamu wa lugha ya Kiswahili, nahau za lugha
ya kiswahili . Hali amabayo ilifanya
kuwa motisha kubwa kwa wasomaji wa mashairi yake kuijua lugha na kuithamini kwa
utukufu wake. Sheikh Kaluta Amri Abedi alitumia kalamu kuweka mchango wake
katika kukuza lugha ya kiswahili, aliandika maandishi yanayofafanua kanuni za
utungaji wa mashairi ya kiswahili,katika kitabu chake alichokiita SHERIA ZA KUTUNGA MASHAIRI NA DIWANI YA AMRI
(1953) – Katika uandishi wake alihamasisha lugha ya kiswahili Tanzania na
Afrika Mashariki kwa umahiri wake:Kaluta aliwahi kutunga mashairi mbalimbali
kwa lugha ya kiswahili ambapo hata alipo andika kitabu cha mashairi chenye
kueleza kanuni za kutunga mashairi washairi wengiwlikipokea kwashangwe kubwa na
kumsifia Rejea Almasi ya Afrika (Uk
81) ” anaeleza hiki ni kitabu ambacho
kimesadia sana kwa wale wanao taka kujifunza utunzi wa mashairi. Ni kitabu
ambacho kinatumika mashuleni na hakuna mshairi wa sasa aliyeandika juu ya
ushairi katika karne ya ishirini ambaye hakulazimika kumnukuu”.
Kaluta akiwa na umri wa miaka 13 tu
alipofiwa na baba yake aliandika ushairi wa kumwombolezea Rejerea katika Almasi ya Afrika (Uk 13-14):
Mola mrehemu baba, babaaliyenizaa,
Mola ni wewe Tawaba, mghofiri dhambi pia,
Peponi mpe maaba,na vyeo mzidishia,
Dua nitakabalia, Mola mghofiri baba,
Baba mwingi wa huruma kwa wema alinilea,
Akanitia kusoma,dini na dunia pia,
Akanifunza ya wema,ya akhera na dunia,
Dua nitakabalia Mola mghofiri baba
Baba nina
mkumbuka, vile nilivyo mjua
Mkarimu hana shaka,mwenye hadhi na sitawa,
Ni mtu alotukuka,vyeo akavipandia,
Dua nitakabalia,Mola mghofiri baba
Huu ni mfano tu wa kazi ya ushairi inayoweza
kuonyesha uwezo wake katika fani ya uga wa mashairi tangu akiwa mtoto mwenye
umri mdogo.
Kaluta Amri Abedi kama karii
Kaluta Amri Abedi
kwasababu ya umahiri wake katika kujishughulisha na lugha ya kiswahili
na uga wa ushairi alichaguliwa kuwa Karii wa mashairi ya kiswahili
(yaani msomaji,
mkosoaji na mwelekezaji wa matumizi na maandishi ya lugha ya kiswahili);
akiwa
Karii wa Ushairi” alipokuwa Tabora
aliandika makala zake kuhusu kiswahili akasema kwa kukitukuza kiswahili
huku
akigusia historia yake na kukimanya kwakwe alisema: “Kwa bahati tu
nilizaliwa katika mji ambao lugha inayosemwa ni kiswahili na utoto
wangu nikasoma karibu vitabu vyote vilivyopatikana na vilivyokuwa
vimeandikwa
kwa lugha ya kiswahili kisha muda wote wa maisha yangu nikalazimika
kukitumia
kiswahili kama chombo maalumu cha kufanyia kazi nilizoshughulika nazo za
semi
na maandiko, ikatokea nikaanza kujali sana maneno na nguvu yaliyo nazo,
ufasaha na jinsi ya kutoa
wazo lilete athari inayotakiwa, ikawa ninapoandika najitahidi kuchungua
sana
maneno kuyachagua na kuyapima na kutwaa
yale tu niliyo fikiri yana nguvu za kutosha kuwasilisha maoni yangu.
Mnyampala (Uk46)
Kaluta alikuwa msomaji wa vitabu vya kiswahili
aliweza kusoma maandishi ya waandishi wa kiswahili na alikosoa na kutoa maoni
yake ili kuhakikisha kiswahili kinatumiwa kwa usahihi wake, hivyo alitumia muda
wake kufuatilia maandishi na kuyafanyia marekebisho makosa ya lugha ya
kiswahili katika maandishi ya waandishi.
Hali hii ilitokana na upenzi wake mkubwa kwa lugha tukufu ya kiswahili.
Kaluta Amri Abedi kama mwanaharakati
Sheikh Kaluta Amri Abedi alichochea
kasi ya matumizi ya lugha ya kiswahili,
kwa madhumuni ya kutukuza lugha ya kiswahili. Mwandishi Mathias Mnyampala
amemfafanua Sheikh Kaluta Amri Abedi juu ya ushupavu wake katika kutetea Misingi
Imara ya Lugha ya Kiswahili. Anasema “Alikuwa hodari wa Mijadala kwa namna
zote, kwenye mashindano ya dini wakati akiwa yungali kiongozi wa dini,
alipambana kwa hoja na jamaa wengine katika lugha ya kiswahili kwa hoja
zilizokiuka alishinda katika mambo mbalimbali mororo ya kidunia,” Pia alishinda
malumbano yaliyotokea baina yake na Dkt Lyndon Harris kutokana na mashairi ya
Guni hasa yaliyo ndani ya kitabu cha kilicho tafsiriwa na Mwl. Julius K.
Nyerere kilicho andikwa na Shakespeare kinachoitwa Julius Kaisari .Mnyampala (Uk.
46 – 47)
Sheikh Kaluta Amri Abedi alisisitiza zaidi
lugha ya kiswahili huku akionyesha umma kwamba kiswahili ni lugha pekee
inayofaa kuwa ya Taifa na Serikali, alisisitiza kuwa lugha ya kiswahili
inazungumzwa na watu wengi zaidi kwa saababu imesheheni maneno mengi ya kibantu
na sarufi yake ni ya kibantu hata imekuwa rahisi zaidi wananchi kujua na
kujifunza kuliko lugha za kigeni.
Kwa msisitizo mkubwa Sheikh Kaluta Amri
Abedi kwa kubainisha uzuri wa lugha iliyotukuka, lugha ya kiswahili alifikia
kuandika maandishi ya kulikejeli kundi la watu wanaofanya juhuhudi za kujifunza
lugha ya Kiingereza, Kiarabu,na Kifaransa kwamba watazijua kwa kiasi tu, hata
kundi la wanaodhaniwa wana kijua kiingereza hakika yake ni kuwa hawakijui vilivyo,
wakisema wanakisema cha matata matata, wakiandika pia wanaandika cha matata
matata, na vyovyote vile ambavyo kujulikana kwalugha za kigeni kwa watu wengi
kutakuwa kuzijua lugha hizo juu juu tu Mnyampala (Uk48).
Ukweli Sheikh Kaluta Amri Abedi alikuwa na mapenzi ya dhati kwa lugha ya
kiswahili, hata kumbukumbu yake iliyosomwa kwenye mkutano tarehe 18/01/1962
yenye kichwa “HATIMA YA KISWAHILI” iliashiria jinsi Sheikh Kaluta anavyoshika
kalamu kwa makini kuweka bayana mapenzi makini kwenye lugha nzuri na makini ya
kiswahili akitia motisha kwa washairi wa lugha ya kiswahili pamoja na watumiaji
wa lugha ya kiswahili kuenzi, kutukuza na kuweka nia njema ya ari thabiti ya
kujifunza lugha iliyotukuka lugha ya kiswahili.Mnyampala
(Uk.47).
Sheikh
Kaluta Amri Abedi alitafsiri Kurani Tukufu kwa lugha ya Kiswahili Mnyampala (Uk14).
Alipokuwa Waziri wa Sheria alitafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili, hali hii
ilifanya shauku ya watu kujifunza sheria kwa lugha ya Kiswahili. Mnyampala (Uk.
60).
Kaluta Amri Abedi
kama mwenyekiti wa chama cha kiswahili Afrika mashariki
Sheikh Kaluta Amri Abedi alifunguliwa wigo mpana
wa kuitukuza lugha na uzuri wake pale alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama
cha Washairi wa Kiswahili kwa Afrika Mashariki,
katika kipindi hicho Sheikh Kaluta Amri Abedi alihamasisha matumizi ya
kiswahili akielezea lugha ya Kiswahili kuwa ni tunu waliyopewa kuwaunganisha,
katika kipindi hicho alishauri kiswahili
kutumiwa katika elimu ya awali, kati na
vyuo vikubwa. Kwahiyo mchango wa Kaluta
Amri Abedi ni mkubwa sana katika maendeleo na ukuaji wa lugha ya kiswahili na unafaa kuigwa na Watanzania na wana Afrika
Mashariki kwa upana wa mawazo yake katika kuienzi lugha yetu ya asili
Kiswahili.
Kaluta Amri Abedi akiwa
mwanasiasa
Sheikh Kaluta Amri Abed akiwa katika nyanja za
siasa alitumia uwanja wa siasa katika kufanya juhudi za kuhakikisha ustawi wa
lugha ya kiswahili katika matumiz, Kaluta akiwa waziri wa sheria alipiginia
kiswahili kitumiwe katika shughuri za bunge, na ulisisitiza kiswahili kitumiwe
katika kutafsiri sheria kuweka urahisi kwa sheria kueleweka kwa watu wote wa
Tanzania ambao Lugha ya kiswahili ni lugha rahisi na yenye kueleweka kwa
urahisi, Sheikh Bakri Abedi Kaluta Katika Almasi
ya Afrika ameelezea katika kitabu chake kuwa akiwa waziri wa utamaduni
aliendelea kupigania heshima ya kiswahili .Mara kwa mara alisisitiza juu ya
umuhimu wa kutumia kiswahili katika shule zetu kuanzia shule za msingi hadi
chuo kikuu.Sheikh Kaluta Amri Abedi kuonesha uzalendo katika lugha ya kiswahili
aloiwahi kuwaondoa watoto wake kutoka shule ya msingi Agha Khan ambayo leo
inaitwa Muhimbili, na kuwahamishia shule ya msingi ya Mnazi mmoja iliyo kuwa
ikifundisha kwa kiswahili hiyo ilitokana na alipogundua watoto wake hawawezi
kusoma vitabu vya dini vilivyo andikwa kwa kiswahili, Katika (Uk
209-210). Pia Sheikh Kaluta akiwa waziri wa Utamaduni na maendeleo ya jamii
aliwahi kuwa mmoja ya watu waliopendekeza kuanzishwa kwa Taasisi ya uchunguzi wa
kiswahili ili iwe Taasisi yenye kusimamia matumizi ya kiswahili, Kwa mchango
wake katika shughuli zake kuienzi lugha ya kiswahili Taasisi ya Ukuzaji wa
Kiswahili wliamua kumtunuku cheti cha kumbukumbu ya Jubeleiya TUKI ya miaka75
tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930-2005.
Sheikh Kaluta Amri Abedi ametoa mchango mkubwa katika lugha ya kiswahili akiwa katika nyazifa mbalimbali kama ilivyo oneshwa kuwa alikuwa mwanaharakati wa kiswahili, Mshairi ambapo alitunga mashairi kwa kiswahili na kuimba lakini pia alikuwa mwandishi wa kitabu cha kanuni za kutunga mashairi,alikuwa mwanasiasa aliyetumia mwanvuli wa siasa kuendeleza juhudi za kuitukuza lugha ya kiswahili na kuendelea kuipigania itumike katika shughuli za bunge na pia shule za msingi, sekondari na hata vyuo vikuu,aliwahi kuwa karii na hata mwenyekiti wa chama cha mashairi Afrika mashariki.Wakati wote huu Sheikh Kaluta Amri Abedi alishadadia kiswahili kupewa kipeombele zaidi katika matumizi Tanzania na Afrika mashariki yote.Kwa kweli Sheikh Kaluta Amri Abedi ametoa mchango mkubwa katika kukua kwa lugha ya kiswahili anafaa kuigwa na kuenziwa na Watanzania na Wana Afrika mashariki kwa jumla