Misingi ya Uhakiki katika Fasihi ya Kiswahili
Fasihi, Uandishi na Uchapishaji (Dar Es Salaam University Press, 1993, 260 p.)
SEHEMU YA TATU: UHAKIKI |
12. Misingi ya Uhakiki katika Fasihi ya Kiswahili
T.S.Y. Sengo
Madhumuni
Madhumuni ya makala haya ni kujaribu kuitafakari dhana ya
uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili na misingi inayoitawala na kuisimamia. Katika
jaribio hilo, kutafanywa juhudi za kutoa maelezo ya dhana muhimu, kujadili
misingi iliyopo na kupendekeza mingine, kudadisi na kueleza nafasi na kazi za
mhakiki.
Maelezo
Uhakiki
Uhakiki katika Fasihi ya Kiswahili si taaluma yenye umri mkubwa.
Umri wake haufikii hata robo karne. Dhana hii ya uhakiki kwa lugha ya kawaida,
ina maana ya "upataji wa hakika au kweli ya jambo; maelezo yanayochambua
maandishi kwa kufafanua mambo mbalimbali yaliyomo."1 Upataji wa
hakika au wa kweli ya jambo unahusu ujuzi mkubwa. Ujuzi huu si ule wa kiufundi
na kisanii tu bali wa maarifa na hekima. Ajuaye ni yule mwenye uwezo wa kuona
tofauti katika vitu vya kufanana na mfanano katika vitu tofauti, imani na
itikadi tofauti, mazingira na hali tofauti, dhana na hoja tofauti, kauli na semi
tofauti, na juu ya hayo atajua kuwa akiwezacho kujua si kila kitu na kwamba juu
ya kila mwenye kujua kuna mjuzi zaidi. Hivyo maana ya uhakiki kuwa ni jitihada
ya upataji wa hakika au kweli ya jambo yanazidi kuthibitisha hoja ya wanafalsafa
kuwa kuhakiki sharti kukite katika kujua. Uhakiki hauwezekani kufanywa bila ya
kuwa kinachohakikiwa kinafahamika ndivyo. Maana haya ndiyo yatakayotawala fikira
za makala haya.
Ama kuhusu maana ya pili ya uhakiki kuwa ni "maelezo
yanayochambua maandishi kwa kufafanua mambo mbalimbali yaliyomo," ni dhahiri
kuwa ufafanuzi huo sharti ukite pia katika kujua ndaninnje ya hilo jambo
linalofafanuliwa, na fani ambayo imelipamba jambo lenyewe. Sharti iwekwe wazi
kuwa si kila ufafanuzi ni uhakiki kwani maandishi ya fasihi yana mashiko yake
mbali na yale ya maandishi mengine. Na makala haya yanashughulikia uhakiki wa
maandishi ya kifasihi ambayo ni kazi zote za kisanaa zitumiazo maneno na
viashiria mbalimbali. Na si fasihi yoyote bali Fasihi ya Kiswahili.
Uhakiki ni daraja ya juu ya maelekezo ya kisanii yenye kuwalenga
watu wa aina tatu: wasomaji wa kawaida walio majumbani na maskulini, waandishi
asilia wa kazi za sanaa, na watu wanaodhaniwa wana macho ya kuona na uwezo wa
kutenda na kuyatafakari yasemwayo kwa lengo la kutengeneza. Msomaji hupata
mwongozo wa namna bora zaidi za kumuwezesha kuifahamu kazi ya sanaa kutokana na
viwango tafauti vya uhakiki tafauti juu ya shairi, ngano, riwaya, tamthiliya,
n.k. Mwandishi hupata faraja na hamasa kutokana na uhakiki wa kazi zake, hukua
na kukomaa; wachache labda hupata homa na kuingiwa na baridi kazi zao ziwekwapo
sawa.
Uhakiki katika jadi za Kiswahili ndicho chuo kikuu cha mafundo
makuu. Mathalani, katika maisha ya kila siku, methali huwakumbusha wanajamii:
"Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu;" "Mgema ukimsifu tembo hulitia
maji," na "Haambiliki huachwa akaadhirika," n.k. Hizi ni tahakiki za Idsanaa
zinazotawala maisha ya kweli ya mja ya kila siku Uswahilini.
Kama uhaldki ni daraja kuu, ni wazi kwamba manyakanga wa chuo
hicho sharti wawe watu wa aina yake. Si kila mfafanuzi wa jambo au mpataji kweli
husibu kuwa mhakiki. Ni lazima uhakiki uwe umejikita katika ujuzi wa mtu ambave
mzingiro wake wa kimaisha umepanuka na kupevuka na dari lake la akili na fahamu
lina kina na kimo kikuu. Na ujuzi huo sharti uwe ujuzi ylio ndiwo kwa namna zote
za kuutafutia na kuupatia; sharti uwe ujuzi wa kinadharia; misingi na utendaji
kwa upande mmoja, na uwe wa umbuji mkuu kuhusu maisha ya jamii za watu na yao
yote kwani fasihi huvielezea vyote vinavyowahusu watu hao na wala haichagui vile
vya watu wasio duni wakiwa katika hadhara nyingine. Ama kwa hakika sanaa ya
uhakiki ni sanaa kubwa na nzito inayodai umri na ukomavu wa aina yake. Haya
hayako tu katika fasihi ya Kiswahili, fasihi ya Tanzania au fasihi ya Afrika tu
bali yako katika misingi ya fasihi ya binadamu wowote na popote walipo. Kwa
mfano, Thomas Cooke amepata kuandika kuwa "Ukuzaji wa ladha nzuri katika tungo
za kishairi ndio ukuzaji pia wa tabia njema." Kadhalika, "Hapana jingine
linaloweza kulishughulisha taifa mbali ya uhimizaji wa waandishi
bora."2 Ni wazi kuwa mawazo haya yanaipa sanaa ya uhakiki nafasi,
hadhi na dhima ya namna yake. Kanuni za kitu au jambo zimepewa sifa maalumu hapa
ya kwamba zinahusiana sana na ubora wa tabia za watu, jamii na ubora wa yao.
Mhakiki
Mhakild ni msanii aliyekomaa katika nadharia, misingi na
utendezi wa taalimu yake. Ni mkomavu wa kuona mengi katika sanaa
anayoishughulikia. Tafsiri azitoazo huwa ndizo na zenye kulenga kuwanufaisha
wasomaji, msanii wa kazi inayohakikiwa na hadhira kuu, yaani jamii. Ama mhakiki
hawi ni "mlimaji" wala "mgongaji" kwani hizo ni ila katika sanaa ya kitaaluma,
na si sifa kamwe. "Mlimaji" na "mgongaji" ni mtu atumiaye nguvu za mwili, sana
hasira na hisia mfanano. Mhakiki hutumia ufundi, akili na hekima Kamwe mhakiki
"halimi" wala "kugonga".
Kusifu au kulaumu tu si sifa ya mhakiki bali ni haki yake na
wajibu pia kuipima kazi kwa vigezo vyake na kusema kweli palipo ndipo. Msanii
mstahiki sifa apewe na sababu zitolewe ili sifa hizo ziwe misingi kwa kazi zote
nyingine za mithili hiyo.
Ni stahiki ya mhakiki kuitwa mwalimu kwani choyo na inda ya
kuwaua wasanii watangulizi au wengine si sifa ya mhakiki kama ilivyo kwa mwalimu
azalishaye madaktari, wahandisi na marais. Mhakiki hana gere wala tamaa ya
kutaka awe yeye tu na wengine siwo. Na kwa kuwa mwalimu huyu kapevuka vya
kutosha, upevu na ukomavu wake humpa hadhi ya mapenzi ya kweli. Ndipo Mtume
Muhammad (S.A.W.) alipomfafanua mhakiki kwa maneno yafuatayo: "Ndiye mpenzi
pekee yule ambaye atanionyesha udhaifu wangu na kunipa zawadi kwa kufanya
hivyo."3
Hivyo mhakiki ni yule na lazima awe yule ambaye huwa ni mfasiri
wa jadi ya jamii anayoiwakilisha. Kazi yake hutegemea athari za muundo wa jamii,
hisia, vigezigezi vya vionjo vya mwili, maumbile, wakati, pahala na hali nzima
ya kuwepo kwa dunia ya sanaa ya uhakiki. Mwelekeo wake huwa ule wa ndani - nnje
na wala si ule wa nnje - ndani. Jadi ya jamii moja huitawala jamii na jamii
ikajithaminisha kwayo. Na mhakiki ni mlezi wa jamii yake kwa vile aitakiavyo
kheri ya kuendelea zaidi na zaidi katika matengenezo ya vipengele vyote vya
maisha ya mja bila ya kuua mlolongo wa jadi ya sanaa wala ya wasanii. Kwa
taadhima kubwa, yafaa ikumbukwe kuwa "mhakiki ni mtu na kila mtu ana mipaka
yake."4
Fasihi ya Kiswahili
Kiswahili kwa asili ni lugha ya Waafrika walioishi pwani ya
Afrika Mashariki kwa karne na karne. Kiswahili ni Kipwani, ni lugha iliyozaliwa
kwa mchanganyiko maalumu wa lugha za Kibantu za jamii za awali ambazo
zililazimika kuwasiliana zilipokabiliana baharini au nchi kavu. Kiswahili ni
lugha ya muungano wa tamaduni kabla na baada ya majilio ya wageni. Historia hii
ya awali iliparaganywa sana na wanasiasa wateule waliojificha katika maziaka ya
utaalamu na, au umisionari.
Waarabu walipofika katika upwa wa Afrika Mashariki waliwakuta
watu na lugha zao. Kuwaita "watu wa pwani" (sawahil) haikuwa na maana ya
kuwa watu hao waliletwa na Waarabu, ama waliwazaa na wanawake weusi wa pwani
hiyo. Waliokuja kutoka kwao walibakia kuwa Waarabu, Wamanga, Washihiri, n.k., na
vizazi vyao vilivyochanganya damu viliendelea, hadi hivi leo, kuitwa Machotara.
Mswahili kabakiza weusi na Uafrika wake.
Hivyo, kanuni za lugha - wiyati na zile za kijamii, zina dalili
zenye nguvu kuwa jamii ya Waswahili wa pwani ya Afrika Mashariki isingeishi bila
ya lugha kusubiri majilio ya wageni kwa vile ni maumbile ya waja kuwasiliana kwa
kutumia lugha. Na kwa fikira za kitumwa ati Kiswahili kilikuwa zao la utumwa,
Wazungu waliwatuma Waarabu kushika watumwa Afrika Mashariki, ukanda wa Sudani,
Afrika Magharibi na kwingineko. Kwa nini basi Kiswahili kizaliwe na ubwana wa
Waarabu waliokuja pwani ya Afrika ya Mashariki tu?
Falsafa nayo inaieleza lugha kuwa ndicho chombo pekee
kinachounda na kutumia dhana. Falsafa hii inayoelezea utamaduni wa Kiswahili
yaweza pia kuielezea Fasihi ya Kiswahili kwa kuwa ni fasihi iliyojitosheleza na
kujikimu kistahiki.
Kwa hiyo, Fasihi ya Kiswahili ni taaluma ya maneno ya kisanii ya
Waswahili, ya Wapwani. Makala haya yatakitisha fikira zake katika kweli hii. Hii
haina maana kuwa madai ya kisiasa na ya kuhalalisha nafasi za kazi na masilahi
ya kimaisha, hayana nafasi. Makala haya yanaheshimu mipaka ya mtumiaji
Kiingereza na Mwingereza; mtumiaji Kichina na Mchina; mtumiaji Kinyanyembe na
Mnyanyembe; na hali kadhalika Mpogoro aliyejifunza na kukitumia Kiswahili na
Mswahili. Hii ni yakini ya kihesabu ambayo haihitaji mizengwe.
Fasihi ya Kiswahili, kwa hali hii ya pili, imekuwa na maana ya
kazi za kisanaa zilizowasilishwa kwa Kiswahili. Inawezekana kuwa na fasihi ya
Wangoni iliyoandikwa kwa Kiswahili. Sharti ionekane kweli iliyo dhahiri kuwa
Ungonini si Uswahilini ingawa miongoni mwa Waswahili, Wangoni nao walikuwemo
kama inavyozidi kujidhihirisha kuwa Wangazija wengi wa Visiwa vya Ngazija wana
asili ya Umakua, Uyao, Umakonde wa kusini ya Tanganyika na kaskazini ya
Msumbiji.
Hali hii ikiwekwa wazi, taaluma hukomaa. Ikionewa kinyaa,
taaluma huzorota. Taaluma haitaki kuficha siri. Ndiyo sababu Fasihi ya Kingereza
inafahamika kuwa ni Fasihi ya Waingereza na Fasihi kwa Kiingereza ndiyo ile
yoyote nyingine iwayo bali hutumia Kingereza ikiwa ndiyo lugha ya mawasiliano.
Na wataalamu wasionee haya fasihi zao za Kikwere, Kigogo, Kibondei, Kikerewe,
Kipare, Kihehe, n.k., kwani zikipambanishwa na ile ya Kiswahili, kila moja ni
fasihi ya hadhi yake na hapana moja iliyo bora kuishinda nyingine katika hali za
kawaida.
Wasiwasi wa baadhi ya wanataaluma wa kudhani kuwa Kiswahili
kimemeza lugha nyingine hivyo bora nao waiue asili va Kiswahili ili kila mtu awe
MswahiB hauna mashiko ya kitaaluma wala ya ukomavu wa kitaalamu. Nao
umewafikishia watafiti wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, kupendekeza kuwa jina la taasisi hapo baadaye liwe Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili na Lugha nyingine za Tanzania na Afrika; ili lugha,
tamaduni na fasihi nyingine nazo zifanyiwe kazi za stahiki zao.
Kinachosemwa katika sehemu hii ya makala ni kuwa Fasihi ya
Kiswahili ni Fasihi ya Waswahili na Uswahili wao. Kadhalika, kwa sasa, Fasihi ya
Kiswahili ina maana ya Fasihi yoyote itumiayo Kiswahili, kwa mfano kazi za
waandishi kama Aniceti Kitereza.5
Misingi
Misingi ni vigezo vikuu na muhimu vya kufanyia kazi. Kwa haja ya
makala haya, baadhi ya misingi hiyo ni pamoja na nadharia (za fasihi, jadi,
utamaduni, n.k.), ukomavu (wa kitaaluma na kiumri), ukweli na haki, uwezo wa
kisanii, mwelekeo, na lengo.
Nadharia
Mhakiki wa kazi za sanaa lazima aelimishwe na ahitimu katika
taaluma za nadharia. Kuna siri nyingi muhimu katika nadharia za kila fani. Hivyo
mhakiki anawajibika kuzimaizi kwa undani sana nadharia za fasihi
anayoishughulikia. Ama ajue kuna sanaa za jadi, taalumaratibu ya sanaa nyingine,
k.v., hadithisimulizi, thieta ya jadi (sanaa za maonyesho), methali, nyimbo,
vitendawili n.k.; na kwamba kila kimoja cha hivi kina nadharia zake. Ajue kuna
nadharia za ushairi kwa jumla na nadharia za ushairi wa Kigogo, ushairi wa
Kimasai, ushairi wa Kiingereza, kadhalika ushairi wa Kiswahili. Ajue kuna
riwaya, tamthiliya, hadithi fupi, na sanaa za muziki; na kwamba kila kimoja cha
hivi kina nadharia zake.
Nadharia ni taalumadhahania ambayo inahitaji uwezo mkubwa wa
mtu. Nadharia zina sehemu kubwa sana katika utenzi wa kitu au jambo lolote la
maana. Mwalimu Kenneth S. Goldstein amepata kuwaambia wanafunzi wake kuwa: "Bila
kupata mafunzo katika nadharia, kuna dalili za wazi kabisa kuwa mkusanyaji
(mchunguzi) hatakuwa anajua ni matatizo yepi yanahitaji utatuzi."6
Katika uhakiki wa fasihi bila kuhitimu katika nadharia, matokeo ni kuwa na watu
wanaojitia katika sanaa hiyo ili "kulima" au 'kugonga" wenzao ili nao wapate
majina. Mfano mzuri wa "ugongaji" ni ule wa mtu anayemtaka kila mtu mwingine
kuwa kama yeye au kuwa yeye kwa fikira na mwelekeo. F.E.M.K. Senkoro7
hafahamiki anadai nini katika misingi iliyowafanya kina Fr. F. Nkwera kusema
"sanaa hutoka kwa Mungu"; au ufafanuzi wa kina John Ramadhani na wenziwe
walipodai kipengele kimojawapo cha fasihi kuwa ni hisi, hadi kuthubutu kutumia
lugha ambayo kabisa haitumiki katika taaluma kwa kuuita kila mtizamo wa watu
hawa "mtizamo uliopotoka," madai ambayo yanakingana na misingi ya kitaaluma.
Kwani angeulizwa: "Wewe ni nani hasa katika fasihi hata uone sisi tumepotoka na
wewe hujapotoka?" angepata taabu kutoa jawabu. Kama alivyopata kusema Mohamed
Bakari kuwa kulithamini shairi, mara nyingine, inampasa mtu kuwa mwizi wa
ulimwengu wa faragha wa mshairi,8 ndivyo iwezavyo kusemwa kuhusu
mhakiki na ulimwengu wake wa faragha kimalezi, kiitikadi, kimwelekeo na
kitaaluma. Mhakiki ni mtu, na watu ni watu na yao. Haimkiniki wahakiki wote wawe
mtu mmoja kwa mawazo, itikadi, mwelekeo, n.k.
Hivyo nadharia ndicho kigezo kikuu cha kumwezesha mhakiki
kufanya kazi yake ya kujenga jengo la taaluma juu ya matofali ya watangulizl
wake. Anayo haki ya kujenga tofali bora zaidi lakini yu mweledi wa adabu za
kutothubutu kubomoa msingi. Umbuji wa lugha yake na uwezo wake wa usanii humpa
fursa ya kuziba ufa bila ya kujenga ukuta kwa hekima na maarifa.
Ukomavu
Katika falsafa ya elimu, kuna hoja zihusuzo "mzingiro wa maisha"
na "dari ya akili". Mambo haya mawili huenda na umri, elimu na safari za kuiga
mazuri. Umri ukizidi, elimu ikipanuka na safari dhahiriya na dhahniya zikiwa
nyingi, mtu hupanua mzingiro wake wa uzoefu katika maisha na kupandisha juu
zaidi kimo na kina cha dari yake ya akili. Maisha yanapoanza katika umri wa
miaka arubaini, kama mtu keshapitishwa katika mfumo bora wa elimu, kapata kisomo
na elimu, hususani huwa mpevu na mkomavu wa mengi. Ukomavu wa kitaaluma
utamfanya amheshimu kila mtu na kila kifanywacho na wengine. Huwa yu mweledi na
mfahamivu wa mbinu na lugha ya kutumia kurekebisha pale ambapo panastahiki. Huwa
yu mtu wa kutoa maoni yake na mara nyingi kukiri kuwa hutafautiana na maoni ya
fulani ama fulani kwa sababu za kimsingi kadhaa.
Kwa kuwa yu mtu mzima kiumri, magomvi ya kitoto ya kushikana
mashati au kumwagiana mchanga si fakhari tena ya mhakiki. Bali huwa mtu mstahiki
wa busara itakiwayo na mwandishi au mtunzi wa kazi ya fasihi, msomaji au
msikilizaji wa kazi hiyo, kadhalika na athari ya kazi kwa jamii yake, kwake
mwenyewe na kwa wahakiki wenziwe.
Ni dhahiri kuwa mhakiki anahitajika awe mpevu katika nadharia na
taaluma kwa jumla, katika misingi ya kitaalamu; na kama ana mwelekeo wa
kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi, kisanii, n.k., awe pia amekomaa katika hayo. Na
msingi wa ukomavu ndio mmojawapo'uliolipa taabu sana bara la Afrika kwa kuwa
viongozi wake wengi kwa robo karne ya mwanzo wa uhuru hawakuwa nao. Ukomavu wa
kisiasa wataka ukomavu wa kiuchumi, kielimu na kiitikadi ili Mwafrika naye
ajihisi kapevuka katika kuchangia ukweli na haki.
Nadharia na ukomavu humfanya mtu aandikapo kuhusu fasihi ya
Kigogo aanze na Ugogo wenyewe, Wagogo wenyewe, na misingi inayoutawala utamaduni
huo. Huu ni mwelekeo wa ndaninnje. Si kweli na si haki kwa mhakiki wa fasihi ya
Kiswahili kutumia nadharia au misingi ya fasihi ya Kiarabu, Kijerumani, Kichina
au Kihindi kwa kisingizio cha kuwa fasihi ni fasihi. Mja ni yuleyule popote
alipo, lakini fasihi yake ni kizaliwa cha utamaduni wa mazingira yake. Si vibaya
kuanza na ndani mwa Mswahili kabla ya kumpambanisha na ndugu yake wa "ubantuni"
au "ubinadamuni". Kwa mfano, undani wa mpwani ni pamoja na athari za bahari na
itikadi zote zitawalazo maisha yake; dini yake. Mpwani haoni haya kukiri ana
Mwenyezi Mungu mwenye uwezo na nguvu, na kwamba mbele yake, yeye Mswahili si
lolote si chochote; kwamba maisha mazima ya mja ni upuuzi, hayana maana ila kwa
mtu afanyaye ibada na kazi za kuzalisha na kubadilisha hali ya kiuchumi,
kisiasa, kijamaa na kuleta amani miongoni mwa watu. Kucha Mwenyezi Mungu ni
adili la maisha, halina kusoma ama kutokusoma. Tambiko, jando, unyago, n.k., ni
sehemu ya jadi ambayo hubadilika kidogokidogo kwa athari za wakati, maendeleo,
n.k. Na kila kimoja katika hivi kina kanuni za mashiko ambazo mhakiki wa
mwelekeo wa ndaninnje sharti aziheshimu.
Makala haya yanadai kuwa kweli isemwe na haki ifanywe kuhusu
kazi za fasihi. Mwandishi anayeimba nyimbo za kimapinduzi sharti atazamwe yeye
mwenyewe alivyo na anavyoishi. Je, yeye mwenyewe ni mwanamapinduzi anayeyajua
mapinduzi? Si mnafiki anayetaka labda kuuza maandishi yake katika soko maalumu?
Au katili linalotaka kuua watu kwa jaribio lake la siasa? Jamii ya mwandishi
itazamwe jinsi inavyompokea na kumthamini mtu huyo. Nayo ipimwe kama kweli inao
uwezo wa kumjua mtu aliye ndiye na mtu asiye ndiye. Je, mwandishi huwachezea
shere watu wake kiasi gani? Kama yu avaa kindenga, chatosha kumtia katika
uwanamapinduzi? Kama yu avaa baraghashiya, yatosha hiyo kumtia katika kundi la
waumini? Elimu yake je? Uwezo wake je? Familia yake je?
Hatua hii huenda ikaonekana imechupa mipaka ya kitaaluma na
kuingilia mambo ya Idbinafsi. Mwono huo ni wa kitaaluma ambao umetoka
nnje ya tamaduni za Kiafrika. Ni mwono wa nnjendani. Uafrikani na
Uswahilioi, mtu huthaminiwa kwa vile alivyo mzimamzima. Na mhakiki
anapoitathmini kazi ya fasihi sharti aitazame kweli na haki katika
ukamilifu wake.
Uwezo
Uwezo wa kisanii katika uhakiki ni jambo la msingi sana. Mhakiki
wa riwaya, kwa mfano, si lazima sana awe mwanariwaya yeye mwenyewe, lakini yafaa
awe msomaji wa riwaya nyingi sana. Awe ni mpenzi, mtafiti na mtu wa kuzitafakari
riwaya. Awe mjuzi wa vigezo na misingi ya riwaya. Ajue riwaya ni nini, miundo na
mitindo mbalimbali, wahusika na matukio mbalimbali, tamathali za usemi ambazo
ndizo ziko katika uhalisia wa jamii inayohusika. Kadhalika mhakiki wa tamthiliya
au wa mashairi, tenzi, ngonjera, nyimbo, n.k. Kanuni za kila fani ya fasihi
sharti zipewe nafasi na haki yake. Uwezo hupatikana kwa ari, mafunzo, ukomavu,
uzoefu, na kukubali kuoneshwa njia. Nao hukua kadiri ya mhakiki akuavyo. Kwa
mfano, kina Kiango9 wa juzi si sawa tena na wa leo. Na kila mhakiki
wa kweli hupigania kukuza uwezo wake siku hadi siku.
Mwelekeo
Baadhi ya wapitiaji au wachambuzi hupenda kuwa na "misimamo"
katika kazi zao. Kwa daraja ya mhakiki, kuwa na ndoto hiyo ni hasara. Msimamo
huwapo katika mijadala ya kishule au labda ya kisiasa. Na mtu sharti asi-mame
alipo ili apiganie upande wake. Mhakiki yeye ni mtoa hoja na sababu. Hoja zake
na sababu zake zionyeshwapo zinatafautiana na za wengine, mhakiki mkomavu
hujifunza haraka iwapo atatosheka na sababu ya kubadili au kuongezea hoja maoni
yake. Kigeugeu cha mhakiki si ila: ni sifa mradi tu aseme wazi kuhusu mabadiliko
hayo. Ni dalili ya kukua na kuendelea.
Mwelekeo huathiriwa sana na mazingira, malezi, nadharia, na
ukomavu wa mtu. Katika Fasihi ya Kiswahili, mhakiki hana nafasi ya kuelekea
kwenye dharau au matusi dhidi ya dini kwani utamaduni wa fasihi hiyo umejikita
katika imani nzito ya kuwako kwa Mwenyezi Mungu mmoja, mitume, malaika, n.k.
Uyakinifu katika fasihi hiyo ni ule wa asilimia kwa mia wa ki-Mungu-mungu; kweli
ambayo haishindani wala kulinganishwa na udhanifu wa kisayansi ambao bado
binadamu anaufanyia kazi. Mifano ni kanuni za maumbile na kanuni za matokeo ni
yakini isiyotoa. Udhanifu wa "atom" iliyosemwa ni chembe ndogo isiyoweza
kubabadilika, leo si "atom" tena, ni "neutron".
Kinyumenyume cha matumizi haya ya uyakinifu na udhanifu
kimekusudiwa kuonyesha kwamba kuna haja ya kuzama zaidi katika mambo kabla
wahakiki hawajayapamia.
Na viwe viwavyo, mja katika ukamilifu wake haishi kwa
mkate tu. Hivyo mielekeo ya uhakiki isiwakanganye wahakiki hadi wakafika
kuparaganyika. Mradi washenzi na waungwana wamo maishani pamoja, watake
wasitake, sharti wahakiki washirikiane kwani huo ndiwo mtihani waliopewa. Na
wahakiki wa Ki-Marx au Ki-Mao sharti wathamini kazi za wahakiki wenzao ambao
fikira zao zimekita kwa "Baba Mtakatifu" au kwa "Muhammad (S.A.W.)" au
"Mizimuni", n.k. Vinginevyo wataulizwa: "Nyinyi ni kina nani kudai haki ya kuwa
wahakiki bora kutushinda sisi ati kwa kuwa tunatafautiana mielekeo? Marx na Mao
wana ubora gani wa kumshinda Yesu na Muhammad?"
Lengo
Lengo la mhakiki ni kujaribu kutumia uwezo wake kusaidia
kuifahamisha kazi anayoihakiki kwa mtu aliyeiandika na kwa msomaji. Katika
jaribio hili, mhakiki akiwa mwalimu, atakosoa penye kustahili na kuelekeza penye
kustahiki. Sifa za wazi atazisema ili wengine wapate kuziiga pindi waonapo
zawafaa. Ila nazo zitaonyeshwa ili mwenye nazo aziache na asiye nazo aziepuke.
Mradi lengo la mhakiki litabakia kuyatengeneza mambo yawe na yazidi kuwa mazuri.
Huu ni wajibu wao kama anavyodai Abdilatif Abdalla kuwa: "Na itakuwa ni wajibu
wao kuyasahihishamakosa yaliyokwisha fanywa.na hao waliotangulia."10
Na watayafanya hayo kitaaluma na kihaki-liliahi, yaani kikwelikweli na kwa
uaminifu mkubwa sana.
Nafasi na Kazi ya Mhakiki wa Fasihi ya Kiswahili
Nafasi
Ni jambo la mantiki kwamba mhakiki ni kiungo cha lazima katika
fasihi yoyote iwayo. Haingekuwa kinyume cha hivyo kuwa katika fasihi ya
Kiswahili mhakiki hana nafasi, haiyumkiniki. Nafasi yake inahitajika zaidi kwa
vile taaluma hii haina umri mkubwa baada ya kuwa imeanza katika miaka ya 1970.
Mzee John Ramadhani na Farouk Topan ni miongoni mwa waasisi wa uhakiki katika
Fasihi ya Kiswahili. Athari ya kazi zao ndiyo iliyowazaa akina Kiango na Sengo
wa siku za uchanga wao, na vijukuu akina Mulokozi na Senkoro; na Mbunda Msokile
ambaye kawa mchambuzi mkuu wa vitabu redioni na kwenye magazeti, hasa
Kiongozi. Ni wazi kuwa mhakiki bado anahitajika sana na ataendelea
kuhitajika sana. Kwani yeye ndiye mwalimu na kiungo cha kazi ya fasihi na jamii
iliyokusudiwa kinyume na wazo kwamba "sanaa yaweza kujisemea
yenyewe".11 Yaweza kweli, lakini sanaa hiyo sharti iwe pamoja na
usanii wa mhakiki.
Kazi
Mwanafunzi wangu A.G.N.M. Gibbe, katika makala yake ya "Dhima ya
Mhakiki"12 amesema ya kutosha. Kiasi kikubwa kaathirika na nyimbo,
mavazi, hamasa na hata fakhari za uwanamapinduzi ambao ulishika sana Afrika
Mashariki na Kati katika miaka 1965/80. Katika Tanzania, uwanamapinduzi
uliofasiriwa na vijana wasomi ulihusu sana jitihada za kina Mao za kukana
uunguungu na kuhimiza uunguwatu. Wachina baada ya Mao wamerudisha imani zao kwa
Mwenyezi Mungu na wanamapinduzi wa Tanzania waliendelea kwenda kuabudu siku za
Jumapili, na walio wakaidi sana hawakuacha kumtaja Mungu waliposhikwa na gego au
malaria. Wengine wengi walibakia na Mwenyezi Mungu wao mmoja na mkweli daima.
Hii haina maana kuwa hapajakuweko wanamapinduzi wa kweli ambao tamaa zao, sala
zao na juhudi zao ni kuyatendea haki, kweli na kazi maisha ya jamii zao ili
mabadiliko ya hali katika elimu, uchumi, siasa (ukweli, upole, uammifu n.k,), na
vipengele vyote vya maisha ya kila siku yawe yakidhihirika kwa kila mwananchi,
na pasiwe mmoja akawa anadai hadiya za kuwa mbele ya wenziwe. Hivyo basi baadhi
ya kazi za mhakiki ni pamoja na:
(i) Kuchambua na kuweka wazi funzo ambalo linatolewa na kazi ya asihi.
(ii) Kuchambua na kufafanua picha za kisanii zilizotumika katika kazi ya fasihi.(iii) Kumshauri mwandishi ili afanye kazi bora zaidi.(iv) Kumuelekeza msomaji ili apate faida zaidi kuliko yale ambayo angeweza kuyapata bila ya dira ya mhakiki.(v) Kuhimiza na kushirikisha fikira za kihakiki katika kazi za fasihi.(vi) Kuweka, kubakiza, na kukuza kiwango cha utunzi na usomaji wa kazi za fasihi.(vii) Kuonyesha kuwa kwa kila kizuri kuna kizuri zaidi na hapana kizuri kisicho dosari.(viii) Kutafiti na kuweka sawa nadharia za fasihi teule.(ix) Kusema kweli ipasayo kuhusu tamaduni na falsafa zinazotawala fasihi.(x) Kuheshimu na kuthamini kazi za waandishi kwa kuzifanyia haki, n.k.
Maoni
Makala haya kwa jumla yamejaribu kupendekeza mambo kadhaa
yanayomhusu mhakiki. Mwandishi wa awali wa kazi za fasihi hakupewa nafasi sana.
Kiwango cha mapitio na uchambuzi wa kazi za fasihi, ambacho kimekuwako tangu
fani hii ilipoanza katika fasihi ya Kiswahili, kimesemwa hakitoshelezi sifa za
kiwango cha uhakiki. Ni maoni ya mwandishi wa makala haya kuwa mhakiki wa fani
ya fasihi sharti awe amesoma siyo nadharia na kazi kadhaa za fasihi tu bali pia
sharti awe amehitimu katika taaluma za falsafa ya fasihi, falsafa ya sanaa kwa
jumla, na katika nadharia za uhakiki na uzoefu wa utendezi wa kazi hiyo.
Kazi, karibu zote zilizochapishwa, zinahusu uchambuzi wa kazi za
fasihi ambazo zinasomwa maskulini. Hivyo lengo kuu ni kujaribu kuzieleza na
kuzifahamisha kazi hizo kwa wanafunzi na kwa walimu wao. Mwalimu John Ramadhani,
Mwalimu Farouk M. Topan, baadaye akina Saifu Kiango, na kufuatiwa na kina
Mwalimu Mwarabu Mponda, Mwalimu M. Mulokozi na F. Senkoro - wote hawa
wamezielekeza kazi zao kwa wanafunzi na walimu wao, iwe ni shuleni, vyuoni au
vyuo vikuu. Kwa mawazo yaliyokusudiwa karatasini humu, wote hao wamekuwa
wakifanya kazi za uchambuzi, ufafanuzi, usaili, upitizi, na sanaa za ualimu.
Uhakiki wataka kiwango cha juu zaidi cha uandishi wa kazi za
fasihi, k.v., Siku ya Watenzi Wote, Kusadikika, Mashetani, Jogoo
Kijijini, na mifano ya hizo; ukomavu wa hali ya juu katika taaluma,
nadharia, falsafa, maisha na uwezo wa kupima na kuamua haki. Lengo liwe ni
kuzihakiki kazi hizo kwa ajili ya wahakiki wapevu ili nao wazihakiki kwa upevu
huo.
Hitimisho
Makala yamejaribu kujadili dhana na misingi ya uhakiki wa fasihi
ya Kiswahili. Fasihi hii ni ya upwa wa pwani ya Afrika Mashariki, na ina umri
mkubwa na athari nyingi za maingiliano ya jamii. Hivyo mhakiki wa kazi zote za
fasihi hii sharti aujue na kwa kiasi kizuri authamini utamaduni wake ambao ni
pamoja na dini za jamii, itikadi na imani zao, falsafa na mielekeo yao, kanuni
na ada zao, ushenzi na uungwana wao, n.k.
Makala yamehimiza utafiti katika fasihi ya Kiswahili na fasihi
za Kimakonde, Kirangi, Kiziguwa, Kikae, Kitumbatu, n.k., ili uhakiki uwe unapiga
ndipo.
Fasihi ya Kiswahili, kwa maana ya fasihi ya Kigogo kwa lugha ya
Kiswahili, au fasihi ya Kimbulu kwa lugha ya Kiswahili, ina nafasi kubwa katika
malezi na elimu ya taifa hili. Muhimu, mhakiki lazima aseme ni fasihi ya watu
fulani anayoishughulikia.
Mwisho wa yote, makala yamesema kuwa uhakiki ni usanii mpevu
sana unaohitaji kula chumvi nyingi katika mengi. Nao umejikita katika kweli na
haki, na usafi wa nia. Na kwa mapendekezo yaliyotolewa, kuna matumaini kuwa
taaluma hii itakuzwa na kukomazwa.
Tanbihi
1. TUKI (1981) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford
University Press, Dar es Salaam, uk. 196.
2. Terry Eagleton (1984) The Function of Criticism.
London, uk. 14 (tafsiri yangu).
3. Mtume Muhammad (S.A.W.) Katika Kauli zake thabiti za
Hadithi za kuaminika.
4. A.G.N.M. Gibbe (1978) "Dhima ya Mhakiki" katika Mulika
12. TUKI, Dar es Salaam, uk. 5.
5. M.M. Mulokozi na D.P.B. Massamba (wh.) (1984) Kiswahili 51/1
& 51/2. TUKI, Dar es Salaam, uk. xi.
6. Kenneth S. Goldstein (1964) A Guide for Field Workers in
Folklore. Folklore Associates. Pennesvlvania Inc., uk. 17.
7. F.E.M.K. Senkoro (1982) Fasihi. Press and Publicity
Centre, Dar es Salaam, uk. i.
8. Mohamed Bakari (1981) "Swahili Islamic Literature and Westem
Literary Critics". Unpublished paper presented at the Conference of the Nile
Valley Countries. IAAS - University of Khartoum, uk. 15.
9. S.D. Kiango na T.S.Y. Sengo (1973) Hisi Zetu, TUKI Dar
es Salaam; Ndimi Zetu (1974) Longman, Tanzania Ltd., Dar es Salaam.
10. Abdilatif Abdalla (1975) "Utangulizi" katika T.S.Y. Sengo.
Shaaban Robert. Longman Tanzania Ltd., Dar es Salaam, uk. xxv.
11. Eagleton,k.h.j., uk. 42.
12. Gibbe,k.h.j., kur.
2-8.