Misingi ya Uhakiki katika Fasihi ya Kiswahili
Fasihi, Uandishi na Uchapishaji (Dar Es Salaam University Press, 1993, 260 p.)
SEHEMU YA TATU: UHAKIKI |
11. Mhakiki, Uandishi na Jamii
J.L. Mbele
Tumezoea kumfikiria mhakild kama mtu anayehusika sana na ukuaji,
ustawi, na ueneaji wa fasihi na kazi zingine za sanaa. Lengo la makala haya ni
kuichunguza fikra hiyo, ili kujaribu kuielewa zaidi nafasi ya mhakiki katika
uandishi na jamii.
Njia moja ya kuielewa nafasi ya mhakiki katika uandishi ni
kuitafiti historia ya uhakiki, kujaribu kuelewa jinsi mhakiki alivyojitokeza
kama mtaalamu wa fasihi, tofauti na msanii mwenyewe. Swali muhimu hapa ni, je,
wahakiki walikuwepo tangu fasihi ilipoanza? Yaelekea kuwa wahakiki kama kundi la
watu tofauti na wasanii wenyewe hawakutokea wakati ule fasihi ilipoanza.
Walitokea baadaye. Kabla ya wahakiki kuwepo, wasanii wenyewe ndio waliokuwa
wahakiki. Hadi leo, wasanii hawajaacha kuwa wahakiki. Katika kuitunga kazi ya
sanaa, msanii hujiuliza maswali, hujikosoa, na hivyo kuirekebisha kazi yake,
mpaka anaporidhika nayo. Mara kwa mara msanii huishia kutoridhika na kazi yake,
akaizuia isionekane na jamii, na pengine huiharibu kabisa na kuitupilia mbali.
Kwa upande mwingine, jamii nayo daima imekuwa ni mhakiki wa kazi za sanaa.
Wanajamii huihakiki kazi ya sanaa kulingana na viwango vyao mbalimbali. Ni wazi,
basi, kuwa wadhifa wa mhakiki umeshikiliwa tangu zamani na watu wote wahusikao
na kazi ya sanaa, na sio wahakiki peke yao. Msanii na jamii nao ni wahakiki;
jambo hilo lafaa kuzingatiwa, maana linapuuzwa au kusahauliwa.
Kutokea kwa kundi la wahakiki ambao walikuwa tofauti na wasanii
lilikuwa ni zao moja la maendeleo ya mgawanyiko wa kazi katika jamii. Historia
ya mgawanyiko huu ni ndefu, na hatuwezi kuijadili hapa, lakini ndiyo
iliyosababisha kuwepo kwa wanasayansi, wanafalsafa, wahunzi, waandishi, wahakiki
na kadhalika. Mgawanyiko huu bado unaendelea. Hata katika uwanja wa uhakiki
wenyewe tunaona maendeleo ya mgawanyiko huu; leo tunao sio tu wahakiki, bali pia
wahakiki wa wahakiki. Hata wakati mwingine husemekana kuwa wahakiki ni wengi
kuliko waandishi.
Kundi la wahakiki lilitokea likiwa na shughuli ya kuichambua
kazi ya sanaa na kutoa nadharia ya sanaa yeyewe. Kwa kuwa watu hao walipata
uzoefu mkubwa katika kazi hiyo, walifanikiwa kutoa mawazo mengi muhimu kuhusu
kazi za sanaa, na pia kuitajirisha nadharia ya sanaa. Mhakiki wa kale wa
Kigiriki, Aristotle, alifanikiwa kutoa nadharia kuhusu sanaa za ushairi na
tamthilia kwa kuzichunguza kazi za sanaa za wakati wake. Kwa mfano, kwa
kuzichunguza tendi za msanii maarufu Homer, aliweza kutoa nadharia juu ya tendi
- muundo wake, namna zinavyowasilisha mawazo, hisia na dhamira zake, na namna
zinavyowaathiri watazamaji.1
Hata hivyo, kuzuka kwa wahakiki, watu ambao si wasanii, watu
waliojiweka baina ya msanii na jamii kwa madhumuni ya kuieleza kazi ya sanaa kwa
jamii, kulizua masuala ya kutatanisha. Tatizo moja lilikuwa lile la
kujihalalisha. Je, mhakiki ni mtu anayehitajika kweli, au amejipachika tu hapo
alipo? Ni kweli kuwa anamsaidia msomaji? Kama jibu ni ndiyo, kwa kiwango gani?
Wahakiki wanasema kuwa wanamsaidia pia mwandishi. Je kuna ukweli katika rai
hiyo? Wahakiki wanasema kuwa wao ni kiungo kati ya mwandishi na jamii. Swali ni,
je, bila kuwepo hao wahakiki, uhusiano kati ya mwandishi na msomaji ungezorota
au kupotea kabisa? Maswali kama haya yamewakera wahakiki, na kuwafanya wajaribu
kujihalalisha. Hata kule kujiuliza au kuyajadili maswali kama hayo sio jambo la
kawaida kwa wahakiki. Kimya hiki nacho ni mbinu ya kujipatia nafasi ya heshima,
maana kuyajadili maswali hayo kungeweza kutoa mambo hadharani juu ya nafasi ya
wahakiki ambayo wahakiki wenyewe hawangependa yatoke.
Juhudi za kujihalalisha zimewafanya wahakiki wafikie hatua ya
kudai kuwa wao ni muhimu au wajuzi zaidi kuliko hata waandishi najamii. Wahakiki
wamefikia hatua ya kujisema kuwa wao ni waalimu wa msanii na msomaj Mawazo ya
aina hiyo yametolewa na mhakiki maarufu wa Kirusi, Lunacharsky, ambaye anasema
kuwa mhakiki bora zaidi ni yule wa ki-Marx. Anasema kuwa mhakiki wa ki-Marx "kwa
kiasi kikubwa ni mwalimu... katika kujaribu kumfundisha mwandishi ifaavyo,
mhakiki wa ki-Marx lazima pia amfundishe msomaji. Naam, msomaji lazima
afundishwe kusoma."2
Lunacharsky anamwona mhakiki kama huyu kuwa ni mtu anayetuta
hadharisha kuhusu sumu inayonoga, anayetuvumbulia vito vilivyofichika, na
kadhalika.3 Kwa misingi hiyohiyo Fikeni Senkoro, mhakiki anaveonekana
kuathiriwa na mawazo ya Lunacharsky. anasema:
Mhakiki huifunza jamii namna ya kupokea na kuifurahia kazi ya sanaa na uandishi. Kazi ya sanaa ya uandishi ni kama chakula kilichokwishapikwa na kuungwa vizuri. Uhakiki ni sehemu mbalimbali za ulimi zenye kuifanya jamii iukubali utamu wa chakula hicho, iuchukie uchungu wa chakula hicho au ukali, na iugundue utepetepe wa chakula hicho4
Maoni hayo ya Lunacharsky na Senkoro ni ya kuwatukuza wahakiki
kupita kiasi. Mtu anaposikia maneno hayo anaweza kudhani kuwa mwananchi wa
kawaida akishanunua riwaya au kazi nyingine ya fasihi huzunguka au hupaswa
azunguke huko na huko akimtafuta mhakiki wa kumsomesha kazi hiyo. Ukweli ni
kwamba yeyote anayenunua riwaya kama hiyo hujikalia chini akajisomea. Kila
msomaji ana uwezo wa kuielewa kazi ya fasihi, ingawa namna ya kuielewa huwa ni
tofauti kwa wasomaji mbalimbali. Wananchi wa kawaida hawasomi tahakiki zetu.
Aghalabu tahakiki hizo hazina ladha kama kazi zenyewe za fasihi. Kutokana na
hali hii, sisi wahakiki tunalazimika kutumia mabavu kuwafanya raia wasome
tahakiki zetu. Raia hao ni wanafunzi wa fasihi, a'mbao hawana njia ya kukwepa
balaa hilo, maana wanatarajia kufaulu mitihani ili wasonge mbele kijamii katika
mfumo huu wa kibepari tunamoishi. Hata kama mhakiki binafsi hatumii mabavu,
mfumo wa elimu unatekeleza jukumu hilo barabara.
Wazo la kuwa mhakiki humfundisha msomaji kuielewa na kuifurahia
kazi ya fasihi linaleta picha ya kuwa maana ya kazi ya fasihi imejificha ndani
ya kazi hiyo, na kuwa mhakiki ndiye bingwa wa kuitoa maana hiyo humo
ilimojificha ili watu wa kawaida waweze kuiona. Kumbe maana ya kazi ya fasihi
sio kitu kilichokwisha kutengenezwa na kufungiwa katika kazi hiyo ya fasihi.
Maana ya kazi ya fasihi hutokea pale msomaji anapoisoma, ni zao la juhudi ambayo
msomaji huifanya wakati anaposoma kazi hiyo. Ndio maana kazi moja ya fasihi huwa
na maana mbalimbali kwa wasomaji mbalimbali. Kila msomaji huweza kupata maana
fulani kutokana na upeo wa mawazo yake, uzoefu wake wa kusoma kazi za fasihi,
itikadi yake, hisia zake, na kadhalika. Kusema kuwa kazi ya fasihi ni kama
chakula kilichokwishapikwa ni kuitweza dhana ya fasihi. Kazi ya kuisoma fasihi
sio kazi ya kula tu, bali ni ya kupika pia. Kutokana na mambo hayo, tunaweza
kuona kuwa maana anayoiona mhakiki katika kazi ya fasihi ni moja tu kati ya
maana zinazoweza kuonekana. Wala hatuwezi kusema kuwa anachokiona mhakiki ni
sahihi au bora zaidi kuliko yale yote ambayo jamii huona. Kimsingi, mhakiki ni
mmoja tu kati ya wasomaji.
Wazo la kuwa wahakiki ni muhimu sana na waalimu wa mwandishi na
msomaji limeota mizizi sana. Waandishi wengi mashuhuri hukubali kuwa ni wahakiki
ni waalimu wa waandisni. Abdilatif Abdalla, mshairi maarufu wa Kiswahili,
anakubaliana na Senkoro kuwa mhakiki ni mwalimu wa mwaiidishi na wa msomaji.
Anasema kuwa ingawa mshairi anafahamu sana katika nafsi yake taratibu anazofuata
katika kuandika shairi lake, anaweza kushindwa kabisa kuzieleza taratibu hizo;
bali "mhakiki aliye mwelewa wa kazi yake ataweza kuziona bila ya taabu kubwa;
pengine hata aweze kumtoa kombo mtunzi mwenyewe."5 Abdilatif Abdalla
anakubaliana na Senkoro pia kuwa kazi ya sanaa ni kama chakula, na kuwa jukumu
la mhakiki ni kumsaidia msomaji kukila chakula hicho.6
Wasanii wengi hawana wazo la kuwa mhakiki ni mwalimu wao. Wengi
hujitambua kuwa wao ndio waalimu. Wazo hilo limeelezwa vizuri na msanii wa
fasihi simulizi, yeli Mamoudou Kouyate wakati wa kusimulia utendi wa Shujaa
Sundiata.
Mimi ni yeli. Ni mimi, Yeli Mamoudou Kouyate, mwana wa Bintou Kouyate na Yeli Kedian Kouyate, bingwa katika sanaa ya kusema... Nilipata ujuzi wangu kutoka kwa baba yangu Yeli Kedian, ambaye aliupata toka kwa baba yake; historia haina kisichojulikana kwetu; twawafundisha wajinga kiasi kile tu tunachoamua kuwafundisha. kwani ni sisi tunaotunza funguo za milango kumi na mbili ya Mali7
Mwanahistoria D.T. Niane anatueleza kuwa "milango kumi na mbili
ya Mali" anayoitaja msanii huyu ni majimbo ya mwanzo kabisa ya himaya ya
Mali.8 Maneno hayo ya Yeli Kouyate yanatuonyesha msanii anayejitambua
kuwa yeye ndiye mwalimu. Ni maneno yanayoonyesha kujiamini kwa msanii na
kujivunia ujuzi wake. Hatusikii lolote kuhusu mhakiki hapo. Uhusiano uliopo ni
ule tu baina ya msanii na wasikilizaji wake.
Naye Chinua Achebe, mwandishi wa Nigeria, anasema kuwa anaiona
kazi yake ya uandishi kuwa ni ile ya kuwa mwalimu wa jamii yake, jamu
iliyodunishwa na kupotoshwa na ukoloni. Lengo lake ni kuifanya jamii hiyo
ijitambue tena na kujiamini.9
Wahakiki kama Lunacharsky na Senkoro wanakubali kuwa mwandishi
ni mwalimu, lakini bado wanampa umuhimu zaidi mhakiki. Senkoro anasema: "Japo
mwandishi ni mwalimu pia, lakini yeye ni mwalimu wa jamii tu. Mhakiki anao
ualimu kwa jamii na pia kwa mwandishi".10
Tatizoni kuelewa kwa nini au kwa vipi wahakiki wamejitukuza
kiasi hicho, hata kuwateka mawazo baadhi ya waandishi ili nao waukubali utukufu
huo wa wahakiki. Yawezekana kuwa kujitukuza huko kwa wahakiki kumetokana na hali
ya kisaikolojia ya kujitambua kuwa wao ni tasa, hawazalishi fasihi; kuwa wao ni
duni wakilinganishwa na waandishi ambao ndio wanaosababisha fasihi kuwepo.
Haikosi kuwa wahakiki hujitambua kuwa wao humtegemea mwandishi kama kupe
amtegemeavyo kiumbe mwingine. Bila waandishi, kuwepo kwa wahakiki kungekuwa
mashakani, lakini waandishi wanastawi hata bila wahakiki kuwepo. Kisaikolojia,
hali hii ya kujitambua kuwa ni duni au dhaifu yaweza kusababisha tabia ya ugomvi
au kujitukuza kwa huyo anayejiona duni. Kujitukuza kwa wahakiki kunaweza kuwa na
misingi hiyo.
Kujitukuza kwa wahakiki kunaweza kuelezwa kwa namna nyingine
pia. Ninamwunga mkono Anthony Cronin aliyesema kuwa kazi ya uhakiki lu namna ya
kujitafutia madaraka. Cronin anasema pia kuwa kazi bora za fasihi hazisababishwi
na mawaidha ya wahakiki. Kwa maneno yake mwenyewe,
criticism is of course...a kind of politics, an attempt to escercise power. It is impossible to remember an important instance where what apoet did was a result of what a critic (who was not also a poet and usually a friend) said.11
Katika juhudi hizo za kujihalalisha, kujitukuza, na kujitatutia
madaraka, wahakiki wametunika mambo ambayo yanaweza kuwapunguzia hadhi. Kama
nilivyodokeza, sio kawaida kwa wahakiki kujadili suala la umuhimu wao katika
uandishi kinaganaga. Hawakuthubutu kukubali kuwa hata bila wao kuwepo, fasihi
ingendelea kustawi. Kukubali ukweli huo ni kujimwagia unga wao.
Kama nilivyodokeza pia, kimsingi mhakiki ni mmoja tu kati ya
wasomaji. Hatuna ushahidi wa kuwa lile analosema mhakiki kuhusu kazi ya fasihi
ndilo pekee sahihi, au ndilo sahihi kuliko wanayosema wengine. Hatukatai kuwa
mhakiki mwenye uzoefu anaweza kuwa na upeo mpana sana kuhusu kazi ya fasihi,
hasa kwa kuwa anaweza kuilinganisha kazi hiyo na kazi zingine za fasihi. Lakini
hata hao wahakiki maarufu wanakuwa na upungufu wa namna fulani. Kwa mfano,
mhakiki maarufu wa ki-Marx, Georg Lukacs, alizipenda kazi fulani tu za fasihi,
za wakati uliopka, na wala sio zile za kimajaribio za wakati wake. Alizithamini
zile alizoziona zina uhalisi wa kihistoria na kijamii. Jambo hilo lilisababisha
kutokubaliana kati yake na mhakiki mwingine, ambaye pia ni msanii maarufu,
Bertolt Brecht. Brecht alikuwa na fikra za kuzithamini hata zile kazi zenye fani
na miundo ya kimajaribio. Tunaona kuwa Lukacs alikuwa na upeo finyu kuhusu
fasihi. Mhakiki mwingme mashuhuri, F. Leavis, naye alikuwa na ufinyu huo,
alizithamini kazi za fasihi za watu fulani tu, akaziona ndio fasihi halisi ya
Kiingereza. Waandisbi wengi wa Kiingereza hakuwathamini.
Yawezekana pia kuwa wakati mwingine wahakiki hawazitambui au
kuzisoma kazi fulani za fasihi. Huu nao ni upungufu. Kushindwa huku kwa wahakiki
kuzihakiki kazi zake za fasihi kulimfanya mwandishi maarufu wa Ireland, George
Bemard Shaw, aamue kuchapisha tahakiki alizoziandika yeye mwenyewe juu ya kazi
zake.12
Ingawa wanadai kuwa wao ni waalimu wa mwandishi na msomaji,
wahakiki mara kwa mara huwa na mawazo yaliyopotoka. Chinua Aehebe amewashutumu
sana wahakiki wenye mawazo ya kikoloni, ambao wanawabughudhi
waandishi.13 Naye Wole Soyinka amewashutumu wahakiki wanaopiga kelele
kuwa mwandishi aiandikie jamii wakati wao wenyewe hawajiulizi wanamwandikia
nani. Soyinka anadokeza kuwa mara kwa mara wahakiki hao huwaandikia watu wa
kiwango chao ili wapate umaarufu na kupandishwa vyeo katika vyuo
vikuu.14
Mamboyote hayo yanatuonyesha kuwa wahakiki sio miungu. Mhakiki
Tigiti Sengo amewahi kusema kuwa:
Mhakiki si Mungu wa kusema kila kitu ili wengine wafuate. Hata Mungu katuheshimu sisi binadamu kwa kutuacha huru kuchagua na kujua baya na zuri. Hivyo, lazima pia ajue jinsi anavyoweza kuzungumza katika uhakiki wake na wasomaji wake. Haja na kusudi ni kupanua na mawazo wala si juu ya mtu mmoja kuwatawala kimawazo wengine.15
Katika mazingira ya leo, ambayo ni ya mfumo wa kibepari, mhakiki
anajikuta katika hali ambayo hairidhishi, ingawa yeye mwenyewe anaweza
asiitambue. Karl Marx na Frederick Engels walisema kuwa ubepari ulipojiimarisha
umeangusha hadhi ya aina mbalimbali za kazi. Himaya ya fedha, ambao ndio
ubepari, imewafanya watu wanaofanya kazi mbalimbali kuwa ni vibarua tu wa
kulipwa. Hata mambo kama ndoa, ambayo twayaona yana heshima sana, yamegeuzwa na
kuwa mambo yanayotawaliwa na fedha.16 Wazo hilo limejadiliwa namna
hiyohiyo na wanafalsafa kama Georg Lukacs 17 na Theodor
Adorno.18 Akizungumzia uhakiki, Adorno anasema kuwa katika mazingira
ya ubepari, kazi ya mhakiki imekuwa ni ile ya kutangaza bidhaa, maana kazi za
fasihi zimegeuzwa na ubepari kuwa ni bidhaa. Mhakiki amekuwa ni mchuuzi wa hizo
bidhaa, hali ambayo imeangusha hadhi yake.19 Kwa kuzingatia hoja
hiyo, tunaona kuwa kuna jukumu la kuikwamua kazi ya uhakiki na uandishi kutoka
katika mfumo wa kibepari, ili waandishi waweze kupumua kwa raha na kuandika
kufuatana na uhalisi wa hisi zao badala ya kuvutwa na soko la bidhaa kama ilivyo
sasa, ili pia wahakiki waweze kurudia hali yao ya kuwa watafiti wenye kuipenda
fasihi na wenye lengo la kushirikiana na waandishi na jamii ili wote tuweze
kuifahamu na kuifurahia zaidi fasihi.
Marejeo
1. Aristotle (1985) On Poetry and Style, kimefasiriwa na
G.M.A. Grube. The Bobbs - Merrilt Company, Inc., Indianapolis.
2. Anatoly Lunacharsky (1973) On Literature and Art.
Progress Publishers, Moscow, uk. 18 - 19.
3. Lunacharsky, uk. 19.
4. F. Senkoro (1973) "Ndimi na Hisi za Wahakiki", Kioo
cha Lugha, 3 uk. 5.
5. Abdilatif Abdalla (1975) "Utangulizi" kwa T.S. Sengo,
Shaaban Robert: Uhakiki wa Maandishi Yake. Longman, Dar es Salaam, uk.
xxiii.
6. AbdilatifAbdalla, uk. xxiii.
7. Angalia D.T. Niane (1960) Soundjata, ou l'epopee
mandingue. Presence Africaine, Paris, uk. 9 (Tafsiri ni yangu).
8. Niane, uk. 9.
9. Chinua Achebe, (1576) "The Novelist as Teacher" katika
Morning Yet on Creation Day. Anchor Books, New York, kur. 55-60.
10. Senkoro, uk. 5.
11. Anthony Cronin (1976) "A Massacre of Authors."
Encounter (April 1956), uk. 25.
12. Angalia D.H. Lawrence (1965) (Mh) Selected Non - Dramatic
Writings of Bernard Shaw. Houghton, Boston, uk. 309
13. Chinua Achebe (1976) "Colonialist Criticism," m.y.k., kur.
3-24.
14. Wole Soyinka (1984) "The Critic and Society: Barthes,
Leftocracy and other Mythologies," katika Black Literature and Literary
Theory, kimehaririwa na Henry Louis Gate, Jr. Methuen, New York, kur. 27-57.
15. T.S.Y. Sengo (1973) "Uwanjawa Uhakiki", Kioo
cha Lugha, 3, uk. 11.
16. Karl Marx na Frederick Engels (1988) Manifesto of the
Communist Party. William Reeves Booksellers Ltd., London, uk. 9.
17. Angalia, kwa mfano, Georg Lukacs, (1978) "The Writer and the
Critic," katika Writerand Critic, kimefasiriwa na Professor Barthur Kahn,
Merlin Press, London, uk. 198-226.
18. Angalia Theodor Adomo, (1982) "Cultural Criticism and
Society", katika Prisms, kimefasiriwa na Samuel na Shierry Weber, The MIT
Press, Cambridge, Massachusetts, kur. 17-34.
19. Adomo, k.h.j., uk.
20.