Kwa kutoa mifano kutoka katika jamii yako, jadili dhima mbalimbali za fasihi simulizi huku ukirejelea vipera mbalimbali vya utanzu huu wa fasihi.
Kwa kutoa mifano kutoka katika jamii
yako, jadili dhima mbalimbali za fasihi simulizi huku ukirejelea vipera
mbalimbali vya utanzu huu wa fasihi.
Kwa kutoa mifano
kutoka katika jamii yako, jadili dhima mbalimbali za fasihi simulizi huku
ukirejelea vipera mbalimbali vya utanzu huu wa fasihi.
Fasihi simulizi
ni utanzu mmoja wapo kati ya tanzu za fasihi ambao una dhima mbalimbali kwa kwa
jamii husika. Hata hivyo kabla ya kuangalia dhima za fasihi simulizi ni vyema
kwanza kutalii fasili ya fasihi simulizi.
Mulokozi, M.M
(1996) anasema, Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na
kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.
TUKI (2004) wanasema
Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi
kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na
vitendawili.
Hivyo basi
Fasihi Simulizi ni fasihi inayotokana na maneno ambayo huzungumzwa, hutolewa au
kuimbwa ambapo mtungaji na mwasilishaji hutumia sanaa. Baada ya kuangalia maana
ya fasihi simulizi sasa tuangazie dhima mbalimbali za fasihi simulizi kwa
jamii.
KIINI
Kuburudisha;
tanzu mbalimbali za fasihi simulizi
hutumika kama nyenzo ya burudani katika nyanja mbalimbali za kijamii.
Mfano wa
tanzu hizo ni kama vile hadithi, ushairi (nyimbo mbalimbali), semi
(methali, vitendawili). Tanzu hizi hutoa burudani katika sehemu
mbalimbali, mfano nyimbo, zipo nyimbo ambazo hutumika kutoa burudani
katika
sehemu mbalimbali kama vile harusini-nyimbo za harusi, nyimbo za nyiso
hutoa
burudani jandoni na unyagoni. Vilevile katika siasa zipo nyimbo ambazo
hutumika
kutolea burudani na uhamasishaji wakati wa kampeni za kisiasa kwa mfano wimbo wa tumejipanga,mwaka huu wataisoma
(ccm). Hivyo basi kutokana na utanzu huu wa nyimbo kutumika kama chombo cha
burudani katika nyanja mbalimbali huonesha dhahiri kuwa ni kwa namna gani
fasihi simulizi inatimiza wajibu wake kwa jamii.
Kuelimisha; kupitia fasihi simulizi jamii hujipatia elimu ambayo huwasaidia kuijua vizuri historia yao, utamaduni, siasa ya nchi yao pamoja na itikadi. Mfano katika historia zipo kazi za fasihi simulizi ambazo huonesha historia, kazi kama utendi wa Fumo Lyongo kuhusu historia ya jamii ya Wangozi, utendi wa Shaka Zulu ambao hutupatia historia na utamaduni wa watu wa Afrika kusini. Pia ndani ya tendi hizo kuna masuala ya uongozi pamoja na siasa. Vilevile zipo methali ambazo huelimisha watu kufanya kazi kwa bidii ili kujiongezea nafasi yao kiuchumi, kwa mfano; “mgaagaa na upwa hali wali mkavu”. Kadhalika katika upande wa afya zipo methali zinazotoa elimu mfano “kinga ni bora kuliko tiba”. Hivyo basi utoaji huo wa elimu katika nyanja tofauti tofauti huonesha ni kwa namna gani fasihi simulizi ilivyo na dhima kubwa kwa jamii.
Kuhifadhi historia na utamaduni wa jamii; katika suala
hili pia fasihi simulizi haikuwa nyuma kwani zipo kazi mbalimbali ambazo
hutumika kama nyenzo kuu na muhimu za kuhifadhia amali za jamii kwa mfano
visasili na visakale hutunza historia na utamaduni wa jamii husika, mfano;
kisasili cha kibo na mawenzi hutunza historia ya Tanzania kuhusu mlima
Kilimanjaro. Pia zipo methali ambazo hutunza utamaduni wa waafrika hususani Tanzania
mfano; “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu”, methali hii hutunza utamaduni wa
kiafrika kuwa wadogo lazima wawasikilize na kuwaheshimu wakubwa. Kadhalika
katika siasa kupitia kipera cha lakabu ya baba wa taifa huonesha historia ya
kiongozi wa Taifa la Tanzania.
Kuhamasisha umoja na mshikamano; suala hili pia
hufanywa na aina hii ya fasihi simulizi katika jamii na hujidhihirisha katika
Nyanja mbalimbali kama vile siasa, zipo methali ambazo uhamasisha suala hili:-
“Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu”, “Kidole kimoja hakivunji chawa”. Kwa
upande wa nyimbo zipo pia ambazo huhamasisha suala hili kama vile nyimbo za
chapuzo mfano; wawe-kilimo, kimai-uvuvi. Vileveli zipo nyimbo ambazo
huhamasisha umoja na mshikamano wakati wa michezo.
Kukuza lugha; fasihi simulizi hujikita pia katika
suala hili la ukuzaji lugha kupitia vipera mbalimbali ambavyo hufanyika katika
nyanja mbalimbali kwa mfano nyanja ya elimu, vipo vipindi mbalimbali redioni na
hata kwenye luninga ambavyo hutumika kufundishia lugha hasa kwa watoto kwa
kupitia vipera vya fasihi simulizi kama vile vitendawili na methali, zipo pia
chemshabongo na hadithi mbalimbali. Vilevile ipo michezo ya watoto ambayo
hukuza lugha kama vile kauli tauria, mfano; “Katibu kata wa kata ya mkata alikataa katakata kukata miti katika kata
ya mkata”. katika siasa uibukaji wa misimu mfano, chakachua, ngangari nk.
pamoja na nyimbo hasa wakati wa kampeni husaidia kukuza lugha. Pia shughuli
mbalimbali za kijamii mfano harusi, misiba kupitia nyimbo za watani pia hutoa
mchango mkubwa katika kukuza lugha.
Kuonya na kukosoa jamii; zipo tanzu na
vipera mbalimbali vya fasihi simulizi ambavyo hujihusisha zaidi na kuiweka
jamii katika nafasi iliyobora zaidi. Mfano; kimaadili kuna methali zinazoonesha
maadili mema katika jamii mfano; “Samaki
mkunje angali mbichi”, “Mkaidi
hafaidi mpaka siku ya iddi”. Vilevile kiuchumi zipo methali ambazo huonya
na kukosoa wale wote wenye tabia za kivivu katika kujitafutia maisha mfano, “Mtegemea cha ndugu hufa masikini”, “Fanyakazi kama mtumwa uishi kama mfalme”.
Vilevile kuongeza kipato; kupitia fasihi
simulizi watu hujiajiri na kujipatia kipato. Kwa mfano; watu hujishughulisha na
utanzi wa nyimbo mbalimbali kama vile nyimbo za kisiasa, kiuchumi pamoja na
nyimbo za kiutamaduni ambapo kwa namna moja au nyingine huwasaidia katika suala
zima la kujipatia kipato na kusukuma mbele gurudumu la maisha kwa ujumla.
HITIMISHO
Hivyo basi, kutokana na fasihi simulizi kujihusisha na masuala mtambuko katika jamii ya leo ni dhahiri kuwa maendeleo ya sanaa jadi yanapiga hatua na kamwe hayawezi kupotea kabisa, ila tu, upo uwezekano wa kubadilika kulingana na maendeleo ya jamii husika.