NADHARIA HUTUMIWA SANA KATIKA UTAFITI
Nadharia
NADHARIA HUTUMIWA SANA KATIKA UTAFITI
MAANA YA NADHARIA
(Williady, 2013), Nadharia
ni
maelezo yakinifu kuhusu kitu, tajiriba, mahalifa au upumbavu na mafanikio au
maangamizi yanayochomoza katika jamii. Hivyo nadharia hufungamana na mambo
mbalimbali ya jamii kama vile mbinu, maarifa, tasinifu, mikabala na mienendo
mbalimbali ya jamii.
1. NADHARIA YA UPOKEZI (MWITIKO WA MSOMAJI)
Nadharia ya
Upokezi (mwitiko wa msomaji) ambayo husisitiza nguvu ya msomaji. Nadharia ya
Upokezi (Reception Theory) iliasisiwa na wahakiki wa waasisi wa Kijerumani
mwishoni mwa miaka ya 1960.Miongoni mwa
waasisi wa nadharia hii ni Robert C. Holub,Hans Robert Jauss na Wolfagang Isser.Katika kitabu chake
Reception Theory (1984), Holub anaelezea nadharia ya Upokezi kuwa ni Mabadiko ya jumla ya umakinikiaji
kutoka kwa mwandishi na kazi yake kwenda kwa matini na msomaji”
Nadharia ya
upokezi inaakisi mabadiliko ya mbinu katika historia ya fasihi na ilizingatiwa
kama jibu kwa jamii,wanazuoni na maendeleo ya fasihi huko Uerumani
Magharibi mwishoni mwa miaka ya 1960.Kwa
mujibu wa Holub, nadharia ya Upokezi ulikuwa ni njia ya Kimapnduzi kwa wahakiki
wa kisasa.
Waitifaki wa
nadharia hii wanashiilia msimamo kuwa kazi ya fasihi hupata maana baada ya
matini na msomaji kuadhiriana.Msomaji au mpokeaji ndiye huipa maana kazi ya
fasih.
Kwani huiona na
kuilinganisha na uzoefu wake wa maisha. Kielelezo hiki kipya cha uhakiki
hutilia maanani dhima ya msomaji.Hans Robert Jauss katika makala yake “The change in the Paradigm of Literary Scholarship” (1926) ambaye anachukuliwa
kama mmoja wa mihimili ya nadharia hii ya Upokezi anaelezea umuhimu wa
kuielezea kazi ya Fasihi.Isser anaiona kazi ya Fasihi kama
kitu au tukio lililo nje ya muktadha na historia.
Anasema kuwa ili
kazi ya fasihi ieleweke ni lazima ushiriki
wa msomaji uoane au upatane na maana inayojitokeza katika kazi ya
Fasihi.
Kwa hiyo basi ,
nadharia ya Upokezi hufasili Fasihi kama
mchakato wa namna msomaji na wanavyoathiriana.Uzoefu wa maisha wa msomaji
unaweza kutoa tafsiri tofauti kwa kazi ya fasihi kutoka msomaji mmoja na
mwingine.
2.NADHARIA YA ONTOLOJIA YA KIBANTU.
Nadharia
ya Ontolojia ya Kibantu. Kuna wataalamu mbalimbali waliozungumzia nadharia hii.
Kwa jumla, wataalamu hawa wameeleza maana ya Ontolojia kuwa ni mtazamo unaohusu
kuwepo kwa kitu katika dunia na kuangalia vitu katika uhasilia wake (Nicholaus
2011).
Ontolojia
inaweza kutazamwa kwa namna tatu: kama taaluma, kama falsafa na kama nadharia.
Hivyo kwa kuwa utafiti huu ulichunguza “Mabadiliko ya kiuandishi kutoka kanuni
za Ki-Aristotle kwenda kanuni za jadi ya Ki-Afrika”, kipengele cha Ontolojia ya
Kibantu kinachoweza kutumika katika kazi za fasihi, tuliona ni vyema kutumia
Ontolojia kama nadharia katika utafiti huu, kwani imewezesha utafiti huu
kufikia malengo yake, pia ilihusiana na mada iliyoshugulikiwa.
Kimsingi
kuna mitazamo minne kuhusu Ontolojia ya Kibantu. Mitazamo hiyo ni, ule wa
falsafa ya kisiasa (Itikadi ya kisiasa), mtazamo au falsafa ya Kihikimati
(Sagacty), wanafalsafa waliojikita katika kurekodi imani katika utamaduni wa
mwafrika (Ethnofilosofia), na falsafa ya Kiuweledi.
Wanaitikadi
wa kisiasa walichunguza masuala ya undugu wa kifamilia, ujamaa na kujitegemea
ndani ya Afrika. Wanasiasa hao ni Julius Nyerere, Leopold Senghor na Kwame
Nkurumah. Lengo lao lilikuwa ni kutaka kutafuta uhuru wa kweli kwa waafrika ili
kurudisha heshima kwa mwafrika kama ingewezekana.
Mtazamo
wa Kihikimati umejikita katika masuala ya uhuru, hekima na desturi za watu.
Waanzilishi wa mtazamo huu wameshawishika kwamba falsafa ya kiafrika haiangalii
vitu vyote vinavyohusu kazi. Lengo lao walitaka kuonesha kwamba ujinga sio hali
ya kifalsafa na ujinga upo kwa kila jamii, ujinga wa mwenzako waweza kuwa uhuru
kwake. Waanzilishi wa falsafa hii ni Odera H. Oruka na Marcel Griaule’s.Marcel
Griaule’s alifanya mazungumzo na Oyotemmeli kiongozi wa kabila la Wadogoni na
matokeo yake walipata falsafa ya kidini ya wadogoni.
Ethnofilosofia
hujishughulisha na ukusanyaji wa mitazamo ya kiulimwengu kutoka katika tamaduni
mbalimbali za waafrika. Hii imejikita katika masuala ya imani, masimulizi na
misemo ya watu. Muunganiko huo umeunganishwa na Paulin Hountondji. Wengine waliojihusisha na falsafa ya kiafrika
katika mtazamo huu ni Placid Tempels, Leopald Senghor, John Mbiti na Alex
Kagame. Hivyo, mtazamo huu umejikita zaidi katika masuala ya mila, desturi na
imani za jamii.
Falsafa
ya Kiuweledi imejikita katika uchambuzi na ufafanuzi wa ukweli. Zaidi inajihusisha
na uhakiki, na hoja ndizo sifa za msingi kwao. Waanzilishi wa falsafa hii ni
Paulina Hountondji, Kwasi Waredu, Odera Oruka na Peter Bodunrin. Wanasema kuwa
falsafa ya kibantu kwa sasa inaitwa Metafilosofia, na imejikita katika
kuangalia maudhui ya msingi. Wao wanahoji kwamba falsafa ya Afrika ni ipi?
Roberto
(1996) anasema Ontolojiani nadharia inayohusu kuwapo, yaani ni nadharia
inayoangalia yaliyokuwepo na yale ambayo hayakuwepo, halisi na yasiyo halisi,
tegemezi na vinavyojitegemea.
Parrinder
(1969) anasema kuwa nadharia ya kibantu inahusisha mwafrika na imani yake.
Hujumuisha maisha, mazingira pamoja na fikra zake. Pia anasema kuwa mawazo ya
mwafrika hujengwa katika misingi ya nguvu mbalimbali ambazoni Mungu, binadamu,
wanyama, mimea na kadhalika.
Wataalamu
wengine waliozungumzia nadharia ya Ontolojioa ni: Husserl (1913), Tugendhat
(1928), Wolff (1928), Gruber’s (1993), Bolzano (1996), Guariono (1998),
Wamitila (2008) na Cocchiarella (2007).
Kwa
jumla, wataalamu hawa wameeleza mengi juu ya nadharia hii, jambo
lililosisitizwa sanana wataalamu wengi waliojadili nadharia hii ni kuhusu
uchaguzi wa Ontolojia nzuri na namna ya kutumia nadharia hii. Wanasema
Ontolojia nzuri ni ile inayohusisha njia za Kisayansi na kutupatia njia chache
na rahisi ambazo zitaelezea mambo mbalimbali katika ulimwengu. Pia nadharia hii
inatukuza sana Ubantu na kumuona mwafrika kama kiumbe bora mwenye uwezo wa
kubuni na kusimamia mambo yake kwa usahihi. Mbali na kutumia Ubantu (U-Afrika),
nadharia hii inaeleza mambo kadhaa ambayo ni sehemu ya ufahari kwa waafrika,
mambo hayo ni pamoja na dhana ya familia pana, kuamini uzazi kuwa ndio njia ya
uzima wa milele, yenye kuhashiria umuhimu wa binadamu, na Ugumba ni laana na
utupu kwa binadamu, kuabudu katika Mungu na miungu na kuheshimu Wahenga. Pia
huhusisha na imani kuhusu uchawi, na sihiri, na ndani yake kuna masuala ya
uganga. Pia umri kwa waafrika una nafasi kubwa sana katika jamii na unabeba
hekima za mtu.
3.UJUMI (AESTHETICS)
Ujumi ni nini?
Ujumi ni tawi la falsafa linaloshughulika na uzuri, ubaya,
ladha, n.k.
AU
Ujumi ni elimu ya sheria na kanuni za sanaa.
Neno ujumi kwa kiingereza linajulikana kama “Aesthetics”.
Neno hili limetoholewa kutoka katika lugha ya kigiriki “Ais -
thesis”, likiwa na maana ya “Hisia” (Feelings), hasa hisia za akilini
(Mental perception).
Alexander Gottlieb Baumgarten (mjerumani) ni miongoni mwa
wanafalsafa yalioshungulikia kwa kina juu ya falsafa hii ya Ujumi. Baumgarten
alidokoa baadhi ya mawazo fasaha kutoka kwa Leibniz. Leibniz alizungumzia mambo
makubwa mawili amabayo ni LOGOS na ETHOS.
LOGOS, ni mantiki itokanayo na neno la maharifa au sababu
ipelekeayo uwelewa mpya au kuyachekecha mawazo makuukuu na kupata neno lenye
kuchukua mkondo mpya.
ETHOS, ni desturi ama mguso, tabia ama kaida Fulani ndani ya
jamii ambazo hufanya matakwa yahusuyo jamii Fulani tu.
Baumgarten, alikiendeleza kipengele cha mguso na hisia na
neno “Aesthetics” likaanzishwa.
Kabla falsafa mpya ya Aesthetics haijachukua kasi yake, hapo
awali masuala ya hisia yaliwekwa chini ya nadharia ya hisia za akili (mental
perception). Dhana ya ujumi ilitoka kwenye nadharia ya hisia za akili katika
karne ya 18 na kuitwa “Falsafa ya uzuri” au “Falsafa ya sanaa” au yote mawili
kwa pamoja. Baadaye ujumi uliachana na
falsafa na kuwa tawi linalojitegemea la elimu.
Kabla ya Baumgarten, ushairi na sanaa kwa ujumla ilijadiliwa
kitaalamu katika kapumoja. Hii inamaana kwamba ushairi haukutofautishwa na
muziki au uchoraji ama ususi, vyote vilielezwa kwa pamoja.
Baumgarten akaigawa dhana hii katika maeneo mawili ambayo ni
uzuri na sanaa.
1.
UZURI (The good or the truth).
Uzuri ni ukamilifu wa hisia za akili unaoleta kulitazama
jambo au mambo Fulani katika mtazamo chanya, haijalishi, kwani mwingine anaweza
kulichukulia jambo hilo kimtazamo hasi lakini mtazamo wake hauondoi uzuri wa
chanya kwa atazamaye chanya.
2.
SANAA
Sanaa ni ufundi wa kuunda jambo. Twaweza kuueleza uzuri
kupitia sanaa. Sanaa yaweza kuupambanua uzuri kwa viwango vya juu zaidi kuliko
jambo lolote lile.
Tafadhali
wasiliana na mwl. Majumbeni kwa,
0762 – 957493
0768 – 625660
4. NADHARIA YA UFEMINISTI ( Mtazamo wa kike)
(Williady, 2015) Nadharia hii inahistoria ndefu duniani, ikimaanisha ni moja ya nadharia zilizopata kutokea miongo mingi iliyopita.
chanzo cha kuibuka kwa nadharia hii ni vuguvugu la kutaka kufuta kabisa
uonevu wa mwanaume kwa mwanamk. nadharia hii inadai kuwa chimbuko la uonevu na ukandamizaji unaofanywa na wanaume kwa wanawake ni uroho wa mwanaume katika kumtawala mwanamke. Kwaufupi, ajaenda kuu ya ufeministi na mafeministi ni kumaliza kabisa utawala wa mwanaume kwa mwanamke.
moja ya wadau waliochangia sana kuendelea kwa nadharia hii kwa kasi ni Adrew Dworkin. Mwaka 1976, akiwa katika mji mkuu wa Uingereza, London, alitoa mapendekezo makali katika kukomesha utawala wa mwanaume kwa mwanamke, Dworkin anasema: Ili kufanikisha, tunahitaji kubomoa kabisa muundo wa mihimili ya utamaduni wa jamii kama vile sanaa, kanisa, sheria, kaya zinazodhibitiwa na baba, jamii na taswira zote za asasi, mila, desturi ambazo zinamwona mwanamke kuwa mtu ovyo.
WATAALAMU MBALIMBALI WALIVYOZUNGUMZIA MAANA YA UFEMINISTI
Nadharia
ya Ufeministi imefasiliwa na wataalamu mbalimbali kama vile:
Wamitila
(2003:253), hii ni nadharia ambayo imewekewa msingi na msukumo mkubwa pamoja na
nia ya kupigania ukombozi wa mwanamke kutokana na pingu za kiutamaduni, kidini,
kijamii, kisiasa na kiuchumi. Hii ni nadharia ambayo inasaili na kudadisi
itikadi ya kiume ambayo imekuwepo katika jamii kwa kipindi kirefu. Kudadisi pia
fasiri za kiume za fasihi pamoja na mikabala ya kiubabedume.
Ntarangwi
(2004:45), ni nadharia ambayo inajaribu kukiuka mitazamo ya kiume ambayo yaelekea
inatumiwa sana katika jamii.
Mukobwa
M. nadharia ya ufeministi imetokana na mkondo na harakati za kutetea haki za
wanawake ulimwenguni na imejikita katika imani ya usawa wa kijinsia, kijamii,
kisiasa na kiuchumi.
(Williady, 2015) Ninadharia iliyojaribu kuvunja mwiko wa mfumo dume hapa dunia kwa kuanzisha mapambano ya usawa wa kijinsia, bilashaka majaribio haya bado hayajafanikiwa.
Kwa
jumla, nadharia ya ufeministi ni nadharia iliyojikita katika kupinga ukandamizaji
wa mwanamke katika jamii hususan katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, na
kiutamaduni.
KUIBUKA KWA UFEMINISTI NA HARAKATI ZA KUIENDELEZA NADHARIA HII
Uhakiki
wa kifeministi ulishika kasi miaka ya 1960 na kuendelea kukua na kuishia kuwa
muhimu katika miaka ya hivi karibuni. Zipo kazi kadhaa zilizoandikwa kabla na
kulimulika suala hili kwa namna moja ama nyingine. Kazi kuu mbili
zinazorejelewa hapa ni A Room of One’s Own ya Virginia Woolf na A virdiction of the Right of women ya
Mery Wollsto Necraft.
Hata
hivyo, kazi iliyoishia kuwa na mchango mkubwa katika kuuweka msingi wa uhakiki
wa ufeministi ni kazi maarufu ya mwandishi wa Kifaransa, Simone de Beauvoir
iitwayo, The Second sex, 1952 katika
kitabu hiki, mwandishi huyu anachukuwa mkabala wa kiharakati kwa kushambulia na
kukosoa baadhi ya asasi zinazochangia katika kumdhalilisha au kumdunisha
mwanamke. Asasi kuu anazozishambulia ni ndoa, dini na utamaduni.
Nadharia
ya ufeministi ilichimbuka huko Marekani katika harakati za kukomesha biashara
ya utumwa mwaka 1830. Wanawake wakaanzisha harakati za kupigania haki za
mwanamke.
Wamitila
(2006:160-161) na Ntarangwi (2004:52-56) wamebainisha malengo mbalimbali ya
ufeministi.
Ni
kweli kwamba kuna baadhi ya malengo ya ufeministi yanakinzana na maisha halisi
ya mwanamke wa Kiafrika lakini baadhi ya malengo hayo yanasawiri maisha halisi
ya mwanamke wa kiafrika kama ifuatavyo:
Kubainisha
umuhimu wa mwanamke, kutokana na mwanamke kukulia katika jamii zenye mfumodume.
Umuhimu wake haukuonekana, ndiyo maana ikaanzishwa nadharia ya ufeministi
ambayo yenyewe iligundua umuhimu wa mwanamke katika jamii. Umuhimu wake upo
katika Nyanja zote za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Mfano, katika nyanja
ya kisiasa mwanamke anaweza kuwa kiongozi bora na mwenye ushauri. Hili
linajidhihirisha katika riwaya ya Barua
Ndefu Kama Hii iliyoandikwa na Mariama Bâ (1994). Mwandishi anathibitisha
hili anaposema:
“Tunayo karibu miaka ishirini ya uhuru! Lini tutampata mwanamke wa
kwanza awe waziri atakaye husishwa na maamuzi yatakayoongoza nchi yetu huko tuendako?
Kumbe nguvu walizonazo wakina mama, uwezo wao wa kupambana, na kujihusisha kwao
bila kutegemea kupata faida yoyote ni mambo ambayo hayahitaji tena
kuthibitishwa. Wanawake wamewainua wanaume wengi kwenye ngazi za juu.” (uk.82)
Katika
nyanja ya kijamii, mwanamke ni mlezi wa familia. Mfano, Ramatulayi anailea
familia yake kwani ameweza kulipa bili ya maji, umeme bila hata kumtegemea
mwanaume. Mfano, mwandishi anasema:
“Licha ya mzigo niliokuwa nao tangu zamani, nikaubeba na ule uliokuwa wa
Modu. Ununuzi wa vyakula muhimu ulinishughulisha kila mwisho wa mwezi.
Nilihakikisha kwamba sikuwa na upungufu wa nyanya au mafuta, viazi mviringo na
vitunguu wakati ambapo vyakula hivi viliadimika sokoni… Nilikuwa mwangalifu
kuzilipa bili za maji na umeme pindi zilipofika.” (uk.69)
Lengo
hili la ufeministi linakinzana na maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika, kwa
kuwa mwanamke wa Kiafrika anaonekana hana umuhimu katika jamii, pia anaonekana
kuwa dhaifu ambaye hawezi kuiendesha familia yake bila msaada wa mwanaume hii
ni kutokana na jamii nyingi kuendeshwa na mfumodume.
Kuorodhesha
kuwa kihistoria wanawake wamekuwa ni tegemezi na wasaidizi wa wanaume, ni kweli
kihistoria wanawake wamekuwa wategemezi na wasaidizi wa wanaume. Mfano katika
tamthiliya ya Nguzo Mama iliyoandikwa
na Penina Muhando (2007) tunaona mhusika BI MOJA alivyokuwa akimtegemea mume
wake na kutaka anunuliwe kanga. Mwandishi anasema:
“BI
MOJA: (kwa Shaabani): Kama ulijua kufika
sasa hivi nipe hela ya kanga bwana meli meli hii hainikosi leo utanipa hela
hizo kanga nikakate. Mwezi wa tatu huu kanga sizijui.
Shaabani: Nimekuambia mimi hela
sina. Sasa unataka nikaibe?”(uk.31-32)
Ni kweli kwamba mwanamke
wa kiafrika amekuwa tegemezi katika jamii, kwani humtegemea mwanaume katika
mambo mbalimbali ya kifamilia. Kwa mfano kutafuta au kununua mahitaji ya
nyumbani kama vile chakula, mavazi yake na watoto wake au kulea watoto wake.
Kuondoa
ukandamizaji wa mwanamke kutokana na pingu za kiutamaduni, kijamii, kidini,
kisiasa na kiuchumi. Jamii nyingi za Kiafrika zimejengeka katika mfumodume,
hivyo basi jamii zinamkandamiza mwanamke kutokana na pingu hizo. Katika
kulithibitisha hili waandishi wa kazi za fasihi nao hawakuwa nyuma
kulizungumzia katika kazi zao na lengo ni kuondoa mfumodume uliojengeka muda
mrefu katika jamii.
Kwa
upande wa kiutamaduni mwanamke ameonekana kukandamizwa kwa kuonekana hana
mamlaka hata ya kurithi mali za mumewe au zake mwenyewe, badala yake hata
akifiwa na mumuwe anapigwa, anafukuzwa na kudhalilishwa. Penina Muhando
anayathibitisha haya katika tamthiliya yake ya Nguzo Mama kwa kumtumia BI SABA pale anaposema:
“Akalia
Bi Saba tena akalia
Hana wa kumsaidia
Mumewe kafa nduguze wakaja juu
Pesa wamechukua senti tano haikubaki
Vyombo
na nguo zote wakagawana
Roho ilimpasuka Bi Saba kuwaona hao
ndugu
Walivyogombania mali wasiyoichuma…
Sasa
juu ya yote haya wamerudi kufagia
Hata
ufagio wamebeba
Na lawama kumtupia eti pesa
kazificha.” (uk.39)
Pia
mwanamke anaonekana anajishughulisha na kazi mbalimbali za kujiletea maendeleo
yake binafsi lakini anarudishwa nyuma kwa kukandamizwa na mwanaume. Penina
Muhando anayathibitisha haya kwa kumtumia BI PILI ambaye alikuwa anapika pombe
ili kujikwamua katika hali ngumu ya maisha lakini mumewe SUDI alizichukua hela
zote alizokuwa alizozipata. Kwa mfano, mwandishi anasema:
“BI
MSIMULIZI: Upishi wa pombe balaa ulimzushia
Visa na
mikasa Bi pili havikumuishia
Pesa
alizipata kutokana na hiyo pombe
Lakini visa
vya pombe hiyo pesa hazikufidia”
SUDI: (kwa Bi Pili) Nani kalewa? Umeninywesha wewe?
Wee!hawara
zako ndiyo wamekutia jeuri unaninyima pesa.
Toa pesa
sasa hivi (Anampiga) Bi Pili anakimbia huku akilia.” (uk.16)
Vilevile,
mwanamke alikuwa anakandamizwa kwa kulazimishwa kurithiwa na kaka au ndugu wa
mume pindi anapofiwa na mumewe. Mwandishi analithibitisha hili katika riwaya ya
Barua Ndefu Kama Hii pale anaposema:
“Tamsiri, zitapike hizo ndoto zako
za kutaka kuniposa.
Umeshakaa nazo kwa siku arobaini.
Kamwe sitokuwa mkeo.”(uk.81)
Kwa
upande wa kisiasa, mwanamke amekuwa akikandamizwa kwa kuonekana hawezi kuwa
kiongozi bora wa kuiongoza nchi ndio maana hata nafasi za wanawake zilikuwa
chache huko bungeni. Katika riwaya ya Barua
Ndefu Kama Hii iliyoandikwa na Mariama Bâ mwandishi anayadhihirisha haya
kwa kumtumia Ramatoulayi ambaye akilalamika kuhusu ukandamizwaji wa wanawake
huko bungeni pale anaposema:
“Wanawake
wanne, Dauda, wanne miongoni mwa wabunge mia moja uwiano gani huu wa kimzaha! Wala
hakuna uwakilishaji wa kimkoa” (uk.81)
Kwa
upande wa kijamii, mwanamke amekuwa akikandamizwa kwa kupigwa na mumewe bila
sababu zozote za msingi. Hili linajidhihirisha katika riwaya ya Rosa Mistika iliyoandikwa na Euphrase
Kezilahabi (1988) kwa kumtumia mhusika Zakaria ambaye alikuwa anampiga mkewe
bila sababu. Mwandishi anasema:
“Regina
tangu aolewe hakuwa na raha! Alikuwa akisumbuliwa na kuteswa na mumewe kwa kosa
lisilokuwa lake. Katika kijiji chote cha Namagondo hapakuwa na mwanamke
aliyekuwa akipigwa karibu kila juma kama Regina. Wanawake wengi kijijini
walijiuliza kwa nini hakutaka kumuacha bwana wake. wengine walimuonea huruma,
wengi lakini walimuona mjinga.” (uk.3)
Pi,
mwanamke alikuwa anakandamizwa kwa kuonekana kuwa yeye ndiye mwenye majukumu ya
malezi, kwa hiyo hata watoto wakiharibika anayelaumiwa ni mwanamke. Euphrase
Kezilahabi analithibitisha hilo pale anaposema:
“Lete hiyo barua iko wapi? Pamoja
na shilingi ulizopewa unafikiri sisi hapa maskini. Rosa alipigwa tena na tena.
Makofi yalikwenda mfululizo hata damu zikamtoka puani na mdomoni. Baba
nihurumie sitarudia tena… Zakaria hakujali alichukua fimbo na kuongozana na
bintiye mpaka chumba cha watoto hali akinguluma lazima unioneshe barua hiyo
unataka kuniletea umalaya wa mama yako hapa.” (Uk.7)
Vilevile,
mtoto wa kike alikuwa anaonekana hana thamani katika jamii, na watoto wa kiume
ndio waliopewa kipaumbele. Euphrase Kezilahabi anathibitisha haya katika riwaya
ya Rosa Mistika kwa kumtumia Zakaria
ambaye kabla ya kumpata mtoto wa kiume alikuwa anamnyanyasa sana mke wake
lakini baada ya kujifungua mtoto wa kiume manyanyaso yaliisha na alimpenda sana
mkewe. Mwandishi anasema:
“Zakaria alirudi nyumbani siku
hiyo. Alikuwa amekwisha pata habari hizo njiani. Alimbeba mtoto. Alimpa pongezi
mke wake. Regina sasa mji huu umekuwa wako. Asante Regina alijibu akitabasamu,
alijiona anauwezo wa kuzungumza.” (uk.24)
Lengo
hili linakinzana na maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika, kwani mwanamke
hatakiwi kurithi mali yoyote pindi wazazi wake wanapofariki au mumewe
anapofariki. Pia mwanamke kushindwa kupewa nafasi ya kutoa maamuzi yoyote
katika masuala ya kiukoo. Kwa upande wa dini mwanamke anakandamizwa na
kuonekana dhaifu hivyo kutokuwa na nafasi ya kuongoza waamini. Mfano, dini ya
Kiislamu na baadhi ya madhehebu ya Kikristo.
Lengo
lingine ni kuzitambua na kuzibainisha dhamira kuu katika kazi zilizoandikwa na
wanawake. Dhamira kuu ni dhamira inayomsukuma mwandishi katika kuandika kazi ya
fasihi. Baadhi ya waandishi wanawake wameonesha dhamira kuu katika kazi zao
kama ifuatavyo:
Nguzo Mama
iliyoandikwa na Penina Muhando (2007) imebeba dhamira kuu ambayo ni ukombozi wa
mwanamke. Ukombozi huo upo katika nyanja mbalimbali kama vile kijamii,
kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa. Mfano, mwandishi ameonesha wanawake
wanavyojishughulisha katika kuinua uchumi wao, kwani walikuwa wakiuza vitambaa
na kupika pombe. Mwandishi anathibitisha haya kwa kusema:
“BI TANO: Yaani mnasema mimi
mvivu siyo nimezunguka mji mzima na zigo hilo halafu mnaniambia mimi mvivu.
Nawaambia watu hawataki kununua au mnataka niwagawie bure.”
BI NANE: Lakini kwa nini wakatae
kununua hivi, mbona vile vya mwanzo walivinunua? (uk.16).
Vilevile,
Katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii iliyoandikwa
na Mariama Bâ (1994) suala la ukombozi wa mwanamke limejitokeza kama dhamira
kuu. Ukombozi huu umejikita katika nyanja za kisiasa, kiutamaduni, kijamii na
kiuchumi.
Mfano,
katika nyanja ya kijamii, mwandishi ameonesha jinsi ya kumkomboa mwanamke
kielimu, pale anaposema:
“…Shangazi Nabu anampeleka Nabu mdogo katika
shule ya Kifaransa huko. Huko Nabu alijifunza aina mbalimbali za mapishi,
matumizi ya pasi na zana za kutumia na kumenyea...” (uk.39)
Lengo
hili linakinzana na maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika, kwa kuwa tangu
mwanzo wanawake walikuwa hawaruhusiwi kuwa viongozi, badala yake wanaume ndio
waliochukuwa jukumu hilo la uongozi katika jamii. Pia, wanawake hawakuruhusiwa
kupata elimu wakitegemezwa katika majukumu ya nyumbani na kuandaliwa kwenda
kuolewa na kuja kuwa walezi wa familia.
Kuichunguza
historia ya kifasihi ya jadi ya kike na kuwamulika waandishi wa kike
waliotambua hali za wanawake na ambao wanaweza kuchukuliwa kama vielelezo kwa
wasomaji wao. Hapo awali kazi mbalimbali za kifasihi za jadi za kike zilielezwa
na waandishi wa kiume. Lakini nadharia hii imemulika waandishi wa kike
wanaotambua hali mbalimbali na wameamua kuandika kazi mbalimbali ambazo
zinaelezea matatizo ya wanawake. Mfano, katika tamthiliya ya Nguzo Mama mwandishi anaelezea jinsi
wanawake wanavyonyanyaswa na kuachiwa majukumu ya kulea familia, kuchukuliwa
mali zilizoachwa na waume zao baada ya kufariki. Mfano, mwandishi anasema:
“…Haa! Shemeji mmerudi kuchukua hata kitanda!
Hata sufuria! Nitalala wapi na nitapikia wapi jamani!” (uk.39)
SUDI:
Haya nipe pesa ulizokwisha kupata.
BI
PILI: Hee! Kwa nini nikupe?
SUDI: Leta pesa upesi kabla
sijakukong’ota.” (uk.13)
Mariama
Bâ naye ni kielelezo kwani ameelezea matatizo mbalimbali yanayowakumba wanawake
na namna wanavyokabiliana na matatizo hayo. Mfano mwandishi anasema:
“… Ramatulayi, Acha nisikilize
mimi zaidi; Redio ya Kankan ilinifahamisha kwamba ulikataa kuolewa na Tamsiri.
Ni kweli? Ndio.” (uk.87)
Mwandishi anaonesha jinsi mhusika Ramatulayi
alivyojitambua na kukataa kurithiwa na Tamsiri, pia anamkataa Dauda ambaye
alitaka kumrithi baada ya kufiwa na mume wake.
Kupitia
lengo hili tunaona wanaufeministi wameongelea kuhusu wanawake tu ambao ni
vielelezo katika kazi za fasihi, lakini wapo wanaume ambao wamezungumzia
masuala mbalimbali yanayowahusu wanawake. Mfano, Shaaban Robert aliyeandika Wasifu wa Siti Binti Saad.
Kudhihirisha
kuwa kuna sifa fulani za kike na uzoefu fulani wa kike katika uwazaji, hisia,
kutathmini, kujiangalia na kuuangalia ulimwengu wao wa nje. Uzoefu fulani wa
kike unajitokeza katika uwazaji na jinsi wanavyousawiri uhalisi. Kazi ambazo
zinamsawiri mwanamke kwa njia chanya, mfano ni riwaya ya Kiwasifu ya Shaaban
Robert Wasifu wa Siti Binti Saad. Kuna mashairi kadhaa aliyoyatunga mwandishi
ambayo yanaendeleza suala hili la uchanya wa wanawake katika jamii. Mfano wa
usawiri wa wahusika linathibitishwa pale mwandishi anaposema:
“Siti
binti Saad,
Ulikuwa
mtu lini,
Ulitoka
shamba,
Na
kaniki mbili chini,
Kama
si sauti,
Ungekula
nini?” (uk.22)
Hisia:
mfano, katika riwaya ya Barua Ndefu Kama
Hii kupitia mhusika Daba alivyomwambia mama yake kuhusu Benetuu. Mwandishi
anasema:
“Hasira ya Daba iliongezeka zaidi
jinsi alivyozidi kuichambua hali ilivyokuwa. “Mama! Vunja ndoa yako! Achana
naye mtu huyu hajatuheshimu, si wewe wala si mimi… sitaki kukuona unagombania
mwanaume na mwanamke mwenye umri sawa na mimi.” (uk.52)
Lengo
hili la wanaufeministi, linaendana na hali halisi ya wanawake wa Kiafrika, kwa
kuwa mawazo ya mwanamke jinsi anavyojiwazia yeye mwenyewe au kuwawazia wanawake
wenzake hutofautiana . vilevile, hisia za mwanamke zinaweza kudhihirika katika
maandishi na kuonesha jinsi wanavyowaza katika hali ya kawaida.
HITIMISHO
Lengo
la nadharia ya ufeministi lilikuwa ni kuondoa unyanyasaji wa kijinsia hasa kwa
mwanamke. Hivyo basi, malengo ya ufeministi yalijikita katika kumnasua mwanamke
kutoka katika pingu za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii. Malengo haya
ndiyo yanayoleta ukinzani wa maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika. Hali hii
imeleta mabadiliko katika maisha ya wanawake wa kiafrika, kama vile kutaka haki
ya elimu, kumiliki mali, kurithi mali, kutaka nafasi za uongozi, pia kuwa na
maamuzi ya kifamilia au kiukoo, katika kupingana na pingu za maisha.Nadharia ya Uhemenitiki
Uhemenitiki ni taaluma inayohusiana
na uelewaji na kutafsiri matini. Chimbuko la nadharia hii ni katika uchambuzi
wa falsafa katika matini za kidini, hususani dini ya Kikristo. Waasisi
wanaohusishwa na chimbuko la nadharia hii ni kama vile Friedrich Schleiermacher
(1768-1834),Wilhem Dilthey (1833-1911) na Martin Heidegger (1889-1976).
Msingi mkubwa wa nadharia ya Uhemenitiki ni
imani ya kwamba matendo ya binadamu yanaathiriwa kwa njia mbalimbali na asasi tofauti zilizoko katika
mazingira yake. Msingi huo unatupeleka katika dhana ya kuibua umuhimu wa
kuelewa njia au mbinu za uelewaji wa maana za matini. Madai ya msingi ya
nadharia ya Uhemenitiki yanahusisha dhana mbalimbali kama vile duara la kihemenitiki, utukuzaji pamoja na ile ya ufufuaji wa kisarufi, kisaikolojia na
kimuktadha (Senkoro, 1987; Wamitila, 2002 katika Ponera, 2010).
Akizungumzia suala la Mviringo au Duara la Kihemenitiki, Senkoro (1989:9) anasema:
“…katika usomaji
kuna mviringo wa kihemenitikiambao humfanya msomaji aende mbele na nyuma,
kushoto na kulia mwa yale yaongelewayo katika kaziya fasihi.Hadhira huwa
wanabashiri na kuhusisha mambowanayoyapitia maishani mwao”.
Kulingana na nadharia hii ya
Uhemenitiki huwa kuna ugumu wa kuwepo kwa uwiano kati ya malengo na maana
asilia ya mtunzi dhidi ya uelewaji wa maana aipatayo msomaji. Uelewaji wa maana
kwa msomaji huhusisha kuyajua mambo mbalimbali yaliyomzunguka mtunzi wakati au
kabla ya kuitunga kazi husika. Ni vigumu kuelewa malengo na maana asilia ya
mtunzi iwapo msomaji au mhakiki hatahusisha mambo hayo. Kwa kufanya hivyo,
ndipo msomaji atakuwa amelitalii duara la kihemenitiki. (Ponera, 2010).
Dhana ya Utukuzaji katika nadharia ya
Uhemenitiki inamaanisha jumla ya makisio mbalimbali ambayo msomaji au mhakiki
wa kazi ya fasihi huwa nayo punde aishikapo kazi yoyote ya kifasihi. Makisio
hayo hujengwa akilini mwa msomaji
kulingana na misingi mbalimbali kama vile anwani yake (jina na picha ya
kitabu), kiwango cha usomi, utamaduni, upeo wa uelewa, pamoja na ulinganisho wa
kazi zozote zilizotungwa na watunzi wengine zinazofanana na hiyo (Wamitila,
2002).
Wamitila (2002:193) anafafanua kuwa
dhana ya Ufufuaji, hususani ule wa
kisaikilojia iliasisiwa na Dilthey (1833-1911).
Alisisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa msomaji au mhakiki kufufua
muktadha asilia wa kazi inayohusika na kujaribu kujiweka katika muktadha huo
ili aweze kuipata maana asilia ya matini. Kwa mujibu wa mawazo yake, kazi
mbalimbali za kifasihi zinaweza kuwa na maana mbalimbali kwa wasomaji
mbalimbali. Aidha, dhana ya ufufuaji inasisitiza kuwa ili kuielewa na
kuitafsiri maana ya matini lazima msomaji au mhakiki azame katika kuuelewa
mtindo. Hapa neno ‘mtindo’ limetumika kumaanisha muktadha wote wa mfumo wa
maneno na sentensi zilizotumika katika matini.
Dhana hizi zinazobeba madai ya
msingi ya nadharia ya Uhemenitiki zinahusiana kwa kiasi kikubwa. Gadamer (1960)
ambaye amenukuliwa na Senkoro, (1987:7) anasema:
“Taaluma ya Uhemenitiki hujihusisha na
utafutaji wa maana ya kazi ya fasihi
kwa kuuliza maswali muhimu
manne:
i. Ni nini maana ya fasihi?
ii. Je, maana hii inahusianaje
na kusudi la mwandishi?
iii. Je, tunaweza kuzielewa kazi za fasihi
za tamaduni na historia tofauti na zetu?
iv. Je, ni rahisi kupata
uelewaji wa ndani wa kazi ya fasihi au huu hutegemea
mazingira na historia ya
hadhira ihusikayo?”.
Kuyajibu maswali haya kulihusisha
kwa pamoja dhana za Duara la Kihemenitiki,
Ufufuaji na Utukuzaji ambazo zinaunda madai ya msingi ya nadharia hii. Misingi
ya nadharia hii ilitumika katika kuendesha utafiti uliofanywa unaohusu
vipengele vya msingi vya kiufafanuzi. Misingi hiyo ni ile iliyomo katika dhana
tatu muhimu zilizomo katika nadharia hii ambazo ni Duara la Kihemenitiki,
Ufufuaji na Utukuzaji.
Hivyo, taswira zinazojitokeza
katika ushairi wa Kaluta Amri Abedi zilichunguzwa kwa kuhusianishwa na
vipengele vingine vya kimaisha kama vile matukio ya kihistoria yaliyojiri kabla
au wakati wa utunzi, tabia na mwenendo halisi wa Sheikh Kaluta Amri Abedi
mwenyewe, hali halisi ya maisha tangu kipindi cha baada ya kazi husika kutungwa
hadi sasa, na jiografia ya alipokuwa mtunzi (duara la Kihemenitiki). Aidha,
uchunguzi ulihusisha fikra binafsi za mtafiti kuhusiana na lugha na taswira
mbalimbali zijitokezazo katika Diwani ya
Amri (Utukuzaji). Vilevile uchambuzi wa data ulizingatia mtindo mahsusi
ambao Kaluta Amri Abedi aliutumia katika utunzi kwa kuulinganisha na matumizi
ya lugha ya wakati huo (Ufufuaji).