Misingi ya Uhakiki katika Fasihi ya Kiswahili
Fasihi, Uandishi na Uchapishaji (Dar Es Salaam University Press, 1993, 260 p.)
SEHEMU YA TATU: UHAKIKI |
13. Mchango wa Wanawake Katika Maendeleo ya Ushairi wa Kiswahili Katika Kipindi cha Urasimi (1600 - 1900)
M.M. Mulokozi
1.0 Utanguliv
Kipindi cha kuanzia kama mwaka 1600 hadi 1900 kimeitwa "Muhula
wa Urasimi" (Taz. Kezilahabi 1983) katika historia ya ushairi andishi wa
Kiswahili kwa sababu karibu watunzi wote wa wakati huo walishikilia kwa dhati
kanuni za kimapokeo za kisanaa na kifikra.
Muhula huu wa ushairi wa Kiswahili umechunguzwa na kujadiliwa
sana na wataalamu, kwa mfano, Steere (1867); Dammann (1940); Hichens (1941);
Harries (1962); Knappert (1967 na 1977); Kezilahabi (1973 na 1983); Arnold
(1973); Ohly (1973 na 1977); Abdulaziz (1979); na Mulokozi (1975 na 1982).
Katika maandishi ya wataalamu hao, majina fulanifulani ya
washairi mashuhuri wa enzi hizo huwa yanatokea mara kwa mara. Baadhi ya majina
hayo ni Mwengo bin Athumani, mtunzi wa Utenzi wa Tambuka (1728); Sayyid
Aidarus, mtunzi/mfasiri wa Hamziya (1749) Sayyid Abdallah bin Nasir,
mtunzi wa Inkishafi (1800), Ali Koti mtunzi wa mashairi (1800-1835);
Muyaka bin Haji, mtunzi wa Diwani ya Muyaka (1800 - 1840); Mwana Kupona,
mtunzi wa Utenzi wa Mwana Kupona (1858); na Sayyid Mansab Adbulrahmani
(1831 - 1922) mtunzi wa Waji Waji, Dural Mandhuma; n.k.
Majina haya yanaweza kumfanya msomaji aamini kuwa watunzi wote
mashuhuri wa ushairi wa enzi hizo, isipokuwa Mwana Kupona, walikuwa ni
wanaume.1
Madhumuni ya makala haya ni kuonyesha kuwa utunzi wa ushairi
andishi katika kipindi cha urasimi haukufanywa na wanaume tu; kwamba labda
wanawake walitoa mchango mkubwa zaidi kuliko ilivyoelezwa na wachunguzi
waliotangulia.
Wanawake watakaojadiliwa hapa ni wafuatao: Mwana Khamisi Mwinyi
Mvita, Binti Lemba, Mwana Saida Amin, Mwana Bukhalasi, Nana Somo, Mwana Kupona,
Saada Taji Arifina, na watunzi wengine wa kike wasiofahamika majina yao.
Itadhihirika kuwa tungo za zamani kabisa katika lugha ya
Kiswahili ambazo bado tunazo huenda zilitungwa na wanawake. Kadhalika,
itaonekana kuwa mchango wa washairi wa kike katika kukomaza sanaa na maudhui ya
ushairi katika kipindi hicho ulikuwa mkubwa. Mwisho, tutajaribu kuonyesha kuwa
yumkini baadhi ya mashairi ambayo watunzi wake hawafahamiki, hasa yale yenye
kuielezea kwa usahihi hali ya unyonge wa mwanamke, yalitungwa na wanawake.
2.0 Baadhi ya Watunzi wa Kike
2.1 Mwana Khamisi Mwinyi Mvita (Kame ya 17)
Mtunzi huyu ametajwa na William Hichens (1941) kwamba ndiye
aliyetunga shairi la "Mzungu Migeli." Hichens hatuelezi kama mtunzi huyu alikuwa
mwanamke au mwanamume, lakini jina lake, "Mwana Khamisi" laonyesha huenda
alikuwa mwanamke. Katika Kiswahili neno "Mwana" kwa kawaida huambatishwa na
majina ya wanawake. Kama maelezo haya ni sahihi, basi Mwana Khamis ndiye mtunzi
wa kwanza wa ushairi wa Kiswahili anayefahamika kwa jina. Shairi la Mwana Khamis
linasema hivi:'
Mzungu Migeli u mwongo
Mato yako yana tongo
Kwani kuata mpango
Kwenda kibanga uani?
Shairi hili linasemekana lilitungwa na Mwana Khamis
kumtahadharisha Mreno Miguel, aliyekuwa rafiki yake, juu ya mipango fulani ya
kuwaangamiza Wareno (Michens 1941: 123). Hatuna hakika juu ya maelezo haya.
Yawezekana vilevile kuwa shairi hili lilitungwa kuwasimanga Wareno ambao wakati
huo walikuwa wakiitawala Mombasa. Kulihali shairi hili halimsifu Miguel.
Mbali na shairi hili hatuna mashairi mengine ya Mwana Khamis.
Kama yalikuwepo labda yamepotea na hayakumbukwi tena.
2.2 Mwana Shekhe Lemba (1663)
Habari za mwandishi huyu hazifahamiki sawasawa. Katika beti 556
na 557 za utenzi wake wa pekee tunaoufahamu, Siri li Asirari,
mtunzi anatuambia kwamba yeye ni "Mwana Mwarabu" na kwamba baba yake
anaitwa Shekhe Bwana Lemba. Anazidi kutuarifu kuwa yeye mwenyewe alizaliwa
katika kitongoji kiitwacho Kivundoni (ubeti 558). Kwa mujibu wa maelezo ya
Dammann, kitongoji hicho kiko katika mji wa Pate (Dammann, 1940:274, Tanbihi Na.
4). Katika mji wa Lamu vilevile kiko kitongoji chenye jina hilo. Mtunzi
anaendelea kutueleza kuwa alimaliza kutunga utenzi wake siku ya 20 ya mwezi wa
kwanza baada ya Ramadhani mwaka 1074 A.H. (1663/4 B.K.) (beti 561 - 62).
Kutokana na maelezo hayo, yaelekea kuwa Mwana Lemba aliishi Pate
(au labda Lamu) kunako karne ya 17. Hivyo yu miongoni mwa watunzi wa mwanzo
kabisa wa tendi za Kiswahili wanaofahamika; kwa kweli utendi wake huenda ndio wa
zamani zaidi kuliko tendi zote zinazofahamika leo.2
Utendi wa Mwana Lemba unaitwa Kisa cha Anzaruni au
Siri li Asirari (Siri Sirini). Utendi huu unasimulia kisa cha
mfalme dhalimu "kafiri" aliyeit wa Anzaruni ambaye alikuwa na tabia ya
kuwaandama na kuwatesa Waislamu. Mfalme huyo alikuwa na hirizi iitwayo "Siri
Sirini" na "Nuru Nuruni" (ubeti 212) ambayo ndiyo iliyokuwa kinga yake.
Ingawa Anzaruni hakuwa muumini, lakini hirizi yake ilikuwa
imeandikwa majina ya Mungu, na ilikuwa na nguvu za kumlinda kila aliyeivaa
asidhurike.
Yuwa tena Muhamadi
napa kwa Mola wadudi,
alio pweke wahidi
hirizi hinu ni enzi (ubeti 464)Wala kitu kitindao
wala kitukushieo
hakuna, kilinganao
kama ya hinu hiriziHirizi hinu, rasuu,
nda isimu huukhuu
za Mola alio yuu,
wa rehema na mbawazi.
(beti 468 - 69)
Mtume Muhamadi anapopala habari za uovu wa Anzaruni, jinsi
anavyowashambulia wasafiri na kuwanyang'anya mali na wake zao, anaamua
kumshambulia. Kama kawaida, shujaa wa upande wa Waislam ni Sh. Ali, mkwe wa
mtume. Shujaa huyo anapigana na Anzaruni lakini hafanikiwi kwa sababu Anzaruni
ana kinga ya hirizi aliyoivaa kichwani. Baada ya kuona kuwa hakuna mafanikio,
Mtume Muhamadi anaomba dua, Mungu anamsikia na kutuma kozi ambaye anatua
kichwani kwa Anzaruni na kumnyang'anya hirizi yake. Anaipeleka hirizi hiyo kwa
Mtume. Baada tu ya kupokonywa hirizi yake Anzaruni anaishiwa nguvu na kuuawa.
Baadaye Mungu analeta jeshi la malaika elfu 70,000 kumsaidia Mtume.
Baada ya vita Waislamu wanarejea Madina na kumkuta mwenzao
Abubakari bin Abi Kuhafa akiwa mgonjwa sana. Hapo mtume anamwekea hirizi kifuani
na Abubakari anapona mara moja. Utendi unamalizika kwa maelezo marefu kuhusu
nguvu ya majina ya Mungu ambayo yameandikwa katika hirizi ya Siri li Asirari.
Utendi huu unaelezea majilio ya enzi mpya za Uislamu na
kuutukuza ushindi wa Waislamu "wema" dhidi ya madhalimu. Ushindi huu unatokana
na nguvu za Allah ambazo zinawakilishwa na hirizi. Hivyo mtunzi huyu anachukua
imani ya jadi ya Kiafrika kuhusu nguvu ya uganga (hirizi) na kuipa umbo na
maudhui mapya ya Kiislamu. Utendi huu unaeleweka vizuri hata kwa Waafrika
wasiokuwa Waislamu.
Mtazamo wa Kiafrika wa utenzi huu unadhihirika pia katika
mtazamo wa mtunzi kuhusu suala la uzazi. Tendi na hadithi nyingi za Kiafrika
hutukuza uzazi na kulaani ugumba. Katika utendi huu, tunamwona mtunzi akiomba
apewe uzazi:
Huombea wangu wana,
na wa nduu zangu, Rabana,
Wakue, wawe mashina
watoze thandu na mizi
(ubeti 548)
Ubeti huu unadhihirisha pia ufundi wa mtunzi huyu katika kutumia
sitiari.
2.3 Mwana Said Amin (Karne ya 18/19)
Kazi pekee ya mwanamke huyu tunayoifahamu inaitwa Utendi wa
Fatuma (Dammann, 1940: 92 - 140). Katika ubeti wa 438, mama huyu anajiita
"mwandishi" wa utendi huo, lakini katika ubeti wa 440 anajiita "mtunzi". Hadi
sasa bado kuna mjadala kuhusu mtunzi wa utendi huo. Je, Mwana Said aliutunga au
aliunakili tu kutoka katika kazi ya mtu mwingine? (taz. Knappert 1979:120 -
137). Hatuwezi kulijibu swali hili; tunachoweza kusema kwa hakika ni kwamba mama
huyu kwa njia fulani alihusika na utendi huu, na hivyo amechangia katika
kuhifadhi fasihi ya Kiswahili.
Kwa mujibu wa ubeti wa 444, Utendi wa Fatuma
ulimalizwa kuandikwa mwaka 1222 A.H. (1807 B.K.). Knappert (1979:121) anafikiri
kwamba ulitungwa katikati' ya karne ya 18.
Utendi huu husimulia kisa cha Fatuma binti ya Mtume Muhamadi,
hasa uhusiano wake na Sh. Ali kabla na baada ya kuoana. Fatuma ni shujaa mwenye
hadhi ya pekee katika Uislamu - yu mfano wa mwanamke bora na adili anayestahili
kuigwa na wanawake wote. Utendi huu unatilia mkazo sifa hii ya Fatuma. Utendi
unafundisha kuwa upendo na uadilifu ni bora kuliko mali na utukufu. Fatuma
anaposwa na wafalme na watukufu wengine, lakini wote anawakataa na kuamua
kuolewa na kijana fukara Ali.
Uzalendo wa mtunzi unajitokeza wakati anapouombea baraka mji
wake wa Lamu:
Haja yenye ta'azimu,
ya Rabi, uwakirimu,
wokowe nti ya Amu,
na majimbo yothe pia!
(ubeti 138)
Pamoja na kuombea nchi yake, mtunzi anaelekea kuyafikiria
maslahi ya wanawake. Fatuma ni shujaa wa wanawake. Hili linajitokeza katika
tabia na sifa zake. Mfano mmoja ni wakati anapoposwa na Ali. Mungu anatoa mahari
ya kumlipa Fatuma ili akubali ndoa, lakini Fatuma anaikataa na kueleza kwamba
"mahari" pekee anayoitaka ni kuwaombea toba wanawake wenzake:
Fatuma katazakara
kamwambia mhuhtara,
"Natiya kesho akhira,
ni shufa'e nisaa!Nataka kesho ni pweke,
niombee wanawake
zambi zao ziwepuke
siku ya nyota na ndoaNdiyo maharia
takayo katika nia,
naye anitungulia,
kula yambo humwelea"
(beti 304 - 306)
Utendi huu umeandikwa katika lugha tamu yenye kutiririka vizuri
sana. Hapana shaka kuwa mtunzi alikuwa ni bingwa. Utendi una hisia nzito, na
baadhi ya beti zinagusa moyo wa msomaji. Tazama kwa mfano, beti hizi zinazoeleza
wasia wa Fatuma kwa mumewe Ali:
Ali kipendi tyangu
takupa wasia wangu,
nitendea mume wangu,
wakati wa mautia!Ukutiapo wakati
wa kunegema mauti,
Haidari itafiti
hirizi yangu, sikia!Ewe Aba 1-Hasani,
nakuusia yakini,
hirizi yangu shingoni,
sinivuwe nakwambia.Hii ni hirizi yangu,
na iwe shingoni mwangu
kesho mbee za Mungu
ndipo nendapo kuvua
(beti 413 - 416)
Lugha ya utendi huu inakaribiana sana na lugha zetu za Kibantu.
Wengi wetu wanaweza kuyatambua kwa urahisi baadhi ya maneno ya kale
yanayotumika, k.m.,
Kwikwi (ub. 242)
|
: Elfu
|
Mitima (ub. 40)
|
: Mioyo
|
Mnunaye (ub. 411)
|
: Nduguye (mdogo)
|
Yakamaa (ub. 239)
|
: Yakaisha
|
Maninga (ub. 5)
|
: Macho
|
Nikomele (ub. 27)
|
: Nimemaliza
|
2.4 Mwana Bukhalasi (Karne ya 19)
Hatujui mengi juu ya mtunzi huyu wala idadi ya tenzi alizotunga.
Tuna hakika kuhusu utungo wake mmoja tu uitwao Utendi wa Masahibu (Allen
1971: 130 - 268). Neno "Mwana" linadokeza kuwa mtunzi huyu labda alikuwa
mwanamke. "Bukhalasi" ni jina la baba yake.3
Mtunzi mwenyewe anatueleza kuwa alizaliwa Mombasa na alitunga
katika lahaja ya Kiamu, lakini hatwambii ni lini alizaliwa au kuutunga utendi
huu.
Na malenga makhsusi
alotunga kwa nafusi
ni mwanawe Bukhalasi
pasi wa pili kungia
Lugha awezonudhumu
ni Kiswahili cha Amu
kwa kuwa hukifahamu
ndipo akanudhumia
Na mui alozalika
pulikani tatamka
ni Mvita kwa haqiqa
yeye na wazazi pia
(beti 1066 - 1068)
Kwa kuwa hati ya mswada alioutumia Allen ni sawa na ya Utendi
wa Ayub, ulionakiliwa na Muhamadi bin Juma mwaka 1905 (Allen 1971), tunaweza
kukisia kuwa labda utendi huu pia ulinakiliwa na mwandishi huyohuyo. Hivyo
tarehe ya utunzi wa utendi huu huenda siyo baada ya mwaka 1905. Yumkini huu ni
utungo wa karne ya 19 au hata kabla.
Utendi wa Masahibu unasimulia kisa cha mgogoro kati ya
tajiri mwadilifu na mfalme dhalimu. Tunaelezwa kuwa tajiri:
Ali na wingi wa utu
na kulla mtu ni kitu
na kupendeza kwa watu
kwa heshima kujetea
(ubeti 73)
Ni mtu msalihina
ibada kipenda sana
kwa usiku na mtana
Molawe kinyenyekea
(ubeti 79)
Akipendwa na watwana
na vijakazi nisana
siku wakitomwona
wasiwasi huwangia.
(ubeti 82)
Bali mfalme alikuwa mwovu na katili kupindukia:
Tena mno akitisha
na raia kutumisha
kutua na kuwatwisha
ndiyo yake mazoea
(ubeti 19)
Pili lake sultani
ni mchache wa imani
kuwatesa maskini
kwake haoni vibaya
(ubeti 20)
Ali hajali yoyote
wala kutenda lolote
na raia zake wote
wali wakimtukia
(ubeti 22)
Tajiri anapostawi zaidi kutokana na biashara ya baharini mfalme
anamwonea kijicho na kuamua afukuzwe mjini. Tajiri anatangatanga na kuwa fukara
wa mwisho lakini hata hivyo haachi kushikilia maisha ya unyofu. Mwishowe anafika
katika nchi moja ambamo anakutana na tajiri mwingine ambaye zamani alipata
kumuuzia bidhaa. Tajiri huyo vilevile ni mnyofu anayetumia mali yake kuwasaidia
wenye shida. Baada ya kuelezwa masahibu ya tajiri mwenzie, anamwonea huruma na
kumkusanyia jeshi linalomwezesha kurejea kwao na kupigana na kumfukuza yule
mfalme dhalimu. Katika mapambano jeshi hilo linasaidiwa na raia, ambao wamechoka
kuonewa na wanaasi na kufanya mapinduzi. Mwishoni tajiri mwadilifu anakuwa
mfalme wa mji ule.
Utenzi huu una mwelekeo wa kimaendeleo, unalaani dhuluma, na
kuonyesha kuwa umma ukishirikiana na jeshi unaweza kumwondoa mtawala mwovu.
Unafundisha kuwa mali lazima itumike kuwafaa watu; si vizuri kwa tajiri kujiona
na kuwa na kiburi. Huu ndio mchango mkubwa wa kimaudhui aliotuachia mtunzi Mwana
Bukhalasi.
Kifani, huu ni utenzi wa majaribio ambao mtunzi anautumia
kusimulia hadithi ya kubuni (fiction). Hivyo, tunaweza kusema kuwa
mwanamke huyu ni miongoni mwa watangulizi wa utunzi wa hadithi za kubuni au
riwaya katika fasihi ya Kiswahili. Tofauti pekee ni kwamba "riwaya" hii
imeandikwa kishairi badala ya kuandikwa katika nathari.
2.5 Nana Somo (Labda Karne ya 18)
Hatuna habari kamili za mtunzi ajulikanaye kwa jina la Nana
Somo. Tunachojua ni kwamba, kwa mujibu wa jina lake, alikuwa ni mwanamke, na kwa
mujibu wa lugha aliyoitumia huenda aliishi sehemu za Pate au Lamu. Muundo na
msamiati wa lugha yake unaonyesha kuwa huenda mshairi huvu aliishi katika karne
ya kumi na nane au kabla.
Nana Somo ametunga utendi uitwao Vita vya Hunaini
(Umenukuliwa na P. Ridhiwani, TUKI). Kwa wakati huu hatuna habari zozote kuhusu
maandishi yake mengine. Hata hivyo, utenzi huu pekee unathibitisha kuwa Nana
Somo alikuwa ni mshairi bingwa na ambaye mchango wake katika fasihi ya Kiswahili
ni mkubwa.
Kwa ufupi, Utenzi wa Vita vya Hunaini husimulia kisa cha
mapambano kati ya Uislamu na "Ukafiri" huko Arabuni enzi za Mtume Muhamad.
Mashujaa wa utendi huu ni Mtume Muhamadi, Sh. Ali bin Abitwalib, Abubakari na
wafuasi wao. Wapinzani wao, ambao mtunzi anawaita "maluuni" ni Maliki bin Aufi,
Said bin Ashirafu, Dhatil Himari na wafuasi wao. Wababe wakuu utamboni ni Sh.
Ali upande wa Waislamu, na Dhatil Himari upande wa wasio Waislamu. Pambano la
mwisho kubwa ni kati ya wababe hawa wawili. Katika pambano hilo Ali anamshinda
na kumwua Himari. Ushindi huo wa Ali ni ishara ya ushindi wa Uislamu dhidi ya
"ukafiri"
Ufundi wa mtunzi unajitokeza katika usimuliaji. Anafaulu
kudumisha taharuki au msisimko katika masimulizi yake, kumfanya msomaji
ashawishike kuendelea kusoma hadi mwisho wa utendi. Tazama, kwa mfano, beti
zifuatazo (84 - 91) ambazo zinaonyesha welewa mkubwa wa hulka ya binadamu mwenye
kushikilia lengo fulani:
Wali kati majilisi, kwa direi na libasi,
Wakutene mafarisi, na uda za kuwaniaWakutene majifiri, Maliki katafakari
Pawele kwimba shairi, na kilio akaliaKimba kitafuna meno, na kuiuma mikono
Ghadhabu zikenda mno, shungi mtanga katiaAkipasua na nguo, mwilini aveeyo
Jamii wakuteneo, wote wakimwangukiaKipija mayowe kimba, kikoroma kana simba,
Hata kuvuka kiemba, kwa ghadabu kumngiaWakanena asikari, wata huzuni amiri,
Na huyo tumwa Bashiri, tutakwenda kumuuaMtume tukuwetee, pamwe na bumu amuye
Aili yake isiye, nisimsaze mmojaMaliki akifahamu, nia za wale kaumu,
Kangiwa na tabasamu, na moyo ukamtua.
Katika beti hizi, Maliki, kiongozi wa wasio Waislamu, anataka
mapambano yaanze lakini anachelea kuwa wenzake watampinga, hivyo anafanya visa
ambavyo vinafaulu kuwashawishi wamuunge mkono.
Tukio jingine linaloonyesha jinsi mtunzi anavyoielewa fika tabia
ya binadamu ni wakati Himari anapopambana na Ali. Kwa akili kubwa mkewe Himari
anavua ukaya wake na kumpa mtumwa wake ampelekee Himari na amwambie kuwa
asipomuua Ali na kuurejesha huo ukaya ukiwa na damu basi ajue kuwa hatokubali
kukutana naye tena nyumba moja (beti 772 - 78). Mbinu hii inafaulu kumwongezea
Himari mori wa mapambano.
Utendi huu unajaribu kuhuisha historia ya ushindi wa Uislamu
huko Arabuni katika karne ya saba. Ushindi huo uliashiria mapinduzi makubwa
katika jamii ya wakati huo, na umekuwa ni ishara ya tumaini na kichocheo cha
mapambano ya Waislamu hadi leo hii. Hivyo mtunzi huyu anatumia historia na
visakale kuhalalisha na kuendeleza mapambano ya jamii yake ya wakati alioishi.
2.6 Mwana Kupona Bt Mshamu (kama 1810 - 1860)
Mwana Kupona ndiye mshairi mwanamke anayefahamika zaidi, japo
ufundi wake wa utunzi, kama anavyokiri mwenyewe katika ubeti wa 92, si mkubwa.
Mwana Kupona alizaliwa Pate, labda kunako mwaka 1810. Anafahamika kwa utenzi
wake uitwao Mwana Kupona aliotunga kumwusia binti yake, Mwana
Hashima bt. Sheikh (1841 - 1933) kama mwaka 1858. Utenzi huu umechapishwa
katikavitabu vingi (k.m. Allen 1971: 55 - 75) na unasomwa sehemu zote za pwani
ya Afrika Mashariki. Kadhalika, utenzi huu umekuwa ukisomwa mashuleni. Hivyo,
hakuna haja ya kueleza mengi katika makala haya.
Mwana Kupona aliutunga utenzi huu wakati wa ugonjwa wake
alipojihisi kuwa yuakaribia kuiaga dunia. Aliukusudia uwe ni mwongozo kwa binti
yake, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka kama 18. Huo ulikuwa ni mwaka
1858. Miaka miwili baadaye Mwana Kupona alifariki dunia.
Hivyo, basi, utenzi huu ulikusudiwa uwe ni badala ya mzazi, utoe
maonyo na mawaidha ya kumwongoza msichana katika maisha yake, hasa ya unyumba.
Mafunzo yaliyomo katika utenzi huu ni yale yaliyokuwa yakifuatwa na wanawake wa
tabaka la juu lililoishi katika majumba ya mawe katika miji ya mwambao. Kimsingi
funzo kubwa linalotolewa ni kuhusu utii:
Kwanza mwanamke anatakiwa amche Mungu:
La kwanda kamata dini
Faradhi usiikhini
na sunna ikimkini
ni wajibu katitia
(ubeti 12)
Pili, awatii watawala:
Tena mwanangu idhili
mbee za makabaili
uwaonapo mahali
angusa kuwenukia
(ubeti 15)
Tatu, awatii wazazi:
(Radhi) Nda Mungu na Mtumewe,
baba na mama wajuwe
na ya tano nda mumewe,
mno imekaririwa
(ubeti 23)
Nne, amtii mume:
Keti naye kwa adabu,
usimtie ghadhabu,
akinena simjibu,
itahidi kunyamaa
(ubeti 28)
Kilala siikukuse,
mwegeme umpapase,
na upepo asikose,
mtu wa kumpepea
(ubeti 62)
Mpumbaze apumbae,
amriye sikatae,
Maovu kieta yeye
Mungu atakulipia.
(ubeti 36)
Sehemu kubwa ya utenzi huu ni kuhusu wajibu wa mke kwa mumewe,
na namna mwanamke anavyopaswa kutenda awapo miongoni mwa watu wa aina
mbalimbali.
Kwa ufupi, Mwana Kupona hakuwa mwanamapinduzi. Utenzi wake
haukukusudiwa kubadilisha mfumo wa jamii bali kuudumisha kama ulivyokuwa. Ni
utenzi unaoendeleza unyonge wa mwanamke. Hata hivyo, utenzi huu ni muhimu katika
fasihi ya Kiswahili kwa vile umetuachia rekodi nzuri ya ada na mila za unyumba
za wakati huo, na ni kipimo kizuri cha kiwango cha mwamko wa wanawake wa tabaka
la juu kuhusu masuala hayo.
2.7 Saada Thji li Arifina (Karne ya 18)
Mpaka hapa tumejadili tungo za wanawake ambazo, kwa kiasi
kikubwa, hazikugongana na mfumo wa jamii uliokuwepo; watunzi hawakuwa waasi,
walikuwa watiifu.
Saada Taji yu tofauti; yeye ni mlalamishi, ni mtetezi wa
wanawake, ni mpinzani wa hali iliyopo, hasa katika maisha ya ndoa. Kwa bahati
mbaya hatuna tungo nyingi za mwanamke huyu, wala habari zake. Shairi lake pekee
tulilo nalo ni lile lililochapishwa na Knappert (1979: 192 - 3) kwa jina la
"Malalamiko ya Mke". Shairi linalalamika juu ya mateso yanayomsakama mwanamke
huyu nyumbani mwa mumewe. Mume wake kila mara anamnunia, ameacha kuja nyumbani
mwake, amempora mahari yake, na sasa anataka kumpa talaka. Shairi hili linagusa
moyo sana. Baadhi ya mistari yake inasema hivi:
Sikwima, siwasilepo
kukanda na kupapasa
kwa mume siambilepo
neno iwi kukusa
Wala simetendilepo
la unashiza kabisa
nali mwenye, ni mwangusa
ni mtiiye muowa...
Ni wazi kuwa mama huyu anayafuata kwa makini mafunzo ya unyumba
(kama yalivyoelezwa na Mwana Kupona). Hata hivyo, mumewe haridhiki:
Sasa ali awiile
haji hapiti nyumbani
na mahari atwazile
hata poso za zamani
Mwishowe Saada anagundua kwamba utii wake hautamsaidia ikiwa
atakuwa amefungwa pingu:
Mnyuamoyo kikiri
si ada kutiwa pingu...!
Hili ni shairi la pekee linaloonyesha kuwa kufuata mafunzo ya
Mwana Kupona si lazima kufanikishe unyumba.
3.0 Washairi Wasiofahamika Majina
Wapo washairi wengi wa kike walioacha tungo bora lakini ambao
majina yao hatuyafahamu. Wengi wa washairi hao ni waimbaji wa fasihi simulizi.
Nyimbo nyingi za Kiswahili, hasa zile zenye kuhusiana na shughuli za wanawake,
hutungwa na wanawake wenyewe na kueleza hisia za dhati za wanawake hao juu ya
hali zao (mfano mzuri ni nyimbo za kubembeleza watoto zilizonakiliwa na Velten
1903: 16 - 17).
Mbali na tungo simulizi, zipo pia tungo za wanawake
tulizozipokea katika maandishi ambazo zinadhihirisha ufundi wa wanawake hao
kisanaa na unyonge wao kimaisha. Mfano mzuri ni wimbo wa majibizano kati ya mama
na binti yake kuhusu suala la ndoa. Binti analalamika kuwa anateswa na mumewe,
japo anajitahidi kufuata mafunzo ya mama yake kuhusu unyumba:
A. Mamangu we hunambia kwamba ukae nae sana mumewu
Mkhadae kwa ada na esha umpoke kulakwe na nguo
Kula nala na nguwo navaa siyo mume unindoziwo
B. Lakini nani yule mumewo akupaye kulakwe na nguwo?
A. Namwiza yuna tabia mbi na khuluka kama jogowo
Kula kwake kwa maneno mawi na nguo ina masumbuo
Kucha kucha silali kwa tenge kutendea inda na pwewo
Kunambia ondoka tutete tusikize wanzi wapitawo
Tusikize wawinda wa mwitu na wa pwani wendao mwambawo
Nawauza munambie kweli hali ndiyo watu wakaawo
Nizuiwe na wangu wandani hapa mtu mmoya ayawo
Nizuiwe na wangu wazazi sina nyumba moya ningiawo
Shairi hili linaonyesha kuwa wanawake hawakuwa watiifu tu
nyakati zote, wakati mwingine walisaili hali zao na kuzihakiki jamii zao. Huu ni
ukweli mmojawapo unaojitokeza katika tungo tulizoachiwa na washairi wanawake wa
enzi za urasimi.
4.0 Tamati
Makala haya yamedhihirisha mambo kadha:
Kwanza, yamedhihirisha kuwa palikuwa na watunzi wanawake
waliotoa mchango mkubwa katika ushairi wa Kiswahili wa kipindi cha Urasimi. Papo
hapo, makala yameonyesha kuwa bado yapo mapengo mengi katika habari
tunazozifahamu kuhusu watunzi hao wa kike. Hivyo utafiti zaidi unahitajika.
Pili, makala yamepitia kwa ufupi maudhui na sanaa ya kazi za
watunzi hao wanawake. Imedhihirika kuwa hawakuwa na fikra za aina moja, baadhi
walikuwa ni watetezi wa mfumo wa jamii uliokuwepo, baadhi walikuwa ni wahubiri
wa dini na maadili, na baadhi walikuwa ni wahakiki wa jamii. Hata hivyo, wote
walikuwa ni waumini wa dhati wa dini ya Kiislamu, na kwa jumla maudhui yao
hayakuvuka mipaka ya mafundisho ya dini hiyo.
Labda suala ambalo lafaa kujadiliwa ni kuhusu umuhimu wa kazi
hizi na nyingine ambazo kijuujuu huonekana kuwa ni za kidini. Nafikiri umuhimu
wa tungo hizi unategemea mambo mawili: kwanza ni maudhui na sanaa yake, pili ni
wakati.
Kimaudhui, tendi za aina hii husimulia kisa cha ushindi wa
Uislamu dhidi ya mifumo ya jadi huko Arabia katika karne ya saba. Kihistoria
ushindi huu haukuwa wa kidini tu, bali ulikuwa ni wa kijamii. Uislamu ulileta
mapinduzi katika mfumo wa jamii na fikra wa wakati huo, na hivyo ulikuwa ni
tukio la kimaendeleo. Hivyo, kihistoria maudhui ya tendi na tungo nyingine za
aina hii yana manufaa hata kwa wasomaji wasioamini.
Kiwakati, tendi hizi ziliandikwa kwenye kipindi kigumu cha
mapambano kati ya Waswahili na wavamizi wa kigeni, hasa Wareno. Hivyo tendi za
aina hii zilikuwa ni silaha ya mapambano hayo. Ingawa zilitumia visa na ishara
za kidini, lakini visa na ishara hizo ziliweza kuhusishwa na mapambano ya wakati
uliopo, na kuwaaminisha Waswahili kuwa ushindi wao dhidi ya wageni ni sawa na
ushindi wa Uislamu dhidi ya "ukafiri". Kwa hiyo si jambo la kushangaza kuona
kuwa mtunzi wa Siri li Asirari anawaweka wazungu na
"makufari" katika daraja moja anapozungumzia uwezo wa hirizi ya "Siri Sirini".
Ambao kwamba wendiwa
Hirizi huitukuwa,
u pamoya na Moliwa
Rabi mterehemeziU pamoya naye Mungu,
Muumba nti na mbingu,
hata akiwa mzungu
Maisha memhifazilyapokuwa kafiri
ya Rabi memsitiri,
milele hana hatari
kula takapobarizi
(Siri li Asirani, beti 214 - 216)
Kwa upande wa sanaa, tunatumaini kuwa makala haya yamethibitisha
kuwa ufundi wa utunzi si milki ya wanaume peke yao. Watunzi hawa wanawake kwa
kila hali ni mabingwa wa matumizi ya lugha kisanaa katika uteuzi na upangaji wa
maneno yao, katika matumizi ya lugha kutoa picha za mawazoni kama vile sitiari
na ishara, katika matumizi ya vipengele vingine vya nudhumu, kwa mfano, vina,
mizani na takriri, na katika mbinu za kusimulia hadithi bila kumchosha msomaji.
Hatuna shaka kuwa mchango wa kina mama hawa katika ushairi wa Kiswahili ni
mkubwa na unastahili kutambuliwa.
Tanbihi
1. Kwa mfano. usemi wa Kezilahabi (1983: 144) kuwa
"Utenzi wa Mwana Kupona 1858) ndio utenzi pekee wa zamani
ulioandikwa na mwanamke" unahitaji kusahihishwa.
2. Utendi pekee unaoweza kuwa wa zamani zaidi ni Hamziya.
Bali tarehe ya Hamziya inatatanisha. Knappert (1979:104) anafikiri
uliandikwa mwaka 1652, lakini baadhi ya wataalamu (k.m., Mkelle 1976;
Hichens, 1939:10), wanaeleza kuwa ulitungwa mwaka 1749.
3. Maendelezo ya jina hili "Bukhalasi" hayana hakika sana.
Mnukuzi Allen (1971:130) anatueleza kuwa alilinukuu jina hilo kwa kubahatisha tu
kwa vile herufi yake moja (inayowakilishwa na "kh") ilikuwa imechafuliwa na doa
na haikuweza kusomeka sawasawa.
Marejeo
Abdulaziz, M. (1979) Muyaka: Nineteenth Century Swahili
Popular Poetry. Kenya Literature Bureau, Nairobi.
Aidarus, S. (1749/1652) Hamziya. MS uko katika Maktaba ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Allen, J.W.T. (1971 Tendi. Heinemann, London.
Arnold R. (1973) "Swahili Literature and Modern History: A
Necessary Remark on Literary Chriticism" Kiswahili 42/1 &
43/1: 68 - 73.
Dammann, E. (1940) Dichtungen in der Lamu Mundart des
Suaheli. Hamburg.
Gerard A. (1981) African Language Literatures. London.
Harries L. (1962) Swahili Poetry. Oxford University
Press, London.
Hichens, W. (1941) "Swahili Prosody" Swahili 33/1
(1962/3).
Kezilahabi, E. (1973) "The Development of Swahili Poetry 18-
20th Century" Kiswahili 42/2, 43/1:62-67.
(1982) "Uchunguzi katika Ushairi wa Kiswahili" katika TUKI
Makala za Semina III 144-163
Knappert. J. (1967) Traditional Swahili Poetry. E.J.
Brill, Leiden.
(1979) Four Centuries of Swahili Verse. Heinemann,
London. Mkelle, M.B. (1976) "Hamziya, the Oldest SwahUi Translation"
Kiswahili 46/1
Mulokozi, M.M. (1975) "Revolution and Reaction in Swahili
Poetry" Kiswahili 45/2.
(1982) "Protest and Resistance in Swahili Poetry"
Kiswahili 49/1 25-54.
Muyaka bin Haji (1940) Diwani ya Muyaka (Mh. W. Hichens).
Witwatersrand University Press, Johannesburg.
Mwana Bukhalasi (?) Utendi wa Masahibu katika
Allen, 1971: 130- 268.
Mwana Khamisi Mwinyi Mvita (1660?) "Mzungu Migeli" katika
Hichens 1941: 123.
Mwana Kupona (1858) Utendi wa Mwana Kupona
katika Allen 1971. Mwana Said Amin (?) Utendi wa Fatuma katika Dammann
1940: 92- 140.
Mwana Shekhe Bwana Lemba (?) Siri li Asirari katika
Damman 1940: 214-275.
Nana Somo (karne ya 18) Utendi wa Vita vya Hunaini. (Mh.
P. Ridhiwani). TUKI, 1986.
Nasir, Said Abdallah (1800) Al-Inkishafi (Mh. Hichens,
1939, Chapa ya 2, 1972). Oxford University Press, Nairobi.
Ohly, R. (1973) "Historical Approach to Swahili Literature as
Heretofore an Open Question" Kiswahili 43/2: 79-87.
Ohly, R. (1980) "The Bitter Attraction ofthe Bourgeoisie" katika
Schild, U (Mh.) The East African Experience: Essays on English and
Swahili Literature. D. Reimer Verlag, Berlin.
Saada Taji (?) "Malalamiko ya Mke" katika Knappert 1979: 192-3.
Sharrif, I.N. (1985) "Review ofFour Centuries of Swahili
Verse (J. Knappert) Kiswahili 51)
Steere, E. (1906 Ch. ya kwanza, 1867) Swahili Tales. Bell
and Daldy, London.
Topan. F.M., (Mh) (1971) Uchambuzi wa Maandishi ya
Kiswahili. OUP, Nairobi.
TUKI (1983) Makala za Semina ya Kimataifa ya
Waandishi wa Kiswahili Jz. III: Fasihi. TUKI, Chuo Kikuu Dar
es Salaam.
Velten, C. (1903) Desturi za Wasuaheli. Goettingen.
Whiteley, W. (1969) Swahili: The Rise of a National
Language. Methuen.
London.