UHUSIANO WA MOFOLOJIA NA MATAWI MENGINE

 

Swali hili tumeligawa katika sehemu kuu tatu, sehemu ya kwanza ni utangulizi, sehemu ya pili na mwisho ni hitimisho. Kwa kuanza na utangulizi ni kama ifuatavyo;


Mofolojia ni tafsiri ya neno la Kiingereza “Morphology”. Etimolojia ya neno hili ni Kiyunani “morphe” lenye maana ya muundo au umbo. Aurbach (1971:106) katika Mgullu(1999). Wataalam mbalimbali wamejaribu kutoa maana ya mofolojia katika uwanja wa Isimu.

Mgullu (1999:96) akimnukuu Mathews (1974) anasema kuwa mofolojia ni tawi la taaluma ya isimu ambalo huchunguza maumbo ya maneno na hususani maumbo ya mofimu. Maana hii haijitoshelezi kwani udhaifu wake uko wazi kuwa imezungumzia mofimu kama umbo au maumbo ya maneno ambapo sikweli kwani mofimu ni dhana dhahania ambayo husitiriwa ndani ya mofu.

Mtaalam mwingine ni Hartman (1972) akinukuliwa na Mgullu anasema kuwa mofolojia ni tawi la sarufi ambalo hushughulika na uchunguzi na uchambuzi wa maumbo, fani na aina za maneno yalivyo sasa pamoja na historia zao. Tafsiri hii inaonekana kuchukua vipengele vingi kidogo lakini tatizo lake ni kuwa haijaweka wazi ni kipengele kipi cha fani anachokimaanisha, kwani fani inajumuisha vipengele vingi kama vile: muundo, mtindo, matumizi ya lugha na vingine vingi.

Naye Habwe na Karanja (2004) wanaeleza kuwa mofolojia ni neno linalotumiwa kumaanisha utanzu wa Isimu unaoshughulikia muundo wa maneno. Hajazungumzia kipengele muhimu sana cha maumbo ya maneno.
Mohamed (1986:3) anasema kuwa mofolojia ni taaluma ya sarufi inayochunguza umbo la maneno. 

Fasili hii ina makosa ya kisarufi kwenye umbo la maneno. Kisarufi haiwezekani kusema umbo la maneno bali inatakiwa kuwa maumbo ya maneno au umbo la neno. Ukiachilia kosa la kisarufi hajataja vipengele vinavyoshughulikiwa na mofolojia kama mofu, mofimu, alomofu na neno kama lilivyo lengo la mofolojia.

Kihore na wenzake (2012:7) wao wanaelezea mofolojia kama tawi la sarufi maumbo ambalo huchunguza maneno na aina za maneno. Maana hii haijitoshelezi kwa sababu inaonyesha tu kwamba mofolojia inajishughulisha na kuchunguza maneno lakini hawajasema ni katika kiwango kipi. Na hivyo bado kunahitajika maana nyingine.

Matinde (2012:94) anadai kuwa mofolojia au isimu maumbo ni utanzu wa isimu ambao huchunguza, hupambanua na kuchanganua maumbo ya maneno na aina zake. Hujikita katika viambajengo vya msingi katika lugha mahususi, viambajengo hivi ni: mofu, mofimu na alomofu. Katika taaluma ya isimu mofolojia humaanisha muundo na maumbo ya maneno. Maana hii inakubalika katika taaluma hii kwa sababu imejaribu kuifafanua taaluma ya mofolojia na imejaribu kugusia vipengele muhimu kama vile: maumbo ya maneno na aina zake pamoja na muundo.

Kwa mujibu Hartman (1972), anasema kuwa fonolojia wa sauti zinazotumiwa katika lugha fulani na uwamilifu wao ndani ya mfumo wa lugha inayohusika. Hartman naye anaiona fonlojia kuwa ni taaluma ambayo inayojukumu ya kuzichunguza sauti zinazotumiwa katika lugha fulani pamoja na uwamilifu wa kila sauti katika mfumo huo. Tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa, fonolojia ni taaluma inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa sauti katika mfumo wa lugha mahususi.     

Fudge (1973), fonolojia ni kiwango kimoja wapo cha lugha fulani kilicho na kipashio vidogo zaidi kuliko vipashio vyote vya lugha, vipashio vya kifonolojia ni fonimu na alofoni zake. TUKI (1990), wanasema kuwa fonolojia ni tawi la isimu amablo hushughulikia uchambuzi wa mfumo wa sauti zinazotumiwa katika lugha fulani. Tunaona hapa kuwa fonolojia inaelezwa kama taaluma maalum ya isimu ambayo kazi yake ni kuchambua mfumo wa sauti zinazotuwa katika lugha fulani. Katika fasili hii mambo mawili yanajitokeza, kwanza fonolojia ni sehemu ya lugha fulani na pili kuwa folojia ya lugha fulani huwa na fonimu na alofoni zake.

Richard (1985), anasema sintaksia ni taaluma inayohusu namna maneno yanavyoungana ili kuunda sentensi na vilevile sheria ambazo husimamia uundaji wa sentensi. Katika fasili hii mtaalamu huyu hajatuonesha namna ambayo maneno yanavyoweza kuunda sentensi. TUKI (1990), wanaeleza kuwa sintaksia ni tawi la sarufi linalojishughulisha na uchanganuzi wa mapangilio na uhusiano wa vipashio katika sentensi. Fasili hii haituoneshi uhusiano wa vipashio katika sentensi ni upi na wanamna gani.

Massamba na wenzake (1999), anaeleza kuwa sintaksia ni utanzu wa sarufi unaojihusisha na uchunguzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio vyake. Tunaona kuwa utanzu huu huchunguza sheria na kanuni zinazofuatwa katika kuyapanga maneno ili yalete maana iliyokubalika na kueleweka katika lugha husika. Kwa ujumla sintakisia ni tawi la isimu linalojishughulisha na kanuni, sheria na mpilingilio wa maneno katika sentensi ili kuweza kuunda sentensi, kanuni hizo ni kama vile sentensi lazima iwe na maana, upatanisho wa kisarufi na kanuni zingine nyingi.  

Richard (1985), anaeleza kuwa semantiki ni stadi ya maana, anaendelea kusema kuwa awali neno semantiki lilitumika kumaanisha sayansi yaani maana. Kwa mtazamo huo semantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha ya mwanadamu. Habwe na Karanja (2004), wanaeleza kuwa semantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha ya mwanadamu.
Matinda (2012), anaeleza kuwa semantiki ni taaluma inayochunguza maana katika kiwango leksia, kiwango cha tungo au sentensi na kiwango cha usemi wa matini. Kwa ujumla semantiki ni taaluma inayojuhusisha na uchunguzi na uchambuzi wa maana za maneno, tungo au kiufungu fulani cha matini.

Baada ya kuangazia fasili mbalimbali zilizojikeza katika swali, ufuatao uhusiano na utofauti wa mofolojia na matawi mengine ya isimu.  Kwa kuanza na uhusiano kati ya mofolojia na fonolojia ni kama ifuatavyo;

Uhusiano baina ya mofolojia ni kuwa vipashio vya kifonolojia ndivyo hutumika kuunda vipashio vya kimofolojia. Vipashio vya kifonolojia kama vile fonimu ambapo mfuatano wa fonimu ndio huunda vipashio vya kimofolojia ambavyo ni mofu. Kwa mfano fonimu /i/, /m/, /b/,/a/ huunda mofimu _imb-a, ambapo mofimu ‘imb’ ni mzizi wa kitenzi ‘imba’ na “a” ni kiambishi tamati maana. Hivyo neno ‘imba’ limeundwa na mofu mbili na fonimu nne.
Pia mfano mwingine ni katika neno “anasoma” limeundwa na fonimu /a/,/n/,/a/, /s/, /o/, /m/, /a/ lenye fonimu saba  na mofu nne yaani “a-na-som-a” ambapo mofimu “a” huwakilisha nafsi ya kwanza umoja, mofimu “na” huwakilisha njeo au wakati uliopo, mofimu “som” ni mzizi wa neno au kitenzi na mofimu “a” huwakilisha kiambishi tamati maana.

Mofolojia na fonolojia hutumika katika uchunguzi na uchambuzi wa lugha za binadamu, Massamba (2012), anafafanua kuwa  kila lugha ya binadamu ina mfumo wake wa sauti ambao huongoza ujezi wa maneno wa lugha hiyo, ama kwa hakika fonolojia hujishughulisha na jinsi sauti za lugha zinavyotumika. Hii ikiwa na maana kwamba fonolojia huchunguza na kuchambua sauti za lugha za binadamu kulingana na uamilifu wake katika lugha husika na mofolojia hujihusisha na maumbo ya maneno katika mfumo wa lugha za bianadamu.
                              Kwa mfano neno ‘baba’ limeundwa na sauti /b/,/a/,/b/,/a/ na muundo wa
                              maneno si wowote ule bali lazima ufuate mfumo na taratibu za 
                              zinazokubalika katika lugha husika.
Tunaweza kuona jinsi gani mofolojia na folojia inaweza kuchakata lugha ya binadamu ili kuweza kupata mfumo ambao unakubalika katika kanuni na sheria za lugha za fulani.

Mofolojia na fonolojia yote ni matawi ya isimu, hapa tunaweza kuona taaluma zote hizi zinaunda maarifa na mpangilio wake katika uundaji wa maneno au tungo zenyekuleta maana, kwa hiyo fonolojia hushughulikia jinsi sauti hizo zinavyotumika, zinavyounganishwa na kupangwa katika lugha yoyote mahususi ili kuunda tungo zenye maana. Hivyo taaluma ya mofolojia na fonolojia zinafanya kazi kama taaluma za isimu katika kuchakata lugha.

Mofolojia inahitajika sana katika taaluma ya fonolojia, kanuni za kifonolojia hutumika kueleza maumbo ya kimofolojia ambayo yanaathiriana, kwa mfano kipashio [mu] kama kinavyojitokeza katika mifano hapa chini kinajitokeza kama /mw-/ inapofuatwa na irabu yaani /mu/®[mw]-I ≠u  kwa mfano:- muizi→mwizi, mu-alimu→mwalimu na muaka→mwaka na kanuni hii hujulikana kama kanuni ya uyeyushaji.

Pia ili mofu iwe na muundo sahihi ni lazima itegemee mpangilia mzuri wa fonimu. Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili  neno “amekuja” ukibadili mpangilio  wa fonimu na kuwa “jakuame” haiwezi kuleta umbo sahihi katika lugha ya Kiswahili.
Mofolojia na fonolojia japo kuwa zinahusiana ila kwa upande mwegine husigana kama ifuatavyo;
Mofolojia na fonolojia hutofautiana katika vipashio, matawi haya ya isimu yanatofautiana katika upande wa vipashi ambavyo vinaunda mofolojia na fonolojia ambavyo kwa upande wa fonolojia kipashio cha msingi ni fonimu ambacho ni kitamkwa kilichobainifu katikaa lugha fulani maalumu ambacho kinawezaa kujenga maneno yenye maana au kinachoweza kubadili maana za maneno.
                              Kwa mfano, a) neno ‘pata’ ukitoa sauti /p/ na kuweka sauti /b/ na kuweza
                              kubadilika na kuwa ‘bata’.
                                                   b) neno ‘kaka’ ukitoa sauti /k/ na kuweka sauti /p/ na kuweza
                              kubadilika na kuwa ‘paka’.
Pia, mofolojia kipashio chake cha msingi ni mofu ambacho kina uamilifu yaani kilicho na kazi ya kisarufi na ambacho hakiwezi kunjwa vunjwa au kugawanywa katika viapande vingine vidogo vidogo.
                              Kwamfano,  Pat+an+ish+a katika neno patanisha kuna mofimu nne ambazo ni
(1)   Pat (2)-an (3)-ish (4)-a   
Kutokana na mifano hiyo tunaweza kusema kunautofauti wa vipashio kati ya mofolojia na fonolojia.
Ufuatao ni uhusiano baina mofolojia na sintaksia kama ifuatavyo.
Mofolojia ni kitengo kingine cha lugha ambacho kwa mujibu wa Rubanza (1996), ni taaluma inayoshughulikia  vipashio vya lugha kuunda maneno. Kutokana na fasili hii kipashio cha msingi katika uchambuzi wa kimofolojia ni mofu ambacho huunda maneno ambayo ndiyo hutumika kuunda darajia ya sintaksia. Vilevile maumbo ya kimofolojia huathiri vipengele vingine vya kisintaksia. Sintaksia ni tawi la isimu linaloshughulikia upangaji wa maneno na kuyahusisha maneno hayo katika tungo ili yalete mpangilio unaokubalika kisarufi katika lugha husika. Uhusiano wake uko kwamba mofolojia hushughulika na namna maneno yanavyoundwa, maneno hayo hayawezi kuachwa pweke pweke bali huwekwa katika mpangilio maalumu ili kupata tungo inayokubalika, na hivyo mpangilio huo maalumu katika tungo ndiyo sintaksia
1.      Mtoto anacheza
2.      Watoto wanacheza
Katika mifano hii tunaona kwamba mofimu m-na-wa-katika upande wa kiima zimeathiri utokeaji wa mofimu a-na-wa-katika upande wa kiarifu. Pia kanuni za mfuatano na mpangilio wa mofimu au viambishi zikifuatwa huunda maneno katika miundo ya kisintaksia.
                              Mfano: 1. Alicheza = a-li-chez-a
       2. Anaimba=a-na-imb-a
Kwa ujumla kipengele cha umoja na wingi katika maumbo ya kimofolojia ndicho kinachoathiri umbo linalofuata na kuathiri muundo wa sentensi nzima.
 Kusigana baina ya  mofolojia na sintaksia ni kama ifuatavyo;
Tofauti kati ya mofolojia na sintaksia hujidhihilisha katika vipashio vyake, tofauti hizi hujionyesha au kujidhihirisha kwenye vipashio ambapo kipashio cha msingi cha mofolojia ni mofu ambavyo mofu hizo huwa na kazi mbalimbali kisarufi, hutofautiana na kipashio cha msingi cha sintaksia ambacho neno ambapo neno au maneno hayo hutumika kuunda miundo mbalimbali ya sentensi.  
                     Kwa mfano, Pig+an+ish+a katika neno piganisha kuna mofu nne ambazo ni
(1)   Pig (2)-an (3)-ish (4)-a  
Na kipashio cha sintaksia ambacho ni neno huundwa kama ‘mama anapika’
Kutokana na mifano hiyo imeweza kudhihirisha utofauti uliopo baina ya vipashio vya msigi vya mofolojia na sintaksia. 
Hali kadharika kuna uhusiano baina ya mofolojia na semantiki, uhusiano huo unajidhihilisha kama ifuatavyo;
Mofolojia na semantiki zina uhusiano mkubwa kwani wakati mofolojia inapojishuhulisha na uchambuzi na uchunguzi wa maneno na semantiki hutumia maneno hayo kutoa maana inayokubalika katika isimu. Maneno yanayoshughulikiwa na mofolojia sharti yawe na maana ambapo maana hiyo hushughulikiwa kwa kiwango kikubwa na taaluma ya semantiki. Ni wazi kwamba lugha yoyote ile inahitaji kuwa na maana. Katika uundaji wa maneno ambayo ni taaluma ya mofolojia  ni lazima kuzingatia maana ya maneno katika lugha husika.
                          Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili neno “piga” ukibadilisha mpangilio wake  
                          na ikawa “igap” maana ya msingi ya neno hili inapotea kwani “igap” halitakuwa
                          neno la Kiswahili tena labda katika lugha zingine za ulimwengu lakini si katika
                          Kiswahili.
Hivyo, tunaona katika uhusiano huo mofolojia ndiyo msingi mkuu wa semantiki.
Mofolojia na semantiki ni taaluma ambazo kwa upande mwengine husigani, hivyo ufuatao ni utofauti uliopo baina ya mofolojia na semantiki.
Mofolojia hujikita zaidi katika uundaji wa maneno na maumbo ya maneno katika lugha kupitia njia mbalimbali kama vile uambishaji, udondoshaji, urudufishji, uambatanishaji wa maneno, wakati semantiki hujikita na kujihusisha na uchunguzi wa maana katika kiwango cha maneno na sentensi kwa ujumla wake.
                               Kwa mfano, kanuni ya uambatanishaji katika mofolojia hujitokeza kama hivi
(1)   Bata+mzinga= batamzinga,
(2)   Askari+kazu= askarikazu
                             Kwa mfano, semantiki huonyesha au hutoa maana ya maneno au sentensi
                             kama neno ‘nyanya’ lina maana ya ‘bibi’ na lina maana ya ‘kiungo cha mboga’
Kutokana na mifano hiyo inathibitisha utofauti kati ya mofolojia na taaluma nyingine za isimu ikiwemo semantiki kama ilivyojidhilisha katika mifano.
Kwa ujumla, mofolojia uhusiana na kusigana na matawi megine ya kiisimu kama vile fonolojia, semantiki na sintaksia lakini kwa kiasi kikubwa taaluma hizi zina husiana ukilingananisha na kusigana, kwani mofolojia hutegemea sana taaluma ya fonolojia  ambapo inachota fonimu na kuzitumia kuunda maneno, hutegemea pia taaluma ya sintakisia ambapo maneno yanayopatikana kwenye mofolojia yanahitaji yawe na mpangilio maalum. Semantiki inahitajika pia katika mofolojia kwani kama ilivyojadiliwa haiwezekani maneno yaliyoundwa na mofolojia yakose maana, hapa napo mofolojia inahitaji semantiki ifanye kazi. Hoja hizi zinaweza kufikia hitimisho kwamba kutokuwepo kwa taaluma moja kati ya fonolojia, sintaksia na semantiki kutasababisha mofolojia ishindwe kufanya kazi katika uundaji wa lugha  hivyo tunaona mofolojia ni kitovu cha matawi yote kwani ndiyo msingi mkuu kwasababu taaluma nyingine hutumia maneno kufanya kazi zake za kimsingi.   


















MARELEJEO
Aubach, T. (1971). Transformational Grammar: A guide for Teachers. Research Associates Inc:
                       Washington.
Besha, R.M. (2007). Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es Salaam: Mackmillan Aidan.
Fudge, E.C. (1973). Phonolog: Theory and Analysis. Themsoy Learning Amazon.
Habwe, J. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Dar es salaam: TUKI.
Kihore. (2012). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu. Dar es salaam: TUKI.
Massamba, D.P.B. (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sarufi: Sekondari na Vyuo.
                        Dar es salaam: TUKI
Massamba, D.P.B (2012). Misingi ya Fonolojia. Chuo kikuu Cha Dar es Salaam: TATAKI.
Matinde, R.S. (2012). Dafina ya Lugha. Mwanza: Serengeti Educational publishers.
Mgullu, R.S. (1999). Mtaala wa Isimu. Nairobi: Longhorn.
Mohamed, A. M. (1986). Sarufi Mpya. Dar es salaam: Press and Publicity Centre.
Rubanza, Y. I. (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.

Powered by Blogger.