FASIHI

 

UHAKIKI WA RIWAYA YA KUSADIKIKA

UTANGULIZI

Katika kujadili vipengele mbalimbali vya Fani na maudhui vilivyotumiwa katika riwaya ya kusadikika iliyoandika na Shaaban Robert Washiriki hatukujikita zaidi katika kujadili maana ya riwaya za wataalamu mbalimbali bali tuliweza kujadili kazi hii kwa kuchambua vipengele vya fani na maudhui kutokana na masimulizi ya nchi ya Kusadikika. Masimulizi ya kitabu kwa kifupi.

Riwaya ya Kusadikikani kitabu kinachoelezea masimulizi ya nchi ya kusadikika ambayo mwandishi ameanza kwa kusimulia tukio la kushitakiwa kwa Karama ambaye ndiye Mhusika mkuu kwa tuhuma za kuihujumu serikali ya Kusadikika. Kwa maelezo ya Waziri Majivuno aliwasilisha mashitaka haya mbele ya Mahakama eti kwa sababu Karama alikuwa akitoa elimu ya sheria ambayo kwa Mtazamo wa Waziri huyu alidai kuwa angewafanya raia wa kusadikika kuelewa haki zao ambako kungepelekea wananchi hao kutotii serikali au kwa namna nyingine kungekomesha unyanyasasaji, uonevu na uongozi mbaya wa watawala wa kusadikika na hivyo waziri Majivuno alijawa hofu kubwa sana. Riwaya imeendelea kusimulia namna mshitakiwa Karama alivyowasilisha utetezi wake mbele ya Mahakama ya Kusadikika iliyoundwa na Mfalme na Madiwani. Karama aliwasilisha utetezi huo kwa kuthibitisha jinsi serikali ilivyoshindwa kuthamini michango mbalimbali ya wananchi wake kwa kuelezea historia wajumbe mbalimbali waliojitoa kwenda kufanya utafiti wa namna ya kuendeleleza nchi yao. Masimulizi yake yaliwataja hasa wajumbe 6 waliotumwa mipakani au pande zote 6 ambazo nchi ya kusadikika inapakana nayo. Pande hizo niKaskazini, Mashariki, Kusini, Magharibi, Mbinguni na Ardhini.

Hatima ya wajumbe hawa ambao walikuwa wazalendo waliishia Kifungoni pindi waliporejea kutoka walikotumwa. Mwisho wa riwaya hii mwandishi anaelezea hukumu ya Karama ambapo Mahakama iliyoongozwa na Mfalme ilivyomtoa hatia mtuhumiwa kwa kauli moja ya kuwa hana hatia na Mfalme kuagiza wajumbe wote waliokuwa wanatumikia kifungo kufunguliwa na kulipwa fidia kwa kunyanyaswa pamoja na jitihada zao.

 Baada ya muhtasari wa masimulizi ya nchi ya kusadikika niliweza kujadili vipengele vinavyounda Fani na Maudhui ya kazi ya riwaya ya kusadikika kama ifuatavyo;-

Fanini ujuzi au Mbinu mbalimbali azitumiazo msanii kuwasilisha ujumbe au Fikra zake kwa hadhira aliyoikusudia. Fani inaundwa na vipengele vya Mandhari, Wahusika, muundo, Mtindo na Matumizi ya lugha. Maudhui ni jumla ya mawazo yanayowasilishwa na msanii wa kazi ya kifasihi katika kazi yake. Maudhui huundwa na vipengele vya Dhamira, Ujumbe, Falsafa, Migogoro, Mtazamo na Msimamo. Uchambuzi wa Vipengele mbalimbali alivyovitumia mwandishi wa riwaya hii ya Kusadikika ni:

Mandhari: ambayo humaanisha mahali au sehemu ambayo tukio linafananyika. Mwandishi ametumia mandhari ya Kufikirika ambayo haiwezi kujidhihirisha kwa macho ya kawaida (haionekani) kwani ni nchi inayoelea angani. Pia ametumia mji wa sadiki na mipaka au pande sita zinazopakana na nchi hii za Kaskazini, Mashariki, Kusini, Magharibi, Ardhini na Mbinguni.

Wahusikani mtu au watu, wanyama, na mimea anaotumia mwandishi katika kuwasilisha kazi yake kwa hadhira iliyokusudiwa. Kwa kiasi kikubwa Mwandishi ametumia Wahusika ambao aliowapa majina yanayosawiri tabia zao na wahusika ambao hawabadiliki badiliki ;-

Karama, Huyu ni mhusika mkuu ambaye pia alikuwa Jasiri na Shujaa, Mwanasheria, Mzalendo mtetezi wa haki na Mshitakiwa. Vilevile mhusika huyu alichorwa mwema kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Majivuno, Waziri wa kusadikika, mwenye uchu wa madaraka, mwenye haiba, asiye na uzalendo, kiongozi anayelindwa na Mfalme na asiye na shukurani. Mfalme, Kiongozi wa kusadikika, Katili, Mjinga, mwenye tama ya uongozi, mkuu wa baraza la Mahakama. Madiwani, Wasaliti, wakuu wa mahakama, waonevu, wakatili, wenye dhuluma na sio wazalendo. Mudir wa sheria, mwanasheria wa serikali, Mjinga, msaliti na asiye mzalendo. Buruhani, Mjumbe wa kaskazini, Jasiri, Mzalendo mpenda haki, Mwanaharakati, Mfungwa na maskini. Msanii anasema “Hii ilikuwa safari ya ujasiri iliyotaka uthabiti na matumaini, mwenye heshima, hodari na mwaminifu alitakiwa ajitolee mwenyewe kwa safari hii” uk.12. Fadhili, Mjumbe aliyetumwa mashariki, Jasiri, Mzalendo, mpenda haki, Mfungwa na maskini. “Mtu mwenye sifa njema alitakiwa kujitolea mwenyewe kwa ujumbe wa mashariki na mtu kama huyu alipatikana upesi sana kuliko ilivyokuwa ikitazamiwa” uk.16. Kabuli, Mjumbe wa kusini, jasiri, Mzalendo, Mpenda haki, Maskini na mfungwa. Auni, Mjumbe wa Magharibi, Jasiri, Mzalendo, Mpenda haki, Mwananchi wa kawaida na mfungwa. Sapa na Salihi, walikuwa vipofu, wananchi wa magharibi, Sapa alikuwa mwenye tama na wivu, Sapa alikuwa mpole, Sapa aliomba upofu. Radhaa, mjumbe wa mbinguni, Jasiri, mzalendo, mpenda haki, Mfungwa na Maskini. Amini, mjumbe wa ardhini, Jasiri, mpenda haki, mzalendo na mfungwa. Wahusika wengine ni wananchi, bwana Taadabuni, katibu wa serikali, bwana Komeni, Amiri jeshi, bwana fujo, mlinda hazina, bwana Baromini na wananchi wa pande zingine.

Muundo,ni namna au jinsi mwandishi anavyopangilia visa na matukio katika kazi yake ya kifasihi. Mwandishi ametumia muundo wa moja kwa moja ambapo katika mpangilio wa masimulizi ameanza mwanzo wa kisa kwa kuonesha jinsi mashitaka yalivyowasilishwa, kukafuatiwa na utetezi wa mshitakiwa au kile mwandishi alichokiita maombezi mbele ya Mfalme na Madiwani kwa kusimulia historia ya kusadikika kupitia wajumbe sita waliotumwa pande sita na kuishia kifungoni kama sehemu ya pili ya kisa na hatimaye alimalizia kwa kuelezea hukumu ya kesi ya Karama ambapo Mfalme na Madiwani walionesha kuwa mtuhuma hakuwa na hatia na kufunguliwa kwa wajumbe sita na kuachiwa huru huku Mfalme akiamuru walipwe fidia.

Mtindo.Ni namna mwandishi anavyoiumba kazi yake ya kifasihi. Mwandishi Shaaban Robert ametumia mitindo mbalimbali katika kazi hii ya riwaya ya kusadikika kama vile, ametumia maswali hasa katika sehemu ya mwisho ya kitabu, ametumia dayalojia kati ya Sapa na Salihi uk. 29, ametumia masimulizi kwa kiasi kikubwa katika kazi hii ambayo kwake ndio mbinu kuu pamoja na matumizi ya nafsi ya pili na tatu umoja na nafsi ya tatu wingi sehemu kubwa ya riwaya.

Lugha. Mwandishi ametumia lugha ngumu ambayo si rahisi kueleweka kwa msomaji kutokana na kutumia misamiati isiyoeleweka. Hali hii ya kutumia lugha ngumu ililengwa kukwepa makucha ya wakoloni. Mfano wa misamiati hiyo ni sudusi, takirifu, kafaungo, hutasawari, akapatilizwa, ali, kujikagajuu, Kuyabisika, kujikaga, Kadura n.k. Pia mwandishi ametumia vipengele vya Tamathali za semi ambazo ni ;- Methali. Kitanda usichokilalia hujui Kunguni wake. Msiba wa kujitakia hauna kilio. Lila na fila hawatangamani. Misemo. Kumtosa mshitakiwa katika bahari ya maangamizi. Tashibiha. Umri wake mkubwa ulizofanya nywele zake za kichwani kuwa nyeupe kama fedha. Uso wa kipofu wa kwanza ulikuwa na furaha kama bwana harusi. Alikuwa na tabia ya kuficha siri kama kaburi lifunikalo maiti. Anamaneno kama kitabu Tashihisi. Giza limezalo nuru na ufupisho uoni wa macho. Wakati una mabawa kama ndege uk. 11. Jina la Kitabu (KUSADIKIKA). Jina la kitabu linasawiri yaliyomo katika riwaya hii kwani limetokana na neno “sadiki” likimaanisha “Amini” hivyo linaweza kusemwa kuwa ni kuaminika. Mwandishi anatuonesha kuwa Wasadikika ni wajinga kwani hawakujihusisha na uchambuzi wa masuala yake waliishia kuamini na kukubali kila jambo mwandishi anasema “Imani ya Kusadikika ni nguzo imara ya majengo ya utawala wa Wasadikika” wakati mataifa mengine yalipojifananisha kwa mambo kama vile enzi, uwezo na fahari nyingine taifa la kusadikika lilijivuna kwa sababu ya kusadiki mambo yaliyotoka vinywani mwa watu wake” uk. 4-5. Kwa washiriki wa uchambuzi huu wanakiri kuwa kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kuchambua haya katika vipengele vya fani na maudhui alivyotumia msanii Shaabani Robert katika riwaya ya Kusadikika ingawa si vyote vilivyotumika katika vipengele hivi tumeweza kuviainisha. (rejea masimulizi ya kitabu) KIPENGELE CHA MAUDHUI.

Maudhui ni jumla ya mawazo aliyonayo msanii katika kazi yake ya kifasihi, Kipengele cha maudhui kinaundwa na ujumla, dhamira, migogoro, falsafa, Msimamo/Mtazamo. Dhamira mbalimbali Dhamira kuu ni Ukombozi: Dhamira hii ndio kuu katika riwaya ya kusadikika iliojikita kwenye ukombozi wa kifikra na ukombozi wa kisiasa. Mwandishi amemtumia mhusika karama aliyeanzisha elimu ya sheria yenye lengo la kuwezesha wananchi ili wawezekushiriki katika mambo mbalimbali ya nchi. Ukombozi wa kisiasa unarejelea harakati zilizoongozwa na Karama na wajumbe sita zenye lengo la kuleta mabadiliko katika nchi ya kusadikika kuhusu haki na uongozi (viongozi). Msanii anasema “Kwa nini wanasiasa wa kusadikika hawakuwaacha kama Karama kujishughulisha na mambo yaliyowapita vimo vyao” Matabaka. Hali ya wahusika kuwa na hadhi au makundi au madaraja tofauti tofauti. Katika riwaya ya kusadikika ameonesha matabaka ya namna mbalimbali kama;- Tabaka la viongozi na wananchi, matajiri na wasomi na wasio wasomi na wenye haki na wasio na haki. Katika kudhihirisha matabaka haya mwandishi ameeleza kwa mifano baadhi ya maeneo haya anasema “Sheria za wasadikika zilikuwa hazimuamuru mshitakiwa kujitetea juu ya ushahidi wa mshitaki. Aghalabu mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu. Hapana shaka salama ya watu wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi ya kusadikika” uk.7. Uongozi Mbaya. Mwandishi amedhihirisha hili kwa kuwatumia wahusika waziri Majivuno, Wafalme, Madiwani na matajiri ambao ndio waliochorwa kwa taswira ya kuwa Wanahaki zaidi kuliko wananchi wa kawaida. Tunapozungumzia uongozi mbaya ni hali ya utawala kutowajali kwa kuwasaidia wananchi wa kawaida kisiasa, uchumi, na kijamii. “Aghalabu Mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu” uk.7. Uzalendo na ujasiri. Uzalendo ni hali ya mtu kuipenda nchi yake na kujitoa kuipigania katika mambo mbalimbali yanayokwamisha maendeleo. Mwandishi anasema “pigano la kufa na kupona lilikuwa mbele yake” uk.8. “alikuwa hana silaha nyingine za kuokolea maisha ila zana hizi” uk.9. “Msema kweli hukimbiwa na marafiki zake, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa Kitambo nikajinyima ushirika wa milele unaotazamiwa kutokea baada ya kushindwa kwa uongo”uk.9. Mwandishi amewatumia wahusika Karama, Buruhani, Fadhili, Kabuli, Auni, Radhaa, Amini kuonesha ujasiri na uzalendo walijitoa na kufanyakazi katika masahibu mengi tena bila ya kukata tama huku baadhi wakiishia kifungoni. Hatimaye waliweza kushinda. Mwandishi anasema “kwa kazi zake bora na uaminifu mwingi hakushukuriwa bali kuvunjiwa kadiri, aliaibishwa kuwa alileta uzushi ulikuwa hauna faida katika nchi zaidi ya hayo alitumbukizwa katika kifungo cha maisha” Ujinga. Hali ya watu kutoelewa mambo mbalimbali ya msingi kijamii kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi. Mfano haki sheria na uongozi nakadhalika. Shaaban Robert amethibitisha uwepo wa ujinga katika nchi ya kusadikika kupitia viongozi na wananchi waliosadiki mambo yao na kuyakana ya nje. Pia mwandishi amewatumia wananchi waliohudhuria mahakamani siku ya kwanza ya mashitaka. Msanii anasema “Baadhi ya watu wachache waliokuja barazani kusikiliza kesi hii walimsikitikia mshitakiwa wengi walikuwa wakinong’onezana kuwa msiba wa kujitakia hauna kilio” uk 7. “ujinga wao haukuyazuia maendeleo tu lakini hasa ulirudisha nchi nyuma vilevile” uk. 14. “Twaona kuwa mshitakiwa hana hatia ila alikuwa akitafuta jinsi ya kuisaidia sheria ya kusadikika kwa njia ngeni” Maelezo haya ni matokeo ya ufumbuzi wa ujinga uliokuwa umekithiri kwa viongozi wa kusadikika na wananchi wake. Uonevu na Ukandamizaji (kukosekana kwa haki). Hali ya kutothaminiwa, kupewa haki na kuhukumiwa bila ya kufanya kosa lolote, na wakati mwingine kutopewa nafasi ya umuhimu katika tabaka fulani la watu “sheria za kusadikika zilikuwa hazimuamuru mtu yeyote kujitetea juu ya ushahidi wa mshitaki” uk.7. Buruhani, Fadhili, Kabuli, Auni, Radhaa, Amini walifungwa tena kwa kunyanyaswa Mwandishi anasema “Natoa amri watu sita waliotajwa wafunguliwe mara moja, inasikitisha sana kwa dhuluma juu ya watu hawa hazikutengenezwa mpaka leo. Gereza ni makao ya wahalifu na watu hawa si wahalifu” Mhusika mkuu karama pia alishitakiwa na Waziri majivuno kwa hulka tu za ukandamizaji. Umaskini. Ni hali ya kutomudu kujipatia mahitaji mbalimbali ya kila siku kwa kiwango kinachoridhisha (cha kutosha) Mwandishi anasema “kwa kukosekana kwa Madaraja mito inafanya shida juu ya watu walio ng’ambo moja kukutana na Ng’ambo nyingine, maradhi hayajapata uuguzaji, vifo vya mapema hapa katika mwaka mmoja jumla yake yatisha kuliko ile ya vifo vitokeavyo katika nchi nyingine katika karne moja” Uk. 25. Pia “Aghalabu Mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu. Hapana shaka salama ya watu wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi ya kusadikika” uk. 7. Maelezo haya yanaonesha uwezekano mkubwa wa uwepo wa kundi kubwa la watu masikini ambao ndio walioguswa na sheria za kusadikika. Dhamira nyingine ndogondogo zilizomo katika riwaya hii ni tamaa iliyooneshwa kupitia Salihi na Majivuno, Unafiki na woga wa wananchi wa kusadikika, utengano na kukosekana kwa umoja. Migogoro. Hali ya kutoelewa au kuridhishwa na jambo fulani na kupelekea kutoelewana kwa makundi au pande mbili za watu. Katika riwaya hii kuna migogoro ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Migogoro ya kijamii. Mfano wa migogoro ya kijamii ni mgogoro wa Sapa na Salihi uliotokea baada ya Sapa kuomba upofu kutokana na tama ya Salihi kutamani vitu vya Sapa, Mwandishi anasema “kwa sababu hii tuliafikiana kushirikiana kila kitu atakachoomba tukaandikiana hati mbele ya Kadhi. Palepale mwenzangu aliinua mikono yake juu akaomba upofu” uk.30 Mgogoro nafsia: ni hali ya mtu kuhofia jambo fulani na kupelekea mtu huyo kuwa namsongo wa mawazo, Mwandishi amemtumia waziri Majivuno aliyekuwa na hofu ya kupoteza madaraka na kukomeshwa kwa ukandamizaji endapo wananchi wataelewa sheria mbalimbali za kusadikika waliokuwa wakielimishwa na Karama. Hatimaye aliamua kumshitaki katika baraza msanii anasema “Upelelezi huo ulidhihirisha bila ya shaka yoyote kuwa mshitkiwa akiwafunza watu sio kuomba msamaha na huruma katika baraza tu lakini hata kuzibatilisha hukumu za baraza la kusadikika kwa njia zote hii inaonesha kuwa mgogoro mkubwa utakuwako kati ya sheria za nchi na watu wake” uk 2. Migogoro ya Kiuchumi. Mgogoro wa walionacho/matajiri ambao ndio waliopewa haki na upendeleo na Maskini walionyimwa haki hata mbele ya sheria na mahakaka.Katika nchi ya kusadikika watu hawa hawakuweza kabisa kushirikiana.Mwandishi anasema “Aghalabu Mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu. Hapana shaka salama ya watu wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi ya kusadikika” uk. 7. Migogoro wa Kisiasa. Huu ni mgogoro unaowahusisha wanaharakati wazalendo walioongozwa na karama dhibi ya serikali na viongozi wan chi ya kusadikika. Wanaharakati hao walihitaji mabadiliko na walichoshwa na uonevu wa viongozi wao, mgogoro huu ndio uliopelekea wananchi kuishia kifungoni pindi walipojitolea kudai mabadiliko. Ujumbe. Uongozi mbaya unachangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maendeleo ya wananchi. Kuwepo kwa hali ya uzalendo katika nchi ni chachu ya maendeleo na mafanikio katika jamii. Suala la uelimishaji (elimu) ni muhimu katika utambuzi wa wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii.Tamaa na viongozi kujali maslahi kunapelekea hali duni ya wananchi walio wengi. Viongozi wanapaswa kuthamini haki za wananchi wanaowatumikia. Msimamo wa Mwandishi. Msimamo wa mwandishi katika riwaya hii ni wa kimapinduzi kwani anaonesha jinsi jamii ilivyopaswa kujituma tena kwa ujasiri, kupigania haki na mabadiliko ya wananchi wote. Mtazamo wa Mwandishi. Mtazamo wa mwandishi wa riwaya hii ni wa Kiyakinifu kwani kwa kiasi kikubwa umeakisi mambo ambayo yanaweza kufuatwa katika kufanikisha maendeleo ya jamiii yeyote kama vile mgongano wa mawazo uzalendo na ujasiri, uelewa na mambo mengine. Aidha yapo baadhi ya maeneo yanagusia mtazamo wa kidhanifu kama vile kusadiki kila kinachosemwa na watawala. Falsafa ya mwandishi. Falsafa ya mwandishi ni ya wema hushinda ubaya, amedhihirisha hili kupitia mhusika Karama aliyechorwa kama mtu mwema dhidi ya Majivuno aliyechorwa kama mtu mbaya. Kwa taswira hii Karama amewakilisha wema wote katika jamii ya wasadikika na Majivuno anawakilisha wabaya wote katika jamii hiyohiyo. UCHAMBUA WA KITABU CHA MAISHA YANGU NA BAADA YA MIAKA HAMSINI-MWANDISHI: SHAABAN ROBERT UTANGULIZI Kitabu cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini ni riwaya iliyoandikwa na Shaaban Robert (1936-1946) yenye insha na mashairi yanayoelezea mambo aliyoyafanya kuanzia umri wa ujana mpaka uzee wake, pamoja na mafanikio mbalimbali aliyoyafikia, changamoto alizokumbana nazo na namna alivyozitatua. DHAMIRI YA MTUNZI Kwa mujibu ya kamusi ya Karne ya 21(2011) inafafanua kwamba, dhamiri ni ile azma, kusudio au nia ya kufanya jambo. Katika muktadha wa kifasihi tunaweza kusema dhamiri ni lile lengo au kusudi la mtunzi katika kuitunga kazi yake. Na hii inatuthihirishia kwamba, kila mtunzi husukumwa na jambo fulani (ama zito ama jepesi) katika utunzi wake. Hakuna mtunzi anayetunga kazi yake katika ombwe. Mwandishi yoyote yule hata kama anaandika tungo za kubuni, kwa kawaida huwa amesukumwa na jambo au mambo fulani aliyowahi kusikia, kushuhudia katika fikra zake au katika hali halisi maishani; na fikra hizo hujengwa na mambo fulani ya tajiriba halisi katika maisha halisi. Hivyo Shaaban Robert katika kitabu chake cha “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini” suala la msingi lililomsukuma mpaka kuandika kitabu hiki ni kutaka kuweka kumbukumbu nzuri juu ya maisha yake kwa yale yote ambayo aliyafanya akiwa kama mwandishi maarufu wa Afrika Mashariki na Kati, hususani kwa vizazi vijavyo ambavyo havikupata bahati ya kumwona mwandishi huyu, kwa hiyo kwa kupitia kazi yake hii waweze kujifunza mengi na kupata mafanikio katika maisha. NADHARIA YA UHALISIA Kwa mujibu wa Ntarangwi (2004) anasema nadharia hii katika upana wake, humaanisha uwakilishi wa uhalisi wa mambo katika fasihi. Nadharia hii ilizuka katika karne ya kumi na tisa hususani kwa lengo la kupinga mkondo wa ulimbwende. Mhalisia huamini katika matokeo ya mambo na ukweli anaouzingatia ni ule unaoweza kuonekana na kuthibitishwa kwa tajirba. Vile vile, wanauhalisia huiamini demokrasia kama hali ya maisha, na malighafi ya kuelezea maisha ya kawaida, ya kadiri na ya kila siku. Hivyo basi uhalisia hujikita katika mambo yaliyopo, tukio mahsusi na matokeo yanayoweza kuthibitika. Imani ya mhalisia ni kwamba kazi ya fasihi yapaswa kuwaweka wanajamii husika katika ulimwengu wao wa kawaida, wa kweli, na halisi. Hivyo basi hata picha za ulimwengu atakazoumba msanii, zapaswa kudhihirisha hali hiyo. Mhakiki anayezingatia nadharia hii ya uhalisia, hupembua namna mtunzi alivyodhihirisha uhalisi wa mambo kupitia maudhui aliyoyazingatia na wahusika aliowasawiri. Hivyo basi, mhakiki hutizama jinsi ukweli ulivyodhihirishwa katika juhudi za mtunzi za kuchora hali halisi ya mambo katika wakati maalum. Kwa muhtasari basi msanii anatarajiwa kusawiri wahusika, matukio na mandhari yanayokubalika na kuaminika katika jamii ya wakati wake. Ufahamu wa mazingira na maisha anayoyalenga mtunzi ni nguzo muhimu kwa mhakiki wa kihalisia. Shida inayoletwa na nadharia hii ni kuchukulia kwamba uhalisi na maana yake hauna utata wowote katika jamii yoyote, ni kwamba unachukulia kuwa watu wote katika jamii hiyo wanaona uhalisi mmoja na kuwa na fasili sawa kuhusu maisha yao. Haki na uaminifu; Shaaban Robert anaona kuwa uaminifu na kutenda haki ni nuru ya maisha bora kwa mwanadamu hapo baadaye. Dhamira hii inajidhihirisha katika insha yake ya Umri uk.2 anasema, “Milango ya nyuma ya kuifikia bahati ilikuwa mingi lakini haikunishawishi hata kidogo”. Suala hili linahusisha hata katika jamii zetu za leo, kwani watu wengi hutumia milango ya nyuma katika kufikia mafanikio. Kwa mfano; kwa kutoa rushwa, ufisadi nk. Dhuluma na uonevu; Shaaban Robert anaeleza kuwa dhuluma na uonevu vimekuwa ni vipingamizi vikubwa katika mafanikio ya mtu ya kila siku, kwa mfano kama vile kunyimwa jambo fulani au kukandamizwa kwa sababu fulani ni ukuta katika maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla. Jambo hili linajibainisha katika uk.1 “Mara kwa mara niliposimama wima kuiendea niliteleza nikaanguka chini. Nilipotaka kunyoosha mkono kuishika yalitokea mazuio ambayo sikuyatazamia au nilifungiwa milango ya mbele nisionane nayo”. Vilevile katika insha ya Mwandishi S. Robert ameonesha ni kwa namna gani alivyodhulumiwa katika uchapaji wa kazi zake. Kwa mfano, uk.78 anasema; “Kwa kazi yangu iliyoweza kuleta sh.25000/- kwa vitabu 5000/- katika mwaka 1954 sikupewa hata pesa moja ya shaba kwa muda wa miaka kadhaa…sikupata kitu kwa kazi yangu iliyoleta karibu sh.15000/- kwa vitabu 5000/- katika mwaka 1958”. Pia anaonesha ni kwa namna gani alivyozidi kudhulumiwa na hata wale ambao walichukua madaraka baadaye. Mfano; uk.79 “Nilikuwa mtumishi wa bure na mtu wa chini kuliko pembe nyeusi yoyote iliyopata kuwako katika ulimwengu huu. Kwa nani? Kwa wale waliofadhiliwa na waliotajirishwa na waliotumikiwa na waliofunzwa na kazi zangu” Katika jamii yetu ya leo hususani Tanzania tunaona mambo haya yamekithiri sana. Hivyo basi, ili jamii iweze kuondokana na hali hii ni lazima iungane pamoja na kupinga dhuluma na uonevu. Pia kwa kuzingatia haki ya mwandishi S. Robert anasema; uk.80 “Mwandishi si mtu wa ajabu awezae kuishi kwa kula hewa na kunywa ukungu. Ni mtu wa desturi ambaye kama watu wengine wa desturi, hafarijiwi na hasara”. Ugumu wa soko la vitabu; Mwandishi ameonesha ugumu wa suala hili pale alipofungua duka la vitabu lakini watu hawakuhamasika kununua vitabu hivyo, hali hii ilitokana watu wengi kutokujua kusoma na kutokana na utamaduni wa jamii hiyo katika suala zima la usomaji wa vitabu kwani hawakujua thamani yake, kama asemavyo; uk.110 “Walikuwa katika tarehe ya ujinga wa kujua kuwa mazoea ya kusoma yalikamilisha utu wetu katika dunia. Hawakufahamu kwamba katika vitabu ndimo ghala za utamaduni wa elimu zilimopatikana”. Hali hii inahalisika sana katika jamii ya leo kwani watu wengi wanajua kusoma lakini hawana utamaduni wa kusoma hivyo husababisha soko la vitabu kuwa gumu. Uzalendo; Suala hili limeoneshwa na S. Robert jinsi gani alivyokuwa mzalendo kwa nchi yake (Tanganyika) katika kupinga mifumo yote ya kiutawala wa kikoloni ambaye ilimdharau mwafrika hususani katika kipengele hiki cha kisiasa, kuwa mwafrika hawezi kufanya chochote. Mfano uk.75 “Mwafrika aliweza kufanya nini? Alikuwa mtu gani mbele ya watu?” hali hii ilimfanya Shaaban Robert kujitoa muhanga katika kushiriki misafara mbalimbali ya kisiasa ili kuhamasisha maendeleo ya mwafrika, japokuwa gharama zote za safari hiyo zilikuwa juu yake. Na hii ilitokana na hali ya uzalendo iliyojaa kifuani mwake, kama asemavyo katika uk.74“Sikuwa na kago juu ya ari hii. Alivyokuwa kila mtu ndivyo nilivyokuwa mimi vilevile. Nilitekwa na uzalendo kama alivyotekwa mtu yoyote mwingine. Sikupenda kuwa mgeni katika nchi ya asili na uzazi wangu”. Hivyo basi suala hili la uzalendo linahalisika katika jamii ya sasa, kwani watu mbalimbali huingia katika siasa na kutetea maslahi ya haki zao ili kujipatia maendeleo hivyo mwandishi anaitaka jamii ya sasa kujitoa muhanga katika kupingana na utawala mbovu uliojaa dharau kwa wale wanaowaongoza. Kifo na maisha; Haya ni mambo yaliyomo ndani ya jamii, kama binadamu tunapaswa kuyapokea, kuyakubali na pia kuangalia ni kwa namna gani tutakabiliana nayo. Shaaban Robert anaeleza ugumu wa maisha ya upweke na ukiwa na jinsi alivyoyakabili baada ya kufiwa na mkewe Amina. Uk.4 “…mauti yake ya mapema yalikuwa ni msiba na hasara kubwa kwangu.” Lakini Shaaban Robert anatuonesha kwamba pamoja na matatizo hayo jamii inapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu kwani upo wakati mwingine mzuri ujao. Mapenzi ya dhati; Shaaban Robert anaonesha mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo kwa mkewe baada ya kifo. Mfano katika uk.3 anasema, “…tokeo hili lilikuwa pigo kubwa sana kwangu na msiba katika nyumba nzima. Marehemu huyu alikuwa johari ya maisha yangu, tegemeo na mshauri mwema”. Vilevile alionesha mapenzi ya dhati kwa kuwajali wanae ambao nao walikuwa na upweke wa kumkosa mama yao, alionesha upendo mkubwa kwao kwa kutoacha mwanya wa kujisikia wakiwa. Mfano aliwapatia elimu; uk.5 anasema, “…niliwapenda kwa mapenzi sawa kama baba na mama, nikawatunza kama mboni za macho yangu”. Shaaban Robert anaiasa jamii kuwa suala la kulea watoto baada ya kifo cha mzazi mmoja si la mama tu, bali hata baba kama mzazi anapaswa kuwalea watoto walioachwa tena kwa mapenzi yote ya baba na mama, hivyo si budi jamii kubadilika katika hili. Nafasi ya mwanamke; Mwandishi Shaaban Robert anamuona mwanamke kama kiungo muhimu sana katika safari hii ya maisha, anamchukulia katika nafasi mbalimbali kama ifuatavyo: · Mwanamke kama tegemeo na mshauri mwema. Mfano; uk.3 “…marehemu huyu alikuwa jahari ya maisha yangu, tegemeo na mshauri mwema”. · Pia anamuona mwanamke kama mtu mwenye ushirikiano na asiye mvivu. Mfano; uk.3 “…alinisaidia katika mambo mengi wakati wa maisha yetu pamoja ambayo yangalinishinda kuyatenda mimi peke yangu”. Pia hata katika isha ya Idara ya Utawala Shaaban Robert anaeleza uhodari na uchapakazi wa mke wa Mudir. Mfano; uk. 61 “bibi huyu alikuwa hodari na mcheshi sana” · Vilevile anaona mwanamke kama mlezi muhimu sana. Kwa mfano; uk.5 “…nilisikitishwa mno kwa ukosefu wa malezi ya mama yao lakini nilikuwa sina uwezo wa kumwita arudi duniani tena”. · Shaaban Robert anamuona mwanamke kama pambo na faraja katika maisha ya ndoa. Anasema katika uk.3 “Sura yake ilikuwa jamali kwa kimo cha kadirio, uso wake ulikuwa mviringo wa yai, nywele nyeusi za kushuka, paji pana, nyusi za upinde, macho mazuri yaliyokuwa na tazamo juu ya kila kitu, kope za kitana, masikio ya kindo yasiyopitwa na sauti ndogo, meno ya mwanya…” · Mwanamke pia ameoneshwa kama mtu mpole na mwenye heshima. Jambo hili Shaaban Robert ameliweka wazi makusudi ili jamii iweze kuiga na kubadilika kwani wanawake wengi sasa wamepungukiwa na hilo. Mfano; uk.37 “Mke huyu wa pili alikuwa mpole, mwenye madaha na heshima, alikuwa na sura ya haya ambayo ilichuana na utawa kama uso kwa kioo”. Kufanya kazi kwa bidii; Kwa kiasi kikubwa Shaaban Robert ameonesha mfano hai katika utendaji bora wa kazi akiwa kazini, kwani alikuwa ni mtu wa kujituma na vilevile alikuwa ni kiongozi mzuri na mwenye kupenda kushirikiana na wafanyakazi wenzake. Amelibainisha hili kama nyenzo kuu na muhimu sana katika kazi wakati wote, kwani kupitia nyezo hii kuna manufaa mengi sana kama vile kupendwa na watu, kupandishwa cheo na hata kuaminiwa sana ndani ya jamii. Jambo ambalo jamii ya leo yapaswa kuiga. Mfano; uk.41 “Niliaminiwa sana hata kuliko nilivyotazamia. Mapendeleo niliyotendewa yalikuwa mengi sana”. Pia hata katika uk.40 “Nilitenda yote yaliyokuwa katika uwezo wangu kutimiza wajibu”. Pia hata katika Insha ya Idara ya Utawala makarani walikuwa ni wachapakazi. Utu wema, urafiki na uhusiano mzuri na watu; Jambo hili Shaaban Robert ameliona kama nguzo muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu yoyote. Anasihi kuwa maisha ya uadui ni maisha mabaya yasiyo na furaha, hakutaka uadui, kumkwaza mtu, aliishi kwa wema na kujenga urafiki daima. Na hivi ndivyo inavyopaswa kuwa kwa mwanadamu yoyote yule kuenenda, kwani hayo huleta maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla. Mfano; uk.39 “…miguu yangu ilikuwa tayari kwenda kutafuta urafiki…maisha ya uadui kila upande ni mazito kwa mtu yeyote”. Utii na unyenyekevu; Shaaban Robert ameonesha hali ya utii na unyenyekevu kwa wakuu wake wa kazi na hata wafanyakazi wenzake. Mara zote alijidunisha na kujishusha ilihali akiacha watu waseme juu ya uzuri na ubora wake. Mfano; uk.43 alipopandishwa cheo alisema, “Kisha moyo ulinikua kwa kuona kuwa kazi yangu ilikuwa imehesabiwa na kuonekana thamani yake, wakati mimi mwenyewe nilikuwa nimeidunisha”. Uk.45 “Sifa ilikuwa kubwa kuliko niliyotenda, nikainama chini kwa haya; na huzuni ilikuwa kubwa vilevile moyo ukanilemea”. Shaaban Robert anatuonesha kwamba suala hili aliliona tangu hapo mwanzo na ndiyo maana anaifundisha jamii kuwa yapaswa kutenda vivyo hivyo ili iwe taa ya kuangaza na sabuni ya kung’arisha maisha yao. Suala la mirathi; Mwandishi Shaaban Robert anatuonesha ugumu uliopo katika suala zima la ugawanyaji wa mirathi. Suala hili linahalisika hata katika maisha yetu ya sasa tunaona jinsi ndugu wanavyopingana na hata kuchukiana kwa sababu ya mirathi. Kutokana na hali hii Shabaan Robert hajasita kutuonesha umuhimu wa kuacha wasia juu ya ugawanyaji wa mali. Kwa mfano; uk. 48 “Choyo cha warithi mbalimbali kilifanya magawanyo kuwa magumu ajabu” Ubaguzi wa rangi na matabaka; Enzi za ukoloni kulikuwa na ubaguzi wa rangi wa watu weupe na weusi katika mambo mbalimbali ya kijamii, mfano; kusalimiana kwa kushikana mikono, vyombo vya usafiri vilikuwa katika madaraja, daraja la kwanza walikuwa watu weupe (wazungu) wakati daraja la tatu walikuwa watu weusi (waafrika). Vilevile hata sehemu za malazi zilikuwa katika misingi ya kiubaguzi. Shaaban Robert alilionesha hili katika uk.50 “Karibu ningalilala nje Korogwe kwa ukosefu wa malazi ya abiria waafrika”. Pia uk.52 “Huyo alikuwa ni mzungu, hakuwa tayari kushikana mikono na mimi”. Pia hata katika Insha ya Msuso uk.105 anasema; “Mtu yoyote aliyekuwa si mweupe katika Afrika kusini hakuwa na ustahili, dhamani wala heshima ya uanadamu. Aliweza kutendewa ukatili wowote ambao haukuwezekana kujaribiwa hata kwa wanyama wa porini bila ya lawama katika nchi nyingine za ulimwengini.” ya mambo haya leo hii yapo hata katika jamii yetu japo yanajidhihirisha kwa namna nyingine. Leo ubaguzi kati ya matajiri na masikini, wenye vyeo na wasionavyo ni mkubwa sana. Wema na ubaya; Mwandishi huyu ameonesha nguvu kubwa ya wema juu ya ubaya, anasema palipo na wema ubaya hushindwa na kutupwa kabisa. Mfano; uk.51 anasema kwamba, “Idadi ya watu wema ni kubwa siku zote kuliko jumla ya watu wabaya”. Katika jamii yetu ya leo wema upo lakini bado unamezwa na ubaya kwa kiasi kikubwa kutokana na woga, uroho wa madaraka, ubabe wa baadhi ya watu, nk. Ila Shaaban Robert anaipa jamii suluhu ya ubaya kuwa yatupasa kuwa wema. Dharau; Suala la kudharauliwa kwa waafrika lilioneshwa wazi na wazungu pamoja na wahindi. Hii ni pale ambapo hata kama mwaafrika angekuwa na cheo cha juu kuliko mzungu bado mzungu angeheshimiwa sana kuliko mwaafrika huyo. Shaaban Robert katika utumishi wake alilionja hili na lilimpa mfadhaiko mkubwa sana. Mfano; uk.54 anasema, “Nilikuwa ni radhi kuwekwa chini ya wakubwa wangu lakini niliona dharau wadogo kuwekwa juu yangu”. Uhalisia wa jambo hili ndani ya jamii yetu ya leo lipo katika sehemu mbalimbali za kazi, kwani watu wanaangalia undugu, urafiki na mahusiano mengine ambayo hayana hadhi yoyote katika cheo fulani. Dhamira nyingine zilizojitokeza katika kazi hii zipo katika insha mbalimbali, kwa mfano Insha ya “Naondoka Mpwapwa” kuna dhamira ya umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike, ujasiri na tamaa ya mali. Masuala haya ni masuala ambayo yapo katika jamii yetu ya sasa, hivyo ni vyema jamii ichukue mazuri yote na kuacha mabaya kama vile tamaa ya mali. Pia katika Insha ya “Idara ya Utawala” dhamira ambayo imejitokeza ni suala zima la utawala, ambapo mwandishi anatueleza ni kwa namna gani viongozi wanavyotakiwa kuwajibika katika nafasi zao za kazi. Kwa mfano; uk.61 mwandishi amemuonesha Mudir na masaidizi wake jinsi walivyokuwa wakiwajibika. vilevile katika Insha ya “Nilikuwa Mshairi” kuna dhamira ya umuhimu wa ushairi. S. Robert anaonesha ni kwa namna gani ushairi ulivyo muhimu, kwani huweza kutunza kumbukumbu na uhai wa mwandishi. Mfano; uk.64 “Mauti huua mwili wa mwandishi ukawa vumbi tupu kaburini lakini mchoro alioandika wakati wa maisha yake hudumisha uhai wa jina lake duniani milele”. Kipengele kingine cha Maudhui ni Mgogoro;Ni hali ya kutokuelewana baina ya pande mbili yaani mtu na mtu, mtu na kikundi au mtu mwenyewe na nafsi yake.Migogoro mbalimbali imeweza kujitokeza ambapo tunaweza kuigawa katika vipengele vifuatavyo; Mgogoro wa nafsi,Mgogoro wa kiuchumi,Mgogoro wa kijamii na Mgogoro wa kiuchumi. Katika mgogoro wa nafsi tunamwona Shaaban Robert akionesha hali ya kujiuliza juu ya maisha mazuri yakoje na je afanye nini ili awe na jina zuri duniani. Mfano; uk.2 “Ukosefu wa jina zuri ni ukiwa mkubwa duniani. Jambo hili sikulipenda.” Suluhisho la mgogoro huu; Shaaban Robert aliamua kufanyakazi kwa bidii na kuwa mtu mwema. Mgogoro mwingine wa nafsi unajitokeza kwa S. Robert kwamba ni kwa vipi angepata mke aliye na sifa kama za Amina! (mke wake wa kwanza ambaye ni marehemu). Anasema uk.37 “Nilikuwa na marafiki na wenye huruma kadha wa kadha lakini, kati yao palikuwa hapana mtu niliyeweza kumwita mke. Nafasi yake ilikuwa haina mtu nyumbani”. Suluhisho la mgogoro huu, alimpata mke wa pili aliyekuwa na sifa alizozihitaji. Pia kuna mgogoro wa kijamii ambapo umetokea pale Shaaban Robert alipodharauliwa kuhusu cheo chake. Hii ilijitokeza pale ambapo S. Robert hakutendewa haki kazini kwake, kwani badala ya kuwekwa wa kwanza katika orodha ya mshahara kutokana na cheo chake aliwekwa mwishoni kwa kuwa tu yeye alikuwa ni mwaafrika. Suluhisho la mgogoro huu Shaaban Robert aliamua kuandika barua kwa mkuu lakini barua hiyo haikufanyiwa kazi. Basi S. Robert aliamua kuvumilia. Uk.55 “Katika ulimwengu watu wengine walikuwa wamepatwa na madhila kuliko yaliyonipata mimi wakavumilia. Mimi nilikuwa ni nani nisivumilie?” Mgogoro mwingine wa kijamii ni kati ya S. Robert na ndugu wa mke wake. Chanzo cha mgogoro huu ni uchoyo wa baadhi ya warithi wa mirathi. Suluhisho lake ni pale S. Robert alipowapa uhuru wa kuchagua sehemu waliyotaka na zile zilizoachwa kuwa zake na watoto wake. Uk.48 “Basi nilitoa shauri kuwa isipokuwa mimi na watoto wangu kila mrithi alikuwa na idhini ya kuchagua sehemu yake katika shamba apendalo, na sehemu zisizochaguliwa itakuwa haki ya watoto na mimi. Shauri hili lilisuluhisha mambo kama uchawi”. Pia mgogoro wa kijamii mwingine ni kati ya S. Robert na msimamizi wa safari, chanzo cha mgogoro huu ni ubaguzi au dharau, hii ilijionesha pale ambapo S. Robert alipoambiwa kushuka katika lori la daraja la pili ili kuwapisha wahindi wanne wakati yeye alistahili kuwa katika hilo gari kutokana na yeye alistahili kuwa mfanyakazi wa serikali. Suluhisho la mgogoro huo S. Robert na watoto wake aliwapisha na kushuka. “Msimamizi wa safari, mhindi vilevile, hakuona mtu mwingine wa kushuka ila mimi”. Katika mgogoro wa kiuchumi tunamwona Shaabani Robert akilalamika namna alivyodhurumiwa pesa za manunuzi ya vitabu vyake,uk 78 anasema “Kwa kazi yangu iliyoweza kuleta sh 25000/= kwa vitabu 5000 katika mwaka 1954 sikupewa hata pesa moja ya shaba kwa muda wa miaka kadhaa….sikupata kitu kwa kazi yangu iliyoleta karibu sh 15000/= kwa vitabu 5000 katika mwaka 1958.Suluhisho la mgogoro huu ni kwamba Shaabani Robert alizidi kuwa mvumilivu pasipo kuvunjika moyo katika kazi yake ya uandishi uk 79 anasema…..sijavunjika moyo,tena ningali nayo bado furaha katika uandishi kama alivyo bi-arusi kwa mpenzi wake.Katika maisha baadhi husumbuka na wengine hucheka. Ujumbe; mwandishi S. Robert ametoa ujumbe wa aina tofauti tofauti kwa lengo la kuiasa na kuionya jamii ili iweze kubadilika na kufikia maendeleo yenye kuleta tija kwa mtu binafsi, jamii na taifa kwa ujumla. · Kufanya kazi kwa bidii ni msingi mzuri katika maisha. Mfano S. Robert alifanya kazi kwa bidii na ndio maana alifanikiwa katika maisha yake yote na hivyo kujijengea jina zuri. · Jambo la msingi na bora katika maisha ni kutokata tamaa, hata kama tunashindwa kupata mafanikio makubwa ni bora kupata kidogo kuliko kukosa kabisa. S. Robert anasema kuwa; uk 2. “Jaribu dogo la wema ni bora kuliko kubwa la ubaya”. · Utu wema ni matendo mazuri. Shaaban Robert anatuasa tuwe na matendo mema, matendo mema yaoneshwe nyakati zote. Mfano; mahusiano mema na marafiki, kauli nzuri kwa watu nk. · Haki na uaminifu katika maisha humfanya mtu aheshimike na kukubalika wakati wote. · Shaaban Robert anatuasa kuwa na mapenzi ya dhati katika maisha kwani hutufanya kuishi vyema. · Suala la kumtegemea Mungu katika kila jambo ni muhimu, na kitu kizuri kinatoka kwa Mungu. Mfano; mke mwema au mume mwema. · Suala la malezi ni la watu wote wawili na sio suala la mmoja. Hivyo hakuna budi baba na mama kushiriki kikamilifu katika malezi hasahasa baba. · Hakuna haja ya kujilimbikizia madaraka na majukumu kwani maisha ya duniani ni ya mpito. · Uandishi ni silaha muhimu katika utunzaji wa kumbukumbu za kihistoria. · Nafasi ya elimu itolewe kwa watu wote. · Ni vema kuwa wavumilivu katika kufanikisha jambo Fulani. Falsafa ya mtunzi; Shaaban Robert anaamini kuwa mtu hupendwa na kukubalika kwa watu kutokana na matendo yake mazuri kama vile, kauli njema, ufanyaji kazi kwa bidii, utii na unyenyekevu, msamaha, uvumilivu na kuwa na moyo wa kujitoa. Anasema; “Wema hushinda ubaya na haki ya mtu haipotei”. Mtazamo; Mtazamo wa S. Robert ni wa kimapinduzi anaona kuwa kufanya kazi kwa bidii huleta maendeleo. Msimamo; Shaaban Robert ameonesha msimamo wa aina mbili kwanza msimamo wa kidhanifu ambao umetokana na imani yake aliyoishikilia kwamba Mungu ndiye tegemeo. Na anatudhihirishia kwamba mtu akimtegemea Mungu atafanikiwa. Pili ameonesha msimamo wa kiuyakinifu kwani anaeleze kuwa, mtu anayefanya kazi kwa bidii na mwenye ushirikiano na maadili mema ndiye hujitengenezea jina zuri katika jamii. Na hii inajidhihirisha wazi katika Maisha yake ya kabla na baada ya miaka hamsini na ndiyo maana mpaka leo anakumbukwa. Baada ya kuangalia maudhui katika insha mbalimbali sasa tuangalie umbo la ndani na la nje katika ushairi. Hapa tutachambua mashairi pamoja tenzi. Kwa kuanza na shairi la “Amina” katika umbo la ndani (maudhui) kwa kutumia nadharia ileile ya Uhalisia. Mwandishi S. Robert ameonesha dhamira mbalimbali kama ifuatavyo: Mapenzi ya dhati na ndoa; Shaaban Robert anaeleza mapenzi yake ya dhati kwa Amina (marehemu) anaona kwamba Mungu ndiye anayefunga na kufungua mapenzi. Mfano; katika ubeti wa 2 uk.4 anasema; 2. “Nilitaka unyanyuke, kwa kukuombea dua, Sikupenda ushindike, maradhi kukuchukua, Ila kwa rehema yake, Mungu amekuchagua, Mapenzi tuliyofunga, hapana wa kufungua” Dini na imani kwa Mungu: Shaaban Robert anaamini uwepo wa Mungu ndio maana katika ubeti wa 2 anamwombea mke wake dua kwa Mungu ili ayashinde maradhi. Anaamini kuwa Mungu hashindwi na kitu lakini kwa mapenzi yake ameamua kumchukua. Maadili mema na maonyo: hali hii imejidhihirisha pale Shaaban Robert alipokuwa anawaasa watoto wake katika utenzi wa Hati na Adili, juu ya kuwa na maadili mema. Anataja mambo kama adabu na utii, utu wema, umuhimu wa mwanamke kujitunza, kujali wakati, umuhimu wa elimu, kuepuka fitina, kumcha Mungu, kuwaheshimu wazazi, mapenzi ya dhati katika ndoa, kuepuka uvivu, kutii mamlaka, kutunza ahadi nk. mfano katika ubeti wa 34. Anaelezea uvumilivu katika maisha ya ndoa. 34. “Na mume msishindane, Wala msinuniane, Jitahidi mpatane, Ndiyo maisha ya ndoa” Pia katika ubeti wa 36 anaelezea usafi na kutunza mazingira; 36. “Nyumba yako inadhifu, Kwa kufagia uchafu Kila mdudu dhaifu Asipate pa kukaa” Maana ya kifasihi ya ubeti huu ni kwamba, mwanamke anapaswa kutunza mwili, moyo na akili yake ili visije vikaingiliwa na mawazo machafu/fikra potofu ambazo zitadhoofisha mahusiano/mapatano katika ndoa au familia yake. Umuhimu wa elimu: katika ubeti wa 31, uk 10. Shaaban Robert anaonesha jinsi gani elimu ilivyomuhimu katika maisha. Anasema; . 31. “Elimu kitu kizuri, Kuwa nayo ni fahari, Sababu humshauri, Mtu la kutumia”. Heshima kwa wazazi: ili kuishi maisha mema na yenye baraka, Shaaban Robert anawaasa Hati na Adili wawaheshimu wazazi na wala wasioneshe dharau ili wapate taadhima. Mfano katika ubeti wa 36.uk.26 anasema; 36. “Tatu baba na mama, Wataka taadhima, Na kila lililojema, Ukiweza watendee”. Vivyo hivyo hata katika jamii yetu ya leo tunaona jinsi gani watoto na vijana wengi wanavyo wadharau wazazi wao na hata watu waliowazidi umri. Hivyo basi si budi jamii kubadilika kwani heshima ni kitu muhimu sana katika maisha. Ujane: Shaabani Robert anaonesha athari za kuondokewa na mume au mke na pia umuhimu wa mke na mume. Mfano; ubeti. 13:1 “Dunia mume na mke, kwa watu hata wanyama” Vilevile anaonesha umuhimu wa kuwa pamoja kati ya mume na mke. Mfano; ubeti 3:3 “Adamu pasipo mke, Mungu hakuona vyema”, Katika uhalisi suala la ujane lipo na halikwepeki ni kitu ambacho kinaumiza sana iwapo mmoja anaondokewa na mwezi wake. Umuhimu wa ndoa; katika shairi la Ndoa ni Jambo la Suna Shaabani Robert anasisitiza kwamba katika dini ya kiislamu ndoa ni kitu muhimu sana katika maisha ya duniani, hivyo anawahamasisha vijana waoe kwani ndoa ni jambo la kheri na ni suna kutoka kwa Mtume. Pia anawahamasisha vijana waache zinaa. Ubeti 8:2 “Huko kubibirishana, ni haramu vitabuni”, Ubaya wa unafiki; hii inajitokeza katika shairi la “Ndumakuwili” mwandishi anaonesha ubaya wa mtu mnafiki na jinsi alivyo kwani si rahisi kumtambua kama anavyosema katika ubeti 2. 2. Hujivika pande zote, mkapa akavikika, Litengezwalo lolote, hangui huridhika, La sharia au tete, lisemwalo hutosheka, Ndumakuwili si mwema, hujidhuru nafsia. Hata katika jamii yetu ya leo watu kama hao wapo, hivyo mwandishi anaiasa jamii kuachana na tabia ya ndumakuwili kwani hukwamisha maendeleo. Umuhimu wa shukrani; katika shairi la “Namshukuru” mwandishi anatufundisha kwamba katika maisha tunapaswa kuwa watu wenye shukrani kwa Mungu katika kila jambo. Mfano, ubeti.10 uk 104. “Namshukuru Manani, mwenye uwezo arifu, Hafi maji baharini, mzawa kufa kwa sefu, Mambo yake yanafani, kila akiyasarifu, Alhamdulillahi, namshukuru Latifu”. Nafasi ya mwanamke: Shaaban Robert hakuacha kujadili suala la mwanamke katika jamii. Hili linajidhihirisha kwenye utenzi wa “HATI”, anamuasa binti yake kuwa awe mtii, msafi, mpishi bora, mvumilivu katika ndoa nk. mfano katika ubeti wa 33.uk.10 anasema; 33. “Upishi mwema kujua Na mume kumridhia Neno analokwambia, Kwako itakuwa taa”. Ujumbe; katika mashairi yake mwandishi S.Robert ametoa ujumbe huhimu sana katika kuiasa jamii kama ifuatavyo: · Maisha ya kumtegemea Mungu ni yenye fanaka. · Jamii yapaswa kuzingatia elimu kwani ni mwanga wa maisha. · Ili vijana wafanikiwe katika maisha wanapaswa kuwa na utii na adabu. · Tuwe makini katika katika maneno tutamkayo yasiwe na athari mbaya kwa jamii, kama matusi, kunena uongo nk. · Kupekuwa uvivu na kufanya kazi kwa bidii ni silaha ya maendeleo. Baada ya kuangalia umbo la ndani katika ushairi sasa tuangalie umbo la nje katika ushairi. Kwa kutumia nadharia ya Umuundo-mpya. Nadhari ya Umuundo-mpya ni zao la nadharia ya Umuundo. Nadharia hii inatumia neno Umuundo-mpya kuonyesha mtizamo wa kimuundo katika fasihi ambao ulitokea baada ya ukinzani wa nadharia ya Umuundo. Japo dhana hii haiwezi kupewa maana moja maalum, imehusishwa na maendeleo kutoka au katika kazi za Derrida (1973, 1976), Lacan (1977), Kristeva (1981, 1984, 1986), Althusser (1971) na Foucault (1978, 1979a na b, 1981, 1986). Kazi hizi nazo zilichangiwa na kazi za Ferdinand de Saussure na Emile Benveniste (kuhusu isimu-jamii ya umuundo). Nadharia hii ya Umuundo-mpya hujikita zaidi katika kusisitiza kuwa maana inaweza kubadilika kulingana na miktadha husika. Kwa mfano. Maana ya neno tajiri hutofautiana katika lugha mbalimbali na hata kati ya miundo tofauti ya lugha moja, na hutegemea matumizi na muktadha wa matumizi hayo. Ndipo sasa hapana maana moja ya neno au fungu la maneno. Kulingana na nadharia hii basi, neno 'mama' kwa mfano, huwa halina maana ya kindani inayotokana na lugha husika bali huwa na maana za kijamii zilizotokana na lugha hiyo na ambazo zinakinzana na kubadilika kulingana na mazingira na kipindi cha kihistoria. Kwa kuanza na kipengele cha mtindo: Mtindo; kwa mujibu wa Senkoro (2011), “Mtindo katika kazi ya fasihi ni ile namna ambavyo msanii hutunga kazi yake na huipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni au kawaida za zilizofuatwa kama ni zilizopo (za kimapokeo) au ni za kipekee”. Kwa ujumla mtindo uliotumiwa na mwandishi ni wa kipekee kabisa kwani ameweza kuchanganya insha,mashairi pamoja na tenzi ambazo kwa ujumla huelezea maisha yake S.Robert hususani katika insha, na katika mashairi na tenzi kuna majonzi, mawaidha, maonyo na maadili. Katika kipengele cha mashairi mtindo uliotumika ni wa kimapokeo kwa sababu amezingatia urari wa vina na mizani, urari wa mishororo, kibwagizo na utoshelevu katika kila beti. Mfano ubeti wa 2 katika shairi la “Amina” anasema; 2. “Nilitaka unyanyuke, kwa kukuombea dua, Sikupenda ushindike, maradhi kukuchukua, Ila kwa rehema yake, Mungu amekuchagua, Mapenzi tuliyofunga, hapana wa kufungua” Muundo; kwa mujibu Senkoro (kashatajwa), “muundo hutokana na umbo na mpango wa kazi ya fasihi; kwa hiyo hapa ndipo tutapata katika ushairi wa Kiswahili, mashairi yenye miundo mbalimbali iainishwayo na idadi ya mistari (vipande/mishororo) katika kila ubeti, mathalani mashairi ya uwili, utatu, unne” nk. Muundo uliotumika katika mashairi yote na tenzi zote ni muundo wa tarbia yaani mistari minne katika kila beti. Mfano, shairi la Amina ubeti.1 uk.4 Anima umejitenga, kufa umetangulia, Kama ua umefunga, baada ya kuchanua, Nakuombea mwanga peponi kukubaliwa, Mapenzi tuliyofunga hapana wa kufungua. Vilevile hata katika “UTENZI HATI” na “UTENZI WA ADILI” mwandishi ametumia muundo wa tarbia (mistari minne). Mfano; utenzi wa ADILI uk. Kijana lete kalamu, Nina habari muhimu, Napenda uifahamu, Dadayo kasha zamuye, Matumizi ya lugha; mwandishi ametumia lugha fasaha na inayoeleweka na wote hasa katika upande wa insha, lakini katika upande wa ushairi kwa kiasi fulani ametumia msamiati wa lugha ya kiarabu. Mfano katika shairi la “Namshukuru” kuna maneno kama vile, Illahi, Alhamdulillahi, Latifu, rakadha, ashrafu, nk. Vilevile ametumia tamathali za semi kama vile: Tashbiha: shairi la “Amina” ubeti wa 1:2 uk.4 “Kama ua umefunga baada ya kuchanua”. Neno “kama” ni tashbiha inayotumika kulinganisha vitu viwili. Vilevile hata katika “UTENZI WA HATI” uk.7 ubeti wa 7:4 tunaona tashbiha zikijitokeza. Anasema, “Nakupenda kama Hidaya” na ubeti wa 6:3 anasema, “Tunza kama sahibu” pia uk.7 ubeti wa 5:3 “Itunze kama fedha” Takriri: urudiaji wa neno, sentensi au kifungu cha maneo ili kusisitiza jambo. ubeti wa 1:3 na 4 “Nakuombea mwanga, peponi kukubaliwa” pia ubeti wa 4:3 “Nawe wangu penzi, peponi utaingia”. Neno “peponi” limerudiwa ili kuonesha msisitizo kwamba baada ya maisha haya kuna maisha mengine peponi (mbinguni). Pia uk.6 ubeti wa 5:2 “Nijaze kadha wa kadha”, vilevile katika “UTENZI WA HATI” neno “hati” limejitokeza mara nyingi mfano, ubeti wa 1, 2, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 17, 18, 19… pia neno binti katika ubeti wa 1, 92, 93, 94, 95. Ritifaa: Ngure (2003:128) ni kitu kisicho na uhai kama vile maiti huwa kinasemeshwa kana kwamba nafsi yake ingali hai. Mfano; katika shairi la Amina S.Robert anaongea na marehemu Amina kana kwamba yu hai. Hii imejidhihirisha katika shairi zima. Mfano; ubeti wa 4 na 5 Tashihisi: kukipa kitu kisicho hai uwezo wa kutenda. Mfano; ubeti wa 6:2;3 uk.5 anasema, “Vumbi tena likiunga, roho likirudishiwa, Mauti yakijitenga, mapenzi yatarejea”, Pia katika UTENZI WA HATI uk.7 ubeti wa 6:1 anasema, “Dunia ina aibu”. Hapa dunia inapewa sifa ya ubinadamu ya kuona aibu. Vilevile uk.8 ubeti wa 17:3 anasema, “Sauti yendavyo mbio”. Hapa napo sauti inapewa uwezo wa kukimbia kama kitu chenye uhai. Pia uk.27 ubeti wa 43:2 “Viungo vyake husema”. Viungo mbalimbali vya mwili vinapewa uwezo wa kusema kama binadamu. Sitiari: kitu kupewa jina la kitu kingine. Hii ni katika “UTENZI WA HATI” uk.13 ubeti wa 50:3 anasema, “Mtu mwongo ni msongo”. Mtu mwongo anafananishwa na mtu asiyechezwa unyago/asiyefundwa. Pia hata katika uk.17 ubeti wa 81:1 chungo inafananishwa na kitu kilichooza. Anasema, “Chongo mbaya ni uvundo”, vilevile uk.26 ubeti wa 37:3 baba anafananishwa na mbegu. “Baba yako ni mbegu”, uk.15 ubeti wa 64:1 mama anafananishwa na kitu cheupe, kitu safi. Anasema “Mke ni nguo nyeupe”, Jazanda (matumizi ya picha na ishara). Ubeti wa 1. Katika shairi la Amina Mwandishi anasema; “Amina umejitenga, kufa umetangulia, Kama ua umefunga, baada ya kuchanua”, Hapa anafanisha kifo cha Amina na jinsi ua linavyonyauka. Pia hata katika shairi la ndoa, mwandishi ametumia neno kunguru akimaanisha wale watu wasio tulia katika ndoa zao. Taashira: maana inayotajwa si ile inayomaanishwa. Mfano uk.7 ubeti wa 6:1 katika “UTENZI WA HATI” anasema “Dunia ina aibu” pia uk.16 ubeti wa 73:1 na 74:1 anasema “Tumbo la rutuba”, “Tumbo hili la dhahabu”. Mwandishi anaposema “tumbo la rutuba” ni dhahiri kuwa anamaanisha tumbo la uzazi la mwanamke. Pia anaposema “tumbo hili la dhahabu” anamaanisha tumbo lenye thamani na la pekee wengine hawana. Misemo: ni kauli fupifupi zenye ujumbe mzito. Kwa mfano: uk.9 ubeti wa 20:1 “Dunia ni Mvurugo” yaani inamaanisha kuwa duniani kuna mabaya na mazuri, hivyo tunapawa kuwa waangalifu. Pia uk.6 ubeti wa 5:1, “Ulimwengu una adha” pia uk.13 ubeti wa 54:1 “Ulimi wa pilipili” Methali: uk.9 ubeti wa 22:2 “Cheche huzaa moto” yaani kitu kidogo chaweza kuleta madhara makubwa. Pia uk10 ubeti wa 28:1 “Dunia mali ya roho” pia katika shairi la “UJANE” uk. 82 ubeti wa 4:1 “Ujane neno la feli, kugombana watu wema”, Taswira: katika “UTENZI WA HATI” uk.26 kuna taswira ya “hereni”. Hapa mwandishi anamfananisha hati na pambo la sikioni, anaona kuwa binti yake akizingatia hayo atafanikiwa maishani. Pia kuna taswira ya “pilipili” (kitu kichungu) ubeti wa 54. “UTENZI WA HATI” anamuasa mwanae asiwe na ulimi kama wa pilipili bali awe na kauli ya upole na faraja siku zote. Jina la kitabu; “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”. Jina hili linasadifu kabisa yaliyomo katika kitabu, kwani, kazi yake yote mwandishi ameigawa katika sehemu kuu mbili sehemu ya kwanza ni Maisha yangu na sehemu ya pili ni Baada ya Miaka Hamsini. Vilevile katika kuelezea maisha yake ameelezea kwa mtindo wa insha, mashairi na utenzi. Na katika kila kichwa cha insha, shairi na utenzi vimesadifu kabisa yaliyomo ndani yake. Kufaulu kwa mwandishi; Mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, kwani mambo aliyoyandika yana halisika katika maisha yetu ya kila siku. Kutokufaulu kwa mwandishi; Mwandishi ameelezea mambo mengi kwa kufuata imani ya dini ya kiislamu na kusahau kwamba anaowaandikia ni mchanganyiko wa imani tofauti tofauti. Pia amejikita zaidi katika mambo dhahania kama vile Mungu. Vilevile hata lugha aliyoitumia kwa kiasi fulani ina msamiati wa kiarabu hasa katika ushairi, hivyo inawawia vigumu kuelewa wale wasiojua lugha ya kiarabu. Hitimisho; Sisi kama wachambuzi wa kazi hii tunamwona S. Robert kama kivuli kinachoishi, kwani mambo mengi aliyoyaeleza bado yapo katika jamii ya leo na kazi yake bado inamashiko na itaendelea kuwa na mashiko hata kwa vizazi vijavyo.


 


Powered by Blogger.