Fasihi ya watoto na fasihi simulizi
Wamitila (2003: 44), anaeleza kuwa fasihi simulizi ni dhana inayotumika kurejelea kazi ambazo kimsingi hupokezanwa kwa njia ya masimulizi au kwa mdomo. Anaendelea kueleza kuwa fasihi hii hutumiwa katika jamii kwa njia ya kupashana maarifa inayohusu utamaduni fulani, historia ya jamii, matamanio yao, mtazamo wao na historia yao.
Aidha, Njogu (2006: 2) anaeleza kuwa, fasihi simulizi ina ubunifu na uhai wa kipekee wenye kutoa fursa njema ya kuibua nadharia za kijamii, kiuchumi na kisiasa, pia aina hii ya fasihi ni uti wa mgongo wa maendeleo ya binadamu. Kwani ndani yake kuna masimulizi, maigizo, tathmini za mazingira na mahusiano ya kijamii. Kwa ujumla fasihi simulizi ni sanaa inayotumia lugha ya mazungumzo ya ana kwa ana kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira husika.
Lyimo (2014), anaeleza kuwa fasihi ya watoto ni fasihi iliyotungwa ama na watu wazima au watoto wenyewe yenye kutumia lugha na hukusudiwa kusomwa au kutendwa na watoto. Ingawa kwa ujumla fasihi hii ya watoto haitofautiani sana na ile ya watu wazima kwa dhana ya kutumia sanaa ya lugha. Fasihi ya watoto ni mpya kwa kiasi fulani katika masikio ya wanafasihi hasa wakongwe, fasihi hii si mpya kwa maana ya watoto kutohusishwa katika fasihi kwa ujumla bali ni kutokana na kutotazamwa kwa kundi hili kwa upekee wake katika utunzi na uchambuzi wa kazi za fasihi.
Bakize (2013: 61- 70), wanaendelea kueleza kuwa fasihi ya watoto inafahamika katika jamii nyingi za Tanzania, Kenya, na maeneo mengi ya Afrika kwa kiasi kikubwa ni ile iliyo katika baadhi ya vitabu vya hadithi (ngano) na nyimbo za kitoto za makabila mbalimbali. Katika maeneo mengi kazi za watoto kama ushairi, riwaya na tamthiliya bado hazijafahamika vyema.
Fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zote zimepiga hatua kubwa kimaendeleo. Hii ni kutokana na kuwa fasihi simulizi kwa sasa na fasihi andishi ya watoto zinaonekana kupiga hatua katika vipengele mbalimbali. Kutokana na ukweli huu ni wazi kuwa fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zimepiga hatua kimaendeleo kwa hoja zifuatazo;
Kuongezeka kwa uandishi wa kazi za fasihi ya watoto, kwa mujibu wa Mulokozi katika Semzaba (2008: 4), anasema kuwa kufikia mwaka 2008 mradi wa vitabu vya watoto ulikuwa umechapisha zaidi ya vitabu mbalimbali 250 na kuvipeleka mashuleni. CODE (2015), wanasema kuwa kufikia mwaka 2015 mradi wa vitabu vya watoto ulikuwa umechapisha na kupeleka mashuleni vitabu vya Kiswahili na Kiingereza zaidi ya 350. Baadhi ya vitabu hivyo ni pamoja na Vipaji vya Helena, Zindera, Sababu Mimi ni Mwanamke, Sara na Kaka Zake na vingine vingi vilivyo chini ya mradi wa vitabu vya watoto. Ingawa uandishi wa vitabu wa fasihi ya watoto umekuwa lakini hatuna budi kukiri kuwa uandishi huo sio linganifu kwani machapisho mengi yanaonekana kuendelea katika riwaya fupi na hadithi andishi. Aidha, fasihi simulizi inaonekana kupiga hatua kimaendeleo ambapo baadhi ya kazi za fasihi simulizi zimewekwa kwenye maadishi na kusimuliwa kwa hadhira lengwa ambayo ni watoto. Mfano, katika kitabu cha Sababu Mimi ni Mwanamke mhusika mimi anasimulia visa mbalimbali tangu mwanzo wa kitabu hadi mwisho wa kitabu, kutokana na ukweli huu basi tunaweza kusema kuwa fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zote zimepiga hatua kubwa.
Kuongezeka kwa uchapishaji wa kazi ya fasihi ya watoto, kwa mujibu wa Ngugi (2009), anaeleza kuwa kutokana na kutambua kuwa watoto pia ni sehemu ya jamii pana inayohitaji kuhudumiwa kifasihi, kila shirika la uchapishaji ilitenga idara maalumu ya kushughulikia fasihi ya watoto na vijana. Mfano, katika shirika la Oxford University Press tunapata mradi wa kusoma, Phoenix ina Hadithi za Kwetu, Longhorn ina Hadithi Kolea na Sasa Sema, East African Publishing House ina msururu wa vitabu kwa viwango mbalimbali, Paukwa (umri wa miaka 0-7), Vitabu vya Nyota (umri wa miaka 7-9), na Vitabu vya Sayari (umri wa miaka 10-13). Aidha, katika fasihi simulizi kuna visasili, visakale na hadithi mbalimbali kama vile, hadithi za Abunwasi, kisakale cha Rwanda Magele, Alfu lela Ulela. Kutokana na mifano hii, ni wazi kuwa fasihi andishi ya watoto na fsihi simulizi zimepiga hatua hasa kwa kuongezeka kwa mashirika ya uchapishaji wa kazi za fasihi ya watoto.
Hali ya usomaji wa fasihi ya watoto, kwa mujibu wa CODE (keshatajwa), wanasema kuwa usomaji wa vitabu hasa nchini Tanzania bado upo chini. Kwa kiasi kikubwa watoto wanaosoma kazi hizi za fasihi ni wale walio katika shule zilizo ndani ya mradi wa vitabu vya watoto Tanzania, shule hizo ni zile zilizo katika wilaya kumi za mradi kama vile Kongwa mkoani Dodoma, Morogoro, Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro, Kibaha, Kisarawe, Bagamoyo, Rufiji mkoani Pwani na Dar es Salaam.
Watoto wengine walio nje ya mradi pengine husoma tu vitabu vichache vya hadithi wanavyo bahatika kupata katika maktaba au sokoni. Tunaona nchini kenya hali hii ya usomaji imeongezeka kwa mujibu wa Ngugi (2009), walimu walionekana kuwa na mielekeo chanya kwa vitabu vya ziada kwani walitumia mikakati mbalimbali kwa njia ya kuwahimiza watoto kusoma. Baadhi ya mikakati hiyo ni kuwapa watoto mazoezi kusoma, kuwa na majadiliano darasani kuhusu hadithi iliyosomwa na kuwa na usomaji wa pamoja darasani. Vilevile, hali ya usimuliaji wa kifasihi simulizi umeongezeka, mfano, kuna vipindi mbalimbali vinavyoonyeshwa kwenye runinga kuhusu watoto kama vile kipindi cha Watoto Bomba kinachoonehwa ITV na vipindi vingine vinavyohusu watoto, masimulizi yanayosimuliwa na mababu zetu kuhusu visa mbalimbali na hadithi hizi mara nyingi husimuliwa wakati wa jioni ambapo hadhira inakuwa imetulia. Kwahiyo, kutokana na kuongezeka kwa usomaji wa kazi za fasihi andishi ya watoto kama tulivyoona nchini Kenya ni wazi kuwa fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zimepiga hatua kimaendeleo.
Ufundishaji wa fasihi andishi ya watoto, Wamitila (2008:338) anasema kuwa kozi ya fasihi ya watoto ilianza kufundishwa rasmi katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika Idara ya Fasihi, Mawasiliano na Uchapishaji mwaka 2012 katika semista ya kwanza. Hii ndio inatufanya tuitazame fasihi ya watoto kwa upekee wake, mfano kwa upande wa Tanzania mpaka sasa fasihi ya watoto kama taaluma inafundishwa katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Mtakatifu Agustino (tawi la Mtwara), Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Elimu cha Moshi. Aidha nchini Kenya vipo vyuo vikuu ambavyo vinafunza fasihi ya watoto kwa kiwango cha shahada ya kwanza na uzamili vyuo hivyo ni pamoja na Chuo cha Kenyatta, Bewa la Marst la Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Chuo cha Mount Kenya. Aidha, katika upande wa fasihi simulizi hali ya ufundishaji wa fasihi simulizi imepiga hatua kubwa kwani fasihi simulizi hufundishwa shuleni ngazi ya sekondari na vyuoni. Kutokana na mifano hiyo ni dhairi kuwa fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zimepiga hatua kimaendeleo hususani katika ufundishaji.
Uenezaji wa fasihi ya watoto katika magazeti na mitandao ya kijamii, kutokana na utafiti uliofanywa na Ngugi (keshatajwa), kuhusu hali ya fasihi ya watoto hususani nchini kenya ulilenga kubainisha tabia ya usomaji wa magazeti miongoni mwa wanafunzi wa shule ya msingi, matokeo ya utafiti huu yalithibitisha kuwa watoto wanapenda kusoma aina mbalimbali ya magazeti, miongoni mwa magazeti ni pamoja na Daily Nation, Sunday Nation, Taifa Jumapili, Taifa Leo, Sunday Standard, Maneno na Sara. Gazeti la Daily Nation lilionekana kupendwa na watoto wengi wanaopata magazeti kwa sababu gazeti hili huwahudumia watoto na vijana kwa kuwa linalenga maudhui mbalimbali yanayo wavutia watoto na vijana wa viwango tofautitofauti. Aidha kwa upande wa mitandao ya kijamii Njue (2015), anasema kuwa zipo tovuti mbalimbali kwenye mitandao ambazo huwa na hadithi mbalimbali za watoto kwa lugha ya Kiswahili kama vile watoto wangu. blog sport.com, International Children`s Digital Library na Swahili Language. Pia, fasihi simulizi imeenea sana katika mitandao ya kijamii na kwenye magazeti. Kwa hiyo tunaona kuwa watoto wanaweza kujisomea hadithi na hata kusikiliza vitabu vinaposomwa katika mitandao, hii ni hatua kubwa kimaendeleo.
Kuongezeka kwa tafiti kuhusu fasihi andishi ya watoto, kwa mujibu wa Mulokozi (2012: 51-66), anasema kuwa mpaka sasa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuna tasnifu mbili za umahili zote za mwaka 2016 na tasnifu moja ya uzamivu ya mwaka 2014, hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni kuna tafiti zimefanywa katika fasihi ya watoto na nyingine zinaendelea kufanywa katika vyuo mbalimbali vinavyofundisha fasihi ya watoto, mfano wa tafiti hizo ni zile zilizofanywa na Njue (2015), Ngugi (2009) na Omuya (2017), tafiti hizi zinashughulikia mada mbalimbali kuhusiana na fasihi ya watoto. Lakini pia, kuna tafiti nyingi zilizofanywa kuhusu fasihi simulizi kama vile, Ruth Finegan, Rose Mwangi na Taban lo Liyong hawa walifanya tafiti mbalimbali kuhusu fasihi simulizi. Hii ni ishara kuwa fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zimepiga hatua za kimaendeleo.
Kwa Ujumla, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia fasihi ya watoto na fasihi simulizi zinakwenda sambamba kimaendeleo. Hii ni kutokana na athari chanya za sayansi na teknolojia katika fasihi simulizi na fasihi andishi y watoto.
MAREJELEO
Bakize, L. H (2013) Changamoto Zinazoikabili Fasihi ya Watoto Tanzania katika Kiswahili,
Juzuu. 76 Dar es Salaam: Taasisi ya Taaluma za Kiswahili. Kur. 61-70.
CODE. (2015) Reading Code: Assessing a Comprehensive Readership Initiative in Tanzania.
Kutoka www. academia. edu/… /Reading Code.
Lymo, E. B (2014) Usaguzi wa Kijinsia katika Vitabu vya Kiswahili vya Fasihi ya Watoto na
Mtazamo wa Wadau nchini Tanzania: Tasnifu ya Uzamivu ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (Haijachapishwa).
Omuya, R. A (2017) Tathmini ya Usimilishwaji wa Biblia kama Fasihi ya Watoto Tanzania:
Tasnifu ya Umahiri ya Chuo Kikuu cha Kenyattta. (Haijachapishwa).
Mulokozi, M. M (2012) Makuadi wa Soko Huria (Chachange S. Chachange) katika Muktadha wa
Riwaya ya Kihistoria katika Fasihi ya Kiswahili: TATAKI: Kur. 51- 66.
Ngugi, P. M. (2009) Language and Literacy Education: The state of Children`s Literature in
Kiswahili in Primary School in Kenya. Tasnifu ya Uzamivu Chuo Kikuu cha Vienna
(Haijachapishwa).
Njue, G. J. (2015) Tathmini ya Hadithi za Watoto katika Mtandao. Tsnifu ya Umahiri ya Chuo
Kikuu cha Kenyatta (Haijachapishwa).
Semzaba, E. (2008) Marimba ya Majaliwa: Dar es Salaam: E& D Vision Publishing Ltd.
Wamitila, K. W. (2003) Kazi ya Fasihi (1): Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi. Nairobi
Vide~Muwa Publishers Ltd.