TAHAKIKI-KIMBUNGA
JINA LA DIWANI:
KIMBUNGA
MWANDISHI: HAJI
GORA HAJI
WACHAPISHAJI:
TUKI
MWAKA: 1995
UTANGULIZI
Kimbunga ni diwani
inayozungumza juu ya mawaidha mbali mbali katika maisha pamoja na suala zima la
ujenzi wa jamii mpya.Katika diwani hii,mwandishi ametoa maadili na maonyo mbali
mbali pamoja na mbinu mbalimbali za kufuata ili kufanikiwa katika suala zima la
ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
MAUDHUI;
DHAMIRA KUU-Ujenzi wa jamii mpya
Mwandishi
amejadili dhamira ya ujenzi wa jamii mpya katika kazi yake.Mwandishi ameonesha
vikwazo mbali mbali vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini, Vikwazo
hivyo ni kama vile uongozi mbaya,rushwa,tamaa, ukosefu wa elimu, ukoloni
mamboleo, n.k.
Katika
kujadili dhamira hii mwandishi ameonesha mbinu/njia mbalimbali ambazo jamii inapaswa
kuzitumia katika suala zima la ujenzi wa jamii mpya hapa nchini,hizo
ndizo dhamira ndogo ndogo;
1.
Uongozi Mbaya
Mwandishi
ameonesha kuwa Uongozi bora unahitajika kwa jamii yoyote ile ili kuleta ufanisi
mzuri katika utendaji na utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwani Uongozi mbaya
unasababisha kushindwa kufikia malengo.Kutokana na uongozi mbaya ndiyo maana
jamii hufikia kufanya mpinduzi ili kuuondoa uongozi uliopo na kusimika uongozi
mpya ili kuijenga jamii kwa upya.
Katika
shairi la “Kimbunga” (uk 1) mwandishi
anaongelea juu ya mapinduzi yanayofanywa na tabaka la chini dhidi ya tabaka
tawala.mwandishi anasema;
‘’kimbunga mji wa siyu,kilichowahi kufika,
Si kwa yule wal huyu,ilikuwa patashika,
Kimeing’owa mibuyu,minazi kunusurika,
Nyoyo zilifadhaika’’.
Mwandishi
ametumia mji wa Siyu kama kielelezo
kizuri kwa jamii yeyote inayotaka kufanya mapinduzi ili kuondoa viongozi
wabaya/wabovu na kuleta viongozi bora.Katika mapinduzi hayo mwandishi
amefafanua kuwa wananchi wengi ndio wanaoathirika na wachache hunusurika.
Shairi
la “Madanganyo”
mwandishi anazungumzia jinsi uongozi mbaya unavyowadanganya wananchi na jinsi
unavyowaathiri na kuwakera wananchi.Wananchi hushiriki katika shughuli za
uzalishaji mali (miradi mblimbali) lakini matunda ya jasho lao huliwa na
wachache.Wachache hao husahau wale waliosulubika katika uzalishajina na mtokeo
yake wananchi wanaishia kuishi maisha ya taabu.Katika Ubeti wa
6,msanii/mwandishi anasema;
“Mlitupigia mbiu, tulimeni ushirika,
Tukakatana miguu, kwa mapanga na mashoka,
Manufaa kwa wakuu, wadogo yetu mashaka,
Wezeni
kutukumbuka, mjue nasi wenzenu.”
Shairi
la “Wenye
Vyao Watubana” mwandishi amejadili namna matajiri jinsi
wanavyowagandamiza,kuwanyonya na kuwabana wale wasio na chochote yaani
maskini.Mwandishi anawaomba viongozi wawatetee ili kuepukana na hali hii.Hii ni
kutokana na uongozi mbaya ndiyo maana hali kama hii ipo nchini lakini viongozi
hawachukui tahadhari yeyote ile.Katika ubeti wa 7,mwandishi anasema;
“Maji yamezidi unga,kwa lodi wa darajani,
Kujitolea mhanga,kwa bei hawezekani,
Mvao wake wa kanga,ni shilingi elifeni,
Wakubwa tuteteeni, wenye vyao watubana.”
Shairi
la “Kibwangai” linajadili dhana ya usaliti wa viongozi wetu
kwa wananchi wanaowaongoza. Mwandishi ameonesha jinsi wananchi wanavyowachagua
viongozi wao lakini viongozi hao wakishapata madaraka au wakishashika nyazfa
wanageuka na kuwasaliti wananchi
waliowachagua.Katika ubeti wa 7,msanii
anasema;
“Kibwangai
lipoona, ni mtu kakamilika,
Akaanza kujivuna,na dharau kuzidiya,
Wala hakujali tena,wenzake walowambiya,
Akahisi hawi nyani,umbo lile litadumu.”
Katika
Shairi hili manii ametumia taswira ya Kibwangai kuwakilisha viongozi
wasaliti na nyani kuwakilisha wananchi wanaoongozwa na akina Kibwangai yaani watawaliwa.
Katika
shairi la “Hili Mnatutakiya”,mwandishi
anaonesha jinsi vyombo vya dola kama vile polisi ,jeshi n.k namna
vinavyoshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda raia na
kuwashughulikia wahalifu.Katika ubeti wa
1,msanii anasema;
Twasema kinaganaga,tumechoka vumiliya,
Wenzetu mkatubwaga,hasa ukiangaliya,
Hao wezi mwafuga,wazidi kutuibiya,
Hakuna watendewalo,ndipo wakapamba moto.
Msanii
ameonesha kuwa vyombo hivyo ndivyo
vinavyowalinda wezi,majambazi na matapeli.
Kwa
ujumla msanii wa diwani hii anaona kuwa ili tujenge jamii mpya
lazima tuwe na uongozi bora unaowajali wananchi wake.
2.
Kupiga vita rushwa
Rushwa
ni kikwazo kimojawapo kinachokwamisha kujenga jamii kwa upya.Kutokana na rushwa
kuota mizizi katika jamii haki hupotea
bali wachache wanafaidi matunda ya nchi
na wengine wanaendelea kuumia.Katika Shairi la “Rushwa” mwandishi anasema;
“Rushwa kajenga kambi,na kuondoka hataki,
Afanya kila vitimbi,mkaidi hashindiki,
Tumzushiyeni wimbi, isiwe kutuhiliki,
Tumchimbie handaki,rushwa tukamzikeni.”
Katika
ubeti huu,mwandishi anatuonesha kuwa lazima jamii yetu ipinge rushwa ili haki
na usawa vitawale kwani kupiga vita rushwa ni njia pekee itakayosaidia kujenga jamii mpya ambayo mwandishi
ameipendekeza.
3.
Umuhimu wa Elimu
Ili tuijenge
jamii mpya ni lazima watu wapate elimu na waelimike bila kujali umri wala jinsia.Mwandishi
anawahimiza wazee kujiunga na kisomo chenye manufaa ili wafute ujinga wa
kutojua kusoma na kuandika.Katika shairi la “Kisomo cha Maarifa” ubeti wa
2,Msanii anasema;
Kisomo cha manufaa,tusomeni kwa haraka,
Isiwe tunakataa,kwa kuwa tumekongeka,
Roho si inochakaa,mwili ndio hupayuka,
Tusomeni kwa haraka,kisomo cha maarifa.
katika
shairi hili mwandishi anawahimiza wazee wajiunge na kisomo cha elimu ya watu
wazima kwa sababu wakishaelimika watakuwa na uwezo wa kupanga mipango yao ya
maendeleo.
Mwandishi
anaonesha kuwa elimu ni silaha madhubuti katika kufanikisha zoezi zima la
ujenzi wa jamii mpya kwani bila
kuwa na wasomi katika jamii kama hii
yetu zoezi la ujenzi wa jamii mpya halitaweza kufanikiwa.
4.
Ukoloni mamboleo
Ukoloni
mamboleo ni kitendo cha nchi kuwa na uhuru wa bendera lakini kimaamuzi
inatawaliwa na nchi nyingine.Ukoloni mamboleo ni kikwazo kikubwa
kinachokwamisha maendeleo ya uchumi hapa nchini.Na ili tuweze kufanikisha
ujenzi wa jamii mpya hapa nchini hatuna budi kupiga vita ukoloni
mamboleo.Katika shairi la “Chuwi” Mwandishi anaonesha jinsi
ukoloni mamboleo unavyoathiri maendeleo ya uchumi hapa nchini.Ukoloni mamboleo
unawaathiri watu wa tabaka la chini wasio nachochote na kuwanufaisha matajiri
au tabaka la juu. Katika ubeti wa 6 mwandishi anasema:-
“Ambao ni matajiri, kwao anapowafikiya,
Huweza kujisitiri, salama kujipatiya,
Walokuwa mafakiri, huzidi kuwaoneya
Huyu ndiye Chuwi gani?
Mwandishi
ameeleza kuwa ukoloni mamboleo huingia kwa njia mbali mbali katika nchi
zinazoendelea.Hivyo mwandishi anatahadharisha kuwa tuepukane na mbinu (njia)
hizo na tuupinge ukoloni mambo leo kwa nguvu zote ndipo tutaweza kujenga jamii
mpya.
5.
Umuhimu wa kujitawala
Ili
tuweze kujenga jamii mpya ni lazima tujitawale katika Nyanja zote za
kifikra,kisiasa,kiutamaduni pamoja na kiuchumi. Katika shairi la “Afrika “Mwandishi anaeleza kuwa ili
tuweze kujitawala ni lazima tuepukane na
unafiki,vibaraka (wasaliti),tusikate tama na tudumishe amani. Katika ubeti wa 3
msanii ansema:-
“Wasaliti wazikishe, wasiwe wenye kuzuzuka,
Tamaa uwakatishe, yasiwe wanayotaka,
Katu wasiwawezeshe, wabakiye kuzuzuka,
Washindike mahusuda,wasopenda bara letu.”
Katika
shairi la “Kujitawala”
Mwandishi anaeleza umuhimu wa kujitawala kwa jamii yoyote ile.Mwandishi
anaonesha kuwa, kujitawala ni pale umma unapokuwa na mamlaka ya kuamua mambo
yao wenyewe bila kuingiliwa au kuwekewa vikwazo vyovyote.Katika Ubeti wa 1 Msanii anasema:-
“Kujitawala
si kwema,kuliko kutawaliwa,
Kujitawala ni umma,kila yao kuamua,
Kujitawala si kama,ulanguzi na rushwa
Katika
shairi hili la ‘kujitawala’ mwandishi anaonesha faida mbalimbali za kujitawala
kama vile kuwepo kwa demokrasia, kuwepo umoja naushirikiano,kuwepo haki na
usawa,amani hudumishwa,vile vile mila na desturiza nchi zinadumishwa.Hivyo
mwandishi anatuasa kuwa ili tujenge jamii mpya ni lazima tujitawale
kisiasa,kiuchumi,kiutamaduni na kifikra.
6.
Umuhimu wa kazi na kuwajibika
Kazi
ni nguzo muhimu sana ya ujenzi wa jamii mpya.Mwandishi amesisitiza umuhimu wa
kazi na kuwajibika.katika shairi la “Kazi” Mwandishi anatuonesha kuwa
kazi ndio msingi wa maendeleo. Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na
tuepukane na njaa. Ubeti wa 1,mwandishi
anasema;-
“Pesa huletwa na
kazi, ni njia zipitiayo,
Hutopata
matumizi,iwapo kazi hunayo,
Hata njaa
hukuhizi,uvivu na angamiyo’’
Katika
shairi la “Uokolewe”,mwandishi
anasisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano ili kuinua uchumi wetu.
Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa
bidii na kutumia vyema rasilimali
zetu ili kuinua uchumi wetu.
Katika
shairi la “Dumizi” mwandishi
anakemea tabia ya baadhi ya watu kukaa
bila kazi (uvivu) na kuanza maisha ya
kunyonya.Hivyo mwandishi anapiga vita unyonyaji unaofanywa na baadhi ya watu.
Hivyo msanii
aniasa jamii kujihusisha na ukulima, uvuvi, utalii na viwanda ili kujenga jamii
kwa upya.
7.
Mapenzi na ndoa
Katika
diwani hii,mwandishi ameonesha kuwa mapenzi yamegawanyika katika pande kuu
mbili ambazo ni;Kuna mapenzi ya kweli na mapenzi ya udanganyifu.
Katika
shairi la “Usimpige Mkeo “ mwandishi anasema kuwa haifai mwanaume kumpiga
mke wake na vile vile mwanaume hatakiwi
kumwekea mkewe masharti magumu.
Shairi
la “Hongera”
mwandishi anawaonya wanandoa (bibi na bwana) wasiwe na tabia ya kufukuzana
wawapo nyumbani. Amewapa kila mmoja maadili yake kwa mwenzake. Beti za (4-5) mwandishi anasema:-
4-
“Bi
arusi yangu shika, uyatie akilini.
Muumeo akifika, anapotoka kazini,
Mpe mema mamlaka, aliwazike moyo,
Hongera!
5- “Bwana arusi sikia, ukiwa kwako nyumbani,
Maneno ya kutupia,hayafai asilani,
Kauli njema tumia, na lugha iwe laini,
Hongera”
Katika
shairi la “Sifa ya Mke” msanii
anaonesha kuwa sifa kubwa ya mwanamke ni tabia na wala si sura.Sifa ya tabia njema humpa mwanamke
taadhima,huruma,utiifu na hata uhodari. Anaeleza kuwa mwanamke anapaswa kuwa mtulivu,asiwe kiruka njia, asiwe na ufedhuli
wa aina yoyote,uovu, n.k.
Katika
shairi la “Sitaki”mwandishi anakemea mapenzi ya udanganyifu yaliyoshamiri
katika jamii zetu kwa wakati huu. Mwandishi anasema:-
“Rabi
sinipe mapenzi,hakuna wa kuamini,
Wapendwa wenye ujuzi,ni wachache duniani,
Penzi la siku hizi,kuhadaana nyoyoni,
Mapenzi yamepotea, sasa ni adimu sana,”
Ni
kweli mapenzi ya siku hizi hutawaliwa na pesa na yamejaa ulaghai wa kila aina
pamoja na udanganyifu.Mwandishi anaitaka jamii kutambua kuwa mapenzi ya pesa si
mapenzi ya kweli hivyo ni vyema yapigwe vita.
8.
Maonyo na maadili mema katika maisha
Mwandishi
amekuwa mwalimu mzuri wa walimwengu kuhusiana na harakati mbali mbali za
maisha.Mawaidha aliyoyatoa mwandishi ni kielelezo kizuri kinachofaa kufuatwa na
kizazi hiki.Maadili na maonyo haya ni ya muhimu sana katika maisha.Maadili hayo
ni kama vile:-
(a)Malezi bora katika jamii ni njia pekee ya kuiweka
jamii katika msingi bora wa maisha.Katika shairi la“Vijana wa Zanzibar”
Mwandishi ameonesha matendo ambayo vijana wa siku hizi wanayatenda ambayo si mazuri pia ni ya kusikitisha.vijana wa siku hizi hawana
utii,ni wajeuri, ni wadanganyifu,ni majambazi na pia hudharau mila na desturi
zetu za asili na kukimbilia tamaduni za kigeni.Katika ubeti wa 2 msanii anasema:-
“Mwawacha yenu ya hapa,ambayo yako mazuri,
Kutii na kuogopa,mwaona hakuna kheri,
Mwayavamia kwa pupa,kwa kedi na ujeuri,
Mila zetu za fakhari,wacheni kuzipotosha.”
Kulingana
na ubeti huu mwandishi anaonesha kuwa suala la malezi bora ni muhimu sana
katika jamii ili kuwaandaa vijana wetu kuendana na mazingira wanamoishi.
Kwa ujumla,
katika suala la malezi mwandishi anaifundisha jamii kuwa,samaki mkunje angali
mbichi.
b)Umuhimu wa kuwathamini wazazi
Mwandishi
ameonesha kuwa kuna umuhimu wa kuwaheshimu na kuwathamini wazazi.Katika shairi
la “Wazazi” msanii ameonesha kuwa wazazi ndiyo ngao ya
mtoto; hivyo mtoto hatakiwi kuwakasirikia,kuwaudhi wala kuwachikiza bali
anatakiwa kuwa na mapenzi nao.Wajibu wa wazazi kwa mtoto ni kumpa chakula, mavazi,malezi mema pamoja na
elimu.Katika ubeti wa 4 msanii anasema;
“Wakatafuta walimu,kukupatia ujuzi,
Wakakufunza elimu,pamoja na matumizi,
Sasa ni mtu timamu,waendelea na kazi,
Usiwaudhi wazazi,hiyo ndiyo yako ngao”
Katika
shairi la “Ulezi Kazi” Mwandishi ameonesha jinsi mama (wazazi)
wanavyohangaika kubeba mimba hatimye kuzaa na kuanza kazi ya ulezi wa mtoto
hadi anapofikia umri wa kujitegemea. Mwandishi anaonesha kuwa wazazi hupata
taabu na shida mbalimbali katika ulezi wao.Hivyo mwandishi anashauri wazazi
wathaminiwe na wapewe heshima zote wanazostahili.
c)Kuepukana na umbea
Umbea
ni ile tabia ya kutoa maneno au habari bila kutumwa. Mwandishi anaona tabia hii
si nzuri,kwani huweza kutenganisha marafiki au ndugu kwa njia ya uchonganishi.
Katika
shairi la “Wacha Hayo” mwandishi anaishauri jamii iepukane na umbea na
badala yake ijishughulishe na shughuli za uzalishaji mali.Madhara ya umbea ni
kama vile majungu,uchochezi,n.k. Umbea pia husababisha utengano baina ya ndugu
au marafiki.Ubeti wa 1 mwandishi anasema;
“Wacha
kupika majungu,na kuleta uchochezi,
Kuwajaza walimwengu,kasumba zile na hizi,
Hicho kimoja kifungu,huletesha ubaguzi,
Tuacheni ubaguzi,huvunja mafanikiyo.”
Katika
shairi la “Hayafai Mitaani”
mwandishi anaionya jamii kuwa si jambo la busara au zuri kusambaza au
kupeleka taarifa ya jambo fulani sehemu ambayo haihusiki.Anaona kuwa ni busara
sana endapo jambo fulani limefanyikia sehemu fulani liishie huko huko
lilikotokea na haifai kulipeleka sehemu isiyohusika.Si tabia nzuri kupeleka
mitaani kwa watu wasiohusika. Katika ubeti wa 2 unasema:-
“Yanayosemwa kunini, huko huwa yamekisha,
Haifai asilani,
mitaani kufikisha,
Kwani siri ya
mwituni, si vyema kuelewesha,
Ya kunini
huishia kunini.”
Hivyo
mwandishi anatushauri kuwa jambo moja likitendeka sehemu moja ni bora liishie
katika sehemu hiyo na hakuna haja ya kulipeleka sehemu nyingine.
(d)Kuepukana na udokozi (tabia ya wizi)
Udokozi
ni ile hali ya kunyemelea vitu visivyo vyako kwa lengo la kuiba au
kunyang’anya.Katka shairi la ‘Paka’mwandishi anakemea tabia hii
kwani si nzuri.Tabia hii ipo miongoni
mwa wanajamii.Mwandishi anaonya kuwa tabia hii huhatarisha maisha ya wahusika
yaani wenye tabia hii.Mwandishi amemtumia paka kuwakilisha watu wenye tabia
hiyo.Aidha mwandishi anaendelea kuelezea
kuwa tabia hii husababisha uchokozi,ugomvi pamoja na chuki katika maisha.
(e)Umuhimu wa shukrani katika maisha
Mwandishi
anaieleza jamii umuhimu wa kutoa shukrani pale mtu anapofanyiwa hisani na mtu
mwingine. Katika shiri la “Punda”
mwandishi ameonesha jinsi baadhi ya watu wasivyo na shukrani kwa
wenzao ple wanapotendewa mema.Mwandishi ameonesha kuwa mwandamu asiye na
shukrani hata umfanyie wema kiasi gani hawezi kutoa shukrani.Ameelezea kuwa mtu
asiye na shukrani ni vyema kuachana naye au kumtenga (kutengana naye) kabisa.
Anasema;
“Punda hakumbuki wema,hata kwa mchunga wake,
Humpa mwingi mtama, na maji anufaike,
Katu haiwi salama, shukrani zake mateke,
Ndiyo tabia ya punda,kurusha rusha mateke,
Kuchunga
akikushinda, muwachiye ende zake.”
Katika
ubeti huu,mwandishi anasisitiza umuhimu wa kutoa shukrani pale tunapofanyiwa
fadhila au jambo jema.
UJUMBE
Ø
Dhana
potofu ya kudhani bila ya kuwa na uhakika wa mambo haifai katika jamii kwa
sababu hupotosha ukweli wa mambo.
Ø
Mapenzi
na ndoa ya dhati ni muhimu katika jamii zetu
Ø
Ukoloni
mamboleo, uongozi mbaya,rushwa na ukosefu wa elimu ni baadhi ya vikwazo vya
ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
Ø
Maadili
mema na maonyo ni njia pekee ya kuiweka jamii katika misingi ya haki na usawa.
FALSAFA
Mwandishi
anaamini kuwa maadili mema na maonyo ni njia pekee ya kuiweka jamii katika
msimamo na mwenendo bora wa maisha na
anatetea misingi ya haki na utu katika jamii.
MSIMAMO
Msimamo
wa mwandishi una hali ya udhanifu kwani amejadili baadhi ya mambo kwa kudhani
tu bila kuwa na misingi ya kisayansi.
FANI
1. MITINDO
Mwandishi
wa diwani ya KIMBUNGA ametumia mitindo ifuatayo:-
(a) Mtindo wa kuhoji
Ni mtindo Swa kuuliza maswali ambayo ama
majibu yake yako wazi au hayako wazi.
Mashairi yaliyotumia mtindo wa kuhoji au kuuliza maswali katika diwani
hii ni “Mnapata Kitu Gani?” na “Nimuite Jina Gani” .
Katika
shairi la “Mnapata Kitu Gani?”
,mshairi anasema;
“Wavutaji wa sigara, nauliza nijibuni,
Ni ipi yake tijara, mwapata faida gani,
Nipeni jawabu bora, ambayo ya kuamini,
Ni ipi tijara yake, nambiyeni mvutao”
Katika
shairi la “Nimuite Jina Gani” ,mshairi
anasema:
“Ninalo suali langu, wamalenga msikiye,
Ilivyo na ndugu yangu, na mimi ndiye kakaye,
Amemuowa mwanangu, aliye nihusu miye,
Mke nimuite vipi, mwanangu au shemegi”
(b) Mtindo wa msisitizo au takriri
Ni
mtindo ambao neno moja linatokea mwanzoni na linarudiwa katika mishororo au
mistari ya ubeti wa shairi.Shairi lililotumia mtindo wa msisitizo au takriri
katika diwani hii ni “Kujitawala”.Mshairi
anasema;
“Kujitawala si kwema, kuliko kutawaliwa,
Kujitawala ni umma, kila yao kuamuwa,
Kujitawala si kama, ulanguzi na rushwa.
Kujitawala ni mila, nchini kushikiliwa,
Kujitawala aila, kufunzwa yanotakiwa,
Kujitawala si ila, kufanza yaso kuwa”.
( c ) Mtindo wa masimulizi
Ni
mtindo ambao mshairi ama huamua kusimulia hadithi yeye mwenyewe au huwaumba
wahusika wanaosimulia hadithi au kisa
fulani kwa wengine.Shairi lililotumia mtindo wa masimulizi katika diwani hii
ni “Kibwangai”.
Mshairi anasema;
“Kuna hadithi ya kale, kwa babu
nimepokeya,
Kwa manyani zama zile, mkasa ulotokeya,
Nilikuwa mwanakele, hayo nikazingatiya,
Leo nawadokezeya kwa nilivyofahamu”
( d ) Mtindo wa kuto wasia
Ni
mtindo ambao unonesha usia au maagizo ya mtu kwa watu wake ambayo anataka
yatimizwe baada ya kifo chake au kuondoka kwake mahali fulani.Mashairi
yaliyotumia mtindo wa kutoa wosia katika diwani hii ni”Wasia” na “Paka”.
Katika
shairi la “Wasia”,mshairi anasema;
“Wasia wangu nakupa, mwanakwetu zingatiya,
Siingiliye
kwa pupa, ina hatari duniya,
Itakuja
kukutupa, usipopakusudiya,
Kaa kwa
kuiogopa, katu haina shujaa”
Katika
shairi la “Paka”, mshairi anasema;
“Kuna hadithi ya
kale, kwa babu nimepokeya,
Kwa manyani zama
zile, mkasa ulitokeya,
Nilikuwa
mwanakele, hayo nikazingatiya,
Leo
nawadokezeya, kwa nilivyoyafahamu”
( e ) Mtindo wa majibizano
Ni mtindo ambao mshairi anaamua kuwaumba
wahusika wanaozungumza kwa kupokezana maongezi.Shairi lililotumia mtindo wa
masimulizi katika diwani hii “kibwangai”
. Mshairi anasema;
“Pana mmoja kasema, kibwangai
kumwambiya,
Kama tutalokutumia, weza kututimiziya,
Isiwe kurudi nyuma, ewe mwenzetu
sikia,
Wewe tumekuchagua, utumikie
kaumu.
“Kibwangai akasema, hayo
nimezingatia,
Kidete nitasimamia, jitihada
kutimia,
Kwa kusi na kulima, mpate jifaidia,
Sitobadili mawazo, ilipwe yangu
kaumu”
( F ) Mtindo wa kutoa amri
Ni mtindo ambao mshairi
huonekana ama akiamrisha watu kufanya au kutofanya jambo Fulani au akitoa
maelekezo fulani muhimu kwa wanajamii.Shairi lililotumia mtindo wa kutoa amri
katika diwani hii ni “Usimpige mkeo” (uk.
12). Mshairi anasema:
“Mke hapigwi kwa fimbo,wala hapigwi
mateke,
Hupigwa kwa mapambo, hilo ndilo
pigo lake,
Usiyaharibu mambo, utajuta mwisho wake,
Kupiga piga si kwema, kaa nae kwa salama”
( g )Mtindo wa kidato
Ni mtindo ambao mshairi
hutumia baadhi ya mistari iliyofupishwa maneno au silabi tofauti na mistari
mingine ambayo huwa na silabi au maneno mengi. Mashairi yaliyotumia mtindo wa
kidato katika diwani hii ni “Usimalize”,“Hongera”,
“kimbunga”, “kazi”, “Dumuzi”,“chuwi”, na “Madereva”.
Katika
shairi la “Usimalize”, mshairi
anasema:
“Haifai kumaliza, kumi utumie tisa,
Moja utudunduliza, kuna halafu na sasa,
Weza kujihakibiza, usijipige msasa,
Akiba
haichakai,
Katika shairi la “Hongera” ,mshairi anasema;
“Biarusi yangu shika,uyatie
akilini,
Muumeo akifika,anapotoka kazini,
Mpe mema mamlaka, aliwazike moyoni,
Hongera”.
(h)
Mtindo wa nafsi
Ni mtindo ambao mshairi anaweza kutumia nafsi
umoja,nafsi wingi au nafsi kikundi kwa lengo la kufikisha ujumbe au maudhui
fulani kwa jami.Kuna nafsi za aina tatu (3),yaani nafsi ya kwanza (umoja na
uwingi),nafsi ya pili (umoja na uwingi, na nafsi ya tatu,(umoja na
uwingi).Mwandishi wa diwani hii ametumia mtindo wa nafsi kama ifuatavyo:
i.
Matumizi
ya nafsi umoja (nafsi ya kwanza umoja na nafsi ya pili umoja):
Katika mtindo huu mshairi
huzungumzia jambo ambalo linamuhusu mtu mmoja pekee.Hujumuisha ahadi,matamanio,
sifa mawaiza na maonyo.Mashairi yaliyotumia nafsi ya kwanza umoja katika diwani
hii ni “uchawi”, “kipaji” na
“sitaki”. Kwa mfano katika shairi la “sitaki”,
mshairi anasema:
“Wanaopenda nawapende, mimi siye
asilani,
Nimejitenga upand, singie mwao
kundini,
Moyo nimepiga konde, usiweze kutamani,
Mapenzi yamepotea, sasa ni adimu
sana”.
Pia
mashairi yaliyotumia mtindo wa nafsi ya pili umoja katika diwani hii ni “usimpige
mkeo” , “kurumbizi” , “usimalize” ,“Paka”, “Dawa ya deni kulipa”, “ Sifa ya mke”
na “Wasia”.Kwa mfano katika shairi la “kurumbizi”, mshairi anasema;
“Siye wewe kurumbizi, wa kubughudhi
kuichaka,
Si mema mapendekezi, ukae ukikumbyuka,
Kuponda haipendezi, ambacho
kinakuweka,
Usiwe mpopotozi, na hayo ukatamka,
Mbona unaghafilika, nakuhasa kulumbizi”
ii.
Matumizi
ya nafsi wingi (nafsi ya kwanza wingi);
Katika mtindo huu mshairi
huzungumzia jambo au suala linalohusu kundi fulani la watu,akiwemo na yeye
mwenyewe. Mashairi yaliyotumia mtindo wa nafsi ya kwanza wingi katika diwani
hii ni “kisomo cah manufaa” , “Rushwa” ,
“Wenye vyao watubana” , “Usafi” , “Wacha hayo” ,“dhamana” .Kwa mfano katika
shairi la “Rushwa” ,mshairi anasema:
“Rushwa kajenga kambi, na kuondoka
hataki,
Afanya kila vitimbi, mkaidi
hashindiki,
Tumzushiyeni wimbi, isiwe kutuhiriki,
Tumchimbie handaki, rushwa tukamzuikeni.”
iii.
Matumizi
ya nafsi kikundi (nafsi ya tatu wingi);
Katika mtindo huu mshairi huonekana
ama akisimulia hadidhi, akitoa hotuba au akizungumzia kundi fulani la watu
kuhusu suala au jambo muhimu.Mashairi yaliyotumia mtindo wa nafsi ya tatu
uwingi katika diwani hii ni “Hili mnatutakia”, “wazazi”
“Dumuzi”
. Kwa mfano katika shairi la “ Hili
mnatutakia”,mshairi anasema;
“Wakijua
unapesa, nyumbani watakujia,
Usiku wa saa tisa, ndani kukuingilia,
Mara wakakukabasa,
na vyako kuangamiya,
Hakuna
watendewalo, ndipo wakapamba moto.”
( B ) MUUNDO
Mwandishi
wa diwani ya hii ametumia miundo tofauti tofauti kwa kuzingatia vigezo
mbalimbali kama ifuatavyo:-
Ø Kigezo
cha idadi na mishororo:
Kwa kuzingatia kigezo
cha idadi na mishororo kwa kira ubeti mshairi ametumia miundo ifuatayo;
(a) Muundo wa tathlitha
Ni muundo ambao kila ubeti unakuwa na
mistari mitatu.Shairi lililotumia muundo wa tathlitha katika diwani hii ni “kujitawala”. Mshairi anasema;
“kujitawala si kwema, kuliko
kutawaliwa,
Kujitawala ni umma, kila hayo
kuamua,
Kujitawala si kama, ulanguzi
na rushuwa.”
(b) Muundo wa tarbia:
Ni muundo ambao kila ubeti unakuwa na
mistari minne. Mshairi ametumia muundo wa tarbia katika mashairi takrimu yote.
Miongoni mwa mashairi hayo ni “Afrika”
(uk. 1-2), “kisomo cha manufaa” , “vielezeo” , “kiswahili”, “ uokolewe”,
“madanganyano” , “wenye vyao watubana” , “chaka”, “kibwangai” , “usimpige
mkeo”, “Rushwa” , “usafi” ,“ vitendawili”,“beni” ,“Hili mnatutakia” , “Wazazi”,
na “ si vyema”.Kwa mfano, katika shairi la “usafi”, mshairi anasema:
“kipindupindu twajua, maradhi
yanohiliki,
Usafi ni yake dawa, kufanyiza
hatutaki,
Hatua ikichukuwa, serikali
twaichukia,
(c) Muundo wa takhmisa
Ni muundo ambao kila
ubeti unaundwa kwa mistari mitano.
Mashairi yaliyotumia muundo wa takhmisa katika diwani hii ni
“kurumbizi,“Punda”, na “Bahati”. Kwa mfano katika shairi la “kirumbizi”,
mshairi anasema:
“siye wewe kirumbizi, wa kubughudhi
kichaka,
Si mema mapendekezi, ukae ukitumbuka,
Kuponda haipendezi, ambacho kinakuweka,
Usiwe mpopotozi,na hayo ukatamka,
Mbona unaghafilika,
nakuhasa kurumbizi,”
Ø Kigezo
cha idadi ya vipande
Kwa kuzingatia idadi ya vipande kwa kila mchororo
katika ubeti wa shairi mwandishi wa diwani hii ametumia muundo wa vipande
viwili (ukwapi na utao).Huu ni muundo ambao kwa kila mshororo (mstari)
wa ubeti wa shairi kunakuwa na vipande viwili,yaani kipande cha kwanza (ukwapi)
na kipande cha plili ( utao).Mashairi
yote ya diwani hii yametumia muundo wa vipande viwili.Kwa mfano katika shairi
la “ulezi kazi”,mshairi anasema;
“kulea mwana ni kazi, natakan
ifahamike,
Hii tabu ya uzazi, hupita majir yake,
Hubakia kwa mlezi, mzigo kichwani
mwake,
Kazi kumlea mwana, uzazi ni uraufu,
Ø Kigezo
chya aina ya vituo:
Kwa kuzingatia kigezo cha aina ya vituo,mwandishi wa
diwani ya KIMBUNGA ametumia miundo ifuatayo:-
(a) Muundo wa kituo bahari
Kituo bahari ni mstari wa mwisho wa ubeti wa shairi
ambao hujirudiarudia kwa kila ubeti. Mashairi yaliyotumia kituo bahari katika
diwani hii ni “kimbunga” (uk. 8-10), “Afrika” , “Kiswahili”, “Uchawini” ,
“usimpige mkeo”, “usafi”, “Vitendawili” ( “mtu wa namna hiyo”, “hongera”,“kazi”
, “Hili mnatutakia”, “ Wazazi”, “Sivyema” , “ karumbizi”, “Punda”,“Paka”,
“ulezi kazi”, “ Dhamana” , “Vijana wa Zanzibar”, “wacha hayo “, “usimalinze” (,
“ndiye avumaye”,“makarafuu” ,“Dawa ya deni kulipa”,“mpewa hapokonyeki” ,
“Bahati”, “Si uzito wa latili” ?, “Hayafiki mitaani” “Dumuzi” , “Chuwi”,
“madereva” ?, na “Sitaki” .
Katika shairi la “wazazi”,mshairi
anasema.
“wazazi ni yako ngao, udumu
na kuwaenzi,
Usikasirike nao, kaa nao kwa mapenzi,
Wakifurahika hao, juwa huna
pingamizi,
Usiwauzi wazazi, hiyo ndio
yako ngao,
Baada ya kukuzaa, wakawa na
kubwa kazi,
Chakula cha kuvaa, kukuwekea simanzi,
Wala hawakuzubaa, kukupa mema
malenzi,
Usiwauzi wazazi, hiyo ndiyo yako
ngao.”
(b) Muundo wa kituo nusu bahari
Kituo
nusu baharini ni mstari wa mwisho wa ubeti wa shairi ambao sehemu tu ya
mshororo (mstari) hujirudia kwa kila ubeti wa shairi.Mara nyingi katika kituo
nusu bahari, kipande kimoja tu cha mshororo wa mwisho wa ubeti hurudiwa katika
beti za mashairi. Mashahiri yaliyotumia muundo wa kituo nusu bahari katika
diwani hii ni “mnapata kitu gani?”, “
Wasia” , “Nimuite jina gani”, “kasa”, “ Sifa ya mke” .
Katika
shairi la “ nimute jina gani” , mshairi
anasema:-
“Ninalo
suali langu, wamalenga msikie,
Ilivyo na ndugu yangu, na mimi
ndiye kakaye,
Amemuowa mwanagu, aliye nihusu mie,
Mke nimuite vipi, mwanangu au shemeji.
Nimuite vipi mke, na hata
ielekee,
Kwani ni mjomba wake, na mume ni kakae,
Jina gani litumike, mkwe au
shemejie,
Lipi litaelekea, mwanangu au shemeji.”
(c) Muundo wa kituo kimalizio
Kituo
kimalizio ni mstari wa mwisho wa ubeti wa shairi ambao haujirudiirudii kwa kila
ubeti.Hii inamaana kuwa kwa kila ubeti wa shairi kuna kuwa na mstari wa mwisho
(kituo) na tofauti au usiofanana na beti nyingine.Mashairi yaliyotumia muundo
wa kituo kimalizio katika diwani hii ni “kisomo
cha manufaa”, “vielezeo” , “uokolewe” , “madanganyano” , “ kujitawala”,
“kibwangai” , “Beni” , “minazi chotara” , “kipaji” na “tenga” .katika shairi la “kibwangai”. Mshairi anasema;
“kibwangai
lipoona, ni mtu kakamiliya,
Akaanza
kujivuna, na dharau kuzidia,
Wala hakujali tena, wenzake
walimwambiya,
Akahisi hawi nyani, umbo lile litadumu,
Kawa na tabia moja, nyani
walipomwendea,
Akajifunga mkaja, mijiwe
kuwalushia,
Hakujali zao haja,
wala kuwahurumia,
Kapiga na kukemea, pia na
kuwashutumu.”
Ø Kigezo
cha muundo kwa kuzingatia mpangilio wa mashairi:
Katika
kigezo au kipengele hiki kinachochungunzwa ni jinsi/malenga mshairi
alivyoyapanga mashairi yake ndani ya diwani.Kinachoangaliwa kwa makini ni kama
mashairi yamepangwa kwa utaratibu maalumu au mashairi yamechanganywa; mfano
uchanganyaji wa mashairi ya mapenzi,
kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Je mshairi ameyapanga mashairi ya kimapenzi
peke yake, akaja mashairi ya kisiasa baadae kuchumu, kiutamaduni,n.k? Mwandishi wa diwani ya KIMBUNGA hajayapanga
mashairi yake kwa usahihi au maalumu kwani amechanganya mashairi ya kimapenzi,
kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
MANDHARI
Mshairi
wa diwani ya KIMBUNGA ametumia mandhari yafuatayo:-
(a) Mandhari ya bara ya Afrika
Mshairi
anazungumzia mambo,kero, shida au matatito mbalimbali yanayokabili bara la
Afrika, ikiwemo nchi Tanzania kupitia mashairi ya “Afrika” , “Kiswahili” , “vijana wa Zanzibar”.Mshairi ametaja nchi
moja wapo ya bara la afrika ambalo ni Tanzania, hasa Zanzibar.
Pia, mshairi ametaja maeneo kama mji wa Siyu
na pori la Bweleo, ambayo yamo ndani ya bara la Afrika.Mandhari ya bara la
Afrika yanaibua dhamira za unafiki,usaliti,amani,chazo/asili ya Kiswahili,
upotoshaji wa mila,mmomonyoko wa maadali wa maadili (uvutaji wa bangi na
ujambazi/wizi),ukosefu wa uzalendo na utoaji wa wasia.
(b) Mandhari ya
porini,baharin na shambani. Mandhari yote haya yanaibua dhamira za
umaskini,unyonyaji,uongozi mbaya,dhuluma na usaliti.
Kwa kumalizia,
diwani hii iliandikwa na Haji gora Haji mnamo mwaka 1994 akizungumzia kwa kiasi
kikubwa matukio yanayohusu nchi za bara za Afrika, hasa katika visiwa vya
Zanzibar nchini Tanzania ingawa maudhui yake yanasadifu wakati tulionao hivi
sasa katika nchi zinaziendelea, ikiwemo nchi ya Tanzania.
WAHUSIKA
Mwandishi
wa diwani ya kimbunga ametumia
vikundi kama ifuatavyo:-
(a) Wahusika wanasiasa na wabepari
Mshairi
amewatumia wahusika wanasiasa na mabepari katika mashairi ya “kimbunga” , “Afrika” ,“Madanganyano” na “wenye vyao watubana” . Wahusika hawa
wanawakilisha tabaka la juu (tawala) linalonyonya, linalodhurumu, linaloonea na
linalokandamiza tabaka la chini.Wahusika wanasiasa ni wabinafsi, waongo,
wasaliti, wadhulumaji, waqnafiki na wasiowajibika katika kazi zao.
(b) Wahusika
wakulima
Mshairi
amewatumia wahusika wakulima katika shairi la”madanganyano”, wahusika hawa wanawakilisha watu wa tabaka la
chini,maskini na wanaonyonywa na kukandamizwa na watu wa tabaka la juu (viongozi
na mabepari au matajiri)
c)Matumizi ya Lugha
Mwandishi
ametumia lugha rahisi iliyoshehenezwa lahaja ya Kiunguja yenye mafumbo na
taswira mbali mbali pamoja na tamathali
za semi kidogo na misemo kwa kiasi.
d)TAMATHALI ZA SEMI
Tashibiha
Ø
Kwenye
shairi la “Sifa ya Mke” (uk 40)
·
Ufedhuli
na uovu kama yake mazoea.
·
Awe
kama malaika mzuri kupindukiya
Tafsida
Mwandishi
ametumia mbinu ya kufumba kwa kusema maneno makali,machafu,matusi kwa kutumia
tafsida.Mfano shairi la “Nyang’au”linahusu
tamaa,Paka” linahusu wizi, shairi la “Dumuzi” linakemea uvivu,n.k.
Mbinu Nyingine za Kisanaa
Takriri
Mwandishi
ametumia takriri ili kuweka msisitizo mfano shairi la “Kujitawala” (uk 7-8)
neno kujitawala
limerudiwarudiwa.
Matumizi ya Taswira
Mwandishi
ametumia taswira nyingi kama vile;
Kimbunga …(uk 1)…..Kuashiria mapinduzi
Kibwangai…(uk 9)….Kuashiria viongozi wasaliti
Nyani…..(uk 9)…….Kuashiria wananchi waliosalitiwa
Chuwi…..(uk 42)…..Kuashiria ukoloni mamboleo, n.k.
Jina la Kitabu
Jina
la Kitabu Kimbunga halisadifu yale
yaliyomo ndani ya kitabu kwa sababu hatuyaoni mageuzi yoyote ambayo anayajadili
katika kitabu hiki zaidi ya mashairi ya maadili mema na maonyo ya
kimaisha.Asilimia kubwa ya mashairi katika diwani hii yamejadili juu ya maonyo
na maadili katika maisha.
Kufaulu kwa Mwandishi
Kimaudhui
Mwandishi
amefaulu ;
Ø
Kutoa
maadili mema na maonyo katika jamii
Ø
Kujadili
dhamira ya ujenzi wa jamii mpya
Ø
Ameonesha
mbinu mbalimbali za kufuata ili tufanikiwe katika ujenzi wa jamii mpya
Kifani
Ø
Ametumia
lugha rahisi, mafumbo, taswira, n.k.
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui
Ø Baadhi ya
maadili aliyoyajadili katika diwani hii ameyajadili kidhanifu,ni sawa na yale
tunayoyapata makanisani, ambayo yana nafasi ndogo sana katika ujenzi wa jamii
mpya
Ø Vile vile
amejadili masuala mbalimbali kidhanifu hasa anapomhusisha Mungu.Kama vile
masuala ya kipaji (uk 38-39), bahati (uk 36), umaskini (uk 35).
Kifani
v Mwandishi
ametumia lahaja ya Unguja badala ya
Kiswahili sanifu ivyo ni vigumu
kueleweka kwa watu wote.
v Diwani hii ni ya
hali ya chini sana katika muundo,mtindo na baadhi ya vipengele vingine vya
kisanaa.