FONIMU
Fonimu ni nini
TUKI (1990:45) wanasema fonimu ni kipashio kidogo kabisa cha kifonolojia kinachobadili maana. Hyman (1975:59) yeye anasema fonimu ni kipashio kidogo kabisa cha sauti kinachoweza kutofautisha maneno yenye maana tofauti. Mfano: ‘bata’ kuwa ‘pata’. Fonimu inawakilishwa katika maandishi kwa kutumia alfabeti za kifonetiki katika mabano mshazali / /.
2.1.1 Historia ya Fonimu
Dhana ya fonimu ina historia ndefu sana ambayo ilitokana na nadharia ya wanamuundo inayoitwa “nadharia ya fonimu”. Katika kuitalii historia hii tunaanza na asili ya istilahi ‘fonimu’ na kisha tutaangalia ‘nadharia yenyewe ya fonimu’.
Kwa miaka mingi dhana ya fonimu ilikuwa katika akili za wanaisimu wa wakati huo lakini istilahi yenyewe iliundwa baadaye sana. Hata hivyo, wanaisimu wanatofautiana juu ya nani alianzisha istilahi hiyo na au kuipa fonimu dhana inayot6umika hivi leo. Jones (1957) anasema istilahi hiyo iliundwa na Baudouin de Courtenay. Robins (1967) naye anaunga mkono mawazo hayo kwa kusema kuwa de Courtenay alitumia neno la Kirusi fonema katika kitabu bchake cha ‘Theory of Phoneme’ cha 1884. Hata hivyo, Firth (1957) yeye anasema kuwa inaelekea kuwa de Courtenay aliiazima istilahi hiyo kwa mwanafunzi wake Kruszewiski aliyeitumia katika insha yake iliyochapishwa mwaka 1879 alipokuwa akielezea athari za mkazo katika Rig-Veda.
Pia anaongeza kwa kusema kuwa wazo la fonimu lilikuwamo katika fikra za wanafonetiki na wanaotografia ambao walitofautisha unukuzi mpana na unukuzi finyu. Kwa mfano mwanafoetiki wa Kiingereza, Henry Sweet alitofautisha unukuzi mpana na unukuzi finyu kwa kuseama kuwa: Unukuzi mpana ni ule unukuzi wa kifonemiki (/ /) (kifonolojia) ambao huonyesha tofauti za uamilifu wa sauti na unukuzi finyu ni ule wa kifonetiki ([ ])ambao unaonyesha sifa zote za kimatamshi za sauti. Kufanya hivi inamaanisha kwamba walielewa kwamba kuna sifa za suati ambazo zina maana katika lugha fulani na nyingine hazina maana. Zile zenye maana ndizo zilijulikana baadaye kama sifa za msingi ambazo zinaunda ‘fonimu’ na zile zisizo za msingi pamoja na za msingi zinaunda ‘foni’.
Krámský (1874)5 anadai kuwa mwanazuoni wa kwanza kuitumia istilahi fonimu ni Dufriche-Desgenettes katika mkutano wa Societe de Linguistique de Paris (24 May 1873) ambapo aliitumia kama kibadala cha neno moja la kijerumani sprachlaut ‘sauti’ (taz. Revue Critique, 1873:368) badala ya ‘son du langage’. Mtu wa pili kulitumia neno hili ni Havet (taz. Havet, “Ol et UI en fransais”, Romania, 874:321) kamaanavyonukuliwa na Krámský. Krámský pia akimnukuu Jakobson (1871:396-397) anasema kutoka kwa Havet akalitumia de Saussure katika kazi yake ya Memoire sur le System Primitif des Voyelles dans Langues Indoeureopèennes ingawa ni katika mtazamo wa kihistoria zaidi.
Kutoka kwa de Saussure neno fonimu lilitumiwa na Kruszewsky (1851-1887) mwanafunzi wa de Courtnay ambaye mwaka 1880 alichapisha mapitio ya Memoire ya de Saussure ambapo alitumia istlahi fonimu kwa mara ya kwanza kama kipashio cha kifonetiki na sauti kama kipashio cha kifiziolojia ya sauti. Mwaka 1881 akaamua kukiita kipashio cha kifonetiki ambacho hakionekani kuwa ni fonimu ingawa hakutoa maana yake, kwa hiyo aliipa fonimu dhana mpya.
Anderson (1985:67)6 anaona kuwa ni de Courtinay ndiye aliifasili fonimu kuwa fonimu ni maumbo ya sauti ya saikofonetiki yanayoweza kubadilikabadilika. Anderson anasema kuwa de Courtinay aliiweka katika uwakilishi wa kisaikofonetiki wa mofimu ambazo huweza kubadilika badilika. Hapa ndipo tunaona kwamba kuna michakato ambayo inazibadili sauti hizi kutokana na kanuni za mfuatano wake katika lugha.
Kwa ujumla maelezo ya Krámský juu ya historia ya fonimu hukubaliwa na wanaisimu. Utofauti wa wanaisimu hawa ni kuwa wengine walitilia msisitizo mwanzilishi wa istilahi fonimu na wengine mwanzilishi wa dhana ya fonimu kama itumikavyo leo na de Courtinay huonwa kuwa ndiye wa kwanza kutumia dhana ya fonimu kama itumikavyo leo
2.2 Mawazo ya de Courtenay na de Saussure kuhusu sauti za lugha za Binadamu
2.1 Mawazo ya Baudouin de Courtenay
Alizaliwa 1845 huko Poland. Alianza kujishughulisha na nadharia ya fonimu na ubadilishanaji wa kifonetiki mwaka 1868. Anadai kuwa dhima ya sauti, yaani lugha ilivyojengwa katika hisia za watu, haitokei kwa namna sawa na umbo lake linalotamkwa. Hali hii husababisha kuwepo kwa maumbo mawili yanayojitegemea ambapo moja tunaweza kuliita fonimu na lingine ni sauti zinazotamkwa (za usemaji). Kwa hiyo, de Courtenay anaweka tofauti kati ya sauti kama zinavyobainishwa na wasemaji wa lugha katika bongo/akili zao na sauti kama vitu halisi vinavyotamkwa. Anadai kuwa katika uchunguzi na uchanganuzi wa mfumo wa lugha wa sasa kuna mambo mawili amabyo yanachunguza:
a) Kuchunguza na kuchanganua kile kinachotamkwa na b). Kuchunguza kile kilichokusudiwa katika ubongo wa msemaji.
Hapa tunaweza kuvibainisha vitu vilivyomo katika akili ya msemaji: 1. sauti zote za lugha yake (fonimu) (sifa bainifu za sauti za lugha yake), 2. mfuatano wake, 3. uamilifu wake, 4. lafudhi, 5. mkazo, 6. kiimbo, 7. mawimbisauti na uamilifu wake, 8. maana za maneno ya lugha yake. Matumizi sahihi ya vipengele hivi ndiyo unayofanya wazungumzaji waelewane. Hata hivyo, wakati mwingine msemaji wa lugha anaweza kutamka umbo fulani la sauti likiwa na umbo tofauti na lile analokijua msemaji katika akili yake na alilolikusudia. Ikiwa atatamka si kwa mkengeuko mkubwa, wasemaji wenzake wanaweza kumwelewa anamaanisha nini:
Mfano: ‘ngombe’ badala ya ng’ombe, kurara badala ya kulala, safyulia badala ya sufuria, r«ha badala ya raha, nk
Kwa mujibu wa de Courtenay uwanja unaoshughulikia sauti za lugha zinazotamkwa na msemaji kwa kutumia alasauti anauita athropofoniki na ule unaoshughulikia sauti kama zilivyo na zinavyokusudiwa katika ubongo wa msemaji unaitwa saikofonetiki (Anderson 1985:65).
Kwa hiyo katika uchanganuzi na uchunguzi wa lugha tunachunguza kile kinachotamkwa na kile kilichokusudiwa ubongoni mwa msemaji. Anthropofoniki hushughulika na uchanganuzi wa sauti kwa kuzingatia fisiolojia (umbo halisi linalotamkwa, hii leo fonetiki) na saikofonetiki hushughulikia sauti kama mfumo wa uhusiano wiani baina ya sauti na maana na zinavyohusiana (hii leo fonolojia) (de Courtenay 1871;1972:58; Anderson, 1985:65). Hivyo, aliona kuwa kuna vipengele viwili vya kujifunza mfumo wa lugha kisinkronia, yaani kipengele cha umbo kama kilivyo wakati huo, na kipengele cha kisaikolojia. Pia aliiona saikofonetiki ni ya kisaikolojia zaidi na huchanganua sauti kwa mtazamo wa mofolojia na uundaji wa maneno (jinsi sauti zinavyofuatana katika kuunda maneno ya lugha. Hivyo, kipengele cha kisaikolojia cha sauti husaidia katika kutofautisha maneno na maana zake; kitu ambacho ni kazi ya fonimu. Kwa jumla tunaweza kusema kuwa de Courtenay alitambua kuwa dhana ya saikofonetiki ilikuwa imekitwa katika upambanuzi wa sauti.
¨ Alitambua viwango viwili vya uwakilishi wa sauti: kiwango cha fonetiki=anthropofoniki na kiwango cha fonolojia= saikofonetiki
¨ Fonimu zilikuwa na sifa pambanuzi na zilihusishwa na ubongo/saikolojia lakini haziwezi kuwakilisha maana zikiwa peke yake.
2.2 Mtazamo wa Ferdnand de Saussure Kuhusu Sauti za Lugha za Binadamu
Alizaliwa mwaka 1857 huko Geneva Switzerland. Alijishughulisha sana na isimu akiwa amejiegemeza katika isimu muundo na semiotiki. Alitoa mchango mkubwa sana katika isimu kiasi cha kujulikana kama ‘baba wa isimu kileo’. Miongoni mwa michango yake mikubwa ni kuweka wazi tofauti iliyopo kati ya kile alichokiita ‘langue’ (lugha) na kile alichokiita ‘parole’ (utendaji). Kwa maelezo yake ‘langue’ ni ile sehemu inayowakilisha uelewa wa mzungumzaji wa uhusiano uliopo kati ya sauti na maana. Yeye anasema kuwa lugha ni mfumo wa alama. Anasema kuwa alama zina pande mbili na ili alama iweze kuitwa ‘alama ya kiisimu’, kama alivyokusudia de Saussure, ni lazima kuwe na (i) Mtajo (/kitaja/kitajo = significant), yaani kitu kinachotaja na ‘kitajwa’ (signifie), yaani dhana au kitu halisi. Tukiunganisha na mawazo ya de Courtenay tunaweza kusema kuwa katika saikolojia au akili ya msemaji wa lugha kuna sifa bainifu za sauti na dhana/vitu halisi. Kati ya vipengele hivi viwili mtajo huonyesha tofauti baina ya alama moja na nyingine katika mfumo mmoja na kitajwa ndiyo taarifa inayowakilishwa na mtajo. Kitajo/kitaja cha kitu/dhana ngeni hakimo katika akili ya mzawa na hii inathibitisha nadharia tete ya Sapir na mwenzake inayodai kuwa lugha ya mtu inatawaliwa na mazingira anayoishi. De Saussure anaendelea kusema kuwa mfumo wa alama ndio ujengao maarifa ya pamoja ya jamiilugha moja (licha ya tofauti ndogo ndogo za watu binafsi katika jamii hiyo).
Parole (utendaji katika lugha) huhusu usemaji kwa ujumla, yaani jinsi lugha inavyotumiwa na msemaji mmoja mmoja. Ni utumiaji wa mfumo wa alama alionao mzawa wa lugha katika akili yake.
Kwa mujibu wa de Saussure dhana ya langue (lugha) na parole (utendaji) ni zaidi ya fonetiki na fonolojia, lugha kwake yeye inahusisha mfumo wa vipengele vyote vinavyohusiana kama vile vya kileksika (neno), kisarufi na kifonolojia. Utendaji kwa mujibu wake unahusisha mambo yote yanayotamkwa au kusemwa na si maneno tu. Aliona kuwa langue na parole huweza kutofautina kutokana na mambo kadhaa yanayoweza kumwathiri msemaji katika usemaji wake kama vile uchovu, usingizi, njaa, kuteleza kwa ulimi, nk na akajikuta anasema kile ambacho hakukusudia. Katika utendaji kuna makosa mengi yanayosababishwa na mambo mengi na hivyo, mwanaisimu anapaswa kujishughulisha zaidi na lugha (langue) na si utendaji. Anasema kazi ya mwanaisimu ni kuchunguza vipashio (faridi) mbalimbali vya sauti na sheria zinazotumika katika kuviunganisha ili kujenga mfumo wa lugha.
Anasema pia unapotofautisha langue na parole unakuwa unatofautisha mambo ya muhimu na yale yasiyo ya muhimu na kile ambacho ni cha kiibinafsi na cha kijamii. Kwake yeye parole si ya muhimu sana. Hata hivyo, ifahamike kuwa taaluma ya utoaji wa sauti (parole = utendaji) na taaluma ya mfumo wa sauti za lugha (langue = lugha) huhusiana sana. Utendaji una nafasi kubwa sana katika kuuelewa mfumo wa sauti za lugha. Ili uuelewe mfumo wa sauti za lugha ni lazima uzielewe sauti mbalimbali zinazotumika katika lugha hiyo.
Massamba (2012) anasema kuwa de Saussure anadai kuwa dhana ya alama inakamilika ikiwa na mtajo na kitajwa vimeungana na haviwezi kutenganishwa. Dhana hushikamana na sauti na sauti huwa ni alama ya dhana (an idea becomes fixed in a sound and a sound becomes the sign of an idea). Kutokana na melezo haya ni wazi kwamba hatuwezi kupuuza utendaji (parole) kuwa humo ndimo mtajo/kitaja kinamojitokeza na pia hakuna alama pasipo kitaja/mtajo. Hivyo, utendaji si kitu cha kupuuzwa.
Aidha, kuhusu muundo wa sauti, de Saussure anasisitiza kwamba kilicho muhimu kuhusu sauti za lugha ni kwamba zinatofautiana. Kwa hiyo sauti zilizo katika mtajo/kitaja zisibainishwe kwa sifa zinazozitambulisha tu bali na kwa thamani yake katika mfumo mzima wa sauti na zinavyotofautiana na mfumo maalumu. Massamba (keshatajwa), anasema kuwa mawazo ya de Saussure kuhusu alama ya kiisimu inatupeleka kwenye dhana ya ukinzani. Kutokana na hili tunaona kuwa dhana ya alama ya kiisimu ‘inafanana sana na dhana ya fonimu kama ilivyoeleweka hapo baadaye. Kwa de Saussure alama ndiyo msingi wa mfumo wa kiisimu kama ambavyo fonimu, katika nadharia za baadaye, ilikuja kuchukuliwa kama msingi wa fonolojia. Hata hivyo, yeye hakutumia neno fonimu kuwakilisha sifa ya upambanuzi na hatuwezi kuiona alama ya kiisimu sawa na fonimu. Alama ina vitu vingi ndani mwake tofauti na fonimu isipokuwa zile sauti za mwigo.
2.3 Mitazamo Mbalimbali Kuhusu Dhana ya Fonimu
2.3.1 Mtazamo wa Prince Nikolaj Trubertzkoy Kuhusu
Huyu ni mmoja miongoni mwa wanafunzi wa Shule ya Mawazo ya Prague ambao walivutiwa na kuamua kuyaendeleza mawazo ya de Courtenay na de Saussure. Huyu alikuwa ni Profesa wa Filolojia huko Viena Austria. Yeye alibainisha matawi mawili yanayoshughulkikia sauti ambapo tawi la kwanza ni lile linalojulikana kama fonetiki – kama sayansi inayoshughulikia sauti katika uumbwaji wake halisi kifiziolojia, kiakustika na kimasikizi. Lile la pili ni fonolojia kama sayansi inayoshughulikia uamilifu na utofautishaji wa sauti katika mfumo wa lugha. Yeye alilenga kuitumia nadharia ya alama ya de Saussure katika kuweka wazi zaidi dhana ya fonimu katika uwanja wa fonolojia. Trubetzkoy, tofauti na de Saussure aliamini kuwa fonetiki na fonolojia haziwezi kutenganishwa. Wanafunzi wa shule hii ya Prague waliichukulia fonimu kama kipashio changamani kinachojitokeza katika mfumo wa sauti. Ilichukuliwa kuwa ina sifa pambanuzi kadhaa ambazo zinaipa fonimu utambulisho wake. Anadai pia kuwa dhana ya upambanuzi inakwenda sambamba na dhana ya ukinzani. Ukinzani ni tofauti ya sauti inayopelekea tofauti ya maana.
[A] phonemic system presupposes a system of oppositions… But opposition is not exclusively a phonological concept, it is a logical one, and the role it plays in phonology is strongly reminiscent of its role in psychology. It is impossible to study phonological oppositions (of which phonemes are only the terms) without analyzing the concept of the opposition from the point of view of psychology and logic. (Trubetzkoy 2001[1936]:15)
Anadai kuwa fonimu moja inaweza kuwa tofauti na fonimu nyingine iwapo, na iwapo tu, kuna uhusiano wa kiukinzani baina ya fonimu hiyo na fonimu nyingine inayotofautishwa nayo. Ukinzani huu unachukualia sifa zile ambazo memba wa ukinzani hutofautiana na zile ambazo memba wake wa ukinzani huchangia. Ukinzani unaangaliwa katika uhusiano wa kiukinzani uliopo baina ya jozi za fonimu mbili au kadhaa. Mfano: /p,b/ na /t,d/ (vipasua vya midomo na vipasuo vya ufizi). Trubetzkoy huona kuwa ukinzani ndiyo kiini na msingi wa fonimu kwani fonimu zote zina uhusiano wa kiukinzani. Kwa hiyo, hatuwezi kuibaini fonimu kwa kuchunguza sifa za vijenzi vya kitamkwa kikiwa peke yake. Kitamkwa kinachunguza kifonimu kikiwa katika mfumo ili kubaini zile sifa zinazokifanya kikinzane na nyingine. Hivyo, tunaangalia ni vitamkwa gani ambavyo kitamkwa hicho kinakinzana navyo.
Trubetzkoy aliainisha aina kadhaa za ukinzani kulingana na idadi na aina ya sifa kinzani pambanuzi. Ni lazima sifa zinazounda ukinzani ziwe zile pambanuzi tu. Fonimu zenye uhusiano wa karibu huunda makundi asilia na zile zisizo na ukaribu haziundi makundi asilia. ALiona kuwa kuna uainishaji kimantiki (wa ukinzani pambanuzi) na uainishaji wa kifonolojia (wa ukinzani pambanuzi)
Uainishaji kimantiki wa ukinzani pambanuzi unaainishwa kwa misingi ya:
(a) Uhusiano wa ukinzani katika mfumo mzima wa ukinzani ambapo tunapata ukinzani kiuwili, ukinzani kiwingi, ukinzani kiwiani na ukinzani kipekee, na muundo wa mifumo ya kifonimu ambao umekitwa hapo
(b) Uhusiano wa ukinzani baina ya memba (vitamkwa) wa ukinzani ambapo tunapata ukinzani kibinafsi, Karibiani (kimwachano taratibu) na kisawa
(c) Kiwango cha nguvu ya ukinzani ambapo tunapata ukinzani imara na usio imara.
A. Uhusiano wa Ukinzani katika Mfumo mzima wa Ukinzani katika lugha fulani.
- Ukinzani kiuwili: Hutokea pale jumla ya sifa za kifonetiki zinazopatikana kwa memba wote (wawili) wa ukinzani hupatikana kwa memba hao tu. Kwa mfano: /p,b/. Katika mfumo mzima wa ukinzani hakuna tena sauti yoyote yenye sifa za [+midomo, +kipasuo, -mpumuo]. Sifa hizi hazipatikani kwa memba wengine wa ukinzani katika mfumo huo kama, [f,v,µ], [w] na [m], yaani hazina msingi mmoja wa ukinzani.
- Ukinzani kiwingi: Jumla ya sifa za kifonetiki zinazochangiwa na memba (wote) wa ukinzani na zinaweza kupatikana kwa memba hao tu au zinaweza pia kupatikana katika jozi nyingine ya ukinzani. Kwa mfano: /p,b,f,v,/ zote ni zina sifa ya midomo [ph, p, b] huwa katika ukinzani kiwingi.[ph – p] za midomo, si nazali, vipasuo na [b] pia ina sifa hizo. [p,b, ph] zote ni ]+midomo, +vipasuo, -nazali]
- Ukinzani kiwiani: Ukinzani unaotokea kwa kuhusisha mfumo mzima wa ukinzani katika lugha ambao unategemea kama uhusiano uliopo baina ya memba wa kundi moja la ukinzani unafanana na uhusiano uliopo baina ya memba wa kundi jingine la ukinzani au makundi kadhaa ya ukinzani katika mfumo huo huo. Kwa mfano: uhusiano wa ukinzani baina ya /p/ na /b/ ni wiani kwani uhusiano huo wa ukinzani unapatikana pia katika /t/ na /d/ au /k/ na /g/ [+ghuna na –ghuna: /p:b, t:d, k:g = p:t:k na b:d:g/
- Ukinzani kipweke: Unatokea pale ambao uhusiano wa ukinzani baina ya memba wa kundi fulani haufanani na ule wa memba wa kundi jingine. Kwa mfano: Katika Kiswahili /l/ na /r/ au /h/. Ukinzani wa sauti hizi haupatikani kwa memba wengine. [kitambaza, kimadende]
B. Uhusiano wa ukinzani baina ya memba (vitamkwa) wa ukinzani
- Ukinzani kibinafsi: hutokea pale ambapo memba mmoja wa ukinzani katika kundi anakuwa na sifa ya kifonetiki ambayo mwenzake hana: Mfano: /p/:/b/ (ughuna) [kuwa au kutokuwa na sifa fulani); [ph]: [p], nk.
- Ukinzani karibiani: Hutokea pale ambao memba wa ukinzani hukinzani kwa kiwango fulani tu cha sifa ile ile moja. Kwa mfano: kiwango cha sifa ya mviringo wa midomo kati ya sauti /O/ na /u/ kama kinavyojitokeza katika lugha nyingi za Kibantu kikiwemo Kiswahili.
- Ukinzani Kisawa: Ukinzani huu hutokea pale ambapo huwezi kuelezea kwamba memba mmoja wa ukinzani ana sifa fulani na mwingine hana na huwezi kusema kwamba memba wote wanatofautiana kwa viwango tu vya sifa ile ile. Kwa mfano: /t/ na /p/ au /t/ na /k/.
Hata hivyo, anadai kuwa aina za mifano katika kuelezea ukinzani hutegemeana na fonimu katika lugha husika. Kuna uhusiano wa ukinzani wa kimajumui na wa lugha maalumu.
C. Uhusiano wa Ukinzani kulingana na kiwango cha uimara wa ukinzani
- Ukinzani Imara: ni ule ambao haubadili-kibadiliki na unasemekana kuwa una nguvu. Huu ni ukinzani wa kudumu. Mfano: ukinzani kati ya /p/ na /b/, /d/ na /k/ katika Kiswahili
- Ukinzani usio Imara: Ni ule ambao unabadilika-badilika. Kwa mfano: /r/ na /l/ kuwa /d/,
Uainishaji wa Ukinzani pambanuzi Kifonolojia
Ukinzani pambanuzi wa kifonolojia unaweza kuainishwa kwa kuzingatia sifa za sauti, yaani sifa za kivokali, kikonsonanti na za kiarudhi.
- Ukinzani wa kivokali ni ule unaotokana na aina mbalimbali za kiwango cha kukosekana kwa kizuizi katika utamkaji wa sauti, viwango vya uwazi katika njia ya mkondohewa. Vokali ni sifa ya kiukinzani inayohusishwa na irabu kwa kuwa irabu ndizo zinazojenga sifa hii. Kwa mujibu wa Trubetzkoy sifa inayofanya kitamkwa kiitwe irabu ni kule kutokuwepo kwa kizuizi chochote katika mkondohewa katika utolewaji wake. Mfano: /a,i,u,/ nk
- Ukinzani wa sifa za kikonsonanti unahusishwa na konsonanti. Kinachofanya kitamkwa kiitwe konsonanti ni kule kuwepo kwa kizuizi katika mkondohewa wakati wa utamkaji wake.
- Ukinzani wa sifa za kiarudhi: huhusishwa na vipashio vya kimuziki wakati wa utamkaji. Vipashio kama vile kiimbo, mkazo, toni, nk
Trubetzkoy anadai pia kuwa tofauti za kifonimu zinahusiana moja kwa moja na tofauti za kimaana. De Saussure aliichukulia alama kama wiani, hasi na kinzani kwa maana kwamba ili uitofautishe alama moja na nyingine basi angalia jinsi inavyokinzana na nyingine, yaani angalia kile ambacho haina (dhana au kitu kilicho kinyume chake). Trubetzkoy yeye anaitofautisha fonimu moja na nyingine kwa kuangalia sifa za kifonetiki kwani anadai kuwa fonimu ni mkusanyiko wa sifa za kisauti ambazo zinaijenga na wala si dhahania kama ilivyo alama kwa mtazamo wa de Saussure. Anadai pia kuwa fonimu inajipambanua na haina sifa za ziada na ina kiwango kikubwa cha muundo ndani: Kwa mfano; /uingi/ [wiNgi], katika umbo hili fonimu iangalie umbo la ndani kwa kiwango kikubwa. (Hapa panahitaji mjadala)
Trubetzkoy anaaamini kuwa fonimu si dhana dhahania pekee bali pia inaweza kubainishwa kwa sifa za kifonetiki. Hivyo, aliona kuwa umbo la ndani na umbo la nje ni sawa sawa na kile kinachotumika kutofautisha uwakilishi wa kifonetiki ndicho hutumika kutofautisha uwakilishi wa kifonolojia. Hii ni dosari kwani kuna baadhi ya maumbo ya nje ambayo ni tofauti na maumbo ya ndani.
2.3.2 Daniel Jones (1881 – 1967)
Alizaliwa mwaka 1881 huko London. Yeye aliitazama fonimu kama kipengele chenye sura mbili, ile ya kudhihirika kimatamshi na ile ya kudhihirika kisaikolojia. Kisaikolojia huitazama fonimu kama vijenzi vya kisaikolojia ambapo kisaikolojia anaifasili fonimu kama sauti ya usemaji ambayo taswira yake inaonekana akilini na ambayo imekusudiwa kutolewa katika mchakato wa usemaji. Kinachotamkwa ni kiwakilishi cha picha iliyoko akilini au inatofautiana kidogo na ile picha ya akilini kulingana na mazingira ya kifonetiki. Katika kuielezea fonimu ni muhimu kuyazingatia mambo kama akili, hisi, mawazo, picha na vitu vingine vya kisaikolojia. Hata hivyo si wakati wote kile kilichomo akilini kinaweza kutolewa kama kilivyo katika matamshi. Pia anadai kuwa unapotaka kuanza kuiweka lugha yako katika maandishi kwanza uandike kifonemiki. Kimatamshi aliifasili fonimu kama familia ya sauti zitamkwazo ambazo huhesabiwa kama kitu kimoja (Jones 1957 [1973]:90,191). Kwa hiyo kwake yeye sura ya kisaikolojia na kimatamshi zote ni za muhimu ingwa yeye alipendelea zaidi fasili ile ya kimatamshi (inayoendana na utamkaji) na kuona kuwa ni ya muhimu katika ujifunzaji wa lugha kuliko ile ya kisaikolojia. Kutokana na kuitilia maanani fasili hii aliifasili upya fonimu kwa kusema kuwa ni “familia ya sauti za kusemwa, katika lugha fulani maalumu, ambazo zinachuliwa katika uumbwaji wake kama sauti moja na zinazofanana au zinazohusiana ambapo kila memba wa familia hiyo (alofoni) hutumika kwa kudhibitiwa na mazingira ya utokeaji ya kifonetiki. Hii ina maana kwamba mazingira ya kifonetiki ya utokeaji wake hauruhusu memba yeyote aliyemo katika familia hiyo kutokea katika la mazingira yale yale ya kifonetiki ambamo memba mwingine hutokea”. Kwa hiyo fonimu ni familia ya sauti inayotumika katika lugha fulani na alofoni zake. Adai kuwa ni vigumu kusema kwamba lugha fulani ina fonimu fulani kwani fonimu butegemea mazingira yanayoizunguka. Kuna sauti katika lugha zinatamkwa lakini hazimo katika orodha ya fonimu na bado wazawa wanaelewana kwa kutotilia maanani tofauti hizo. Kwa mfano: [ph] na [p] katika Kiswahili, [a)] na [a], nk. Ili kutofautisha sauti za kusemwa katika lugha na fonimu ni lazima kwamba fonimu ziwe zina kikomo na zisizobadilishana mazingira ya utokeaji wake. Fonimu ni ni suati ya kawaida ya lugha pamoja na vibadala vyake vyote vya kiajali (alofoni). Mfano: /u/ na /u9/, /a:/ na /a/, nk. Alofoni kwake yeye hujulikana na memba wa fonimu moja. Sauti ya kusemwa ni ni sauti yenye ukomo wa thamni ya kifonetiki inayozalishwa na alasauti. Kila sauti ya kusemwa (foni) huwa si badilikaji katika utokeaji wake. Lugha nyigni ina sauti nyingi sana za namna hii zinazojibainisha ila si lazima kila moja iwe na alama yake ya kifonetiki bali huangukia katika kundi moja la sauti liitwalo fonimu. (Fonimu ni kundi la sauti zinazohusina kiuumbwaji katika lugha fulani ambazo zinatumika katika mfuatano wa matamshi kiasi kwamba hakuna sauti mojawapo itatokea katika mazingira ambamo nyenziye inaweza kutokea). Sauti za kusemwa (foni) zilizo katika fonimu moja haziwezi kutofautisha maana. Jones hakutaka kuhusisha fonimu na maana kwani alisema fonimu zinahusika sana na sifa za kiutamkaji. Foni tofauti katika fonimu moja huita alofoni na unukuzi wake ni wa kialofoni.
Massamba (2012) anasema kusema kuwa fonimu ni familia ya sauti ambayo inatokea katika mazingira ya ukamilishani baina ya fonimu moja na nyingine ina maana haidhihiriki wazi kimatamshi. Kinachodhirika katika matamshi ni memba wake. Ule umoja unaowaweka memba katika familia moja ndio ujengao dhana ya fonimu. Memba mmoja wa familia moja hawezi kutokea katika mazingira yale yale ya kifonetiki ambamo memba mmoja amejitokeza. Kitu cha msingi ni si kuitazama fonimu katika upambanuzi wake bali ni kuangalia msambao wa utokeaji wa memba wake katika mazingira tofauti tofauti ya kifonetiki. Memba wa familia moja ya sauti ni lazima watokee katika msambao kamilishani au mgawanyo wa kimtoano. Kwa mfano:
Fonimu: [b, b̰ , ɓ, ɓ̥,bw, by, nk]. Kwa hiyo, memba mmoja akitokea mwingine hatokei. Katika nlugha ya Kiswahili memba anayetokea katika msambao wa maneno ya Kiswahili ni /b/ tu.
2.3.3 Mtazamo wa Edward Sapir (1884 – 1939)
Alizaliwa Ujerumani na aliishi Marekani. Alikuwa Mwamerika wa kwanza kuzungumzia suala la fonemiki (Aderson 1974:20). Alianza kwa kusema kuwa mzungumzaji wa lugha hutambua kuwa lugha yake ina idadi ndogo tu ya sauti pambanuzi na kwamba zipo sauti katika lugha nyingine ngeni zinazofanana na sauti za lugha yake ingawa hutumika tofauti (Sapir 1921-42,-43). Lakini pia kutokana na kauli yake tunaona kwamba aliona kuwa lugha zote huchota sauti kutoka katika bohari moja la sauti na kila lugha ina idadi fulani ya sauti ambazo huzitumia tofauti na lugha nyingine. Kwa mfano: Mzungumzaji wa Kiswahili anajua kuwa ana sauti chache na baadhi ya sauti zake nyingine zinapatikana katika lugha nyingine lakini zinavyotumika katika lugha nyingine ni tofauti na zinavyotumika katika Kiswahili.
Vilevile huiona fonimu kama mfumo wa ndani ya akili ya mzungumzaji na ni kipengele cha kisaikolojia. Fonimu haina msingi katika sifa za kifonetiki za kitamkwa bali kipashio bayana kabisa chenye thamani ya kisaikolojia kinapolinganishwa na vitamkwa vingine katika mfumo huo kilicho katika akili ya mzawa na ambacho ni umbo la ndani la kitamkwa kinachojidhihirisha halisi kimatamshi kupitia michakato ya utoaji sauti ya lugha. Aliiona fonimu pia kuwa si dhahania bali fonimu za lugha zilichaguliwa kutoka katika vitamkwa vya kifonetiki vinavyojitokeza katika lugha hiyo. Kwa hiyo, bohari la sauti la lugha huweza kugawanyika katika makundi mawili: Fonimu na vibadala vyake. Baadhi ya sauti ni za msingi ambazo huunda fonimu zinazojitokeza katika udhihirisho wa kifonetiki wa kisaikolojia na katika utamkaji halisi na nyingine hazitokei katika mfumo wa fonimu ila hujitokeza kifonetiki katika mazingira maalumu ambamo zile za msingi hazijitokezi. Mfano: [n,N,,µ], fonimu ya msingi ni /n/.
Kwake, sauti hubeba fonimu, hivyo sauti ni kidhihirisho cha fonimu. Sauti huwa katika mtiririko wa kiakili wa vipengele vya kifonetiki ambao husikika kutoka katika kusudi la ndani ya akili. Hivyo huona lugha ni ya kisaikolojia kabisa na fonimu ni tukio la kisaikolojia.
Sapir huona kuwa fonimu si kitu kinachohusishwa na sifa za kifonetiki bali hubainishwa tu na vipengele vya kifonetiki ambavyo vina thamani ya kisaikolojia kwa kupitia uhusiano wake na maumbo mengine katika mfumo huo na msingi wa vipandesauti vya kifonetiki kupitia muundo wa sauti wa lugha (husika). Fonimu ni lazima ilinganishwe na sauti nyingine katika mfumo huo. Ni vigumu kuelewa saikolojia ya mchakato wa kifonetiki mpaka uelewe ruwaza nzima/mfumo wa sauti za lugha husika. Kwa mfano: ni lini sauti [], [µ], [N] zinajitokeza katika lugha ya Kiswahili. Ruwaza hiyo imegawanyika katika kundi la sauti zinazozalishwa na alasauti lakini hazina maana katika lugha hiyo na zile zenye thamani ya kiisimu ambazo ni za ndani ambazo huzipata katika akili yake kupitia kujifunza kwa jamii (fonimu). Hivyo Sapir anabainisha viwango viwili vya sauti yaani cha kifonetiki na cha kisaikolojia. Fonimu si ya kinasibu bali huchukuliwa katika vipande sauti vya kifonetiki vilivyopo katika lugha. Kwa kusema kuwa fonimu ni tukio la kisaikolojia Sapir hamaanishi kuwa ni ya kuzaliwa nayo bali mtu huikuta katika jamii yake na hujifunza. Hivyo basi husisitiza kuwa lugha ina asili ya kijamii kama shughuli ya kijamii ya binadamu.
2.3.4 Mtazamo wa Leonard Bloomfield (1887 – 1949)
Alizaliwa Chicago Marekani. Alishughulikia masuala ya lugha kisayansi na kimpangilio maalumu (kijarabati). Hudai kuwa kwa mtazamo wa mwanafizikia au mwanafiziolojia kunaweza kuwa na sauti nyingi za usemaji zisizo na ukomo ambazo huweza kutamkwa lakini ni sehemu ndogo tu ya hizo sifa huhusishwa na maana na zilizo muhimu kwa mawasiliano. Kwa hiyo, huiona fonimu kuwa inahusishwa na maana. Hivyo ni ile tu sehemu yenye maana katika tamko ndiyo huitambulisha fonimu. Anasema kuwa, kwa kuwa tunaweza kutambua sifa pambanuzi za usemaji kwa kuangalia maana tu, hatuwezi kuzitambua [sifa hizo] kwa kutumia vigezo vya kifonetiki peke yake. Hii inamaanisha kuwa ni sifa maanifu tu sauti katika usemaji ndiyo inayotufanya tuitambue sauti hiyo kuwa fonimu. Ufanyaji kazi wa lugha unategemeana na tabia ya wazawa iliyokubalika ya kutenga sifa fulani za sauti na kuzipuuza nyingine. SIfa zisizofungamana na maana hazina umuhimu katika mawasiliano. Katika kila jamiilugha baadhi ya matamshi yanafanana katika umbo na maana. Pia sifa bainifu na zisizobainifu za sauti hutegemeana na mazoea ya watumiaji, yaani kila lugha huwa na sauti zake bainifu. Fonimu hutambulikana kwa kuzitambua sauti za lugha husika na kuelewa jinsi zinavyotumiwa na wazungumzaji ili kuleta maana (zinavyofanya kazi katika mfumo). Bloomfield aliifasili fonimu kuwa ni kipande kidogo kabisa cha sifa bainifu ya sauti (Language 1933:79). Ametoa fasili hii kwa kigezo cha sifa bainifu/pambanuzi. Jozi ya mlinganuo finyu hutumika kubainisha fonimu.
Zifuatazo ni sifa za sifa bainifu/pambanuzi na zisizobainifu/pambanuzi za Bloomfield kama zilivyofupishwa na Dinneen (1967:253).
1. Sifa bainifu huwa katika mafungu na kila moja ya mafungu hayo huitwa fonimu.
2. Haiwezekani kutoa sifa bainifu bila kuwa na sifa zisobainifu.
3. Fonimu za lugha si sauti bali ni zile sifa za sauti ambazo mzungumzaji amejifunza kuzizalisha na kuzitambua. Kwa mfano: [+ghuna, +kaakaa laini, -fuliz],
4. Sifa zisizobainifu ni nyingi na zile bainifu ni chache na hazibadilikibadiliki (zina kikomo). Hii ndiyo maana inasemekana kuwa kila lugha inachota sehemu tu ya sauti zikitazamwa na zile zilizopo katika bohari kuu la sauti.
5. Wazungumzaji wasio wazawa wanaozitamka sifa bainifu za lugha ngeni hujitahidi waeleweke lakini huzitamka kwa lafudhi tofauti kutokana na makosa ya mtawanyo wa sifa zisizobainifu. Huingiza sifa zao ambazo si bainifu katika lugha watamkayo. Kwa mfano: Kiswahili: Yaani wale watu watakaokuja (tamka kifipa, kiha, kisukuma, kikinga, nk (viarudhi) ) au table, question, pronounciation [pr«nUnsieiSn]
6. Sifa zisobainifu hutokea katika mtawanyo wa aina yoyote ile lakini huwa na mpaka katika mabadiliko yake.
7. Kwa kuwa kila lugha ina fonimu zake, zinazotokana na sifa bainifu tofauti, wazungumzaji wageni hutamka (sifa bainifu) fonimu za lugha zao za awali zinazoonekana kufanana na za lugha ngeni watamkayo lakini huwa wanakiuka utamkaji wa (sifa bainifu) fonimu za lugha hiyo ngeni wanayojaribu kutamka. Hii ni kwa sababu kila lugha ina sifa zake bainifu. Mfano Wazungumzaji wengi wa Kiswahili hawawezi kutamka Irabu /«/, /U/, /E/, /U/, /Ï/: father, first, bird, but, not (pot),
8. Kinachosaidia mawasiliano baina ya mgeni na mzawa ni jitihada za mzawa kujaribu kufidia matamshi yenye makosa ya msemaji mgeni (kuzibainisha sifa bainifu za lugha yake katika akili yake). Kwa mfano: Mzungu; ugali, kunywa, gift,
9. Ugumu huja pale ambapo fonimu mbili au tatu za lugha ngeni hufanana na fonimu za lugha ya mzawa wa lugha fulani.
10. Ugumu huja zaidi kama lugha ya kigeni inatumia sifa bainifu ambazo hazitumiki katika lugha ya mzawa. Waswahili wanavyoingiza sifa zao katika Kiingereza na kinyume chake. Advertisement /«d’vä:tIsm«nt/ (Bre)., garage /gÏraZ/ au /g«ra:dz/
Pia alianisha fonimu katika aina mbalimbali; mfano:
1. Fonimu msingi sahili: kama /p/, /b/, /d/, n.k.
2. Fonimu changamani – hutokea pale ambapo fonimu moja moja zinapoungana na kuwa kama kitu kimoja. Kwa mfano Irabu unganifu - / aI / na [ä], [N], []
3. Fonimu za upili hutokana pia na muunganiko wa fonimu mbili au zaidi (vipambasauti pia huwa katika kundi hili kwa mujibu wa Bloomfield). Kwa mfano: nd, ng, mb (ndoo, nguo, mboga, unzali, toni)
Pia aliainisha fonimu zenye sauti ya ukelele (vipasuo, kimadende na vikwamizi) na sauti za kimuziki (nazali, vitambaza na Irabu).
Kwa hiyo, basi Bloomfield anasisitiza zaidi ubainifu wa fonimu unaodhihirika katika sifa yake ya kutofautisha maana na upekee unaotokea katika kuunganika kwake kuunda kipashio kikubwa. Sifa za kifonetiki zina umuhimu katika kusaidia kuipa fonimu utambulisho wake (utofauti wa sifa za sauti zinazosikika). Anadai pia kuwa fonimu zikiwa chache katika mfumo basi kunakuwa na nafasi kubwa ya kuwa na sifa zisizobainifu. Ni rahisi mtu ambaye lugha yake ina fonimu nyingi kuzisikia sauti za lugha yake katika lugha nyingine lakini zikawa hazina maana katika lugha hiyo. Kwa mfano: Mtang’ata anaweza kuusikia mpumuo kwa msemaji wa Kiswahili sanifu, mwingine unazali, ukipasuo ndani, nk.
Kwake yeye fonimu ni kiashirio dhahiri cha usemaji na kipengele kinachoweza kuchukuliwa kuwa ni dhahania ni ule mfumo ambamo fonimu huwamo. Yaani ule uwezo wake wa kutofautisha maana ni dhahania na ni muhimu katika kuibainisha fonimu kwa mujibu wa Bloomfield.
***Linganisha na kulinganua mawazo ya Trubetzkoy na Bloomfield katika kuielezea dhana ya fonimu.