SEC-LUGHA-TAFSIRI NA UKALIMANI
TAFSIRI NA UKALIMANI
Tafsiri
ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo
yaliyo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa bila
kubadilisha maana ya ujumbe.
DHANA MBALIMBALI
Ø Uhawilishaji – ni uhawilishaji wa ujumbe au mawazo
kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine kwa njia ya maandishi au mazungumzo.
Ø Mfasiri – ni mtu yeyote anayejishughulisha au
kufanya tafsiri. Ni mtu mwenye taaluma au ujuzi wa kutafsiri na ambaye
anajishughulisha na shughuli hizo.
Ø Matini – ni wazo au mfululizo wa mawazo wenye
utoshelevu wa kimaana na unaohitaji kutafsiriwa. Matini yanaweza kuwa neno,
kirai, kishazi, sentensi au aya.
AINA ZA MATINI.
a)
Matini Chanzi (M.C)
–
ni matini iliyo katika lugha yake ya awali kabla ya haijatafsiriwa.
b)
Matini Lengwa (M.L)
–
ni matini iliyo tafsiriwa kutoka lugha yake ya awali.
c)
Mtini Elezi – ni matini ambayo
huegemea upande wa mwandishi.Mfano matini za kisheria,
maandishi binafsi kama vile shajara
(diary),wasia, nk.
d)
Matini Arifu – ni matini
ambayo hulenga kutoa taarifa au maarifa kuhusu jambo fulani.
Mfano vitabu vya
taaluma na masomo mbalimbali. Nk.
(e)
Matini Amili –
ni matini ambazo huegemea upande wa hadhira,mwandishi huchoochea hisia
za wasomaji na
kuwafanya watende kama ambavyo yeye mwandishi anataka wafanye au watende. Mfano
kadi au barua za mwaliko, matangazo mbalimbali kama vile ya vipodozi, jeshi nk.
DHANA
MBALIMBALI
Ø Lugha Chanzi – ni lugha iliyotumika kuandika
matini chanzi.
Ø Lugha lengwa – ni lugha inayotumika kufanyia
tafsiri au ni lugha inayotumika kuandikia matni lengwa.
Ø Kutathmini tafsiri – ni kitendo cha
kusoma kwa matini iliyo tafsiriwa na kuitolea hukuuamu juu ya ubora na udhaifu
wake. Wakati mwingine hujulikana kama kuhakiki tafsiri.
Ø Tafsiri pana - -ni tafsiri inayozingatia maana na
mtazamo wa kiujumla kuhusu jambo au dhana inayozungumziwa wakati katika matini
chanzi jambo au dhana hiyo imeelezwa katika umahususi wake. Mfano kutafsiri
neno “kisamvu” kama vegetable ni
tafsiri pana kwani imetazama katika ujumla ikiwa kisamvu ni aina fulani tu ya
vegetable.
Ø Tafsiri Finyu – ni tafsiri ambayo jambo au dhana
hufafanuliwa katika misingi ya umahususi wake wakati katika matini chanzi
imeelezwa kiujumla jumla. Au ni tafsiri inayotoa maana finyu zaidi kutoka maana
inayolingana na matini chanzi. Mfano kutafsiri neno ‘filling station” kama “sheli”
ni tafsiri finyu kwa sababu Sheli ni
aina moja tu ya kituo cha mafuta.
Ø Tafsiri mbovu/ tenge -ni tafsiri
ambayo imepotoshwa kiasi kwamba maana inayokusudiwa katika matini chanzi ni
tofauti kabisa na maana inayotolewa katika matini hiyo. Tafsiri tenge huweza
kusababishwa na mambo kadhaa kama vile ;-
·
Kutojua
maana halisi ya neno lililo tumika katika matini chanzi.
·
Tofauti
za kiutamaduni kati ya lugha chanzi na lugha lengwa.Mfano kutafsiri neno “Rarely” badala ya often ni tafsiri.
Kutafsiri neno corporal punishment
kama adhabu ya viboko badala ya adhabu ya kifo kisheria ni tafsiri tenge.
Ø
Tafsiri rejeshi
– ni
mchakato wa kutafsiri matini ambayo tayari imeshatafsiriwa kutoka lugha fulani
na kuirejesha tena katika lugha chanzi kwa lengo la kuitathmini tafsiri hiyo.
Mfano Ikiwa tafsiri ilifanywa kutoka Kiswahili kwenda kiingereza basi
tunapoitathmini tafsiri hiyo kwa kutumia tafsiri rejeshi tunaitafsiri tena toka
Kiingereza kwenda lugha ya kswahili.
Ø
Tafsiri sahihi – ni tafsiri
ambayo kwa kiasi kikubwa ina kubalika na kuvumilika kwa sababu muundo na
maudhui ya matini chanzi vimezingatiwa katika matini lengwa.
UMUHIMU/
DHIMA YA TAFSIRI
Ø
Ni
njia ya mawasiliano inayofanya kazi kati ya watu au jamii mbili zinazotumia
lugha tofauti. Mfano Kiswahili na Kiingereza.
Ø
Ni
nyenzo ya kueneza utamaduni. Mfano kupitia dini,vitabu vimetafsiriwa kwa lugha
mbalimbali.Mfano I will mery when I want
– Kiingereza Nitaoa nitakapotaka –
Kiswahili
Ø
Ni
mbinu ya kujifunza lugha – mfasiri anapofanya kazi ya kutafsiri matini
mbalimbali hukutana na changamoto mbalimbali na anapofaya jitihada za kutatua
matatizo hayo hujikuta anajifunza lugha.
Ø
Tafsiri
ni kiliwazo cha mfasiri – tafsiri humfanya mfasiri afurahi,aridhike na
aburudike hasa anapopata suluhisho la changamoto za kutafsiri zilizokuwa zinamkabiri.
Ø
Tafsiri
ni kazi au ajira kwani umpatia mtu kipato.
SIFA
ZA MFASIRI BORA
Ø
Awe
mahari wa lugha husika yaani azifahamu lugha zote mbili.
Ø
Awe
mjuzi wa tekinolojia habari na mawasiliano (Tehama) kwasababu baadhi ya
kazi
atalamika kutumia vifaa mbalimbali kama vile Tanakilishi (kompyuta).
Ø
Afahamu
vizuri watu jamii na utamaduni wao.
Ø
Apende
kujisomea na ajiendeleze kulingana na mabadiliko ya jamii yaani ajue vitu
vingi.
Ø
Afahamiane
na watu wengi wa fani au sekta mbalimbali kwa kazi atakazofanya ni za watu
mbalimbali na tofauti tofauti.
Ø
Ajue
misingi ya tafsiri.
Ø
Awe
na misamiati ya kutosha na ajue kanuni au sheria za lugha husika.
MAADILI
YA MFASIRI
Ø
Awe
mwaminifu kwa wateja wake na matini aliyopewa.Mfano katika itikadi.Mfano
mfasiri si mlevi kabisa lakini analetewa matini inayosifia pombe,hapaswi
kubadili chochote kutokana nayeye kutopenda pombe bali anapaswa kuitasiri kama
ilivyo,huo ndo uaminifu wa mfasiri.
Ø
Awe
na bidii katika kazi yake ili afanye kazi kwa wakati na awarudishie wateja wake
kwa wakati bila kwazo au mgogoro wowote na wateja wake,Hii itamsaidia mfasiri
aendelee kuaminiwa na kuletewa kazi za kutafsiri.
Ø
Awe
nadhifu wa moyo na muonekano yaani katika mavazi,kauli kwa wateja n.k ili
aendelee kuaminiwa na wateja wake.
Ø
Anapaswa
kuzingatia taratibu za kazi yake.Mfano makubaliano na mteja wake yanapaswa yawe
kimaandishi na mkataba utaje jina la mteja,jina la mfasiri, aina ya kazi nk.
Ø
Awe
na ushirikiano na watafasiri wenzake pamoja na watu mbalimbali wa sekta
nyingine.
Ø
Aepuke
vishawishi au asiwe na tamaa.Anapaswa kuwa na msimamo yaani asijipendekeze kwa
mteja wala asijishushe Mfano kupunguza bei.
MAMBO YA
KUZINGATIA WAKATI WA UCHAMBUZI WA MATINI.
Uchambuzi
wa matini - ni kusoma matini husika na
kuielewa kabla ya kuanza kuitafsiri.Mambo ya kuzingatia wakati wa uchambuzi wa
matini ni kama yafuatayo;-
Ø
Kubaini
lengo la matini yaani mfasiri anapaswa abaini lengo la matini chanzi.
Ø
Kubaini
lengo la kufasiri.Mfasiri ni lazima ajue lengo mahususi la tafsiri yake.Je
anataka msomaji apate athari inayolingana na ile ya wasomaji wa matini chanzi.
Ø
Kubaini
wasomaji na umbo la matini lengwa -
mfasri hana budi kufahamu hadhira ya matiini chanzi na abaini hadhira mahususi
ya matini lengwa yake.Mfano elimu,umri na tabia nk. Kwa upande wa umbo mfasiri
afahamu tafsiri hiyo itasomwa kama kitabu, jarida ama gazeti n.k.
Ø
Kubaini
mtindo wa matini chanzi-mfasiri anapaswa abaini mtindo wa matini chanzi kwani
mtindo wa matini chanzi unapaswa ulingane na ule wa matini chanzi mfano ikiwa
matini chanzi ni shairi basi hata matini lengwa inapaswa iwe shairi n.k.
Ø
Kubaini
ubora na mamlaka ya matini chanzi–ubora na mamlaka ya matini chanzi hubainika
kwa kuangalia lengo la maadhishi na mahitaji ya matini aliyoandika.Mamlaka ya
matini chanzi hudhihirika kwa kangalia iwapo matini chanzi imeandikwa vizuri
pamoja na hadhi ya mwandishi wake.Mfano ikiwa ni matini ya Kiswahili basi
iandikwe na mwanasheria gwiji.
Ø
Usomaji
wa matini mara yamwisho - mfasiri asome
mala ya mwisho matini chanzi huku akipigia mstari istilahi na maneno muhimu ya
matini hiyo ili yasisahaulike kuzingatiwa kwa umakini wakati wa kutafsiri.
VIPENGELE
VYA UCHAMBUZI WA MATINI.
Kuna vipengele vikuu vitatu ambapo kila
kipengele kina hatua kadhaa ndogondogo kama ifuatavyo:-
( a ) Kusoma matini nzima au yoe -faida
au vipengele vyake vidogovidogo ni kama vile
Ø
Husaidia
kuandaa marejeleo muafaka kama vile kamusi ya lugha ya kwanza na yapili.
Ø
Husaidia
kuandaa orodha ya istilahi na visawe
Ø
Kugawa
Sehemu au vipengele miongoni mwa wafasiri hasa kama matini ni kubwa.
( b ) Kuchambua matini yenyewe –
uchambuzi wa matini hulenga kupata sifa bunifu za matini
husika.Kipengele hiki kina hatua
tano kama vile:-
Ø
Kubaini
lengo la mwandishi, kama vile kubeza,kusifu,kukweza,kukashifu au kutoegemea upande
wowote katika uandishi,mwandishi anaweza kuwa na mitazamo miwili au zaidi.
·
Mtazamo
chanya kwa mtendwa. Mfano yanga yaichabanga simba.Mwandishi huyu
ametumia neno chabanga ni mtazamo hasi yaani au kwani amefurahia samba
kufungwa.
·
Mtazamo
chanya kwa mtenda.Mfano yanga yafuta uteja kwa Simba. Mwandishi huyu anaonesha anafurahia yanga kuifunga
simba.
·
Mtazamo
wa kati– mfano yanga yaifunga simba 3 kwa 0 (sifuri),Mwandishi huyu haoneshi
kuegemea upande wowote.
Ø
Kubaini
lengo la mfasiri au mteja– mfasiri ajiulize kwanini anataka kutafsiri matini
husika?.Na kwanini mteja wake anataka itafsiriwe?.Hivyo mfasiri anapaswa
kuepuka upendeleo au kuegemea upande mmoja badala yake awe na msimamo au
mtazamo wa katikati.
Ø
Kubaini
hadhira na umbo la matini – mfasiri ajiulize maswali kama vile: hii ni aina
gani ya matini? Aina hii ya matini hutafsirika vizuri kwa njia ya aina gani?,
Hadhira lengwa ya zao la tafsiri ni ipi? Na inalengo
gani?,Mfano Elimu, Umri, Mahali wanapo ishi nk. Zao la tafsiri iwe
katika umbo gani? Mfano Ripoti, tasirifu,
kiatabu nk.
Ø
Kubaini
mtindo wa matini – ni muhimu sana mtindo wa
matini chanzi ujitokeze kwenye
matini lengwa yaani tafsiri yake. Mfano monolojia, Dayalojia, Hadithi, lugha za
mitaani, mitindo ya kidini nk. Mitindo hii ikiwa umetumiwa katika matini chanzi
inapaswa ijitokeze pia katika matini lengwa.
Ø
Kubaini
ubora na mamlaka ya matini chanzi –ubora wa matini chanzi hutokana na
kuzingatia vipengele mbalimbali vya kiisimu vya lugha.Mamlaka ya matini chanzi
hutokana na hadhi na ubobevu wa maadishi katika taaluma husika.Mfano matini ya
kisheria ni vyema iandikwe na mwanasheria gwiji maana yake mwanasheria mbobevu.
( c).
Kusoma matini kwa mara ya mwisho – katika kipengele hiki mfasiri asome
tena matini chanzi kutoa taswira au kuweka alama maneno au mambo muhimu katika
matini hiyo, baadhi ya mambo ay maneno muhimu yanayo paswa kuwekewa alama
ni :- Majina mahususi ya watu, Sehemu,
mwaka nk. Maneno, virai au sentensi ambazo hazitafsiriki kiurahisi.
HATUA/
MCHAKATO WA KUTAFSIRI MATINI
Ili kupata matini lengwa inayoeleweka na
kukubalika kwa hadhira ni lazima mfasiri apitie hatua mbalimbali katika
kutafsiri. Hatua hizo ni kama zifuatazo:-
1.Maandalizi – katika hatua
hii mfasiri anapaswa kusoma matini chanzi mara kadhaa ili kujilidhisha kuhusu
maudhui yake,mtindo wake na kuziwekea alama maalum Sehemu au vipengele
vinavyopaswa kupewa kipaumbele.Vilevile chunguza usuri wa matini chanzi,
historia ya mwandishi,utamaduni wake,mazingira ya uandishi ,malengo yake na
hadhira ya matini hiyo kama mfasiri ni mgeni zaidi katika utamaduni huo
inapaswa kujisomea zaidi kuhusu utamaduni huo.Usuri huendana na uchambuzi wa
vipengele vya kiisimu ambapo mfasiri huandika msamiati na istilahi, maneno ya
kiutamaduni na Sehemu ngumu kueleweka ili azifanyie kazi.
2.Uchambuzi
–
katika hatua hii mfasiri hufanyia kazi yale aliyobaini ktika hatua ya
Maandalizi. Hatafuta visawe vya msamiati na istirai ngumu au ngeni kwa kutumia
marejeo mbalimbali kama vile Ensaikolopidia na kamusi. Inashauliwa kuwa mfasiri
awe na kompyuta au daftari au faili kwa ajili ya kutunzia msamiati au istirahi
zitakazo tumika
.
3.Uhawilishaji – katika hatua
hii mfasiri huhawilisha taarifa kutoka kwenye matini chanzi kwenda kwenye
matini lengwa.Mfasiri anatakiwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa isipokuwa
anapotumia tafsiri ya neno kwa neno.
4.Kusawidi
rasimu ya kwanza
–Baada ya kazi ya tafsiri inayo patikana baada ya uhawishaji wa visawe kutoka
lugha chanzi kwenda lugha lengwa kukamilika ni rasmu ya kwanza ya tafsiri.
Rasimu ya kwanza ya tafsiri iliyo sawidiwa inaweza kuwa na dosari kadhaa kwa
hiyo haifai kupelekwa kwa mteja au hadhira lengwa kama ilivyo,hivyo basi
mfasiri hulazimika kuidurusu rasimu hiyo ili kuondoa dosari
5.Udurusu
wa rasimu ya kwanza
– Baada ya rasimu ya kwanza kukamilika lazima ipitiwe tena na kurekebishwa au
kudurusiwa na mfasiri hupata fursa ya kwanza ya kuitathimini na kuifanyia
marekebisho tafsiri yake mwenyewe. Kazi ya kudurusu haipaswi kufanya haraka.Hatua
hii ya kudurusu huhusisha shughuli zifuatazo:-
Ø
Kusahihisha
makosa ya kisarufi na miundo isyoeleweka vizuri.
Ø
Kuonesha
sehemu zenye tafsiri ya mzunguko na zenye
matumizi
Ø
Kurekebisha
sehemu zenye muunganiko mbaya au tafsiri tenge zinazozuia mtiririko mzuri wa matini.
Ø
Kuhakiki
usahihi na kukubalika kwa maana zinazowasilishwa katika matini lengwa.Katika
shughuli hii tunaangalia kama kuna mambo yameongezwa, yamepunguzwa,yamepotoshwa
au kubadilishwa.
Ø
Kuhakiki
kukubalika kwa lugha iliyotumika katika tafsiri kwa kuzingatia umbo lililo
tumika kuwasilisha matini lengwa na mada ya matini chanzi.
Ø
Kama
iwapo mada au ujumbe mkuu wa matini chanzi unajitokeza waziwazi katika matini
lengwa.
6. Kusomwa kwa rasimu ya pili na mtu mwingine -Msomaji wa
rasimu ya pili anaweza kuwa mfasiri mwingine au mhakiki au muhariri wa tafsiri,pia
anaweza kuwa mteja wa tafsiri inayohusika au mtu mwingine yeyote mwenye uwanja
uliotafsiriwa.
7.Kusawiri
rasimu ya mwisho–katika
hatua hii mfasiri hufanyia kazi maana na mapendekezo ya msomaji ambaye amempa
kazi yake matokeo ya kufanyia kazi maoni hayo humwezesha kuandhika rasimu nzuri
ya mwisho ambayo ndio humfikia hadhira.
MBINU
/ AINA/ NJIA ZA KUTAFSIRI
Katika kutafsiri matini kuna njia, aina,
au mbinu nne kama zifuatazo:-
A.
TAFSIRI YA NENO
KWA NENO
–Ni mbinu ya tafsiri ambayo maneno yake hutafsiriwa kiupeke upeke kwa
kuzingatia maana za msingi za lugha chanzi lakini kwa kufuata sarufi hasa
sintaksia ya lugha lengwa.Mfano
i)
Kiingereza => pull up your socks
Vuta
juu yako soksi
Kiswahili => vuta socks
zako juu
ii)
Kiswahili => mtoto wa
nyoka ni nyoka, Kiingereza => A child of snake is snake.
FAIDA
YA MBINU HII
Ø
Husaidia
kujua muundo wa kisarufi wa lugha chanzi
Ø
Hutumiwa
na wanaisimu katika kuchambua sarufi ya lugha mbalimbali.
UDHAIFU
WA MBINU HII
Ø
Mbinu
hii inashindwa kufikisha ujumbe wa lugha chanzi katika lugha lengwa ya sarufi
kwa sababu kunakuwa na upotoshaji wa maana ya lugha chanzi latika lugha lengwa.
Ø
Misemo
hutafsiriwa kwa makosa.
B. TAFSIRI YA KISEMANTIKI
Ni mbinu au njia ya tafsiri ambayo
huegemea zaidi kwa mwandishi wa matini chanzi ambapo maana na vipengele
vidogovidogo hutiliwa maanani. Aina hii ya tafsiri hufanya kazi ya tafsiri iwe
na taarifa nyingi.Mara nyingi tafsiri ya kisemantiki hujali zaidi maana na
muundo wa matini chanzi. Mfano:
Kiingereza
:Tanzania
electric suppy company ltd,
Kiswahili
:Shirika
la ugavi wa umeme Tanzania.
Kiingereza: where is a
purpose, there is no failure.
Kiswahili: palipo na nia, hapana kushindwa.
Kiswahili: hapa kazi tu.
Kiingereza: here job only
Mifano hiyo hapo juu inaonesha kwamba
kila neno katika matini chanzi limetafsiriwa katika lugha lengwa hivyo basi
matini lengwa zimekuwa na taarifa nyingi ambazo sio sahihi,mbinu hii ina uwezo
mkubwa wa kuendeleza lugha lengwa kwa kuingiza miundo ya maneno toka lugha
chanzi kwenda lugha lengwa . mfano:-
Ladies
and gentlemen: Mabibi na mabwana.
At
the end of the day – mwisho wa siku
Under
the chair manship of – chini ya uwenyekiti wa
C. TAFSIRI YA
KIMAWASILIANO.
Ni tafsiri ambayo huzingatia kueleweka
kwa ujumbe kwa hadhira lengwa.Huzingatia historia, muktadha, utamaduni na
itikadi ya mzungumzaji wa lugha lengwa.Hivyo ni tafsiri inayoilenga hadhira
kwani humjali zaidi msomaji wa matini lengwa. Ni tafsiri iliyowazi, huru, na
inayoeleweka kwa urahisi na wakati mwingine hujulikana kama tafsiri huru. Hii
ndio aina ya tafsiri au mbinu inayoonekana kuwa na mashiko zaidi kwasababu
haina utata wowote kwa hadhira ya lugha lengwa. Mfasiri hapaswi kufungwa na
miundo ya lugha chanzi kwani kinacho lengwa ni kueleweka kwa ujumbe kwa
hadhira. Mfasiri hufuata sarufi ya lugha lengwa na yuko huru kutafuta maneno au
mafungu ya maneno na nahau,misemo,methali,tamaduni na mazingira ya lugha lengwa
katika kueleza ujumbe unaotolewa na matini chanzi.Mfano;
Kiingereza: Tanzania
Electric supply campany limited
Kiswahili: shirika la
umeme Tanzania.
Kiingereza: there is a
purpose, there is no failure
Kiswahili: penye nia pana
njia
Tafsiri zilizotolewa katika mifano hapo
juu zimefanyika kwa kuzingatia miundo na maana zake katika lugha lengwa ndio
maana hatuoni kila neno lililokuwa limetafsiriwa pwekepweke.Aidha misemo katika
mfano wa pili umetafutiwa msemo unao fanana nao katika lugha lengwa badala ya
kutafsiri kisisisi.
FAIDA
ZA MBINU HII
Ø
Mbinu
hii hutumiwa kutafsiri matini nyingi duniani.
UMUHIMU
WA MCHAKATO WA KUTAFSIRI
Ø
Husaidia
mfasiri kufanya maandalizi yote muhimu ya kutafsiri yanayohitajika.Hii inapelekea
kupata maana sahihi za istilahi mbalimbali.
Ø
Humsaidia
mfasiri kutoa tafsiri sahihi ya matini chanzi kwenda kuwa matini lengwa.
Ø
Humfanya
mfasiri hutafsiri kwa kuzingatia mazingira na utamaduni wa hadhira lengwa, n.k.
Ø
Hufanya
kazi ya tafsiri isiwe na makosa madogomadogo ya kimaana na kimuundo.
Ø
Hurahisisha
kazi ya kutafsiri na kuifanya iwe nyepesi zaidi isiyo na shida.
UMUHIMU
WA TAFSIRI KATIKA JAMII.
Ø
Husaidia
kuleta istilahi za kufundishia. Mfano Kiingereza kimetafsiri maneno mengi toka
lugha ya kigiriki na kiratini.
Mfano Kigiriki kiingereza
Physics physics
Chemia Chemistry
Ø
Husaidia
kutafsiri istilahi mbalimbali za kimataifa toka lugha chanzi kwenda lugha
lengwa.
Mfano Kiingereza Kiswahili
Asprin Aspirini
Tyre Tairi
Globalization Utandawazi
E-mail Barua pepe
Fax Nukushi
Ø
Husaidia
katika kubuni na kuunda majina ya biashara katika lugha ya Kiswahili.
Mfano Sabuni chapa foma
inatokana na foam.
Sabuni chapa Kodrai –
inatokana na Codray
Kileo chapa Konyagi – inatoka
na Cognac
Ø
Husaidia
kutafsiri vitabu mbalimbali vinavyosomwa na watu wote.
Ø
Husaidia
kuleta istilahi za kisayansi na kitekinolojia katika lugha ya Kiswahili.
Mfano:Kiingereza Kiswahili
Radio Redio
Television Televisheni
Computer kompyuta/Tanakilishi
Ø
Husaidia
kuleta uhai wa lugha yaani kubadilika kimsamiati kulingana na wakati hasa
kuakisi matukio mablimbali. Mfano
Mfano Kiingereza Kiswahili
Stakeholder - mwanzo – washika dau
- sasa – wadau
Globalization
- Mwanzo – udandazi
-Sasa - utandawazi
Ø
Husaidia
sana katika vyombo vya habari, mfano redio, runinga na magazeti.
HASARA
ZA TAFSIRI KATIKA UTAMADUNI
Ø
Tafsiri
zimesababisha jamii za Afrika kuiga utamaduni wa nje.
Ø
Tafsiri
imesababisha mivutano ya makundi ya kidini kati ya nchi kwa nchi na jamii kwa
jamii.
Ø
Baadhi
ya njia za tafsiri husababisha kwenda kinyume na sarufi ya lugha lengwa au
utamaduni wa lugha lengwa.Mfano I like banana more than orange-Mimi penda ndizi
zaidi kuliko chungwa.
Ø
Husababisha
matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili hasa pale ambapo mzungumzaji anaamua kuzungumza
lugha mbili katika uzungumzaji wake.
UKALIMANI
Ni
uhawilishaji wa ujumbe ulio katika mazungumzo kutoka lugha chanzi kwenda
lugha lengwa. Au ni uhawishaji wa mawazo moja kwa moja kutoka lugha moja ya
mazungumzo kwenda lugha nyingine ya mazungumzo bila kubadili maana.
Mkalimani – ni mtu
anayefanya kazi ya kuhawilisha ujumbe ulio katika mazungumzo toka lugha chanzi
kwenda lugha lengwa.
SIFA
ZA MAKALIMANI BORA.
Ø
Awe
mjuzi wa hali ya juu wa lugha husika na utamaduni wake.
Ø
Ajue
lugha zaidi ya mbili hasa za kimataifa.
Ø
Awe
na ujuzi au maarifa ya kutosha ya mada au taaluma husika.
Ø
Awe
na ujuzi wa taaaluma ya ukalimani.
Ø
Awe
machapakazi,mdadisi na we mpenda kujienedeleza kupata habari.
Ø
Awe
na kipaji katika kutunza kumbukumbu kuteua msamiati sahihi haraka, kuunda istilahi
zinazo kubalika na awe na ulumbi yaani uwezo wa kushawishi na mvuto wa
kiuzungumzaji.
MAMBO
YA MSINGI KATIKA UKALIMANI.
Kuna mambo mbalimbali ya msingi ya
kuelewa kuhusu ukalimani.Baadhi ya mambo hayo ni kama yafuatayo:-
Ø
Ukalimani
ni mchakato wa uhawilishaji wa ujumbe wa mazungumzo ya papo kwa papo.
Ø
Ukalimani
unahusu lugha ya mazungumzo au alama.
Ø
Katika
ukalimani kuna wahusika watatu ambao ni mzungumzaji, mtalijumani na
msikilizaji.
Ø
Ukalimani
huzingatia sarufi, utamaduni, muktadha wa tukio na mada.
Ø
Ukalimani
unahusu lugha mbili tofauti ambazo ni lugha chanzi na lugha lengwa.
UMUHIMU
WA UKALIMANI.
Ø
Ni
daraja linalounganisha watu au jamii zinazozungumza lugha tofauti.Mfano
kimakonde kwenda Kiswahili.
Ø
Husaidia
katika masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa.Mfano katika utatuzi wa
migogoro, n.k.
Ø
Husaidia
kufanikisha vikao,mikutano na makongamano ya kimataifa na kitaifa.
Ø
Hutumika
kama mbinu ya kufundishia lugha ya pili.
STADI
ZA UKALIMANI.
Mkalimani anapaswa kuwa na stadi kuu nne
(4) mbali na ujuzi wake wa hali ya juu wa lugha. Stadi hizo ni;
1.
Stadi
ya kusikiliza.Mfano matamshi,lugha,maneno na kuwa makini na kile kinacho semwa.
2.
Stadi
ya kuzungumza mbele za watu.Stadi hii huambatana na mavazi,usijipambe sana na
punguza maelezo yasiyo na msingi.
3.
Stadi
ya kujenga kumbukumbu.
4
Stadi
ya kufupisha.
AINA
ZA UKALIMANI
Kuna aina mbili za ukalimani ambazo ni:-
1.
Ukalimani
fuatizi –Ni
ukalimani ambao mkalimani huzungumza kisha humpa nafasi mkalimani ili
akalimani.Mkalimani akimaliza humpisha mzungumzaji na zoezi hili huendelea hadi mwisho.Ukalimani
wa aina hii hufaa katika mijadala yaani kunapokuwa na mazungumzo ya maswali na
majibu kama vile mkalimani atahitaji kuchukua nukuu na kumbukumbu.Ukalimani huu
hufanyika katika mikutano ya wanahabari,mikutano ya kisheria ya pande mbili na
kwenye kundi dogo la watu,mikutano ya kidini na hospitalini.Njia hii hutumika
zaidi kwa vile haina gharama kubwa kutokana na gharama za vifaa
vinavyotumika kuwa ndogo na urahisi wa kuvimudu.
Ø
Udhaifu wa aina hii ni kuwa hutumia muda mrefu zaidi
kwani hoja moja husemwa mara mbili kwa lugha mbili tofauti na kwa kusubiriana.
2.
Ukalimani sawia
au sambamba – Ni
aina ya ukalimani unaoshughulika na uhawilishaji wa ujumbe kutoka lugha chanzi
kwenda lugha lengwa,ambao hufanyika papo kwa papo wakati mzungumzaji anaendelea
kuzungumza.Mzungumzaji na mkalimani huwasilisha ujumbe kwa pamoja bila
kusubiriana na wakati mwingine mzungumzaji humwacha mkalimani nyuma kwa sekunde
mbili au tatu.Mzungumzaji hasitishi mazungumzo kumpisha mkalimani na mkalimani
hamsubiri mzungumzaji kama ilivyo katika ukalimani fautizi.
ZANA
ZA UKALIMANI
Maendeleo ya sayansi na teknolojia
yameibua zana mbalimbali ambazo husaidia katika zoezi zima la ukalimani hata
hivyo zana za ukalimani hutegemea aina ya ukalimani wenyewe na muktadha
unaohusika katika ukalimani huo.
BAADHI
YA ZANA AMBAZO HUTUMIKA KATIKA
UKALIMANI.
1.
Kituturi.
2.
Paneli
pokezi na tolezi ya sauti.
3.
Maikrofoni.
4.
Kompyuta.
5.
Jozi
ya visikizo
Vilevile kituturi huwa kinapaswa kuwa
kisicho ruhusu sauti nyingine kusikika ndani zaidi ya ile ya mzungumzaji,hii
husaidia mkalimani kusikiliza sauti ya lugha chanzi kwa utulivu mkubwa. Mkalimani
humuona mzungumzaji wa lugha chanzi kupitia dirisha lenye kioo angavu la chumba
hicho na wakati mwingine mkalimani huweza kumuona mzungumzaji wa matini chanzi
kupitia kompyuta.
DHANA
MBALIMBALI ZA UKALIMANI
1.
Ukalimani wa
kijamii
– ni ukalimanni unaofanywa katika muktadha unaohusu jamii. Mfanii huduma za
afya, ujenzi wa shule n.k.
2.
Ukalimani wa
mahakamani
– ni ukalimani ambao hufanywa na wanasheria katika mahakama mbalimbali za
kisheria.
3.
Ukalimani wa mikutanoni – ni ukalimani
ambao hufanywa katika mikutano ya kitaifa na mataifa.Aghalabu hufanywa ndani ya
jengo au ukumbi maalumu.
4.
Ukalimani wa
kitabibu
– ni ukalimani ambao hufanywa katika sekta ya afya kwaajili ya kuchunguza maradhi
pamoja na kutoa tiba au ushauri kwa wahusika.
5.
Ukalimani wa
habari
– ni ukalimani amabao hufanywa katika vyombo mbalimbali vya habari hususani
ambapo lengo lake ni kufanya maudhui au taarifa ya habari iweze kuwafikia
walengwa.
6.
Ukalimani
sindikizi
–ni ukalimani ambao mkalimani huambatana na jopo la uongozi au wataalamu katika
ziara Fulani.Mfano kuongoza watalii.
7.
Ukalimani wa
lugha ya alama
– katika dhana hii ya ukalimani wa lugha ya alama huwa ndio lugha chanzi kwa
ajili ya viziwi (wasio sikia/bubu) kama kundi moja la watu ambapo mkalimani
huweza kutoa ujumbe kutoka lugha ya kusemwa kwenda lugha ya alama au kutoka
kwenye lugha ya alama kwenda ujumbe wa kusemwa.
MAMBO
YA KUZINGATIA KATIKA UKALIMANI.
Mkalimani anatakiwa kuzingatia mambo
mbalimbali kama vile;
1.
Lugha – makalimani
anatakiwa ajue lugha chanzi na lugha lengwa ikiwa ni pamoja na lafudhi ya
mzungumzaji ayasikie vizuri mazungumzo na kuielewa vizuri habari anayo zungumza
kisha aihawilishe bila tatizo lolote.
2.
Mazungumzo – mkalimani
anatakiwa ajue aina ya mazungumzo atakayo kalimani ili aweze kuteua msamiati
mwafaka katika mada na mazungumzo hayo.Mazungumzo hayo yanaweza kuwa ya
kitaaluma,kidini au kisiasa.
3.
Hadhira – mkalimani
lazima ajue hadhira inayopokea ujumbe na hana budi kuifanya hadhira iwe na ari
na utayari wa kumsikiliza ili iweze kupata ujumbe.Kuijua hadhira kunamsaidia
mkalimani kuchagua maneno na mtindo wa mazungumzo ili kuiwezesha hadhira kuelewa
kinachosemwa.
4.
Muktadha – mkalimani anatakiwa
azingatie muktadha husika wa tukio.
5.
Ujumbe – Mkalimani
azingatie ujumbe unaowasilishwa na mzungumazaji.Katika kukalimani kuzingatia
zaidi ujumbe na kuvaa uhusika zaidi kuliko muundo na mtindo wa lugha chanzi.
6.
Lengo la mazungumzo–mkalimani
anatakiwa kuzingatia lengo la mazungumzo na aoneshe hisia za mzungumzaji.Mfano
huzuni, au furaha.
DHIMA
ZA UKALIMANI
Ø
Ni
kiungo cha mawasiliano kati ya jamii ya lugha moja na nyingine – mawasiliano
hayo yanaweza kuwa ya kitaaluma,kidini au kisasa.
Ø
Husaidia
kueneza utamaduni husika katika jamii tofauti–kupitia ukalimani jamii hupata
kujua tamaduni za jamii nyingine hususani mazungumzo yanayohusu utamaduni,vyakula
na michezo mbalimbali.
Ø
Husaidia
katika shughuli za kidiplomasia–ambapo kunakuwa na watumiaji wa lugha tofauti
mfano kuhusu migogoro.
Ø
Hadhira
au wasikilizaji wamazungumzo huweza kujifunza lugha nyingine kwa kujua maana ya
maneno na hata muundo wa lugha ngeni.
TOFAUTI
KATI YA TAFSIRI NA UKALIMANI
1.
Kimaana
Ø
Tofauti katika
uwasilishaji–tofauti
uwasilishaji kwa njia ya maandishi lakini ukalimani inawakilishwa kwa njia ya
mazungumzo.
Ø
Muda wa
maandalizi–tafsiri
hupewa muda wa kuandaa kabla ya kuanza kutafsiri lakini ukalimani hauna muda wa
kujiandaa.
Ø
Tofauti katika
hadhira–ukalimani
hadhira yake ni ya papo kwa papo, lakini tafsiri haina hadhira ya papo kwa
papo.
Ø
Vifaa ambatani
katika utendaji–ukalimani
hutumia vifaa kama vile visikizi, vya masikioni,vituturi n.k lakini tafsiri
vifaa vyake ni kama vile karatasi na kalaamu, kompyuta n.k.
Ø
Tofauti katika
gharama
– katika ukalimani gharama hulipwa kwa saa lakini katika tafsiri hunalipwa kwa
ukurasa.
Ø
Ukongwe
na umri – ukalimani ni mkongwe zaidi kwani ulianza kabla ya kugunduliwa kwa
maandhishi lakini tafsiri ilianza baada ya kugunduliwa kwa maandishi.
UFANANO
KATI YA TAFSIRI NA UKALIMANI
Ø
Zote
ni njia au daraja la kuunganisha pande mbili–yaani lugha chanzi na lugha lengwa
na matini chanzi na matini lengwa.
Ø
Zote
huwa na dhima au lengo la kurahisisha mawaslilano.
Ø
Zote
zinahusisha vijenzi katika utendaji wake – kama vile matini chanzi na matini
lengwa, lugha chanzi na lugha lengwa.
Ø
Taaluma
zote mbili huendeshwa kwa namana mbili – yaani kwa kutumia mashine na kwa
kutumia mtu.
Ø
Taaluma
zote mbili huhusisha wataalamu na namna mbili – yaani wataalamu wa lugha na
wataalamu wa uwanja wa lugha husika yaani mkalimani na mfasiri watambue watu wanao wafanyia tafsiri na ukalimani.
MATATIZO
KATIKA TAFSIRI.
1.
Tofauti za
kiisimu–
tofauti za maumbo,muundo na maana kati ya lugha ya Kiswahili na lugha za kigeni
husababisha upungufu katika kutafsiri.Maumbo ya Kiingereza huruhusu kauli
nyingine ili kuonyessha wingi na umoja
wa wahusika.Mfano wa maumbo hayo huweza kutoa tafsiri pana zaidi na wakati
mwingine linapo tafsiriwa katika matini lengwa hasa katika lugha ya Kiswahili
hulazimika kubadili matini. Mfano
Kiingereza Kiswahili
No enterance usiingie
ndani
Quite please usipige
kelele
Katika mifano hapo juu ni kwamba tafsiri
ya Kiswahili hujibana zaidi kwani ukisema usipige kelele ina maana mimi sio
wewe na kwa upande mwingine katika baadhi ya muundo wafasiri huhawilisha ruwaza
na kisintaksia za Kiingereza katika Kiswahili na kufanya tafsiri kuwa tenge.
Mfano Kiingereza Kiswahili
Nine thouthands tisa elfu
Five million tano milioni
2.
Tofauti za
kiitikadi–katika
tafsiri za vitabu na magazeti itikadi na hisia za wafasiri zinaweza kuathiri
matokeo ya tafsiri zao.Mfano matini inasifu pombe,unaambiwa utafsiri na wewe hupendi
pombe kabisa,hii ni tofauti za kiitikadi kwani kutokana na mfasiri kutopenda
pombe anaweza kuibadili matini hiyo badala ya kusifia pombe ikaonesha kuchukia
pombe.
Mfano Kiingereza Kiswahili
Merchant of venice mbepari wa venisi
Katika jina la kitabu hicho nyerere alitafsiri
kama mabepari wa venisi badala ya wafanya biashara wa venisi ambayo ndio
tafsiri sahihi ya merchant.Mfasiri huyu alisema hivyo kutokana na itikadi alizo
nazo kuhusiana na wafanyabiashara kuwa ni mabepari hivyo ni wanyonyaji
3.
Tofauti za
mitindo –
maranyingi ni vigumu kueleza dhana au taarifa kwa kufuata mtindo unaotokiwa
katika uwanja huo hivi inamaana kwamba Kiswahili kama zilivyo lugha nyingine za
kiafrika hazijawa na tofauti dhahiri za mitindo. Mfano
Kiingereza Kiswahili
Lend me
your ears naomba
mnisikilize
May I
have your attention
Taarifa ya kingereza inaonekana kuwa
pana zaidi kuliko ya kiswahili kwasababu kuna maana nyingi za kuzungumza jambo
moja.
4.
Tofauti za
mazingira na mila
– kwa kawaida mazingira,mila na desturi kati ya watumiaji wa lugha chanzi na
lugha lengwa maranyingi hufanya tafsiri kuwa ngumu. Mfano maneno kama “karibu
tena” yanapotumiwa na mswahili anapomuaga mgeni wake hayana maana ya moja kwa
moja na yale ya Kiingereza “welcome again” bali humaanisha “goodbye”
5.
Toafauti za
misemo vitendawili na nahau –maneno haya huendana na watu wa utamadunu fulani
unaotofautiana kati ya jamii moja na nyingine.Mfano funga vilago (msemo),enda
joshi (nahau),popo mbili zavuka mto (kitendawili), mwenda pole hajikwai (methali)
kwa kuwa vitendawili, nahau, misemo na methali huendana na utamaduni wa watu
fulani hivyo tafsiri ya maneno kama hayo huweza kukumbwa na matatizo kama vile
kutopatikana kwa visawe katika lugha lengwa.
6.
Tofauti za
kifasihi
–taarifa zilizomo katika fasihi huandaliwa kusanii hivyo huhitaji wasomaji
wafanye bidii katika uchambuzi ili wapate maudhui ya fasihi husika kwani bila
kusoma kwa makini hawataweza kupata maudhui ya fasihi husika.Mfano katika
mashairi ya shaban Robert kuna shairi lenye kichwa “ua” mfasiri anaanza kujiuliza je ua linalozungumziwa hapa ni lipi?
Ua kama pambo, mpenzi au muuwaji. Je mfasili atatoa fasili ipi katika lugha lengwa bila kpoteza
maana katika matini chanzi,hili pia ni tatizo
katika tafsiri.
UTOSHELEVU
KATIKA TAFSIRI
Katika kuangalia utoshelevu katika
tafsiri hutazama mambo mbalimbali kama vile;
1.
Kupata
msaada wa vitabu mbalimbali. Mfano kamusi.
2.
Kutumia
mbinu mbalimbali za tafsiri. Mfano tafsiri ya neno kwa neno mawasiliano nk
3.
Kuzingatia
kanuni, sheria na taratibu za matini asli ya au matini chanzi.
4.
Mfasiri
azingatie sana utamaduni wa lugha lengwa.
MBINU
ZA KUTATHMINI/ KUHAKIKI TAFSIRI
Kutathimini
au kuhakiki tafsiri ni kitendo cha kitendo kuisoma kwa makini
iliyotafsiriwa na kisha kuitolea hukumu juu ya ubora na udhaifu wake.Kuhakiki
au kutathimini tafsiri hulenga kubaini
iwapo tafsiri hiyo ni Tafsiri pana,Tafsiri tenge (mbovu),tafsiri finyu aua
Tafsiri sahihi.
MBINU
MBALIMBALI ZA KUTATHIMINI/ KUHAKIKI MATINI
Katika kuhakiki au kutathimini matini
kuna mbinu sita zinazotumiwa,nazo ni;
1.
Ulinganishaji wa
matini,Ni
mbinu ambayo ni kongwe na ndiyo mbinu ambayo hutumiwa zaidi na wafasiri au
wataalamu wengi wanapotathimini au kuhakiki matini mbalimbali.Hapa
kinachofanyika ni kwamba matitini iliyotafsiriwa yaani tafsiri huchukuliwa na
kulinganishwa na matini chanzi yake ili kuona iwapo vipengele vyote muhimu vya
kimuundo na vya kidhima vimezingatiwa katika tafsiri hiyo.Kazi hii ya
kutathimini huweza kufanywa na mfasiri mwenyewe au mtu mwingine.
Mfano: Matini chanzi – The chairperson had spoken
for almost a hour
Matini
Lengwa-Mwenyekiti alikuwa akihutubia kwa takribuni saa moja
Je kama ni wewe
unafanya tathmini ya hizo tungo ungezitathminije kwa kutumia mbinu ya
ulinganishaji matini?
2.
Kutumia tafsiri
Rejeshi,Ni
mchakato wa kutafsiri matini ambayo tayari imeshatafsiriwa katika lugha Fulani
(lugha lengwa) na kuirejesha tena katika lugha chanzi kwa lengo la kuitathmini
matini hiyo.
Mfano: Kama tafsiri ilifanywa kutoka Kiswahili
kwenda kiingereza basi inapofanyiwa tathmini kwa kutumia tafsiri rejeshi basi
tafsiri hiyo itatafsiriwa tena kutoka katika lugha ya kiingereza kwenda katika
lugha ya Kiswahili
Tafsiri rejeshi
inachangamoto kwani inawezekana makosa yapo katika tafsiri ya mtu wa pili
anayetathmini na wala si katika tafsiri ya awali iliyofanywa.Hivyo upo uwezekano
wa kusema tafsiri iliyofanyika ni mbaya ati tu kwasababu matokeo ya tafsiri
rejeshi hayalingani na matini chanzi halisi lakini upo uwezekano wa kuonesha
ubora wa tafsiri husika pia.
3.
Kupima uasili,Tafsiri bora
haipaswi kusomeka kama tafsiri.Hii ina maana kwamba mtu anaposoma tafsiri yako
asijue kama ni kazi iliyotafsiriwa badala yake inatakiwa isomeke kama vile
imeandikwa katika lugha lengwa hiyohiyo.Hivyo hali ambapo tafsiri husomeka kama
vile imeandikwa katika lugha lengwa hiyo hiyo ndio ambayo huitwa
uasili.Inashauriwa mfasiri mwenyewe au mtu mwingine anaisoma kazi hiyo,pia hasa
inashauriwa apewe mtu mwingine tena bila kuambiwa kwamba kazi hiyo ni tafsiri.
4.
Kupima
uelewekaji,Katika
mbinu hii kinachoangaliwa ni kueleweka kwa maudhui yanayotolewa katika tafsiri
hiyo.Mtu anayepima uelewekaji atajiuliza yeye mwenyewe,je maudhui katika kazi
hii yataeleweka kwa wasomaji au kazi hii inazungumzia nini?.Hivyo inashauriwa
kwamba mfasiri ampe mtu mwingine ili kuepuka kujipendelea.Ni muhimu kuzingatia
kuwa mtu anayepelekewa kazi hiyo inashauriwa awe mfasiri.
5.
Kupima
usomekaji,katika
mbinu hii ya kupima usomekaji mfasiri au mhakiki atapima tafsiri husika ili
kuona iwapo inasikika vizuri masikioni mwa msikilizaji na kama ina mtiririko
unaokubalika katika lugha lengwa.Hapa kunakuwa na watu wawili mmoja anasikiliza
na mwingine anasoma kwa sauti.
6.
Kupima
ulinganifu,Hapa
mhakiki anaangalia umakini wa mfasiri katika kutumia kwa namna inayofuata
vipengele vyote muhimu vya matini kama vile msamiati,istilahi,maudhui au maneno
muhimu yanayobeba maudhui.Maana yake ni kwamba kama neon limejirudia rudia
katika tafsiri usibadilishe,mfano;Aim-nia,lengo,madhumuni,kusudi,azma,shabaha
n.k.Hivyo kama neon ‘’Aim’’ umelitafsiri kama lengo basi popote
litakapojitokeza kwa mara nyingine katika matini basi libaki hivyo hivyo bila
kubadili badili.