TAHAKIKI- CHUNGU TAMU
DIWANI : CHUNGU
TAMU
MWANDISHI:
THEOBALD MVUNGI
WACHAPISHAJI:
TPH
MWAKA: 1985
UTANGULIZI
Chungu
Tamu ni diwani iliyoandikwa na Theobald
Mvungi miaka ya 1980.Katika diwani hii
mwandishi anaimulika jamii na kuichunguza kwa makini.Anakosoa na kutoa
mapendekezo ili wananchi waondokane na machungu yanayowaandama na kuonja utamu
ambao utawafikisha kwenye kheri.Katika diwani hii mwandishi ameonesha dhahiri
jinsi Uchungu na Utamu vinayotangamana katika harakati zote za maisha ya
mwanadamu.Kwa ufupi,diwani hii ni kipaza sauti
kinacholia kwa sauti kali kuujulisha ulimwengu juu ya uchungu
unaoiandama jamii yetu ya Tanzania .
MAUDHUI
DHAMIRA
KUU; UJENZI YA JAMII MPYA
Suala
la ujenzi wa jamii mpya limezishughulisha fikra
za wanafasihi wengi hapa
Tanzania .Jamii endelevu ni jamii mpya ambayo haina
ubaguzi,matabaka,uongozi mbaya,yenye kufuata misingi ya haki na usawa.Jamii
iliyojikomboa katika Nyanja zote yaani kiuchumi, kisiasa,kiutamaduni na kifikra.Wanafasihi wa Afrika wanaitaka jamii
hiyo ijengwe kwa kufuata misingi ya haki na usawa kwa kila mtu. Wanafasihi wa
Afrika wameonesha dhahiri kuwa jamii iliyoachwa na wakoloni ilikua zimeoza na
hivyo zinahitajika juhudi kubwa ili kuondoa uozo huo.
Nchini
Tanzania suala la jamii endelevu
lilianza mara tu baada ya kupata uhuru na kuimarishwa zaidi wakati wa Azaimio
la Arusha. Watanzania walitaka wajenge jamii yenye kufuata misingi ya haki na
utu,jamii isiyokuwa na matabaka,jamii yenye viongozi waliotakasika, jamii yenye
demokrasia ya kweli,jamii isiyo na unyonyaji wa
aina yoyote ile,jamii ambayo hatamu za uongozi zingekuwa mikononi mwa
wakulima na wafanyakazi,jamii isiyo na dhuluma ya aina yoyote,n.k.Hadi
mwandishi anaandika diwani hii anaonyesha kuwa
jamii bado haijafanikiwa kuifikia lengo la kujenga jamii mpya.
Mwandishi
ameonesha vikwazo mbali mbali
vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya na endelevu hapa nchini na mbinu za
kujikwamua kutoka kwenye vikwazo
hivyo.Mwandishi ametoa mapendekezo
ambayo anaamini kuwa endapo jamii itayafuata
itafanikiwa kuijenga jamii mpya
na endelevu.Mbinu hizo ndizo dhamira
ndogo ndogo za diwani hii kama ifuatavyo;
1.
KUPINGA DHULUMA
Dhuluma ni tendo lisilo la haki,tendo la
uonevu,ukatili au uovu. Dhuluma hupingana na haki.Suala la dhuluma hurudisha
nyuma maendeleo ya jamii na hivyo ni kikwazo kikubwa cha ujenzi wa jamii
endelevu.Suala la dhuluma limemshughulisha sana mwandishi wa diwani hii,katika
shairi la “Chatu na kuku” Katika ubeti wa mwisho mwandishi anasema;
Basi babu
akatua,
Funda akajimezea,
Mimi tama imejishikia,
Huzuni imenisaliti,
Kwa chatu kukosa dhati,
Ndipo nikapanga hizi beti,
Ziwe kama ndiyo
hati
Ukumbusho wa huyu dhulumati.
Katika shiri la
“Chatu na Kuku”, mwandishi amelijenga kitaswira kuonesha jinsi wakoloni (chatu)
walivyoingia Afrika na kuendeleza dhuluma.Chatu
amewakilisha wakoloni na kuku
anawakilisha wananchi (Waafrika) walioonyonywa na kudhulumiwa na wakoloni. Mayai ya kuku yanawakilisha mali ghafi
waliyodhulumu wakoloni kutoka hapa Afrika.
Katika
shairi la“Chanzo ni Wenye Kauli” mwandishi anaonesha jinsi ulanguzi
unavyosababisha dhuluma katika jamii.Mwandishi ameonesha kuwa chanzo cha
ulanguzi ni upungufu wa bidhaa muhimu,tamaa,pamoja na uzembe toka kwenye vyombo
vya dola. Ulanguzi husababisha
rushwa,magendo na hivyo haki haitendeki katika jamii.
Mwandishi
anasema;
“Mianzo tukiijua,
Mipango tujipangia,
Kamwe pasiwe na njia,
Ulanguzi kurudia,
Iwe tu twahadithia,
Mithili historia”.
Katika
shairi la “Kademokrasia Katoweka”mwandishi anasema;
Ya msiba atayetamka,
Udikteta waja haraka,
Mtemi na walomzunguka,
Wawatia raia mashaka,
Dhuluma yatangazwa fanaka.
Mwandishi
anaonesha jinsi wananchi wanavyodhulumiwa demokrasia yao ya kutoa maoni yao
hadharani.Demokrasia inapokosekana,dhuluma ya kutawala kwa mabavu huendelezwa.
Katika
shairi la “Wengine Wabaki Taabuni”,mwandishi
anajadili juu ya dhuluma wanayoiendesha wakubwa dhidi ya watu wa tabaka la
chini.Ameonesha kuwa majambazi wanayo idhini ya kufanya kila jambo kwa
wanyonge,kwani hayo majambazi hulindwa na wakubwa.Anaendelea kueleza kuwa
dhuluma inayoendeshwa na majambazi hapa nchini ni njama za walinzi (vyombo vya dola).Mwandishi Anasema;
“Majambazi wanayo idhini,
Kufanya lijalo akilini,
Na hawataingia nguvuni,
Ma’na walinzi wamo njamani,
Tabu yaanzia kileleni.”
Mwandishi
anaeleza kuwa tabu inaanzia kileleni
maana yake ni tabu au dhuluma inaanzia kwa wakubwa.Hivyo ili tufanikishe
suala la ujenzi wa jamii mpya ni lazima
tujitoe mhanga kupambana na kila aina ya dhuluma katika jamii.
2. KUFANYA KAZI
KWA BIDII
Uzembe
na kutowajibika ni kikwazo kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya jamii yoyote
ile.Jamii yoyote ile yenye viongozi wazembe,viongozi wasiowajibika au wananchi
wasiojua wajibu wao daima itabaki nyuma kimaendeleo.Mwandishi anaitaka jamii
yetu ijue umuhimu wa kazi na kuwajibika katika suala zima la maendeleo.
Mashairi kadhaa katika diwani hii yanasisitiza kuhusu umuhimu wa kufanya kazi
ili kuleta maendeleo ya jamii.Katika shairi la “Daktari askari”.Mwandishi anasema;
Saa moja jioni Landova inaingia,
Majeruhi sita na waganga pia,
Majeruhi vibaya wanalalama,
Waganga wao na sisi kazi tukaanza,
Hakuna kuamkiana au sijui nini.la,
Wagonjwa wengi misuli walikatika,
Wengine risasi walichimbiwa ,
Tukawekea damu,
Wa kushonwa,tukawashona,
Wakupasua ,tukapasua.
Katika shairi la
“Daktari Askari”,mwandishi anaonesha jinsi waganga wanavyojua umuhimu wa
kuwajibika katika kazi yao ya utabibu. Ameonesha kuwa wale waganga
waliwahudumia majeruhi kwa bidii wakati wa vita.Hivyo kila mtu anatakiwa
kuwajibika kama wale waganga ndipo tutaweza kulisukuma mbele gurudumu letu la
ujenzi wa jamii endelevu.
Katika
shairi la “Chanzo ni Wenye Kauli” mwandishi anaonesha utekelezaji na
uwajibikaji mbovu unavyosababisha rushwa, magendo na ulanguzi katika jamii yetu
Katika shairi hili mwandishi ameonesha dhahiri kuwa uzembe toka kwenye vyombo
vya dola ndio umechangia uwajibikaji kuwa mbovu.Mwandishi anasema;
“Chombo hiki kuzembea,
Chanzo kilichozidia,
Magendo kuyatetea,
Watu kuwasaidia,
Chombo kilididimia.”
Katika
shairi la “Wimbo Wake Hotubani” wandishi anaonesha utekelezaji mbaya wa maazimio unavyochangia kuzorota kwa
maendeleo ya jamii yetu.Katika shairi hili,mwandishi ameonesha kuwa viongozi
wetu wametuna ofisini na shambani hawaingii, wanatumia madaraka vibaya,maagizo
ni midomoni bila utekelezaji, kila siku-mchana kutwa wanakunywa na kulewa,
n.k.Utekeleaji wao uko kwenye hotuba,Mwandishi anasema;
“Cheo kiko mkononi,
Agizo li mdomoni,
Mchana kutwa ndotoni,
Wimbo wake hotubani,
Raia kazi fanyeni.”
Katika
shiri la “Wengine Wabaki Taabuni”,mwandishi anaonesha jinsi uzembe
kazini,kutowajibika ipasavyo,usaliti pamoja na rushwa unavyorudisha nyuma
utekelezaji mzuri wa maazimio tunayojiwekea.Mwandishi anaitaka jamii ifahamu na kutambua umuhimu wa kazi na
wajibu wa kila mmoja katika jamii ndipo tutaweza kufanikisha kuijenga jamii
mpya.
3.
UONGOZI MBAYA
Suala
la uongozi mbaya limekuwa tatizo sugu kwa nchi nyingi za Afrika.Waandishi wengi wameonesha jinsi
ambavyo viongozi wengi walioshika madaraka baada ya mkoloni kuondoka
walivyoteka nyara uhuru uliopatikana,kwa hiyo mabadiliko yakawa rangi ya ngozi
tu,kwani wananchi wengi waliendelea kuteseka katika umasikini wao.Katika shairi
la “Tishio
la Binadamu”mwandishi anasema;
Mashindano ya silaha,yamekuwa ni mchezo,
Wakubwa waona raha,kwa silaha waundazo,
Mabomu yaso na siha,ndiyo yawapa uwezo,
Urusi na Marikani,dunia mwaipa adha.
Mwandishi
anakemea juu ya uongozi unaotumia mabavu, Mfano mzuri mwandishi anakemea nchi
za Urusi na Marekani ambazo ni wanachama wenye kura ya VETO kwenye umoja wa
Mataifa zinavyotumia mabavu kuzikandamiza nchi zisizo na nguvu kisilaha.
Mwandish anasema;-
“Kuyasujudu
mabavu, mwadai tusilotaka,
Maoni yetu chakavu, sawa nguo ya miaka,
Ni pengi penye makovu, nchi zilivyopasuka,
Mabomu yateketeza,waundaji mwafurahi!”
Shairi
la “Chini
ya Mti Mkavu” mwandishi analaani uongozi unaoendeleza dhuluma katika
jamii.Anakemea juu ya uongozi mbaya usiojali maslahi ya wengi,uongozi usiopiga
vita umaskini hapa nchini, n.k.
Katika
shairi la “Wanajua Kuvumilia”,mwandishi analaani ahadi za uongo
zinazotolewa na viongozi wetu.Ameonesha kuwa viongozi wetu hawasemi ukweli bali
uongo ndio umetawala midomo yao.Katika shairi hili mwandishi analaani vibaya
viongozi ambao hawafiki vijijini kwa wananchi waliowachagua ili kujionea hali halisi ya maisha
wanayoshi.Mwandishi anasema:-
“Afadhali kuimba ukweli,
Wimbo mchomo mkali,
Wimbo, unalilia hali,
Ya vijiji vilivyo mbali,
Kwa wale wasio kauli.”
Katika
shairi la “Udongoni” mwandishi anawakumbusha viongozi wajibu wao katika
jamii.Mwandishi anasema:-
“Lanikumbusha wajibu,
Kujenga si kuharibu,
Naahidi kujaribu,
Kulinda tulichojenga.”
Mwandishi anaona
kuwa Uongozi bora ni msingi mkubwa katika ujenzi wa jamii mpya hivyo anaiasa
jamii kupiga vita Uongozi mbaya ili kujenga jamii endelevu hapa nchini.
4.
KUWEPO NA
DEMOKRASIA YA KWELI
Demokrasia
ni mfumo wa kuendesha serikali iliyochaguliwa na watu kwa manufaa ya watu
wenyewe.Demokrasia inahitajika sehemu yoyote ile ili kuwaruhusu wananchi kutoa
maoni yao kwa uhuru bila wasi wasi au kikwazo chochote.Katika shairi la“Mjanja
yu Mashakani” mwandishi anasema;
Kumezuka mkatao,miaka ya themanini,
Watu wafanya jutio,hawasemi chinichini,
Hawasemi tena ndio,haitoki midomoni,
Wamevumilia sana,mwisho wa uvumilivu.
Mwandishi
anajadili kuhusu mfumo wa demokrasia
ambao umejitokeza miaka ya 1980 kote ulimwenguni.Mfumo huu ni ule wa kupinga
sera ya chama kimoja na kuingia katika mfumo wa vyama vingi (mageuzi).Katika
shairi hili mwandishi anaonesha kuwa mfumo wa vyama vingi umewaamsha wananchi
wengi kutoka usingizini na kuanza kutetea haki zao.Hata hivyo,mwandishi
anaonesha kuwa wale viongozi waliojilimbikizia madaraka na vyeo mbali mbali
wamehofia sana mfumo huu na hivyo hufanya kila mbinu ili kuudidimiza.Viongozi
wanaong’ang’ania madaraka ndio wanaohofia mfumo huu.
Shairi
la “Kademokrasi
Kametoweka”linapinga uongozi mbaya barani Afrika.Mwandishi ameonesha
kuwa demokrasia inapopokonywa na viongozi wachache,udikteta huota mizizi na
kuung’oa huchukua muda mrefu.Hali hii inasababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe
katika baadhi ya nchi barani Afrika.Mfano wa nchi hizo ni Jamuhuri ya Watu wa
Kongo,Uganda,Burundi,Sierra Leone,n.k.Utawala wa nguvu hurudisha nyuma
maendeleo ya bara la Afrika na nchi nyingine za ulimwengu wa tatu ambako hakuna
demokrasia ya kweli.Mwandishi anasema:-
“Barani mabavu yatumika,
Dikteta asijeanguka,
Na majungu pia ayapika,
Udikteta pasi shufaka,
Nasimulia ya Afrika
Mwandishi
anaonesha kuwa mabavu yanatumika ili kumlinda dikteta asije akaangushwa kwa
kufuata mfumo wa demokrasia ya kweli.Madikteta hao hutumia vyombo vya dola kama
vile polisi, jeshi,magereza na mahakama ili kutetea maslahi yao.Kwa ujumla anatoa
pendekezo kuwa, ili tuweze kujenga jamii
mpya hatuna budi kujenga na kudumisha demokrasia ya kweli katika harakati zetu
za maisha.
5. MATABAKA
Matabaka
ni hali ya watu kuishi kufuatana na madaraka walionayoya,uchumi na siasa
n.k.Msanii ametumia vielelezo halisi kufikisha ujumbe kwa jamii.Katika shairi
la “Wimbo
wake
Hotubani” mwandishi anasema;
Magavana majimboni,
Wasambazao nchini,
Wapewa kubwa idhini,
Na watune ofisini,
Wasoingia shambani,
Kwa sifa madarakani.
Mwandishi
anadhihirisha matabaka yaliyopo nchini mwetu. Magavana wanawakilisha tabaka la juu (viongozi) na punda na ngamia
wamechorwa kitaswira kuwakilisha wananchi wanyonge wanaoteswa na kunyanyasika.
Katika shairi la
“Wengi
Wabaki Taabuni” mwandishi
anasema;
Mesikia kilio
gizani,
Jamaa apita njiani,
Ghafla akakabwa kooni,
Kapigwa kabari ya kihuni,
Yaitwa demokrasi guni.
Mwandishi
anaonesha kuwa,kuna matabaka ya aina mbili katika jamii yaani tabaka la
wachache wanaofurahia maisha na tabaka la wengi wanaoteseka taabuni.
Kwa ujumla
mwandishi ameonesha kuwa mgawanyiko wa watu katika matabaka huleta utengano
katika jamii.Ili tuweze kufaulu kuijenga jamii mpya (endelevu) hatuna budi
kupiga vita matabaka yaliyoshamiri katika jamii.Lengo liwe kuijenga jamii yenye
kufuata misingi ya haki na usawa.
6.KUEPUKA
VITA (UHASAMA)
Vita
husababisha uhasama katika jamii.Huleta ugomvi na kutokuelewana miongoni mwa
watu.Vita hurudisha nyuma maendeleo ya jamii.Vita huleta athari mbaya katika
jamii.Mfano vifo,umasikini,ugumu wa maisha.Katika shairi la “Tishio
la Binadamu”,mwandishi anasema:-
“Mashindano
ya silaha,yamekuwa ni mchezo,
Wakubwa wanaona raha,kwa silaha waziundazo,
Mabomu yaso na silaha,ndiyo yanawapa uwezo,
Urusi na Marekani, dunia mwaipa adha”
Mwandishi
anaitahadharisha dunia kuwa vita kuu vinanukia.Hii ni kutokana na uhasama
uliopo kati ya nchi na nchi pamoja na utengenezaji wa silaha kali kutoka Urusi
na Marekani.Kutokana na hali hii dunia nzima sasa iko mashakani juu ya
vita.Mwandishi anaendelea kueleza kuwa mashindano ya silaha yamekuwa ni mchezo
na nchi kubwa zinaona fahari kuzitengeneza.Hivyo mwandishi anaitaka jamii itakayojengwa iepukane daima na suala la
vita.
7.SUALA
LA MAPENZI
Mwandishi
amejadili aina mbali mbali za mapenzi katika diwani hii kama ifuatavyo;
Mosi,mapenzi
ya mtu na nchi yake.Haya mapenzi tunayaona katika shairi la “Daktari
Askari” ambapo tunona kuwa,wakati wa vita kati ya Uganda na Tanzania
raia,wanajeshi,manesi,n.k.walijitolea kwa moyo wa dhati kwenda kupigana ili
kuikomboa nchi yao.Mapenzi haya ni ya kweli na dhati.Mapenzi ya Iddi Amini Dada
kwa nchi yake hayakuwa ya dhati ndiyo maana alitumia mabavu kuiongoza nchi
yake.
Pili,Mapenzi mengine kati ya mtu na nchi yake
yanapatikana katika shairi la“Ngulu Wapaona”Katika shairi hili
msanii anaonesha umuhimu wa kuwa na
mapenzi na kwenu (nchi yako) hata
kama ni porini. Msaanii anamtaka kila mtu kuthamini kwao hata kama kuna
karaha.Anaonesha kuwa kwenu ni kwenu na
ukuthamini na kukuheshimu kwa raha na Baraka.
Tatu,mapenzi kati ya mwanamme na mwanamke.Mapenzi haya
mwandishi ameyagawa ktika makundi makuu
mawili ya mapenzi ya dhati na yale ya udanganyifu.Mashairi yanayoongelea
mapenzi ya dhati ni yale ya “Daktari Askari”,“Thomas
na Doto”,“Manzese Mpaka Ostabei”pamoja na lile la“Takukumbuka Daima.”
Mashairi
yanayoongelea mapenzi ya udanganyifu ni kama vile “Usiwe Mwonja Asali”, “Fikra
za Waungwana”.
Mapenzi ya dhati
ni ya kuheshimiana,Mapenzi yasiojali
hali au kipato cha mtu. Mapenzi ya uaminifu. Mapenzi kati ya Daktari Adam na Eva katika shairi la “DaktariAskari”
yalikuwa ya dhati, bila kujali kwao au utaifa.Hali kadhalika mapenzi kati ya Thomas
na Doto yalikua ya dhati bila kujali
rangi au taifa.Na mapenzi kati ya Mashaka na Dorothy yalikuwa ya dhati bila
kujali pesa au utajiri. Mapenzi ya dhati husababisha uvumilivu katika
maisha.Mapenzi ya dhati huzaa matunda mema katika ndoa,yaani hujenga ndoa za
uaminifu.Hivyo mapenzi ya dhati huzaa ndoa za kudumu,ndoa zisizojali
rangi,utajiri,utaifa au hali ya mtu.Ndoa za uaminifu zilizotokana na mapenzi ya
dhati Katika diwani hii ni zile kati ya daktari
Adam na Eva, pamoja na ile ya Mashaka
na Dorothy.
Mapenzi
ya udanganyifu nayo pia huzaa ndoa za udanganyifu na mara nyingi ndoa hizo huwa
hazidumu.Katika shairi la “Usiwe Mwonja
Asali”,msanii anaonesha jinsi mapenzi ya udanganyifu yanavyosababisha uchumba
wa udanganyifu.Msanii anaishauri jamii kuwa ukiwa na mchumba msiwe na tabia za
kujamiiana ovyo,bali mpaka mtakapooana.
Katika
shairi la “Fikra za Waungwana” mwandishi anadhihirisha wazi jinsi mapenzi
ya udanganyifu yanavyosababisha ndoa za ulaghai. Mwandishi anasema:-
“Mume
wangu nakupenda, Joseph amenikuna,
Nimekula naye tunda, ninampenda sana,
Na usifanye inda, mimi ni wako kimwana,
Nitaishi kwa mpango, kwako na kwake Joseph.”
Kwa
ujumla mwandishi anaitaka jamii yetu
idumishe mapenzi na ndoa za dhati.
5.
NAFASI YA MWANAMKE PAMOJA NA UHURU WAKE KATIKA JAMII.
Mwandishi amemchora mwanamke katika nafasi mbali mbali
kama ifuatavyo;
Mosi,amemchora kama mwanamapinduzi na jasiri.Katika shairi
la “Daktari
Askari”mwanamke ameoneshwa akifanya kazi za kimapinduzi sawa na zile za
mwanamme.Mwanamke anapigana vita ili aikomboe nchi yake.
Pili,mwanamke amechorwa kama mtu mwenye mapenzi
dhati katika jamii.Katika shairi la “Manzese Mpaka Ostabei”
linamwonesha Dorothy akiwa na mapenzi ya dhati kwa Mashaka . Hali kadhalika
katika shairi la “Daktari Askari linamwonesha Eva akionesha mapenzi ya dhati kwa
Daktari Adam.
Tatu,mwanamke
amechorwa kama kiumbe laghai, asiye mwaminifu hususani katika suala a mapenzi
na ndoa.
Haya yote tuayoyaona katika shairi la “Fikra
za Waungwana”.
Mwisho,mwanamke
amechorwa kama mzazi na mlezi katika jamii.Katika shairi la
“Manzese mpaka Ostabei”,mwanamke amechorwa kama mzazi na mlezi na hii nafasi
inawakilishwa na Dorothy ambaye alimzaa mtoto na kumlea baada ya kuolewa na
Mashaka.
Kuhusu
uhuru wa mwanamke,msanii ameleta mjadala juu ya uhuru wa mwanamke,uhuru wa
kuolewa na wanaume wawili kama afanyavyo mwanaume kwa kuoa wake wawili au
zaidi.
Katika
shairi la “Fikra za Waungwana” mwandishi anasema;
“Mume wangu nakupenda, Josefu amenikuna
Nimekula naye tunda, nampendelea sana,
Ila usifanye inda, mimi ni wako kimwana,
Nitaishi kwa mpango, kwako na kwake Josefu.”
Msanii
anajadili dhamira hii kupitia mhusika
Anna.Katika shairi hili, Anna ana mume wake (Nania) lakini kwa upande mwingine
anampenda Josefu ambaye ni mume wake wa
pili. Anna haoni sababu ya kutokuwa na wanaume wawili.
Msanii anaonesha
kuwa uhuru anaoutaka Anna ni wa kuishi au kuwa na wanaume wawili na huo ndio
msimamo wa Anna.
Hata baada ya
kesi yake kupelekwa mahakamani,Anna alibaki na msimamo huo huo.Hali kadhalika
majaji walishindwa kutoa hukumu,kwani hakuna sheria inayozuia mwanamke kuwa na
wanaume wengi kama walivyo wanaume ambao huwa na wanawake wengi.
Lakini
swali la kujiuliza ni kuwa, je mwanamke
ana haki ya kuwa na wanaume wawili katika jamii?,Hakuna sheria inayomzuia
mwanamke kuwa na wanaume wawili lakini mila na desturi ndiyo zinazomzuia
mwanamke kuwa na waume wawili. Hivyo ni kutokana na kasoro hizo ndiyo maana
anapinga kasoro hizo,kudai uhuru wake wa kuolewa na wanaume wawili kwa wakati
mmoja kama mwanaume anavyooa wake wawili au zaidi kwa wakati mmoja. Hivyo
anaishauri jamii kuona inaweka wazi sharia zinazohusiana na suala hili.Majaji
walishindwa kuhukumu kesi ya Nania- hii ni kwasababu hakuna kifungu cha sheria
kinachomzuia mwanamke kuolewa na wanaume wawili kwa wakati mmoja.
UJUMBE
v
Ni
lazima tujitoe mhanga ili kutetea wanyonge
v
Dhuluma,unyonyaji,kutowajibika
pamoja na uongozi mbaya ni baadhi ya vikwazo vinavyokwamisha ujenzi wa jamii
mpya.
v Mashindano ya
kutengeneza silaha kwa mataifa makubwa huhatarisha amani duniani.
v Demokrasia ya
kweli ndiyo njia pekee ya kuendeleza mfumo wa mageuzi hapa nchini na katika
nchi nyingine za ulimwengu wa tatu.
v Mgawanyiko wa
watu katika matabaka husababisha kukosekana kwa umoja na mshikamano katika jamii.
v Mapenzi ya dhati
yanahitajika katika jamii na ni lazima yadumishwe. Mapenzi ya ulaghai yapigwe
vita kwa hali zote.
v
Suala
la mapenzi na ndoa waachiwe wawili wanaopendana na si maamuzi ya wazazi.
FALSAFA
Ø
Mwandishi
anaamini itikadi itakavyowatetea wanyonge, yenye kuleta haki na usawa kwa kila
mtu. Analaani wizi, dhuluma,udikteta,unyonyaji na kila aina ya uovu.Vile vile
anatetea uhuru katika mapenzi na ndoa.
MSIMAMO
Ø
Mwandishi
wa diwani hii ana msimamo wa kimapinduzi kwani ameonesha matatizo mbali mbali
yanayozikumba jamii zetu na mbinu za kuondokana na matatizo hayo. Miongoni mwa
matatizo hayo ni uongozi mbaya, ulanguzi, dhuluma,rushwa,n.k pamoja na namna ya
kuyatatua matatizo hayo.
FANI
1. MTINDO
Mwandishi
wa diwani ya UCHUNGU TAMU ametumia mitindo ifuatayo:-
(a) Mtindo wa
masimulizi
Ni mtindo ambao mwandishi au mshairi anamuumba
mhusika katika shairi akisimulia hadithi ili kufikisha maudhui yaliyokusudiwa
kwa jamii.Mashairi yaliyotumia mtindo huu katika diwani hii “Chatu na Kuku”, “Dakitari Askari”, “Thomas na Doto” na “Manzese Mpaka Ostabei” .Mashairi
haya unapoyasoma utadhani unasoma hadithi kuliko tungo za kishairi.
Katika
shairi la “Chatu na Kuku” , Babu
anaonekana akimsimulia Mjukuu wake hadithi baina ya marafiki wawili, ambao ni Chatu
na Kuku.Mwandishi
anaonesha masimulizi ya Babu kama ifuatavyo:-
“… … hapo zamani sana,
Katika
enzi zao za ujana,
Asemacho
alikiona.
Ati chatu aliwahi kuwa rafiki ya kuku,
Mie nikaguna kwa dukuduku,
Labda chatu wa mbali si wa huku,
Si chatu yule mwenye mabaku.
… … Naam hadithi ikasonga,
Chatu na kuku wakala amini,
“Tushirikiane
tusifanyiane maovu,
Lakini kila mmoja akae kwake!”
Katika
shairi la “Manzese Mpaka Ostabei” ,kuna
mianzo maalumu ya kifomula ya hadithi za fasihi simulizi kama ifuatavyo:-
“Hadithi njoo,
Manzese uende,
Kariakoo
upite,
Mwisho wako Ostabei …
… … Na hadithi
ikaawa,
Tamu na isoisha
hamu”.
(b) Mtindo wa tenzi
Ni
mtindo ambao mshororo (mstari) mmoja wa shairi huundwa na kipande kimoja tu.
Aghalabu,mshororo mmoja na ubeti wa shairi la mtindo wa tenzi huwa na mizani
(silabi) kati ya 6 hadi 11 tu.
Tenzi
huwa na ulinganifu wa silabi za mwisho kwa kila mshororo au mtari wa
ubeti.Mashairi yaliyotumia mtindo wa tenzi katika diwani hii ni “chanzo ni
Wenye Kauli”, “Wimbo Wake
Hotubani”,“Kademokrasi Katoweka” . “Wengine Wabaki Taabuni” , “Shairi la
Udongoni”.
“Usiwe Mwonja
Asali na “Takumbuka Daima” .Kwa mfano,
katika shairi la “Takukumbuka Daima” , mshairi anasema;
“Takukumbuka daima,
Kazi ikija
hatima,
Nitarudi
himahima,
Nikuone wa
heshima.
Wajua moyo
wangu,
Kwako hauna
ukungu,
Kukuaga ni
uchungu,
Kama kuikosa
mbingu”.
( c ) Mtindo wa kidato
Ni
mtindo ambao mshairi hutumia baadhi ya mistari iliyofupishwa maneno au silabi
tofauti na mistari mingine ambayo huwa na silabi au maneno mengi.Mbinu ya
kidato hutumiwa na mshairi kwa lengo maalumu hususani katika kufikisha ujumbe
wake kwa jamii iliyokusudiwa.Mashairi yaliyotumia mtindo huu katika diwani hii
ni “Chungu Tamu” , “Chatu na Kuku”
,“Dakitari Askari” , “Wanajua Kuvumilia”,”Ngulu Wapaona” , “Chungu na Tamu
,“Thomas na Doto” na “Manzese Mpaka Ostabei” . Katika shairi la “Chungu Tamu ,Mshairi anasema:
“Mekumbusha pia
matumaini,
Ya wale walio
chini,
Wavuja jasho la
ziada,
Na kunyimwa
faida.
Matumaini yao,
kesho kuwa nafuu,
Sikwamba wende
juu,
La, ila angalau
wasile makombo,
Ya mfumo
ulo kombo”
( d) Mtindo wa
majibizano
Ni
mbinu inayotumiwa na wasanii kuumba wahusika wa kazi za kifasihi wanaozungumza
kwa kupokezana.Mashairi yaliyotumia mtindo wa majibizano katika diwani hii ni “Chatu na Kuku” na “Dakitari Askari. Katika shairi la “Chatu na Kuku” kuna
majibizano kati ya Babu na Mjukuu kama ifuatavyo:-
“Babu akageuza
kiazi kisiungulie,
Akasema tulia
“”mzee”.
Ati mie
“mzee!
Vuli kumi na
tano zilikuwa bado kwangu
Niliuliza: “Kuku
alizikwaje?”
Ati kuku
walichimba kwa mikono na kucha,
Na chatu
alitumia meno yake,
haya!
Nilimuuliza babu
tena,
“Hadithi ya kweli?”
Babu akameza
funda la kiazi na maji”
Katika
shairi la “Dakitari Askari” kuna majibizano
kati ya Evadora Wesana na Adam Kiende, pia Luteni Bwege na Kapteni Adam Kiende,
kama ifuatavyo:-
“Kweli wewe
nasoma Makerere,
Na hii Kapteni
yetu,
Yeye napenda
wewe,
Cheo gani iko
ndani ya jeshi ya adui?”
“Kapteni”,
nilijbu.
Luteni akauliza,
“Doctors where college?
Safari hii
nikaogopa makofi,
“Makerere”. Jibu fupi.
( e) Mtindo wa
kuhoji
Ni
mtindo unaotumiwa na washairi wa kuuliza maswali ambayo ama majibu yake yako
wazi au hayako wazi.Mashairi yaliyotumia mtindo wa kuhoji katika diwani hii ni
pamoja na “Thomas na Doto”, “Chatu na Kuku”, “Dakitari Askari” na “Manzese Mpaka Ostabei”.
Katika
shairi la “Thomas na Doto”, mtindo wa kuhoji (kuuliza maswali) umetumika ka
ifuatavyo:-
“Kwahiyo mama
alia,
Mzee afoka kwa
kukemea,
Kwa nini mweusi
wachukua?
Weupe
hujajionea?
Wakasema
wakasema,
Thomas kimya
kainama”.
Katika
shairi la “Dakitari Askari”, mtindo wa kuhoji (kuuliza maswali) umetumika
katika beti hizi;
“Kweli wewe
nasoma Makerere,
Na hii Kapteni
yetu,
Yeye napenda wewe,
Cheo gani iko
ndani ya jeshi ya adui?
“Kapteni”, Jibu
fupi
Luteni
akauliza.
“Doctors where
college?
Safari hii
nikaogopa makofi,
“Makerere” Jibu
fupi.
( f ) Mtindo wa msisitizo au takriri
Ni
mtindo ambao neno moja linatokea mwanzoni na linarudiwa katika mishororo au
mistari ya ubeti wa shairi.Shairi lililotumia mtido wa msisitizo au takriri
katika diwani hii ni “Manzese Mpaka Ostabei” .Mshairi anasema:
“Sijui,
Je hiyo harufu ya dhuluma,
Je vishindo vya majambazi,
Je, je, je … … je, nyingi,
Jiji
salama,
Watu hadaa,
Yayumkinika,
labda.
Hadithi
yawanogea,
Naona mwajiramba
na kutumbua macho,
Kigori anawababaisha,
Kigori mke wa Kitwana,
Wote weusi wa
mkaa,
Jirani zao
waliwatania, … …
Ndiyio,
Dorothy alikuwa binti Shibe,
Dorothy rafiki yake Mashaka,
Mashaka bini
njaa,
Njaa ya kila kitu,
pamoja nay a kupendwa … …”
( g ) Mtindo wa
kikufu au pindu
Ni
mtindo ambao neno au sehemu ya neno ya mshororo inayomalizia huanzia katika
mshororo (mstari) wa ubeti unaofuata.Shairi lililotumia mtindo wa kikufu au
pindu katika diwani hii ni“Manzese Mpaka Ostabei” . Mshairi anasema:
Ndiyo,
Dorothy alikuwa
binti Shibe,
Dorothy rafiki
yake Mashaka,
Mashaka bini njaa,
Njaa ya kila kitu, pamoja na ya
kupendwa… …”
( h) Mtindo wa
nafsi
Ni mtindo ambao mshairi anaaweza kutumia nafsi
umoja, nafasi wingi au nafasi kundi kwa lengo la kufikisha ujumba ua maudhui
Fulani kwa jamii. Kuna nafasi za aina
tatu (3), yaani nafasi ya kwanza (umoja na wingi), nafasi ya pili (umoja na wingi)
na nafasi ya tatu (umoja na wingi). Mwandishi wa diwani hii ametumia mtindo wa
nafasi kama ifuatavyo:
(i) Matumizi ya nafsi umja (nafsi ya pili umoja)
Katika
mtindo huu mshairi huzungumzia jambo au suala linalomhusu mtu mmoja pekee. Hujumuisha sifa,mawaidha na maonyo.Mashairi
yaliyotumia mtindo wa nafsi ya pili umoja katika diwani hii ni “Usiwe Mwonja Asali” na “Ngulu Wapaona” . Kwa mfano katika shairi la “Usiwe Mwonja
Asali” (uk. 36-37), mshairi anasema:
“Basi umwitaye
mwali,
Yafaa umwache
mbali,
Umwambie kwa
kauli,
Ukishamjua
hali,
Sahau kamba ni
mwali,
Usiwe mwonja
asali”.
(ii) Matumizi ya nafsi wingi (nafsi ya kwanza
wingi)
Katika
mtindo huu mshairi huzungumzia jambo au suala linalohusu kundi fulani la
watu,akiwemo na yeye mwenyewe.Mashairi yaliyotumia mtindo wa nafsi ya kwanza
wingi katika diwani hii ni “Chini ya mti
Mkavu” , na “Chanzo ni Wenye Kauli”.
Kwa mfano katika shairi la “Chini ya Mti Mkavu”, mshairi anasema:
“Tulio wengi
twajua, hawa wanatudhulumu,
Chakula kutumezea,
kwa niaba ya kaumu,
Kwa maringo
watembea, matumbo yenye karamu,
Lakini yajulikana,
kujua tu haitoshi”
(iii) Matumizi ya nafsi kikundi (nafsi yatatu
wingi)
Katika
mtindo huu mshairi huonekana ama akitoa hotuba, akisimulia hadith au akizungumza
na kundi fulani la watu kuhusu suala au jabo
muhimu.Mashairi yaliyotumia mtindo wa nafsi ya tatu wingi katika diwani
hii ni “Mjanja Yu Mashakani”, “Wanajua
Kuvumilia”, “Chatu na Kuku” , “Chungu Tamu”, “Dakitari Askari”. “Thomas na
Doto” (uk. 37-42) na “Manzese Mpaka Ostabei”. Kwa mfano katika shairi la “Mjanja Yu
Mashakani”, mshairi anasema:
“Na wengi
wametambua, ukweli ulifichika,
Wongo
wameugundua, hasira zimewawaka,
Hasira
isopungua, kwa ishirini miaka,
Mana
ililimbikizwa na kusakamwa moyoni”
( j) Mtindo wa kuandika jibu katika mashairi
Mwandishi
ameonesha upekee wake katika kuandika diwani kwa kutunga shairi lenye
jibu.Mtindo wa kuandika jibu katika mashairi umejitokeza katika shairi la
“Takukumbuka
daima”
.Mshairi anasema:
“Moyoni
nitatetema,
Kukuaga wangu
mwema,
Ulaya
mmenituma,
Nashukuru kwa
heshima.
Takukumbuka
daima,
Kazi ikija
hatima,
Nitarudi
himahima,
Nikuone wa
heshima”
Jibu:
“Safari na iwe
njema,
Nakutakia
uzima,
Nitauguza
mtima,
Takukumbuka
daima”.
2. MUUNDO
Mwandishi
wa diwani ya CHUNGU TAMU ametumia miundo tofautitofauti kwa kuzingatia vigezo
mbalimbali kama ifuatavyo:-
Ø Kigezo cha idadi ya mishororo:
Kwa
kuzingatia kigezo cha idadi ya mishororo kwa kila ubeti,mshairi ametumia miundo
ifuatayo:-
(a) Muundo wa
tarbia
Ni muundo ambao kila ubeti unaundwa na mistari
minne.Mashairi yaliyotumia muundo wa tarbia katika diwani hii ni “Chungu Tamu” , “Tishio la Binadamu” , “Chatu
na Kuku” . “Chini ya Mti Mkavu” . “Mjanja Yu Mashakani” , “Wanajua Kuvumilia” , “Radi ya Kiangazi”
, “Shairi la Udongoni” , “Fikira za
Waungwana” , “Mfereji Maringo” na
“Takukumbuka Daima”.Kwa mfano, katika shairi la “Chini ya Mti Mkavu”, mshairi anasema:
“Tulio wengi
twajua, hawa wanatudhulumu,
Chakula
kutumezea, kwa niaba ya kaumu,
Kwa maringo
watembea, matumbo yenye karamu,
Lakini
yajulikana kujua tu haitoshi”.
(b) Muundo wa takhmisa:
Ni
muundo ambao kila ubeti unaundwa kwa
mistari mitano.Mashairi yaliyotumia muundo wa takhmisa katika diwani hii ni
“Kademokrasi Katoweka” na “Wengine
Wabaki Taabuni” . Kwa mfano, katika
shairi la “Kademokrasi Katoweka”
(uk.30-31), mshairi anasema
“Barani mabavu
yatumika,
Dikiteta asije
anguka,
Na majungu pia
ayapika,
Udikiteta pasi
shufaka,
Nasimulia ya
Afrika”.
(c) Muundo wa sabilia
i
muundo unaohusu mashairi yanayoundwa kwa mistari sita na kuendelea katika kila
ubeti. Mashairi yaliyotumia muundo wa
sabilia katika diwani hii ni “Dakitari
Askari”,“Chanzo ni Wenye Kauli” ,
“Wimbo Wake Hotubani” , “Ngulu Wapaona” , “Chungu na Tamu”, “Usiwe Mwonja Asali” , “Thomas na Doto” , “Manzese Mpaka
Ostabei” na “Wasia” . Kwa mfano katika shairi la “Usiwe Mwonja
Asali” , mshairi anasema:
“Basi umwitaye
mwali,
Yafaa umwache
mbali,
Umwambie kwa
kauli,
Ukishamjua
hali,
Sahau kamba ni
mwali,
Usiwe mwonja
asali”.
Ø Kigezo cha idadi ya vipande:
Kwa
kuzingatia idadi ya vipande kwa kila mshororo katika ubeti wa shairi,
Mwandishi
wa diwani ya CHUNGU TAMU ametumia miundo ifuatayo:
(a) Muundo wa kipande kimoja (ukwapi)
Ni
muundo ambao kwa kila mshororo (mstari) wa ubeti wa shairi kunakuwa na kipande
kimoja tu. Mifano ya mashairi ya muundo
wa kipande kimoja katika diwani hii ni “Chungu Tamu” (uk. 1) “Chatu na Kuku”
(uk.2-10), “Wanajua Kuvumilia” (27),
“Shairi la Udongoni” (uk.35-36), “Takukumbuka Daima” (57), “Wasia”
(uk. 58), “Thomas na Doto” (uk.
37-42), “Usiwe Mwonja Asali” (uk. 36-37),
“Chungu na Tamu” (uk. 34-35), “Ngulu Wapaona”
(uk.33-34), “Wimbo Wake Hotubani”
(uk. 29-30) na “Chanzo ni Wenye Kauli” (uk. 28). Kwa mfano, katika shairi la “Takukumbuka
Daima” (uk. 57), mshairi anasema:
“Moyoni
nitatetema,
Kukuaga mwangu
mwema,
Ulaya
mmenituma,
Nashukuru kwa
heshima”
(b) Muundo wa vipande viwili (ukwapi na utao):
Huu
ni muundo ambao kw akila mshororo (mstari) wa ubeti wa shairi kunakuwa na
vipande viwili, yaani kipande cha kwanza (ukwapi) na kipande cha pili
(utao). Mifano ya mistari ya muundo wa
vipande viwili katika diwani hii ni “Tishio la Binadamu” (uk.1-2), “Chini ya
mti Mkavu” (uk.10), “Mjanja Yu Mashakani”
(uk.26-27), “Radi ya Kiangazi”
(uk.32-33), “Fikira za Waungwana” (uk. 54-56)mshairi anasema:
“Ana
unanichukia, si ajabu hunitaki,
Sijui nilokosea,
kwako mimi sipendeki,
Josefu nd’o
wamjua, wampenda kwa malaki,
Ana wangu wa
nyumbani, sema nakusikiliza”.
Ø Kigezo cha aina ya vituo:
Kwa
kuzingatia kigezo cha aina ya vituo, mwandishi wa diwani ya CHUNGU TAMU
ametumia muundo wa kituo kimalizio. Kitu
kimalizio ni mstari wa mwisho wa ubeti wa shairi ambao haujirudirudii kwa kila
ubeti. Hii ina maana kuwa kwa kila ubeti
wa shairi kunakuwa na mstari wa mwisho (kituo) wa tofauti na usiofanana na beti
nyingine. Mashairi yote ya diwani hii
yametumia muundo wa kituo kimalizio.
Katika
shairi la “Chini ya Mti Mkavu” (uk.10), mshairi anasema.
“Yametusibu
jamani, wote tulio nchini,
Mioyo yaenda
chini, kicheko cha maskini,
Twajilamba
midomoni, hatunacho cha tumboni,
Utii umetuponza, laiti tungelijua.
Tulio wengi
twajua, hawa wanotudhulumu,
Chakula
kutumezea, kwa niaba ya kaunu,
Kwa maringo
watembea, matumbo yenye karamu,
Lakini yajulikana, kujua tu haitoshi”,
Katika
Shairi la “Chungu Tamu ” (uk. 1),
mshairi anasema:
“Mekumbusha pia
matumaini,
Ya wale walio
chini,
Wavuja jasho la
ziada,
Na kunyimwa faida.
Matuini yao,
keshokuwa nafuu,
Si kwamba uende
juu,
La, ila angalau
wasile makombo,
Ya mfumo ulo kombo
3. MADHARI
Mshairi
wa diwani ya CHUNGU TAMU ametumia mandhari yafuatayo:-
(a) Mandhari ya bara la Afrika.
Mshairi
anazungumzia matatizo mbalimbali yanayolikabili bara la Afrika, zikiwemo nchi
za Tanzania na Uganda, kupitia mashairi ya “Dakitari Askari” (uk. 11-26), “Kademokrasi Katoweka” (uk.30-31). “Thomas na Doto” (uk.37-42) na
“Manzese Mpaka Ostabei” (uk. 42-54).
Baadhi ya maeneo ya Tanzaniayanayotajwa ni Ostabei, Manzese, Buguruni, Bukoba,
Kagera, Forodhani, Tabora na Shule ya Sekondari Mchanganyiko iliyopo Dar es
Salaam. Eneo la Uganda linalotajwa ni
Chuo Kikuu cha Makerere, Mandhari ya bara la Afrika yanaibua dhamira za
umasikini, uonevu, dhuluma, udikteta, uongozi mbyaya, unyonyaji, athari za
vita, ukombozi, usaliti, matabaka na mapenzi.
(b) Mandhari ya nchi za Urusi na Marekani.
Mshairi
anajadili namna nchi zilizondelea, zikiwemo Urusi na Marekani, zinavyoona
ufahari kushindana kutengeneza silaha za moto, kama vile mabomu na silaha
nyingine za kisasa. Mshairi anahofia
kutokea vita ya tatu ya dunia. Mshairi
anatumia mandhari haya katika shairi la “Tishio
la Binadamu” (uk. 1-2). Mandari
ya nchi za urusi na Marekani yanaibua dhamira za athari za vita, ukombozi wa
kifikra, ukombozi wa kisiasa, hofu udikteta na ufahari.
(c) Mandhari mengine yanayotajwa katika diwani
hii ni hotelini, baa, jeshini, nyumbani kwa kuku, nyumbani kwa chatuk msituni,
kambini, ufukweni na jikoni
4. WAHUSIKA
Mwandishi
wa diwani ya CHUNGU TAMU ametumia baadhi ya wahusika waliotajwa majina yao
waziwazi kama ilivyo katika riwaya na tamthiliya kama ifuatavyo:-
(a) Katika shairi la “Dakitari Askari”(uk.
11-26), mshairi ametumia wahusika wafuatao:
Adam Kiende, Evadora Wesana, Luteni Bwege, manesi, Meja Mtanda, Josefu
Manyai, Idi Amini Dada na Daktari Ngalakere.
(b) Katika shairi la “Thomas na Doto” *uk.
37-42(, mshairi ametumia wahusika wafuatao:
Thomas, Doto, Mzee Roland (Baba wa Thomas), Rosalind (mama wa Thomas) na
Roda (dada wa Thomas).
(c) Katika shairi la “Manzese Mpaka Ostabei”(uk.
42-54), mshairi ametumia wahusika wafuatao:
Dorothy, Mashaka, Waziri Jonathan Shide (baba wa Dorothy), mama Dorothy,
baba Mashaka, mama Mashaka na Gabrieli (mtoto wa Waziri wa Ulanguzi, msomi na
jirani wa kina Dorothy).
(d) Katika shairi la “Chatu na Kuku” (uk. 2-10),
mshairi ametumia wahusika wafuatao:
Chatu, Kuku, Paku, Watoto wa Nyoka na Vifaranga vya Kuku.
Kadhalika,
mwandishi wa diwani ya CHUNGU TAMU ametumia wahusika vikundi kama ifuatavyo:-
(a) Wahusika wanasiasa
Mshairi
amewatumia wahusika wanasiasa katika mashairi ya “Chungu Tamu” (uk.1), “Chini
ya Mti Mkavu” (uk. 10), “Mjanja Yu Mashakani” (uk. 26-27), “Wanajua Kuvumilia”
(uk.27), “Wimbo Wake Hotubani” (uk. 29-30), “Shairi la Udongoni” (uk. 35-36) na
“Chanzo ni wenye Kauli” (uk. 28).
Wahusika hawa wanawakilisha yafuatayo:-
v Tabaka la juu (tawala) linalonyonya, linalodhulumu,
linaloonea na linalokandamiza tabaka la chini.
v Viongozi
wasiowajibika na wazembe.
v Viongozi
wanaoongoza kidikteta (kwa mabavu).
v Viongozi
wasaliti na wanaotumia mali za umma kwa maslahi yao binafsi.
(b) Wahusika wakulima (walima korosho na mihogo),
wavujajasho, watwana, punda na ngamia.
Mshairi
amewatumia wahusika hawa katikamashairiya “Chungu Tamu” (uk.1), “Chini ya Mti
Mkavu” (uk.10), “Mjanja Yu
Mashakani” (uk.26-27), “Wanajua
Kuvumilia” (uk. 27) na “Wimbo Wake Hotubani” (uk.29-30). Wahusika hawa wanawakilisha watu wa tabakala
chini, masikini na wanaonyonywa na kukandamizwa na watu wa tabaka la juu
(viongozi na matajiri)
(c) Wahusika waganga (madaktari, matabibu,
manesi).
Mshairi
amewatumia wahusika hawa katika shairi la “Dakitari Askari”(uk. 11-26)
kuwakilisha watu wachapakazi, wazalendo, wawajibikaji na wenyekujitolea katika
kazi yao ya utabibu na majukumu mengine wanayopewa.
(d) Wahusika mapadri.
Mshairi
amewatumia wahusika hawa katika shairi la “Daktari Askari” (11-26) kuwakillisha
watu wavumilivu, waaminifu, wanyenyekevu na wanaojitolea maisha yao kueneza
habari za Mungu bila malipo yoyote.
Mshairi anawawakilisha watu wanaofanya kazi za wito; wasiofikiria
kulipwa chochote. Kimsingi watu wasio na
wito hawawezi kuvumilia kazi ya kumtumikia Mungu kupitia upadri. Mshairi anaeleza kuwa Adam Kiende na wenzake
walijiunga namafunzo ya upadri. Mshairi
anaeleza kuwa Adam Kiende na wenzake walijiunga na mafunzo ya upadri wakidhani
watapata raha eti kwa vile walikuwa wanaona mapdri wanapelekewa mikate na
vinono vingine, lakini walishindwa kuendeleakwa sababu hawakuwa na wito.
MATUMIZI YA LUGHA
Aina
ya lugha iliyotumika ni sanifu yenye misemo,nahau na methali, tamathali za
semi,mbinu nyingine za kisanaa pamoja na ujenzi wa taswira.Lugha ya kishairi
yenye uchaguzi maalum wa maneno (diction) imetumika.
MISEMO, NAHAU NA
METHALI
·
Imetumiwa
na mwandishi kwa lengo la kuwasilisha ujumbe kwa jamii husika. Mfano:-
Ø Sasa mwaleta
shari (msemo) – uk 7
Ø Umoja ni nguvu
(methali) –uk 6
Ø Kuvaa
masulupwete (msemo) – uk 48
Ø Ndoa ni fumbo
(msemo) – uk 42
Ø Usinawe kwa
ulimbo (msemo) – uk 42
Ø Mapenzi hayana
mipaka (msemo) – uk 40
Ø Utajichimbia
kaburi (msemo) – uk 9
Ø Lakini haikutiwa
chumvi mitaani (msemo) – uk 12
TAMATHALI ZA
SEMI
TASHIBIHA
Ø
Maoni
yetu chakavu,sawa nguo ya miaka (uk 2)
Ø
Macho
yao mekundu mithili wavuta bangi (uk 6)
Ø Kwa msikilizaji
husisimua mithili filamu za wachunga ng’ombe
Ø Shaba kama maji
(uk 12)
Ø Kichwa chake
kama cha kifutu (uk 38)
Ø Mwili ukamjaa
harara kama jini lililokosa mbuyu (uk 41)
Ø Tumbo lake kubwa
kama pipa (uk 50)
Ø Kichwa kidogo
kama cha chatu (uk 50)
Ø Mweusi kama
kiatu cha jeshi (uk 50)
Ø Utaonekana kama
kinyago cha kuchonga (uk 12),n.k.
TASHIHISI
v Kifo kimeniita
(uk 4)
v Njaa inawasaliti
(uk 6)
v Kicheche pia
ameapa (uk 7)
v Huzuni
imenisaliti (uk 10)
v Katika ile
baridi kali,mabomu ya mikono,yakatubusu miguuni (uk 16)
v Vichaka
vikawakaribisha (uk 38)
v Taa za waka kwa
maringo (uk 44)
v Jiji lasema hali
ngumu (uk 44)
v Mapenzi hayana
mpango, yakikanywa zaidi,hayana akili ati (uk53)
v Mioto ikapasua
anga (uk 11), n.k.
SITIARI
§
Ushairi
ni sukari tamu (uk 1)
§
Utoto
ni kito (uk 2)
§
Yeye
alisema dunia ni raha na tabu (uk 2)
§ Umaskini ni
mzigo (uk 11)
§ Wote weusi wawa
mkaa (uk 45)
TAFSIDA
·
Usiwe
mwonja asali (uk 37)
·
Walipenda
faragha (uk 51)
·
Dora
ana kitu tumboni (uk 54)
·
Nimekula
naye tunda (uk 56)
TABAINI
v Kuwaza na
kuwazua
v Lakini usikubali
raha tu, kumbuka na karaha (uk 13)
v Aponya aua
(uk 17)
KEJELI
·
Nyie
yawafalia,mfanyakazi ya kuchoma na kuuza mkaa (uk 45)
·
Wa
Manzese atakulisha taka (uk 52)
·
Jina
lenye ugonjwa wa kaka (uk 52)
·
Iweje
binti shibe aende kwa omba omba (uk 52)
DHIHAKA
Ø Ati mchumba,
mchumba siye Baraka (uk 52)
MBINU NYINGINE ZA KISASA
TAKRIRI
Ø
Mateka,
mateka wapenzi (uk 22),
Ø
Adamu,
machozi (uk 20)
Ø
je
je, je….je nyingi (uk 43),
Ø
Mateka,
Mateka, wapewa (uk 22)
Ø Tukanyata,
tukanyata tukakaribia Mbarara (uk 16)
MDOKEZO
Ø
Je
je je…je nyingi (uk 43)
Ø
Si
mganga wa tunguli…(uk 14)
Ø Sijui yaah
yaah…(uk 44)
Ø Sijui
Mashaka…(uk 53)
Ø Kati yao
huyu…!(uk 51)
Ø Profesa Idd
Amin…(uk 19)
Ø Ikawa nakupenda
lakini…
NIDAA
·
Ati
mie mzee1!
·
Ghafla
mwewe huyu!
·
Umeshituka!
·
Mwauzunika
nini!
·
Kwa
hamu ya umoja!
TASHTITI
v Hujisikia wezi
wakiomba Mungu kabla ya kwenda huko waendako? (uk 13)
v Wewe mwana
–kibarua, hujioni? (uk 49)
MJAZIO
Ø Twaona
wanaopelekewa chai, mikate, karanga, mayai…(uk 13)
Ø Ndugu mwenyekiti
nadhani, labda, pengine, ningependekeza, kwa maoni yangu, kwa mfano
tungeliweza….(uk 15)
ONOMATOPEA(TANAKALI SAUTI)
·
Lo!
(uk 4)
·
Loooo!
(uk 20)
LUGHA YA KIINGEREZA
·
Movement
order (uk 14)
·
Surrender
(uk 17)
·
Doctor
where College? (uk 18)
·
Life
President? (uk 19)
·
-Good
Doctor (uk 19)
·
My
first fiancé (uk 20)
·
But
this is war sir (uk 20)
·
Look
Adam. My parents are dead. I am alone (uk 23)
·
Sir
is that a request or an order? (uk 24)
·
Two
doctors fighting for no reason (uk 25) n.k.
TAFASIRI YA
MOJA KWA MOJA
Ø
Fomu
wani (uk 48)
UJENZI WA TASWIRA
Mwandishi
ametumia baadhi ya taswira ili kufikisha ujumbe kwa jamii aliyoiandika. Baadhi
ya taswira hizo ni kama vile:-
v
Chatu
(uk 2)…..Inawakilisha wadhulumaji (wakoloni)
v Kuku
(uk2)……Inawakilisha wadhulumiwa (Waafrika)
v Vifaranga (uk
9)….Inawakilisha mali ghafi
v Mjanja (uk
25)….Viongozi wanaoshikilia mfumo wa chama kimoja
v Watwana (uk
25)….Wananchi wanaotaka mabadiliko au uongozi mbovu
v Ngulu (uk
33)….Vijiji, sehemu isiyo na maendeleo, sehemu iliyosahaulika
v Zabibu (uk
42)…..Msichana au mwanamke
MANDHARI
Kitabu
hiki kiliandaliwa miaka ya 1980. Na matukio yanayosimuliwa katika kitabu hiki
yanazungukia nchi za Afrika ya Mashariki hususani Tanzania na Uganda. Hata
hivyo, maudhui ya kitabu hiki yanasadifu kipindi hiki cha sasa katika nchi yoyote ile ulimwengu wa
tatu.
JINA LA KITABU
Jina la diwani
hii“Chungu Tamu’’ linasadifu yaliyomo ndani ya kitabu. Msanii ameonesha kuwa,
baada ya kupita katika machungu na kuamua kupambana nayo ndipo utamu utafuata.
Anaitaka jamii itumie kila mbinu kupambana na vikwazo vinavyokwamisha jamii
isiweze kuupata utamu (ujenzi wa jamii mpya endelevu).Aidha msanii anaonesha
kuwa katika maisha,uchungu na utamu havitengamani.Vile vile msanii ameonesha
dhahiri kuwa, wananchi wa kawaida ambao ndio wazalishaji wanakula “Chungu”
lakini viongozi ambao si wazalishaji wanakula “Tamu”.
KUFAULU KWA
MWANDISHI
KIMAUDHUI
Mwandishi
ameongelea masuala ambayo yanaisakama jamii yetu katika wakati huu tulio nao.
Ameonesha mbinu mbalimbali za kufuata ili kufanikisha suala zima la ujenzi wa
jamii mpya.
KIFANI
Mwandishi
amefaulu kutumia miundo changamano,mitindo changamano,lugha ya kishairi pamoja
na ujenzi wa taswira.
KUTOFAULU KWA
MWANDISHI
v
Lugha
imejaa taswira kwa kiasi kikubwa na hivyo msomaji wa kawaida hawezi kuambulia
ujumbe wowote.Hivyo amewanyima baadhi ya wasomaji uhondo wa kazi yake.
v Msanii metumia
lugha ya Kiingereza (kigeni) katika baadhi ya mashairi.Huu ni udhaifu wa
mwandishi,kwani anakinyima Kiswahili sanifu nafasi ya kuenea.Vile vile kwa mtu
asiyefahamu Kiingereza atashindwa kupata ujumbe.