TAHAKIKI-FUNGATE YA UHURU
DIWANI : FUNGATE
YA UHURU
MWANDISHI:
MOHAMED S. KHATIBU
WACHAPISHAJI:
DUP
MWAKA: 1988
UTANGULIZI
Fungate
ni kipindi cha siku saba baada ya harusi.Ni kipindi ambacho Bwana na bibi
harusi hula na kunywa tena milo ya kuchagua wakati wote wa fungate.Fedha na
vifaa vitumiwavyo na maharusi huwa ni vya kuazima au kuchangiwa(si lazima viwe
vyao) Wanapewa kutoka kwa ndugu na jamaa
zao na wanawekewa vijana wa kuwahudumia.Wachangaji hufanya hivyo kwa sababu
wanajua kuwa fungate ni ya muda mfupi(siku saba tu),hivyo huvumilia.
Fungate
ni lazima iwe na kikomo.Ikizidisha kikomo hicho ibadili jina labda iitwe
unyang’anyi,ulimbwende,uvivu,uzembe au jina lolote lenye kashfa hasa unafiki au
usaliti.Mwandishi wa diwani hii ameimwaga ghadhabu hiyo kwa hao maharusi
waliohesabu ukarimu waliotendewa kuwa ni
upumbavu.
Uhuru
ni neno linalopendwa sana na wanasiasa wa ubepari au ujamaa.Hekaheka za
uhuru(kudai,kuomba au kupigania) zinaweza kufananishwa na shughuli za kutafuta
mchumba,kupeleka posa kulipa mahari,na kufunga ndoa.
Katika
kipindi chote cha uhuru, watu, hususani viongozi,hufurahi na kufanya sherehe
ambazo huwagharimu raia-mali na vitu mbalimbali.Lakini kwa kuwa uhuru ni kitu
cha thamani kama maharusi,raia hukubali kugharimia sherehe hizo.Lakini sherehe
za uhuru kama fungate hutazamiwa iwe ya muda mfupi –labda mwezi mmoja au miwili.
Raia wanchi
zilizopata uhuru barani Afrika walikuwa na shauku ya kupata maendeleo lakini
hawajafikia lengo lao hadi sasa kwa sababu viongozi wetu wanaendeleza Fungate
ya Uhuru.Hivyo viongozi wanchi za Afrika wamewasaliti wananchi wao
waliowachagua.Katika utangulizi mwandishi anasema;
Nikate tamaa?
Kwani twendavyo hatufiki,
Vile ipasavyo hayakamiliki,
Mambo yalivyo ni unafiki,
Tumesalitiwa!
MAUDHUI
Fungate
ya Uhuru ni diwani inayojadili kwa mapana sana juu ya matatizo mbalimbali
yanayokwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa Tanzania.Matatizo hayo ni kama vile
usaliti,unafiki,wizi,hujuma,udanganyifu,rushwa pamoja na uongozi mbaya.
DHAMIRA KUU: UJENZI WA JAMII MPYA.
Mwandishi
anajadili kwa kiasi kikubwa suala la ujenzi wa jamii mpya.Mwandishi
anaitaka jamii itupilie mbali unyonyaji ,uonevu,
dhuluma,udanganyifu,wizi,unafiki,umasikini,uongozi mbaya na ukandamizaji wa
watu wa tabaka la chini ili kuijenga jamii kwa upya.Jamii ambayo hatamu zote za
uongozi (utawala,siasa na uchumi) zitakuwa mikononi mwa wakulima na wafanyakazi
kwa misingi ya haki na usawa.
Itikadi ya
kujenga jamii mpya ilijengeka juu ya siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo
ilitangazwa mwaka 1967 baada ya kutangazwa kwa
Azimio la Arusha.Hadi 1988,mwandishi anaandika diwani hii anaonesha kuwa
bado hatujafanikiwa kujenga jamii mpya hapa Tanzania.Hii inatokana na sababu
zifuatazo;
Kwanza,bado kuna dhuruma, usaliti,unyonyaji na wizi
wa mali za umma.katika shairi la
“Wingu’’ mwandishi anasema;
Bado,
Wingu limetanda,
Limetanda.
Na kutughubika ghubi,
Mvua,
Lakini hainyeshi,
Hainyeshi,
Ukame umetanda waa!
Mimea,
Tulipanda kwa miongo,
Kwa miongo,
Yote imekauka!
Pia
katika shairi la “Wizi”mwandishi
ameonesha dhahiri kuwa wizi umo ikuluni,bomani,kanisani,misikitini na
hekaluni.Mwandishi ameonesha kuwa dini za wabariki wezi,polisi hulinda wezi na
majeshi huhalalisha wizi.katika ubeti wa
1 mwandishi anasema;
Wizi umo;
Kanisani,
Msikitini,
Hekaluni
Wanyang’anywao ni waumini.
Pili,Bado kuna matabaka katika jamii zetu.Mwandishi
ameonesha kuwa kuna tabaka la wenye nacho na tabaka la wasionacho.Tabaka la juu
(utawala) unaolinyonya tabaka la chini(tawaliwa).Mfano katika shairi la “Fungate”
mwandishi ameonesha jinsi tabaka tawala linavyofurahia maisha kwa kuishi katika
majumba mazuri, kutembelea magari ya kifahari, n.k.
Katika
shairi la”Waja wa Mungu”mwandishi
anaonesha jinsi tabaka la chini linavyoishi kwa shida.Kwa mfano, kula kwa
shida, kulala kwa shida, kuvaa kwa shida, hawapati elimu na huduma nzuri za
afya.
Tatu,Bado kuna uongozi mbaya katika jamii zetu.Mfano katika
shairi la “Viongozi wa Afrika”mwandishi
anashutumu vikali viongozi wanaotumia
madaraka yao vibaya na kugandamiza watawaliwa.Mwandishi
anasema;
“Viongozi
wa Afrika,
Wanaotawala kwa mabavu,
Kujifanya ni washupavu,
Wao wachache ni werevu,
Na umma wote ni mpumbavu,
Wanafiki,
Wazandiki”.
Pia
katika shairi la “Njama” mwandishi anaonesha
jinsi viongozi wanavyotumia njama mbalimbali kulinyonya tabaka
tawaliwa.Viongozi wanatumia njama mbalimbali ili kuhakikisha kuwa hakuna
anayewapinga wala kuhoji hata kidogo.
Nne,Bado kuna unyonyaji wanaofanyiwa wakulima katika
kuuza mazao yao.Mwandishi
ameonesha kuwa wakulima hunyonywa na kudhurumiwa na kupewa bei kidogo
wakati wa kuuza mazao yao.Katika shairi
la “Naona” linadhihirisha haya katika ubeti wa
6,Mwandishi anasema;
Naona
Wanakwenda gulioni
Mazao kuyazabuni
Wanapata bei duni
Na kubaki maskini
Unyonge ulele.
Kutokana
na matatizo ya wizi,rushwa,uongozi mbaya,dhuluma,
uonevu na unyonyaji ndiyo maana tumeshindwa kujenga jamii mpya.
Mwandishi ameonesha mbinu mbalimbali ambazo jamii
inapaswa kuzitumia ili kuijenga jamii
mpya na hizo ndizo dhamira ndogo ndogo
za diwani hii kama zifuatazo;
1. UONGOZI MBAYA
Uongozi
mbaya ni kikwazo kikubwa katika ujenzi
wa jamii mpya.Katika shairi la”Fungate” mwandishi ameonesha jinsi
viongozi wanavyotumia madaraka yao vibaya kwa kuwanyonya wananchi wa
kawaida.Katika ubeti wa 1 mwandishi
anasema;
Fungate ya uhuru,bado inaendelea,
“Harusi” wana nuru,wazuri wanavutia,
Wengi inawadhuru,na tena wanaumia
Mwandishi
anaeleza kuwa tangu tupate uhuru hadi leo bado viongozi wetu wapo Fungate
wakila na kunywa huku wananchi wakiendelea kuteseka na maisha magumu,hivyo
mwandishi anaitaka jamii kuung’oa
uongozi mbaya na kusimika uongozi uliobora unaowajali wananchi wake .
Katika shairi la
“Viongozi
wa Afrika”mwandishi anakemea
viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kujinufaisha wao wenyewe, wenye
hisa katika viwanda,mabenki,makampuni au mashamba ya mabepari kuwa ni
wasaliti.Mwandishi anawakemea wale viongozi wenye upendeleo,wanaotumia pesa za
umma kwa kuendeshea sherehe.Mwisho anawakemea viongozi wanaopokea rushwa na
amewaita magaidi au mafisadi.
Katika
shairi la “Utawala” mwandishi
amehimiza kuangusha utawala wa kibepari ambao unawanufaisha wachache na walio
wengi hunyonywa,hugandamizwa,huonewa na kunyanyaswa na hao wachache.
Katika
shairi la “Kinyang’anyiro” mwandishi anaonesha jinsi viongozi
walivyokimbilia kushika madaraka (hasa enzi za uhuru) lakini wanashindwa kuleta
maendeleo hapa nchini.
Kwa ujumla
mwandishi anapendekeza kuwa, ili tujenge jamii mpya lazima tuwe na uongozi
bora.
2. UMOJA NA USHIRIKIANO
Mwandishi
anaona kuwa ili tujenge jamii mpya ni
muhimu tuungane sote tuwe kitu kimoja.Katika
shairi la “Unganeni” mwandishi
anawataka wananchi wote wa Afrika kuungana ili kuendeleza mapambano ya kuleta
haki na usawa. Anasema:-
“Wafanyakazi wa Afrika,tuunganeni,
Na wakulima kadhalika,tushikaneni,
Makabwela
mnaosumbuka,tukutaneni,
Tujiandae kwa mapambano yalo marefu,
Ushindi ni wetu”.
Mwandishi
anaitaka jamii hasa tabaka la chini kuungana na kuendeleza mapambano dhidi ya
viongozi wanafiki,mabepari, mamwinyi,wanaonyonya,wanaonyanyasa,wanaowatesa,
wanaowadhulumu na kuwagandamiza watu wa tabaka la chini. Katika shairi la “Nikizipata
Bunduki‘’anapendekeza matumizi
ya silaha ili kuondokana na matatizo hayo yote.Hivyo ili tujenge jamii mpya ni
lazima tuungane tuwe kitu kimojakwani ‘’Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’.
3. UJASIRI
NA KUJITOA MHANGA
Mwandishi
anaona ili kuijenga jamii kwa upya ni
muhimu kuwa na ujasiri,kutoogopa vitisho.Katika shairi la “Gorila” ubeti wa1
mwandishi anasema;
Gorila,jasiri!
Wa Afrika,shujaa,mshupavu,umevinjari,
Mtutu shika,mevaa,ukakamavu,uko tayari,
Gorila,ruwaza,wa kizazi kipya
Mwandishi
anaitaka jamii hasa vijana kuwa jasirii na shujaa katika harakati za kuleta
mapinduzi.Pia wanamapinduzi wanatakiwa wawe wavumilivu kwa sababu ujenzi wa
jamii mpya sio lelemama,ni safari ndefu yenye vikwazo vingi.
Vile
vile katika shairi la “Umma” mwandishi anahimiza ujasiri katika kuleta mapinduzi katika jamii. Mwandishi nasema:-
“Umma,
Uliovinjari,kuangamiza mtabaka,
Hima,
Uwe tayari,wala usiwe na shaka,
Ongoza mapinduzi,
Ya wafanyakazi,
Hadi ushindi.
Hivyo mwandishi
anaitaka jamii ijitoe mhanga ili kufanikisha suala la ujenzi wa jamii mpya.
4. KUFANYA
MAGEUZI (MAPINDUZI)
Mwandishi
anapendekeza mbinu ya kufanya mageuzi ili kufanikiwa katika suala zima la
ujenzi wa jamii mpya.Katika shairi la “Umma” mwandishi anawaasa wanajamii
wajiandae kuangamiza matabaka yaliyokithiri katika jamii.
Mwandishi
anapendekeza mbinu mbalimbali za kufanya mageuzi (mapinduzi) ambazo ni;
Kwanza,jamii
hasa watu wa tabaka la chini waungane ii kuondoa viongozi wanaotumia madaraka
waliyopewa kwa manufaa yao binafsi. Katika shairi la “Ungameni” mwandishi
anasema;
Msimamo wa kitabaka,tuwekeni,
Bepari wote kuwashika,wawe ndani,
Na mamwinyi bila ya shaka,wambaroni,
Tusizubae,kazi ianze,twangoja nini?
Wakati ni huu.
Pili,mwandishi
anapendekeza kutumia silaha katika mageuzi hayo ikiwa unyonyaji hautaondoka kwa
amani.Mfano
Katika shairi la “Siku Itafika” na “Nikizipata
Bunduki”na“Utawala” mwandishi
anapendekeza yafanyike mgeuzi ili
kuuangusha utawala unaojinufaisha na
kuendeleza matabaka katika jamii.
Katika
shairi la “Mjamzito”mwandishi anaonesha jinsi watu wanavyoogopa harakati za mapinduzi katika jamii zetu.
Katika
mashairi ya “Ni vita si Lelemama” na
“Maendeleo ya Umma” mwandishi
anaonesha jinsi suala la mageuzi lilivyo gumu, ingawa anamatumaini kuwa umoja na ushirikiano wetu utatufanya tushinde.Pia
anaamini kuwa unyonyaji na uonevu hautadumu milele,kwani kuna siku,saa,dakika
na nukta itafika uovu wote utaondolewa kwa nguvu.
Katika
shairi la “Joka La Mdimu” mwandishi anatoa mfano wa tawala dhalimu
zilizoondolewa kwa nguvu kwa ushirikiano wa tabaka la chini. Katika shairi hili
mwandishi anaonesha jinsi wananchi
walivyoshirikiana katika kuutokomeza ukoloni hapa nchini.
Hivyo
ili nasi tufanikiwe kujenga jamii mpya hatuna budi kufanya mapinduzi (mageuzi).
5. SUALA
LA UZALENDO
Uzalendo
ni ile hali ya kuipenda nchi kwa dhati na hata kuifia. Msimamo wa mwandishi ni
kuwa hataihama nchi yake hata kwa kutishiwa njaa,maafa au umaskini.Pia
ataipigania nchi yake ili iwe salama.Hivyo hata sisi hatuna budi kuipigania
nchi yetu kwa hali na mali ili kuondoa udhalimu uliopo.Katika shairi la “Nchi
Yangu” mwandishi anasema;
Naipenda nchi yangu,
Naipenda,naipenda nitakufa naipenda.
Tailinda nguvu zangu,tailinda,
Tailinda kwa maafa tailinda,
Sitakwenda kwa wenzangu,
Sitakwenda,sitakwenda hata sifa sitakwenda,
Nitakwenda huku kwangu,nitaganda,
Nitaganda kwa ulofa nitaganda.
Mwandishi anaona
kuwa,tukiwa na uzalendo na nchi yetu tutafanikiwa kujenga jamii mpya,kwani
usaliti wa viongozi wetu utaanguka na kila mmoja ataipenda nchi yake kwa dhati.
6. UKOLONI
MAMBOLEO
Ukoloni
mamboleo ni ile hali ya nchi kupata uhuru wa bandia (kisiasa) lakini njia zote
za uchumi hutawaliwa au hubaki mikononi mwa mabepari au watu wa nchi
nyingine.Katika shairila “Ruya” mwandishi anasema;
Ruya,menitoa shamba,mji kuuramba niwe utumwani?
chini umwinyini,
nimo kifungoni!
Ni ‘’huru’’ machoni!
Ruya,hivyo wanitimba,kunifunga kamba,za ukoloni,
Njozi niondokee!
Mwandishi
anaona kuwa wazungu ndio walioondoka katika ardhi ya Afrika lakini unyonyaji
bado upo na unaendelea.Viongozi waliochukua madaraka baada ya uhuru bado
wanaendeleza zile taratibu zilizoachwa na wakoloni.
Katika shairi la
“Kunguru”
mwandishi anaonyesha athari za ukoloni mamboleo hapa nchini.Katika shairi hili
mwandishi anazungumzia juu ya kuondoka kwa ukoloni mamboleo.Hivyo mwandishi
anaonesha kuwa ili tujenge jamii mpya ni lazima tupige vita ukoloni mamboleo
ili tuwe na uhuru wa kuamua mambo yetu wenyewe.
7. WIZI WA MALIYA UMMA
Mwandihi
wa diwani hii ameshindwa kuficha hasira yake dhidi ya wizi.Ameutaja wazi kuwa
wizi umo kanisani,msikitini,Ikuluni na bomani.Waandishi wengi hukwepa kutaja
ukweli kama huu. Asemacho mwandishini kwamba,sehemu zote za jamii zimeoza.
Zamani watu wengi waliamini kuwa viongozi wa dini wana maadili wasiyoweza
kuyakiuka.Kwa hiyo,maovu hayo yasingetokea huko. Lakini sasa viongozi hao na
wale wa Ikulu wamejiunga na wahalifu. Lililo baya zaidi ni kuwapo kwa “Walinzi”
wanaolinda hao wezi.Katika shairi hili la “wizi” mwandishi anasema;
Wizi umo;
Kanisani,
Msikitini,
Hekaluni,
Wanyang’anywao ni waumini.
Kwa kifupi wizi
umehalalishwa na kubarikiwa na kuonekana kama ni jambo la kawaida kabisa.
Mwandishi hasemi tufanyeje lakini kwa mtiririko na mantiki ya mashairi
yake mengine,mwandishi anashauri ufumuaji na usafishaji wa jamii nzima.Katika shairi la“Kunguru” mwandishi pia
anajadili Suala la wizi .Japo amefumba
lakini anawaelimisha wasomaji kuhusu wezi waliotimuliwa na
kutawanywa.Baada ya muda wezi wakajitayarisha kwa mbinu tofauti na kuendeleza
wizi wao. Mwandishi anatanabaisha raia kuhusu kuwapo kwa wezi hawa na marafiki
zao.Katika shairi la “Joka la Mdimuni” mwandishi
anatanabaisha watu kuhusu uwezekano wa wakoloni kurudi kwa umbo tofauti lakini
kwa athari zile zile.Katika shairi la “Naona“ mwandishi anaonesha taabu wanazopata wakulima
na malipo duni wanayopewa kwa mzao yao.Anamaliza kwa msimamo huu;
‘’Naona
Ni fukara wakulima
Wamepigwa ulitima
Kwa wengine ni neema
Kwao wao ni nakama
Wamekosa haki!
8.
KUPIGA VITA UKASUKU WA VIONGOZI WETU
Mwandishi
amekemea tabia za viongozi na watendaji wengine kukubali kila lisemwalo bila
kufikiri au kwa hofu tu,si nzuri.Tabia hii ya ukasuku anauita ugonjwa
unaohitaji tiba (tiba yenyewe hakuitaja).Ugonjwa huu hudunisha akili.Mwandishi
anaonyesha chanzo na athari zake.Katika
shairi la “Ukasuku” mwandishi anasema;
“Kupea
kwa ukasuku
Rais huhubiri
Wabunge hukariri
Wasomi huhariri
Na taifa husimama”.
Mwandishi anawachunguza viongozi wa bara la Afrika na
kuwaona kuwa ni mabepari,madikteta,wenye ukabila,wabadhirifu wasiojali raia wao
wapenda hongo.Wote amewakemea na kuwakanya wasitende hivyo. Amewapa majina
yanayowafaa- wahaini, wasaliti, majasusi n.k.Mwandishi anastahili pongezi kwa
kuweza kuwakemea, badhi ya viongozi badala ya kuwasifu.
UJUMBE
v Uongozi
mbaya,wizi wa mali ya umma,rushwa na kukosekana kwa haki,ukasuku na matumizi
mabaya ya mali ya umma ni vikwazo kikubw
katika ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
v Umoja na
ushirikiano ni njia moja wapo ya ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
v Mfumo wa ujamaa
ni mfumo wa pekee utakaomkomboa mtu mnyonge,yaani ndiyo utakaoleta hali nzuri
kwa wakulima na wafanyakazi.
v Ili tujenge
jamii mpya ni lazima tuwe na ujasiri wa kujitoa mhanga,tuwe wazalendo na nchi
yetu na tufanye mapinduzi (mageuzi ya kweli) katika jamii.
v Ukoloni mamboleo
ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
v Mapenzi ya kweli
ni yale yasiyojali fedha au hali ya mtu.
FALSAFA
Mwandishi
anatetea itikadi ya ujamaa yenye kuleta haki na usawa kwa kila mtu.Analaani
wizi,dhuluma na majivuno ya kirasimu. Mwandishi angependa nchi iongozwe kwa
haki na usawa.Vile vile anatetea mapenzi ya kweli katika maisha.
MSIMAMO
Mwandisi
ana msimamo wa kimapinduzi,kwani ameonesha matatizo mbali mbali yanayozikumba
jamii zetu na mbinu za kuondokana na matatizo hayo.Miongoni mwa matatizo hayo
ni uongozi mbaya,wizi wa mali ya umma,rushwa na dhuluma, n.k.
FANI
1. MITINDO
Mwandishi
wa diwani ya FUNGATE YA UHURU ametumia mitindo ifuatayo:-
(a)
Mitindo changamano
Huu
ni mtindo unaohusisha mashairi yenye kutumia mtindo wa kimapokeo na mtindo wa kisasa.
(i) Mtindo wa
kimapokeo
Huu
ni mtindo unaofuata au unaozingatia urari wa vina, mizani na beti za
mashairi. Mashairi yaliyotumia mtindo wa
kimapokeo katika diwani hii ni”Kuntu Sauti ya Kiza” (uk. 33), “Ladha ya Maji
Katani” (uk. 35-37),“Mcheza Hawi Kiwete” (uk.37-38), “Sakubimbi” (uk.44), “Paka
Shume” (uk.45), “Uwapi Uzuri Wako” (46-47), “Ua Si Ruwaza Njema” (uk.47-48) na
“Wewe Peke Yako” (uk.45). Kwa mfano,
katika shairi la “Ua Si Ruwaza Njema” (uk.47-48), mshairi anasema:
“Ua huvishwa mgeni, Mtukufu akifika,
Ni koja la asumini, shingoni linajiweka,
Mara utalibaini, walinzi wamelishika,
Ua si ruwaza njema, tunzo ya mtu kupewa”.
(ii) Mtindo wa kisasa / kimamboleo
Huu
ni mtindo usiofuata au usiozingatia urari wa vina, mizani na beti za
mashairi. Mashairi yaliyotumia mtindo wa
kisasa au kimamboleo katika diwani hii ni “Maendeleo ya Umma” (uk. 2-4),
“Mjamzito” (uk. 7-8), “Ukasuku” (uk.30-31), “Mwinyi mpe ‘Ndiyo’ ” (uk.32), “Siku itafika”(uk.39-40) na”Kinyang’anyiro”
(uk.43-44). Kwa mfano, katika shairi la
“Ukasuku” (uk.30-31), mshairi anasema:
‘’Athari za ukasuku,
Akili mufilisi,mawazo
mepesi,na hayana kasi,
Vipawa vimedumaa’’
( b ) Mtindo wa
tenzi
Ni mtindo ambao mshororo (mstari)mmoja
wa shairi huundwa na kipande kimoja tu.Aghalabu,mshororo mmoja wa ubeti wa
shairi la mtindo wa tenzi huwa na mizani ( silabi ) kati ya 6 hadi 11 tu.Tenzi
huwa na ulinganifu wa silabi za mwisho kwa kila mshororo au mstari wa
ubeti.Mashairi yaliyotumia mtindo huu wa tenzi katika diwani hii ni’kunguru na
Naona.Katika shairi la kunguru
mshairi anasema;
“Kunguru
hawakushituka,
Ila kuzidi
kucharuka,
Raia
wakakusanyika,
Pambano jipya
kuliweka.
Zikatumika na
bunduki,
Wengine wengi
kufariki,
Haba wakahama
miliki,
Lobaki
hawabadiliki”.
(c) Mtindo wa kidato
Huu
ni mtindo ambao mshairi hutumia baadhi ya mistari iliyofupishwa maneno au
silabi tofauti na mistari mingine ambayo huwa na silabi au maneno mengi.Mbinu
ya kidatu hutumiwa na mshairi kwa lengo maalumu hususani katika kufikisha
ujumbe wake kwa jamii iliyokusudiwa.
Mashairi yaliyotumia mtindo wa kidato katika diwani hii ni “Maendeleo ya
Umma” (uk.2-4), “Tumesalitiwa!” (uk. 5), “Haki” (uk.5), “Mjamzito” (7-8),
“Nikizipata Bunduki” (uk. 11-13), “Ruya” (uk. 13-14), “Pungo” (uk. 16-18),
“Viongozi w Afrika” (uk.21 -22), “Afrika” (uk. 22-23),”Ukasuku” (uk. 30-31) “Si
Wewe?” (uk. 38-39), “Siku Itafika”
(uk.39-40) na “Kinyang’anyiro” (uk. 43-44).
Kwa mfano, katika shairi la “Nikizipata Bunduki” (uk.11-13), mshairi
anasema:
“Ningekuwa na
Sauti,
Malaya ngewapa
kazi, ya shamba na ofisini,
Na wezi na
majambazi, wangekuwa viwandani,
Wakosefu,
Marufuku, si
wachafu,
Si halifu,
Sauti
haziwalishi”
(d) Mtindo wa kikufu au pindu
Huu
ni mtindo ambao neno au sehemu ya neno ya mshororo wa kwanza inayomalizia
huanzia katika mshororo wa ubeti unaofuata.
Mashairi yaliyotumia mtindo wa kikufu au pindu katika diwani hii ni
“Nataka Kusema” , “Mkata”, “Kinyang’anyiro” na “Nyayo”. Kwa mfano, katika shairi la “Nataka Kusema”,
mshairi anasema:
“Nataka, kusema
yote,
Yote yaniumizayo
moyo, lakini;
Nna kitata,
siwezi kutamka!
Nataka kutema
mate,
Mate,
yanichafuayo moyo, lakini;
Yamekauka,
jelezi menishika!”
(e) Mtindo
wa kuandika vibwagizo katika mashairi
Kwa
kawaida vibwagizo au viitikio hupatikana katika kipera cha nyimbo lakini baadhi
ya washairi hutumia mbinu ya kuandika vibwagizo au viitikio katika mashairi
wanayoyatunga. Mashairi yaliyotumia
mtindo wa kuandika vibwagizo katika mashairi kwenye diwani hii ni
“Sakubimbi” (uk. 44), “Paka Shume” (uk. 45), “Nia Yangu
Sigeuzi” (uk.46) na “U Wapi Uzuri Wako”
(uk.46-47).
Katika
shairi la “Sakubimbi” (uk. 44), mshairi
anasema:
“Usijione
mwerevu, umestaarabika,
Yakakuvimba
mashavu, na kichwa kukupanuka,
Huo sio
ushupavu, ni ujinga natamka.
Kibwagizo:
Umelichimba kaburi, mzima
utajizika,
Huna tena
ujasiri, sakubimbi umefika”
Katika
shairi la “U Wapi Uzuri Wako” (uk.
46-47), mshairi anasema:
“Sasa ni chano
cha mji, watu wajichanyatia,
Umekwisha
ujuwaji, haya zimekupotea,
Yale
usoyataraji, kwako yamekuhamia.
Kibwagizo:
U wapi uzuri
wako, ya wapi maringo yako”.
(f) Mtindo wa mashairi yenye vina vitatu
Kwa
kawaida mashairi ya kimapokeo huwa na mshororo (mstari) mmoja unaoundwa au
unaogawanywa katika vina viwili yaani kina cha kati na kina cha
mwisho.Mwandishi wa diwani hii ametumia baadhi ya mashairi yenye mstari mmoja
unaoundwa kwa vina vitatu,yaani kina cha kwanza,kina cha pili na kina cha
tatu.Mashairi yaliyotumia mtindo wa mashairi yenye vina vitatu katika diwani
hii ni “Dafina”, “Mkata” na “Waja wa
Mungu”.Kwa mfano, shairi la “Waja wa
Mungu” , mshairi anasema:
“Duniani, nguo mbovu matakoni, mafakiri,
Lakini, nguo tele kabatini, mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu!”
(g) Mtindo wa mashairi yenye vina vinne
Mashairi
ya kimapokeo huwa na mshororo (mstari)
mmoja unaoundwa au unaogawanywa katika vina viwili yaani kina cha kati
na kina cha mwisho.Mwandishi wa diwani ya FUNGATI YA UHURU ametumia baadhi ya
mashairi yenye mstari mmoja unaoundwa kwa vina vinne,yaani kina cha kwanza,
kina cha pili, kina cha tatu na kina cha nne.Mashairi yaliyotumia mtindo wa
mashairi yenye vina vinne katika diwani hii ni “Ruya” na “Gorila”.
Katika
shairi la “Ruya”, mshairi anasema:
“Ruya, unanitonesha, donda lilokwisha, hapo zamani,
Njozi niondokeya!”
Katika
shairi la “Gorila”, mshairi anasema:
“Gorila, jasiri!,
Wa Afrika, shujaa, mshupavu, umevinjari,
Mtutu shika, mevaa, ukakamavu, uko tayari,
Gorila, ruwaza, wa kizazi kipya”.
(h) Mtindo wa
kuhoji
Huu
ni mtindo unaotumiwa na washairi wa kuuliza maswali ambayo ama majibu yake yako
wazi au hayako wazi.Mashairi yaliyotumia mtindo wa kuhoji au kuuliza maswali katika diwani hii ni “Si
wewe?” “Tumesalitiwa!” na “Ruya”.Kwa mfano, katika shairi la “Si
Wewe?” mshairi anasema:
“Si wewe?
Nilokuanzisha kula ubwabwa wa mapenzi,
Ikawa wauchakua kwa ufizi,
Ukatapika kwa kuona jelezi,
Hukujua kutafuna,
Ni wewe umwanagenzi!
Si wewe?
Lonililia kwa kwikwi kaamua kukubeba,
Nikakunyonyesha ziwa la mahaba,
Kapapia hukusubiri kushiba,
Na sasa umepaliwa,
Ni wewe unayejutia”.
(i) Mtindo wa msisitizo au takriri
Huu
ni mtindo ambao neno moja linatokea mwanzoni na linarudiwa katika mishororo au
mistari ya ubeti wa shairi .Mashairiyaliyotumia mtindo wa msisitizo au takriri
katika diwani hii ni “Nchi Yangu”, “Dafina”.Kwa mfano katika shairi la “Nchi
Yangu” ,mshairi anasema:
“Naipenda nchi yangu,
Naipenda, naipenda nitakufa naipenda.
Tailinda nguvu zangu, tailinda,
Tailinda kwa maafa tailinda,
Sitakwenda kwa wenzangu,
Sitakwenda,sitakwenda hata sifa sitakwenda,
Nitakwenda huku kwangu,nitaganda,
Nitaganda kwa ulofa nitaganda
(j) Mtindo wa nafsi
Huu
ni mtindo ambao mshairi anaweza kutumia nafsi umoja,nafsi wingi au nafsi kundi
kwa lengo la kufikisha ujumbe au maudhui fulani kwa jamii.Kuna nafsi za aina
tatu (3),yaani nafsi ya kwanza (umoja na wingi),nafsi ya pili (umoja na
wingi)na nafsi ya tatu (umoja na wingi).
Mwandishi wa diwani hii ametumia mtindo wa nafsi kama ifuatavyo:-
(i) Matumizi ya nafsi umoja (nafsi ya kwanza
umoja na nafsi ya pili umoja):
Mshairi
huzungumzia jambo linalomhusu mtu mmoja pekee.
Hujumuisha ahadi,matamanio, sifa, mawaidha na maonyo. Mashairi
yaliyotumia nafsi ya kwanza umoja ni “Nikizipata
Bunduki” , “Ruya”, “Nataka Kusema” na
“Mkata”.Kwa mfano kama mshairi la “Nikizipata
Bunduki” mshairi anasema:
“Nikivipata
Vitara,
Nitawachinja wakubwa,wanaonyonya masikini,
Namali zao kukabwa, kugaiwa watu duni,
Tafilisi,
Ubinafsi, kwa upesi,
Na kwa kasi,
Sauti haziwafishi!”.
Pia
mashairi yaliyotumia mtindo wa nafsi ya pili umoja katika diwai hii ni “U Wapi
Uzuri Wako”,“Si Wewe?”,“Paka Shume” na “Sakubimbi”. Kwa mfano katika shairi la “U Wapi Uzuri
Wako”,mshairi anasema:
“Sasa ni chano cha mji, watu wajichanyatia,
Umekwisha ujuwaji, haya zimekupotea,
Yale usoyataraji,
kwako yamekuhamia”.
(ii) Matumizi ya nafasi wingi (nafsi ya kwanza
wingi)
Mshairi
huzungumzia jambo au suala lialohusu kundi fulani la watu akiwemo nayeye
mwenyewe.Mashairi yaliotumia mtindo wa nafsi ya kwanza wingi katika diwani hii
ni “Unganeni!” ,“Utawala”,“Ukasuku” ,“Ni Vita Si Lelemama” na “Siku Itafika”
.Kwa mfano katika shairi la “Unganeni”,mshairi anasema:
“Kunyonywa pia
kunyanyaswa, tukataeni,
Kuteswa na
kukandamizwa, tukupingeni,
Si kusengenyewa
si kuteswa, tuchukieni,
Tujadhibike, turaghibike, tujadibike,
Potelea mbali!”.
(iii) Matumizi ya nafsi kikundi (nafsi ya tatu
wingi)
Mshairi
huonekana ama akisimulia hadithi, akitoa hotuba au akizungumzia kundi fulani la
watu kuhusu suala au jambo muhimu.
Mashairi yaliyotumia mtindo wa nafsi ya tatu wingi katika diwani hii ni
“Naona” (uk. 41-42), “Maendeleo ya Umma” (uk.2-4),
“Viongozi wa Afrika”
(uk.21-22), “Wengine” (uk.24), “Wizi” (uk.25), “Waja wa Mungu (uk.27) na “Kunguru”
(uk.26-27). Kwa mfano katika shairi la
“Naona” (uk.41-42), mshairi anasema:
“Naona
Jasho
lawatiririka
Na majembe na
mashaka
Wakulima
wameshika
Mashamba yao
kufyeka
Ni wachapakazi!
Naona
Ni fukara
wakulima
Wamepigwa ulitima
Kwa wengine ni
neema
Kwao wao ni
nakama
Wanakosa haki!”
2. MUUNDO
Mwandishi
wa diwani ya FUNGATE YA UHURU ametumia miundo tofautitofauti kwa kuzingatia
vigezo mbalimlbali kama ifuatavyo:-
Ø Kigezo cha idadi ya mishororo:
Kwa
kuzingatia kigezo cha idadi ya mishororo kwa kila ubeti mshairi ametumia miundo
ifuatayo:-
(a) Muundo wa tathnia
Ni muundo ambao kila ubeti unaundwa na mistari
miwili .Shairi lililotumia muundo wa tathnia katika diwani hii ni”Mjamzito”
(uk.7-8), Mshairi anasema :
“Mjamzito amelazwa thieta!
Lazima kupasuliwa.
Chake kitoto, Tumboni kinatweta,
Hawezi kujifungua”.
(b) Muundo wa tathilitha.
Huu
ni muundo ambao kila ubeti unaundwa kwa mistari mitatu. Mashairi yaliyotumia muundo wa tathilitha
katika diwani hii ni “Fungate”, “Waja wa
Mungu”, “Sakubimbi”, “Paka Shume”, “Wewe Peke Yako” “Nia Yangu Sigeuzi” na “U Wapi Uzuri Wako” .Kwa mfano, katika
shairi la “Fungate” , mshairi anasema:
“Karamu za fahari, mabembe ya kupepewa,
Na mafumba mazuri, wamekwisha jijengea,
Watembea kwa magari, hivi zimewazowea”.
(c) Muundo wa tarbia:
Ni
muundo ambao kila ubeti unaundwa kwa mistari minne.Mashairi yaliyotumia muundo
wa tarbia katika diwani hii ni “”Nahodha Mtwesi “Gorila” ,“Kunguru” (uk.26-27),
“kuntu Sauti ya Kiza” “Ni Vita Si Lelemama” ,“Wingu” ,“Mcheza Hawi
Kiwte” na “Ua Si Ruwaza Njema” Kwa mfano, katika shairi la “Nahodha
Mtwesi”,mshairi anasema:
“Nahodha mtwesi, Chombo chenda joshi,
Stadi wa kukisi, hupendi ubishi,
Mahiri, jasiri wa ari, hukeri,
Hatwendi mrama”
(d) Muundo wa takhimisa.
Ni
muundo kila ubeti unaundwa kwa mistari mitano. Mashairi yaliyotumia muundo wa
takhimisa katika diwani hii ni “Unganeni”, “Tumesalitiwa” ,“Ningekuwa na
Sauti”, “Wizi” “Utawala” (uk.28-29), “Njama” ,“Nyayo” na Ladha ya Maji Katani ,Kwa mfano, katika
shairi la “Tumesalitiwa” mshairi
anasema:
“Nikate tama?
Kwani twendavyo, hatufiki.
Vile ipasavyo, hayakamiliki.
Mambo yalivyo, ni unafiki
Tumesalitiwa!”
(e) Muundo wa sabilia:
Ni
muundo unaohusu mashairi yanayoundwa kwa mistari sita na kuendelea katika kila
ubeti. Mashairi yalyotumia muundo wa
sabilia katika diwani hii ni “Maendeleo ya Umma” (uk.2-4), “Nchi Yangu” (uk.6),
“Dafina”, “Nikizipata Bunduki” ,“Pungo” ,“Mkata”, “Viongozi wa Afrika” ,“Wengine” , “Ujamaa” ,Mwinyi
Mumpe Ndiyo” ,“Si Wewe?” “Siku
Itafika” na “Naona” .Kwa mfano, katika
shairi la “Pungo”,mshairi anasema:
“Kilingeni mwari ametulia,
Na mganga anamwangalia,
Pepo anajitamkia,
Jina anamtajia,
Na chanzo cha udhia,
Mwele tamwachia,
Awe huria.
Na fiya,
Pamoya,
Na wana”
Ø Kigezo cha idadi ya vipande:
Kwa
kuzingatia idadi ya vipande kwa kila
mshororo katika ubeti wa shairi, mwandishi wa diwani ya FUNGATE YA UHURU
ametumia miundo ifuatayo:-
(a) Muundo wa kipande kimoja (ukwapi)
Huu
ni muundo ambao kwa kila mshororo (mstari) wa ubeti wa shairi kunakuwa na
kipande kimoja tu. Mifano ya mashairi ya
muundo wa kipande kimoja katika diwani hii ni “Maendeleo ya uma” (uk.2-4), “Pungo”, “Viongozi wa Afrika” ,“Wengine” , “Wizi”,“Kunguru”, “Utawala” ,“Njama” ,“Wingu” ,“Si Wewe?” ,
“Siku Itafika”,“Naona”,
“Kinyang’anyiro” na “Joka la
Mdimuni”.Kwa mfano katika shairi la “Kunguru”, mshairi anasema:-
“Kunguru
wakabadilika,
Uchafu wao
wakaweka,
Maradhi
yakaongezeka,
Nibadala ya
kutoweka”
(b)Muundo wa
vipande viwili (ukwapi na utao)
Huu
ni muundo ambao kwa kila mshororo (mstari) wa ubeti wa shairi kunakuwa na
vipande viwili, yaani kipande cha kwanza (ukwapi) na kipande cha pili
(utao).Mifano ya mashairi ya muundo wa vipande viwili katika diwani hii ni
“Fungate”,”Nataka Kusema” , “Nyayo”,
“Kuntu Sauti ya Kiza” , “Ni Vita
Si Lelemama”, “Ladha ya Maji Katani” “Mcheza Hawi Kiwete” , “Sakubimbi”, “Paka
Shume”, “Wewe Peke Yako” ,“Nia yangu Sigeuzi”, “U Wapi Uzuri Wako” na “Ua Si
Ruwaza Njema”.Kwa mfano katika shairi la “Ua Si Ruwaza Njema”. mshairi anasema:
“Ua tunzo ya mahaba, wapenzi wanahusika,
Ishara ya usuhuba, wawili kukutanika,
Lakini na makahaba, na wao hujipachika,
Ua si ruwaza njema, tunzo ya mtu kupewa”.
(c) Muundo wa vipande vitatu (ukwapi, utao na
mwandamizi).
Huu
ni muundo ambao kwa kila mshororo (mstari) wa ubeti wa shairi kunakuwa na
vipande vitatu, yaani kipande cha kwanza (ukwapi), kipande cha pili (utao) na
kipande cha tatu (mwandamizi). Mifano ya
mashairi ya muundo wa vipande vitatu katika diwani hii ni “Dafina” (uk.8-10)
“Mkata” (uk.19-20) na “Mja wa Mungu”
(uk.27). Kwa mfano, katika shairi
la “Mja wa Mungu” (uk.27). Mshairi anasema:
“Duniani,ni maradhi ni masikani, mafakiri,
Lakini, dawa tele kabatini, mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu!”!.
(d) Muundo wa vipande vinne
Huu
ni muundo ambao kwa kila mshororo (mstai) wa ubeti wa shairi kunakuwa na
vipande vinne. Mifano ya mashairi ya
muundo wa viipande vine katika diwani hii ni “Ruya” (uk.13-14) na “Gorila” (uk.14-15). Kwa mfano katika shairi la “Gorila”
(uk.14-15), mshairi anasema:
“Gorila, jasiri!
Wa Afrika, wavuka, mingi mito, yenye hatari,
Wa panda shuka, inuka, na uzito, wa lako
gobori,
Gorila, ruwaza wa kizazi kipya”.
Ø Kigezo cha aina ya vituo:
Kwa
kuzingatia kigezo cha aina ya vituo, mwandishi wa diwani ya FUNGATE YA UHURU
ametumia miundo ifuatayo:-
(a) Muundo wa kituo bahari
Kituo
bahari ni mstari wa mwisho wa ubeti wa shairi ambao hujirudia kwa kila ubeti.Mashairi
yaliyotumia muundo wa kituo bahari katika diwani hii ni “Dafina”, “Ningekuwa na
Sauti”, “Gorila,”Waja wa Mungu” “Mcheza
Hawi Kiwete”,“Njama”,“Ladha ya Maji Katani”,“Kinyang’anyiri” na “Ua Si Ruwaza Njema” .
Katika
shairi la “Ua SiRuwaza Njema”
(uk.47-48), mshairi anasema:
“Ua tunzo ya
mahaba, wapenzi wanahusika,
Ishara ya
usuhuba, wawili kukutanika,
Lakini na
makahaba, na wao hujipachika,
Ua si ruwaza njem, tunzo ya mtu kupewa
Ua likiwa mtini,
hua linanawirika,
Huwa na kubwa
thamani, hapo lilipojishika,
Likitiwa mikononi, si muda linanyauka,
Ua si ruwaza njem, tunzo ya mtu kupewa”.
(b) Muundo wa kituo nusu bahari
Kituo
nusu bahari ni mstari wa mwisho wa ubeti wa shairi ambao sehemu tu ha mshororo
(mstari) hujirudia kwa kila ubeti wa shairi.
Mara nyingi katika kituo nusu bahari, kipande kimoja tu cha mshororo wa
mwisho wa ubeti hurudiwa katika beti za mashairi. Mashairi yaliyotumia muundo
wa kituo nusu bahari katika diwani hii ni ”Kuntu Sauti ya Kiza” na “Si
Wewe?” .
Katika
shairi la ”Kuntu Sauti ya Kiza” (uk.33), mshairi anasema:
“Si mlaji wa
vinyesi, mizoga na masalia,
Hayarambi
makamasi,na banguzi kubugia,
Hata samaki wa
tasi, shombo analikimbia,
Kuntu Sauti ya Kiza, nyuki hatwai
vichafu.
Nyuki hatui
topeni, na zizini kuingia,
Sijamwona
karoni, mikojo kufakamia,
Haingii na
chooni, hata chenye mazulia,
Kuntu Sauti ya Kiza, nyuki hatwai
vichafu”.
(c) Muundo wa kituo kimalizo
Kituo
kimalizio ni mstari wa mwisho wa ubeti wa shairi ambao haujirudiirudii kwa kila
ubeti.Hii ina maana kuwa kwa kila ubeti wa shairi kunakuwa na mstari wa mwisho
(kituo) wa tofauti na usiofanana na beti nyingine. Mashairi yaliyotumia muundo wa kituo
kimalizio katika diwani hii ni “Fungate” , “Unganeni”,“Maendeleo ya Umma” Nchi yangu, “Nahodha Mtwesi”, “Mjamzito”
,“Nikizipata Bunduki”,
“Ruya”,“Pungo” (uk.16-18), “Nataka Kusema”, “Mkata”,“Viongozi wa
Afrika”,“Afrika”, “Wengine”,“Wizi” ,“Kunguru” ,“Utawala” ,“Ukasuku” “Nyayo”,“Ni Vita Si Lelemama” ,“Wingu” ,“Siku
Itafika” ,”Joka la Mdimuni’’ na “Naona”.
Katika
shairi la “Nataka Kusema” (uk.18),
mshairi anasema:
“Nataka kutema
mate,
Mate
yanichafuayo,moyo, lakini:
Yamekauka, jelezi menishika!
Nataka, kulia
kite,
Kite,
yanikeketayo moyo, wenzangu,
Hayatatoka, machozi yametweka!”
3. MANDHARI
Mshairi
wa diwani ya FUNGATE YA UHURU ametumia mandhari yafuatayo:-
(a)
Mandhari ya bara
la Afrika.
Mshairi
anazungumzia kero, shida au matatizo mbalimbali yanayolikabili bara la Afrika,
ikiwemo nchi ya Tanzania, kupitia mashairi ya “Unganeni” ,“Nikizipata Bunduki”
,“Gorila” ,“Viongozi wa Afrika” ,“Afrika”,“Ni Vita Si Lelemama” na “Utawala” .Mshairi ametaja baadhi ya nchi
za bara la Afrika kama vile Tanzania, Afrika ya Kusini na Namibia.Pia, mshairi
ametaja jina la chama cha kisiasa kimojawapo kinachoopatikana nchini Tanzania ,
Chama cha Mapinduzi, kudhihirisha kwamba yanaoongelewa kwenye diwani yake
yanahusu nchi ya Tanzania.Jina hili la chama cha kisiasa limetajwa katika
shairi la “Ni Vita Si Lelemama”
(uk.34). Mandhari ya bara la
Afrika yanaibua dhamira za rushwa,
umasikini, uonevu, dhuluma, udikteta, uongozi mbaya, unyonyaji, unafiki,
usaliti,matabaka, mapinduzi au mageuzi, wizi wa mali ya umma na ushirikiano.
(b) Mandhari ya mabara ya Amerika na Ulaya.
Mshairi
anajadili namna nchi zilizoendelea, zikiwemo nchi za bara la Amerika na Ulaya,
zinavyonyonya, zinavyoonea na zinauvyokandamiza nchi zinaendelea zzinamiliki
uchumi na siasa za nchi zinazoendelea.
Mshairi anatumia mandhari haya katika shairi la “Afrika”.Mandhari ya
mabara ya Amerika na Ullaya yanaibua dhamira za ukoloni mamboleo, unyonyaji,
umasikini na ukombozi wa kisiasa.
(b)
Mandhari mengine
yanayotajwa katika diwani hii ni ikulu, kanisani, msikitini, bomani, ofisini,
shambani, dukani, gulioni na gengeni.katika shairi la “Wizi” . na mandhari
ya nyumbani katika shairi la “Mkata”.
Mandhari yote haya yanaibua dhamira za umasikini, unyonyaji, uongozi
mbaya, wizi wa mali ya umma, dhuluma, unafiki, usaliti na matumizi mabaya ya
vyombo vya dola
C)MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi
ametumia lugha sanifu yenye lahaja ya Kiunguja.Lugha hii imejaa misemo mbali
mbali,tamathali za semi na taswira.
Misemo
Imetumika
kwa wingi.
Mfano:
·
Nahodha
mtwesi chombo chenda joshi (uk 5)
·
Waja
wa Mungu (uk 20)
·
Paka
shume (uk 34)
·
Utakiona
cha mtema kuni (uk 24)
·
Joka
la mdimuni (uk 31) n.k.
TAMATHALI ZA SEMI
Tashibiha
Mfano
shairi la “Mkata” (uk 15):-
·
Kitandani
nilalapo kama dema la samaki…
·
Mbu
ndani kama ndege wa vitani…
·
Matopeni
hujazika mithili nimo karoni…
·
Nimekoni
kama ndizi natokota na kufoka
Sitiari
Mfano
shairi la “Uwapi Uzuri Wako” (uk 35)
·
Sasa
ni chano cha maji, watu wajichanyatia
·
Bao
la mkahawani, kila mtu akaliya
·
Sasa
jamvi la wageni,wajapo huwapokeya.
Kejeli
·
Shairi
la “Fungate” (uk 1) linakejeli tabia
za baadhi ya viongozi wetu wanaoendelea kuifaidi Fungate ya Uhuru.
·
Shairi
la “Kuntu Sauti ya Kiza” mwandishi
anatumia nyuki kukejeli baadhi ya tabia chafu za watu.
Tafsida
Mwandishi
ametumia Tafsida kuyasema maneno makali, machafu, matusi.Mfano shairi la “Paka Shume” linajadili suala la
kumendea vitu vya watu kwa njia isiyo halali.Hata neno lenyewe fungate ni tafsida.
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
Takriri
Katika
shairi la “Mkata” (uk 15), “Dafina” pamoja na shairi la “Nchi Yangu”baadhi ya maneno yamerudiwa
sana.
Mjalizo
Katika
shairi la “Mkata” (uk 15).
Mdokezo
Katika shairi la
“Mwinyi Mpe Ndiyo”
UJENZI WA TASWIRA
·
Neno
Fungate
linaleta taswira ya ulimbwende wa maharusi linaashiria viongozi.
·
Shairi
la “Mjamzito”
(uk 5) linajenga taswira ya viongozi waoga katika jamii. Viongozi wasioweza
kutatua matatizo ya wananchi.
·
Shairi
la “Paka
Shume”(uk 34) linajenga
taswira ya udokozi.
·
Shairi
la “Viongozi
wa Afrika”(uk 15) linajenga taswira ya viongozi wanaotumia
madaraka vibaya.
JINA LA KITABU
Kwa
ujumla jina la kitabu Fungate ya Uhuru linasadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu.Mwandishi ameonesha jinsi viongozi wetu walivyo kwenye
fungate ya Uhuru.Hali kadhalika wananchi bado wanaendelea kugharamia sherehe
mbali mbali za viongozi kwa njia ya michango kama vile kodi,mchango wa mwenge,
n.k.
KUFAULU KWA
MWANDISHI
Kimaudhui
v
Mwandishi
amefaulu Kuonesha matatizo mbali mbali ya jamii zetu na mbinu za
kuyaondoa/kuyatatua matatizo hayo.
Kutofaulu kwa Mwandishi
v
Mashairi
mengi yanahusu siasa na hivyo kuwa kama
mahubiri ya kisiasa.
v Amesisitiza
mfumo wa chama kimoja badala ya mfumo wa mageuzi na kitabu hiki kiliandikwa wakati mfumo wa
mageuzi umepamba moto dunia nzima.
v Kumfanyia Mwinyi
kampeni ni udhaifu,hii ni kutokana na ukweli kuwa Rais Mwinyi hakuweza kuondoa
matatizo aliyoyajadili na ndiyo maana hadi sasa yapo.
v Amekemea uongozi
mbaya,lakini hakuonesha chanzo cha uongozi mbaya na mbinu mbali mbali za
kuwapata viongozi bora hapa nchini.
v Kutumia lahaja
ya Kiunguja ni udhaifu mwingine wa mwandishi,kwani anakinyima Kiswahili sanifu
uwanja wa kukua na kuenea