FALSAFA ZA KIAFRIKA KATIKA RIWAYA YA BWANA MYOMBEKERE NA BI BUGONOKA


Dhana ya falsafa imefasiliwa na wataalam mbalimbali kama vile Njoroge na Bennaars (1986) wanafasili falsafa kuwa ni jaribio lolote la watu kufikia jibu au itiko la masuala muhimu ya maisha. Hivyo wao huona kuwa falsafa hupuuza visakale na mazingaombwe.


Odera (1990) anafasili falsafa kuwa ni taaluma ambayo kanuni za msingi kuhusu asili, binadamu, na jamii huchunguzwa na kujadiliwa. Mtaalam huyu alitazama falsafa kwa mtazamo wa kitaaluma pekee wakati falsafa huweza kutazamwa kwa mtazamo ambao falsafa ni kama mtazamo.
Kwa ujumla falsafa ni mawazo yaliyopo katika mwendo yakitaka kujua tumetoka wapi na tunaelekea wapi.

Falsafa ya kiafrika imekuwa ikizua mjadala mkubwa miongoni mwa wanataaluma ambapo kuna baadhi ya wataalam ambao huamini kuwa Afrika hakuna falsafa hasa wataalam wenye mtazamo wa kimagharibi. Wataalam hawa hupingana na kauli kwamba, Afrika kuna falsafa ambayo huweza kwatofautisha waafrika na watu wa maeneo mengine mfano wa wataalam hao ni kama George Friedrich Willhelm Hegel, ambaye alikuwa ni mwanafalsafa wa kimagharibi. Mtazamo mwingine ni ule ambao wanafalsafa wanakubaliana kuwa Afrika kuna falsafa wanasema ilianza mnamo karne ya 20 yaani kuandikwa na kusomwa. Pia katika kipindi cha nyuma falsafa ilikuepo hasa kwa kupitia fasihi simulizi. Wanafalsafa ambao wanathibitisha hoja hii ni kama wafuatao.

Temples (1945) ambaye hakuwa mwafrika lakini alithibitisha uwepo wa falsafa ya kiafrika, anasema falsafa ya waafrika inajidhihirisha katika mifumo mbalimbali ya kijamii, mila, desturi na fasihi. Anaendelea kueleza kuwa falsafa ya kiafrika hufasiliwa katika vipengele vya dini asilia, ngoma, matambiko fasihi simulizi na itikeli.

Odera (1990) anasema falsafa ya kiafrika ni mkururo wa mawazo na mjadala wa kifikra halisi za kiafrika inayoendelezwa na waafrika wenyewe ndani ya miktadha halisi ya kiafrika. Hivyo basi fasili yake imejiegemeza zaidi katika kuangalia fikra mbalimbali ambazo huonyeshwa na waafrika wenyewe juu ya mambo mbalimbali.

Mbiti (1960) anaeleza kuwa Falsafa ya Kiafrika ni uelewa wa maisha ya Kiafrika, mtazamo, mantiki na uchukulizi wa mambo unaotegemea maadili ambayo Waafrika wanayawaza, wanayatenda na kuyafanya katika mazingira tofauti ya maisha yao. Falsafa hii hujidhihirisha kwa kupitia dini, itikeli na maadili waliyonayo wenyewe. Hivyo basi maelezo haya yanajiegemeza katika hoja ya kuyafahamu maisha na mazingira ya Waafrika kupitia mitazamo ya kimaisha na kile wanachokiamini.

Hivyo basi waafrika wana falsafa yao ambayo huweza kuwatambulisha miongoni mwa jamii zingine zinazowazunguka.  
Bwana Myombekere na Bi Bugonoka ni riwaya ambayo imetungwa na Aniceti Kitereza mnamo 1945 kwa lugha ya kikerewe, katika kipindi hiki mswada huu haukufanikishwa kuchapishwa. Mnamo mwaka 1969 ndipo alipoamua kuufasili mswada huu kwa lugha ya Kiswahili japokuwa alikuwa anaumwa, na ukachapishwa mwaka 1980. Riwaya hii huzungumzia kwa ujumla mila na desturi mbalimbali ambazo hupatikana katika jamii ya wakerewe ambao hupatikana katika kisiwa cha Ukerewe. Mila na desturi hizo zimejadiliwa katika riwaya hii, hupatikana pia katika jamii mbalimbali za kiafrika, pia yamesaidia kuibua falsafa mbalimbali za kiafrika.
Vifuatavyo ni vipengele mbalimbali vya falsafa ya kiafrika ambavyo vimejitokeza katika riwaya ya Bwana Myombekere na Bi Bugonoka.

Falsafa ya ubuntu, kwa mujibu wa Samweli (2015) anafafanua falsafa hii kuwa ni ile hali ya kumjali mtu au kumsaidia binadamu mwingine kama nafsi yako, anaendelea kusema mtu mwenye utu hawezi kumfanyia mtu mwingine jambo ambalo yeye asingependa kufanyiwa. Falsafa hii imejitokeza pale ambapo Bwana Myombekere alipokwenda kutafuta ndizi kwa ajili ya kutengeneza pombe aina ya empahe ambayo alitakiwa aipeleke kwa wakwe zake ili kulipa adhabu aliyokuwa amepewa. Baada ya kufika kwa rafiki yake aitwaye Nkwesi na kumweleza alionyesha utu, kwani alikubali kumpa Myombokere ndizi pasipo malipo yoyote yale. Mwandishi analithibitisha hili pale anaposema
                                    “ …  Nkwesi akamwambia hivi, “Kama wamekwambia pombe tu,
                                    usiwe na udhia, ndugu yangu migomba ipo. Labda kama
                                   wamesema kitu kingine, lakini kama ni hiyo pombe tu
                                   uliyosema tutaipata uwapelekee, wanywe.”  …Ukurasa 69.
Hivyo basi hali hii ambayo imejitokeza kati ya Nkwesi na Myombokere inadhihirisha utu kwani Nkwesi alichukulia tatizo alilokuwa nalo Myombokere kama ni la kwake ndiyo maana aliamua kumpa ndizi bila kudai au kuomba ujira wowote ule. Pia utu unajidhirisha pale wake wa Nkwesi wote wanne walipojitolea kwenda kumsaidia kwenda kubeba ndizi alizokua amezinunua kwa ajili ya kutengenezea pombe iliyokuwa ikihitajika kwa wakwe zake. Aghalabu falsafa hii imejidhihirisha pale ambapo shemeji wa Myombekere yaani mume wa dada yake alikubali kwenda kuwasaidia kupalilia mtama na mawele. Mwandishi anathibitisha pale anaposema,
                                    “hayo si kitu, yasikusumbue, mke wangu, kwasababu
                                  huwa tunawaona watu kila mara wanasaidiana, hata
                                  wakiwa watu tu wasio na ukoo hata kidogo, sembuse
                                   yeye aliye nipa kujenga niache kumsaidia? Nikiacha
                                   kumsaidia hiyo ni fedheha kubwa mno kwangu…” (ukurasa 237)
Kutokana na hali hii huonyesha kuwa falsafa ya Ubuntu ni vema ikatiliwa mkazo miongoni mwa jamii kwani kutokana na utu huweza kupelekea mendeleo miongoni mwa wanajamii na jamii kwa ujumla.

Vilevile falsafa ya uzazi, kwa mujibu wa Samweli (keshatajwa) anaeleza kuwa katika jamii za kiafrika suala la uzazi limekuwa likitiliwa msisitizo sana kwasababu, uzazi ndiyo muhimu sana katika familia nyingi za kiafrika.  Kutokana na hali hii mwanamke ambaye hana uwezo wa kuzaa huwa hathaminiwi sana miongoni mwa familia nyingi za kiafrika. Hali hii pia imejitokeza katika riwaya tajwa pale ambapo dada wa Myombokere walipokuwa wakimtukana Bugonoka kutokana na hali ya kutozaa. Mwandishi anathibitisha hili pale anaposema;
                                    “… .Wewe ni mwanamke gani,usiyezaa! Kisha hustahili
                                    kuolewa na ndugu yetu Myombekere na uzuri wake,
                                    usije ukamwambukiza ugumba wako kefule!’ …Ukurasa 8.
Suala la uzazi limekuwa likithaminiwa sana kwa mwanamke ambaye anauwezo wa kuzaa, katika riwaya hii inajidhihirisha pale ambapo Myombekere anatoa utofauti kati ya familia yenye mtoto na ambayo haina mtoto, hili hudhihirika pale anaposema;
                                     “...Myombekere akajibu, “Hapana shemeji, kuzaa ndiyo bora,
                                     tena ndiyo kuzuri kabisa, kushinda vyote, sababu wahenga wetu
                                    walisema hivi: asiyekuwa na mtoto hutuma mguu wake. Mwenye 
                                   huwa na heshima miongoni mwa watu kuliko wewe mwenye kutuma   
                     mguu wako; japo ukiwa na mingi kuliko kiasi, vilevile huwa kazi
                     bure. Tazama, sasa kitoto hicho ulichonacho nacho hicho, kinapolia
                    nyumbani humu, hutuchangamsha sote waliomo…”  (ukurasa 225)
Hivyo basi katika falsafa za kiafrika suala la uzazi hupewa kipaumbele sana na kukitokea tatizo la uzazi mwanamke ndiye hulaumiwa sana. Pia hutumia njia mbalimbali ili aweze kupata mtoto kwasababu kuwa na mtoto ndiyo utajiri mkubwa. Vilevile suala la uzazi limejitokeza katika ukurasa wa 227.

Fauka ya hayo falsafa nyingine ni uduara, kwa mujibu wa Tempels (1945) anasema utamaduni wa mwafrika upo katika uduara kwani uduara huu huweza kuonekana katika nyumba, vyombo vya kulia chakula yaani sahani, bakuli, mitungi na urithishaji wa majina. Falsafa hii imejitokeza katika riwaya tajwa pale ambapo Myombekere ametoka kumchukua Bugonoka kwa wazazi wake mwandishi anasema
                    “… Mgawaji pombe akaichota, akampa, Myombekere
                    akaipokea akainywa kefu, iliyobaki akaigawa mke wake
                    Bugonoka na Binti Kanwaketwa, na mwanamke mzee,
                   wakainywa, wakaimaliza…”   (ukurasa 110)
Katika sehemu hii uduara umejitokeza pale ambapo watu mbalimbali walitumia chombo kimoja kunywea pombe ambayo walikuwa wamepewa. Hali hii ya kutumia chombo kimoja imejidhihirisha tena katika ukurasa wa 240 pale ambapo wakulima wa umoja na watu waliosaidia kupika walipo kuwa wakinywa empahe kwa kutumia chombo kimoja. Kwahiyo hali hii huonyesha uduara miongoni mwa jamii mbalimbali za kiafrika. Pia falsafa hii imejidhihirisha pale ambapo walikuwa wakicheza ngoma. Mwandishi anasema;
                   “… Hapo sauti ya ngoma hizo yaani emilango
                   zikapasua hewa. Katika mji wa Omukama wa
                   wanaume kikawa kivumbi; mlio wa ngoma
                   ulipochanganyikana na mvumo wa makelele
                  ya watu wengi kukawa na sauti kama ya ngurumo
                 ya radi…”   (ukurasa 201)
 Pia hali hii ya kucheza ngoma imejitokeza pia katika Omukamazi wa wanawake pale katika ukurasa wa 192. Hivyo basi halihii huonyesha uduara au umoja na ushirikiano ambao hujitokeza katika jamii mbalimbali za kiafrika na hupelekea maendeleo miongoni mwa jamii na nchi kwa ujumla.
Kadhalika falsafa ya nguvu uhai, kwa mujibu wa Tempels (1945) anaeleza kuwa nguvu uhai ni msingi wa vitu vyote duniani. Anaendelea kueleza kuwa Mungu ndiye mwenye nguvu uhai kubwa kuliko viumbe wengine wote. Pia katika riwaya hii huonyesha kuwa jamii huamini uwepo wa Mungu na kila kitu ni mali yake pia ndiye mwenye maamuzi na vitu vyote. Mwandishi analithibitisha hili pale ambapo Myombekere anasema
                             “…Sasa sisi hapa tulipo, tu watu wa nani hasa?
                             Bugonoka hakuchelewa kumjibu, alitamka upesi
                            akasema, Tu watu wa Mungu hasa…”  (ukurasa 128)
Katika falsafa ya nguvu uhai hunyesha kuwa wanajamii wa ukerewe huamini katika uwepo wa Mungu kwani yeye ndiye mwenye mamlaka juu ya kila kitu ambacho hupatikana ulimwenguni hii pia inathibitika katika ukurasa wa 274 wakati Myombekere anasema Manani ndiye mwenye kuruhusu wapate mtoto au la. Hivyo basi falsafa hii huonyesha kuwa waafrika huamini katika Mungu ambaye huabudiwa tofauti tofauti katika jamii za kiafrika.

Aghalabu falsafa ya uchawi, kwa mujibu wa Samweli (keshatajwa) anaeleza kuwa uchawi upo na uwezo wa kuwadhuru watu. Hivyo basi jamii nyingi za kiafrika hutumia uchawi ikiwa ni njia moja wapo ya kuweza kuwasaidia katika mambo mbalimbali ambayo yanawazunguka katika jamii zao. Katika riwaya tajwa uchawi umejidhihirisha pale ambapo mwandishi anasema
                              “… Baba na ndugu yangu wakapata uchungu
                              sana wakanena, Ondoka twende pamoja, huwezi
                              tena kukaa hapa, sababu wachawi hawa wameanza
                             tangu siku nyingitazama jinsi wameharibu utumbo
                              (kikaziwakotumeshuhudia wazi…” (ukurasa 21)
Katika sehemu hii wake wenza wa bibi huyu walimdhuru mwenzao na kupelekea kupata tatizo la kutoka mimba. Pia uchawi kama falsafa ya mwafrika imejitokeza tena katika ukurasa wa 103 pale ambapo Nakutuga anasema “alivaa hirizi ili kujilinda na ugonjwa uliyonipa kwenda chopi”. Jamii nyingi za kiafrika zimekuwa zikitumia uchawi kama ni moja wapo ya njia ya kuonyesha fahari pia wametumia njia hii kuwadhuru watu wengine.
Aidha falsafa ya uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke, kwa mujibu wa Samweli (keshatajwa) anasema mwanamke ni kiumbe dhalili ya mwanaume. Hivyo huwa hakwezwi katika falsafa ya kiafrika huwa na jukumu la uzazi na ulezi. Falsafa hii imejitokeza katika riwaya tajwa mwandishi analithibitisha hili pale anaposema
                                                     
                              “…kwani mwanamke huolewa ili akae pamoja na mumewe
                              kumpikia chakula, kumtandikia kitanda, na kumlimia chakula
                              na hasa kabisa kumzalia watoto na kuwalea basi…”(ukurasa 228)
 Hivyobasi falsafa hii huonyesha uhusiano ambao huchukuliwa miongoni mwa wanawake na wanaume, katika falsafa hii mwanamke anaonekana kuwa dhalili au kiumbe dhaifu juu ya mwanaume. Kutokana na hali hii imepelekea wanawake wengi wa kiafrika kutokuwa na uamizi juu ya masuala mbalimbali yanayo wazunguka.
Aghalabu falsafa ya uganga, kwa mujibu wa Samweli (keshatajwa) anasema uganga huweza kutoa ufumbuzi wa matatizo yaliyoshindikana katika jamii. Hivyo basi kupitia uganga watu mbalimbali wamekuwa wakitatuliwa matatizo yao. Falsafa hii imejitokeza kama ifuatavyo;
                              “…leo safari hii usimtazame tu; utamtafuatia kwa
                               waganga dawa au hirizi za kumkinga maovu
                               yanayomharibia mimba, uovu ulio kwa mke wako
                             au labda kwako mwenyewe mjini mwako humu.” (ukurasa 225)
Pia uganga ulisaidia kufukuza ndege waliokuwa wakila mawele kule shambani. Katika jamii za    kiafrika uganga umesaidia familia mbalimbali kuweza kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ambayo yalikuwa yakiwakabili.
Aghalabu falsafa ya kifo, kwa mujibu wa Mbiti (1960) anasema kifo humuondoa mtu taratibu kutoka sasa na kumpeleka zamani. Anaendelea kusema kwamba mtu hufa taratibu mpaka watu wanaomkumbuka waishe. Pia anaendelea kusema kwamba watu mbalimbali katika jamii huogopa na kukwepa kifo. Kuwapo kwa falsafa ya kifo kunajitokeza pale ambapo mhusikaMyombekere na Bugonoka wanapata taarifa juu ya tanzia ya shangazi yake Bugonoka. Mwandishi anasema;
                              “…wametuletea tanzia ya kama shangazi ya mke wangu
                             amekufa, lakini amepigwa na radi…Lakini kisa ni kilicho
                             nileta kwako hapa, nimekuja kwa ajili ya kukuuliza: Sasa
                            mke wangu, amekwisha kuwa mjamzito hivi, anaweza kuwalilia
                          wafu na kukaa matangani?” (ukurasa 234)
Kupitia riwaya tajwa mwandishi anaonyesha jinsi wanajamii wanavyoogopa kifo, na athari zake miongoni mwa jamii.
Falsafa ya kazi, kwa mujibu wa Samweli (keshatajwa) anaeleza kuwa kazi ni jambo linalothaminiwa sana katika jamii za kiafrika. Katika jamii za kiafrika mtu ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kujishughulisha na kazi mbalimbali aliweza kufanikiwa katika shughuli hizo, pia haikuwa rahisi kuweza kupata janga la njaa katika nyumba au familia yake. Anasema
                           “…Nitengenezee jembe mimi nipate kulima viazi, kwa sababu
                           naona mwaka wa kulima mawele umepunguka, sitasumbukia
                          bure kulima chakula cha kupata hasara tu, maana matembele
                       (mbegu ya viazi) ni tele kwa wakulima.” (Ukurasa 133)  
Hivyo basi kutokana na ukulima wa Bugonoka wa mazao mengi ulimsaidie kuweza kuepukana na janga kubwa la njaa. Vilevile falsafa hii imejitokeza katika ukurasa wa 237, katika jamii za kiafrika kuna jamii ambazo hujikita katika kufanya kazi mbalimbali ambazo zilipelekea maendeleo na kuepukana na hali ya utegemezi.
Kwa ujumla riwaya ya Bw Myombekere na Bi Bugonoka imesaidia kuonyesha falsafa mbalimbali ambazo hupatikana miongoni mwa jamii mbalimbali za kiafrika. Falsafa hizi zimeonekana kuwa ni mwongozo muhimu kwa waafrika hawa kwani kutokana na uwepo wa falsafa hizi. Jamii mbalimbali za kiafrika zimefanikiwa kujua miiko na tamaduni ambazo ni muhimu zikafuatwa miongoni mwa jamii husika. Hivyo basi kutokana na uwepo wa wa falsafa hizi huonyesha kuwa waafrika wana falsafa yao ambayo huwaongoza na kuwatofautisha na jamii nyingine.

                                                       
                                                               



                                            

                                                            MAREJELEO.
Kitereza, A. (1980). Bw. Myombekere na Bi. Bugonoka na Ntulanalwo na Bulihwalo: Juzuu ya 
                                 Kwanza. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.
Mbiti, J. (1960). African Religions and Phylosophy. New York: Praeger Publisher.
Njoroge na Bennars. (1986). Philosophy and education in Africa.Nairobi Transafrica
Odera, H. O. (1990). Trends in Contemporary African Phylosophy. Nairobi. Shirikon Publisher.
Samwel, M. (2015). Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: Mevel Publisher.
Temples, P. F. (1945). Bantu Phylosophy. London: Presence African Publishers.
Powered by Blogger.