SIMULIZI


 ILIPOISHIA: Wakati mazungumzo yakiendelea, mume wa Lina alifunga breki nje ya nyumba ya Eg na kupiga honi ana shida na mke wake huyo…

“Pii pii piii!”
JIRUSHE MWENYEWE SASA…
Eg ndiye aliyechungulia nje baada uya kusikia honi ya gari, akashtuka sana na kusema…
“Ha! Lina, shemeji Semi…”
“Kweli?”
“Mungu tena, amesimamisha gari hapo nje.”
“Mungu wangu, sasa?”
“Hata sijui! Kwani amefuata nini huku? Au ametonywa ishu nzima?”
“Hapana, atakuwa ana shida na mimi. Lakini sasa nimeshavaa itakuaje? Si ataniona nimekuwa rasmi sana kuliko huyo niliyemsingizia?”
“Na kweli.”
Semi alipiga tena honi, Eg akatoka. Lina alivua gauni la kitchen party na kuvaa alilokwenda nalo kisha naye akatoka. Ndugu na marafiki wa Eg nao wakafuata hadi kwenye gari…
“Shem mambo?” alisalimia Eg…
“Poa, mzima wewe?”
“Mimi mzima. Karibu sana.”
“Asante sana.”
“Huyu ndiye shemeji kwa Lina?” ndugu mmoja wa Eg aliuliza akiamini Semi ndiye bwana harusi mtarajiwa…
“Eee, ndiyo huyu.”
“Oo! Karibu sana shemeji…sisi leo mambo yatakwenda vizuri kabisa ukumbini…bibiye atapendeza kupita kawaida,” aliropoka yule ndugu bila kujua kwamba anakaribia kulipua bomu.
Kilichosaidia ni kwamba, maneno yake yalifunga ufahamu wa Semi kwani kule kusema sisi leo mambo yatakwenda vizuri, Semi alijua ni sherehe ambayo mkewe alishamwambia ipo.
Kule kusema bibiye atapendeza kupita kawaida hakukumfanya Semi ahisi kitu kwani ni kweli mke wake alitoka nyumbani na gauni zuri la kitenge ambalo alisema atalivaa kwenye kitchen party ya rafiki yake, ubaya uko wapi sasa!
“Sawa jamani, nawatakia sherehe njema, nimekuja kumpa maagizo huyu, mimi nakwenda Morogoro nikichelewa nitarudi kesho.”
“Sawa mume wangu,” alisema Lina. Mwanamke mmoja akadakia…
“We, bado hajawa mume wako, atakuwa mumeo ukishafunga naye ndoa.”
Lina na Eg walishtuka sana kwa kauli hiyo, walijua sasa mambo hadharani lakini katika hali isiyotarajiwa, Semi akajibu…
“Tufunge ndoa mara ngapi? Shemeji Eg hujawaambia nini?” akawasha gari na kuondoka huku akicheka.
Mambo yalikuwa mambo, mkorogano ulitawala kila aliyesema, aliyesikia alitafsiri vingine kabisa.
Hata yule mwanamke aliyejibiwa kwamba ‘tufunge ndoa mara ngapi?’
alijua ameambiwa kwa kutaniwa kwani alijua ile kitchen party ya Lina, muoaji mwenyewe ndiye yule. Na Semi naye alijua yule mwanamke ameuliza kwa sababu ya ugeni, hajui kama Lina yupo kwenye ndoa ndiyo maana akamwambia Eg, ‘shemeji Eg hujawaambia nini?’
***
Lina aliendelea kujipamba, magari mawili ya kukodi yakafika kwa ajili ya kupelekwa ukumbini.
Shamrashamra ukumbini zilinoga kama si kuvutia, kwani kila kitu kilikwenda sawasawa. Lina pamoja na kwamba alitegemea michango lakini yeye mwenyewe kwa kupitia kwenye mfuko wa James alichangia fedha kwa kiasi kikubwa na kusababisha bajeti kwenda ilivyopangwa.
Shughuli ilikuwa nzuri, waalikwa walikula la kunywa na wakasaza huku kila mmoja akimpongeza Lina.
Lakini muda mwingi wa sherehe hiyo, Lina alipenda kuinamisha kichwa ili kukwepa macho ya watu akiamini pengine kuna ambaye atakuwa anamjua. Mbali na macho ya watu, awali kabisa Eg alishawatangazia waalikwa kuachana na kupiga picha kwa kutumia kamera za kwenye simu zao. Na wala hakukuwa na mpiga picha aliyekodishwa.
Baada ya shughuli hiyo, Lina alikwenda kulala kwa Eg baada ya kumpigia simu mume wake na akamwambia hatarudi toka Morogoro.
Usiku Lina alianza kuchati na James…
“Baby sherehe ilikuwa nzuri sana, nimemaliza kazi bado kwako ndoa wikiendi ijayo.”
“Niko fiti baby, mipango yote tayari. Tutakwenda fungate wapi baby?” aliuliza James swali lililomuumiza sana Lina kwani alijua kwenda fungate ni kubumbulua mambo kwa mume wake, atamuaga anakwenda wapi!”
“Popote pale my dear,” alijibu Lina.
Kama wangekuwa wanaongea kwa sauti angeshangaa kusikia sauti ya Lina inazungumza kwa unyonge wa hali ya juu.
“Basi niachie mimi, nitachukua hoteli nzuri sana tena kubwa ya hapa mjini. Au unataka twende nje ya mji kama Zenji?”
“Noo! Hata hapa Dar panatosha sana my love.”
Walichati mpaka saa tisa kasoro lakini muda mwingi akili ya Lina ilikuwa haipo sawa. Kuna wakati alitamani hata kufunguka lakini alishindwa kwa sababu walishafika mbali na angesababisha mawazo ya James kuamini kwamba wanawake ni wabaya sana.
Siku ya ndoa ndiyo ikafika sasa, Lina alikuwa anajiandaa kivyake na James kivyake walikubaliana wakutane kanisani na kuungana kuingia ndani kwa ibada ya ndoa.
“Uko wapi Lina?”
“Kwa dada, ndiyo tunataka kutoka kwenda saluni my dear.”
“Lina usinitibue, kwa dada saa hizi wakati unajua kanisani tunatakiwa saa nane kamili mchana, sasa uende saluni saa sita hii utamaliza muda gani? Kanisani utakuja saa ngapi na ndoa itafungwa saa ngapi au hutaki tufunge ndoa Lina?”
“Nitamaliza mapema tu.”
Mara Lina akakata simu…
“Khaa! Yaani Lina kanikatia simu mimi? Ana maana gani?” alijiuliza James. Alipopiga tena iliita bila kupokelewa…
“Afadhali isingepatikana ningesema chaji imeisha, sasa hapokei ana maana gani?” James aliendelea kuwaza…
Lina alichukua Bajaj ambayo ilimfikisha nyumbani kwake akiwa amechoka sana. Ile anaweka simu mezani tu, mumewe Semi akaichukua.
“Kuna mtu nataka kumpigia nijue alipo halafu simu yangu haina hela,” alisema akiminya vitufe.
Moyo wa Lina ulilipuka kwani alikumbuka kuwa ndani ya simu hiyo kulikuwa na meseji za James ambazo hakuzifuta na zilisomeka vibaya kama zingeonwa.
Alitaka kupeleka mkono kumpokonya mume wake lakini alijua akifanya hivyo pia angempa picha mbaya kama nia yake haikuwa kupekua meseji.
Semi alipiga simu na kuongea na mtu ambapo alisikika akisema…
“Wee kama nilivyokwambia, hakikisha unatumia kila njia ili tuujue ukweli wa mambo. Unajua hakuna kitu kibaya kama mke awe wako halafu kumbe kuna mwingine anamwona ni mke wake, hiyo ndiyo maana yangu kuu.
“Sawa kaka, sawasawa, fanya uchunguzi wako halafu utanipa majibu.”
Lina aliishiwa nguvu, miguu ilimtetemeka, akataka kukaa lakini akajisikia kuumbuka. Alitamani kuuliza kinachoendelea, pia akashindwa.
Semi hakuwa na nongwa, alimrudishia simu yake huku akimwangalia usoni ambapo Lina aliamua kuukimbiza uso wake pembeni.
“Pole na starehe,” alisalimia Semi, Lina akashindwa acheke au ajibuje…
“Nzuri.”
“Mambo yaliisha salama?”
“Ndiyo.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo, kwani umesikia nini?”
“Nimesikia umenisaliti.”
Lina moyo ukamfanya paa! Mpaka akajishika kifua kwa hofu…
“Mungu wangu,” alisema ndani kwa ndani…
“Pole lakini, maana kulala nje ya nyumbani nako...” Semi alisema huku akicheka, kidogo Lina akajua mumewe anafanya utani kwani kwa anavyomfahamu asingeweza kucheka kama angekuwa analo jambo moyoni.
Lakini bado yale maneno aliyoongea mumewe na mtu kupitia simu yake kwamba achunguze mtu anaweza kusema ni mke wake kumbe kuna mwanaume mwingine naye anasema ni mke wake yalimtesa akilini.
Alienda chumbani huku akifungua simu kuangalia namba iliyopigwa, akabaini ni ya mtandao ambao anao na yeye hivyo aliisachi…
“Issac Majurila ni nani, mbona sijawahi kumsikia,” aliwaza moyoni. Aliamua kumsaka ili kujua mumewe alimwambia amchunguze nani ambaye anaweza kuwa mke wa mtu kumbe kuna mwingine anasema ni mke wake!
***
“He! Kumbe leo ni Jumapili, nilisahau kabisa, nikajua utachelewa kazini,” alisema Semi akiwa ameingia chumbani ambapo hata Lina mwenyewe alishtuka, akakumbuka kwamba, alifunga ndoa jana yake Jumamosi, amelala na James usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili.
“Mh! Mi mwenyewe kusema za ukweli nilijua leo ni siku ya kazi,” alisema Lina akiendelea kushangaa. Mara simu yake iliingia meseji, akaisoma chapchap...
“Baby leo ni Jumapili, sasa umeondoka bila kusema utakuja muda gani?”
Lina aliijibu palepale…
“Mchana nitakuwa hapo baby, hata mimi nilisahau kabisa kwamba leo ni Jumapili, sijui ni kwa nini wote tulisahau.”
“Oke, ilitokea tu, uje basi kwa muda huo.”
Bahati nzuri pale nyumbani napo, Semi aliaga anakwenda kwenye shughuli zake hivyo Lina akabaki yeye na msichana wa kazi tu. Ikawa ni nafasi yake ya kurudi hotelini aliko James.
Alikwenda sebuleni, akazima tivii maana alimkuta mumewe Semi ameiwasha akitazama mambo mbalimbali. Lina aliizima kwa sababu alihisi inamchanganya, kwa wakati huo alihitaji kutafakari zaidi kwa kitendo alichokifanya.
Kwanza alijua amemfanyia kitendo kibaya sana James, kufunga naye ndoa ambayo ni batili. Alihisi huruma anatakapogundua wakati mwenzake mapenzi yote aliyaelekeza kwake kama mke.
Pili, alimini kuwa James anajua amejikomboa kwa kupata mke na yeye anapitia sera za kike maana yake ametoa mkosi, sasa kumbe badala ya kuondoa mkosi amejiongezea…
“Hivi huu mtego nitawezaje kujinasua nao? Ni kwa nini nimeuingia? Ni tamaa ya hela au mapenzi ya dhati?” aliwaza Lina. Lakini kwa harakaharaka alipata jibu kwamba, zile laki mojamoja kila kukicha zilimchanganya akili licha ya kwamba ni kweli James ni kijana mtanashati sana.
Lina aliamua kumpigia simu shoga yake, Eg na kumwambia anavyojisikia…
“Halo Lina…”
“Eg…”
“Bee.”
“Naweza kujiua mwenzio.”
“He! Kwa nini Lina, kuna nini kimetokea? Shemeji kajua?”
“Hapana! Ila…”
“Ila nini tena Lina?”
“Unajua nimefanya jambo la kipuuzi sana? James anajua mimi ni mke wake wa ndoa. Halafu sasa, mbaya zaidi ndoa yenyewe ya Kikristo, ni kama loki. Siku akijua nina mume tena wa ndoa nini kitatokea?
“Mtu mwenyewe ana hela, nahisi atanifunga na hakuna wa kunitetea. Najuta Eg, najuta kabisa. Sijui ni kwa nini na wewe rafiki yangu kipenzi hukinikataza?”
“Lina, nisingekukataza mtazamo wako na wangu ni mmoja tu. Kama ni kujuta sasa tujute wote, kwani kwa maneno yako ya saa hizi hata mimi nimegundua hilo…”
“Eg subiri nipokee simu ya James…halooo.”
“Mke wangu Lina…”
“Abee baba.”
“Mwambie dada ukija mchana hakuna kurudi tena huko. Utakuwa unatokea hapa kwenda kazini na kurudi mpaka siku tano tunahamia nyumbani, hivyo ukija beba nguo zako kwenye sanduku chukua teksi.”
“Mh! Sawa baby.”
“Mbona umeguna kwanza?”
“Basi tu, nafikiria jinsi ya kumwambia huyo dada.”
“Unafikiria jinsi ya kumwambia dada? Kwa nini ufikirie? Mimi si mume wako kwa sasa? Tena wa ndoa.”
“Ni kweli my love.”
“Sasa?”
“Oke, nimekuelewa.”
James alikata simu na kumwacha Lina katika mawazo kibao…
“Da! Nimeingia mkenge kwa kweli. Hapa sina cha kujitetea, siwezi kutengua ndoa tena. Imefungwa imefungwa tu. Kinachotakiwa ni kuamua moja, kusuka au kunyoa…
“Semi mume wangu akijua sijui nini kitatokea. Da! Balaa! Hivi kama ni tamaa, tamaa gani ya hivi mimi Lina mimi? Haya mambo si yanaweza kufika kwa wazazi? Yakifika nitajiteteaje?”
Lina alikosa ujasiri wa kufikiria kiasi kwamba alianza kutoa machozi mwenyewe…
“Mungu wangu, nisaidie mimi. Nimekwaa tatizo kubwa.”
Kwa upande wake James baada ya kumkatia simu Lina naye alizama kwenye maswali kibao huku akikosa majibu ya moja kwa moja…
“Ni kwa nini Lina anamuogopa dada yake kiasi hicho? Yeye si mke wangu wa ndoa? Sasa nini kitamfanya huyo dada azuie Lina kuondoka?
“Halafu, kwani mbona siku ya harusi ukumbini sikumwona huyo dada yake akitambulishwa? Maana kama ndiye ameishi naye alitakiwa kutambulishwa kama mzazi wa Lina kwa hapa Dar es Salaam.”
Kifupi wote walikuwa katika wakazi mgumu sana, kila mmoja alikuwa na maswali yake yaliyokosa majibu ya moja kwa moja kwa pale.
***
Mchana ulifika, Lina mapigo ya moyo yaliongezeka kwa sana. Kila dakika ilipokatika aliitupia macho simu yake akiamini James atapiga…
“Huyu atapiga sasa hivi,” alisema moyoni. Aliwaza amwambie nini mume wake, Semi ili aondoke kurudi hotelini aliko James lakini pia alijiuliza akienda bila nguo ataelewekaje kwa mumewe huyo?
Kama aliota, simu ya James iliita. Aliitupia macho kwa dakika moja nzima mpaka akakata. Ikapigwa tena ndipo akapokea…
“Baby…
“Mbona hufiki? Nikufuate?”
“Noo baby, nilikuwa naweka nguo zangu kwenye begi nakuja.”
“Poa.”
James akakata simu kwa dalili zote kwamba amekasirika na mwenendo wa Lina kwa siku ile.
Lina alimpigia simu mume wake ili amdanganye kitu…
“Baby…”
“Ee baby…”
“Kuna balaa juu ya balaa,” alisema Lina…
“Lipi tena baby?”
“Yaani Eg ana dada yake alikuwepo kwenye sherehe ya jana, amefika kwake ameumwa ghafla kakimbizwa Muhimbili…”
“Duu! Balaa. Sasa?”
“Sasa nakuomba ruhusa niende Muhimbili mchana huu maana Eg naye anakwenda.”
“Sawa! Lakini huyo atakuwa amekula kitu kibaya, unajua sherehe sherehe hizi mambo hayo hutokea. Ngoja nikupe namba ya Dokta Matingisha ukifika umpigie ili asaidie.”
“Itakuwa vizuri baby.”
Lina aliachia tabasamu, akapata akili. Alichukua begi, akatoa kwenye kabati lake nguo za zamani kibao na kuziweka kwenye begi.
Kama vile hiyo haitoshi, akafunua godoro ambapo pia mlikuwa na nguo nyingine, nazo akazitia kwenye begi mpaka likavimba. Akachukua Bajaj hadi hotelini alipo James.
***
Eg alikuwa hana hili wala lile, simu ya shemeji yake Semi ikaingia kwake…
“Mh! Huyu shemeji vipi, si kawaida yake kunipigia simu,” alisema moyoni Eg huku akiwaza apokee au la! Akaamua kuipokea…
“Haloo shem…”
“Shemeji poleni sana na mgonjwa jamani! Aisee,” alisema mume wa Lina…
“Mgonjwa?” alihoji Eg…
“Si Lina ameniambia kwamba…”
Eg alikata simu haraka sana. Akampigia Lina…
“Shoga…”
“Ee shoga vipi?” alisema Lina…
“Umemwambia shemeji nina mgonjwa?”
“Ha! Ndiyo Lina, kakupigia? Please mwambie unaye, nimemwambia ni dada yako amelazwa Muhimbili anaumwa sana tumbo la kuendesha na yuko hoi…”
“Oke, tena huyo anapiga ngoja nipokee…
“Haloo shem…”
“Shem, naona mtandao unasumbua…Lina kaniambie una mgonjwa.”
“Eee, unajua nilidhani unasema wewe ndiyo una mgonjwa ndiyo maana nikauliza mgonjwa gani?! Dada yangu bwana, anasumbuliwa na tumbo tukamkimbiza Muhimbili.”
“Da! Poleni sana, lakini Mungu atamsaidia.”
“Asante sana shemeji.”
“Oke shemeji. Sisi tupo, yeye kaniambia anakuja Muhimbili.”
“Ee, na mimi naelekea huko shemeji yangu.”
“Sawa, baadaye.”
***
Lina alifika hotelini, akasukuma mlango na kuzama kwenye chumba alichomo mume wake wa pili James…
“Hodi.”
James alifungua mlango, ukawa wazi mpaka mwisho. Lakini alionekana kukunja sura na kupoteza uchangamfu kuliko siku nyingine.
“Karibu.”
Lina aligundua James hakuwa sawa…
“Baby kama haupo sawa, kuna nini?”
“Lina, mimi ni nani kwako?”
“Mume wangu.”
“Unatakiwa kumsikiliza dada ‘ako au mimi?”
“Wewe.”
“Basi naomba unisikilize kuanzia sasa.”
“Kwani sikusikilizi baby? Mbona mimi nakusikiliza sana jamani.”
“Lakini si kwa kiwango kinachotakiwa Lina, ongeza usikivu wako kwangu. Mbona mapema sana kuanza kuonesha si msikivu!”
“Nisamehe mume wangu.”
“Oke, yamepita nakupenda sana.”
“Asante baby, nakupenda pia.”
Walikumbatiana wakaganda kwa muda huku kila mmoja akimtazama mwenzake machoni, mwishowe wakaachia tabasamu laini, wakapanda kitandani ambako Lina ndiye aliyeanzisha kupeana muwashawasha kwa James naye akapokea, wakakukuruka mpaka wakaingia uwanjani kuanza mchezo.
***
Usiku uliingia, Lina alikuwa akipiga mahesabu ni uongo gani atamwambia mume wake akaeleweka ili asirudi nyumbani siku hiyo. Kwa siku hiyo kumpigia asingeweza maana muda wote James alikuwa yuko naye beneti. Akaamua kutuma meseji.
“Baby, hali ya dada’ke Eg bado si nzuri. Naomba nilale hospitali maana naye Eg ana mgonjwa mwingine pale kwake.”
Baada ya kutuma meseji hiyo, kila sekunde Lina alikuwa akiiangalia simu yake ili kuona kama meseji ya majibu itaingia.
Zilikatika dakika kumi meseji yake haijajibiwa, mwishowe akaanza kuingiwa na wasiwasi kwamba huenda mume wake hajapenda ruhusa hiyo na kama ndivyo, ataagaje kwa James ili arudi nyumbani. Mara, meseji ya mume wake Semi iliingia.
“Sijakubaliana na wewe, Eg aangalie utaratibu mwingine wa mtu wa kulala na mgonjwa wake na si wewe.”
Ni kujikaza tu, lakini Lina alibadilika rangi muda uleule ila alijichangamsha ili kutompa nafasi James kumsoma. Moyoni alijua kuna ugumu mkubwa kwa James kumkubalia aondoke. Kwanza atasema anakwenda wapi?
“Mh! Nimeyavulia nguo mwenyewe, lazima niyaoge sasa,” alijisemea moyoni huku akianza kutetemeka mpaka James akajua.
“Vipi baby mbona kama unatetemeka?”
“Wala, niko fiti tu.”
Kwa mbali Lina alipata akili kwamba, amtumie meseji Eg na kumwambia apige simu kwake aseme kuna shangazi mgonjwa amepelekwa Muhimbili muda huo, awahi Muhimbili.
Baada ya kujiridhisha kwamba itakuwa sawasawa, Lina alituma meseji hiyo kwa Eg ambaye alijibu kwa ufupi poa! Lakini akatuma nyingine akimuuliza apige simu au atume meseji?
“Piga kabisa,” alijibu Lina.
Alijifanya anakwenda chooni ili simu ya Eg ikiingia ipokelewe na James na ikibidi ujumbe huo upokelewe na yeyeyeye James.
Ile anafika chooni tu, simu yake ikaita. James akatupa jicho kwenye skrini, akasoma jina akamwita Lina.
“Baby…”
“Abee…”
“Kaka Semi.”
Kaka Semi ni mume wa Lina. Wakati anakwenda hotelini hapo aliamua kubadii jina la mume wake, badala ya kuandika My Huzband kama ilivyokuwa mwanzo, akaandika kaka Semi akiamini kwamba anaweza kupiga wakati yeye yupo na James itakuwa soo kuonekana My Huzband!
Lina alitoka mbio huku mapigo ya moyo yakimwenda kasi kwa sababu hakutegemea kama mumewe angepiga simu muda ule.
Lina aliipokea simu kutoka kwenye mikono ya James akiwa haamini maana alijua kuwa hata kama James angeamua kupokea na kusema ‘mwenye simu yuko mbali’ au ‘subiri kidogo’ ingekuwa soo kwake.
Pia alijua kuwa, James angeweza kuipokea simu hiyo kwa lengo la kusalimiana na shemeji yake huyo aitwaye Semi kwa mujibu wa jina la kwenye skrini ya simu.
Lina alijifanya anaipeleka simu hiyo sikioni huku akiikata halafu akajifanya anaongea.
“Shikamoo kaka Semi…mimi sijambo, za huko? Hawajambo wote? Sisi tunaendelea vizuri, utakuja lini? Haya karibu sana, shemeji yako utamuona tu ukija, yupo! Haya kwa heri kaka.”
Alipomaliza kusema kimagirini, alituma meseji kwa mumewe.
“Kuna daktari kapita wodini, nitakupigia. Lakini pia nitakuja nilikuelewa.”
Alichokitaka Semi ni hicho kujua kwamba, kukataa kwake Lina asilale hospitali alielewa. Mara, ikaingia simu ya Eg, Lina akiwa amesimama dirishani, James akatupia tena macho na kumwambia...
“Eg anapiga, ngoja nipokee nimsalimie…shemeji mambo? Ee…yupo…nani? Amelazwa..? Hospitali gani? Hebu ongea na Lina huyu hapa shemeji…”
“Haloo…amelazwa? Anaumwa nini? Oke, nakuja basi.”
Lina alikata simu na kumgeukia James…
“Vipi?” aliuliza James…
“Mh! Majanga… itabidi niende hospitali.”
“Ameniambia aisee. Da! Sasa si itabidi nikupeleke?”
“Utanipeleka? Si ulisema unapenda wiki nzima ushinde ndani tu!”
“Ni kweli, lakini sasa wewe utaendaje?”
“Nitachukua Bajaj…”
“Kwanza leo nataka kukwambia jambo, mambo ya kupandapanda Bajaj yaishe, sitaki kuona. Nitakununulia gari tukimaliza fungate, kwa hiyo itabidi ujifunze kuendesha…ila leo nenda na teksi,” alisema James huku akimwagiza Lina kutoa pesa kwenye brifkesi…
“Nichukue shilingi ngapi?”
“Unayoona inatosha.”
Lina alitumbukiza mkono akaibuka na shilingi elfu hamsini…
“Nimechukua hamsini.”
“Sawa, kawape pole wote.”
Lina alichukua Bajaj hadi nyumbani kwake ambapo alimkuta mumewe, Semi. Swali la kwanza alilokumbana nalo kwa mumewe ni kuhusu pete ya ndoa na ya uchumba…
“Baby, hivi hizo pete ulizipeleka tena kwa sonara nini, maana naziona zinang’aa sana siku mbili hizi.”
“Nilipeleka zikaoshwa. Niliona zimeanza kuingia giza.”
“Oke, zimekuwa nzuri sana,” alisema Semi bila kujua kwamba zile ni pete mpya ambazo alizinunua James kwa ajili ya ndoa hiyo.
***
Lina amefika kwake, kazi ikawa kumsikilizia James akipiga kuulizia kuhusu mgonjwa. Aliumia sana moyoni kiasi kwamba alitamani kumwandikia meseji amwambie ukweli kwamba yeye ni mke wa mtu, tena kwa ndoa lakini kila alipofikiria kuhusu hilo akiamini hata James alifunga naye ndoa alikosa la kufanya.
Eg alimpigia simu Lina na kumuuliza kama dili lao lilitiki au la! Alipoambiwa limetiki, akacheka sana na kukata simu huku moyoni akisema…
“Lakini sisi tuna hatari sana. Ni kweli Lina ataweza kudumu na James kwa muda mrefu bila kujulikana? Sidhani aisee!”
***
Saa kumi na mbili jioni, Lina akiwa chumbani simu yake iliita. Na muda huo aliamua kwa makusudi kuwa chumbani akijua lazima James atapiga…
“Haloo,” alipokea kwa sauti ya chini, mume wake alikuwa amekaa sebuleni…
“Vipi mgonjwa?”
“Mgonjwa hali mbaya James, hivi hapa daktari ndo ameingia sasa hivi.”
“Mh! Sasa itakuaje? Ahamishwe hospitali.”
“Sijajua ndugu watasemaje maana waliondoka na hawajarudi. Hivi nilitaka kukwambia naomba nilale nitoke asubuhi kuja huko.”
ITAENDELE BAADAE ....NAITAJI COMMENT YAKO KABLA SIJAENDELEA ILI NIJUE KAMA
Powered by Blogger.