NADHARIA

 

Nadharia ni dhana iliyofafanuliwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo Wafula na Njogu (2007.7) nadharia ni jumla ya maelekezo yanamsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu.


TUKI (2004:300) nadharia mawazo, maelezo au muongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza kutatua au kutekeleza jambo fulani. Tunakubaliana na fasihi iliyotolewa na Wafula na Njogu, kutokana na kwamba fasihi hii imetaja vitu muhimu kama vile maelekezo ambayo ndiyo yanayomuongoza msomaji au mhakiki ili asivuke mipaka ya mawazo ya hiyo nadharia aitumiayo ili kufanikisha kazi kwa ufasaha. Tumejadili nadharia ya uchanganuzi nafsi kama ifuatavyo;

Nadharia ya uchanganuzi nafsi imeasisiwa na Sigmund Freud, Carl Gustav na Jacques Lacan. Sigmund Freud (1856-1939) kuna utambuzi wa kawaida na utambuzi bwete. Utambuzi wa kawaida ni sehemu ya ubongo ambayo kimsingi hupanua na kudadavua yanayoendelea hususani mchana. Utambuzi bwete hufanya kazi wakati binadamu anapolemazwa na usingizi. Baadhi ya mambo anayoshuhudia binadamu mchana yanaingia kwenye utambuzi bwete wake na kutokea katika ndoto zake usiku. Mambo yanayopatikana katika utambuzi bwete yana sifa hasi, Sigmund Freud anasema kuwa, binadamu huyaficha na kuyabania kwenye utambuzi bwetemambo ambayo hawezi kuyasema hadharani. Matamainio yasiyokubalika, makatazo yajamii, fikra na kauli zilizoharamishwa na miiko ya kijamii hubanwa katika utambuzi bwete. Fikra hizo ndizo zinazochipuka kwa njia ya ishara za ndoto, mitelezo ya kauli yaani maneno au kauli zinazotutoka bila wenyewe kukusudia. Pia huhusisha masuala ya saikolojia, matukio yaliyomtokea mtu yanayomwathiri. Mgonjwa hupaswa kusimulia kila kitu kama vile ndoto, hadithi na visasili na matokeo mengine. Lakini Carl Gustav Jung alikataa kuwa binadamu huzaliwa na matamanio ya kingono. Aliona mtoto anazaliwa katika hali ya unyoofu na usafi. mfano katika hadithi ya mtoto shujaa tunaona ushujaa unaonesha unyoofu na ukweli wa watoto.

Tumejadili nadharia ya Umarx kama ifuatavyo; maana ya Umarx, Wamitila (2006:132) anasema, Umarx ni falsafa ya yakinifu hasa kwa kuwa pana msisitizo mkubwa kwenye msingi wa hali ya kiyakinifu ya maisha kama mazingira ya kuishi kuliko mawazo katika maisha ya binadamu likimaanisha kwamba mawazo yake hayategemei kwenye dhana dhahania kama vile urembo, ukweli au ndoto bali yanajiegemeza kwenye uhalisia unaooneka.

Nadharia ya Umarx iliainishwa na Karl Marx mwaka 1818-1863 na Fredrick Engles (1820-1895) katika nadharia hii Marx amejikita katika historia ya jamii kwa kupitia hoja zifuatazo. Historia ya maisha ya binadamu inaweza kuelezwa katika misingi yakinifu, kiuchumi ambayo itachukuwa njia za uzalishaji mali pamoja na miundo ya kiuchumi, kuondoa matabaka katika jamii. Mfano Urusi, Ulaya, Amerika Kusini umiliki njia kuu za uzalishaji mali uwe chini ya umma. Maendeleo ya kijamii yanasukumwa na ukinzani yakinifu. Urazini wa binadamu umeundwa na itakadi, urazini umeunda namna ya kufikiri tabaka tawala linaunda kila kitu kama dini, maadili, siasa na sheria za jamii.

Hivyo basi mawazo ya uchanganuzi nafsi na Umarx yanauhusiano kama ifuatavyo;
Nadharia ya Uchanganuzi nafsi na Umarx zinahusiana katika ndoto, nadharia hizi humuhusisha binadamu pale anapopiyia mambo mbalimbali, changamoto au matatizo hivyo huwa na wazo la kuyabadilisha mazingira yake na huja kama ndoto ya kuwa anatenda. Mfano, katika katika kitabu cha Roza Mistika kilichoandikwa na Kezilahab, nadharia ya Uchanganuzi nafsi imejitokeza kumuonyesha Rosa alipokuwa safarini kuelekea masomoni aliyaota yale mambo ambayo mama yake alikuwa akimuonya juu ya maadili. Pia katika nadharia ya Umarx tunaona tabaka la chini lina ndoto ya kutokea kwa mabadiliko ya uongozi mbaya wenye uozo, mfano katika kitabu cha Usiku Utakapokwisha mwandishi Msokile anamuonyesha Gonza akiwa na ndoto ya kuondokana na umaskini na kwenda kuishi Zambia ambapo aliamini maisha yatakuwa rahisi na ataweza kupata kazi (uk. 48). Hivyo, tunaona nadharia hizi humuonyesha binadamu kama mwenye ndoto ya kufikia kitu fulani au kupata kitu fulani.

Uhusiano mwingine upo katika matamanio, watu hutamani kufanya vitu mbalimbali ila kutokana na miiko ya jamii, mila na desturi au uongozi hushindwa kufikia haja zao au matamanio. Nadharia ya Umarx kupitia kitabu cha Vuta N`kuvute mwandishi Shafi Adam tunamuona Ysmini alikuwa na matamanio ya kuolewa na kijana wa rika lake na sio mzee kutokana na kwamba hakuwa na matamanio ya fedha (uk. 3). Aidha, katika nadharia ya Umarx tunaona jamii ina matamanio ya kuondokana na matabaka, rushwa, ubaguzi wa rangi, uongozi mbaya, ukoloni mamboleo. Mfano, tunamuona Denge katika Vuta N`kuvute anasema;
                   Pale inapoyumkinika kutumia mbinu za dhahiri basi tuzitumie kadri ya
                   uwezo wetu. Pale ambapo hapana budi kutumia njia ya siri kwani
                   mapambano yetu ni vuta N`kuvute wao wanavuta  kule sisi tunavuta   huku (uk. 113). 
Hivyo, tunaona matamanio ya kuondokana na umaskini na hali ngumu ya maisha.
Pia, uhusiano mwingine upo katika historia ya binadamu, binadamu na maisha yake yanayomzunguka huwa na tabia ya kubadilika kutokana na mazingira yake. Mienendo fulani huanzia zamani mtoto anapokuwa, malezi na baadae kujitokeza akiwa mkubwa. Katika nadharia ya Uchanganuzi nafsi katika riwaya ya Roza Mistika tunamuona Roza katika hatua ya ukuaji wake alikosa malezi mazuri kutoka kwa baba yake Zakaria. Hivyo, kupelekea kufanya mambo aliyoshindwa kuyafanya akiwa anakuwa kutokana na ukosefu wa elimu ya malezi. Mwandishi anasema;
                         Hivyo ndivyo alivyolelewa, hivi ndivyo alivyotunzwa, hivi ndivyo
                         alivyochungwa na baba yake, tangu siku hiyo alikoma kutembea na mvulana
                        yeyote hakufahamu kwamba Roza alikuwa katika rika baya na kwamba ukali
                       ulikuwa haufai (uk. 9).
Hivyo, tunaona Roza alipoenda masomoni alianza uhusiano wa kimapenzi na wanaume mbalimbali ambapo ilimpelekea kuachwa na mpenzi wake Charles. Katika Umarx tunaona historia ya jamii ipo katika utabaka, uongozi mbaya na rushwa. Mfano, katika tamthiliya ya Kivuli Kinaishi mwandishi Mohamed anasema;
                      Sote tunaishi, sote tuliangamia sura zetu zimo ndani ya viwliwili ndani ya
                     watoto wetu, mawazo yetu (uk. 118).
Hivyo, tunaoana mabadiliko huanzia na kuwepo kwa historia fulani katika jamii ambayo haikubaliki na wengi.

Pia nadharia ya Uchanganuzi nafsi na Umarx zinafanana kama ifuatavyo;
Zote zinazeleza matamanio ya binadamu, katika Uchanganuzi nafsi tunaona mtoto huzaliwa na matamanio ya kingono, na baadae kujidhihurisha anapokuwa mkubwa. Mfano katika riwaya ya Roza Mistika tunamuona Roza akiwa na matamanio pale aliopokuwa akitumiwa barua na pesa na mchumba wake Charles alikuwa akinunua nguo za nusu uchi na kuvaa, hivyo kupelekea ndugu zake kumgombeza. Katika nadharia ya Umarx kuwepo kwa matabaka, rushwa na uongozi mbaya hupelekea jamii kihitaji mabadiliko kutokana na mapenzi ya dhati kwa nchi yao. Mfano katika kitabu cha Usiku Utakapokwisha katika kuondokana na umaskini Gonza anasema
                 Panapo wezekana panawezeka panaposhindikana panashindikana na
                  sababu itafutwe na kutolewa hadharani ili kuondoa umaskini ni lazima
                   tutafute chanzo cha umaskini (uk. 8).
Hivyo, nadharia hizi zinafanana kwa kuonesha matamanio dhahiri na yale ya kisaikolojia yaani saikoanalisisi.

Zote zimeeleza utambuzi wa mwanadamu, katika nadharia ya Uchanganuzi nafsi tunaona binadamu hutambua kuwa jambo hili kulifanya kutokana na misingi ya jamii yake na katika Umarx jamii inautambuzi wa mambo mbalimbali ambayo yatawasaidia kuleta mabadiliko. Mamba hayo ni kama vile uongozi bora, jamii yenye haki na usawa. Kwa mfano katika kitabu cha Vuta N’ Vute tunamuona Yasmini ana utambuzi kuwa hawezi kuolewa na mtu aliyemzidi umri na asiyempenda kwa ajili ya mali, hivyo aliamua kutoroka (uk. 3).  Pia katika kitabu cha Kivuli Kinaishi.  Mwandishi anasema;
                    Sote tunaishi sote tuliangamia sura zetu zimo ndani ya viwiliwili
                     ndani ya watoto wetu mawazo yetu yamo ndani ya bongo zao.
                     Imani na itikadi imo ndani ya maisha yao (uk. 118).

Aidha, zote huwa katika uhakiki wa nadharia za kazi za fasihi, nadharia ya Uchanganuzi nafsi na nadharia ya Umarx zote huelezea mambo yanayosawidi jamii. Hivyo, mhakiki hutumia nadharia hizi mbili katika kubaini kazi ya kifasihi mfano, katika riwaya ya Roza Mistika mwandishi ameonesha masuala ya unyanyasaji kwa kumtumia Regina anavyonyanyaswa na mumewe. Mwandishi anasema; Lakini Regina tangu aolewe hakuwa na raha (uk. 3). Hivyo, huonesha unyanyasaji wa wanawake katika jamii. Mawazo haya hujadiliwa katika nadharia ya Uchanganuzi nafsi. Pia, katika riwaya ya Vuta N`kuvute tunamuona mhusika Denge kama mwanaharakati ambaye anapinga vikali rushwa, matabaka na ubaguzi wa rangi. Mawazo haya hujadiliwa katika nadharia ya Umarx ambapo uozo katika tabaka tawala huondolewa kutokana na msuguano wa kiyakinifu.
             

Kutokana na nadharia hizi mbili tunaweza kubaini tofauti zifuatazo;
Nadharia ya Uchanganuzi nafsi imejikita zaidi juu ya masuala ya kisaikolojia, tunaona kuwa binadamu hupenda vitu vingi lakini haonyeshi hisia zote kulingana na mila na desturi. Mfano, katika riwaya ya Roza Mistika mwandishi anasema;
                    Roza alihitaji kuwafahamu wanaume kwahiyo kutokana na malezi ya namna,
                    Roza alianza kuwatazama wanaume kama watu asiopaswa kundamana nao
                    na hata kuzungumza nao (uk. 9).
Hivyo, tunamuona Roza aliathirika kisaikolojia. Umarx unajikita zaidi juu ya uhalisia msuguano wa kiyakinifu si wa kimawazo mfano kuondoa matabaka, uongozi mbaya, rushwa katika jamii. Mfano katika riwaya ya Vuta N`kuvute mwandishi anasema;
                        Wakati tunapambana na adui lazima tutumie mbinu zote tunazoweza kutumia
                        mbinu za dhahiri basi tuzitumie kadri ya uwezo wetu……. Pale ambapo
                        hapana budi ila kutumia njia ya siri basi itumike (uk. 113)
                        
Tofauti nyingine inajitokeza katika waasisi, nadharia ya Uchanganuzi nafsi imeasisiwa na Sigmund Freud, (1859-1939), Carl Gustav John pamoja na Jacques Lacan. Huku nadharia ya Umarx imeasisiwa na Karl Marx, (1818-1863) na Fredrick Engels, (1820-1895) walifahamiana kupitia Makala.
Katika Umarx nadharia hii imejikita zaidi katika falsafa yakinifu na kuangalia mawazo ambayo sio dhahania bali katika uhalisia unaoonekana katika maendeleo ya jamii. Mfano, katika riwaya ya Usiku Utakapokwisha mwandishi amejadili matatizo yanayoikumba jamii na matokeo yake, mwandishi anasema;
                 Kifo kilichotokea kati ya mama na watoto wake wawili hiko Buguruni
          kinasikitisha. Ukweli ni kwamba haya ni madhara ya ufukara na umaskini watu
         hawakuwa na kazi kwa muda mrefu na maisha yao yamekuwa yakitegemea mno chakula
       kilichotokana na kuuzwa kwa vyombo vyao vya ndani………..(uk.7)
 Lakini nadharia ya Uchanganuzi nafsi imejikita katika dhana dhahania na ufahamu. Mfano, katika Vuta N` kuvute tunaona Yasmini anashindwa kukataa kuolewa na Bwana Raza kutokana na mapenzi ya wazazi wake. Hivyo, alikuwa na matamanio ya kutoroka (uk. 3).
Hitimisho; nadharia hizi mbili zimechangia vilivo kuhusisha fikra, mawazo, ndoto na matamanio ya banadamu. Utanzi Fulani wa jamii unazaliwa kutokana na mfumio wajamii kisiasa, kiuchumi, itikadi pamoja historia ya miundo ya jamii. Hivyo mabadiliko yanajitokeza katika jamii kutokana na ukinzani yakinifu na matamanio ya mwanajamii kuwepo kwa haki na usawa katika kuongoza jamii nzima.



                                           MAREJELEO
Kezilahabi, E (2011). Roza Mistika. Nairobi: Kenya Literature Bureau.
Mohamed, S (1990). Kivuli Kinaishi. Oxford University Press.
Msokile, M (1990). Usiku Utakapokwisha; popular publications Ltd: Maisha na Muungano wake.
Shafi, A. (1999). Vuta N` Kuvute; mkuki na nyota publishers.
Wagula, R., Njogu, K (2013). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi; Nairobi: Print point limited.
Wamitila, K. (2012). Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi; Nairobi English Press
Powered by Blogger.