Fasihi
Fasihi
Fasihi (kutoka neno la Kiarabu فصاحة fasAHa kwa maana ulumbi) ni utanzu (tawi) wa sanaa ambao hutumia lugha ya mazungumzo au maandishi ili kufikisha (kuwasilisha) ujumbe kwa hadhira husika.Vipengele vinavyounda fani ya fasihi ni kama ifuatavyo: fani ni umbo la nje la kazi ya fasihi; maudhui ni umbo lake la ndani
Fani
Katika kazi yoyote ya fasihi ni lazima pawepo na ustadi wenye kuleta mvuto fulani kwa hadhira (wasikilizaji au wasomaji) husika. Ustadi (ufundi) huo unaovutia hadhira huitwa fani, ambayo hujumuisha mambo kama vile:- Muundo - ni mtitiriko/msuko/mpangilio wa matukio / visa
- Mtindo - ni mbinu inayotumiwa na fanani ili atofautiane na fanani mwingine
- Wahusika - ni watu au vitu vyenye uhai au la ambavyo hutumiwa na fanani katika kazi yake
- Mandhari - ni eneo ambalo fanani hulitumia kujenga matukio na au mtiriko katika kuumba kazi yake
- Matumizi ya lugha - ni lugha anayotumia fanani katika kujenga wasifu wa wahusika kihaiba kazi yake
Maudhui
Pamoja na fani, kazi yoyote ya fasihi huwa na ujumbe na malengo mbalimbali ambayo hukusudiwa yaifikie jamii husika. Yale yote ambayo msanii wa kazi ya fasihi anakusudia yaifikie jamii husika huitwa maudhui. Maudhui ya kazi ya fasihi hujumuisha:- Dhamira
- Ujumbe/Mafunzo
- Mgogoro
- Falsafa/msimamo na
- Mtazamo
Sifa za fasihi
- Fasihi ni utanzu wa sanaa
- Kazi ya fasihi ni kujaribu kusawiri vipengele vya maisha, mahusiano, na hisia za watu katika jamii husika.
- Fasihi ni maelezo ya fani na maudhui.
- Fasihi ni ufundi unaotumia lugha ili kulete mguso au hisia fulani za watu katika muktadha fulani.
Aina za fasihi
Fasihi ndiyo aina pekee ya sanaa inayotumia lugha kujitambulisha au kujitofautisha na aina nyingine za sanaa. Kuna aina kuu mbili za fasihi nazo ni:- Fasihi simulizi - huwasilishwa kwa lugha ya mazungumzo/masumilizi
- Fasihi andishi - huwasilishwa kwa lugha ya maandishi
-
- Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia ya lugha ya mazungumzo au masimulizi ya mdomo
- Fasihi andishi huwasilishwa kwa njia ya lugha ya maandishi
Fasihi simulizi
Fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mazungumzo ya mdomo ili kufikisha ujumbe kwa hadhira. Aina hii ya fasihi ndiyo iliyokuwapo tangu zamani kabisa mwanadamu alipoanza kuishi yaani ilianza pale mwanadamu alipochangamana na wenzake katika kufanya mambo mbalimbali mfano,shughuli za biashara,kilimo,na nyinginezo.Utanzu huu wa fasihi simulizi una vipera au aina kuu nne, nazo ni:
- 1. Hadithi.
- 2. Ushairi.
- 3. Semi.
- 4. Maigizo.
Kufanana kwa fasihi simulizi na fasihi andishi
Kimsingi fasihi ni moja ingawa imegawanyika katika sehemu kuu mbili, yaani, fasihi simulizi na fasihi andishi. Mbali na mgawanyiko huo kuna mambo ambayo yanafanana katika fasihi zote mbili. Mambo hayo ni pamoja na:- Zote hutumia ufundi wa lugha ili kuwasilisha ujumbe kwa hadhira husika
- Zote zina dhima inayofanana katika jamii, yaani, kuelimisha na kuburudisha jamii
- Zote zina wahusika ambao ni Fanani na Hadhira
- Zote zina vipengele vya Fani na Maudhui
- zote zinaweza kukashifiwa na wasanii mbalimbali ikiwa hawajaridhishwa na mbinu za lugha zilizotumika
Tofauti kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi
Na. | Kipengele | Fasihi simulizi | Fasihi andishi |
---|---|---|---|
1 | Uwasilishwaji | Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo pamoja na vitendo | Fasihi andishi huwasilishwa kwa njia ya maandishi bila vitendo |
2 | Umri | Fasihi simulizi ni kongwe kuliko fasihi andishi | Fasihi andishi ni changa kuliko fasihi simulizi |
3 | Umilikaji | Fasihi simulizi humilikiwa na jamii nzima, ni mali ya jamii | Fasihi andishi humilikiwa na mwandishi, ni mali ya mwandishi |
4 | Tanzu | Fasihi simulizi ina tanzu nyingi kuliko fasihi andishi | Fasihi andishi ina tanzu chache kuliko fasihi simulizi |
5 | Hadhira | Hadhira ya fasihi simulizi ni watu wote katika jamii | Hadhira ya fasihi andishi ni wale tu wanaojua kusoma na kuandika |
6 | Mabadiliko | Fasihi simulizi hubadilika haraka kutegemeana na mahitaji ya hadhira na wakati | Fasihi andishi haibadiliki haraka kutegemeana na mahitaji ya hadhira na wakati |
7 | Utunzi | Fasihi simulizi hutungwa kwa muda mfupi | Fasihi andishi hutungwa kwa muda mrefu |
8 | Mazingira ya uwasilishaji wake (mandhari) | Huambatana na tukio maalumu la jamii | Kusoma au kusomewa ni ya kufikirika au mahali popote |
9 | Marekebisho | Mtunzi/msimulizi anaweza kurekebisha kazi yake wakati wa kuwasilisha au baadaye kidogo | Kitabu kikishaandikwa ni vigumu kukifanyia marekebisho mpaka toleo jipya litakapoandikwa |
10 | Uhifadhi | Huhidhiwa kwa njia ya kichwa (kichwani) kwa sehemu kubwa na sehemu ndogo sana huhifadhiwa kwenye maandishi, vinasa sauti au kanda mbalimbali za kurekodi | Huhifadhiwa kwa njia ya maandishi (vitabu) |
11 | Gharama | Fasihi andishi ina gharama ndogo ukilinganisha na fasihi andishi | Fasihi andishi ina gharama kubwa ukilinganisha na fasihi simulizi |
12 | Wahusika | Fasihi simulizi mara nyingi hutumia wahusika wa kubuni wasio binadamu | Fasihi andishi hutumia wahusika wa kubuni ambao mara nyingi ni binadamu |
13 | Uhai | Fasihi simulizi ni hai kuliko fasihi andishi | Fasihi andishi si hai kuliko fasihi simulizi |