uhakiki wa fasihi andishi
uhakiki wa fasihi andishi
|
DHANA YA UHAKIKI Uhakiki ni kitendo cha kutathmini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Kwa kiwango cha elimu ya sekondari mhakiki anafanya kazi ya uhakiki ili kuonesha mambo yanayojitokeza kama vile, dhamira, migogoro, ujumbe, falsafa, mtazamo, msimamo n.k DHIMA YA UHAKIKI NA NAFASI YA MHAKIKI Uhakiki ni kazi ambayo ina mchango mkubwa sana katika kazi za fasihi. Kwa msingi huo uhakiki una dhima zifuatazo: Husaidia wasomaji kuilewa kazi ya fasihi kwa urahisi Watunzi wa kazi za fasihi hutofautiana katika matumizi ya lugha na taswira, hivyo mhakiki anapofanya kazi ya uhakiki anamsaidia msomaji kuelewa vipengele hivi kwa kuvifafanua kwa lugha rahisi. Husaidia ukuaji wa kazi za fasihi Mhakiki anapoonesha ubora na udhaifu wa kazi ya mtunzi fulani, watunzi wengine pia watafunguka kifikra na kutunga kazi iliyobora zaidi. Uhakiki hukuza uelewa wa mhakiki Kwa kuhakiki kazi mbalimbali za fasihi, mhakiki hujiongezea maarifa ya lugha pamoja na mambo yanayotokea katika jamii. NAFASI YA MHAKIKI Mhahiki ana nafasi kubwa katika kazi za fasihi, Mhakaki ndiye anafafanua kazi ya fasihi ili hadhira iweze kumwelewa vizuri mtunzi wa kazi hiyo. Kwa hiyo hapa mhakiki anasaidia kurahisisha mawasiliano kati ya hadhira na mtunzi. Vilevile mtunzi huwaonyesha watunzi ubora na udhaifu wa kazi zao. Kwa kufanya hivyo huwawezesha watunzi kufanya kazi bora zaidi. HATUA ZA KUFUATA WAKATI WA KUFANYA UHAKIKI Hatua anazopitia mhakiki ni pamoja na hizi zifuatazo: Kwanza ni kuisoma kazi ya fasihi; hapa mhakiki anatakiwa kuisoma kazi husika ya fasihi kwa kina na kuielewa vizuri. Pili ni kuainisha na kuchambua mambo muhimu yanayojitokeza katika kazi hiyo katika vipengele vya fani na maudhui. Tatu ni kutoa tathimini au kuelezea ubora na udhaifu wa kazi inayohusika. MAMBO YANAYOCHUNGUZWA WAKATI WA KUFANYA UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI Maudhui Maudhui katika fasihi hujumuisha mawazo na pengine mafunzo mabalimbali yaliyomsukuma mtunzi ama msanii hadi akatunga kazi fulani ya sanaa. Huwa msanii huyo amakesudia hadhira yake ya wasomaji, wasikilizaji au watazamaji wayapate mawazo au mafunzo hayo; kwa hiyo haya twaweza kuyaita lengo la msanii kwa hadhira yake. Mawazo na mafunzo haya hayazuki hivihivi tu, kwa hiyo wakati wa kuyachambua na kuyajadili ni lazima yahusishwe na hali halisi ya kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi zilizopo katika jamii, hali hizi ndizo zilimzaa, zilimlea na kumkuza msanii. Wakati wa kuchambua kazi za kifasihi mhakiki ni lazima ajiulize amaswali yafuatayo:
Fani Fani katika fasihi ni ule ufundi wa kisanaa anaoutumia msanii katika kazi yake. Mambo mabalimbali yanaweza kuunda ama kubomoa kazi ya kutegemeana na vile msanii kayatumia. Mambo yanayochunguzwa katika fani wakati wa uhakiki wa kazi za fasihi ni pamoja na haya yafuatayo: Wahusika Wahusika ni watu au viumbe waliokusudiwa wawakilishe tabia za watu katika kazi za fasihi. Wahusika wa fasihi ni wa aina kuu tatu: Wahusika wakuu; hawa ni wale wanaojitokeza kila mara katika kazi za fasihi tangu mwanzo hadi mwisho. Maudui ya kazi ya fasihi huwa yanamzungukia na hata kutolewa na mhusika mkuu zaidi ya wahusika wengine. Mara nyingi jambo hili limewafanya wahusika wakuu wawe midomo ya wasanii. Wahusika wadogo; hawa hujitokeza hapa na pale katika kazi ya fasihi ili kuukamilisha ulimwengu wa kazi hiyo. Wakati mwingine wahusika wadogo huweza kusaidia kujenga dhamira fulani katika kazi ya fasihi na wakati mwingine wahusika hao huweza kusaidia kukuza dhamira kuu ya kazi ya fasihi. Wahusika bapa; ni wahusika ambao hawabadiliki, hatuwaoni wakipita hatua mbalimbali za mabadiliko katika maisha yao. Wanabaki kuwa walewale katika kazi yote ya fasihi. Wakati wa kuchambua kipengele cha wahusika, maswali yafutayo hayana budi kutafutiwa majibu yake:
Fasihi ni sanaa itoayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama kuandikwa. Kipengela cha lugha ni muhimu sana katika fasihi kwani ndicho hutenganisha fasihi na sanaa nyinginezo. Matumizi ya lugha katika fasihi yapo ya aina mbalimbali, kuna tamathaili za semi, misemo, nahau, methali, lahaja za wahusika, uchaguzi wa msamiati, miundo ya sentensi. Tamathali za semi Tamathali za semi ni maneno, nahau au sntensi ambazo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kutia nguvu katika maana, mtindo, na hata sauti katika maandishi ama kusema. Hizi wakati mwingine hutumiwa kwa njia ya kuipamba kazi ya fasihi na kuongeza utamu wa lugha. Baadhi ya tamathali za semi ni pamoja na hizi zifuatazo: Tanakali za Sauti Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani au namna kitendo kilivyofanyika. Tashbiha Hii ni mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha; ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’, ‘ja’. mfano, Mwembamba kama sindano; Chichi na Aisha wanao uzuri sawa na wa malaika. Hii ni mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai (sifa za kibinadamu). Mfano, "Sungura aliposhindwa, akasema sizitaki hizi mbichi". Takriri Ni mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano, alikimbia, alikimbia, alikimbia hadi akashika nafasi ya kwanza Ukinzani Ukinzani ni mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokinzana. Sitiari Ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo ‘ni’ ama ‘kuwa’. Mfano; Maisha ni mlima, juma ni mwamba. Taswira Ni matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji. Taashira Ni matumizi ya lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina au kitu fulani kinatumika kumaanisha kitu kingine chenye uhusiano na kile kilichotumiwa. Mfano; Jembe – mkulima, Mvi – mzee Majazi Hii ni aina ya sitiari ambayo itajapo sehemu tu ya kitu hapo hapo sehemu hiyo huashiria na kuwakilisha kitu hicho. Mfano; roho – mtu (Ajali ile imepoteza roho tano) Lakabu Ni mbinu ya mhusika kupewa/kubandikwa jina na wahusika wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia/sifa zake. Chuku Ni kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu, kutilia Chumvi. sisitizo bayana Tamathali hii husisitiza maana ya sentensi kwa kutumia kinyume. Kwa mfano; alikuwa ni msichana mzuri, ukimwona kwa mbali huwezi kujua kama anakuja au anakwenda. Tabaini Hii ni tamathali ya semi ambayo kwayo maneno au mawazo yanayokinzana hutumiwa katika sentensi ili kuleta msisitizo wa wazo ama mawazo yatolewayo. Mfano; Usimwamini mtu. Atakuchekea kwa meno meupe huku ndani anakuchukia kwa roho nyeusi. Punda afe, mzigo wa bwana ufike. Tashititi Hii ni tamathali ya semi ambayo kwayo swali linaulizwa huku jibu lake linafahamika waziwazi. Kwa mfano, ikiwa mtu kapoteana na rafiki yake kwa muda mrefu halafu ghafula wanakutana huweza kumuuliza, “Aisee, ni wewe?” ijapokuwa anajua kuwa ni yeye. Mjalizo Katika tamathali hii sentensi huwa ni mfuatano tu wa maneno yasiyo na viungo vyovyote. Mfano; - Nilikaa, nikasubiri nikachoka
Ni fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi:
Tamathali hii hutia chumvi kuhusu uwezo wa viumbe, na kuhusu tabia zao na kuhusu sifa zao kwa madhumu ni ya kuchekesha au kusisitiza. Mfano; Dah, cheki yule demu, ana mlima wa kiuno, Alipoachwa na mpenzi wake alilia hadi machozi ya damu. Uzungumzi Nafsiya Mhusika hujizungumzia, ama kwa kuongea au kuwaza, bila kukusudia kusikika na yeyote. Ritifaa Mbinu ya kuzungumza na mtu aliyekufa (au asiyekuwepo) kana kwamba yuko pamoja nawe. Kuchanganya Ndimi Kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili. Mfano, "alisimama kwanza kwa muda, before he went aliniambia nisimwambie mtu yeyote yule, you know!" Kuhamisha Ndimi Ni kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili. Kinyume na Kuchanganya ndimi (ambapo mwandishi huchanganya maneno katika sentensi moja, katika kuhamisha ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu. Mfano: Kazi hii ni ngumu sana, sitaweza kuifanya. People are trying to convince me to stay here but I think I can't, I must go! Methali Methali ni sehemu ya lugha ambayo inaweza kufananishwa na kiungo cha lugha na kitoweo cha lugha pia…hutumiwa kwa kuyatafakari na kuyapima maisha, kufunzia jumuiya na kututawalia jamii na mazingira ya binadamu. Methali hufunua falsafa ya jamii na hekima ya wale wanaoitumia katika mazungumzo yao. Pale ambapo methali zimetumika katika kazi mbalimbali za fasihi mara nyingi zimejenga fani na maudhui ya kazi hiyo. Misemo na Nahau Mara kwa mara matumizi ya misemo na nahau katika kazi za fasihi hushabihiana sana na yale ya methali. Misemo hutumika wakati mwingine kutambulisha mazingria maalum au kuijulisha hadhira wakati unaohusika katika kazi ya fasihi inayoshughulikiwa. Jambo hili linatokana na sababu kuwa misemo huzuka/huibuka na kutoweka kufuatana na hali mbalimbali za kimazingira. Nahau ni msemo uliojengwa kwa kutumia maneno ya kawaida lakini ambao huwa umesitiri maana tofauti na ile inayobebwa na maneno hayohayo katika matumizi ya kawaida. Mfano:
UHAKIKI WA MASHAIRI Maana: - Shairi ni utungo wa kisanaa wenye mpangilio maalum wa lugha ya mkato unaowasilisha mawazo au ujumbe kuhusu mwanadamu au mazingira yake na hufuata utaratibu fulani. Aina za mashairi Mashairi yapo ya aina mbili:
Mashairi ya arudhi Haya ni mashairi yanayofuata kanuni za kimapokeo au arudhi za utunzi wa mashairi. Arudhi/kanuni hizi ni pamoja na:
Mashairi huru Pia hujulikana kama mashairi ya kimapinduzi. Haya ni mashairi yasiozingatia lazima ya arudhi na hivyo huwa na muundo huru. Sifa zake kuu huweza kuwa:
SIFA ZA MASHAIRI Mashairi huwa na sifa maalum zinazoyatambulisha kama kazi ya kishairi, yawe ya kimapokeo au kimapinduzi. Sifa hizi ni kama vile:
Dhima ya mashairi
Uhakiki wa Mashairi Uhakiki wa shairi ni kuvunjavunja shairi katika sehemu zake na kuzichunguza kwa makini ili kueleza ujumbe, dhamira, maudhui na hali ya vipengee vya shairi. Uchambuzi wa mashairi huweza kufanywa kwa hatua. Hatua za uhakiki
Vipengee vya Uchambuzi Wa Mashairi
|