FONOLOJIA NA FONETIKI YA KISWAHILI FONOLOJIA YA KISWAHILI UTANGULIZI NA USULI WA TAALUMA YA FONOLOJIA
FONOLOJIA NA FONETIKI YA KISWAHILI
FONOLOJIA YA KISWAHILI UTANGULIZI NA USULI WA TAALUMA YA FONOLOJIA
MUHADHARA WA I: FONETIKI NA FONOLOJIA KWA UJUMLA:
Neno
fonolojia linatokana na maneno mawili ya Kigiriki phone-sauti za
kusemwa na logos- taaluma/mtalaa. Masimulizi yanadai kuwa taaluma hii
ilianza zamani sana kati ya mwaka 460 kabla ya Masia huko India ya kale,
ambapo mtu aliyeitwa Panini, na ambaye huaminika kuwa ni baba wa isimu aliandika kuhusu fonolojia ya Kisansikritikatika matini aliyoiita Shiva Sutras. Ni katika andiko hili ndipo alipobainisha kuwepo kwa dhanna ambazo leo hii hujulikana kama fonimu, mofimu na mzizi.
Baada ya andiko hilo, habari za taaluma ya fonolojia ni kama zilipotea
kabisa katika uwanja wa isimu hadi ilipofika karne ya 19 ambapo
wanaisimu wengine waliibuka na kuzungumzia upya masuala ya fonolojia.
Miongoni mwa wanaisimu wa mwanzo wanaotajwa kujihusisha na fonolojia ni
Mpolandi "Jan Baudouin de Courtenay",(pamoja na mwanafunzi wake wa zamani "Mikołaj Kruszewski" alipobuni neno fonimumnamo
mwaka 1876, na kazi yake, ijapokuwa hairejelewi sana, inachukuliwa kuwa
ni mwanzo wa fonolojia mamboleo. Mwanaisimu huyu si tu alishughulikia
nadharia ya fonimu, bali pia vighairi vya kifonetiki (ambavyo leo huitwa
alofoni na mofofonolojia). Maandishi ya Panini(Sarufi ya Kisanskriti) pamoja na Jan Baudouin de Courtenay yalikuja kuwa na athari kubwa kwa anayeaminika kuwa baba wa nadharia ya Umuundo Mamboleo, Ferdinand de Saussure, ambaye pia alikuwa ni profesa wa Sansikriti.
Wanaisimu wote hawa walikuwa wanajaribu kulinganisha sauti za lugha za
Asia Mashariki na za Ulaya, lengo lao likiwa ni kujua mizizi ya lugha
zilizoitwa India-Ulaya. Kutokana na mkabala huo, katika kipindi
hicho isimu ilikuwa Isimu-linganishi tu. Kutokana na tafiti zao hizo
waliweza kupata maneno yenye sauti na maana zilizolingana, kufanana au
kukaribiana. Utafiti huo uliweza kugundua jamii mbili za lugha ambazo ni
jamii ya lugha za Kirumi na jamii ya lugha za Kijerumani. Baadhi ya
wanaisimu mahususi kabisa wanaokumbukwa kuchangia katika maendeleo ya
fonolojia ni pamoja na:
(i) Jan
Baudouin de Courtenay (1845-1929) Kama ilivyoelezwa hapo awali, huyu ni
mwanaisimu aliyebuni dhanna za foni na fonimu. Katika nadharia yake,
alidai kuwa sauti za mwanadamu ni za aina mbili—foni na fonimu. Alisema
kuwa foni ni sauti za kutamkwa tu lakini fonimu ni sauti za lugha. Hata
hivyo, de Courtenay hakutumia istilahi za foni na fonimu (kama
zinavyotajwa sasa) bali alitumia istilahi za anthrophonics—foni na
psychophonics—fonimu. Yeye alidai kuwa foni zipo karibu sana na taaluma
ya kumuelewa binadamu pamoja na alasauti zake ambazo kwa hakika
hutofautiana sana na za wanyama wengine. Na kuhusu fonimu, alidai kuwa
zinahusu kumwelewa binadamu pamoja na akili zake na namna anavyofikiri
katika akili yake. Alidai kuwa, mara nyingi, binadamu hupokea
kinachotamkwa na kufasiliwa.
(ii) Ferdinand
de Saussure (1887-1913): Ni mwanaisimu wa Kiswisi anayejulikana kama
baba wa isimu kutokana na mchango wake alioutoa katika taaluma hii. Yeye
anakumbukwa zaidi kutokana na uwezo wake wa kutofautisha dhanna
alizoziita langue-mfumo wa lugha mahsusi, parole-matamshi ya mzungumzaji wa lugha husika na Langageambayo
hufafanuliwa kuwa ni uwezo alionao mzungumzaji wa lugha mahususi wa
kuzungumza na kuelewa matamshi ya mzungumzaji mwingine wa lugha
hiyohiyo. Ni sehemu ya lugha inayowakilisha maarifa kati ya sauti na
alama. Ni mfumo wa alama kwa maana ya kiufundi tu. Dai lake la msingi ni
kuwa alama inategemea vitu viwili-kitaja na kitajwa-hivyo ili
mawasiliano yafanyike, mfumo wa ishara lazima ufahamike na ukubaliwe na
wanajamii wote. Kwa upande wa parole, anadai kuwa ni matendo uneni.
Ni namna lugha inavyotamkwa katika hali halisi na mtu mmoja mmoja. Dhanna ya paroleinalingana na dhanna ya performance(utendi) ya Noam Chomsky. Katika lugha, parole ni matamshi tofauti ya sauti moja-alofoni. Wanaisimu wanaonekana kukubaliana na madai ya Saussure
kwa kuwa inaelekea kuthibitika kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja
kati ya kitaja na kitajwa [alama (lugha) na kinachowakilishwa
(masilugha)], bali makubaliano baina ya wazungumzaji wa lugha moja
husika ndiyo hutawala.
(iii) Nikolai Trubetzkoy (1890-1939) Ni miongoni mwa waanzilishi wa taaluma ya fonolojia akichota mizizi ya taaluma ya isimu kutoka katika Skuli ya Prague. Mwanaisimu huyu aliandika misingi ya fonolojia kwa kutumia maarifa yaliyoibuliwa na Ferdinand de Saussure.
Ni mtaalamu wa kwanza kufasili dhanna ya fonimu. Aliandika vitabu vingi
kwa lugha ya Kijerumani, miongoni mwake ni Grundzüge der Phonologie
(Principles of Phonology, 1939), ambapo ni katika kitabu hicho ndimo
alimotoa fasili ya fonimu pamoja na kubainisha tofauti baina ya fonetiki
na fonolojia.
(iv) Noam Chomsky (1928-) Huyu ni mwanaisimu wa Kimarekani anayevuma sana kwa mchango wake katika taaluma ya isimu kwa ujumla. Dhanna za competence (umilisi/umahiri) na perfomance(utendi)
zimemfanya awe maarufu ulimwenguni. Dhanna hizi zinaelezea tofauti
baina ya maarifa na udhihirishaji wa maarifa hayo ya mtumiaji wa lugha.
Katika fonolojia, Chomsky anakumbukwa kwa ufafanuzi wake wa dhana
ya fonimu kwa mtazamo wa kisaikolojia. Anapochunguza dhanna hii, hudai
kuwa fonimu ni tukio la kisaikolojia, hivyo fonimu zimo kichwani mwa
mzungumzaji wa lugha.
Daniel Jones
(1881-1967) Ni mwanafonetiki kinara na maarufu kabisa katika nusu ya
kwanza ya karne ya ishirini. Ni Mwingereza msomi ambaye alikuwa na
shahada ya kwanza ya hisabati na shahada ya umahiri wa sheria, shahada
ambazo hata hivyo, hakuwahi kuzitumia. Baadaye, alisomea lugha na
kuhitimu shahada ya uzamivu. Daniel Jones alifunzwa fonetiki na
maprofesa mbalimbali, japokuwa aliathiriwa zaidi na Paul Passyna Henry Sweet.
Hamu yake kuu ilikuwa kwenye nadharia ya fonetiki. Anafahamika zaidi
kwa ufafanuzi wa dhanna ya fonimu kwa mtazamo wa kifonetiki (ufafanuzi
wake tutauchunguza katika sehemu ya mitazamo ya dhana ya fonimu).
FONETIKI NA FONOLOJIA
Fasili
ya taaluma ya fonolojia haiwezi kukamilika, na pengine kueleweka, iwapo
hakuna linalosemwa kuhusiana na taaluma ya fonetiki. Hali hii inatokana
na ukweli kuwa kuna uhusiano wa kinasaba kati ya fonolojia na fonetiki.
Massamba na wenzake (2004:5) wanaeleza ukweli huu kwamba: .... fonetiki
na fonolojia ni matawi mawili tofauti ya isimu lakini yenye kuhusiana
sana. Uhusiano wa matawi haya unatokana na ukweli kwamba yote mawili
yanajihusisha na uchunguzi na uchambuzi unaohusu sauti za lugha za
binadamu. Kutokana na ukweli huu, jitihada za kufasili dhanna ya
fonolojia inaelekea kuwa nyepesi, dhanna hizi mbili zinapofasiliwa kwa
mlinganyo. Tuanze na fonetiki:
FONETIKI NI NINI?
Fonetiki
ni tawi la isimu linalochunguza sauti za kutamkwa na binadamu ambazo
huweza kutumika katika lugha asilia. Massamba na wenzake (kama hapo juu)
wanafasili fonetiki kuwa ni tawi la isimu linalohusika na uchunguzi na
uchambuzi wa taratibu za utoaji, utamkaji, usafirishaji, usikiaji, na
ufasili wa sauti za lugha za binadamu kwa ujumla. Wanasisitiza kwamba,
kinachochunguzwa katika fonetiki ni [maumbo] mbalimbali ya sauti
zinazoweza kutolewa na alasauti za binadamu (yaani sauti za binadamu
zinazotamkwa tu). Kipashio cha msingi cha uchambuzi wa kifonetiki ni
foni. Foni ni sauti yoyote inayotamkwa na binadamu na inayoweza
kutumika katika lugha fulani. Hivyo basi, foni ni nyingi sana na hazina
maana yoyote. Wanafonetiki hudai kuwa foni zimo katika bohari la sauti
(dhanna dhahania) ambalo kila lugha huchota sauti chache tu ambazo
hutumika katika lugha mahususi. Sauti chache zinazoteuliwa na lugha
mahususi kutoka katika bohari la sauti huitwa fonimu.
Matawi ya Fonetiki:
Kuna
mitazamo miwili tofauti kuhusiana na matawi ya fonetiki. Mtazamo wa
kwanza ni unaodai kuwepo matawi matatu; na mtazamo wa pili ni unaodai
kuwepo matawi manne. Mtazamo wa kuwepo matawi matatu unataja fonetiki matamshi, fonetiki akustika (safirishi), na fonetiki masikizi.
Mtazamo wa kuwepo matawi manne (kama Massamba na wenzake (kama hapo
juu), pamoja na matawi tuliyokwisha yataja, wanongezea tawi la fonetiki tibamatamshi.
(a) Fonetiki
matamshi huchunguza jinsi sauti za lugha zinavyotamkwa kwa kutumia
alasauti. Hususani, huchunguza namna na mahali pa kutamkia sauti husika mfano: [p] Ni kipasuo sighuna cha midomo.
(b) Fonetiki
akustika huchunguza jinsi mawimbi ya sauti yanavyosafiri kutoka katika
kinywa cha mtamkaji hadi kufika katika sikio la msikilizaji.
(c) Fonetiki
masikizi hujihusisha na mchakato wa ufasili wa sauti za lugha, hususani
uhusiano uliopo baina ya neva za sikio na za ubongo.
(d) Fonetiki
tibamatamshi ni tawi jipya lililozuka mwanzoni mwa karne hii, ambalo
huchunguza matatizo ya utamkaji ambayo binadamu huweza kuzaliwa nayo au
kuyapata baada ya kuzaliwa. Ni tawi linalojaribu kutumia mbinu za
kitabibu kuchunguza matatizo na kutafuta namna ya kuyatatua mfano: Kuna tatizo la mtu kuzaliwa na paa la kinywa au kaakaa lililogawanyika ambalo huathiri matamshi katika usemaji.
FONOLOJIA NI NINI?
Fonolojia
ni taaluma ya isimu inayochunguza mifumo ya sauti za kutamkwa
zinazotumika katika lugha asilia mahususi za binadamu. Inapolinganishwa
na fonetiki, inasisitizwa kuwa fonolojia ni tawi la isimu linalochunguza
mifumo ya sauti za lugha mahususi tu, kama vile sauti za Kiswahili,
Kiingereza, Kigogo, n.k. Hata hivyo, wapo wanaisimu wanaoelekea
kukubaliana kuwa kuna fonetiki ya lugha mahususi pia, na kuna fonolojia
ya jumla, na fonetiki ya lugha mahususi. Mathalani, Massamba (1996)
licha ya kufasili fonolojia kuwa ni taaluma ya isimu inayochunguza
mfumo wa sauti za lugha mahususi, anaenda mbele zaidi na kudai kuwa
fonolojia inaweza kuchunguza sauti kwa ujumla wake bila kuzihusisha na
lugha mahususi. Akmajian na wenzake (2001), nao wanadokeza
msimamo kama wa Massamba wanapodai kwamba fonolojia inaweza kuchunguzwa
kwa mitazamo miwili tofauti. Kwanza, fonolojia kama tawi dogo la isimu
linalochunguza mfumo na ruwaza za sauti za lugha mahususi ya binadamu;
na pili, fonolojia kama sehemu ya nadharia ya jumla ya lugha ya binadamu
inayohusika na tabia za jumla za mfumo wa sauti za lugha asilia za
binadamu. Katika mhadhara huu, hata hivyo, tutakuwa wafuasi wa mtazamo
unaoona kuwa fonolojia ni tawi la isimu linaloshughulikia mfumo wa sauti
za lugha mahususi tu, hivyo, tunapata fonolojia ya Kiswahili, fonolojia
ya Kiingereza, fonolojia ya Kiha, fonolojia ya Kihehe, na fonolojia ya
Kibena, n.k. Kipashio cha msingi cha fonolojia ni fonimu.
FONIMU:
Ni kipashio kidogo kabisa cha kifonolojia kinachoweza kubadili maana ya
neno. Hivyo basi, fonimu ina maana, kwa kuwa inaweza kubadili maana ya
neno inapobadilishwa nafasi katika neno husika. Foni chache
zilizoteuliwa kutoka katika bohari la sauti ili zitumike kwenye mfumo wa
sauti za lugha mahususi ndiyo fonimu. Hivyo, fonimu ni chache
ikilinganishwa na foni. Idadi ya fonimu za lugha hutofautiana kati ya
lugha moja na nyingine. Mathalani, Kiarabu kina fonimu ishirini na nane
(28), Kiswahili kina fonimu thelathini (30), Kifaransa kina fonimu
thelathini na tatu (33), na Kiingereza kina fonimu arobaini na nne (44).
Sauti ambayo huweza kubadilishwa nafasi yake katika neno lakini maana
ikabaki ileile huitwa alofoni.
Alofonini
kipashio cha kifonolojia kinachotaja hali ambapo fonimu moja hutamkwa
na kuandikwa tofautitofauti bila kubadili maana ya neno. Mfano: Fedha na
feza Sasa na thatha, Heri na kheri. Kwa kifupi, alofoni ni matamshi
tofautitofauti ya fonimu (sauti) moja.
MITAZAMO YA DHANNA YA FONIMU
Juhudi
za kufasili dhana ya fonimu zilizofanywa na wanaisimu mbalimbali
zimezua mitazamo mbalimbali ya namna ya kuchambua dhana hii. Hadi sasa,
mitazamo mitatu ifuatayo ndiyo hujulikana zaidi.
(i) Fonimu kama tukio la Kisaikolojia;
Huu ni mtazamo uliokuzwa na kutetewa na wanasarufi geuzi-zalishi,
mwanzilishi wake akiwa ni Noam Chomksy. Kwa mujibu wa mtazamo huu,
fonimu ni dhanna iliyo katika akili ya mzungumzaji wa lugha. Mtazamo huu
unadai kuwa kila mzungumzaji wa lugha ana maarifa bubu ya idadi na
jinsi ya kutamka fonimu za lugha yake. Chomsky anayaita maarifa haya
kuwa ni umilisi (competence). Anadai kuwa maarifa haya ya fonimu
hufanana kwa kiasi kikubwa miongoni mwa wazungumzaji wa lugha moja
husika. Kinachotofautiana ni jinsi ya kudhihirisha (kutamka) fonimu
hizo, yaani utendi(perfomance). Chomsky anabainisha kuwa kuna
uwezekano mkubwa wa kuhitilafiana baina ya umilisi na utendi kutokana na
matatizo mbalimbali ambayo mzungumzaji hukabiliana nayo. Matatizo hayo
ni kama vile uchovu, ulemavu wa viungo vya matamshi (alasauti za lugha),
athari za mazingira, ulevi, na maradhi. Hivyo, kutokana na hali hii,
fonimu hubaki kuwa tukio la kiakili, yaani kisaikolojia tu.
(ii) Fonimu kama tukio la Kifonetiki; Wafuasi wa mtazamo huu wanaongozwa na Daniel Jones. Daniel Jones anaiona fonimu kuwa ni [umbo] halisi.
(iii) Fonimu kama tukio la kifonolojia;
Huu ni mtazamo wa kidhanifu, ambapo huaminika kuwa fonimu ni kipashio
cha kimfumo, yaani fonimu huwa na maana pale tu inapokuwa katika mfumo
mahususi. Mwanzilishi wa mtazamo huu ni Nikolas Trubetzkoy. Yeye
huamini kuwa fonimu ni dhanna ya kiuamilifu na uamilifu huu hujitokeza
tu fonimu husika inapokuwa katika mfumo wa sauti wa lugha husika. Kwa
mujibu wa mtazamo huu, fonimu ni kipashio kinachobainisha maana ya neno.
Mtazamo huu hutumia jozi sahihi kudhihirisha dai lake. Mathalani,
maneno kama:
- babana bata
yana maana tofauti kwa sababu ya tofauti ya fonimu /b/ na /t/. Mtazamo
huu hujulikana kuwa ni wa kifonolojia. Na kwa hakika, mawazo haya ndiyo
yaliyoshika mzizi zaidi katika taaluma ya fonolojia na ndiyo inayofunzwa
hivi sasa katika sehemu nyingi ulimwenguni.
Tofauti kati ya Fonetiki na Fonolojia
FONETIKI
|
FONOLOJIA
|
Huchunguza sauti za lugha ya mwanadamu kwa ujumla.
|
Huchunguza sauti za lugha mahususi.
|
Ni pana{huchunguza sauti nyingi}
|
Ni finyu {huchunguza sauti chache}
|
Huchunguza sauti zinavyozalishwa
|
Hushughulika na sauti zinavyotumika
|
Ni moja tu duniani kote
|
Ni nyingi kwani kila lugha ina fonolojia yake duniani.
|
Uwasilisho wa suti hutumia mabano mraba mf. []
|
Sauti huwasilishwa na mabano mshazari. mfano //
|
Inahusisha sayansi huru katika uchunguzi wake
|
Haitumii sayansi huru katika uchunguzi wake
|
DHANNA YA FONOLOJIA VIPANDE NA FONOLOJIA ARUDHI
Fonolojia imegawanywa katika aina kuu mbili ambazo ni Fonolojia arudhi na Fonolojia vipande sauti.
(a) Fonolojia vipande sauti;
ni aina ya Fonolojia ambayo hushughulikia uchunguzi wa vipande sauti
vyenyewe. Wanaisimu katika aina hii hubainisha vipande sauti bainifu
katika lugha kama vile alofoni na fonimu pia hueleza fonimu hizo jinsi
zinavyoweza kuathiriana katika maeneo mbalimbali. (Mgullu, 2010).
(b) Fonolojia arudhi;
tawi hili hushughulikia masuala mengine ya sauti ambayo hayaathiri
vipashio vikubwa zaidi kuliko fonimu moja. Pia aina hii huchunguza mfumo
wa kuweka mkazo katika maneno na tungo katika lugha fulani kama vile
kiimbo na muundo wa silabi. (Mgullu, 2010). Fonolojia ya Kiswahili
hujishughulisha na vipengele mbalimbali ambavyo vinahusiana na sauti
pamoja na mpangilio wake wa uundaji maneno katika lugha mbalimbali.
Vipengele hivi ni kama vile; matamshi, kiimbo, mkazo, na mfuatano wa
sauti katika kuunda mofimu na maneno.
(i) Matamshi;
ni utaratibu utumikao katika utoaji wa sauti za maneno ya lugha ya
binadamu. Utaratibu wa matamshi ya sauti za lugha huzingatia mahali pa
matamshi na jinsi ya utamkaji. Mfumo huu ni maalumu kwa sababu binadamu
hutumia ala za sauti na upumuaji katika utamkaji.
(ii) Lafudhi;
ni sifa ya kimasikizi inayomtambulisha msemaji anatoka eneo gani
kijiografia. Lafudhi hutokana na athari ya lugha ya kwanza au mazingira.
Mfano:
· Usiniretee maswara ya ubaguzi wa kikabira hapa (Wakuriya)
· Amemupiga mutoto ya watu juu amemuibia mafaranga makumi mawili (Wakongo)
· Ukikaa nchale, ukichimama nchale (Wamakonde)
· Wewe unakamuaga mang’ombe tu moja
kwa moja (Wasukuma)
· Mbona unakuwa kinganganizi,
nilishakwambia sikupendi rakini
wewe bado unaningangania tu!
(Wahaya)
(iii) Silabi;
ni kipashio cha utamkaji ambacho kwa kawaida ni kikubwa kuliko fonimu
na kidogo kuliko neno. Silabi ni kipashio cha kifonolojia kinachohusu
matamshi ya sauti za lugha zinapotamkwa kwa pamoja kama fungu moja
linalojitegemea kimatamshi. Fungu hilo laweza kujumuisha sauti moja
pekee au sauti mbili kutegemea muundo wa lugha husika. (Massamba na
wenzake, 2004). Mpaka wa silabi hutenganishwa na alama ifuatayo; $
mfano: $ma$,$ma$, $a$,$na$,$ku$,$la$.
(iv) Kiimbo;
ni utaratibu maalumu wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti katika
usemaji wa lugha au kiimbo ni kipengele cha kifonolojia chenye maana ya
kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti za lugha. Vilvile kiimbo ndicho
kinafanya sentensi iwe ya swali, mshangao au maelezo. Mfano.
o John ameondoka?
o John ameondoka!
o John ameondoka.
(v) Mkazo/shadda;
Katika lugha ya Kiswahili kuna namna ya kutamka maneno ili kuleta maana
mbali mbali, kwa mfano neno “barabara” litaleta maana husika kulingana
na jinsi lilivyotamkwa. Hivyo, mkazo ni pale silabi inapotamkwa kwa
kukazwa. Maneno ya Kiswahili huwa na silabi moja ambayo hutamkwa kwa
nguvu zaidi kuliko silabi nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa mkazo,
sauti hupandishwa juu kiasi.
Maneno mengi ya Kiswahili, hasa yale yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho.
Kwa mfano: ba’bu, maya’i, rama’ni (mimi nilikuwa nikitamka ra’mani), baraba'ra (njia).
Baadhi
ya maneno yenye asili ya kigeni, huwa na mkazo katika silabi nyingine.
Kwa mfano: bara'bara (sawa sawa), Alha’misi. Zipo baadhi ya lugha zenye
uwezo wa kuhamisha mkazo na maana ya neno ikabadilika.
Mfano: Kiingereza
A B
· Produ’ce Pro’duce
(zalisha) (mazao)
· Pro’ject Proje’ct
(mradi) (panga mradi)
· Per’mit Permi’t
(ruhusu) (ruhusa)
Katika lugha kama kiingereza mkazo unaweza kuhama na kubadili maana lakini katika Kiswahili mkazo huwa hauwezi kuhama.
(vi) Kidatu, Massamba,
Kihore, na Msajila (2004), wanakitazama kidatu kwa maana ya sauti
isikikayo wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati, au kuwa chini.
Hii humaanisha kwamba katika usemaji, mtu anaweza kupandisha kiwango
cha sauti (yaani akaiweka katika kidatu cha juu), kukishusha kidogo
kiwango hicho na kuiweka sauti katika kidatu cha kati, au kukishusha
zaidi na kuiweka sauti katika kidatu cha chini. Ni muhimu kuelewa kwamba
kupanda au kushuka kwa mawimbisauti na kupanda au kushuka kwa kiwango
cha kidatu ni vitu viwili tofauti. Kupanda au kushuka kwa mawimbisauti
si lazima kuathiri kidatu; wala kidatu si lazima kuathiri kupanda au
kushuka kwa mawimbisauti. Hii ni kwa sababu mzungumzaji anaweza kusema
kwa kidatu cha juu (sauti ya juu), kidatu cha kati (sauti ya kati) au
kidatu cha chini (sauti ya chini) na bado akaweza kubadilisha
mawimbisauti akiwa katika kidatu hicho hicho kimoja. Lakini pia
mzungumzaji anaweza kubadili kidatu. Kwa mfano, anaweza kuanza
kuzungumza kwa sauti ya juu (kidatu cha juu) akamalizia kwa sauti ya
kati (kidatu cha kati) au sauti ya chini (kidatu cha chini).
Othografia;
Kila lugha ina mfumo tofauti wa usemaji na hutumia mfumo tofauti wa
sauti. Kila lugha inakuwa haina budi kubuni mfumo wake wa kuziwakilisha
sauti zake katika maandishi. Mfumo huo wa maandishi ndio ujulikanao kama
othografia. Mfumo huu huwa unawasilisha herufi maalumu zinazobuniwa ili
kuwakilisha sauti za lugha inayohusika kimaandishi. Neno uthografia
lina asili ya kigiriki na maana yake ni utaratibu wa kutumia alama au
michoro ya maandishi kuwakilisha sauti zisikikazo katika lugha.
(vii) Toni; Kwa
mujibu wa Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha (2009:87). Toni ni sifa
inayowakilisha kiwango pambanuzi cha kidatu cha silabi katika neno au
sentensi na ambayo huweza kubadilisha maana ya neno katika sentensi
kisemantiki au kisarufi. Hivyo basi, Toni ni sifa katika lugha ambapo
maana ya neno huathiriwa na jinsi linavyotamkwa. Au. Toni ni kiwango cha
kidatu pamoja na mabadiliko yake ambayo hutokea wakati mtu anapotamka
silabi au neno. Katika lugha mabadiliko ya toni hubadili maana za yale
yanayosemwa na sifa za toni hubainika katika kiwango cha neno na silabi
zake mbalimbali. Lugha nyingi za kibantu kama vile kikuyu na kikamba
zina sifa ya toni lakini lugha ya Kiswahili haina sifa hii. Kuna aina
tatu za toni ambazo ni, Kwanza, toni juu ni toni ambayo hudhihirishwa na
kidatu cha juu. Pili, toni kati ni toni ambayo hudhihirishwa na kidatu
cha kati. Tatu, toni chini ni toni ambayo hudhihirishwa na kidatu cha
chini.
MUHADHARA WA II:
VITAMKWA VYA LUGHA KWA UJUMLA:
SAUTI ZA LUGHA ASILIA
Wanaisimu
wengi wanakubaliana kwamba lugha ya binadamu ni mfumo wa sauti nasibu
zenye kubeba maana na ambazo hutumiwa na jamii fulani ya watu kwa
madhumuni ya mawasiliano ya kimazoea tu ya watumiaji wa lugha
inayosikika kati yao. Sauti nasibu ni sauti ambazo uteuzi wake
haukufanywa kwa kufuata mantiki au vigezo fulani maalumu bali umetokana
na makubaliano ya kimazoea tu ya watumiaji wa lugha husika. Hii ndiyo
maana sauti za lugha mbalimbali zinaweza kufanana sana au kwa kiasi
fulani tu. Na pia zinaweza kusigana sana au kiasi fulani tu.
Mhimili
muhimu wa lugha asilia ni sauti zitumikazo kuunda silabi au mofimu.
Uunganishaji wa mofimu huunda maneno, maneno huunda virai, virai huunda
vishazi na vishazi huunda sentensi. Utaratibu wa kuunganisha sauti
kuunda maneno ni wa nasibu kama ambavyo sauti zenyewe ni za nasibu.
ALASAUTI ZA LUGHA ASILIA
Alasauti
ni viungo vya mwili vinavyotumika katika utamkaji wa sauti mbalimbali
za lugha. Utamkaji wa sauti zitumiwazo katika lugha ya mwanadamu
hufanyika kwa kutumia sehemu au viungo mbalimbali maalumu vya mwili wa
mwanadamu. Katika taaluma ya Isimu sehemu ya maneno yatumikayo katika
utamkaji wa sauti za lugha hujulikana kama ala za sauti.
Ala hizo za sauti za lugha ni:
- Mapafu
- Umio
- Kaakaa gumu na laini
- Ulimi
- Ufizi
- Meno
- Midomo
- Pua, n.k
Kwa kutumia ala hizo mwanadamu anaweza kuzalisha sauti mbalimbali.
FONOLOJIA NA MOFOLOJIA
Fonolojia ni tawi la isimu linalojishughulisha na sauti za lugha mahususi jinsi zinavyotamkwa na mahali zinapotamkiwa.
Mofolojia ni taaluma ya kiisimu inayojishughulisha na maumbo ya lugha jinsi yanavyoundwa na kazi za maumbo hayo katika lugha.
Fonolojia
na mofolojia hutegemeana kwa misingi kwamba mofolojia hutegemea sauti
za fonolojia katika kuunda maumbo mbalimbali. Sauti hizo huunda
silabi,mofimu na maneno. Bila fonolojia mofolojia haiwezi kufanya kazi
wala uchambuzi wa haukamiliki.
Mfano: “baba” umbo hilo limeundwa na :
Fonimu -------4: b+a+b+a
Silabi------- 2: ba + ba
Katika mfano huo utabaini kuwa umbo “baba” ni umbo tu la kimofolojia lakini uchanganuzi wake hutegemea fonolojia.
MUHADHARA WA III:
VITAMKWA VYA MSINGI VYA KISWAHILI SANIFU
Kitamkwa
ni sauti dhahiri inayosikika wakati wa utamkaji wa maneno. Vitamkwa
huwakilishwa kimaandhishi kwa kutumia alama zijulikanazo kama herufi za
alfabeti. Mfano: p,the,dh, n.k
Kitamkwa hujitokeza kama kipande sautikinachojibainisha
kwa dhati yake kwa mfano: p,b, kila kimoja kina ubainifu uliowazi kwa
kuzingatia vitamkwa hivyo vinavyosikika masikioni, ni dhahiri kwamba /p/
hutamkwa tofauti na /b/.
Vitamkwa vya kifonetiki
Tunapochunguza
vitamkwa vya kifonetiki tunazingatia sauti za lugha jumla. Kifonetiki
kitamkwa huzingatiwa jinsi kinavyotamkwa, kusafirishwa, usikikaji wake
na ufasili wa vitamkwa hivyo bila kuvihusisha na lugha fulani maalumu.
Uchambuzi
wa vitamkwa vya kifonetiki huzingatia sifa za jumla za vitamkwa kama
vile kipasuo kutamkiwa kwenye midomo, kuviringa midomo, n.k
Hizo
ni sifa za kitamkwa [p], sifa hizo huweza kujitokeza pia kwenye umbo
[b]. katika kiwango hiki huwa haijalishi kama sauti zinazochunguzwa
zinatumika kuundaa maneno tofauti katika lugha au la.
Vitamkwa vya kifonolojia
Hapa
vitamkwa huchunguzwa katika lugha maalumu jinsi vinavyotamkwa,
vinapotamkiwa na jinsi vinavyohusiana na kuathiriana kimatumizi katika
kuunda maneno. Mfano: pumba,bumba,taka,daka
Katika mifano hiyo vitamkwa [p,b,t,d] vinaleta utofauti wa kimaana vinapotumika katika maneno.
Fonimu kwa ujumla
Fonimu
– ni kitamkwa cha msingi katika lugha kituwacho kuunda maneno ya lugha
fulani maalumu mfano: /p/,/b/,/u/,/m/,/t/,/d/,/a/,/k/,/n/ huweza kuunda
maneno kama[ pumba,tunda,bumba,daka,] n.k. vilevile fonimu huweza
kubadili maana ya neno.
Mfano:
- Pumba – bumba
- Funda – dunda
- Damu – daku
- Taka – daka
Fonimu huweza kubatilisha maneno yaani kuyafanya maneno yawe batili kwa jinsi yalivyoundwa.
Mfano:
- Kaka – gaka
- Sasa – thasa
- Shoga – shosha
Dhanna ya alofoni
Alofoni ni nini?
Mgullu
(1999) akimnukuu Hartman (1972) anasema kuwa alofoni ni sauti mojawapo
miongoni mwa sauti kadhaa zinazowakilisha fonimu moja. Alofoni hutokea
katika mazingira mahsusi (mazingira ya kiutoano).
Aidha,
Mgullu (1999) akimnukuu Ladefoged (1962) anasema kuwa alofoni ni
matamshi tofauti tofauti ya fonimu moja. Pia anasema alofoni za fonimu
moja huunda kundi moja la sauti ambazo;
1. Hazibadili maana ya neno,
2. Hutokea katika mazingira tofauti ya kifonetiki, na
3. Alofoni zote hufanana sana kifonetiki.
Kutokana
na fasili hizo, tunaweza kusema alofoni ni maumbo tofauti tofauti ya
fonimu moja, ingawa maumbo hayo huwa na tofauti ndogo ndogo za
kifonetiki lakini hayaleti tofauti yoyote katika maana za maneno.
Tuchukue mifano ya maneno kutoka katika lugha ya Kiingereza;
tea; eat; writer;
/thi:/ /i:t/ /raita/
Katika maneno yetu hapo juu sauti [th]
inayotokea mwanzoni mwa neno, na sauti [t] inayotokea popote ni alofoni
za fonimu /t/. Sauti hizi hazibadili maana ya maneno, zinatokea katika
mazingira tofauti na zinafanana sana kifonetiki.
Katamba (1996) anasema alofoni zinaweza kujitokeza pia katika maneno:
tea; two; eighth;
/ti:/ /twu/ /eitɵ/
[t] katika /ti:/ hutamkwa wakati midomo ikiwa imesambaa, [tw] katika /twu/ hutamkwa wakati midomo ikiwa mviringo na [t] katika /eitɵ/ ni sauti ya meno. Hivyo [t], [tw] na [t] ni alofoni za fonimu /t/
Katamba,
anasema si kila sauti zenye kubadilishana mazingira basi zaweza kuwa
alofoni katika lugha ya Kiingereza. Kwa mfano sauti /h/ na /ŋ/
hubadilishana mazingira ya utokeaji (sauti /h/ hutokea mwanzoni mwa
silabi ikifuatiwa na irabu mfano; hat, head, n.k wakati sauti /ŋ/
hutokea mwishoni mwa silabi katika konsonanti zilizoungana, mfano;
longer, long, bung n.k), lakini hazifanani kifonetiki hivyo haziwezi
kuwa alofoni za sauti moja.
Aghalabu
alofoni hutumiwa katika muktadha au mazingira ya kifonetiki yaliyo
tofauti, ambapo alofoni moja ikitumika katika mazingira fulani basi
nyingine haiwezi kutumika katika mazingira hayo hayo.
Mbinu za kuzitambua fonimu na alofoni.
Kuna
mbinu mbalimbali za kuzibainisha fonimu na alofoni za lugha fulani.
Mbinu au njia hizo ni kama; kufanana kifonetiki, jozi za mlinganuo
finyu, mgawanyo wa kiutoano na mpishano huru.
(i) Mbinu ya kufanana kifonetiki.
Mbinu
hii huelezea kwamba sauti ambazo huwa na sifa za kifonetiki
zinazofanana basi huchukuliwa kuwa ni sauti za fonimu moja (alofoni).
Kama sauti hazina sifa za kifonetiki zinazofanana basi huchukuliwa kama
ni fonimu mbili tofauti. Kwa mfano tuchunguze sifa za kifonetiki za
sauti /i/ na /u/ katika lugha ya Kiswahili;
/i/ /u/
+irabu +irabu
+mbele +nyuma
+juu +juu
-mviringo +mviringo
Kwa
mujibu wa kigezo hiki, sauti /i/ na /u/ ni fonimu mbili tofauti katika
lugha ya Kiswahili kwa sababu zina sifa tofauti za kifonetiki.
(ii) Mbinu ya Jozi za Mlinganuo finyu.
Kama
anavyoeleza Fischer (1975), mlinganuo finyu ni tofauti ndogo kabisa ya
kifonolojia iliyopo baina ya maneno fulani: aghalabu maneno hayo huwa
na;
· Idadi sawa ya fonimu
· Fonimu zinazofanana isipokuwa moja katika mazingira sawa ya kifonetiki
· Mpangilio wa fonimu uliosawa
· Maana tofauti
Tuchunguze seti ya maneno yafuatayo;
Pia - lia
Paka - taka
Wali - hali
Katika
seti ya maneno hapo juu tunaona kwamba maneno /pia/ na /lia/ yapo
katika jozi mlinganuo finyu kwa sababu yana idadi sawa ya fonimu, yaani
fonimu tatu kila neno, fonimu zinazofanana isipokuwa moja, na mpangilio
wa fonimu ulio sawa na maana zikiwa tofauti. Halikadhalika katika seti
ya maneno /paka/ na /taka/ kwa sababu nayo yana idadi sawa ya fonimu
yaani, fonimu nne zinazofanana isipokuwa moja na mpangilio wa fonimu
ulio sawa. Pia katika seti ya maneno /wali/ na /hali/ tunaona kuwa yapo
katika jozi mlinganuo finyu kwa sababu yana idadi sawa ya fonimu yaani
fonimu nne zinazofanana isipokuwa moja na mpangilio wa fonimu ulio sawa.
Njia hii hutusaidia kuzitambua fonimu za lugha kwa sababu tofauti ya
fonimu moja yatosha kubadili maana za maneno hayo.
(iii) Mbinu ya mgawanyo wa kiutoano.
Hyman
(1975) anasema katika fonolojia, utoano ni dhanna ambayo hutumika
kuelezea uhusiano uliopo baina ya sauti mbili (au zaidi) za fonimu moja
ambazo haziwezi kutokea katika mazingira sawa katika neno. Hii ina maana
kwamba sauti huwa ina mahali/mazingira yake maalum ambayo hayawezi
kukaliwa na sauti nyingine ya kundi moja.
Tuchunguze mifano kutoka katika lugha ya Kiingereza; kuhusu sauti /ph/ yenye mpumuo na sauti /p/ isiyo na mpumuo. Sauti /ph/ yenye mpumuo hutokea mwanzoni mwa maneno tu, kwa mfano katika maneno /phin/, /phen/, /phut/
n.k . Kwa upande mwingine /p/ isiyo na mpumuo hutokea sehemu yoyote ya
neno isipokuwa mwanzoni; mfano katika maneno kama /top/, /cup/, /span/,
/spare/ n.k
Sauti
ambazo ziko katika mgawanyo wa kiutoano huwa hazitofautishi maana za
maneno, isipokuwa sauti hizo hugawana tu mahala pa kutokea au kutumika.
Hivyo sauti hizo huwa ni alofoni za fonimu moja.
Tuchunguze sifa bainifu za sauti /ph/ yenye mpumuo na sauti /p/ isiyo na mpumuo;
/ph/ /p/
+kons +kons
+mpumuo -mpumuo
-ghuna -ghuna
+midomo +midomo
+kipasuo +kipasuo
[ph]
yenye mpumuo na sauti [p] isiyo na mpumuo ni alofoni za fonimu /p/.
Sifa zote za sauti hizi zinafanana isipokuwa moja tu (sifa ya mpumuo).
(iv) Mbinu ya Mpishano Huru.
Huu
ni uhusiano wa fonimu mbili tofauti kubadilishana nafasi moja katika
maneno maalum bila kubadili maana za maneno hayo. Hapa mpishano
unatumika kwa ile maana ya “wewe ondoka, mimi niingie.” Kwa kuwa fonimu
moja inatolewa katika neno fulani na fonimu nyingine inakaa mahali pake
bila kubadili maana ya neno hilo. Mpishano huru unahusisha fonimu mbili
kubadilishana nafasi moja katika neno moja. Fonimu hizo huwa ni tofauti
kabisa kifonetiki hivyo hatuwezi kuziita alofoni.
Tuchunguze mifano ifuatayo;
· /buibui/ na /baibui/ sauti /u/ na /a/ zimepishana nafasi bila kubadili maana ya neno.
· /Wasia/ na /wosia/ sauti /a/ na /o/ zimepishana bila kubadili maana ya maneno.
· /kheri/ na /heri/ sauti /kh/ na /h/ zimepishana bila kubadili maana ya maneno.
Tuchunguze sifa bainifu za kifonetiki za sauti /a/ na /u/ katika maneno /baibui/ na /buibui
/a/ /u/
+irabu +irabu
+mbele +nyuma
+chini +juu
-mviringo +mviringo
Tuchunguze pia sifa bainifu za kifonetiki za sauti /a/ na /o/ katika maneno /wasia/ na /wosia/
/a/ /o/
+irabu +irabu
+mbele +nyuma
+chini +nusujuu
-mviringo +mviringo
Sauti
hizi haziwezi kuwa alofoni kwa sababu zinatofautiana sana kifonetiki.
Pia sauti hizi haziachiani mazingira ya utokeaji wake hivyo ni ngumu
sana kuyaelezea mazingira ya utokeaji wake.
Njia
hizi zitumikapo, aghalabu kwa pamoja, kwa kusaidiana huweza kutusaidia
kutambua fonimu na alofoni za lugha inayofanyiwa uchunguzi.
Alofoni katika lugha ya Kiswahili.
Sasa
tuchunguze dhana ya alofoni kama inavyojadiliwa na wataalamu mbalimbali
wa Isimu ya Kiswahili. Hapa tutaonesha fasili pamoja na mifano ya
alofoni katika lugha ya Kiswahili kwa mujibu wa wataalamu hao.
Massamba
na wenzake (2013) wanasema alofoni ni sura au maumbo mbalimbali ya
fonimu moja. Fonimu za lugha huweza kupata sura tofauti tofauti
kulingana na mazingira katika neno ambamo hutokea. Hii ina maana kwamba
fonimu inaweza kubadilika ikachukua umbo moja kutokana na kutokea kwake
katika mazingira fulani na inaweza pia kubadilika ikachukua umbo jingine
kutokana na kutokea kwake katika mazingira mengine tofauti katika neno.
Wanatoa mifano ya alofoni kutoka katika lugha ya Kiswahili kama
ifuatavyo:
Mofimu za neno Matamshi yake
(a) ki+ti ki+refu [kiti kirɛfu]
(b) ki+ti ki+eusi [kiti ʧeusi]
(c) u+limi m+refu [ulimi mrɛfu]
(d) n+limi n+refu [ndimi ndɛfu]
(e) n+buzi [mbuzi]
(f) n+dama [ndama]
(g) n+gombe [ŋɔmbɛ]
Katika
mifano ya Kiswahili hapo juu, tunaona mabadiliko ya kifonimu
yakijitokeza. Katika mfano wa (b) fonimu /k/ inapofuatiwa na
irabu /i/ halafu kukawa na mpaka wa mofimu, kisha ikafuatiwa na irabu
/e/ hubadilika na kuwa /ch/ ki+eusi = [ʧeusi] na
katika (d) tunaona wazi kuwa fonimu /l/ inapotanguliwa na nazali
/n/ hubadilika na kuwa /d/ [n+limi = ndimi]. Halikadhalika katika
mifano ya (e) na (g) tunaona kwamba nazali /n/ inapofuatiwa na
kitamkwa /b/ hubadilika na kuwa /m/, inapofuatiwa na kitamkwa /d/
hubakia /n/, na inapoafuatiwa na kitamkwa /g/ hubadilika na kuwa /ŋ/.
Hii ina maana kwamba katika mazingira haya sauti [ʧ] ni alofoni yafonimu /k/, [d] ni alofoni ya fonimu /l/ na [m], [n] na [ŋ] ni alofani za fonimu /n/(katika fonolijia herufi hii kubwa hutumika kuwakilisha
dhanna ya nazali) na alama /N/ ikiwa kama kiwakilishi cha fonimu kuu.
Alofoni
hizo hapo juu zimetokana na michakato ya kimofofonolojia (taaluma ya
isimu inayoshughulikia uchunguzi na uainishaji wa vipengele vya
kifonolojia vinavyoathiri maumbo ya mofimu au vipegele vya kisarufi
vinavyoathiri maumbo ya fonimu). Pamoja na kwamba mabadiliko haya
yameitwa mabadiliko ya kifonimu lakini tukichunguza vizuri tutaona
kwamba kwa kiasi kikubwa ni maumbo yaliyobadilika na kwa kiasi fulani ni
fonimu.
Kwa
mfano, mofimu ya ngeli ya tisa {-n-} katika majina kama vile nyumba,
mbuzi, ng’ombe, n.k (inabadilika katika mazingira tabirifu) kuwa mofimu
{m}, {ŋ} na wakati mwingine hubaki vilevile {n}. Mchakato huu huitwa
mchakato wa au kanuni ya konsonanti kuathiri nazali. Hivi kwamba mofimu
{n} hubadilika na kuwa mofimu {m} pale inapokuwa imeitangulia sauti ya
midomo. Halikadhalika fonimu {n} hubadilika na kuwa mofimu {ŋ} pale
inapokuwa imeitangulia sauti ya kaakaa laini.
Kwa
mantiki hii basi maumbo haya yote yatakuwa yanaiwakilisha mofimu moja
yaani ngeli ya tisa {-n-}. Kama hivi ndivyo basi maumbo hayo yatakuwa ni
alomofu na si alofoni.
Alomofu
ni mojawapo ya viwakilishi viwili au zaidi vya mofimu moja ambavyo
hujitokeza katika mazingira tofauti ya mtoano. Massamba na wenzake
(2012)
Katika
data ambayo imetolewa na Massamba na wenzake kuna baadhi ya sauti
ambazo zinatokana na michakato ya kifonolojia au badiliko la kifonolojia
ambapo nazali huiathiri konsonanti inayoambatana nayo ili kurahisisha
matamshi. Sauti zinazoathirika hapa ni sauti za likwidi (kimadende /r/
na kitambaza /l/).
(a) u+limi m+refu [ulimi mrɛfu]
(b) n+limi n+refu [ndimi ndɛfu]
Sauti
/l/ hubadilika na kuwa kipasuo /d/ katika mazingira ya kutanguliwa na
nazali /n/, vilevile sauti /r/ hubadilika na kuwa kipasuo /d/ katika
mazingira ya kutanguliwa na nazali /n/.
Sauti hizi zinatokea katika mazingira ya kiutoano na zinafanana sana kifonetiki hivyo twaweza kuziita alofoni.
Tuchunguze sifa za kifonetiki za sauti /r/ na /d/, na /l/ na /d/
/r/ /d/ /l/ /d/
+kons +kons +kons +kons +ufizi +ufizi +ufizi +ufizi
+kimadende +kipasuo +ktambaza +kipasuo
Mdee (1986), anadai kuwa sauti [x] na [h] ni alofani za fonimu /h/ kama inavyodhihirika katika maneno /kheri/ na /heri/.
Tukichunguza
sauti hizi, ni kweli kwamba hazileti tofauti za maana katika lugha
ya Kiswahili isipokuwa sauti hizi ni tofauti mno kifonetiki.
Wakati sauti /x/ ni ya kaakaa laini, sauti /h/ ni ya glota.
Je, sauti moja inaweza kutamkiwa katika sehemu mbili tofauti?
Matinde
(2012) anasema alofoni ni maumbo mawili au zaidi ambayo huwakilisha
fonimu moja. Anaendelea kwa kusema kuwa alofoni ni matamshi tofauti
tofauti ya fonimu moja ambayo hujitokeza kutegemea mazingira ya utokeaji
wa sauti hiyo.
Matinde,
yeye anatofautiana na wanaisimu kama Mdee ambao wanasema lugha ya
Kiswahili ina alofoni kwa kutumia jozi za maneno /kheri/ na /heri/
wakisema /x/ na /h/ ni alofoni za fonimu /h/. Anasema tukizingatia
vigezo vya kutambulisha alofoni, hizi ni sauti ambazo ni tofauti kabisa
kwa misingi ya sifa bainifu za kifonetiki, hususan jinsi ya kutamkwa na
mahali pa kutamkiwa.
Matinde,
anasema alofoni katika lugha ya Kiswahili sawa na lugha ya Kiingereza,
hudhihirika na vipasuo hafifu, hivi kwamba kipasuo hafifu kinapokuwa
mwanzoni mwa neno kutamkwa kikiwa na mpumuo, ilhali kipasuo hicho
kinapotanguliwa na fonimu tofauti hutamkwa bila mpumuo.
Kwa mfano neno /pale/ kipasuo (p) hutamkwa kikiwa na mpumuo (ph)
lakini kipasuo hicho kinapotanguliwa na fonimu tofauti kwa mfano katika
neno /alipo/ kipasuo /p/ hutamkwa bila mpumuo. Anaendelea kueleza kuwa
hali hii hudhihirishwa pia katika maneno;
Neno Utamkaji
Katika /khatika/
Palipo /phalipo/
Panda /phanda/
Kaa /khaa/
Kwa hivyo, maumbo yote mawili yaani [p] na [ph] ni alofoni za fonimu /p/. Aidha, maumbo [k] na [kh] ni alofoni za fonimu /k/.
Sauti
alizozionesha Matinde kama alofoni ni vibadala tu katika lugha ambavyo
hutokana na tofauti za kilahaja. Lakini pia mtindo wa uzungumzaji
waweza kusababisha vibadala hivi. Ndio maana si ajabu kukutana na binti
wa kimjini akitamka kwa madaa “palipo uzia penyeza mapenzi”.
Matamshi yake ni kama; /phalipho uzia phenyeza maphenzi/
Mpumuo
sio sifa bainifu ya sauti za Kiswahili sanifu. Sifa bainifu za sauti za
Kiswahili ni kama vile; sifa ya ukonsonanti, namna ya kutamka, mahali
pa kutamkia, mkao wa glota na unazali.
MUHADHARA WA IV:
SIFA PAMBANUZI (BAINIFU) ZA VITAMKWA VYA KISWAHILI
SIFA KUU ZA KONSONANTI
Katika
taaluma ya fonolojia konsonanti zina sifa nyingi, hata hivyo sifa kuu
za jumla ndizo hushughulikiwa zaidi. Sifa hizo za jumla ni jinsi
konsonanti zinavyotamkwa,mahali zinapotamkiwa na kundi asilia la sauti
husika.
Sifa
ya jinsi ya matamshi hutusaidia kupata makundi asilia ya konsonanti
kama vile vipasuo,vikwamizi,nazali,vilainisho,viyeyusho na irabu.
AINA ZA SAUTI KONSONANTI
1. Vipasuo ni sauti ambazo hutamkwa kwa mkondo hewa toka mapafuni kuzuiwa na kisha kuachiwa ghafla.
Mfano:
Aina
|
Ghuna
|
sighuna
|
mifano
|
Vipasuo vya midomo
|
b
|
p
|
Papai,baba
|
Vipasuo vya ufizi
|
d
|
t
|
doa, toa
|
Vipasuo vya vya kaakaa gumu
|
ɟ
|
c
|
Juma, chama
|
Vipasuo vya vya kaakaa laini
|
g
|
k
|
gunia, kabati
|
2. Vikwamizi
ni sauti ambazo hutamkwa kwa mkondo wa hewa kuzuiliwa nusu hivyo
kusababisha hewa kukwamakwama wakati wa utamkaji hewa hupenya na kupitia
katika nafasi iliyowazi.
Aina
|
ghuna
|
sighuna
|
mifano
|
Vikwamizi vya mdomo meno
|
v
|
f
|
Vema, fata
|
Vikwamizi vya meno
|
ð
|
θ
|
Dhanna, thumni
|
Vikwamizi vya ufizi
|
z
|
S
|
Zee, saa
|
Vikwamizi vya kaakaa gumu
|
-
|
ʃ
|
- shamba
|
Vikwamizi vya kaakaa laini
|
ɣ
|
x
|
ghala, kheri
|
3. Vizuio
kwamizi ni sauti zenye kutamkwa kwa mkondo wa hewa kuzuiwa na kuachiwa
taratibu kwa kukwama kwama hivyo kuzalisha vizuio kwamizi.
Mfano:
Aina
|
ghuna
|
sighuna
|
Mifano
|
Vizuio kwamizi vya ufizi
|
ɟ
|
c
|
Juma, chuma
|
Katika lugha ya Kiswahili vizuio kwamizi ni vichache mno ila vipo katika ya Ibo, Yoruba, n.k
[PΦ],[bβ],[tθ],[dð],[gz]
4. Nazali/Ving’ong’o
Sauti
hizi hutamkwa kwa hewa kupitia chemba ya pua. Wakati wa kuzitamka sauti
nazali kaakaa laini hushuka chini na kuzuia mkondo hewa unaopitia
kinywani na kupitia puani.
Sauti nazali pia zipo ghuna na sighuna ingawa katika Kiswahili nazali zote ni ghuna kwa sababu hutamkwa kwa msogeano mpana.
Mfano:
Aina
|
ghuna
|
sighuna
|
mifano
|
Nazali ya midomo
|
m
|
-
|
Mama,mtoto
|
Nazali ya mdomo meno
|
ɱ
|
-
|
Mvi
|
Nazali ya ufizi
|
n
|
-
|
Nani
|
Nazali ya kaakaa gumu
|
ᶮ
|
-
|
Nyau
|
Nazali ya kaakaa laini
|
ŋ
|
-
|
Ng’ambo
|
5. Vilainisho (Ligwidi)
Kundi hili linahusisha aina mbili za sauti ambazo ni vimadende na vitambaza.
(i) Vimadende- ni sauti inayotamkwa wakati ala fulani inachezacheza kwenye mkondo wa hewa.
Mfano: /r/ kama katika ramani
(ii) Vitambaza-
ni sauti zinazotamkwa kwa msogeano wa kubana katikati ya chemba ya
kinywa. Hewa hubanwa na kupita kwenye pembe ya ulimi. Mfano: /l/ kama
katika lala
6. Viyeyusho
Ni
sauti za kawaida katika lugha ya Kiswahili na huitwa hivyo kwa sababu
vinatokea baada ya maathiriano ya irabu kuzalisha sauti mpya ambayo
hushiriki sifa za irabu na wakati si irabu kwa asili. Katika Kiswahili
viyeyusho ni viwili tu navyo ni /w/ na /y/.
7. Irabu/Vokali/Vokoidi
Irabu
ni sauti zinazotamkwa kwa msogeano mpana n azote ni ghuna isipokuwa kwa
baadhi ya lugha za nchi fulani kama kichina na kijapani.
Uainishaji wa irabu
Katika kuainisha irabu mambo yanayozingatiwa ni:
(a) Mwinuko wa ulimi
Hapa tunazingatia kama ulimi umeinuka juu kabisa,juu kiasi,chini kiasi au chini kabisa.
- Irabu za juu kabisa (i,u)
- Irabu za juu kiasi (e,o)
- Irabu za chini kiasi (ɛ, ɔ)
- Irabu za chini kabisa (a,ɑ)
(b) Sehemu ya ulimi iliyoinuka
Hapa tunaangalia ulimi kama umeinuka sehemu ya mbele au ya nyuma,hii hutupatia irabu za mbele na irabu za nyuma.
- Irabu za mbele ni (i, e, ɛ, a)
- Irabu za nyuma ni (u, o, ɔ, ɑ)
(c) Umbo la midomo
Utamkaji wa sauti irabu huwa wa umbo la mdomo mviringo au mtandazwa.
- Irabu za umbo mviringo ni (u, o, ɔ)
- Irabu za umbo mtandazwa ni (i, e, ɛ,a, ɑ)
Trapeza ya irabu za Kiswahili
i u (Juu kabisa)
irabu
irabu e O (Juu kiasi) za za
mbele ɛ ɔ (Chini kiasi) nyuma
a ɑ (Chini kabisa)
NAMNA YA KUBAINISHA VITAMKWA
1. KONSONANTI
Uainishaji wa sauti konsonanti huzingatia vigezo vifuatavyo.
(i) Kuanza na kundi asilia la sauti mf. Kipasuo,kikwamizo, n.k
(ii) Kutaja endapo ni ghuna au si ghuna mf. Kipasuo ghuna.....
(iii) Kutaja mahali pa matamshi mf. /p/ ni kipasuo sighuna cha midomo
NB: Vitamkwa ambavyo viko katika makundi yanayojibainisha hayahitajiki kutajwa sifa zake za kimatamshi (ghuna/sighuna) mf.
- Irabu zote
- Nazali zote
- Vilainisho
- Ving’ong’o
- Viyeyusho
2. IRABU
Uinishaji wa irabu huzingatia mwinuko wa ulimi,sehemu ya ulimi iliyoinuka na umbo la midomo (kama ilivyoelezwa hapo juu).
UNUKUZI WA KIFONETIKI
Unukuzi
wa kifonetiki ni namna ya kuziandika sauti za lugha kwa kutumia misimbo
ya kifonetiki kulingana na ALFABETI ZA KISWAHILI ZA KIMATAIFA (AKIKI).
Mambo ya kuzingatia unaponukuu sauti kifonetiki.
(i) Zingatia misimbo ya sauti mf. Ch-C
(ii) Zingatia ubora wa sauti inayonukuliwa mf. ɛ # e
IRABU ZA KUREFUSHA
Irabu za kurefusha huandikwa kwa kutumia nukta pacha ambazo huwekwa mbele ya irabu ndefu. Mfano: dagaa huandikwa /dagɑ:/
FONIMU ZA KISWAHILI KWA UJUMLA KIFONETIKI
S/N
|
KISWAHILI
|
KIFONETIKI
|
1
|
a
|
a, ɑ
|
2
|
b
|
b
|
3
|
ch
|
C, tʃ, č
|
4
|
d
|
d
|
5
|
e
|
e,Ɛ
|
6
|
f
|
f
|
7
|
g
|
g
|
8
|
h
|
h
|
9
|
i
|
i
|
10
|
j
|
ɟ
|
11
|
k
|
K
|
12
|
l
|
ɭ
|
13
|
m
|
m, ɱ,
|
14
|
n
|
n
|
15
|
o
|
O,ɔ
|
16
|
p
|
p
|
17
|
q
|
-
|
18
|
r
|
r
|
19
|
s
|
s
|
20
|
t
|
t
|
21
|
u
|
u
|
22
|
v
|
v
|
23
|
w
|
w
|
24
|
x
|
-
|
25
|
y
|
j
|
26
|
z
|
z
|
27
|
sh
|
ʃ
|
28
|
ng
|
ŋg
|
29
|
ng’
|
ŋ
|
30
|
dh
|
ð
|
31
|
th
|
θ
|
32
|
gh
|
ɣ
|
33
|
kh
|
x
|
34
|
ny
|
ɲ
|
KWA KUTUMIA SAUTI ZA KIFONETIKI HAPO JUU NUKUU MANENO YAFUATAYO KIFONETIKI
(i) Chagudoa = [Caŋgudɔa]
(ii) King’ongo = [kiŋɔŋgɔ]
(iii) Maembe = [maƐmbƐ]
(iv) Malighafi = [maliɣafi]
(v) Utambulisho = [utambuliʃɔ]
(vi) Maandalizi = [mɑ:ndalizi]
(vii) Unyonyaji = [uɲɔɲaɟi]
(viii) Kinyang’anyiro = [kiɲaŋaɲirɔ]
(ix) Kichongeo = [kitʃɔŋgƐɔ]
(x) Ubabaishaji = [ubabaiʃaɟi]
MATAMSHI NA MOFIMU
Ilivyo
ni kwamba katika baadhi ya mazingira mofimu zinapokubaliana hutokea
mabadiliko mbalimbali ya sauti. Utokeaji huo wa mabadiliko hufuata
taratibu maalumu za lugha inayohusika. Taratibu hizo hujulikana kiisimu
kama kanuni au sheria. Kuna kanuni nyingi za kifonolojia zinazohusu
lugha, kila kanuni ni matokeo ya mchakato fulani.
Michakato na kanuni za kifonolojia
Sauti zote za lugha ziko katika mpangilio ambao ukikiukwa sauti huathiriana. Kila kanuni hutokana na mchakato fulani.
Uundaji wa kanuni
Kanuni
huanza kuelezea muundo ndani wa sauti inayohusika kisha huelezea muundo
nje wa sauti hiyo. Muundo ndani ni muundo halisi wa sauti fulani ikiwa
katika lugha yake ya asili na muundo nje ni ule unaojidhihirisha kama
sauti hiyo ilivyo katika lugha ingine mfano: kibantu – Kiswahili.
Ufafanuzi wa kanuni
/x/ [y]/N-
/x/ [y]/-N
/x/ = sauti fulani x
= inajitokeza kama
[y] = sauti fulani y
/ = katika mazingira ya
N- = kutanguliwa na sauti fulani
-N = kufuatiwa na sauti fulani
Michakato
Kuna michakato anuwai inayotawala maathiriano ya sauti katika maneno,michakato hiyo ni:
v Michakato asilia ya kiusilimisho
v Michakato asilia isiyo ya kiusilimisho
1. Michakato asilia ya kiusilimisho
Michakato asilia ya kiusilimisho ni taratibu zinazoonesha maathiriano ya sauti katika lugha nyingi duniani.
Usimilisho wa nazali; ni
aina ya usilimisho ambao nazali huathiriwa na konsonanti inayofuatana
nayo hivyo nazali inasimilishwa yaani hutamkiwa mahali pale ambapo
konsonanti inatamkiwa.
Kwa hiyo, / n / [ m ]/ K-
Hivyo
basi, fonimu nazali / n / inapofuatwa na konsonanti ya midomo
inaathiriwa na kuwa nazali ya midomo ili iendane na konsonanti
inayoiathiri.
Mfano
umbo ndani umbo nje
/n+buzi/ [mbuzi]
/n+bwa/ [mbwa]
/n+papai/ [mpapai]
Usilimisho wa Konsonanti; ni
aina ya usilimisho ambao konsonanti huathiriwa na nazali inayofuatana
nayo hivyo konsonanti inasimilishwa yaani hutamkiwa mahali pale ambapo
nazali inatamkiwa. kuna baadhi ya sauti ambazo huathiriwa na nazali “n”
inapokuwa inaandamia yaani kuna sauti ambazo huathiriwa zinapokaribiana
kiasi au moja kwa moja na nazali “n”. Mara nyingi hutokea katika maumbo
ya umoja na uwingi katika maumbo ya maneno
Mfano:-
Umbo ndani Umbo nje
/n+limi/ [ndimi]
/n+refu/ [ndefu]
Hapa
tunaona kwamba sauti [ l ] na [ r ] zinapokaribiana na irabu na irabu
haziathiriki lakini zinapokaribiana na nazali “n” hubadilika na kuwa “d”
/l/ [d]/N-
/r/ [d]/N-
2. Michakato asilia isiyo ya kiusilimisho
(a) Udondoshaji;
mchakato huu unahusu kuachwa kwa sauti fulani katika matamshi wakati
mofimu mbili zinapokaribiana yaani katika mazingira hayo hayo ya sauti
ambayo ilikuwepo hapo awali hutoweka. Kwa mfano irabu /u/ ikifuatiwa na
konsonanti inayofanana nayo kwa sifa za matamshi kama nazali irabu hiyo
hudondoshwa, kama inavyooneshwa hapa chini.
Umbo ndani umbo nje
/mutu/ [mtu]
/mwalimu/ [mwalim]
/muzito/ [mzito]
/u/ [θ]/M-
(b) Uyeyushaji;
wataalamu wengine huita irabu kuwa nusu irabu. Mgullu (1999), anasema
huu ni mchakato ambao irabu za juu /u/ na /i/ hubadlika na kuwa /w/ au
/y/ katika mazingira ya kufuatiwa na irabu zisizofana nazo. Kwa kifupi
ni kwamba /u/ inapofuatiwa na irabu yoyote isiyofanana nayo hubadilika
kuwa [w] na /i/ ikifuatiwa na irabu yoyote isiyofanana nayo hubadilika
na kuwa [y].
Hivyo
uyeyushaji ni kanuni inayoelezea mabadiliko ya sauti (irabu) na kuwa
kiyeyusho kama [w] au [y], hii ni kwa irabu zote za juu zinapofuatana na
sauti zingine zisizofanana nazo. Na sauti hizo hubadilika katika
mazingira ya /u/ hubadilika kuwa [w] inapofuatana na irabu nyingine
isiyofanana nayo na /i/ inabadilika na kuwa [y] pia inapofuatana na
irabu isiyofanana nayo.
Mfano:
Umbo ndani Umbo nje
/mu+ezi/ [mwezi]
/mu+alimu/ [mwalimu]
/mu+izi/ [mwizi]
/mi+aka/ [myaka]
/Vi+angu/ [vyangu]
/u/ [w]/-I; I # u
/i/ [y]/-I; I # i
(c) Muungano/mvutano wa irabu; kanuni
hii hutokea pale ambapo irabu ya mofimu moja inapokabiliana na irabu ya
mofimu nyingine katika mpaka wa mofimu irabu hizo huungana na kuzaa
irabu moja, na irabu hizo sharti moja iwe ya chini na nyingine ya juu.
Mfano:
Umbo ndani umbo nje
/Wa + enye/ [wenye]
/Wa + ingi/ [wengi]
/Ma + ino/ [meno]
/Wa + izi/ [wezi]
/a,i/ [e]/k-k
(d) Tangamano la irabu; Huu
ni mchakato ambao irabu fulani hukubali kuandamana katika mazingira
maalumu. Kwa mfano mofu [i] na [e] katika lugha ya Kiswahili huonekana
kama alomofu au maumbo mbalimbali ya mofu moja ya kutendea na
kutendesha, lakini utokeaji wake hutegemeana na mofu itakayojitokeza
katika mzizi. Kama irabu ya mzizi ni /a/, /i/ au /u/ basi irabu ya
kiambishi cha utendea lazima iwe ni [i] , wakati irabu ya mzizi ikiwa ni
/e/ au /o/ katika kauli ya utendea kiambishi chake kitakuwa ni [e].
Mfano.
Imba --------------imbia
Andika-------------andikia
Funga ------------ fungia
Daka --------------dakia
Oga----------------ogea
Sema --------------semea a
/Utendea/ [i]/-mz+ i
u
(e) Ukaakaishaji; Mgullu
(1999) akimnukuu Les (1984), anadai kuwa ukaakaishaji wa fonimu hutokea
ambapo fonimu zisizo za kaakaa gumu zinapobadilika na kuwa za kaakaa
gumu. Katika Kiswahili sauti za kaakaa gumu zipo mbili tu yaani /ɟ/
na /ʧ/ ambazo ni kwamizi. Anamalizia kwa kusema kuwa ukaakaishaji wa
fonimu hutokea wakati ambapo fonimu zisizo vikwamizi hubadilika na kuwa
vikwamizi. Hii katika ukokotozi wake unakuwa kama ifuatavyo.
Mfano:
/ki+enu/ [chenu]
/ki+eusi/ [cheusi]
/ki+ombo/ [chombo]
/ki+umba/ [chumba]
Kanuni; /k/ [ʧ]/-I
Hapa
tunaona kwamba kipasuo cha kaakaa laini /k/ hubadili mahali pa matamshi
na kuwa kikwamizi /ʧ/ cha kaakaa gumu katika mazingira ya kufuatiwa na
sauti irabu /I/
SIFA BAINIFU ZA VITAMKWA
Kila
kitamkwa huambatanishwa na seti ya sifa pambanuzi ambazo husaidia
ubainishaji wa sauti husika. Sifa hizo huwa ni za msingi na za ziada.
Baadhi ya sifa kuu za msingi ni:
1. Ukonsonanti ( + kons); sifa hii hutofautisha konsonanti na irabu ambapo irabu zote ni (-kons) na konsonanti zote ni (+kons)
2. Usilabi (+ sil);
sifa hii huwekwa katika vitamkwa vya msingi vilivyo katika muundo wa
silabi zote. Usilabi huambatanishwa kwenye irabu zote pamoja na baadhi
ya sauti nazali ambazo huweza kusimama kama silabi mfano [m] na [n].
3. Usonoranti (+son);
sifa hii huwekwa katika vitamkwa ambavyo vinatamkwa kwa hewa kupita
bila kubanwa katika chemba ya kinywa au pua. Kundi hili hubeba sauti
zote ambazo ni:
- Irabu
- Viyeyusho
- Vilainisho
- Ving’ong’o
Sifa bainifu za ziada za vitamkwa
1. Ukorona (+ kor); hii ni sifa ya sauti zinazotamwa kuanzia kwenye ufizi kuelekea ndani mf. /r/,/l/,/k/,/g/, n.k
2. Uanteria (+
ant); hii ni sifa inayohusu sauti zinazotamkwa kwa kutumia ncha ya
ulimi na vituta vya ufizi au bapa la ufizi kuelekea nje mf. /r/ na /l/
3. Umeno (+ meno); hizi ni sauti zinazotamkiwa kwenye meno mf. /th/,/dh/
4. Uglota (+ glota); sifa hii inahusu sauti za glota tu mf. /h/, /kh/
5. Ukontinuanti (+ kont); sifa hii inahusu sauti ambazo huambatana na muendelezo wa kutoka kwa sauti. Mf. /f/,/v/,/s/
Ustridenti (+ strident); sifa hii huwekwa kwenye sauti zinazoambatana na umuluzi wakati wa kuzitamka. Mf. /s/,/sh/.
MUHADHARA WA V:
MIUNDO YA SILABI ZA KISWAHILI SANIFU
Silabi
Silabi
ni kipashio cha kifonolojia kinachohusu matamshi ambacho kwacho sauti
za Lugha hutamkwa mara moja na kwa pamoja kama fungu moja la sauti.
Silabi ni kila fungu la sauti linalotamkika mara moja na kwa pamoja.
Kuna aina mbili za silabi, yaani silabi funge na silabi huru. Silabi huru ni zile ambazo huishia na irabu.
Kwa mfano; la, ma, kwa, mba, n.k.
Silabi funge ni
zile zinazoishia na konsonanti ambapo katika lugha ya Kiswahili ni
nadra kuzipata maana lugha hii inatumia silabi huru lakini hupatikana
katika maneno ya Kiswahili yenye kutoka katika lugha nyingine za kigeni
na baadhi ya maneno yenye kuathiriwa kifonetiki kwa irabu zake.
Kwa mfano: alhamisi – a-l-ha-mi-si; taksi - ta-k-si,mtu-m-tu,nta-n-ta
Miundo ya Silabi za Kiswahili
- Muundo wa irabu peke yake (I) - Yapo maneno katika lugha ya Kiswahili yanayoundwa na irabu peke yake kama silabi. Mfano; u+a = Ua, o+a = Oa, a+u = Au, n.k.
- Muundo wa konsonanti pekee (K) – Kiswahili hakina maneno mengi yanayoundwa na silabi ambazo ni konsonanti pekee isipokuwa maneno machache ambayo huwa ni ya nazali /m/ na /n/ na huwa zinatumika mwanzoni au katikati ya neno. Mfano; m+ke = Mke, m+bwa = Mbwa, n+chi = Nchi n.k.
- Muundo wa konsonanti na irabu (KI) – Katika muundo huu konsonanti hutangulia irabu. Mfano; b+a = Ba, k+a = Ka n.k.
- Muundo wa konsonanti mbili na irabu (KKI) – Katika muundo huu konsonanti mbili hutangulia irabu. Mara nyingi konsonanti ya pili huwa ni kiyeyusho. Mfano; k+w+a = Kwa, m+w+a = Mwa, b+w+a = bwa, n+d+e = Nde, n.k.
- Muundo wa konsonanti tatu na irabu (KKKI) – Muundo wa namna hii hujitokeza katika maneno machache. Mfano; Bambwa, Tingwa, Tindwa, Mbwa, n.k.
- Muundo wa silabi funge – Huu hujitokeza katika maneno machache ambayo huwa ya kigeni. Mfano; Il-ha-li = Ilhali, Lab-da = Labda,a-h-sa-n-te = ahsante
NB: Silabi hutengwa kwa kutumia alama maalumu mfano: $ba$, $ma$, $m$, $n$
MUHADHARA WA VI:
MOFOFONOLOJIA YA KISWAHILI SANIFU
Mofofonolojia/mofofonemiki ni taaluma ya kiisimu inayoshughulikia uchanganuzi na uainishaji wa vipengele vya kifonolojia vinavyoathiri maumbo ya mofimu katika mfuatano wake.
Mofofonolojia/mofofonemiki ni taaluma ya kiisimu inayoshughulikia uchanganuzi na uainishaji wa vipengele vya kifonolojia vinavyoathiri maumbo ya mofimu katika mfuatano wake.
Mfano:
(a)Funga – fungia
(b)Panga – pangia
(c)Piga – pigia
(d)Sema – semea
(e)Soma – somea
Mofofonolojia
hubeba kanuni mahususi zinazoelezea mazingira ya utokeaji wa alomofu.
Tofauti ya kanuni za kifonolojia na zile za kimofofonolojia.
(i) Kanuni za kifonolojia hazina vighairi, mf. Hakuna vighairi katika utokeaji wa mkazo silabi ya pili toka mwishoni mwa neno.
(ii) Kanuni za kimofofonolojia huwa na vighairi vingi. Mf. Katika kauli ya kutendea.
- /i/ hubeba utendea iwapo mzizi wa neno unaundwa na irabu (a,i,u)
- /e/ hubeba utendea iwapo mzizi wa neno unaundwa na irabu (e,o)
(iii) Kanuni za kimofofonolojia mara nyingi hutegemea mofimu inayohusika.
KANUNI ZA KIMOFOFONOLOJIA
(a) Usilimisho wa nazali; ni aina ya usilimisho ambao nazali huathiriwa na konsonanti inayofuatana nayo hivyo nazali inasimilishwa yaani hutamkiwa mahali pale ambapo konsonanti inatamkiwa.
(a) Usilimisho wa nazali; ni aina ya usilimisho ambao nazali huathiriwa na konsonanti inayofuatana nayo hivyo nazali inasimilishwa yaani hutamkiwa mahali pale ambapo konsonanti inatamkiwa.
Kwa hiyo, n m / - K
Hivyo
basi, fonimu nazali / n / inapofuatwa na konsonanti ya midomo
inaathiriwa na kuwa nazali ya midomo ili iendane na konsonanti
inayoiathiri.
Mfano
umbo ndani umbo nje
n+buzi [mbuzi]
n+bwa [mbwa]
n+papai [mpapai]
(b) Usilimisho wa Konsonanti; ni
aina ya usilimisho ambao konsonanti huathiriwa na nazali inayofuatana
nayo hivyo konsonanti inasimilishwa yaani hutamkiwa mahali pale ambapo
nazali inatamkiwa. kuna baadhi ya sauti ambazo huathiriwa na nazali “n”
inapokuwa inaandamia yaani kuna sauti ambazo huathiriwa zinapokaribiana
kiasi au moja kwa moja na nazali “n”. Mara nyingi hutokea katika maumbo
ya umoja na uwingi katika maumbo ya maneno.
Mfano:-
Umbo ndani Umbo nje
n+limi [ndimi]
n+refu [ndefu]
Hapa
tunaona kwamba sauti [ l ] na [ r ] zinapokaribiana na irabu
haziathiriki lakini zinapokaribiana na nazali “n” hubadilika na kuwa “d”
l d/N-
r d/N-
(c) Udondoshaji;
mchakato huu unahusu kuachwa kwa sauti fulani katika matamshi wakati
mofimu mbili zinapokaribiana yaani katika mazingira hayo hayo ya sauti
ambayo ilikuwepo hapo awali hutoweka. Kwa mfano irabu /u/ ikifuatiwa na
konsonanti inayofanana nayo kwa sifa za matamshi kama nazali irabu hiyo
hudondoshwa, kama inavyooneshwa hapa chini.
Umbo ndani umbo nje
mutu mtu
mwalimu mwalim
muzito mzito
/u/ [θ]/M-
(d) Uyeyushaji;
wataalamu wengine huita irabu kuwa nusu irabu. Mgullu (1999), anasema
huu ni mchakato ambao irabu za juu /u/ na /i/ hubadlika na kuwa /w/ au
/y/ katika mazingira ya kufuatiwa na irabu zisizofanana nazo. Kwa kifupi
ni kwamba /u/ inapofuatiwa na irabu yoyote isiyofanana nayo hubadilika
kuwa [w] na /i/ ikifuatiwa na irabu yoyote isiyofanana nayo hubadilika
na kuwa [y].
Hivyo
uyeyushaji ni kanuni inayoelezea mabadiliko ya sauti (irabu) na kuwa
kiyeyusho kama [w] au [y], hii ni kwa irabu zote za juu zinapofuatana na
sauti zingine zisizofanana nazo. Na sauti hizo hubadilika katika
mazingira ya /u/ hubadilika kuwa [w] inapofuatana na irabu nyingine
isiyofanana nayo na /i/ inabadilika na kuwa [y] pia inapofuatana na
irabu isiyofanana nayo.
Mfano:
Umbo ndani Umbo nje
mu+ezi mwezi
mu+alimu mwalimu
mu+izi mwizi
mi+aka myaka
Vi+angu vyangu
u w/-I; I # u
i y/-I; I # i
(e) Muungano/mvutano wa irabu;
kanuni hii hutokea pale ambapo irabu ya mofimu moja inapokabiliana na
irabu ya mofimu nyingine katika mpaka wa mofimu irabu hizo huungana na
kuzaa irabu moja, na irabu hizo sharti moja iwe ya chini na nyingine ya
juu.
Mfano:
Umbo ndani umbo nje
Wa + enye wenye
Wa + ingi wengi
Ma + ino meno
Wa + izi wezi
/a,i/ e/k-k
(f) Tangamano la irabu;
Huu ni mchakato ambao irabu fulani hukubali kuandamana katika mazingira
maalumu. Kwa mfano mofu [i] na [e] katika lugha ya Kiswahili huonekana
kama alomofu au maumbo mbalimbali ya mofu moja ya kutendea na
kutendesha, lakini utokeaji wake hutegemeana na mofu itakayojitokeza
katika mzizi. Kama irabu ya mzizi ni /a/, /i/ au /u/ basi irabu ya
kiambishi cha utendea lazima iwe ni [i] , wakati irabu ya mzizi ikiwa ni
/e/ au /o/ katika kauli ya utendea kiambishi chake kitakuwa ni [e].
Mfano.
Imba --------------imbia
Andika-------------andikia
Funga ------------ fungia
Daka --------------dakia
Oga----------------ogea
Sema --------------semea a
//Utendea// i/-mz+ i
U
e
//utendea// e/-mz+
o
(g) Ukaakaishaji;
Mgullu (1999) akimnukuu Les (1984), anadai kuwa ukaakaishaji wa fonimu
hutokea ambapo fonimu zisizo za kaakaa gumu zinapobadilika na kuwa za
kaakaa gumu. Katika Kiswahili sauti za kaakaa gumu zipo mbili tu yaani /ɟ/
na /ʧ/ ambazo ni vikwamizi. Anamalizia kwa kusema kuwa ukaakaishaji wa
fonimu hutokea wakati ambapo fonimu zisizo vikwamizi hubadilika na kuwa
vikwamizi. Hii katika ukokotozi wake inakuwa kama ifuatavyo.
Mfano:
ki+enu chenu
ki+eusi cheusi
ki+ombo chombo
ki+umba chumba
Kanuni; k ʧ/-I
Hapa
tunaona kwamba kipasuo cha kaakaa laini /k/ hubadili mahali pa matamshi
na kuwa kikwamizi /ʧ/ cha kaakaa gumu katika mazingira ya kufuatiwa na
sauti irabu /I/
(h) Udondoshaji; wakati mwingine mofimu fulani huweza kudondoka kutokana na mfuatano wa mofimu katika mazingira fulani.
Mfano:
- Wanasoma ---------- hawasomi
- Anasoma ----------- hasomi
- Nilikunywa -------- sikunywa
//njeo iliyopo// θ/- [ukanushi]
// njeo iliyopita// θ/- [ukanushi]
Wakati uliopo unapokanushwa mofu ya wakati huo hudondoka na taarifa yake hubebwa na kiambishi tamati kikanushi cha wakati huo.
(i) Uingizaji/uchopekaji;
hii ni kanuni kinyume cha kanuni ya udondoshaji. Hapa mofimu huingizwa
mahali ambapo haikuwepo awali. Mara nyingi mofimu hizi ni zile mofimu
mahususi ambazo hufanya kazi ya kuimarisha mizizi ya silabi moja.
Mfano:
- j--------- anakuja
- nyw ------- anakunywa
- f --------- amekufa
- l --------- alikula
θ ku/- j,nyw,f,l
(j) Msinyao; hii inahusu irabu ndefu ambapo katika mazingira fulani irabu ya kurefuka inalazimishwa kutokea kama irabu fupi.
Mfano:
- Wa-ana -------- wana
- Wa –enyewe ---- wenyewe
- Ma – ema ------ mema
- Pa – ingi ------ pengi
(a+a) a
(a+e) e
(a+i) e