NADHARIYA YA TAMTHIYA NA DRAMA
1.0 Utangulizi
Tamthiliya ni utanzu mmoja kati ya tanzu tatu kuu za fasihi yaani
Riwaya, Tamthiliya na Ushairi. Tamthiliya hutegemea mazungumzo na
uigizaji ili kuwasilisha ujumbe wake. Katika moduli hii, dhana za Sanaa
za Maonyesho, Drama na Tamthiliya zitafasiriwa, tutaainisha
tamthiliya katika makundi mbalimbali na hatimaye kueleza nafasi ya
tamthiliya katika jamii.
1.1 Dhana za Sanaa za Maonyesho,
Drama na Tamthiya
Sanaa za Maonyesho
Sanaa za maonyesho, kwa mujibu wa Mlama (1983), ni sanaa ambayo
huwasilisha, ana kwa ana, tukio fulani kwa hadhira kwa kutumia usanii
wa kiutendaji. Sanaa za maonyesho huliweka wazo katika hali ambapo
tukio hilo linaweza kutendeka kwa kutumia usanii wa utendaji kama
vile vitendo, uchezaji ngoma, n.k.
Drama
Drama ni taaluma inayohusu uigizaji wa hali fulani iwe ni vitendo,
tabia au hisia za binadamu kwa kufuata taratibu maalumu. Drama ni
aina mojawapo ya sanaa za maonyesho ambayo usanii wa kiutendaji
wake hutegemea zaidi vitendo na uongeaji, tofauti na aina nyingine
kama vile ngoma ambazo hutegemea zaidi uchezaji ngoma na upigaji
muziki. Drama ni sanaa ya maonyesho yenye asili ya nchi za Ulaya.
Tamthiliya
Neno ‘tamthiliya’ linatokana na kitenzi ‘mithilisha’kwa maana ya
kufananisha au kulinganisha. Katika Kiswahili, tamthiliya linatumika
kwa maana ya ‘michezo ya kuigiza’. Katika tamthiliya huwa kuna
ufananishaji ambapo mwigizaji hujifananisha na mhusika wa mchezo
wakati wa kuigiza.
Tamthiliya huwasilisha mambo kimaigizo kwa kutoa picha ya mambo
ambayo yametokea hivyo au yanaaminika yangeweza kutokea hivyo.
Tamthiliya husawiri hali mbalimbali katika maisha ya jamii na ndiposa
ikaitwa tamthiliya kwa kule kujaribu kufananisha mazungumzo na
maigizo hayo kifasihi na hali halisi katika jamii husika.
Mazrui na Syambo (1992) wanaieleza tamthiliya kuwa ni utungo wa
fasihi ambao umebuniwa, kwa kiasi kikubwa, kwa lugha ya Asili ya kitenzi hiki ni Kiarabu.
mazungumzo yenye kuzua na kuendeleza matukio ya hadithi ya
utungo huo.
Lugha ya mazungumzo baina ya wahusika ni alama
kubwa ya tamthiliya. Chanzo cha matukio ya hadithi ya tamthiliya
fulani mara nyingi hupatikana mumo humo katika mazungumzo ya
wahusika wake.
TUKI (2004) nao wanafasili tamthiliya kuwa ni utungo wa kisanaa
ambao huweka wazo fulani katika matendo na mazungumzo.
Kutokana na maelezo haya, tunaweza kusema kwamba tamthiliya ni
aina mojawapo ya sanaa za maonyesho ambayo usanii wa utendaji
wake hutegemea zaidi vitendo na uongeji, tofauti na aina nyingine
kama vile ngoma ambazo hutegemea zaidi uchezaji ngoma na upigaji
mziki. Tamthiliya ni ule utungo ambao unaweza kuwa umeandikwa au
haukuandikwa unaoliweka wazo linalowasilishwa katika umbo la tukio
la kuliwezesha kutendeka mbele ya hadhira (Mulama, P. 1983: 206).
Kigezo kikuu cha tamthiliya ni kuweza kuwasilishwa jukwaani na
kutazamwa na hadhira. Tamthiliya huwa na sifa za kawaida za
maonyesho (Muhando na Balisidya, 1976; Muhando, 1983 na
Mulokozi, 1996). Kila tamthiliya ina sifa za kipekee kulingana na
maudhui yake na jinsi maudhui hayo yalivyowasilishwa (fani).
Hata
hivyo, tamthiliya nyingi zina sifa zifuatazo:
i) Utoshelevu Kimuundo. Tamthiliya nzuri huwa na sehemu tatu
muhimu: Mwanzo, Katikati na Mwisho. Sehemu zake zinatazamiwa
kuingiliana, kujengana na kukamilishana.
ii) Tamthiliya huwa na lengo. Katika zama za Aristotle, kwa mfano,
tanzia ziliwajibika kuzindua hofu na huruma.
iii) Vitendo vyote vinavyofanyika katika tamthiliya vinapaswa
kuchangia katika ufanisi wa dhamira za mtunzi.
iv) Fani. Watunzi wa tamthiliya wanawajibika kutumia mbinu za kisanii
zinazowashajiisha wasomaji au watazamaji kuendelea kusoma au
kutazamia maatokeo ya matendo yanayoigwa. Mbinu hizo ni pamoja na
jazanda, kejeli, ritifaa, tashbihi, tashihisi na uzungumzi
nafsia.
v) Wasanii bora ni wale wanaotunga tamthiliya zinazozungumzia
kadhia zinazoweza kutimia katika maisha ya binadamu.
1.2 Drama za Kijadi
Drama za kijadi ni zile sanaa za maonyesho ambazo zimechimbuka
katika jamii za kiafrika, ikiwemo Tanzania. Sanaa hizo ni pamoja na
Maelezo ya kina yanapatikana katika
Dorsch,S.T.(1965)Aristotle/Horace/Longinus: Classical
Literary Criticism. Penguin: Harmondsworth. ngoma, majigambo, miviga ya
ndoa, harusi, mazishi, jando na unyago,
matambiko, utambaji hadithi, n.k. Katika shughuli hizi watu hufanya
vitendo vya kisanaa kama vile uchezaji ngoma, uimbaji, upigaji muziki
na utongoaji mashairi vikiambatana na matendo ya mwili na matumizi
ya lugha.
Vitendo hivi vya kisanaa ni mojawapo ya njia bora ya kuwasiliana kati
ya watu na watu wengine, au watu na miungu na mizimu, katika
jitihada za kuyakabili mazingira na kuendeleza jamii. Kwa kucheza
ngoma watoto hufundishwa tabia inayotegemewa na jamii utu uzimani.
Kwa kuimba, kucheza na kutenda, miungu huelezwa matatizo ya
ukame, magonjwa, mafuriko, n.k. kwa kutamba hadithi watu
hufunzwa historia ya jamii, tabia nzuri, jinsi ya kuishi na watu wengine
n.k.
1.3 Aina za Tamthiya
Tamthiliya ni za aina kadha. Kila aina ina sifa zake maalum. Kimsingi,
tunaweza kuvitumia vigezo vya muda (duration) na utanzu (genre)
kuzigawa tamthiliya katika aina mbalimbali.
Kwa mujibu wa kigezo cha kwanza, muda, kuna tamthiliya ambazo
huwa na tendo moja na huchukua muda mfupi.
Kwa mfano, tamthliya
ya Samuel Beckett iitwayo ‘Breath’ inachukua muda wa dakika moja
hivi kuigizwa ilhali ‘Maisha Subira’ iliyoandikwa na Omari, S. itachukua
muda mrefu kuigiza.
Kigezo cha muda hutegemea wakati ilhali cha utanzu hutegemea
yaliyomo (maudhui) au mada ya tamthiliya. Kutokana na kigezo hiki
cha pili tunaweza kuainisha vitanzu vifuatavyo:
a) Tanzia (Tragedy)
b) Futuhi/Komedia (Comedy)
c) Melodrama (Melodrama)
d) Kichekesho (Farce)
e) Tanzia–ramsa/Tanzia-futuhi (Tragicomedy)
f) Tamthiliya ya Kihistoria (Historical Play)
g) Tamthiliya Tatizo (Problem Play)
h) Tamthiliya ya Kibwege (Absurd Drama)
1.3.1 Tanzia (Tragedy)
Kijelezi cha Dhana ‘Tanzia’
Tanzia ni aina ya tamthiliya yenye uzito unaodhihirika kihisia au
kifikra. Tanzia huwa na suala, matendo na malengo dhati. Aristotle alikuwa mtu wa kwanza ambaye baada ya kuyatazama maandishi ya
tamthiliya za Kigiriki aliandika maana ya tanzia katika kitabu chake
cha Poetics . Kutokana na uchunguzi wake aliona tanzia kuwa ni
tamthiliya yenye huzuni ambayo inagusa hisia za watazamaji kiasi cha
kuogopesha na kumwonea huruma mhusika mkuu ambaye hupata
janga. Na mara zote huyu mhusika mkuu huwa na mwenendo bora
unaokubalika na jamii. Pia mwenye msimamo. Janga analolipata lisiwe
kubwa kiasi cha kusababisha mtazamaji kuogopa sana hata kushindwa
kumwonea huruma mhusika.
Aristotle aliuona utanzu huu kama ‘mwigo’ au ‘uigaji’ wa tendo ambalo
lina udhati, ukamilifu, ubora na ukuu fulani. Kwa mujibu wa mtaalamu
huyu, tendo hilo lazima liwe na uwezo wa kuwaathiri watazamaji na
kuwafanya waingiwe na huzuni au kihoro pamoja na kuwa na uwezo
wa kuzitakasa hisia za woga au huzuni katika kile alichokiita
mtakasohisia.
Mtazamaji mwishoni mwa tamthiliya alijiona katika hali ile ya yule
aliyeanguka. Hali hii inamfanya atambue nafasi na hatima yake katika
ulimwengu huu na kujiweka mahala pake anapostahili. Lugha
iliyotumika ni ushairi. Tanzia aliyokusudia Aristotle iliwahusu wahusika
wa hali ya mkwezo kama wafalme, malkia, miungu na wengineo.
Watunzi maarufu wa tanzia ya kiyunani ni pamoja na Aeschylus,
Sophocles na Euripedes.
Hata hivyo, dhana ya tanzia sasa
imepanuliwa kama ilivyo hata dhana ya shujaa wa kitanzia.
Augusto Boal ambaye amekuja miaka mingi sana baada ya Aristotle
amefanya uchambuzi wa kazi za tanzia. Anaiona tanzia ya Aristotle
kama aina ya sanaa ambayo inatumiwa na wanasiasa kuwatawala
watu. Muunda wa sanaa ya Kigiriki inagawa watu katika makundi
mawili ya kitawala na kutawaliwa ambayo moja hutoa mawazo na
lingine hupokea. Kule kuogopa na kumwonea huruma mhusika mkuu
ambaye ni mtawala/mkuu ni kuendeleza utabaka uliopo kuwa mambo
hayabadiliki. Boal anaiona tanzia ya Kigiriki kuwa ni ya ukandamizaji
na haifai kuleta mabadiliko ya jamii .
Steiner, G. naye anasema wakati huu tulio nao hakuna kitu kama
tanzia. Anasema mambo yaliyofanya tanzia kuwepo hayapo tena hivyo
tanzia imekufa6
. Mambo ambayo yalikuwa yakimshinda mhusika mkuu
– nguvu za kiungu, hayapo tena kutokana na maendeleo ya binadamu.
Hapo awali katika tanzia mhusika mkuu hakuwa na matumaini ya
mambo kuwa mazuri punde anapoanguka. Huo ulikuwa mwisho wa Aristotle (386 – 322 KM) kitabu hiki kinahusu ‘Sanaa ya Utunzi’.
Mackeon, R. (1974) Aristotle. New York: Random House. Ukrasa wa 21
5
Boal, A. (1979) Theatre of the Oppressed. London: Pluto Press. Ukrasa wa
46, Steiner, G. (1961) The Death of Tragedy. London: Faber &
Faber.
5
kila kitu. Steiner anasema tanzia ilikuwepo wakati wa Sophocles,
Shakespeare na Racine lakini baada ya hapo masuala yote yana
ufumbuzi katika tamthiliya. Hata ushairi ambao ulizifanya kazi za
tanzia zieleweke kwa wachache tu ukapotea na badala yake kuzuka
lugha nathari (prose).
Hivyo tamthiliya zote zenye masahibu makuu
lakini zenye fikra au uelekeo wa ukombozi sio tanzia bali tamthiliya
nzito.
Kwa upande wake, Wole Soyinka anaamini kuwa licha ya kuwepo
mabadiliko katika maisha na fikra za binadamu, bado tanzia, kama
ilivyoletwa na Wagiriki ipo na inahitajika. Soyinka huona kuwa janga
limpatapo mhusika katika tanzia halimhusu yeye binafsi tu, bali
linavuruga hali nzima ya utulivu ya jamii yake. Jamii ya mhusika wa
tanzia ya Kiafrika, kwa mfano, hujumlisha wale waishio na waliokufa –
mizimu na miungu .
Kiwango cha uzito wa tanzia kutokana na Soyinka
ni kikubwa zaidi ukiangalia idadi ya wale wote wanaohusishwa na
janga hilo.
Kimsingi, wasomi wote hawa isipokuwa Steiner wanakubaliana katika
uwepo wa tanzia. Hata kwa Steiner maendeleo ya binadamu
anayoyasifia kuwa yameua tanzia bado yameshindwa kuondoa uovu
katika binadamu, ambacho ni kipengele muhimu kinachosababisha
janga kwa binadamu. Maendeleo ya mahusiano kati ya binadamu yapo
bado kama hapo awali.
Mikondo Minne ya Tanzia
Kuna mikondo minne ya tanzia, nayo ni: Tanzia ya Urasimi (Classical
Tragedy), Tanzia ya Urasimi Mpya (Neo-classical Tragedy), Tanzia ya
Kisasa (Modern Tragedy) na Tanzia ya Kikomunisti (Socialist Realism
Tragedy).
i) Tanzia ya Urasimi (Classical Tragedy)
Hii iliweza kuwepo kutokana na tabaka la mabwanyenye kufadhili
sanaa huko Ugiriki. Hivyo liliitumia tanzia kwa manufaa yake yenyewe.
Mengi yanayojitokeza kwenye tanzia hizi ni kwa ajili ya kukudhi
matakwa ya tabaka hili. Mambo yanayoonyesha hali hii ni ‘status quo’
ambapo mhusika mkuu sharti awe mtu bora ambaye kutokana na
kutokamilika kwake kimatendo kwa ajili ya ubinadamu wake anapata
janga ambalo linamtoa katika hali ya juu aliyokuwa nayo na kuwa
duni.
Aidha, wakati wa urasimi fikra za watu ziliiweka miungu kama yenye
kauli ya wema au uovu katika yote yaliyofanyika duniani; hivyo Soyinka,
W. (1976) Myth, Literature and the African World. Cambridge: Cambridge
University
Press. Kurasa 37 - 60 Yaani ‘hali kama ilivyo’ mawazo haya
yamesababisha mhusika mkuu kuangushwa na nguvu
hizi za kiungu ambazo hawezi kushindana nazo.
Nguvu hizi za kiungu
hutawala matendo na matukio ya wahusika.
Mawazo ya wakati huu yaliheshimu hadhi ya binadamu na kuyaona
maisha yake yenye maana na kuthaminika. Ingawa binadamu si rahisi
kueleweka (ni changamano), anahusika kwa njia moja au nyingine na
masahibu yanayomkuta.
Katika tanzia hizi binadamu yu huru kufuata ushauri wake mwenyewe
na ni katika kufanya hivi ndiyo tabia yake hujitokeza. Ukaragosi hauna
nafasi katika tanzia. Karagosi siku zote haaminiki na hudharaulika,
hivyo hafai kuwa mhusika mkuu. Anatakiwa mtu ambaye ingawa
anakabiliwa na magumu yamshindayo, haonyeshi ukaragosi bali huwa
na msimamo maalum.
Lugha ilitumika pia kukidhi matakwa ya tabaka tawala. Lugha ya
tanzia ilikuwa ya kishairi ambayo ilisababisha mgawanyiko kati ya
watazamaji wa hali ya chini na ya juu. Waigizaji kutenganishwa na
watazamaji kulisaidia upande mmoja kubugia yale ambayo upande
mwingine uliyatoa. kuwepo kwa kiitikio/kibwagizo ilikuwa ishara ya
demokrasia au sauti ya wengi.
Mfano wa tanzia ya urasimi ni Mfalme Edipode . Tanzia hii inaanza na
hali mbaya ya magonjwa ya kufisha katika mji wa Thebe. Watu wa
Thebe wanakusanyika kuzungumza juu ya janga hili. Inabainika kuwa
hali mbaya ya Thebe inatokana na kuuliwa kwa mfalme wa zamani
Laio.
Ili janga litoweke, sharti muuaji ambaye yu miongoni mwa watu wa
Thebe apatikane. Mfalme Edipode anaamua kufuatilia jambo hili
mpaka huyo muuaji aliyelaaniwa apatikane.
Chanzo cha maovu katika
tanzia hii ni utabiri wa hapo kale wa miungu kuwa mfalme Laio
atauawa kwa mkono wa mwanawe mwenyewe ambaye pia atamwoa
mama yake.
Katika uchunguzi wake anagundua kuwa yeye ndiye aliyemuua Laio na
pia kumwoa mama yake. Haya ni matukio maovu ya utabiri ambayo
waliohusika walijaribu kuyakwepa na kushindwa. Anapogundua tanzia
yake, Edipode anajipofusha na kuhamia ughaibuni.
Kabla janga halijamtokea mhusika mkuu, sharti apitie awamu tatu –
‘harmatia, perepeteia na anagnoris’.
Tanzia ya urasimi ianzapo, mhusika mkuu anaonyesha dosari katika
tabia yake – harmatia. Mara nyingi mhusika mkuu huwa amefikia hali
aliyonayo sasa kutokana na dosari. Mhusika mkuu hubadilika pale mambo yaanzapo kumwendea kombo, anapitia awamu ya perepeteia.
Licha ya mambo kumgeukia, anagundua kuwa ana dosari; kitu
alichotenda kimesababisha mabadiliko kutoka ya ufanisi na kuwa ya
kudidimia – anagnoris.
Mhusika mkuu anapaswa kukubali kosa lake na kamwe hafanyi ajizi
kwa kulikimbia janga linalomngojea (catastrophe). Janga linalotokea
husababisha mhusika kufa au wapenzi wake kufa. Mara kwa mara hata
ikiwa mhusika hafi, yanayompata ni mabaya zaidi ya kufa.
Awamu zote ni kumfanya mtazamaji kuondokana na hisia (catharsis)
ili awe mtu bora zaidi baada ya onyesho la tanzia10
.
ii) Tanzia ya Urasimi Mpya (Neo-classical Tragedy)
Wakati huu pia tabaka tawala limechangia katika kuifanya tanzia iwe
kama ilivyo. Tabaka hili ndilo lililomiliki sanaa hivyo liliingiza mawazo
yake katika tanzia.
Huu ulikuwa wakati wa utaifa kwa Waingereza hivyo mambo mengi
yaliyotokea nje ya taifa hili yaliachwa. Isitoshe, katika kudhamini
tamthiliya, Ufalme wa Uingereza ulikataza tamthiliya ya kugusia
mambo ya kidini na kitawala. Ufalme ulikuwa tayari kudhamini
tamthiliya kama chombo cha kuleta burudani tu.
Wakati huu kulikuwepo kwa mwamko wa kifikra uliojulikana kama
‘cartesian rationalism’ – ambao uliweka maanani sana tofauti kati ya
umbo la ndani na la nje – hususan kuhusu tabia ya binadamu11
.
Miungu na mashetani waliendelea kuwepo kwenye tanzia hizi na
walikuwa na uzito. Ila kutokana na mwamko wa fikra mpya
uliokuwepo watu walifanya uchunguzi wa kina kwanza ili kupambanua
kati ya miungu halisi na bandia.
Fikra hizi ambazo zilikuwa uzao wa tabaka tawala zilionekana kwenye
tanzia wakati huu. Mhusika mkuu aliendelea kuwa wa tabaka la juu.
Lugha iliendelea kuwa ya kishairi isipokuwa wakati mwingine watu wa
chini waliongea lugha ya kawaida. Huu ni ubaguzi ambao ulibagua kati
ya watazamaji wa kawaida na wale wa hali ya juu ambao walifuatilia
vizuri zaidi matukio ya jukwaani.
Mwakilishi mkuu wa wakati huu ni William Shakespeare (1564 – 1616)
ambaye licha ya kuona tanzia kuwa ni sababu ya uovu ambao mtu
humtendea mwingine, hakwenda mbali kuonyesha undani wa
mahusiano haya bali aliishia kwenye kuzingatia dhamira sana. Mara
10 Rejelea Baoal (1979) Ibid. 36 – 37 Kwa maelezo ya kina zaidi
11 Grierson, H. Cross Currents in English Literature of the Seventeenth Century. London:
Peregrine Books. Page 99 – 127.
8
nyingi mhusika wake kwenye tanzia alitatanishwa na dhamira yake
mwenyewe.
Mfano mzuri ni tanzia yake ya Hamlet12 ambayo mbali na kuonyesha
uovu utendekao katika jamii pia kuna mvutano wa dhamira kati ya
mhusika huyo huyo mmoja. Kazi zake nyingine ni kama vile Makbeth,
Juliasi Kaizari, Tufani na Mabepari wa Venisi. Izingatiwe kuwa
Shakespeare aliliandikia tabaka tawala hivyo katu hakuonyesha
mgongano wa kitabaka. Alionyesha mambo kuwa ni ya kudumu na
hayabadiliki.
iii) Tanzia ya Kisasa (Modern Tragedy)
Tanzia hii imechipuka kutokana na mabadiliko ya fikra na maisha
yaliyotokea Ulaya katika karne ya 18. Huu ni wakati ambao ubepari
ulianza kushamiri hasa kutokana na kuvumbuliwa kwa mashine
ziendazo kwa mvuke (steam engines). Wakati huu ulijulikana kama
Mapinduzi ya Viwanda (Industrial Revolution). Ni wakati ambao watu
wengi iliwabidi kwenda mijini kufanya kazi viwandani. Miji ikafurika na
hali mbovu za maisha zikajitokeza.
Hali hii ikawafanya wafanyakazi hawa wawe na ufahamu wa unyonyaji
uliokuwa ukiendelea. Msemo mashuhuri wa wakati huo, ‘watu wote
wameumbwa kuwa huru na sawa’ ulichangia kwa kiasi kikubwa katika
kujenga mawazo tofauti na yale ya urasimi mpya. Wanafalsafa
Auguste Comte na Charles Darwin walichangia kwa kiasi kikubwa
kutokana na kazi zao za ‘Positivism’13 na ‘Origin of species’
zilizoandikwa karne ya 18.
Wanafalsafa hawa walihamasisha watu kutumia sayansi kutumia
sayansi katika maswala ya jamii kutafuta chanzo cha matatizo na
kudhibiti matokeo yake. Walihamasisha watu kutafuta njia za kufanya
ili maarifa yote yahudumie matakwa ya wakati uliopo. Hivyo kila tawi
la maarifa likajihusisha katika mambo ya wakati huo.
Tanzia nayo ilienda sambamba na mabadiliko haya. Mungu au miungu
haikuwa tena na nafasi yoyote kwenye maisha ya binadamu. Yote
yaliyomsibu binadamu yalikuwa na chanzo chake katika maisha haya
haya yenye kufahamika na milango mitano ya maarifa/hisi/fahamu.
Rousseau anasimamia msimamo huu kwa kusema kuwa kiini cha uovu
hutokana na jamii na sio nje ya jamii.
Mhusika mkuu aliyekumbwa na janga alitoka katika ngazi yoyote ya
jamii. Mhusika huyu alisakamwa na: mtu mwingine, nafsi yake na
jamii.
12 Shakespeare, W. (1958) Hamlet. London: Penguin.
13 Pia Falsafa ya Umbile. Hii ni falsafa inayozingatia tu mambo yanayoonekana na kujulikana
vyema na wanadamu.
9
Lugha nayo ikabadilika kutoka ya ushairi hadi ya kawaida ili
kurahisisha mawasiliano. Iliunganisha kwa ufanisi zaidi mwigizaji na
hadhira yake. Licha ya lugha kuunganisha mwigizaji na mtazamaji,
bado kiini kikubwa cha tanzia kilibakia kuwa ‘Catharsis’14 kama katika
mikondo ya awali.
Ingawa mtazamaji alijitambulisha na mhusika mkuu kwa yale magumu
yanayompata, Steiner haoni kuangamia kwa mhusika mkuu kuwa ndio
mwisho bali kulitoa fundisho kwa jamii kuwa inaweza kubadilika na
hatimaye kupata mwisho mzuri. Huu mwisho mzuri ungepatikana
aidha kwa kubadilisha hali mbaya ya maisha na kuwa nzuri au kupata
mwisho mzuri kutokana na mawazo ya kidini ya maisha baada ya kifo.
Henrich Ibsen (1828 – 1906) ndiye aliyeashiria mwanzo wa tanzia ya
kisasa kuanzia 1870. Tanzia hizi zilionyesha jinsi misingi potovu ya
jamii ilivyoangusha watu. Katika tanzia yake ‘Ghosts’15 (Mizuka)
mwanamke anashurutishwa kukaa na mumewe ambaye hampendi.
Isitoshe, ni mwanaume ambaye kutokana na tabia yake ametengwa
na jamii. Mtoto wa kiume wanayemzaa anarithi kaswende kutoka kwa
babake. Mwisho wa tanzia kijana wa kiume anahehuka na mama mtu
anapata wenda wazimu. Matukio haya husababishwa kwa kwa sababu
jamii hushurutishwa kufuata maadili potovu.
Arthur Miller (1915 - ) katika tanzi yake ya ‘Kifo cha Mfanyabiashara’
(Death of a Salesman)16 iliyoandikwa 1949, anazungumzia mhusika
mkuu Willy Loman ambaye ni mfanya – biashara. Katika maisha, yeye
anataka apendwe, ajulikane na asifiwe. Anafahamu kuwa mambo yote
haya anaweza kuyapata ikiwa atapata mafanikio maishani.
Kwa Willy mafanikio ni utajiri na anaamini mtu hawezi kupendwa bila
kuwa na mafanikio. Willy anadhani watoto wake hawampendi kwa
sababu hajafaulu maishani. Watampenda tu kama atafanikiwa.
Anaamini kuwa mapenzi ni kitu cha kutafutwa au kununuliwa na
hakitolewi bure. Pia anawaeleza wanawake kuwa hawataheshimiwa
kama hawatakuwa na mali. Anagundua mtoto wake Biff anampenda
kwa dhati ingawa wote hawana mafanikio. Tendo hili linampa fununu
kuwa amekuwa akiamini imani potofu. Fununu inatokea mwisho wa
tanzia ambapo pia Willy anapata ajali ya gari.
Katika ‘A Doll’s House’17, mwandishi Ibsen anaonyesha jinsi mhusika
Nora anavyotaka kubadili maisha yake duni na magumu
14 Yaani ‘mtakaso hisia’, kutoa au kupoza hisia zilizochemka
15 Ibsen, H. (1965) Ghosts. London: Bard.
16 Miller, A. (1968) Death of a Salesman. Nairobi: East African Educational Publishers.
17 Ibsen, H. (1906) A Doll’s House: The Collected Works of Henrich Ibsen Volume VII. London:
Heinemann.
10
yanayosababishwa na mumewe. Nora anaamua kumwacha mumewe
na watoto ili aweze kuamua mambo yake mwenyewe.
A Doll’s House ni tanzia iliyoshambulia ndoa na maisha ya familia kuwa
chanzo cha hali ngumu kwa wahusika.
Hivyo kwa Steiner mhusika wa tanzia hii ya kisasa haangamii kabisa
kwa sababu majibu ya matatizo yake yapo na kama ni anguko ni
anguko la muda tu.
Tanzia za kisasa zina mielekeo tofauti hasa ukizingatia kuwa mawazo
ya binadamu hayana mipaka na watu sehemu mbali mbali hawabanwi
na mawazo na itikadi za aina moja tu.
iv) Tanzia ya Kikomunisti (Socialist Realism Tragedy)
Tanzia hizi zimetokana na mawazo ya Marx na Ukomunisti18 ya kutaka
kuleta jamii isiyo na matabaka duniani. Tanzia za aina hii ni za
matumaini juu ya ushindi wa ujamaa duniani na lazima ziongelee
kuhusu hilo tu. Ni mwiko kwa mhusika mkuu wa tamthiliya hizi
kushindwa kuutangaza ujamaa duniani. Ni tanzia ionyeshayo jinsi jamii
nzima inavyobadilika na kuwa ya kikomunisti. Mwisho wa tanzia hizi
hutakiwa kuwa mzuri kwa ushindi wa ujamaa.
Mawazo yaliyotawala tanzia hizi yalitokana na chama cha Ukomunisti
huko Urusi na ni fikra ambazo zililazimishwa kwa wanaotawaliwa hasa
ukichukulia kuwa jamii hiyo pia ililazimishwa kuwa ya mfumo wa
chama kimoja.
Matabaka ya wakati wa Kigiriki na wa Shakespeare hayatofautiani ya
kipindi hiki. Wananchi wa Urusi walilazimishwa kubugia mawazo
ambayo hawakuyapenda. Huu toka mwanzo ulikuwa ukandamizaji wa
haki za binadamu au uwepo wa uovu kama katika matabaka yote
yaliyotangulia. Wahakiki wa tamthiliya hii wanaposema tanzia haina
nafasi katika jamii yao ni kuwakoga wananchi kuwa wategemee
maisha yasiyowezekana19
.
Lugha iliyotumika ni ya kawaida ili kuleta maelewano bora kati ya
waigizaji na watazamaji. Kulikuwepo na mtengano maalumu kati ya
mwigizaji na mtazamaji.
Miungu haina nafasi kubwa kabisa kwenye tanzia hizi. Mhusika mkuu
wa tanzia hizi ambaye ni mhusika aliyejengwa kipropaganda kwa
manufaa ya siasa ya kikomunisti huitwa mhusika mkuu wa matumaini.
Naye ana sifa zifuatazo:
18 Marx, K. & Engels, F. (1969) The Communist Manifesto: Selected Works Volume I. Moscow:
Progress Publishers. Pages 98 - 137
19 Lunacharsky, A. (1973) On Literature and Art. Moscow: Progress Publishers.
11
o Yeye ni mfano kati ya mifano.
o Amefikia kiwango cha juu zaidi cha ubinadamu, hana ubinafsi.
o Hana makosa yoyote (kama anayo ni madogo sana kama
kukasirika hivi wakati fulani fulani). Na anaweza kuwa na
mambo yasiyofaa ya kujiosha akielekea kwenye kiwango cha juu
cha maisha lakini yasiwe kikwazo kwake.
o Lazima aielewe siasa barabara.
o Awe na akili.
o Awe na moyo wa ushupavu.
o Awe na uzalendo.
o Aheshimu wanawake.
o Awe tayari kujitoa mhanga.
o Ana msimamo mmmoja tu; nao ni kufikia kilele cha ukomunisti.
Hachanganyi weupe na weusi.
o Akipatwa na shida anajua ni lazima aikwepe ili afikie lengo lake.
Mfano mzuri wa tanzia hizi ni ‘The Measures Taken’20 ya Brecht. Katika
tanzia hii, mhusika mkuu – The Young Comrade – anajitoa muhanga ili
wenzake waweze kueneza ukomunisti nchini China. Brecht hakuwa
muasisi wa tanzia hizi isipokuwa alikubali kubadili jamii.
1.3.2Futuhi/Komedia (Comedy)
Futuhi au komedia ni utungo ambao unachekesha na kuchangamsha.
Tamthiliya ya aina hii inaweza kutusawiria picha yakini katika maisha
yetu kwa undani ikitumia dhihaka na kejeli kwa kuchekesha. Futuhi
huficha ukali wa masuto kadri inavyoendelea kutuburudisha. Futuhi
hulenga kurekebisha tabia inazozidhihaki au inazozicheka.
Kusema futuhi inafurahisha haina maana kuwa dhamira yake haina
uzito. Futuhi huzungumzia masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi
kwa njia ya kuchekesha. Futuhi huweza kuwa na sifa zinazotofautiana
– jambo ambalo hutumiwa kama kigezo cha kuainisha aina
mbalimbali. Lakini vyovyote iwavyo, futuhi hujikwepesha na masuala,
kutia hofu au kushtua. Athari ya futuhi (kuchekesha) hutokana na
matendo, mienendo ya wahusika na hitilafu au ila za kuingiliana kwa
kiusemi.
Futuhi huwa na viwango mbalimbali vya kuchekesha. Kwanza, kuna
kiwango hafifu (duni) ambacho huhusishwa na Futuhi ya Chini21. Kuna
20 Brecht, B. (1960) The Measures Taken. The Jewish.
21 Ucheshi unaopatikana katika futuhi ya aina hii ni rahisi kutambulikana na aghalabu waigizaji
hutenda vitendo vya kuchekesha vilivyo wazi.
12
baadhi ya kazi ambapo kiwango cha kuchekesha huwa kigumu
kutambulikana na huhitaji utambuzi mpevu. Hii ni sifa ya aina ya
futuhi iitwayo Futuhi ya Juu22. Aina zingine ni pamoja na: Futuhi ya
Kikanivali, Futuhi ya Kitashtiti, Futuhi ya Maadili, Futuhi ya Mawazo,
Futuhi ya Ucheshi na Futuhi Zimbwe.
Mifano mizuri ya futuhi ni ‘Aliyeonja Pepo’ (Topan, F.), ‘Usaliti Mjini’
(Imbuga, F.), Twelfth Night (Shakespeare, W.), Importance of Being
Earnest (Wilde Oscar), Mkaguzi Mkuu wa Serikali (Gogol, Nikolai), The
Lion and the Jewel (Soyinka, W.) na ‘Masaibu ya Ndugu Jero’ (Soyinka,
W.).
1.3.3Melodrama
Katika zama za urasimi, aina hii ilitumiwa kuelezea aina ya drama au
tamthiliya iliyokuwa na matumizi mengi ya uimbaji au nyimbo (melos).
Kwa hiyo, melodrama ni dhana inayotumiwa kuelezea aina ya
tamthiliya ambayo imetawaliwa na uimbaji wa nyimbo.
Melodrama inafanana sana na tanzia ingawa mara nyingi nguli wa
melodrama humalizika na ushindi, matokeo yake yanasisimua sana na
mwendo wa msuko wake huwa ni wa haraka haraka zaidi. Wahusika
wake huvutia na kufurahisha lakini hawana sifa za kishujaa.
Dhamira ya melodrama huzungukia mvutano kati ya wema na uovu au
ubaya. Miishio ya tamthiliya hizi haina sifa ya mtakasohisia kama ilivyo
na tanzia bali huwa ni aina ya ushindi wa mhusika mwema. Mfano
mzuri ni ‘The Begger’s Opera’ iliyotungwa na mwanatamthiliya wa
Kiingereza John Gay kunako 1728.
1.3.4Kichekesho (Farce)
Kichekesho ni aina ya tamthiliya ambayo huwa na uwezo wa
kusababisha kicheko kingi kutokana na mbinu za kifutuhi ya chini
kama ucheshi, hali zisizokuwa za kawaida au wahusika wasio wa
kawaida kama vile wahusika wa kiume huweza kuvaa mavazi ya
wahusika wa kike na wale wa kike kuyavaa mavazi ya kiume, visa
vingi vya mapenzi ya kuchekesha, mikimbizano jukwaani, matukio ya
kiajabu, kuchezea maneno, nk.
Kichekesho huwa na wahusika, matendo, mazingira na vitushi vya
kuchekesha kwa jinsi vilivyotiliwa chumvi. Ingawa Kichekesho
kinahusiana na Futuhi, kinatofautiana nayo kutokana na sifa yake ya
kudhamiria tu kuibusha kicheko na kutumbuiza. Futuhi pia hutumbuiza
lakini zaidi ya hivyo inalenga kurekebisha tabia inazozicheka.
‘Charley’s Aunt’ ya Brandon Thomas ni mfano wa kichekesho maarufu.
22 Ucheshi wake huhitaji ung’amuzi au akili kuugundua. Kwa kawaida ucheshi wa futuhi ya juu
hufumbatwa katika matumizi ya lugha na ni nadra sana kutegemea matendo au miondoko ya
waigizaji.
13
Kichekesho hiki kilitolewa kwa mara ya kwanza1892. Vichekesho vingi
vya Kiswahili havichapishwi kama vitabu.
1.3.5Tanzia–ramsa/Tanzia-futuhi (Tragicomedy)
Tanzia-ramsa ni aina ya tamthiliya ambayo huonyesha mabadiliko ya
aina fulani yanayogeuza mwelekeo wa matukio ya kitanzia na
kuufanya kuwa tofauti au wa kufurahisha. Hali hii inaweza kupatikana
kwa kuwepo kwa hasidi au mui anayetubu na kuyajutia makosa au
msimamo wake au kuwepo kwa mandhari ya kiulimbwende.
Kimsingi, tanzia-ramsa ni tanzia inayoishia kwa furaha. Kinyume chake
ni Futuhi Zimbwe23. Dhana hii inaakisi kwa kiasi kikubwa baadhi ya
mitazamo ya kidhanaishi ya fasihi ambapo ushujaa na tanzia
havijitokezi katika hali ya kawaida kama vilivyozoeleka.
Hali hii inadhihirika katika tamthiliya kama vile ‘The Cherry Orchard’
(Anton Chekhov, 1904), ‘The Winter’s Tale’ (William Shakespeare,
1611). Utanzu huu wa tamthiliya sio maarufu miongoni mwa
wanatamthiliya wa Kiafrika.
1.3.6Tamthiliya ya Kihistoria (Historical Play)
Hii ni tamthiliya inayojengwa kutokana na mhusika au matukio ya
kihistoria. Mifano ni ‘Kinjeketile’ (Hussein, E.), ‘Mkwava wa Uhehe’
(Mulokozi, M.), ‘Mzalendo Kimathi’ (Ngugi, T) na ‘Mnara Wawaka Moto’
(Rocha Chimerah).
1.3.7Tamthiliya Tatizo (Problem Play)
Tamthiliya hizi pia huitwa Tamthiliya Tasnifu au Tamthiliya Tanzo.
Utanzu huu wa tamthiliya huzungumzia suala fulani katika jamii. Ni
tamthiliya inayojenga dhamira yake juu ya tatizo mahsusi la kijamii.
Dhamira hiyo hujengwa kupitia kwa mhusika mkuu ambaye
anakabiliana na tatizo ambalo ni kielelezo cha mazingira yake ya
kijamii. Katika tamthiliya ya Kithaka wa Mberia, ‘Natala’, kwa mfano,
tatizo la kudunishwa kwa mwanamke, ambalo mhusika mkuu (Natala)
anakabiliana nalo ni kiwakilishi cha hali ya mwanamke katika jamii
nyingi za Kiafrika. Tamthiliya hii inashughulikia suala la mwanamke
katika jamii inayoendelea kutawaliwa na itikadi inayopendelea
wanaume na inayozingatia desturi za kumrithi mke baada ya kifo cha
mumewe.
Mifano mingine tamthiliya tatizo ni ‘Nguzo Mama’ na ‘Lina Ubani’
(Muhando, P.), ‘Kifo Kisimani’ (Mberia, K.),‘Mashetani’ (Hussein, E.) na
‘Mama Ee’ (Mwachofi, K.). Sio lazima mtunzi wa tamthiliya tatizo atoe
23 Aina ya Tanzia-ramsa ambayo huisha kwa namna ya kukatisha tamaa au kusikitisha.
14
suluhisho la tatizo analolishughulikia. Hata hivyo, baadhi ya watunzi
wa kazi za aina hii hupendekeza soluhisho fulani.
1.3.8Tamthiliya ya Kibwege (Absurd Drama)
Hizi ni kazi za sanaa ambazo hupuuza kaida zinazotarajiwa za utunzi
wa tamthiliya. Ni tamthiliya ambazo huelekea kudokeza kuwa maisha
yana uwazi usiokuwa na maana au hayana maana. Waandishi
wanaoakisi mawazo ya aina hii wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na
udhanaishi.
Wahusika wanaopatikana katika tamthiliya za aina hii huweza
kujitokeza katika sura mbalimbali, kubadilisha hata jinsia, masuala ya
maonyesho hayatiliwi maanani, mfuatano wa kiwakati unapuuzwa na
mpaka uliopo kati ya uhalisi na utohalisi huvunjwa.
Katika fasihi ya Ulaya waandishi wanaohusishwa na mtazamo huu ni
Samuel Beckett (Waiting for Godot, 1956 na Endgame, 1959) na
Eugene Ionescu (The Bald Prima Donna, The Lesson, The Chairs na
Rhinocerous). Katika fasihi ya Kiswahili sifa za aina hii zinajitokeza
katika tamthiliya ya ‘Amezidi’ (Mohamed, 1995) na ‘Upotovu’ (Njiru
Kimunyi, 2000).
1.4 Dhima za Tamthiya
Husababisha mawasiliano ya kisanii kati ya makundi mawili ya watu –
waigizaji na watazamaji (hadhira) yatokee.
Huburudisha – tamthiliya inapoonyeshwa jukwaani hutoa burudani.
Hufundisha na hata huhamasisha. Katika tamthiliya huwepo adili
(funzo) na ujumbe ambao unawaelekeza, kuwaadibu, kuwaonya na
kuwaongoza kwenye matarajio ya jamii husika. Taasisi nyingi
zimekumbatia tamthiliya kufundishia malengo yao na pia kwa
propaganda.
Tamthiliya ina nafasi kubwa kukuza lugha ya kiswahili. Lugha ya
tamthiliya ni lugha maalum ambayo hueleza migongano kwa
muhtasari na hii huifanya tamthiliya kuwa mahala pafaapo kwa
kujifunza utaalam huu.
Mapato: kitabu kinapouzwa mwandishi hupata kipato. Tamthliya
inapoonyeshwa jukwaani, viingilio humpatia msanii kipato. Sehemu
nyingi siku hizi wanatamthiliya hupata mshahara. Wasomi na
waandishi wa fani ya tamthiliya huajiriwa katika sehemu nyingi kama
mashuleni, vyuoni, taasisini, redioni na kwenye studio za televisheni.
Tamthiliya ina nafasi ya kipekee katika kuhifadhi zile sanaa za
maonyesho za asili ambazo zimepitwa na wakati na zile ambazo bado
zinatumika kwa kuzitia katika fani ya tamthiliya. Hii licha ya kuzifanya
15
tamthiliya zetu ziwe na upekee wa kitanzania bali pia zitautangaza
utamaduni huu.
Lengo la serikali likiwa ni kumfanya kila mwananchi ajue kusoma na
kuandika, tamthiliya ina nafasi kubwa huko mbele kwani kipengele cha
usomi ambacho sasa ni kikwazo kikubwa kitakuwa kimeondoka.
Tamthiliya zinaweza kutumiwa kufundishia baadhi ya masomo ya shule
za msingi.
1.5 Maswali ya Marudio
1. Tamthiliya ni nini? Eleza kwa kutoa mifano mwafaka.
2. Fafanua sifa zozote SITA zinazoutambulisha utanzu wa tamthiliya.
3. Eleza dhima ya tamthiliya katika jamii.
4. Eleza kwa tafsili dhana zifuatazo:
a) Sanaa za Maonyesho
b) Drama za Kijadi
c) Drama
5. Toa maelezo mafupi kuhusu tanzu za tamthiliya zifuatazo:
a) Futuhi
b) Tamthiliya ya Kibwege
c) Melodrama
d) Kichekesho
e) Tanzia-ramsa
f) Tamthiliya ya Kihistoria
g) Tamthiliya Tatizo