NADHARIYA YA TAMTHILIYA NA DRAMA

NADHARIYA YA TAMTHILIYA NA DRAMA

NADHARIYA YA TAMTHILIYA NA DARAMA
Dhanna za tamthiliya na drama hukanganya sana kwa sababu zimeingiliana sana. Ni kutokana na kuingiliana huku baadhi ya wataalamu wamekuwa wakiifafanua dhanna ya tamthiliya kama drama na kinyume chake. Hivyo, katika muhadhara huu tutajikita katika kufafanua dhanna hizi kama dhanna tofauti.
Dhanna ya Tamthiliya
Tamthiliya imefafanuliwa na wataalamu mbalimbali. Miongoni mwa fafanuzi kuhusu maana ya tamthiliya ni hizi zifuatazo:
Mulokozi (1996:188):
Tamthiliya au drama ni fani ya fasihi iliyokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira Fulani. Hivyo, kwa lugha ya kawaida, tamthiliya huitwa mchezo wa kuigiza….Istilahi tamthiliya inatokana na neno mithali ambalo lina maana ya mfano au ishara ya kitu. Hivyo, katika tamthiliya kitu kimoja humithilishwa au huwakilishwa na kitu kingine.
Katika ufafanuzi huo swali tunalopaswa kujiuliza ni je, tamthiliya ni drama na kinyume chake?
Wamitila (2003:217) anasema:
Tamthiliya ni kazi ya kidrama na ya kimaongezi ambayo huigizwa mbele ya hadhira au kazi iliyoandikwa kusomwa, kimuundo, tamthiliya hugawika katika matendo na maonesho, na mazungumzo huchukua sehemu kubwa katika uwasilishaji wake na maudhui.
Katika maelezo hayo ni vigumu kubaini mpaka kati ya tamthiliya na drama. Mathalani, tunaweza kujiuliza ni wakati gani tamthiliya inakuwa drama na ni wakati gani inaendelea kuwa tamthiliya? Hata hivyo, Wamitila (2010)anatofautisha dhanna hizi kwa kueleza kuwa tamthiliya haiweki msisitizo mkubwa kwenye suala la uwasilishaji wake jukwaani.
Naye Penina Mlama (Wafula, 1999:2) anaeleza:
Tamthiliya ni ule utungo ambao unaweza kuwa umeandikwa au haukuandikwa, ambao unaliweka wazo linalotaka kuwasilishwa katika umbo la tukio la kuliwezesha kutendeka mbele ya hadhira.
Kimsingi katika ufafanuzi huu inaonekana wazi kuwa tamthiliya ni utungo ambao unaweza kuwa umeandikwa au haukuandikwa. Na kwamba utungo huo huwa na matukio ambayo yanauwezesha kutendeka mbele ya hadhira. Kutokana na sifa hii ya kuweza kutendeka mbele ya hadhira, Mulokozi (1996:188) anaiweka tamthiliya katika sanaa za maonesho, sanaa ambazo Muhando na Balisidya (1976) wanasema ni kitendo chochote chenye sifa nne ambazo ni : Mchezo, mchezaji, uwanja wa kuchezea na watazamaji.
Kutokana na maelezo hayo tunaweza kusema, tamthiliya ni andiko la kiuigizaji linalotoa simulio kwa kuonesha maneno na matendo.
Dhanna ya Drama
Drama, kama ilivyo tamthiliya imefafanuliwa na wataalamu mbalimbali. Miongoni mwa fafanuzi kuhusu drama ni hizi zifuatazo:
Wamitila (2003) anaifafanua drama kama aina ya utanzu wa fasihi ambayo kimsingi hudhamiriwa kuigizwa mbele ya hadhira. Anaendelea kueleza kuwa drama inaweza kuwa imeandikwa kama tamthiliya au isiandikwe.
Kimsingi drama ni utanzu wa fasihi ambao unajidhihirisha katika utendaji. Utanzu huu umebuniwa kwa ajili ya thieta kwa sababu wahusika hupewa majukumu ambayo huyaigiza katika jukwaa. Drama ni mabadiliko, ubunifu na usawiri wa uhalisi katika jukwaa (Iwuchukwu, 2008). Kwa hivyo, msingi mkuu wa drama ni tendo. Hoja hii inaungwa mkono na Mineke Schipper katika makala yake ya Origin and Forms of Drama in African Context anapoonesha asili ya neno drama. Anasema:
Originally the ancient Greek word drama means, “action.” This term is said to be used for the first time in connection with what we call drama, about 560 B.C by Greek Thepspis when he enriched his religious singing and dancing choirs with costumed masked person who expressed a part of action in meaningful words and gestures. Since that time drama has been the indication of that art which represents human event in presence of more or less involved audience and which is focused on man.
Hoja hii pia inaungwa mkono na Aristotle ambaye anaifafanua drama kama uigaji wa kitendo. Katika maana hii Aristotle anaihusisha drama na msukumo wa kuiga uliomo kwa wanadamu kwa mfano, watoto wanapocheza baba na mama katika michezo ya watoto huwa wanaiga yale wanayoyaona katika maisha yao ya kila siku. Hii ina maana kuwa uigaji ni sehemu ya maisha.
Hata hivyo, Betolt Bretcht anasisitiza kuwa, drama si uigaji wa kitendo pekee bali pia ni chombo cha ufafanuzi wa hali za kijamii, si burudani pekee bali pia ni chombo cha mabadiliko ya kisiasa na kijamii.
Kutokana na maelezo hayo tunapaswa kufahamu kuwa, kitendo kinakuwa drama iwapo kitendo hicho ni mwigo wa kitendo kilichotangulia. Kwa mfano, simulizi ya muwindaji ambaye anakwenda mwituni na kuua swala na kasha kumpeleka maskani yake hata kama akiwa anacheza si drama. Simulizi hiyo hiyo itakuwa drama kama itatendwa upya mbele ya hadhira ili kuburudisha au kuelimisha. Kijana anayetaka kuwa mwindaji anaweza kujifunza kupitia uwasilishaji huo.
Drama za Kijadi
Kumekuwa na madai kutoka kwa wanazuoni wa Kimagharibi kuwa kabla ya ujio wa wageni (wakoloni), Afrika haikuwa na drama. Madai haya yanaweza kuchukuliwa kuwa ni sahihi kwa kuwa istilahi “drama” ni ngeni. Hata hivyo, madai haya yanapingwa na baadhi ya wanazuoni, miongoni mwao ni Mineke Schipperi katika makala yake ya Origin and Forms of Drama in African Context anaposema:
It is of course not correct to use Western drama, in the way it has developed during last centuries, as criterion to decide whether drama exists in other cultures or not! If for instance, language does not dominate over all the other elements in the performance of a community this does not mean that there exists no drama at all in this community, as it has sometimes been assumed in Western countries. One should always take ito account the norms of the society itself with respect to the forms of drama it appreciates and performs.
Kimsingi jamii ya asili katika Afrika, Tanzania ikiwamo, jamii ambayo utamaduni wake ulikuwa haujaingiliwa na utamaduni wan chi za kigeni, ilikuwa na sanaa za maonesho (drama) ambazo ziligawanyika katika makundi. Muhando na Balisidya (1976) wanataja na kufafanua makundi hayo kama ifuatavyo:
·      Sherehe :zinahusu kuingizwa kwa mwanajamii kwenye kundi la watu wa aina Fulani kutoka katika kundi la watu wa aina ingine. Kwa mfano, jando na unyago, kutoa jina, kuota meno, kusimika viongozi, n.k
Sherehe hizi ziliambatana na madaraka mapya yaliyomkabili mwanajamii katika kuingia kundi jipya. Sherehe hizi, hasa huwa ni kukabidhiwa madaraka ambayo huwekwa katika umbo la vitendo, ukapewa uzuri wa kisanaa ili uweze kudhihirika kwa mkazo zaidi.
·      Ngoma: inaweza kuwa na maana ya chombo, sherehe au uchezeshaji wa viungo vya mwili. Ngoma hizi ni zile ambazo hazikufungwa katika mfumo wa sherehe. Zina malengo ya kuburudisha, kwa hiyo huchezwa wakati wowote wa furaha.
·      Masimulizi ya Hadithi: Katika usimuliaji wa hadithi kuna vipengele vya drama/sanaa za maonesho. Kwa upande mmoja, kuna msimuliaji ambaye ni mshairi, muigizaji, mwimbaji na mwanamuziki.
Ø Ni mshairi kwa sababu husanifu upya matini ya kijadi kwa kutumia uwezo wake, akili yake na ujuzi wake wa fasihi ya jamii husika.
Ø Ni mwimbaji kwa sababu katika sehemu kadhaa zasimulizi yake huimba
Ø Ni mwanamuziki kwa sababu wakati mwingine hutumia vyombo vya muziki k.v. ngoma
Ø Ni muigizaji kwa sababu hutimiza majukumu mbalimbali kwa kutumia ubadilishaji wa sauti, mikono, macho na viungo vingine vya mwili ili kutia mvuto katika usemi wake
Ø Kwa upande mwingine ni drama/sanaa za maonesho kwa sababu hadhira hushirikishwa katika hatua mbalimbali.
·      Kusalia miungu: Hii hutokea panapokuwa na hali ya kuikumbuka mizimu. Katika jamii mbalimbali watu walielekeza kwa miungu mbalimbali, matatizo ambayo wao kwa nguvu zao za kibinadamu yaliwashinda. Hivyo, kusalia miungu kulihusu jamii kuiomba iwaondolee matatizo yao. Na hii hasa ndiyo ilikuwa dhanna iliyotendeka. Mitindo ya kusalia miungu ilitofautiana.
·      Majigambo:Masimulizi ya kujigamba kwa mtu kuhusu mambo ya kishujaa aliyopata kuyatenda maishani mwake. Husimuliwa katika lugha ya kishairi na masimulizi yake huambatanishwa na vitendo vya mjigambi mwenyewe. Mjigambi huyu, mara nyingi akiwa amevalia maleba na akiwa amebeba zana, hutumia vitendo vingi kudhihirisha vile alivyofanya mambo haya ya kishujaa. Mara nyingi hufanyika wakati wa sherehe.

VIJENZI VYA TAMTHILIYA YA KI-ARISTOTLE
Waingereza ndio wa kwanza kuleta tamthiliya. Kazi za William Shakespeare za Julias Kaisari na Mabepari wa Veniszilitumia vigezo vya Ki-Aristotle (Kimagharibi) ambavyo vina sifa kuu nne.
Ø Simulio-lazima kuwe na kisa/mzozo baina ya pande mbili.
Ø Vitendo-hapa kuna matendo na maonesho
Ø Waigizaji-wahusika
Ø Dialojia-mazungumzo ya wahusika (majibizano)
MUUNDO WA TAMTHILIYA ZA MAGHARIBI
Tamthiliya yoyote yenye kufuata muundo wa Ki-Aristotle husukwa katika mgogoro unaochukua muundo ufuatao.
                                                  C                                        
                                
                                  B                          D



 





                                     A                                                 E   
SEHEMU A: Ni mwanzo wa mgogoro katika tamthiliya
SEHEMU B: Ni kukua kwa mgogoro
SEHEMU C: Ni kilele cha mgogoro
SEHEMU D: Ni kushuka kwa mgogoro
SEHEMU E: Ni suluhisho la mgogoro
AINA ZA TAMTHILIYA
Tamthiliya, kama ilivyo kwa tanzu nyingine za fasihi, imegawanyika katika vitanzu au aina kadhaa. Hivyo, katika kipengele hiki tutaangalia aina za tamthiliya.
1.   Tanzaia/Tragedy
Hii ni tamthiliya yenye huzuni inayogusa hisia za watazamaji/wasomaji kiasi cha kuogopesha na kumwonea huruma mhusika mkuu ambaye hupatwa na janga (Semzaba, 1997). Mhusika mkuu huwa ni maarufu, mbabe au shujaa atokaye tabaka la juu. Mtu wa nasaba bora na ambaye huwa anajaribu kubadilisha hali yake na ya jamii inayomzunguka. Katika hatua yake hiyo hujikuta amefanya kosa au amefanya uamuzi usio sahihi, uamuzi ambao husababisha anguko lake.
Misingi ya Utokeaji Wake
·      Iamshe hisia za woga na huruma miongoni mwa hadhira
·      Shujaa lazima awe mtu mwema, sura nzuri, umbo zuri ili yanayomtokea yasitarajiwe
·      Watu huonesha kuumia, kusikitika, n.k kadri mtu anavyoonekana mwema au mzuri wa umbo
·      Anguko la shujaa huja kutokana na uamuzi wake au kosa lake mwenyewe
·      Katika tanzia ya kirasimi, shujaa hutoka katika nasaba bora.
Etimolojia ya neno Tragedy
Neno hili linatokana na maneno mawili ya Kiyunani, yaani Tragos lenye maana ya mbuzi na aeidein lenye maana ya kuimba.
Kuna namna tatu za kueleza chimbuko hili na suala la mbuzi na huzini.
·      Zawadi ya mbuzi ilikuwa ikitolewa kama tuzo kwa mshindi wa nyimbo za kikorasi
·      Mbuzi alitolewa kama kafara kabla wimbo wa kikorasi kuimbwa
·      Kutokana na hoja ya pili, hoja ya tatu inaibuka kuwa: waimbaji na wachezaji katika miviga ya kidithramb walivalia ngozi za mbuzi na wakaonekana kama mbuzi wa kafara na mmoja wao alifanya uigizaji bubu akionesha mateso na kufa na kuibuka upya kwa shujaa. Kutokana na kuuawa kwa mbuzi, watu wanakuwa na huruma, hivyo wanavaa ushujaa na kuvaa vazi la mbuzi na kufa kama mbuzi na kuibuka na ushindi.
Hoja ya pili inaweza kuwa na mashiko zaidi kwani ilihusisha kifo cha mnyama kama kafara au mwigo wake ambao ulileta huzuni ya kifo cha shujaa.
Katika Poetics, Aristotle anaandika kuwa tanzia ilikuwepo kutokana na ufaraguzi uliofanywa na viongozi wa miviga ya kidithramb ambayo ilihusisha nyimbo na ngoma za kumtukuza Dionizius- mungu wa mvinyo na rutuba/uzazi.
Lakini katika Poetics ndipo Aristotle anapotoa ufafanuzi wa tanzia kama ijulikanavyo leo, kuwa ni:
·      Utungo wa kisanaa ambao unawasilisha anguko la mtu shujaa au mwema kutokana na kosa la kufisha alilolitenda au kutokana na uamuzi wake mbaya.
·      Ni mambo ambayo yanamletea mateso na uchungu mhusika shujaa na katika kuanguka huko, hadhira inashikwa na woga na kumwonea huruma shujaa.
Kadri jamii ilivyoendelea ndivyo sanaa ilivyoanza kuwekewa sifa bainifu na hata sharia. Na kwa hiyo, hata ufafanuzi wake uliegemea katika kuonesha sifa maalumu zinazofanya utungo uwe wa kitanzia. Kwa mkabala huu, Aristotle katika Poetics anasema:
·      Tanzia ni mwigo wa tukio (mimesis) kwa mujibu wa sharia za uwezekano au ulazima
·      Na kwamba njia ya kutolea tanzia ni drama, sio nathari (usimulizi) kwa kuwa drama inaonesha kuliko kueleza.
·      Ni tukio la kisanii la kifalsafa zaidi na la kiwango cha juu kabisa kuliko historia. Historia hueleza kile kilichotokea. Tanzia huonesha kile kinachoweza kutokea ikiegemea katika sharia ya uwezekano na ulazima (the law of probability and necessity)
·      Tanzia ni mwigo wa tukio la dhati, lenye ukubwa na ubora wa kisa kinachojitosheleza, wenye kubeba lugha na umbo maalumu lenye misingi sita ambayo ndiyo inayoelezea ubora wake.
Maumbo hayo ni: (ploti,wahusika,uneni,wazo, shani na mahadhi)
Ø Ploti:
·      Huu ni msingi mkuu unaohusu mpangilio wa matukio yanayojenga hadithi
·      Sio hadithi yenyewe, bali ni jinsi mfumo wake ulivyo, jinsi hadithi inavyoelezwa ilivyosukwa. Muundo wake ambao hupaswa kuwa na mwanzo, kati na mwisho.
·      Ni lazima ijitosheleze ikiwa na mshikamano wa matendo
·      Ni lazima iwe ya kiwango Fulani maalumu, kwa ubora wake na ujazo wake. Sio fupi, iwe ya kiulimwengu. Tukio linaloweza kutokea popote.
·      Kuwe na mabadiliko katika bahati na mageuko ya nia – perpeteia. Nia inageuzwa na kutaka kurudishwa katika hali ilivyokuwa.
Ø Wahusika
·      Wahusika ndio hutengeneza na kuunga mkono msuko wa matukio
·      Jinsi wao wenyewe wanavyojituma wakionesha uhusika wao na kuleta athari kwa hadhira
·      Mhusika shujaa awe ni mtu maarufu ili mabadiliko ya bahati yake yakitokea (toka hali nzuri kuwa mbaya) yaweze kuleta athari ya huruma.
·      Anguko la shujaa huletwa na kosa analolitenda, yaani hamartia. Kosa la kufisha la kutesa na kutia uchungu.
·      Anguko hili hutokea sio kwa sababu shujaa ni mkosaji, au ana dhambi, bali kwa kutojua kiasi cha kutosha. Ni matokeo ambayo hayana budi kuwa kutokana na sharia ya uwezekano. Kwa mfano kisa cha  Edipode katika tamthiliya ya  Mfalme Edipode  kilichohusu ndoto iliyoanza na baba yake kuwa atapata mtoto wa kiume ambaye atamuua baba yake na kumuoa mama yake na hatimaye kuleta laana katika jamii nzima.
·      Katika kutapatapa, peripeteia inatokeza anguko zaidi. Ili kupata peripeteia, ni lazima jambo Fulani liachwe kabisa na kugeukia lile la awali, yaani kubadili nia kabisa.

Ø Uneni:
·    Ni namna maneno yanavyosemwa na kuunda maana
·    Uneni lazima uwe ni sahihi katika muktadha ule na kwa jinsi unavyotolewa kuhusiana na anavyoutoa, ploti na tukio la kitanzu.
·    Uneni unaotumia sitiari na tamathali nyinginezo ni bora zaidi.
Ø Wazo
·    Wazo kuu ni lipi?
·    Limefikiriwa kabla ya kusemwa?
·    Ni wazo linaloonekana au la
Aristotle anasema mwanadamu anayetoka tabaka la juu ndiye anayeweza kuwa na hilo wazo au pia anaweza asiwe nalo.
Ø Mahadhi
·    Ni wimbo kama alivyotumia Shakespearekatika kazi zake ambapo anaishia na wimbo, tofauti na kazi za Kiswahili ambazo zinaanza na wimbo kwa mfano katika Lina Ubani, Penina Muhando ameanza na wimbo wa bibi mwanzoni. Lakini pia katika tamthiliya ya Kilio Chetu watunzi wameishia na wimbo. Wimbo una dhima ya kuliwaza na kupoza machungu.
Ø Shani
·    Ni kule kuguswa kwa namna Fulani na wimbo. Ni ule utokeaji unaogusa mtu akawa na hisia na msisimko. Aristotle anasema lazima tanzia iwe na shani.

Istilahi katika Tanzia
            Peripeteia
·    Ni neno la Kiyunani ambapo mtu na kwa muktadha wetu, mhusika katika tamthiliya hubadili nia iliyopaswa kuwa njema na kurudisha kinyumenyume dhamiri iliyokuwa iwe na matokeo mazuri.
·    Mhusika hufanya tukio au kuchukua hatua ambayo humtoa katika usalama na kumwingiza matatani. Kwa mfano, unapokuwa na nia ya kwenda kumsalimu rafiki yako, halafu ghafla unabadili nia na kwenda kwa mchumba wako. Balaa unalolipata kule kwa mchumba wako linatokana na wewe kubadili nia yako ya awali ya kwenda kwa rafiki yako. Na hii ndiyo Peripeteia.
             Anagnorsis
·    Dhanna nyingine inayoenda sambamba na Peripeteia ni Anagnorsis. Balaa ya mhusika mkuu kubadili nia yake ya awali na kuamua kwenda upande wa pili au kuamua kufanya tukio jingine ambalo bila yeye kujua litamwingiza matatani, inafikia wakati sasa anatambua ah!! Nimefanya uamuzi ambao sio sahihi. Huko kugundua ndiyo Anagnorsis yaani tukio la mwanzo la kupata ufahamu.
·    Mhusika mkuu hutambua kuwa amejiingiza matatani kutokana na hatua moja au nyingine. Kwa mfano, unapomwacha mchumba wako mzuri, mwenye mapenzi ya dhati na kuamua kuolewa na jibaba lenye pesa zake kwa kudanganywa. Pale unapogundua oh! Kumbe huyu ni mume wa mtu….. hiyo ndiyo Anagnorsis.
·    Kwa mfano katika Mashetani, baada ya binadamu kumuua shetani anaanza kujiuliza maswali fulani ya kujuta na ansema laity angefuata ule uamuzi wake wa mwanzo.
·    Kwa hiyo Peripeteia unabadili nia na kuingia upande wa pili, na katika upande wa pili unagundua umekosea (anagnorsis)
           Hamartia
·    Baada ya kubadili nia (Peripeteia) na kugundua kuwa amekosea (anagnorsis), mhusika mkuu hufanya kosa fulani na kosa hilo ndio Hamartia.
·    Mhusika hukosea sio kutokana na kosa la kimaadili, bali zaidi kosa la kiutendaji au kiufundi, yaani mtu kulenga vibaya shabaha na kupiga sehemu tofauti na kuzua balaa.
·    Kwa mfano unapotaka kumuua nyoka, badala ya kumpiga kichwa unampiga mkia au unampiga kidogo. Matokeo yake atakugonga wewe.
·    Kosa la namna hii hujutiwa sana na mhusika mkuu kwa sababu huwa ni kosa la kiuamuzi, dhambi au matendo maovu na kosa hili ndilo husababisha anguko au kifo cha mhusika mkuu.
·    Kwa mfano Mfalme Edipode anapogundua kuwa amemuua baba yake na kumuoa mama yake anaamua kujitoboa macho.
            Katharsis (Utakaso)
·      Ili mtu ajiondoe katika hamartia hupaswa kujitakasa na kujitakasa ni kwa kihisia. Tukio hili hujulikana kama Katharsis.
·      Ni tukio au hali ambapo hisia za hadhira au mhusika hubadilika kabisa kutoka katika hisia za masikitiko, huzuni, majonzi au furaha kuu na kuwa kinyume chake.
·      Kwa mfano katika Mashetani, mwisho kabisa Juma anakataa kubadilisha nafasi yake na kuwa binadamu na Kitaru anasikitika sana kuwa alidhulumiwa sana kwa kucheza nafasi ya binadamu, na alitaka kujitakasa kwa kucheza nafasi ya shetani na yeye, lakini bahati mbaya Juma alikataa.
           Hubris
·      Ni matukio au matendo ya kujitapa kupita kiasi au kupindukia na kuonesha kuwa anayejitapa ametia chumvi mno hata kukiuka uhalisia ulivyo. Kujitapa huwa zaidi kuelekeza kukashifu au kudharau miungu au Mungu.
·      Hii hasa huwapata watu wenye uwezo fulani (wanasayansi,wasomi, n.k) au wenye vyeo na mamlaka.
·      Pale wanapokosa unyenyekevu na kujiona bila wao hakuna linaloweza kufanyika.
·      Kutokana na hali hii, hubris huonekana kuwa kama dhambi maana huvuka mipaka ya hali ya kawaida. Kutokana na kutapa huko, husababisha anguko na mateso badaye.
·      Kwa mfano katika Mashetani uk. 9, wako wapi waliokuwa wakijitaoa? Binadamu anacheka hadi kicheko kinamlevya, nah ii ni baada ya kudhani kamuua shetani kumbe wala hakuwa amemuua.
·      Hubris inahusishwa na miungu na kujitapa huku baadaye mhusika huyo lazima apate matatizo.
·      Kujitapa huku kiasi wakati mwingine huwa ni kwa sababu anayejitapa huwa hana uelewa wa kutosha au pengine ni kujisikia kulikopita mipaka.
         Nemesis
·      Kutokana na hali hii, anayesemwa ana hubris hujikuta uso kwa uso na Nemesis yaani kupata kilichostahiki kwa uwiano, kiwe kizuri au kibaya.
·      Nimesis alikuwa malaika wa Kigiriki na alikuwa akiongeza na kupunguza mambo mbalimbali ikiwa hali ni wingi kupita kiasi, hupunguza na ikiwa ni kidogo mno huongeza. Kama ulikuwa ukijitapa kwa sababu ya uwezo wako mkubwa basi unapunguzwa.
·      Kwa mfano huko Marekani, kupigwa kwa Pentagon, Marekani ilikuwa ikijitapa sana hadi ikakufuru kwamba hakuna vita iliwahi fanyika nchini humo. Baada ya pigo hilo Marekani ikaweka uwiano, yaani kwenye uwiano sawa nan chi zingine (ikatoka kwenye kujisifu kuwa nchi isiyoguswa).

     2.  RAMSA/KOMEDIA
Hii ni tamthiliya ambayo huchangamsha na huishia kwa namna ya kufurahisha. Tunaposema inachangamsha na kufurahisha haina maana kuwa dhamira zake si nzito. Tamthiliya hii hushughulikia mambo yale yale yanayoshughulikiwa na tanzia  kama vile; kukata tama, masumbufu ya akili, matarajio, n.k lakini kwa mtazamo tofauti.
ETIMOLOJIA YA RAMSA (COMEDY)
·      Neno ramsa linamaanisha dhanna ya Kigiriki ya Komos
·      Ni kundi la wanaume walioimba na kucheza na kurukaruka wakizunguka sanamu kubwa ya Uume.
·      Jambo hili liliibua miviga iliyozungukia nguvu  ya uume na maana ya vichekesho. Utamaduni huu ulienea Japan na duniani.
·      Ramsa ilikuza sana elimu kuhusu ngono na ushindi wa mungu wa mapenzi – eros.  Sigmund Freud ameandika sana kuhusu hili katika nadhariya yake ya Psycho Analysis.
·      Aristotle alisema mahali pa tanzia ni katika mapigano au katika jukwaa wakati mahali pa ramsa ni bafuni au chumbani – kitandani
·      Kutokea katika mwanzo huu, waigizaji wengi walifanya vichekesho mwanzoni wakianza na vinyago vya uume.
·      Wanadamu walianza kuvaa mafigu (mask) kuchekesha na wakati huohuo kuigiza.
·      Kutokana na hali ilivyokuwa hapo kale, kwa kuwa Komosilihusika na vichekesho tu, mwisho wake ukawa ni vichekesho. Mwisho huu ukachukuliwa kuwa ndio kiini kikubwa cha sanaa ya kiramsa.
·      Kwa hiyo, maana ya ramsa ya awali ya kuelekea viungo vya uzazi ikabadilika na hatimaye Aristotle akaandika kuwa ramsa ichukuliwe kuwa ni tukio/hadithi inayohusu kuinuka kwa kibahati tu kwa mhusika anayevutia hisia za hadhira au anayehurumiwa na hadhira au anayependwa na hadhira.
·      Komedia inatokana na neno Komedia la Kigiriki linalomaanisha sehemu ya kiungo cha uzazi cha kiume. Ni uneni unaolenga kuleta furaha na kicheko. Ni utanzu wa maigizo ambao unalenga kumfanya mhusika mhurumiwa kuwa na ushindi utakaoleta kicheko.
·      Leo dhanna ya ucheshi imetoka katika viungo vya uzazi na kuzingatia zaidi onesho linaishaje kama onesho, ramsa huishia na “wakaishi raha mustarehe”.
·      Ramsa ni mafanikio yaliyojaa ucheshi ya mhusika mkuu ambaye alionekana mwenye bahati mbaya na hadhira ikimsikitikia.
·      Shujaa wa ki-ramsa sio lazima awe mtu maarufu au mbabe/shujaa. Anaweza kuwa mtu wa kawaida. Wahusika wengine pia katika ramsa ni watu wa kipato cha kati na chini kama vile: washona viatu, wauza mitumba, wachoma mishikaki, waalimu, wanafunzi, n.k na dhamira katika ramsa zinahusu watu hawa. Aristotle anasema shujaa wa ki-ramsa:
-       Awe mtu wa wastani hadi chini ya wastani
-       Ni mtu ambaye hatarajiwi kujitokeza, mtu wa nasaba duni
-       Mtu ambaye katika jamii huwa duni na matendo yake ni ya kiucheshi-ucheshi, ila historia humleta na kumkuza hata akatoka akawa “fulani” akaishi raha mustarehe.
-       Ni mhusika ambaye akifanikiwa kila mtu atafurahia na kutoka akiwa ameridhishwa na mwisho huo.
              SIFA ZA RAMSA
·      Ni lazima onesho livutie akili na siyo hisia au mihemko
·      Ni lazima kuwe na matendo bila kufikiria, kana kwamba mtendaji haba habari
·      Ni sharti kuwe na desturi/mila ambazo hadhira inazifahamu toka katika jamii yake
·      Mazingira ya onesho au vipengele vyake visiwiane au kupatana, visifuate utaratibu.
·      Hadhira inapoangalia haipaswi kuogopa au kupata uchungu
·      Wahusika hujaribu kuviepuka vikwazo ambavyo vimewekwa.
·      Inaonesha haja ya kuikomboa nafsi, yaani huona kuwa pamoja na uwepo wa kifo maisha bado yapo na ya thamani.


      Aina za ramsa
v Utani/Vichekesho (Farce)
-       Huonekana ni upuuzi, mambo hugeuzwa kinyume
-       Sura za wahusika hubadilishwa kama vingago
-       Lengo: kuchekesha na ndimo maana yake hupatikana
v Mapenzi/Mahaba (Romance)
-       Wapendanao huwekewa vikwazo kama pesa, kabila, hadhi, dini, lakini hatimaye huvishinda vikwazo hivyo.
v Tashititi/Dhihaka (Satire)
-       Huwahusu viongozi wa siasa au dini
-       Wahalifu, matapeli, wanafiki, wala rushwa, wafanya magendo, waongo, n.k
-       Mhusika mkuu (ambaye ni kiongozi) huwa na sifa hizo. Anadhihakiwa ili aache rushwa, utapeli, udhaifu, n.k
-       Ramsa hizi ni kama njia ya walalahoi kutoa malalamiko yao kwa viongozi wao.
KWA UJUMLA:
Tanzia ni kinyume cha Ramsa kwa maana kwamba, badala ya kuonesha kuinuka na kufanikiwa kwa mhusika duni wa tabaka la chini asiyetarajiwa, tanzia huonesha kuanguka na kushindwa kwa mhusika maarufu, mbabe au shujaa atokaye katika tabaka la juu, mtu wa nasaba bora.
Kwa hiyo, undani hasa wa maana ya ramsa sio tu onesho kumalizika kwa kicheko bali zaidi onesho kumalizika kwa mafanikio ya mhusika aliyeonekana kutofanikiwa. 
    3.  TANZIA-RAMSA
·      Huonesha mabadiliko ya aina fulani yanayogeuza mwelekeo wa matukio ya kitanzia na kuufanya kuwa wa kufurahisha.
·      Ni tamthiliya inayoishia kwa furaha, yaani inachanganya vipengele vya kitanzia na vya kiramsa.
·      Hutumiwa sawa na tamthiliya za kibwege ambazo huonesha kuwa kicheko/furaha ndiyo jibu pekee kwa watu ambao hawana imani na maisha kwa sababu misingi thabiti ya maisha imeondolewa  kama inavyodhihirika katika tamthiliya ya Amezidi.
CHIMBUKO, MABADILIKO NA MAENDELEO YA TAMTHILIYA YA KISWAHILI
     CHIMBUKO:
Tamthiliya hupatikana katika sura mbalimbali duniani kote.
·      Chimbuko: hushabihiana katika nchi mbalimbali na huhusishwa na visakale na matendo ya kidini.
ØUlaya: drama ilitokana na miviga (rituals) na viviga (rites) vya kidini katika jamii ya kale ya Wayunani.
Miviga iliambatana na duru za: kuzaliwa, kufa, kuoza na kuzaliwa upya. Duru hizi zilihusishwa na Mungu aliyeitwa wa Wayunani aliyeitwa Dionizi.
ØIndia: drama ilitokana na tendi za kidini Mahabharata na Ramayana pamoja na miviga iliyoambatana na utendaji wa tendi hizo katika mahekalu ya Kihindi.
ØChina na Japan: drama ilitokana na dansi za miviga ya kidini. Baadaye drama hizo zilijitenga na udini na kuanza kushughulikia masuala ya sanaa na burudani.
ØAfrika: maigizo ya kitamthiliya yalikuwa huko Misri, ambako miviga iliyohusu kufa na kufufuka kwa Mungu wa Misri, Osiris, ilikuwa ikiigizwa kila mwaka kwa miaka kama 2000 (Brocket, 1979 katika Mulokozi, 1996).
-       Pia kulikuwa na maigizo yasiyoandikwa ambayo yalikuwa ni sehemu ya matendo ya kijamii k.v miviga, viviga na ngoma.
-       Kulikuwa na tamthiliya – bubu, maigizo ya watoto na ya watani. Drama hizi zilifungamanishwa na fasihi simulizi.
     Kwa maelezo haya huenda tamthiliya ilichipuka kutokana na mambo
     matano.
·      Miviga na viviga vya kijamii na kidini na tendi.
·      Umithilishaji wa maisha ya kawaida kwa ajili ya burudani, elimu, maonyo na michezo
·      Sanaa za maonesho za kijadi kama vile ngoma na dansi
SANAA ZA MAONESHO ZA MAGHARIBI
Sanaa za maonesho ni nini?
Kabla ya kuona maana ya sanaa za maonesho, tuone kwanza aina za sanaa za maonesho. Balisidya na Muhando, P (1976) katika Fasihi na Sanaa za Maonyesho wanatoa aina tatu za sanaa za maonesho.
   ·    Sanaa za uonesho
Ni aina ya sanaa ambayo uzuri wake umo katika umbo la kudumu, mfano mkeka, vyungu, nyumba, n.k
   ·    Sanaa za ghibu
Ni sanaa ambazo uzuri wake umo katika umbo la kugusa hisia, mfano wimbo, shairi.
   ·    Sanaa za vitendo
Ni sanaa ambazo uzuri wake umo katika umbo la vitendo. Ni lazima uone vitendo vikitendeka.

Sanaa za maonesho: ni sanaa za vitendo ambavyo ni lazima viwe na sifa muhimu ambazo ni:
-       Mchezaji/mtendaji
-       Uwanja wa kutendea
-       Mchezo wenyewe
-       Watazamaji/hadhira
      Udhaifu wa mtazamo huu
-       Umekuwa na dhanna ya mchezo
-       Una sifa nne tu zilizozingatia tamthiliya ya kigeni
-       Uwanja wa kutendea ni maalumu wakati kwa mwafrika ni mahali popote
-       Hadhira ya waafrika huwa ni watazamaji na washiriki tofauti na hadhira iliyooneshwa katika mtazamo wa kigeni
Kwa ujumla sifa hizi nne zinalenga tamthiliya ya kigeni. Kwa hiyo tamthiliya za kimagharibi ilikuwa:
  Ø Lazima ziwe na mahali pa kuonea kinachotendwa 
  Ø Walikuwa na dhanna ya drama (mpangilio wa maneno ambao hufuatana na utendaji wa wahusika)
  Ø Pia kulikuwa na uigizaji (wa tabia, vitendo, n.k)
  Ø Huegemea zaidi katika maandishi. Kwao kisichoandikwa hakina nguvu. Walitumia maandishi ili waafrika waonekane washenzi, wajinga wasio na         maandishi mf. Biblia
  Ø Kulikuwa na mpangilio wa jukwaa, taa za rangi, sauti, mavazi, n.k
TAMTHILIYA ZA KIAFRIKA
    ·   Huzingatia masuala ya dhati ya jamii, yaani yanayotokea kweli katika            jamii.
   ·    Hutumia vipengele vya fasihi simulizi na hazina vipengele vya Ki-                 Aristotle mf. Tamthiliya ya Lina Ubani
   ·    Huwa na ukiukwaji wa Uaristotle. Upangaji wa waletao mgogoro ni              tofauti mf. Sio lazima awe ni mbabe au mkinzani
    ·   Mshindi sio lazima awe mbabe, anaweza kuwa mdogo mf. Daudi katika         Biblia
    ·    Mbabe sio lazima afe mwishoni na kuendeleza tanzia.
Maendeleo ya tamthiliya ya Kiswahili
Ingawa asili ya tamthiliya katika nchi mbalimbali yaelekea kufanana lakini maendeleo yake yalichukua mikondo tofauti kutegemeana na historian a utamaduni wa jamii inayohusika. Katika kipengele hiki tutajikita katika kuangalia maendeleo ya tamthiliya ya Kiswahili kihistoria kama ilivyofafanuliwa na Mulokozi (1996).
      1.   Kabla ya Ukoloni
·      Hakukuwa na tamthiliya zilizoandikwa ili ziigizwe jukwaani
·      Zilikuwepo zisizoandikwa, yaani drama zilizoigizwa kwa ajili ya ajili ya kuoneshwa kwenye shughuli maalumu k.v jando na unyago, kutawazwa viongozi, harusi, mazishi, n.k
·      Zilikuwa na sifa zote za sanaa za maonesho
·      Tamthiliya hizi hazikuwa nap loti ya Ki-Aristotle
     2.   Kipindi cha Ukoloni
Kipindi hiki kilianza mwaka 1890 na kumalizika kama mwaka 1960. Kipindi hiki kilikuwa na aina kuu mbili za tamthiliya mpya za kizungu na vichekesho. Mwishoni mwa kipindi hicho palitokea aina ya tatu ambayo Mulokozi (1996) anasema tunaweza kuiita tamthiliya ya Kiswahili.



Tamthiliya za kizungu
Ø Zilikusudiwa ama kuwaburudisha maofisa na masetla wa Kizungu, ama kufunza Biblia na imani ya Kikristo
Ø Kenya: zilianza kuigizwa Nairobi na Mombasa kabla ya vita vikuu vya kwanza  vya dunia
Ø Tanzania: zilianza kuigizwa shuleni miaka ya 1920, zilitokana na michezo iliyoandikwa na Waingereza k.v Shakespeare
Ø Zilikuwa za kibwanyenye na chache zilifasiriwa kwa Kiswahili mf. Tabibu Asiyependa Utabibu
Ø Pia vilianzishwa vikundi vya kuigiza tamthiliya za Kizungu k.v Tanzania : Dar es Salaam Players (Little Theatre, 1947) na Arusha Little Theatres (1953). Kenya:kulikuwa na National Theatre (1952) iliyotawaliwa na michezo ya wageni hadi miaka ya 1970.
Vichekesho
Ø Ni tamthiliya – gezwa (zilizotungwa papo kwa papo bila kuandikwa)
Ø Zilianza miaka ya 1920 kwa lengo la kuburudisha wenyeji
Ø Zilikuwa na vituko vya kuchekesha na ziliwahusu waliofikiriwa kuwa washamba, wajinga au wasiostaarabika
Ø Ziliendelea hata baada ya uhuru
        Tamthiliya – andishi ya Kiswahili
Ø Zilianza tokea 1950
Ø Nyingi zilikuwa za kidini na ziliandikwa ili kuigizwa tu shuleni na makanisani mf. Imekwisha  ya C. Frank (1951)
Ø Zisizokuwa za kidini zilianza kutungwa kati ya 1952 na 1956
Ø Shughuli za tamthiliya zilisimamiwa na Graham Hyslop, mtumishi wa serikali ya kikoloni ya Kenya, ambaye alianzisha kikundi cha maigizo kwa ajili ya askari mwka 1944. Mwaka 1954 alianza kutunga michezo iliyoigizwa na kikundi chake.
Ø Michezo ya mwanzo kabisa ni: Afadhali Mchawi (1957) na Mgeni Karibu (1957) michezo hii iliigizwa kati ya 1954-1956
Ø Juhudi za Hyslop zilibainika katika vipawa vya wanafunzi wake kwa mf Henry Kuria aliandika tamthiliya iliyoitwa Nakupenda Lakini…. Iliyoigizwa mwaka 1954 na kuchapishwa 1957
Ø Baada ya Henry Kuria motisha ya kutunga ilishika kasi:  Gerishon Ngugi, Nimelogwa Nisiwe na Mpenzi (1961) iliyoigizwa 1956; Nyoike, Maisha ni Nini iliyoigizwa mwaka 1955; Kurutu, Atakiwa na Polisi (1957).
            3.   Kipindi cha Uhuru
·      Tamthiliya ya Kizungu
Ø Iliendelea kuigizwa hasa shuleni na katika kumbi maalumu
Ø Umaarufu wake ulipungua hasa upande wa Tanzania
Ø Tamthiliya muhimu zilianza kutafsiriwa mf Juliasi Kaisari na Mabepari wa Venis (J.K. Nyerere); Makbeth na Tufani (S.S. Mushi)- zote za Shakespeare. Sophocles, Mfalme Edipode (S.S. Mushi); Mkaguzi Mkuu wa Serikali (C. Mwakasaka); n.k
Ø Pia tamthiliya za kiafrika zilizoandikwa kwa lugha za kigeni na lugha nyingine zilifasiriwa mf Ngugi wa Thiong’o: Mtawa Mweusi,  Soyinka, W: Masaibu ya Ndugu Jero (A.S Yahya); Ngugi wa Thiong’o  na  Ngugi wa Mirii: Nitaolewa Nikipenda, n.k

·      Vichekesho
Ø Vilichukua sura tofauti. Badala ya kuwasuta  washamba vilianza kuwasuta wazungu weusi
Ø Hujaribu kuzungumzia matatizo ya watu wa kawaida k.v matatizo ya kifamilia, ukosefu wa kazi, UKIMWI, uhalifu, n.k
Ø Vipo vya kisiasa vilivyozungumzia siasa ya ujamaa, ubinafsiwa viongozi, matatizo ya kuanzisha vijiji vya ujamaa, n,k
Ø Baadhi vilijinasibisha na wanasiasa
·      Tamthiliya – andishi ya Kiswahili
Ø Mashindano ya utunzi yaliyoendeshwa na Youth Drama Association nchini Tanzania yaliwezesha chipukizi kujitokeza, mf  E.Hussein ambaye tamthiliya yake ya kwanza Wakati Ukuta (1969) ilishinda tuzo katika mashindano hayo.
Ø Wahitimu wengi wa fani ya sanaa za maonesho walianza kujitokeza
Ø 1970 – 1994: kuchapishwa kwa tamthiliya nyingi za Kiswahili mf.
ü E. Hussein: Kinjekitile (1969), Mashetani (1971), Jogoo Kijijini na NGao ya Jadi (1989), Arusi (1980), Kwenye Ukingo wa Thim (1989)
ü P. Muhando: Hatia (1972), Tambueni Haki Zenu (1984), Pambo (1975), Nguzo Mama (1982), Lina Ubani (1984), n.k
ü E. Mbogo: Giza Limeingia (1980), Tone la Mwisho (1981), Ngoma  ya Ng’wanamalundi (1988), Morani (1993), Sundiata (1995), n.k
Hawa ni baadhi tu ya watunzi kutoka Tanzania. Huko Kenya watunzi wapya walikuwa wengi. Miongoni mwao ni Thomas, M : Bahati Nasibu (1971); C.N Chacha : Mke Mwenza (1982) na Wingu Jeusi; Jay Kitsao: Uasi (1980), Tazama Mbele (1981), Malimwengu Ulimwenguni (1983) na Bibi Arusi (1983), n.k
ATHARI YA TAFSIRI KATIKA TAMTHILIYA YA KISWAHILI
Baada ya kazi mbalimbali za kigeni kutafsiriwa, na kama ambavyo tunafahamu kuwa tamthiliya hizo zilikuwa na athari ya kiaristotle, tamthiliya ya Kiswahili iliathiriwa katika mambo mbalimbali. Sambamba na kuibuka kwa waandishi wengi wa tamthiliya lakini pia tamthiliya hizo za Kiswahili zilizotungwa zilikuwa na athari mbalimbali za tamthiliya za kigeni kwa mfano suala la muundo, mtindo, dhanna ya umchezo kwa sababu awali drama zetu zilikuwa na udhati, masuala ya ujenzi wa wahusika na kadhalika. Rejelea sifa za kiaristotle na jinsi zinavyojidhihirisha katika tamthiliya mbalimbali za Kiswahili.
Fasihi ya majaribio katika tamthiliya ya Kiswahili
Dhanna ya fasihi ya majaribio inaibuka katika tamthiliya na pengine katika riwaya pia kutokana na athari ya fasihi ya kimagharibi ambayo ilionekana kumeza kabisa fasihi ya kiafrika. Juhudi za watunzi wazawa kujirudisha katika utunzi wenye ladha na asili ya kiafrika ndio msukumo wa kuwepo kwa fasihi inayochanganya vipengele vya kifasihi simulizi katika fasihi andishi na hivyo kuifanya fasihi andishi yenye misingi ya kimagharibi kuwa na vionjo vya kiafrika.
·      Watunzi wengi wa tamthiliya ya Kiswahili wanaiga mbinu na kanuni za tamthiliya ya Ulaya, hasa ya Ki-Aristotle
·      Kisanaa hazitofautiana na tamthiliya za Kiingereza, tofauti ni katika lugha na maudhui tu
·      1970, baadhi ya watunzi hawakuridhika na uigaji huu
·      Walianza kuchota mbinu kutoka katika sanaa za jadi za kiafrika, hivyo wakaanzisha tamthiliya ya majaribio
·      Mfano, E. Hussein alijaribu kutumia utambaji wa ngano katika maigizo yake ya Ngao ya Jadi na Jogoo Kijijini.
·      Hali hiyo imeleta mabishano miongoni mwa wataalamu iwapo tungo hizo mbili ziitwe tamthiliya au tendi.
·      Pia P. Muhando katika Lina Ubani na Nguzo Mama alijaribu kutumia mbinu ya utambaji wa ngano.
·      Mbinu ya majigambo imetumiwa na Muhando na wenzake katika Harakati za Ukombozina Mbogo katika Sundiata.
·      Mbinu ya tendi – simulizi imetumiwa na Mulokozi katika Mukwava wa Uhehe.
·      Majaribio katika tamthiliya ya Kiswahili bado yanaendelea. Mbinu nyingi zinaendelea kutumika ili kuifanya tamthiliya ya Kiswahili iendane na utamaduni na mazingira ya Kiafrika.

Powered by Blogger.