SWALI : Unadhani katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia rejista bado zina umuhimu wowote?

SWALI : Unadhani katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia rejista bado zina umuhimu wowote?
JIBU:
Rejista (pia rejesta au sajili) ni matumizi ya lugha kulingana na muktadha maalum. Miktadha tofauti husababisha aina mbalimbali za lugha. Baadhi ya vipengele vya miktadha hiyo ni mada, eneo la matumizi ya lugha, mahusiano baina ya wahusika, umri, jinsia, wakati, na kadhalika.
KIINI
Rejesta zina umuhimu mkubwa sana katika lugha hasa kulingana na maendeleo yanayoikumba lugha kimatumizi. Umuhimu wa rejesta ni kama ufuatao
Rejesta hutumika Kama Kitambulisho
Rejesta hutofautisha mtindo wa lugha miongoni mwa wazungumzaji. Rejestainawatambulisha wazungumzaji kuwa wao ni kundi fulani. Mfano: Rejesta yawahunzi inawatambulisha kuwa wao ni tofauti na wavuvi ambao nao pia wanarejesta yao. Rejesta ya kanisani au msikitini ni tofauti na rejesta ya jeshini, n.k.
(ii) Rejesta hupunguza Ukali wa Maneno
Rejesta inapotumiwa na kundi la watu, huficha jambo hilo linalozungumziwalisieleweke kwa wengi. Hivyo hadhira inapuuzwa kwa sababu siyo watu wengiwanaoelewa.
(iii) Rejesta Inatumika Ili Kurahisisha Mawasiliano
Rejesta inatumika ili kurahisisha mawasiliano au kupunguza muda wakuwashughulikia watu au wateja wengi. Kwa mfano mganga anayegawa dawahospitalini anaposema “mbili asubuhi, mchana na jioni” akiwa na maana kuwamgonjwa anywe vidonge viwili asubuhi, viwili mchana na viwili jioni. Hapaamefupisha ili aweze kuwahudumia kwa wakati mfupi wagonjwa wengiwanaosubiri kupata dawa.
(iv) Rejesta hupamba Lugha Miongoni mwa Wazungumzaji
Kwa mfano,
Rejesta ya Hotelini.
Mhudumu: Nani wali kuku?Mteja: Mimi hapa!Mhudumu: Nani ugali-ng’ombe?Mteja: Mimi hapa!


Mazungumzo haya kati ya mhudumu na mteja licha ya kurahisishamawasiliano, vilevile yanapamba mazungumzo hayo.
(v) Rejesta huweza Kuwa Kiungo cha Ukuzaji wa Lugha
Kutokana na matumizi ya rejesta mbalimbali, lugha inayohusika inawezakuunda msamiati wake. Kuna baadhi ya maneno ya lugha yanayotokana narejesta mbalimbali.
HITIMISHO
Ukuaji wa lugha ya Kiswahili hutegemea sana usanifishaji wa maneno yanayotumika katika jamii na kupata mashiko.
>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>> 
SWALI 2: Vigezo vipi vya msingi hutumika kuainisha sauti ya kifonetiki mpaka kufikia kubainishia sifa zake pambanuzi.
JIBU
UTANGULIZI
Fonetiki ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa taratibu zote zinazohusiana na utoaji, utamkaji, usafirishaji, usikiaji na ufasili wa sauti za lugha za binadamu kwa jumla. Sauti  za kifonetiki huainishwa kwa vigezo mbalimbali ambavyo huzalisha sifa bainifu za kifonetiki. Sifa za sauti kifonetiki ni sifa za zinazoweza kuitofautisha sauti moja kutokana na sauti nyingine kwa kutumia vigezo vya kifonetiki. Sauti za kifonetiki (foni) huainishwa kwa kuzingatia sifa mbalimbali bainifu kama zifuatazo
KIINI
Vigezo vitumikavyo kubainisha konsonanti na irabu za Kiswahili  ni kama vifuatavyo:
Kwanza, kigezo cha namna ya kutamka, namna ya kutamka Kwa kuzingatia kigezo hiki konsonanti zimegawanyika katika makundi kama vile: Vipasuo: Sauti za vipasuo ambavyo hutamkwa wakati mkondo wa hewa unapozuiwa na hewa kuachiwa ghafla kisha kuzalisha sauti zenye msikiko kama mlipuko fulani

Pili, kigezo cha mahali pa kutamkia , kwa kuzingatia kigezo hiki konsonanti zimegawanyika katika makundi kama vile nazali za midomo, ufizi,mdomo meno,meno na midomo.
Tatu,kigezo cha mkondo wa hewa, Mkondo hewa kutoka mapafuni waweza kupititia katika chemba ya kinywani au ya puani. Kinachosababisha hali hii ni kilimi. Kilimi chaweza ama kuteremka chini kuelekea shina la ulimi na kuruhusu hewa kupita puani au kuinuliwa juu kuelekea upande wa juu wa ukuta wa koo na kuruhusu hewa kupita kinywani. Sauti inayotamkwa huku mkondo wa hewa ukipita puani huitwa sauti  nazali. Mfumo huu wa upokeaji wa sauti wakati mkondo wa hewa unapita puani huitwa Ung’ong’o.

Nne, kigezo cha hali ya glota,  Katika koromeo au glota kuna kitu kinaitwa nyuzi sauti. Nyuzi sauti ni nyama laini zilizoko katika koromeo ambazo zinauwazi katikati unaoruhusu mkondo wa hewa kutoka nje na ndani ya kifua. Nyuzi hizo huwa katika nafasi za aina mbili wakati hewa inapopita. Kuna wakati nyuzi hizo zinakaribiana au kuwa pamoja na wakati mwingine zinakuwa zimeachana. Hewa inapotoka ndani ya mapafu kuja nje kupitia kwenye pango la kinywa au la pua nyuzi hizo zikiwa zimekaribiana au kuwa pamoja, nyuzi hizo husukumwa na kutetemeka.Sauti zinazotolewa wakati huo huwa na mghuno na huitwa sauti ghuna. Zikiwa nyuzi hizi zimeachana, hewa hupita kwa urahisi bila kuzuiliwa, na hivyo hazikwami na kusababisha sauti zinazotolewa kutokuwa na mghuno
Kutokana na vigezo hivyo tunapata sifa zifuatazo kwa konsonanti:
·       Sifa ya kwanza ni midomo: Mkondo hewa unapozuiwa kwa kubana mdomo wa chini na mdomo wa juu kisha ikaachia au ikabanwa kwa kuviringwa huku ikiwa imeacha upenyo kidogo huwezesha sauti kadhaa hutolewa.

·       Sifa ya pili ni midomo-meno: Sifa hii inahusu utamkaji wa sauti ambao kwao meno ya juu, ambayo ni alatuli,hugusana na mdomo wa chini, ambao ni alasogezi, na wakati huohuo hewa inaruhusiwa kupita kwa kukwamizwakwamizwa katikati ya meno.

·       Sifa ya tatu ni ya meno: Sauti hizi hutamkwa kwa ncha ya ulimi ikiwekwa katikati ya meno ya juu na ya chini.

·       Sifa ya nne ni ya ufizi: Sauti hizi zinapotolewa, ncha ya ulimi hugusana na ufizi.

·       Sifa ya tano ni ya kaakaa gumu: Sifa hii inahusu utamkaji wa sauti ambapo ulimi hufanya kazi ya ala sogezi. Ulimi hugusana na kaakaa gumu ambalo ndiyo alatuli.

·       Sifa ya sita ni ya kaakaa laini: Sifa hii huhusu utamkaji wa sauti ambao huandamana na sehemu ya nyuma ya ulimi, ambayo ni alasogezi, kugusa kaakaa laini, ambalo ni alatuli.

Vigezo vitumikavyo kubainisha irabu mbalimbali, irabu hupangwa kutokana na vigezo vitatu:
Sauti irabu huainishwa kwa vigezo vifuatavyo:
 Kwanza ni kigezo cha mwinuko wa ulimi: hapa tunaangalia ulimi umeinuka kiasi gani. Ulimi unaweza kuinuka juu kabisa, juu kiasi au kulala chini kabisa.
Pili ni kigezo cha sehemu ya ulimi iliyoinuka, hapa tunaangalia ulimi umeinuka sehemu gani wakati wa kutamka sauti irabu, kwa mfano ulimi huweza kuinuka mbele, au nyuma
Tatu ni kigezo cha umbo la midomo,wakati wa kutamka sauti irabu midomo huweza kuwa na umbo la mviringo(duara) au mtandazwa.
Kwa vigezo hivyo tunapata sifa zifuatazo za kifonetiki za kuainishia irabu:
        Sifa ya ujuu,ujuu kiasi au uchini
        Sifa ya umbele na unyuma
        Sifa ya umviringo au mtandawza
HITIMISHO
Kwa ujumla sifa za kuainishia sauti kifonetiki ni matokeo ya vigezo vya kifonetiki ambavyo huweka bayana sifa mahususi kwa kila sauti ya kifonetiki.
>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>> 
SWALI 3: Taja na uyafafanuwe kwa kina mambo mawili yanayohusu fonolojia arudhi.
JIBU
UTANGULIZI
Fonolojia arudhi, hizi ni sifa za kimatamshi zinazoambatanishwa kwenye sauti za lugha ya mwanadamu, sifa hizi huitambulisha sauti kimatamshi zaidi na husaidia kubainisha taarifa za msingi kama hali ya msemaji, hisiya za msemaji au umbali alioko msemaji. Fonolojia arudhi huhusu sifa kama shadda, kiimbo, matamshi, lafudhi, kidatu na toni. Kwa mujibu wa swali hili nitarejelea shadda na kiimbo.
KIINI
Shadda/mkazo
Ni utaratibu wa utamkaji wa maneno ambapo silabi fulani hutamkwa kwa nguvu nyingi zaidi kuliko ilivyo katika silabi nyingine za neno hilohilo. • Mkazo unaweza kuchukuliwa kama kilele cha kupanda na kushuka kwa sauti katika utamkaji wa neno. • Silabi yenye mkazo inakuwa na msikiko mzito zaidi kuliko silabi nyingine za neno hilohilo. • Lugha nyingi hasa za kibantu hazitumii mkazo, Lugha nyingi hutumia toni. Kiswahili sanifu hakitumii toni na zaidi hutumia mkazo.
Kiimbo
Kiimbo ni utaratibu maalumu wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza katika utamkaji wa lugha fulani. Kiimbo hugawanyika katika aina kadhaa zifuatazo.
Aina za kiimbo
Kiimbo cha maelezo: Kiimbo cha maelezo ni kile ambacho kwa kawaida msemaji wa lugha akiwa kwenye kidatu chochote kile mawimbi sauti ya usemaji wake yanakuwa takriban katika mstari ulionyooka.
Kiimbo cha kuuliza: Kiimbo cha kuuliza hujitokeza kwa kutumia viwango tofauti vya kidatu kutegemeana na aina ya swali linaloulizwa .
Kiimbo cha amri: kiimbo cha amri hakitofautiani sana na kiimbo cha maulizo.Uchunguzi wa kifonetiki, unaonesha kuwa katika kutoa amri, mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko ilivyo katika kiimbo cha maelezo.
HITIMISHO

Fonolojia arudhi ni kipengele muhimu sana katika ubainishaji wa fonimu za lugha kama Kiswahili kwani husaidia sana kutambulisha hisia na hali ya msemaji kwa ujumla.
Powered by Blogger.