TAFSIRI NA UKALIMANI
TAFSIRI NA UKALIMANI
DHANA, DHIMA NA HISTORIA YA TAFSIRI
Tafsiri
ni uhawilishaji wa mawazo kutoka lugha moja ya maandishi kwenda lugha
ingine ya maandishi. Mawazo yanayoshughulikiwa katika tafsiri sharti
yawe katika maandishi na si vinginevyo, pia mawazo kati ya lugha chanzi
na lugha lengwa sharti yalingane. (Mwansoko, 1996:1).
HISTORIA FUPI YA TAFSIRI
Maendeleo
ya kiuchumi, kisayansi na kiutamaduni yanayofurahiwa leo duniani
yalitokana na juhudi za ugunduzi wa watu wa kale na yalizifikia nchi
mbalimbali kwa njia ya tafsiri.
Inasadikika kuwa sayansi na taaluma za kisasa zilianzia Afrika huko Misri miaka 3000 na zaidi kabla ya Kristo.
Ugunduzi
na ustaarabu wa Ulaya kwa karne za baadaye hususani karne ya 19
ulitokana na ugunduzi wa Afrika. Mbinu kuu katika kueneza elimu hii ya
Wamisri huko Ulaya ilikuwa ni tafsiri. Wasomi wengi wa Ulaya walijifunza
lugha ya Misri na kuishi huko kwa miaka mingi na hatimaye walitafsiri
elimu hii ya Wamisri na mambo yote waliyojifunza huko na kuyasambaza
Ulaya.
Wakati
wa himaya ya Warumi hasa baada ya Ukristo kuenea Ulaya nzima, elimu
hiyo ya zamani ilianza kupigwa vita kwa kudaiwa kuwa ni ya kipagani. Hali hiyo ilisababisha kuibuka kwa kipindi kilichojulikana kama, The dark ages yaani, zama za giza.
Baada
ya Uislamu kuingia na kuimarika, wasomi wengi wa ki-Islam waliipekua
elimu ya kale ya Wamisri wakaifasiri kwa Kiarabu na kuipanua na
kuijaliza kulingana na maendeleo ya wakati huo. Hii ilichochea mlipuko
wa ustawi na maendeleo ya tafsiri.
Karne
ya 19 tafsiri kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya mkondo au mwelekeo mmoja
ambapo vitabu vya waandishi na wanasayansi mashuhuri kutoka nchi
zilizoendelea vilitafasiriwa kwa ajili ya wasomaji wa nchi
zinazoendelea.
Karne
ya sasa inajulikana kama karne ya tafsiri kwa sababu mikataba mingi ya
kimataifa kama ya mashirika ya umma na binafsi sasa inafasiriwa kwa
yeyote anayehitaji taarifa hizo. Maendeleo ya haraka ya teknolojia na
haja ya kueneza mahitaji ya tafsiri vinachochea kukua kwa taaluma hii.
Nchini Tanzania taaluma ya tafsiri haina historia ndefu. Tafsiri ya kwanza katika Kiswahili inayofahamika ni Utenzi wa Hamziyyauliotungwa huko Misri karne ya 13 na kufasiriwa kwa Kiswahili na Bwana Idarus bin Athuman aliyeishi kaskazini mwa Kenya miaka ya 1700 – 1750.
Kipindi
cha ukoloni kazi mbalimbali zilitafsiriwa na wamisionari kwa mfano
Biblia (Injili ya Luka na Yohana), Hekaya za Abunuwasi na hadithi
nyingine, Alfu – Lela Ulela (siku elfu na moja), Safari za Allan
Quartermain, Robinson Cruso, n.k
Baada
ya uhuru wazawa walifanya juhudi za kufasiri vitabu bora vya ulimwengu
kwa Kiswahili mf. Mwl J.K Nyerere alifasiri vitabu viwili vya mwandishi
mashuhuri wa Uingereza William Shakespeare vilivyojulikana kama Juliasi Kaizari na Mabepari Wa Venis. Mwingine ni Paul Sozigwaaliyefasiri kitabu cha Song of Lawino. Kwa
ujumla wananchi wengi waliokuwa na ujuzi wa lugha za kigeni walifasiri
maandishi mbalimbali muhimu kwa lugha ya Kiswahili ili kueneza maarifa
na taaluma kwa wazawa wenzao.
Kutokana
na taaluma ya tafsiri hivi sasa Kiswahili kina hazina ya falsafa,
fasihi, sayansi na ufundi toka lugha za mataifa mbalimbali kama
Uingereza, Ufaransa, Uarabuni, Ureno, n.k
Pamoja
na mafanikio ya shughuli za kifasiri nchini Tanzania baadhi ya tafsiri
zilizopo zinaonesha kasoro katika uchaguzi wa kazi za kufasiri, kazi
zilizofasiriwa toka lugha za asili ni ile ya Anicet Kitereza inayoitwa Bwana Muyombekere na Bibi Bugonoka, Ntulanalwo na Bulihwali (1980) kutoka lugha ya Kikerewe.
Hivi
sasa huduma ya tafsiri nchini Tanzania inatolewa na Idara mahususi za
tafsiri chini ya Taasisi ya iliyokuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili
(TUKI) ambayo sasa inaitwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI),
Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) na International Language
Orientation Services.
Maslahi na haki za wafasiri zinalindwa na kusimamiwa na chama cha wafasiri wa Tanzania kilichoanzishwa mwaka 1981.
DHIMA/KAZI YA TAFSIRI
Dhima
ya tafsiri katika maendeleo ya binadamu ni kubwa kutokana na ukweli
kwamba tafsiri ndio daraja kati ya jamii mbalimbali za watu wanaotumia
lugha zinazotofautiana.
Tafsiri ina dhima zifuatazo:
1. Tafsiri kama njia ya mawasiliano
Tafsiri
hutumika kutolea maelezo ya kibiashara kama vile jinsi ya kutumia
bidhaa zinazouzwa nchi za nje, matangazo ya biashara kupitia broshua
zenye fasiri katika vyombo vya habari na katika nyaraka rasmi kama
mikataba na ripoti za kimataifa, makala za kitaaluma, vitabu vya kiada
na ziada. Tafsiri katika mawasiliano imeongezeka sana kutokana na
utegemezi wa mataifa yanayoendelea kwa nchi zilizoendelea kiuchumi,
kiutaalamu na teknolojia. Hata hivyo, ni muhimu kufanya tafsiri ya
kimawasiliano kwa umakini mkubwa ili kuepuka upotoshaji wa taarifa kwa
mfano katika matumizi ya dawa iwapo mfasiri atafasiri kinyume huweza
kusababisha madhara kwa mtumiaji.
2. Tafsiri kama nyenzo ya kueneza utamaduni
Tafsiri
hutumiwa pia kama nyenzo ya kueneza tamaduni za jamii za ulimwenguni
kupitia tafsiri na mwingiliano wa mataifa mbalimbali mathalan, jamii za
kiafrika utamaduni wake umeathiriwa sana na tamaduni za jamii za Ulaya
kwa mfano chakula na ulaji. Kwa upande mwingine, maandishi ya kitafsiri
yanayoendelea kufasiriwa kutoka lugha moja hadi nyingine yanazidi
kueneza utamaduni mpya kutoka taifa moja hadi lingine.
3. Tafsiri kama mbinu ya kujifunza lugha
Mazoezi
ya kutafsiri humfanya mfasiri apekuwe kwa undani na umakini zaidi
vipengele anuwai vya kiisimu vya lugha. Kadiri mfasiri anavyofanya kazi
ya kufasiri ndivyo anavyokomaza umahiri wake katika lugha na hatimaye
hujikuta mwenye umakini mkubwa katika lugha husika.
4. Tafsiri kama kiliwazo cha mfasiri
Nafsi
ya mfasiri huliwazika na kufurahi kadiri anavyotatua matatizo ya
kutafsiri na hasa anapopata visawe muafaka katika lugha lengwa. Ugumu wa
kazi hii unapotatuliwa huwa ndio furaha ya mfasiri na chachu ya
kuendelea kufasiri kazi nyingine nyingi zaidi.
UAINISHAJI WA MATINI ZA TAFSIRI
Matini za tafsiri zinaweza kuainishwa katika makundi kadhaa:
1. Matini kufuatana na dhanna ya lugha:
Hapa tunapata aina tatu za matini ambazo ni:
(a) Matini elezi:
Hizi ni matini ambazo mwandishi wake hutumia lugha kuelezea hisia zake bila kujali maelezo hayo yatapokelewaje na hadhira.
Mifano ya matini elezi ni kama vile:
v Fasihi iliyobuniwa kwa makini
v Hotuba na nyaraka za viongozi na watu wenye mamlaka
v Wasifu
binafsi, insha, mawasiliano binafsi baina ya watu na hasa yanayohusu
hisia za mwandishi binafsi bila kujali wasomaji lengwa.
(b) Matini arifu:
Hizi
ni matini zinazohusu mada yoyote ile yenye maarifa kwa mfano sayansi,
teknolojia, biashara na uchumi. Matini hizi huwa katika maumbo sanifu
kama vitabu, ripoti, makala katika magazeti au majarida ya kitaaluma.
Matini
arifu zina sifa kuu mbili. Sifa ya kwanza ni kwamba ndizo matini
zinazofasiriwa na idadi kubwa ya wafasiri walioajiriwa katika mashirika
ya kimataifa, kampuni kubwa za binafsi na asasi nyingine za tafsiri,
pili asilimia kubwa ya matini hizi huwa zimekosewa sana hivyo, ni jukumu
la mfasiri kufanya masahihisho yanayohitajika ili kufanya kazi iwe na
ubora zaidi.
(c) Matini amili:
Matini
hizi hulenga kuibua hisia za msomaji na kumfanya afikiri au atende kwa
namna ambayo imekusudiwa na mwandishi wa matini. Mifano ya matini amili
ni kama vile:
v Matangazo
v Propaganda
v Maombi
v Mialiko
v Fasihi pendwa, n.k
Mambo muhimu kuhusu matini amili ni pamoja na:
· Kuonesha uhusiano baina ya mwandishi na hadhira
Mfano:
- Mheshimiwa waziri,
- Kwa heshima na taadhima,
- Wako mtiifu, n.k
· Matini
amili lazima ziandikwe kwa lugha inayoeleweka kwa hadhira mara moja ili
ujumbe uliomo ueleweke kwa urahisi na hadhira itekeleze kwa urahisi na
kama inavyotarajiwa na mwandishi.
Hata
hivyo, kuna matini chache sana ambazo zimejipambanua kuwa ni elezi,
arifu au amili. Matini nyingi huwa na mchanganyiko wa sifa zote huku
sifa moja ikijitokeza zaidi ya nyingine.
2. Uainishaji wa matini kufuatana na istilahi
Uainishaji huu huwezesha kubaini kama matini ni ya kiufundi, nusu kiufundi au isiyo ya kiufundi.
3. Uainishaji wa matini kufuatana na mada
Hii husaidia kubaini kama matini ni ya kitaaluma, kidini, kisiasa, n.k
MBINU/NJIA ZA TAFSIRI
Katika
kufasiri matini kuna mbinu kadhaa zinazotumiwa ili kufanikisha zoezi
hili. Wataalamu wamejaribu kuainisha mbinu mbalimbali za kufasiri.
Mwansoko na wenzake (1996:24-29) ametoa mbinu nne zinazoonekana kuwa
kuu.
(a)Tafsiri ya neno kwa neno (word to word Translation)
Mbinu
hii humaanisha kutafsiri maneno yakiwa peke yake (pwekepweke) kwa
kufuata maana ya msingi ya lugha chanzi na kutokujali muktadha wa lugha
lengwa. Kila neno na kila mofimu hufasiriwa. Msingi wa tafsiri hii ni
matini chanzi au tuseme mpangilio wake ni sawa na ule wa matini chanzi.
Mbinu hii inatumika zaidi katika uchambuzi wa miundo na maumbo ya maneno
katika lugha.
Mfano:
Kiswahili: A - na - lima
Kiingereza: He/she – present – dig
Kiswahili: Tu - na - soma - kitabu
Kiingereza: We - present - read - book
Kiswahili: Wa - ta - enda - mlima - ni
Kiingereza: They - future - go - hill/mount - at
UBORA NA UDHAIFU
Mbinu
hii inasaidia kutoa taarifa fulani za lugha lengwa. Kwa upande mwingine
mbinu hii inaweza kupotosha maana. Haitoi maana kwa uangavu sana.
Mfano, kwa mbinu hii tamathali za semi zinatafsiriwa kisisisi. Kwa
ujumla mbinu hii si madhubuti.
(b) Tafsiri sisisi (Direct Translation)
Hii
ni tafsiri ambayo maneno hufasiriwa kwa maana zake za msingi katika
matini ya lugha asilia lakini kwa kufuata sarufi ya lugha lengwa.
Mfano:
Kiswahili: Dora, huyu ni mama yangu na huyu ni mjomba wangu
Kiingereza: Dora, this is my mother and this is my uncle.
Kiswahili: Huniwezi
Kiingereza: You can’t me (maana haikubaliki)
Kiswahili: Nimekupata
Kiingereza: I have got you
Kiswahili: Tunapanda mbegu
Kiingereza: We are climbing seeds
Kiswahili: Mimi ni moto wa kuotea mbali
Kiingereza: I am the fire of dreaming far (maana haikubaliki)
UBORA NA UDHAIFU
Mbinu
hii inabainisha mahusiano ya wazungumzaji. Kwa kuangalia tafsiri
zinazotokana na mbinu hii tunaweza kujua kuwa wazungumzaji wanahusiana
kwa namna fulani. Kwa upande mwingine mbinu hii inapotosha maana.
Haikubaliki kwa sababu haifuati muktadha sanifu. Zaidi ya hayo, njia hii
haifanyi kazi katika kutafsiri matini za kifasihi. Kwa mfano.
Kiswahili: Mashoto ana mkono mrefu (yaani mwizi)
Kiingereza: Mashoto has a long hand (badala ya Mashoto is a thief)
(c) Tafsiri ya kisemantiki (Semantic Translation)
Hii
ni tafsiri ambayo huzingatia maana iliyotolewa na mwandishi wa lugha
chanzi na hairuhusiwi kufanya marekebisho katika lugha chanzi ili
kukidhi matakwa ya lugha lengwa. Mfasiri anatakiwa kufasiri kila
kipengele katika matini ya lugha chanzi ili kupata maana iliyokusudiwa
katika lugha lengwa. Hapa mfasiri hufasiri kila neno katika sentensi
kama lilivyo katika lugha chanzi lakini kwa kufuata sarufi ya lugha
lengwa.
Mfano:
Kiswahili:
Mwalimu Maeda alizaliwa mwaka 1980
Alianza shule ya msingi mwaka 1987
Alimaliza shule ya msingi mwaka 1993 na kujiunga na shule ya sekondari Manyara 1994
Hivi sasa yeye ni mwalimu wa shule ya sekondari Mbezi Beach
Kiingereza
Maeda the teacher was born in 1980
He started his primary school in 1987
He completed his primary school education in 1993 and joined Manyara secondary School in 1994
Currently, he is a teacher at Mbezi Beach High School.
UBORA WA MBINU HII
Ubora
wa mbinu hii ya tafsiri ya kisemantiki ni ile hali ya kuwa na uwezo
mkubwa wa kuendeleza lugha lengwa kwa kuingiza miundo na misemo toka
lugha chanzi.
Mfano:
Kiingereza Kiswahili
Goodmorning Asubuhi njema
Yours truly Wako mkweli
How are things at home? Habari za nyumbani?
It leads to Inapelekea
Mbali
na kuendeleza lugha, mbinu hii ya kisemantiki husaidia kunukuu maneno
ya mtu mwingine kwani kila neno linatakiwa litafsiriwe jinsi lilivyo
bila kupoteza hata kipengele kimoja. Tena tafsiri hii haipotoshi maana
au umbo la matini ya lugha chanzi katika matini ya lugha lengwa.
UDHAIFU WA MBINU HII
Tafsiri hii ya kisemantiki haitilii maanani nahau na misemo maalumu inayohusiana na utamaduni wa lugha lengwa.
Mfano:
Kiingereza Kiswahili
Veronica married John Veronica alimuoa John
Like father, like son Kama baba, kama mwana
(d) Tafsiri ya Kimawasiliano (Communicative Translation)
Hii
ni tafsiri ambayo huzingatia hadhira ya lugha lengwa kwa kumjali sana
msomaji wa matini hiyo. Hii ni tafsiri huru kwa sababu mfasiri anaweza
kuongeza au kupunguza maneno ya matini ya lugha chanzi wakati wa
kufasiri ilimradi tu ujumbe uwafikie walengwa kwa namna inayotakiwa bila
kupoteza wazo la matini ya lugha chanzi. Mfasiri anao uhuru wa kutafuta
maneno au vifungu vya maneno yanayolingana na nahau, methali, mila na
desturi na mazingira ya lugha lengwa kwa kuzingatia mwelekeo wake wa
kiutamaduni, kihistoria na kimazingira kwa hadhira lengwa.
Mfano:
Kiingereza Kiswahili
Veronica married Chris Chris alimuoa Veronica
Veronica aliolewa na Chris
Pia,
katika tafsiri ya kimawasiliano hadhira lengwa huelewa kwa urahisi
tafsiri ya kimawasiliano kwa sababu ni rahisi kuhusisha kila kisemwacho
na hali halisi katika mazingira yao.
Vilevile,
tafsiri hii huweza kuboresha au kusahihisha kifikiriwacho kuwa
kilipotoshwa na matini ya lugha chanzi ili kiweze kueleweka vizuri
katika matini ya lugha lengwa. Wakati mwingine tafsiri ya kimawasiliano
huweza kubadilika kulingana na mabadiliko ya kihistoria, kiitikadi na
kimazingira.
Hata
hivyo, tafsiri ya kimawasiliano ina udhaifu wa kutokuwa na uwezo wa
kuendeleza na kuingiza miundo au misemo kutoka lugha asilia kwenda lugha
lengwa. Hali hii inatokana na ukweli kuwa tafsiri hii haizingatii
miundo, misemo, na umahiri wa lugha asilia wakati wa kufasiri bali
huzingatia wazo la jumla la kiutamaduni kwa lugha lengwa.
Vilevile,
udhaifu mwingine katika tafsiri ya kimawasiliano hujitokeza pale
mfasiri anapoegemea sana kwenye mawazo, historia, utamaduni, mazingira
na itikadi ya lugha lengwa. Kwa mfano katika mwaka 2002 vyombo vya
habari vilisikika vikitangaza.
His excellency president Sadam Hussein (vyombo vya Iraq)
Gaidi Sadam Hussein (vymbo vya habari vya Marekani)
MCHAKATO WA TAFSIRI
Mfasiri
anapaswa kwanza kuainisha matini kabla ya kuanza hatua ya maandalizi.
Kuainisha matini ni kitendo cha kuzigawa matini katika aina mbalimbali
kutokana na mahitaji yanayotofautiana ya kifasiri kwa kila aina ya
matini. Uainishaji wa matini hujikita katika mikabala mitatu ambayo ni Uainishaji wa matini kufuatana na istilahi, mada na kufuatana na dhima ya lugha.
Baada
ya kuainisha matini, mfasiri hufanya shughuli ya uchambuzi wa matini
kwa mtazamo wa tafsiri lengwa kwa kuzingatia usomaji wa matini nzima,
kubaini lengo na mtindo wa matini chanzi. Uchambuzi wa matini
ukikamilika, kazi inayofuata ni kuifasiri matini chanzi. Mchakato wa
kufasiri ni kipengele muhimu katika tafsiri ambao hufuata hatua saba
zifuatazo.
1. Maandalizi
Katika
hatua hii, mfasiri huhitaji kufahamu vizuri maudhui ya matini ya lugha
chanzi. Mfasiri huisoma matini nzima ya lugha chanzi ili kubaini ujumbe
wake, mtindo wake na kuziwekea alama maalumu sehemu zenye utata au
ugumu. Pia mfasiri hubaini usuli wa matini ili kupata taarifa za
mwandishi, malengo yake, utamaduni wa mwandishi na wasomaji (hadhira) wa
matini chanzi. Vilevile mfasiri huzingatia sifa za kiisimu za matini
chanzi na kuandika katika kijitabu maalumu msamiati na istilahi muhimu
na maneno ya kiutamaduni.
2. Uchambuzi
Katika
hatua hii, mfasiri huchunguza kwa makini maneno pamoja na maelezo
muhimu ya matini chanzi yaliyoandikwa katika hatua ya maandalizi. Zoezi
hili hufanywa kwa kutumia marejeleo mbalimbali kama vile kamusi, orodha
za msamiati na istilahi mpya.
3. Uhawilishaji
Katika
hatua hii, mfasiri huhawilisha mawazo, maana na ujumbe kutoka kwenye
matini chanzi kwenda kwenye matini lengwa. Mfasiri anaweza kufanya
uamuzi juu ya dhanna za kisarufi zinazoweza kutumiwa kwenye matini
lengwa kuelezea maana za matini chanzi kwa wepesi na ubora unaotakiwa.
4. Rasimu ya kwanza
Shughuli
ya uhawilishaji huzaa rasimu ya kwanza ambayo ni matini mpya katika
lugha lengwa. Mfasiri hupata nafasi ya kwanza ya kufanya marekebisho kwa
kuzingatia umbo la matini lengwa kila inapowezekana. Vilevile, mfasiri
anashauriwa muda wote afikirie juu ya hadhira anayoilenga pamoja na
lengo la matini chanzi.
5. Udurusu wa rasimu ya kwanza
Hatua
hii hutoa nafasi ya kwanza ya kusahihisha matini iliyokwisha tafsiriwa.
Mfasiri anashauriwa asome rasimu nzima ya tafsiri kwa sauti ili aweze
kufanya yafuatayo:
- Kusahihisha makosa ya kisarufi na kimuundo ya tungo mbalimbali
- Kunyoosha sehemu zenye tafsiri ya mzunguko na matumizi ya sinonimia zisizo za lazima
- Kuona kuwa maana zilizohawilishwa kwenye matini lengwa ni sahihi ukilinganisha na zile za matini chanzi
- Kubaini iwapo mada au ujumbe mkuu wa matini unajitokeza waziwazi katika tafsiri
6. Kusomwa kwa rasimu ya kwanza na mtu mwingine
Katika
hatua hii, mfasiri humpatia mtu mwingine ambaye huisoma na kuona kama
inaeleweka na ina mtiririko mzuri wa mawazo ili isomeke kama tafsiri
pale inapowezekana. Dhima kuu ya msomaji wa pili ni kuona kama tafsiri
iko sahihi, inaeleweka na ina mtiririko mzuri unaokubalika. Pia msomaji
wa pili huweza kutoa mapendekezo juu ya marekebisho yanayohitajika
kufanywa baada ya kubaini udhaifu wa tafsiri aliyoisoma.
7. Usawidi wa rasimu ya mwisho
Hatua
hii ndiyo hatua ya mwisho katika mchakato wa tafsiri ambao hufanyika
baada ya mfasiri kupata maoni ya msomaji wa pili. Hapa mfasiri huyatumia
mapendekezo na maelekezo ya msomaji wa pili ili kuisahihisha tena
tafsiri yake na hatimaye kutoa rasimu ya mwisho ya tafsiri.
UMUHIMU WA MCHAKATO WA TAFSIRI
Husaidia mfasiri kufanya maandalizi yote muhimu ya tafsiri yanayohitajika na hivyo kupata maana sahihi ya istilahi mbalimbali.
Husaidia mfasiri kutoa tafsiri sahihi ya matini chanzi kwenda katika matini lengwa.
Huwafanya
walengwa kuelewa ujumbe uliomo katika matini chanzi kwani mfasiri
hufasiri kwa kuzingatia mazingira na utamaduni wa hadhira lengwa.
Hufanya kazi ya tafsiri kuepuka makosa madogomadogo ya kimaana na kimuundo katika matini lengwa.
Hurahisisha kazi ya kutafsiri na kuifanya kuwa nyepesi zaidi na isiyochosha.
TOFAUTI KATIKA TAFSIRI
Swali: “Inadaiwa kuwa mfasiri ni msaliti kwani hawezi kukwepa kusaliti matini asilia au matini lengwa.” Jadili.
Kwa
mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu ya TUKI toleo la pili la 2004,
Msaliti ni mtu anayeshirikiana na maadui wa nchi yake, mtu anayefanya
vitendo viovu dhidi ya nchi yake, haini, mtu anayechonganisha ndugu au
majirani ili wakosane.
Kutokana
na fasili ya kamusi juu ya msaliti tunaweza kusema kuwa, msaliti wa
kazi ya tafsiri ni mtu anayekiuka kanuni, sheria na taratibu za matini
chanzi au matini lengwa kwa ajili ya kunufaisha au kukomoa hadhira
lengwa.
Usaliti
wa mfasiri unasababishwa na kuegemea upande mmoja kutokana na upungufu
katika tafsiri. Kwa hakika hakuna matini lengwa iliyo sawa kabisa na
matini chanzi.
Tofauti
za kiisimu, kiutamaduni, kihistoria na kimazingira baina ya lugha
katika matini asilia na matini lengwa hufanya iwe vigumu kutafsiri
mawazo ya lugha moja katika lugha ingine kwa kiwango sawa.
Baadhi
ya mambo ambayo husababisha usaliti katika tafsiri ni pamoja na tofauti
za kiisimu, kifasihi, kiitikadi, kimtindo, misemo, vitendawili, nahau,
mazingira na mila.
1. Tofauti za kiisimu
Tofauti
za maumbo, miundo na maana kati ya lugha ya Kiswahili na lugha za Ulaya
husababisha tafsiri kuwa na upungufu. Maumbo ya Kiingereza kwa mfano
huruhusu kauli nyingine elekezi kutoonesha umoja na wingi wa wahusika.
Mfano huu wa maumbo huwezesha kutoa tafsiri pana zaidi. Kauli hizi
zinapotafsiriwa katika matini lengwa, mathalan Kiswahili hulazimu
kubainisha vipengele vyote.
Mfano:
Kiingereza Kiswahili
No entrance Usiingie ndani
Quiet please Usipige kelele
No smoking Usivute sigara
Kutokana na mifano hiyo ni kwamba tafsiri ya Kiswahili hujibana zaidi. Ukisema Usipige kelele inamaana
wewe na sio mimi au yeye. Kwa upande wa miundo kuna baadhi ya wafasiri
huhawilisha ruwaza za sintaksia ya Kiingereza katika Kiswahili na hivyo
kufanya tafsiri zao kuwa na mushikeri.
Kwa mfano:
Kiingereza Kiswahili
Nine thousand Tisa elfu
Five million Tano milioni
Kwa upande wa maana, maneno mengine katika Kiingereza hayaakisi ipasavyo katika tafsiri za Kiswahili.
Kwa mfano:
Kiingereza Kiswahili
Intensive care unit (ICU) Chumba cha wagonjwa mahututi
Katika maana hiyo hakuna sehemu katika Kiingereza inayotaja mahututi.
2. Tofauti za kifasihi
Taarifa
zilizomo katika fasihi huangaliwa kisanii na hivyo huhitaji wasomaji
wafanye bidii katika uchambuzi ili wapate maudhui ya fasihi ihusikayo.
Kwa mfano; Ndulute (1994) anasema kuwa kutafsiri mashairi ya Shaaban
Robert ni kitu kinachovutia lakini pia ni cha hatari kutokana na mawazo
yake mazito na ya kina, pia falsafa yake na usanii wake kwa ujumla;
mfano katika shairi la Ua mfasiri anaweza kujiuliza je, Ua linalozungumziwa hapa ni lipi? Ua la mmea, penzi au mauaji. Je, mfasiri atatoa fasiri ipi kwa lugha lengwa pasipo kupoteza maana wala kusaliti lugha chanzi.
3. Tofauti za Kiitikadi na Kihisia
Katika tafsiri nyingi za vitabu na magazeti itikadi na hisia za wafasiri zinaweza kuathiri matokeo ya tafsiri zao.
Kwa mfano:
Kiingereza Kiswahili
Merchants of Venice Mabepari wa Venisi
Katika jina la kitabu hicho, Nyerere alitafsiri Merchantskama mabepari badala ya wafanyabiashara ambayo ndiyo tafsiri sahihi zaidi ya Merchants.
Hii inamfanya Nyerere aseme hivyo kwa sababu ya itikadi na hisia
alizonazo kuwa wafanyabiashara ni mabepari hivyo ni wanyonyaji.
4. Tofauti za Mtindo
Mara
nyingi inakuwa vigumu kueleza dhanna na taarifa kwa kufuata mtindo
unaotakiwa katika uwanja huo. Hii ni kwa sababu, Kiswahili kama zilivyo
lugha nyingine za kiafrika hazijawa na tofauti dhahiri za mtindo.
Kwa mfano:
Kiingereza Kiswahili
Lend me your ears Naomba mnisikilize
May I have your attention Naomba mnisikilize
Tafsiri ya Kiingereza inaonekana kuwa pana zaidi kuliko ya Kiswahili, yaani kuna namna zaidi ya moja ya kuulizia jambo moja.
5. Tofauti za Mazingira na Mila
Kwa
kawaida mazingira, mila na desturi kati ya watumiaji wa lugha asilia na
wale wa lugha lengwa mara nyingi hufanya tafsiri kuwa ngumu. Kwa mfano maneno karibu tena yanapotumiwa na mswahili anapomuaga mgeni wake hayana maana ya moja kwa moja na yale ya Kiingereza welcome again bali humaanisha goodbye.
6. Tofauti za Misemo, Vitendawili, Methali na Nahau
Maneno haya huendana na utamaduni wa watu fulani unaotofautiana kutoka jamii moja na nyingine.
Mfano:
- funga virago, enda joshi (nahau),
- mwenda pole hajikwai (methali),
- popo mbili zavuka mto (kitendawili),
- kata shingo, kula kichwa (misemo).
Kwa
kuwa vitendawili, nahau, methali na misemo huendana na utamaduni wa
watu fulani, hivyo tafsiri ya maneno kama hayo huweza kukumbwa na
matatizo kama vile; kutopatikana kwa visawe vya kimuundo vya mafungu
kama hayo katika lugha lengwa.
Tatizolingine ni upatikanaji wa visawe mwafaka vya dhanna na maana zake katika lugha lengwa.
Wafasiri
wamekuwa wakijiuliza kama kweli misemo na tungo za namna hiyo zinaweza
kufasirika inavyopaswa. Misemo ya Kiingereza kwenda Kiswahili inaleta
utata sana katika kufasiri iwapo mfasiri hajui mazingira ya lugha
asilia.
Kwa mfano:
Kiingereza Kiswahili
A hot debate Mjadala wa moto
Mjadala mzito
Mjadala mkali
UMUHIMU WA TAFSIRI KATIKA JAMII
Maendeleo
ya jamii yoyote ile kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi hutegemea sana
maendeleo ya sayansi na teknolojia ndani ya jamii husika. Sayansi na
teknolojia ni uwanja wowote ule unaohusu mada za kimaarifa na kiufundi.
Sayansi na teknolojia inahusu suala la elimu katika uhandisi, tiba,
elektroniki, sayansi ya nyukilia na kadhalika.
Kazi
ya tafsiri ndio msingi mkuu katika jamii kupata maendeleo katika suala
la mawasiliano juu ya masuala yanayohusu siasa, uchumi na utamaduni.
Katika karne hii ya sayansi na teknolojia ambapo dunia inaungana na
kuonekana sawa na kijiji kwa sababu ya utandawazi. Kwa hiyo tafsiri ya
istilahi mbalimbali hasa zile za kisayansi ni muhimu sana kwa maendeleo
ya jamii ya sasa kwa sababu hurahisisha suala la mawasiliano katika
pande zote.
Mfasiri
wa istilahi hasa za kisayansi hana budi kuwa makini sana anapotafsiri
istilahi zinazohusika. Kwa kawaida tafsiri ya istilahi za sayansi na
teknolojia zina lengo moja kuu ambalo ni kutoa ujumbe toka lugha asilia
na kuupeleka katika lugha lengwa kwa kutumia lugha ya kiulimwengu ambayo
haifungamani na utamaduni wa jamii fulani. Kwa hiyo mambo yafuatayo
yanafaa kuzingatiwa katika tafsiri mbalimbali hasa zile za kisayansi.
Kwanza, istilahi sharti ziwe toshelevu yaani ziakisi vilivyo sifa za dhanna zinazowakilishwa. Pili, istilahi sharti zifuate mfumo wa kisarufi wa lugha lengwa. Tatu, istilahi sharti ziwe fupi na zenye kueleweka na Nne, istilahi hasa za kisayansi yafaa ziwakilishe maana moja tu na pale inapowezekana zisiwe na sinonimia.
Mambo
yote manne yaliyotajwa hapo juu yakitekelezeka, tafsiri hutoa au huzaa
matunda mema kwa jamii husika katika nyanja za kisiasa, kiutamaduni na
kiuchumi katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia. Zifuatazo ni
baadhi ya faida za tafsiri kwa jamii lengwa.
1. Kwanza, kazi ya tafsiri ni muhimu kwa jamii husika kwa sababu husaidia kimatumizi katika istilahi za lugha ya kufundishia kwa mfano
lugha ya Kiingereza ambayo hutumika katika suala la kufundishia sehemu
mbalimbali duniani imetafsiri lugha mbalimbali kama vile Kigiriki na
Kilatini.
Mfano:
Kigiriki Kiingereza
Physics Physics
Khemia Chemistry
Kilatini Kiingereza
Moles Molecule
Katika mfano huo, lugha asilia ya maneno ya Kiingereza Physics na Chemistry ni Kigiriki ambapo neno molecule lugha asilia ni Kilatini. Pia katika lugha ya Kiswahili istilahi Fizikia, Kemia na molekiulini
maneno (istilahi) yaliyotafsiriwa kutoka lugha ya Kiingereza.
Wanafunzi, walimu, wahadhiri na jamii kwa ujumla wamefaidika na
wanaendelea kufaidika na matumizi ya istilahi hizo za kisayansi kwa
sababu ya kazi nzuri ya tafsiri.
2. Pili,
kazi ya tafsiri ni muhimu kwa jamii lengwa kwa sababu husaidia
kutafsiri istilahi mbalimbali za kimaarifa au kiufundi kutoka lugha
asilia yaani lugha ambayo haieleweki sana kwa jamii nyingine inayotumia
lugha lengwa na kuweza kueleweka na kutumiwa na wengi kama siyo wote
katika lugha lengwa kwa sababu ya kazi nzuri ya tafsiri.
Kwa mfano:
Kiingereza Kiswahili
Asprin Aspirini
Tyre Tairi
Globalization Utandawazi
E-mail Barua pepe
Fax Namba nukushi
3. Tatu,
kazi ya tafsiri ni muhimu kwa jamii husika kwa sababu husaidia katika
kubuni au kuunda majina ya biashara katika lugha ya Kiswahili ambapo
maneno ya kigeni hupatiwa maumbo ya Kiswahili.
Kwa mfano:
- Sabuni chapa FOMA (kutokana na “foam”)
- Sabuni chapa KODROI (kutokana na “Corduroy”)
- Kileo chapa KONYAGI (kutokana na “Cognac”)
4. Nne,
kazi ya tafsiri ni muhimu kwa jamii lengwa kwa sababu husaidia lugha
lengwa ambayo hutumiwa na wengi ili kujitosheleza katika istilahi
mbalimbali. Kiswahili ni mfano mzuri wa lugha lengwa ya namna hiyo kwa
sababu Kiswahili ni lugha iliyosheheni istilahi ambazo chimbuko lake ni
lugha mbalimbali.
Kwa mfano:
Neno la Kiswahili Chimbuko lake/Lugha
Shati Kiingereza
Shamba Kifaransa
Nanasi Kireno
Shehe Kiarabu
5. Tano,
kazi ya tafsiri ni muhimu kwa jamii husika kwa kurahisisha na
kuchapusha mawasiliano ya kitaaluma kwa waandishi wa vitabu vya
kitaaluma, walimu, wahadhiri na wanafunzi. Pia hurahisisha mawasiliano
katika makongamano ya kawaida na makongamano ya kimataifa kuhusu
maendeleo ya jamii kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi; vilevile kazi ya
tafsiri ni muhimu sana katika mihadhara ya kidini inayoendeshwa
kimataifa katika nchi mbalimbali. Hapa suala la ukalimani hutiliwa
maanani zaidi ili kurahisisha mawasiliano.
6. Sita,
kazi ya tafsiri ni muhimu kwa jamii lengwa kwa sababu vitabu mbalimbali
vinavyosomwa na watu wa matabaka yote katika jamii watu wazima, watoto,
n.k. huweza kueleweka kwa wote kwa sababu ya kazi nzuri ya tafsiri. Kwa
mfano Bibliatakatifu ni kitabu ambacho kimetafsiriwa katika
lugha mbalimbali kwa sababu kinasomwa na watu wa tabaka zote katika
jamii karibu duniani kote.
7. Saba,
kazi ya tafsiri ni muhimu kwa jamii husika hasa karne hii ya sayansi na
teknolojia kwa sababu huwa katika mfumo wa kidhanna na huwakilisha
dhanna moja tu pale inapowezekana.
Kwa mfano:
Kiingereza Kiswahili
Machine Mashine
Prove Thibitisha
Protestant Mprotestanti (Muasi)
8. Nane,
kazi ya tafsiri ni muhimu kwa jamii lengwa kwa sababu husaidia istilahi
za kisayansi na kiteknolojia kutoka lugha asilia kuwa sahihi, kwa
kuandikwa na kutamkwa kwa urahisi katika lugha lengwa.
Kwa mfano:
Kiingereza Kiswahili
Radio Redio
Television Televisheni
Computer Kompyuta
9. Tisa,
kazi ya tafsiri ni muhimu kwa jamii husika kwa sababu husaidia uhai wa
lugha, yaani kubadilika kimsamiati/istilahi kulingana na wakati na hasa
katika kuakisi matukio mbalimbali. Mara nyingi mabadiliko au istilahi
mpya hujitokeza kutokana na mambo mapya yanayoibuka katika jamii na
hivyo kuleta uhai katika lugha lengwa.
Kwa mfano:
Kiingereza Kiswahili
Stakeholders Mwanzo – washika dau
Sasa - wadau
Globalization Mwanzo – Udandarizi
Sasa - utandawazi
HIV/AIDS Mwanzo – Juliana
Sasa - UKIMWI
Uhai
wa matumizi ya maneno hayo umepata mashiko katika siku za hivi
karibuni; awali ilikuwa vigumu sana kwa istilahi hizo kutumiwa katika
lugha ya Kiswahili katika miaka ya mwanzoni mwa 1980 na kurudi nyuma.
Istilahi ambayo ilisikika sana ilikuwa ni ukoloni mamboleo badala ya
neno la sasa la utandawazi.
10. Kumi,
kazi ya tafsiri ni muhimu sana kwa jamii husika hasa katika karne hii
ya sayansi na teknolojia kwa sababu husaidia sana katika vyombo vya
habari kama vile redio, televisheni na magazeti katika kufikisha ujumbe
kwa walengwa wote. Redio, televisheni na magazeti ni vyombo vya habari
vitumikavyo kutolea taarifa hasa zilizo mpya kwa sababu huhusiana na
uvumbuzi mpya wa kisayansi na kiteknolojia. Mara nyingi vyombo hivi
hupata taarifa zake nyingi kutoka Mashirika ya habari ya kigeni kama
vile REUTERS, CNN, SKYNET, n.k ambapo taarifa zake huwa katika lugha za
kigeni kama vile Kiingereza, kwa hiyo vyombo vya habari hulazimika
kuzitafsiri taarifa husika kabla ya kuzitangaza au kuzichapisha.
Kwa
ujumla kazi ya tafsiri ni kazi muhimu sana kwa jamii yoyote ile hasa
katika karne hii ya sayansi na teknolojia. Kwa hiyo, mfasiri anapaswa
kujua taaluma ya somo ambamo istilahi zinatoka kwa sababu ni mtu
anayeshirikisha watumiaji wote wa lugha katika uvumbuzi wa matumizi ya
lugha lengwa. Vilevile, tafsiri ni fani kamili yenye kuhitaji ujuzi,
ustadi na uwezo maalumu wa lugha mbili au zaidi ambazo mfasiri
atazitumia katika kazi yake ya kufasiri.
Mwisho,
kwa kuwa lugha ya Kiswahili matumizi yake yanapanuka kwa haraka sana
tafsiri ya istilahi inapaswa kuwa kazi ya kudumu inayohitaji mpango
maalumu wa utekelezaji ikiwa ni pamoja na kufanya kazi hiyo.
Hasara za Tafsiri katika Utamaduni.
Baada
ya kuelezea faida mbali mbali za tafsiri katika utamaduni wa Tanzania
na Afrika kwa jumla. Zifuatazo ni hasara za tafsiri kwa jamii.
Ø Tafsiri imesababisha jamii za waafrika kuiga utamaduni wa mataifa ya nje.
Kwa
mujibu wa Kamati ya Taarifa za Tovuti Kuu ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania zilizofanyiwa marekebisho mwaka (2015) zinaeleza
kuwa: “Utamaduni wa Tanzania ni matokeo ya athari za kiafrika, kiarabu,
kizungu na kihindi. Maadili, mila na desturi za kiafrika zinabadilishwa
polepole na maisha ya kisasa, ingawa kwa kasi ndogo sana miongoni mwa
jamii ya wamasai”. Kutokana na maelezo hayo ni wazi kuwa, jamii nyingi
za waafrika zikiwemo za watanzania, zimeanza kuathirika kwa kuiga mila
na tamaduni za kimagharibi kupitia tafsiri za kazi mbali mbali za
kijamii na mpaka sasa hali hiyo inaendelea kupitia njia nyengine mbali
mbali kama vile utalii na maingiliano baina ya waafrika, wazungu,
waarabu na wahindi.
Ø Tafsiri imesababisha mivutano na makundi ya kidini kati ya jamii za waafrika.
Ukirudia
historia ya tafsiri katika nchi za ulaya, utaona, mnamo karne ya 16
kulikuwa na muamko mkubwa wa kidini ambao ulianzia Ujerumani na
kusambaa katika maeneo mbalimbali ulimwenguni. Mwamko huu ulipinga
muundo, mwelekeo, falsafa na mafunzo mengi ya kanisa katoliki ya wakati
huo na matumizi ya lugha moja ya kilatini katika misa na mafunzo ya
kidini. Hali hii ilisababisha mgawanyiko katika dini ya kikiristo. Watu
mbali mbali walitafsiri maandiko matakatifu katika lugha mbali mbali.
Kwa mfano Martin Luther King alitafsiri Biblia takatifu kutoka kilatini
kwenda lugha ya Kiingereza (1611) ikaitwa “The King James Bible”, pia
alitafsiri Biblia kutoka Kilatini kwenda lugh ya Kijerumani. Baada ya
kuona tafsiri ya Kilatini imeacha baadhi ya vipengele katika maandiko
hayo matakatifu, Jarome alitafsiri Biblia ya Kigiriki na Kiebrania
kutoka lugha ya Kilatini.
Kutokana
na maelezo hayo ni wazi kuwa, mgawanyiko wa kidini haukuishia katika
nchi za ulaya na katika dini ya kikristo peke yake bali ulienea
ulimwengu mzima zikiwemo nchi za afrika kwa sababu ya kutafsiriwa
maandiko matukufu mbalimbali kama vile biblia, kur-an na vitabu vyingine
vya mafunzo ya dini . Sasa hivi ukichunguza katika dini zote hasa za
uislamu na ukristo utakuta mivutano kati ya waumini juu ya makundi yao.
Kwa mfano katika ukristo utakuta makundi kama vile wakatoliki, wasabato
na kadhalika. Ama kwa upande wa dini ya kiislamu kuna makundi kama vile
suni, ibadhi, shia na kadhalika. Yote hayo yametokana na kufasiriwa kwa
maandiko ya dini na ufahamu wa waumini katika maandiko hayo.
Ø Baadhi ya njia za tafsiri husababisha kwenda kinyume na sarufi ya lugha lengwa au utamaduni wa lugha lengwa.
Hoja
hii anajiegemeza zaidi katika aina za tafsiri ambazo ni tafsiri ya neno
kwa neno, tafsiri sisisi, tafsiri ya kisemantiki na tafsiri ya
mawasiliano. Lakini hapa tuangalie zaidi tafsiri ya neno kwa neno. Mara
nyingi tunapotafsiri sentensi au matini kwa kutumia njia hii, lazima
tufuate sarufi ya lugha chanzi hivyo husababisha makosa ya kimuundo na
kimaana ya lugha lengwa. Mifano ifuatayo inafafanua zaidi.
Kiingereza kwenda Kiswahili:
I / like / banana / s / more / than / orange / s /
Mimi / penda/kama / ndizi / wingi / zaidi / kuliko / chungwa / wingi /
Kiswahili kwenda Kiingereza
Wa / toto / wa / dogo / wa / na / imba / kwa / furaha /
Plural / child / plural / small / they / present continues tense (singular) / by/for / happiness
Unapochunguza
mifano ya hapo juu, utakuta kuwa ufuataji wa sarufi ya lugha chanzi
husababisha kuharibu sarufi ya lugha lengwa na kupoteza maana
inayokusudiwa kutoka lugha chanzi.Vile vile tunapotafsiri methali,
misemo, nahau na matini nyingine za kifasihi, kwa kutumia njia yoyote ya
tafsiri, mfasiri anaweza kwenda kinyume na utamaduni wa lugha lengwa
endapo atakuwa si mzoefu wa utamaduni wa jamii hiyo.
Ø Tafsiri husababisha matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili katika maandishi.
Moja
ya njia ya uchanganyaji wa lugha katika maandishi ni tafsiri. Watu
wengi wanaojishughulisha na kutafsiri matini mbalimbali kwenda lugha ya
Kiswahili huathiriwa na kazi hiyo na kuwasababishia kuchanganya lugha
pale wanapoandika kazi nyingine za Kiswahili jambo ambalo ni kinyume na
utamaduni wa mtanzania. Jambo hili huweza kujitokeza kwa waandishi wa
makala mbalimbali za Kiswahili lakini pia wahariri wa magazeti.
Hapa nataka nifahamike kuwa, sipingi utumiaji wa neno au maneno ya
lugha nyingine kama Kiingereza ambayo yana lengo la kutoa ufafanuzi
zaidi juu ya jambo fulani ambapo mara nyingi maneno hayo huwekwa katika
mabano. Bali nakusudia uchanganyaji wa lugha kwa ujumla. Mfano katika
upekuaji wa makala mbalimbali nimegundua matumizi hayo kama
ifuatavyo:-
“Mimi
ninadhani values za jamii ni kioo ambacho maendeleo yoyote that we
want and to find out kwa udi na uvumba lazima ya reflect, kama we have
not values za maana ni vipi tutaendelea”
Kwa
hiyo mtu anayetumia lugha kama inavyoonekana katika maelezo yaliyopo
hapo juu, mimi kwa maoni yangu naona mtu huyo ameathiriwa na lugha ya
Kiingereza au kutokana na kufanya kazi nyingi za tafsiri.
Kukalimani
Kutokana
na fasili ya TUKI, tunaweza kusema kuwa kukalimani ni kuhawilisha
mawazo moja kwa moja kutoka lugha moja ya mazungumzo kwenda lugha ingine
ya mazungumzo bila kupoteza, kupotosha au kubadili maana. Mtu anaweza
kukalimani mazungumzo ya Kiingereza au Kifaransa kwenda Kiswahili.
Shughuli ya kukalimani inasaidia kuunganisha na kujenga uhusiano mwema
kati ya tamaduni mbili au zaidi kwa njia ya mazungumzo toka lugha moja
hadi lugha nyingine.
Hata
hivyo, wataalamu wa kukalimani sio kwamba wanafasili mazungumzo au
maongezi tu kwa lugha lengwa (ya hadhira), pia hubainisha na kupambanua
dhanna husika kwa mujibu wa muktadha uliopo bila kupoteza lengo la
mzungumzaji wa lugha asilia (fanani). Mkalimani hupaswa kuelewa lengo
mahususi la mazungumzo ili kukalimani kinachozungumzwa kwa usahihi.
Inamlazimu mkalimani kuwa makini sana na tamaduni zinazohusiana sana na
lugha husika.
Wataalamu
wa kukalimani wanapaswa kuwa makini sana katika kuelewa kwa usahihi
kile kinachozungumzwa kwenye lugha asilia na lugha lengwa ili kufafanua
au kueleza wazo au dhanna kwa usahihi. Kwa kawaida, mkalimani hubadili
maneno ya lugha chanzi na kuyaweka katika maana ya lugha lengwa na kisha
kubadili njia ya mazungumzo. Kwa hiyo, shughuli ya kukalimani inahitaji
uwezo mkubwa wa kusikia, kuelewa na kutunza kumbukumbu za kile
kinachozungumzwa.
Mfano wa kukalimani:
Muuza Duka: Karibu shangazi
Mkalimani: welcome aunt
Mnunuzi: Thank you. How are you?
Mkalimani: Asante. Habari gani?
Muuza Duka: Nzuri, nikusaidie nini?
Mkalimani: Fine. What should I sell to you today?
Mnunuzi: I want to buy three kilos of sugar, two packets of tea
Leaves, one tin of powdered milk and two litres of
Cooking oil. How much?
Mkalimani: Ninataka kununua sukari kilo tatu, majani ya chai pakiti
mbili, maziwa ya unga kopo moja na mafuta ya
kupikia lita mbili. Bei gani?
Muuza Duka: Sukari kilo tatu ni shilingi 4,500/- majani ya chai
mazuri ya Tanzania pakiti mbili ni shilingi 1,600/-
maziwa ya unga kopo la NIDO ni shilingi 4,000/= na
lita mbili za mafuta ya kupikia ya alizeti ni shilingi
7,000/- jumla ni shilingi 17,100/-
Mkalimani: Three kilos of sugar is Tsh 4500/-, a good Tanzania
packets of tea leaves is Tsh 1600/-, one tin of NIDO
powdered milk is Tsh 4000/- and two litres of
sunflower cooking oil is Tsh 7000/-. The total is
17,100/- only.
Mnunuzi: Excuse me!Is there washing soap?
Mkalimani: Samahani! Kuna sabuni ya kufulia?
Muuza Duka: Ndiyo! Nina sabuni za miche tu. Sina sabuni za unga
Mkalimani: Yes, I have bar soap only. I don’t have powdered soap
Mnunuzi: How much is it?
Mkalimani: Bei gani?
Muuza Duka: Shilingi mia sita
Mkalimani: Six hundred shillings
Mnunuzi: Okay, please give me two bars. Do you have match
boxes?
Mkalimani: Sawa, nipatie miche miwili. Una vibiriti?
Muuza Duka: Ndiyo kiberiti kimoja ni sh 50/-
Mkalimani: Yes I do. One is 50/-
Mnunuzi: Okay, here is the money
Mkalimani: Sawa. Hizi hapa pesa zako
Muuza Duka: Asante sana na karibu tena
Mkalimani: Thank you and welcome again.
MBINU ZA KUKALIMANI
Kuna mbinu mbalimbali za kukalimani. Hata hivyo wataalamu wengi wa ukalimani wameainisha mbinu kuu mbili ambazo ni Kukalimani papo kwa papo na Kukalimani kwa kufuata dhanna/wazo.
1. Kukalimani papo kwa papo
Kukalimani
papo kwa papo ni mbinu ya kukalimani ambayo hutumika sana katika
taaluma. Mbinu hii humtaka mkalimani kusikiliza na kuongea huku
akionesha ishara mbalimbali kwa mujibu wa mazungumzo yanayoendelea.
Mkalimani anatakiwa kuwa mwelewa na makini katika kutarajia mwisho wa
sentensi ya mzungumzaji wa mada husika katika mazungumzo yanayoendelea.
Kukalimani
papo kwa papo mara nyingi hutumika katika mikutano ya kimataifa, kwenye
mahakama za kimataifa na katika mikutano mikubwa na midogo ya mahubiri
ya kidini. Kwa mfano, wakalimani katika mikutano ya kimataifa hukaa au
husimama wakiwa wamevalia vipokea sauti ambavyo hubanwa kichwani na
kuongea kwa kutumia vipaza sauti vinavyoelekeza sauti zao moja kwa moja
kwa walengwa.
Mkalimani
hawezi kuanza tu kazi ya kukalimani kabla ya kuelewa maana ya sentensi
kwa ujumla. Kwa hiyo hali hii hudhihirisha ugumu wa shughuli ya
kukalimani kwa sababu mkalimani anatakiwa akalimani sentensi aliyoisikia
na kuiweka katika lugha ya hadhira lengwa huku akisikiliza na kuelewa
sentensi inayofuata. Haitakiwi mkalimani atumie muda mrefu kusikiliza
kisha kuongea kwa sababu akifanya hivyo atapoteza baadhi ya maneno
yanayoongelewa na kupoteza maana ya mazungumzo yanayoendelea kwa wakati
huo.
2. Kukalimani kwa kufuata dhanna au wazo
Kukalimani
kwa kufuata dhanna au wazo pia ni mbinu ingine inayotumika katika
shughuli ya kukalimani. Mbinu hii humtaka mkalimani kusikiliza kwa muda
kisha kukalimani kwa lugha ya hadhira lengwa baada ya kupata dhanna
kutokana na maelezo yaliyotolewa na mzungumzaji wa lugha asilia.
Mkalimani anaweza kutulia kwa muda kati ya dakika moja hadi tano kabla
ya kukalimani kilichosemwa na mzungumzaji.
Wakati
mwingine mkalimani huweza kunukuu maneno machache kwenye kijidaftari
ili asipoteze dhanna nzima ya mzungumzaji wa lugha asilia wakati wa
kukalimani kilichosemwa na mzungumzaji. Mbinu hii haitumiwi sana na
wakalimani kwa sababu mara nyingi hushindwa kutoa dhanna nzima kutokana
na ukweli kwamba si rahisi kukumbuka kila neno lililotamkwa na fanani
kwa hadhira lengwa.
UMUHIMU WA KAZI YA KUKALIMANI
1. Kazi
ya kukalimani hurahisisha mawasiliano miongoni mwa jamii mbili au zaidi
zenye tamaduni tofauti. Kazi hii hurahisisha na kuchepusha mawasiliano
ya kawaida au ya kitaaluma. Kwa mfano kazi ya kukalimani hurahisisha
mawasiliano katika makongamano ya kimataifa kuhusu maendeleo ya jamii
katika nyanja za siasa, uchumi na utamaduni.
2. Pili,
kazi ya kukalimani husaidia kudumisha amani ya kisiasa na kiuchumi
duniani. Watu waliofarakana huweza kukaa pamoja na kuzungumza chini ya
wasuluhishi wa kimataifa. Kwa mfano nchi nyingi za kiafrika kama vile
Liberia, Ethiopia, Rwanda, Burundi, Kongo-DRC, Angola, Msumbiji, Siera
Leon, Chadi na Nigeria zimepata utulivu baada ya kusuluhishwa na mataifa
ya nje ambayo yanatumia lugha tofauti na za nchi hizo. Ni kazi ya
kukalimani ndiyo iliyosaidia kujenga maelewano ndani ya tamaduni tofauti
za jamii hizo.
3. Tatu,
kazi ya kukalimani husaidia kudumisha amani ya kijamii duniani. Kwa
mfano wahubiri wengi wa kimataifa huweza kupeleka ujumbe wa Mungu sehemu
mbalimbali za dunia zenye lugha tofauti kupitia ukalimani. Wakalimani
huweza kueleza au kufafanua juu ya maana ya mzungumzaji wa lugha asilia
kwa kutumia lugha ya hadhira lengwa.
4. Nne,
kazi ya kukalimani ni nyenzo muhimu sana ya kujifunzia lugha ya pili.
Kwa mfano mtu anayetumia Kiswahili huweza kujifunza lugha ya Kiingereza
kupitia kwa mkalimani. Mtu wa namna hiyo huweza kujifunza na kuelewa
maana ya maneno mbalimbali, matamshi yake na matumizi yake katika lugha
ya mazungumzo. Mtu anayejifunza lugha ya pili kupitia kwa mkalimani
hufaidika na matumizi mbalimbali ya istilahi tofauti za lugha ya fanani
kwa sababu ya kazi ya kukalimani. Hadhira lengwa huwa makini sana na
kujijengea uwezo mkubwa wa kusikiliza, kusikia, kuelewa na kutunza
kumbukumbu za kile kinachozungumzwa.
5.Tano,
kazi ya kukalimani husaidia hadhira lengwa kujifunza pia mawasiliano ya
ishara kama fanani anatumia njia hiyo ya mawasiliano. Mkalimani huweza
kufasili mawasiliano ya ishara au alama anazozitumia mzungumzaji kwa
kuzungumza kwa lunga lengwa.
Sita,
kazi ya kukalimani husaidia uhai wa lugha kulingana na wakati katika
kuakisi mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni yaliyojitokeza
katika jamii husika. Kwa mfano neno Stakeholder katika lugha ya Kiingereza, mwanzo wakalimani walilitamka kuwa ni washika dau katika lugha ya Kiswahili lakini kwa sasa neno hilo linatamkwa kama wadau katika Kiswahili. Pia neno Low class peoplekatika Kiingereza lilitamkwa kama Makabwelalakini hivi sasa ni walalahoi.
SIFA ZA MKALIMANI
Kuna
sifa mbalimbali ambazo mkalimani anapaswa kuwa nazo. Hii ni kutokana na
ugumu wa kazi ya kukalimani. Hata hivyo, wataalamu mbalimbali wa kazi
ya kukalimani wanabainisha sifa kuu tatu kwa ajili ya mkalimani. Sifa
izo ni elimu ya kutosha juu ya lugha zinazotumika. Elimu ya kutosha juu
ya hadhira na uelewa wa matumizi sahihi ya mbinu za kimawasiliano.
1. Uelewa wa kina juu ya lugha zinazotumika
Mkalimani
mzuri ni yule ambaye ana utaalamu wa kutosha katika lugha zinazotumika.
Kwa mfano kama anakalimani Kiingereza kwenda Kiswahili, mkalimani
anapaswa kuwa mtaalamu au mahiri wa lugha mbili yaani Kiingereza na
Kiswahili. Mbali na kuwa mahiri katika lugha mbili au zaidi, pia ni
vizuri mkalimani akawa na uelewa juu ya dhanna anayoikalimani. Mkalimani
anatakiwa kuwa na uelewa juu ya istilahi zinazotumika katika dhanna
husika. Kama ni mahakamani, mkalimani anapaswa kuwa na uelewa wa hali ya
juu wa istilahi za kisheria au kama ni mahubiri ya kidini mkalimani
anapswa pia kuwa na uelewa juu ya istilahi za ki-Biblia au Kuran.
Vilevile, mkalimani anapaswa kwenda na wakati kulingana na lugha
inavyobadilika katika jamii kutokana na mifumo ya kisiasa, kiuchumi na
kiutamaduni iliyopo kwa wakati huo. Mkalimani anapaswa kuelewa angalau
kwa ufupi juu ya jambo linalotarajiwa kuongelewa mbele ya hadhira kutoka
kwa fanani au mtoa mada kabla ya kuanza shughuli ya kukalimani.
2. Uelewa wa kina juu ya hadhira husika
Mkalimani
anapaswa kuielewa hadhira yake kiumri, kielimu, mazingira ya
kijiografia, mtazamo na matarajio yake. Mkalimani anapokuwa na uelewa wa
kina juu ya elimu ya hadhira yake inamsaidia kutumia lugha inayoeleweka
kwa hadhira. Mkalimani anapokuwa na uelewa wa mazingira ya kijiografia
ya hadhira yake inamsaidia kutumia lugha ambayo haikiuki mila na desturi
za jamii husika. Vilevile, mkalimani anapaswa kuelewa umri wa hadhira
yake kwa ujumla ili aweze kutumia lugha inayojenga uhusiano mwema kati
yake na hadhira lengwa.
3. Uelewa wa kina juu ya matumizi sahihi ya mbinu za kimawasiliano
Mkalimani
anapaswa kutumia mbinu mbalimbali za kimawasiliano anapofanya kazi yake
ya kukalimani. Mkalimani hulazimika kutumia mifano na ishara mbalimbali
zinazoeleweka kwa hadhira yake na zenye kuleta maana isiyo na dhanna ya
kimatusi. Mifano hiyo iwe inahusu hadhira kwa lengo la kuelezea kwa
kina kile kilichotamkwa na fanani. Mawasiliano mazuri huambatana na
matumizi mazuri na sahihi ya maneno, sauti na ishara mbalimbali wakati
mkalimani anapofanya kazi ya kukalimani.
Matumizi
mazuri ya maneno huweza kutoa hamasa kwa hadhira juu ya kupenda na
kuendelea kusikiliza kile kinachoelezwa. Mkalimani anapaswa kuepuka
matumizi ya lugha ya mkato na maneno makali. Mkalimani ahakikishe
istilahi anazotumia zinaeleweka vizuri kwa hadhira yake. Kwa kuwa kazi
ya kukalimani huhusu mazungumzo, mkalimani hana budi kutumia sauti nzuri
na yenye mvuto kwa hadhira yake. Matumizi sahihi ya kupanda na kushuka
kwa sauti ya mkalimani huakisi kwa usahihi dhanna inayoongelewa pamoja
na muktadha wa hadhira yake. Sauti inapaswa kusikika kikamilifu kwa
hadhira lengwa kulingana na mada husika. Mkalimani anapaswa kuepuka
kuongea polepole sana au kwa haraka sana.
Vilevile,
mkalimani anapaswa kutumia ishara ili kusaidia hadhira yake kuelewa
zaidi juu ya neno au maneno yaliyotamkwa. Kwa ufupi ni kwamba,
mawasiliano ya ishara ni aina ya mawasiliano ambapo binadamu hutumia
viungo vyake vya mwili kama vile macho, kichwa, mabega, mikono na
vidole, kwa hiyo mkalimani wakati mwingine humlazimu kutumia viungo
vyake vya mwili ili kujenga uelewa wa kina kwa hadhira yake kutokana na
kile kinachosemwa na fanani.