FASIHI YA KISWAHILI, NADHARIYA NA UHAKIKI (T.S.Y.M. Sengo)

FASIHI YA KISWAHILI, NADHARIYA NA UHAKIKI (T.S.Y.M. Sengo)
Utangulizi  
Kuna kusoma na kupata vyeti baada ya kufanikiwa katika mtihani.
Kuna kuelimika, kwa kupitiya visomo, ujuzi na utunduwizi, tajriba za mawanda ya elimu na/au dari za uwezo wa akili wa viwango mbalimbali. Ila za Msomi ni pamoja na magoda – mikogo, dharau na kedi, utovu wa adabu, ufisidi, ufisadi, hujuma, mbwembwe – ulimbwende, kushindwa au uvivu wa kutenda kazi; ugila-unyimi, inda, choyo, fitina n.k. Sifa za Mwenye elimu ni kutambuwa ujinga alionao, kwamba hajuwi kila kitu wala hajuwi anachokijuwa sana; anajitambua kuwa hayafahamu sana anayoyajuwa; tajriba – uzowefu wake ni ule wa kwao na mwahala alimopitiya – shuleni – kazini, maishani; nnje ya tajriba hizo, hana ujuzi wala fahamu. Na hata huko alikopitiya, hakumaliza yote. Mwenye elimu ana manufaa kwa nafsi yake na nafsi za viumbwa vyote vya Muumba wake. Ni katika manufaa hayo kwamba, akiajiriwa kuhudumiya watu au wanyama na ndege, hata mimeya na misitu, mtu huyo ataonekana akizitowa hizo huduma.



FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI
MUHADHARA WA KWANZA
FASIHI NI NINI?
Dhanna ya fasihi imekuwa ikijadiliwa kwa karne nyingi na wataalamu mbalimbali huko ulaya. Dhanna hii imekuwa ikihusishwa na neno la Kilatini Litera lenye maana ya herufi au maandishi. Neno hilo ndilo limefasiriwa kwa Kiingereza kama Literature.
Mitazamo iliyotawala dhanna hii ni mingi kama ifuatavyo:
(a)    Mtazamo wa kwanza ni ule unaodai kuwa literature ni jumla ya maandishi yote katika lugha fulani. Wellek na Warren wanauelezea mtazamo huu kwa kusema kuwa, “ One way is to define Literature as everything in Print. Wellek na Warren (1986:20)
        Udhaifu wa mtazamo huu:
(i)         Mtazamo huu unapanua sana uwanja wa fasihi na kuingiza vitu vyote ambavyo kwa kawaida watu hawavifikirii kuwa ni fasihi kwa sababu tu vimeandikwa.
Mtazamo huu unabagua sehemu kubwa ya fasihi ya ulimwengu ambayo haikuandikwa au kupigwa chapa (Ambayo ndiyo chanzo cha maandishi ya kifasihi mf. Matambiko, ngoma, majigambo, n.k).Katika taaluma ya fasihi katika Kiswahili neno Literature lilitafutiwa namna ya kuitwa na kupewa maneno kama adabu ya lughana fasihi.
Hatimaye neno fasihi likashinda na kupewa ufafanuzi kuwa ni sanaa ya lugha bila kujali kama imeandikwa au la.
(b)    Mtazamo wa pili ni ule unaodai kuwa Literature ni maandishi bora ya jamii ya kisasa yenye manufaa ya kudumu. Hollis Summers anafafanua kuwa; The word literature in its strictness sense means more than printed words, is one of the fine arts. Mtazamo huu unaupa uzito usanii na uwezo wa kubaini fasihi kwa kuihusisha na maandishi na maandiko bora tu.
(c)    Mtazamo wa tatu; unaitazama Literature kama sanaa ya lugha yenye ubainifu bila kujali kama imeandikwa au la. Kwa mtazamo huu nyimbo na masimulizi ya kisanaa ni fasihi.
Mtazamo huu uliambatana na kuzuka kwa tapo la ulimbwende huko ulaya mwishoni mwa karne ya 18. Tapo hili liliathiriwa na falsafa za watu kama Kant na Hegel (Eagleton 1983:120-21). Mtazamo huu ndio unaotawala kwa sasa na unadai kuwa neno fasihi limetokana na neno la kiarabu lenye maana ya Ufasaha au uzuri wa lugha.Kwa hiyo istilahi Literature (fasihi) katika taaluma ya Kiswahili inatofautiana na istilahi Literature katika Kiingereza. Neno fasihi halihusiani na maandishi wala vitabu bali ufasaha wa kauli. Dhanna hii katika Kiswahili inazingatia aina zote za fasihi, iliyoandikwa na ile ya mdomo.
(d)    Mtazamo wa nne; ulizuka hapa Afrika Mashariki na kuenea miaka ya 1970. Mtazamo huu unadai kuwa.....Fasihi ni hisi ambazo zinajifafanua kwa njia ya lugha..... Waumini wa mtazamo huu ni John Ramadhan, Balisidya,A na Sengo na Kiango katika Hisi Zetu. Mtazamo huu unachanganya mambo matatu ambayo ni fasihi yenyewe, mambo yaelezwayo na fasihi na mtindo wa fasihi ya Kiswahili. Fasihi huweza kuelezea hisi, kadhalika mtindo wa kifasihi mara nyingi ni wa kihisiya bali fasihi yenyewe si hisi.
-   Vivyo hivyo fasihi huweza kuelezea mapenzi lakini fasihi yenyewe si mapenzi.
(e)    Mtazamo wa tano; ni wa karne hii ulioanzishwa na wafuasi wa nadhariya ya umbuji (formalism). Mtazamo huu ulianzishwa na wanaisimu wa Kirusi mwanzoni mwa karne hii miongoni mwao akiwa Boris, Tomashevski, Roman Jakobson na Victor Shklovski. Hawa wanadai kuwa fasihi ni tokeo la matumizi ya lugha kwa njia isiyo ya kawaida ili kuleta athari maalumu. Kwa mujibu wa watu hawa, fasihi hukiuka taratibu za kawaida za matumizi ya lugha katika sarufi ili kumvutia msomaji au msikilizaji.
Lugha ya kifasihi humfanya msomaji aitafakari lugha yenyewe badala ya kutafakari tu ujumbe unaowasilishwa na lugha hiyo.

  Udhaifu wa mtazamo huu
(i)         Unaelemea mno upande wa fani na kupuuza maudhui
(ii)       Unasadifu zaidi ushairi kuliko fani nyingine za fasihi
Kwa maelezo yote yaliyotolewa tunaweza kuhitimisha kuwa fasihi ni sanaa itumiayo maneno teule ya lugha yenye ubunifu inayojaribu kusawiri vipaji vya maisha, mahusiano na hisiya za watu katika miktadha mbalimbali.
CHIMBUKO LA FASIHI
Kuhusu chimbuko la fasihi wataalamu mbalimbali wametoa hoja zao na kuibua nadhariya kadhaa:
1. Nadhariya ya kidhanifu; nadhariya hii hujiegemeza kwenye dhanna zisizoweza kuthibitishwa kisayansi. Nadhariya hii inadai kuwa chimbuko la fasihi ni Mungu.

Nadhariya hii ndiyo kongwe na ilikuwepo tangu kabla ya Kristo na ilitumiwa sana na Wayunani wa huko Ulaya ambao waliamini sana miungu kama wa Ushairi na Muzikiambao waliwaita Muse.

Miungu hawa waliaminika ndio waliowapa watunzi Muhu au Kariha (Msukumo) wa kiroho, nafsi na kijazba wa kutunga kazi zao.

Wanaounga mkono nadhariya hii wanadai kuwa Mungu ndiye msanii mkuu na wa kwanza. Wasomi wa kale waliounga mkono nadhariya hii ni Hesiod, Plato, Aristotle na Socrate.

Udhaifu wa nadhariya hii:
(i)         Nadhariya hii inakataa kuwepo kwa dhanna ya ubunifu kwa watunzi
(ii)       Haichochei kujiamini kwa wasanii na huwafanya wajione kama waigaji tu wa mambo yaliyofanywa na Mungu
(iii)     Huwafanya wasanii waonekane ni watu waliokaribu sana na Mungu kuliko binadamu wengine
(iv)       Huibua dharau miongoni mwa wasanii na kusababisha wajitenge na jamii ya kawaida
     DHIMA YA FASIHI
Fasihi ni sanaa itumiayo maneno teule ya lugha kufikisha ujumbe kwa jamii. Hivyo fasihi ina dhima (wajibu/majukumu) mbalimbali kwa jamii kama ifuatavyo:
v Kuelimisha jamii kupitia vipengele mbalimbali kama nyimbo,hadithi,ngoma,nk
v Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii katika vizazi mbalimbali vya jamii.
v Kuburudisha jamii na kuifanya ijisahaulishe madhila mbalimbali yanayoikuta jamii
v Kukuza na kuendeleza lugha ya jamii.
Hata hivyo unapojadili dhima ya fasihi huna budi kuzingatia dhanna ya utabaka na itikadi.
Tabaka; ni makundi ya watu yanayounganishwa na uhusiano wao na njia za uzalishaji mali na mfumo wa mamlaka katika jamii.
Itikadi; inafafanuliwa kuwa ni imani juu ya yale yasemwayo na jamii na kuyaamini yale yanayohusiana na mahusiano ya kiutamaduni ya jamii tunamoishi.
Dhanna ya utabaka na itikadi zinajitokeza katika fasihi kwa sababu zifuatazo:
(i)         Kwanza fasihi hufungamana na muktadha (mazingira maalumu ya kijiografia), kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na hivyo kila kazi ya fasihi ni zao la muktadha ulioizaa kazi husika.
(ii)       Pili, fasihi hudhihirisha aina fulani ya urazini (kujitambua kibinadamu/kuwa na utashi) na utambuzi wa hali ya maisha alionao mtunzi pamoja na wale anaowawakilisha.
(iii)     Tatu; zipo jamii za aina mbili nazo ni jamii zenye usawa na mshikamano ambazo hazina matabaka nazo huitwa jamii zenye utabaka usio wa kinyonyaji mfano jamii za wavuvi, wafugaji, wakulima, n.k. katika jamii hizo fasihi zao zitabeba dhima tofauti.
Kwa ufafanuzi huo waweza kubaini kuwa kwa ujumla dhima ya fasihi inajikita katika mambo yafuatayo:
-   Itikadi, utamaduni, falsafa, uchumi, siasa, nk.


(a)    Dhima ya itikadi
Kila jamii hutawaliwa na itikadi fulani ambayo ndiyo huzalisha misimamo ya jamii husika katika uzalishaji mali. Kila mtunzi wa fasihi mtiifu kwa jamii yake lazima ataathiriwa na itikadi ya jamii yake na hatimaye utunzi wake kuwa na mwelekeo wa utetezi wa itikadi iliyommeza.
 Mfano:
-   Kipindi cha ukoloni watunzi wengi walibanwa na itikadi za kikoloni na kujikuta wakitetea tabaka la wakoloni. Mifano ya kazi za fasihi kama Mashimo ya Mfalme Suleman, Uhuru wa Watumwa, Hekaya za Abunuwasi, n.k.
Maandishi hayo yalijaribu kutetea itikadi ya ukoloni kwa kuwaonesha wakoloni wa kizungu kama watu wenye uwezo wa hali ya juu, wema na wachapakazi, wenye akili nyingi waliojua kukomboa na kumuendeleza mwafrika. Pia maandishi hayo yalisisitiza maadili ya utii ambao ulisaidia watawala kuwadhibiti watawaliwa kimawazo.
(b)    Dhima ya kiuchumi
Dhima ya fasihi katika uchumi huonekana zaidi kupitia nyimbo za kazi ambazo hutungwa ili ziimbwe wakati wa kufanya kazi ngumu. Mfano: kazi kama kulima, kutwanga,kuvua samaki,kuwinda na shughuli nyingine.
Katika uchumi wa kibepari dhima ya fasihi ilijikita zaidi kwenye kuburudisha,kutafuta pesa kwa kurekodi na kuuza kazi za fasihi. Ni katika kipindi hiki palizuka fasihi pendwa iliyojikita kwenye kujipatia pesa zaidi na kusahau maadili ya jamii.


(c)    Dhima ya kiutamaduni
Katika dhima hii fasihi ina majukumu yafuatayo:
-   Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii
-   Kuburudisha
-   Kukuza lugha
-   Kuelimisha,kuasa na kurekebisha jamii.
Amali za jamii ni pamoja na mila, desturi, mtindo wa maisha, imani, jiografia, visasili, maarifa ya kijadi n.k.
Amali hizi huweza kuendelezwa na kuhifadhiwa katika fasihi na kurithishwa vizazi vijavyo. Kwa mfano; Tamthiliya ya Kinjeketile imehifadhi mengi kuhusu hali ya maisha wakati wa ukoloni wa kidachi. Kurwa na Doto hali kadhalika, Bwana Muyombekere na Bibi Bugonoka Ntulanalwo na Bulihwali, Mirathi ya Hatari na Mashetanini kazi za fasihi zilizohifadhi amali nyingi sana za jamii za kiafrika hasa Tanzania.
Fasihi hasa nyimbo na visasili hutumika kukoleza shughuli za kijamii kama ibada,matambiko,sherehe, n.k. Nyimbo licha ya kuburudisha pia hubeba ujumbe kuhusiana na tukio husika.
Kinafsiya fasihi pendwa kwa mfano ile ya masaibu na vituko vya ujambazi na uhalifu humpa msomaji imani kuwa anashuhudia na kushiriki katika matukio ya ushujaa yanayosimuliwa na hivyo kusisimua mwili na kuridhisha ari yake ya kujihusisha na matendo ya kishujaa.
Malighafi ya fasihi ni lugha, kwa kadiri lugha inavyotumiwa na kufinyangwa na watunzi ndivyo inavyokua na kupanuka. Maneno mengi yanayotumika katika utunzi wa mashairi, riwaya, nyimbo na tamthiliya hufanya lugha ikue. Kwa mfano: katika sanaa ya ushairi maneno kama vina na mizani, mshororo, muwala, tathilitha, takhmisa, tarbia, n.k huchochea ukuaji wa lugha katika jadi ya ushairi ambao huchukuliwa kama ghala la maneno.
Fasihi hubeba elimu za kila aina, baadhi ya watunzi ni mabingwa wa kuonesha ufundi katika maandishi. Mfano: maandishi ya Ngugi wa Thiong’o kama vile Petals of Blood na Nitaolewa Nikipenda vilevile Alamin Mazrui katika: Kilio cha Haki, na F. Katalambula katika Simu ya Kifo husawiri vizuri mandhari ya kijiografia na maneno yaliyokuza watunzi na ujuzi wao katika kumudu lugha.
Hadithi za kisayansi kwa mfano: Jina langu ni Sifuri na Kipeo na Kipeuo na Mahakamani zimekusudia kuwafundisha watoto dhanna hizo za kisayansi kwa njia ya kisanaa.
Elimu ya ukweli sharti iambatane na tabia ya uchunguzi, uchambuzi na udadisi. Tabia hiyo ni usomaji wa uhakiki wa fasihi ya msomaji ambayo humsaidia msomaji kupanua upeo wa kudadisi na kukosoa.
Fasihi hutoa maonyo, huasa na kuiadilisha jamii ili iendane na mila na desturi za jamii husika mfano: hadithi kama vigano vyenye kuhusu tabia za fisi husaidia watoto kujirekebisha kitabia.
(d)    Dhima ya kisiasa
Fasihi imetumika sehemu nyingi sana kuendeleza au kudumaza harakati za kisiasa nchini Tanzania kwa mfano; fasihi imetoa mchango mkubwa sana kupitia ngonjera za Azimio La Arusha. Nyimbo za kizalendo kama Tanzania, Tanzania na Tazama ramani, ni miongoni mwa kazi za fasihi ambazo zimetoa mchango katika siasa. Hadi sasa nyimbo za kizazi kipya zinaendelea kushughulika na siasa mifano ipo mingi ila kwa uchache tu: Ndio Mzee na Sio Mzee (Joseph Haule/Prof.Jay), Tanga Kunani Pale? (Wagosi wa Kaya), Muungano CCM na CUF (Juma Kassim/Juma Nature) n.k

(e)     Dhima ya kifalsafa
Baadhi ya kazi za fasihi hujaribu kuelezea falsafa fulani kuhusu maisha. Falsafa hiyo watunzi wengine huita ukweli wa maisha ingawa si kila wakati ukweli huo hukubalika kwa wote.
Kazi za fasihi za kifalsafa huchambua masuala mazito kuhusu maisha ya mwanadamu duniani na hatima yake. Fasihi hii huchochea wasomaji na wasikilizaji kutafakari masuala hayo kwa umakini na undani zaidi.

Mifano ya fasihi za kifalsafa ni Utenzi wa Al-Inkishafi, Nagona, Mzingile, Karibu Ndani, Kusadikika, Kufikirika, Rosa Mistika, n.k

MUHADHARA WA TATU
FASIHI YA KISWAHILI NI NINI?
Kuhusu dhanna ya fasihi ya Kiswahili kuna mjadala mkali sana miongoni mwa wanazuoni tangu miaka ya 1970-1990.

Mgogoro huu ulizuka kutokana na hofu ya baadhi ya watu kuwa kuna njama za kuwameza Waswahili au kukana juu ya kuwepo kwa kabila au jamii ya waswahili.

Ilidaiwa kwamba waswahili ni watu wenye asili ya Mwambao wa Afrika Mashariki nao wana fasihi yao ambayo huelezwa kwa lugha yao ya Kiswahili.
Kuna wale walioona kuwa waswahili ni kabila au taifa mahususi (Sengo 1987:217) na hivyo wanayo fasihi yao mahususi ambayo ndio inayostahili kuitwa Fasihi ya Kiswahili na zile nyingine zinazotumia Kiswahili ziitwe Fasihi kwa Kiswahili.
Kundi lingine linaamini kuwa hakuna kabila la waswahili na hivyo kwa mantiki hiyo hakuna fasihi ya waswahili (Senkoro 1988:11) anasema; Tunasema kuwa kazi fulani ni fasihi ya Kiswahili au la kutokana na jinsi inavyotambulisha utamaduni wa waswahili, hapa neno “waswahili” halimaanishi kabila la waswahili kwani kabila la namna hiyo halipo leo.
Waswahili hapa ni wananchi wote wa Afrika Mashariki na kati kwa ujumla na si watu wa Pwani tu.

Kundi lingine linaloona kuwa fasihi ya Kiswahili ni fasihi inayoelezwa kwa lugha ya Kiswahili ni kundi la Mazigwa (1991:18) pamoja na Syambo na Mazrui (1992)

Kwa ujumla kutokana na majadiliano hayo unaweza kupata maswali ya msingi kama vile:
-   Mswahili ni nani?
Mswahili kama inavyoelezwa katika HISI ZETU cha Sengo na Kiango; ni: (mzaliwa wa pwani kwa asili, msemaji wa lugha ya Kiswahili kwa ufasaha, muislamu na kwa maana za utani mswahili ni mtu asiyetimiza miadi na mjanjamjanja)
-   Mswahili yukoje?
Mswahili anaweza kujipambanua zaidi kwa nje kupitia mavazi, shughuli za uzalishaji mali, mahusiano yake ya kijamii na kupitia fasihi yake kwa ujumla.
-   Uswahili ni nini?
Uswahili ni mfumo mzima wa maisha ya Mswahili unaomtofautisha na watu wa jamii nyingine, kama ilivyo uchaga kwa mchaga, umasai kwa mmasai au uhaya kwa muhaya.


-   Kiswahili ni nini?
Ni lugha ya waswahili na ndiyo huitumia kuelezea mila zao.
Majibu ya maswali hayo ni nguzo muhimu sana katika kuamua kama kuna fasihi ya Kiswahili au la.
FASIHI YA KISWAHILI NI IPI?
Wataalamu wa fasihi walio wengi na hasa waswahili wanaamini kuwa jamii ya waswahili ipo ingawa yawezekana kuwa waliitwa au kujiita kwa majina mbalimbali kama vile (wa-amu, wapate, wamvita, wapemba au waunguja)
Watu hawa waliunganishwa na lugha moja ya utamaduni wa aina moja na wote ni wenyeji wa Mwambao wa Afrika Mashariki na visiwa vyake na ndio wajulikanao kwa jina la waswahili.
Kuwepo kwa watu hao ni ithibati kuwa wanayo fasihi yao ambayo yapaswa kuitwa fasihi ya Kiswahili ya waswahili na mifano yake ni pamoja na Utendi wa Fumo Liyongo na nyimbo mbalimbali za shughuli za kijamii kama harusi, uvuvi, unyago, misiba, n.k
Kuenea kwa lugha ya Kiswahili sehemu nyingi za Afrika Mashariki kumeifanya lugha hiyo kuwa chombo cha fasihi ya watu wote wanaoitumia lugha hiyo hasa baada ya kuingia kwa wakoloni.
Syambo na Mazrui (1992) wanasema; Hatuna budi kuichukulia fasihi ya Kiswahili kuwa ni ile iliyoandikwa kwa Kiswahili tu bila kujali inazungumzia utamaduni wa Kiswahili au mwingineo maadam imetumia lugha ya Kiswahili na inafuata mbinu za ufasa wa lugha hiyo basi ni fasihi ya Kiswahili.
Kuenea kwa Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki na hata nje ya bara la Afrika kumezua fungu la fasihi ya kigeni katika lugha ya Kiswahili mfano; tafsiri mbalimbali kama Biblia, Mabepari wa Venisi, Bwana Muyombekere na Bibi Bugonoka; Ntulanalwo na Bulihwali (Anicet Kitereza, 1980)zimeibua aina ya fasihi ijulikanayo kama  Fasihi kwa Kiswahili.
Baadhi ya wanafasihi wanaamini kuwa fasihi ya Kiswahili ni ile iliyobuniwa na mswahili tu kwa kutumia lugha ya Kiswahili bila kujali inazungumzia utamaduni wa Mswahili au la.
Wapo wengine wanaoamini kuwa fasihi ya Kiswahili ya Waswahili ni ile iliyobuniwa na  mswahili kuhusu utamaduni wa Waswahili.
Kundi la tatu ni lile linalodai kuwa fasihi kwa Kiswahili ni ile iliyobuniwa na kuandikwa na mtu asiye mswahili au kwa lugha nyingine na kisha ikafasiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
           Mfamo:
-   Mfalme Edipode
-   Takadini
-   Barua Ndefu Kama Hii
-   Mabepari wa Venisi
-   Orodha, n.k
AINA ZA FASIHI YA KISWAHILI KWA JINSI YA UWASILISHAJI
Fasihi ya Kiswahili hugawanywa katika aina mbili kulingana na jinsi ya uwasilishaji.
-   Fasihi simulizi
-   Fasihi andishi
FASIHI SIMULIZI
Ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi. Hivyo fasihi simulizi ni tukio linalofungamana na muktadha fulani wa kijamii. Fasihi simulizi hutawaliwa na mambo yafuatayo:
-   Fanani
-   Hadhira
-   Fani inayotendwa
-   Mahali/mandhari
-   Wakati
-   Tukio lenyewe
Kwa kawaida fasihi simulizi hutungwa kichwani kabla au wakati uleule wa kutamkwa. Hata hivyo fanani huwa na uhuru wa kubadili matini ya utungo wakati wowote ili kukidhi mahitaji ya muktadha na hadhira yake.
Tanzu za fasihi simulizi ni nyingi na hutofautiana kulingana na jamii. Pamoja na wingi wake wataalamu wameziweka katika makundi yafuatayo:
(a)    Mazungumzo
Tanzu zilizomo katika kundi hili ni hotuba, malumbano ya watani, soga na mawaidha.
(b)    Masimulizi (yale yote yanayosimuliwa)
Hapa huingizwa tanzu mbalimbali za hadithi kama vile ngano, hekaya, hurafa, simulizi za kihistoria na kiasili kama vile visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.
(c)    Maigizo
Hapa huingizwa tanzu mbalimbali kutegemeana na shabaha na muktadha.
(d)    Ushairi
Hubeba tanzu kama nyimbo, maghani, tenzi, ngonjera na mashairi.
(e)    Semi
Huwa na misemo kama methali, vitendawili, simo, mafumbo, lakabu na mizungu.
(f)    Ngomezi
Ni fasihi simulizi inayowasilishwa kwa kutumia mlio wa ngoma badala ya mdomo.

FASIHI ANDISHI
Ni sanaa itumiayo maneno teule ya lugha kufikisha ujumbe kwa njia ya maandishi. Kuwapo kwa fasihi andishi hutegemea;
-   Mtunzi –anayetunga kazi ya fasihi
-   Hadhira –mlengwa wa kuisoma kazi hiyo
-   Mchapishaji – anayepiga chapa kazi husika
Fasihi andishi inagawanyika katika makundi mawili ambayo ni:
-   Nudhumu – ushairi (hujumuisha tenzi,ngonjera na nyimbo)
-   Nathari – masimulizi ya kimjazo yanayofuata kanuni za kimasimulizi

MUHADHARA WA NNE
1. SEMI
Semi ni mojawapo kati ya kumbo za fasihi simulizi. Semi hutawaliwa na sifa tambulishi mahususi. Semi hufafanuliwa kama tungo au kauli fupi fupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo maalumu ya kijamii. Kumbo hili lina tanzu zifuatazo.
-   Methali
-   Vitendawili
-   Mafumbo
-   Misimu
-   Lakabu
-   Kauli tauria (tafsida)
(a)    Methali
Ni semi fupi za kimapokeo zinazodokeza fikra au funzo zito linalotokana na tajiriba (uzoefu wa maisha ya jamii).
Mfano:
-   Haraka haraka,haina Baraka
-   Mwenda pole,hajikwai
Mara nyingi falsafa ya methali huelezwa kwa kutumia tamathali hasa sitiari au mafumbo. Methali hubeba hekima na busara ambazo aghalabu hutumika kuonya, kuasa, kutia moyo, kuadilisha na kuadibu.
(b)    Vitendawili
Kitendawili ni usemi uliofumbwa wenye kuchochea fikra na udadisi wa mambo. Vitendawili ni sanaa inayotegemea uwezo wa mtu kutambua, kuhusisha na kulinganisha vitu vya aina mbalimbali katika mazingira yake.
Mfano:
-   Wanangu wawili hushabihiana sana- (maziwa na tui la nazi)
-   Ikiwa ya moto hainyweki ikipoa hainyweki –(supu)
(c)    Mafumbo
Mafumbo ni kauli zenye kuchemsha bongo. Kauli hizi humtaka anayeulizwa atumie akili na udadisi kufumbua fumbo. Mafumbo ni hatua ya juu ya vitendawili.

AINA ZA MAFUMBO
Kuna mafumbo ya kuchemsha bongo na mafumbo majina.
(i)         Mafumbo ya kuchemsha bongo
Ni maswali yenye kutaka kutumia akili na ujuzi ili kujibu .Baadhi ya mafumbo ni ya kimapokeo na mengine hubuniwa na msemaji kwa lengo maalumu.
Mfano:
-   Nina kilo moja ya pamba na kilo moja ya mawe je, kipi ni kizito zaidi? (Jibu: vyote vina uzito sawa)
-   Mtu mmoja alikuwa na ng’ombe fahali wawili akitokea Kenya kuja Tanzania akiwa mpakani ng’ombe mmoja akazaa je, maziwa watakunywa watu wa wapi? (Jibu: Fahali hazai)
(ii)       Mafumbo majina
Huwa ni majina ambayo yamebeba maana fulani inayofungamana na tukio au hali iliyojitokeza kipindi cha kupatikana kwa mwenye jina hilo. Aghalabu hutumika kama njia ya kuhifadhi kumbukumbu inayohusiana na mhusika.
Mafumbo jina huweza kuwa mepesi au mazito kulingana na maana ya fumbo lenyewe lililobebeshwa kwenye jina la mhusika.
Baadhi ya mafumbo jina huwa ya kikabila.

Mfano:
-   Tabu,shida- alipatikana kwa hali hiyo
-   Mwanjaa –alizaliwa msimu wa njaa
-   Mwamvita – msimu wa vita
-   Majuto,riziki,bahati – hali husika
-   Tenahuvo – hana makuu (kipare)
-   Mwendwa – mpendwa (kibena)
-   Gumbo – njaa (kizigua)
-   Aimbora – Baraka (kimachame)

(d)    Simo/misimu
Ni semi za muda na mahali maalumu ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalumu. Misimu ikipata mashiko husanifishwa na kuingizwa katika msamiati, methali au vitendawili.
Mfano:
-   Tamutamu mahonda ukinila utakonda- (msimu uliozuka baada ya kuanzishwa kiwanda cha pombe kali cha Mahonda huko Zanzibar)
-   CCM – Chukua Chako Mapema
-   UPE – Ualimu Pasipo Elimu
-   SU – Soma Ule
(e)    Lakabu
Ni majina ya kupanga ambayo mtu hupewa au hujipa kutokana na sifa au tabia alizonazo. Majina haya hubeba maana iliyofumbwa.
Mfano:
-   Kifimbo,mchonga – Nyerer,J.K
-   Mzee Ruksa – Ali-Hasan Mwinyi
-   Simba wa vita – Kawawa
-   Mkuki uwakao – Jomo Kenyatta
(f)    Kauli tauria/tafsida
Hizi ni kauli zenye mchanganyiko au mfuatano wa sauti zinazotatanisha kuzitamka ambazo hutumiwa kupunguza utusi na ukali wa baadhi ya maneno.
Mfano:
-   Wauwao wawe wao wauwa wewe wauawa
-   Wale wali wale wali wao
-   Pema ujapo pema ukipema si pema tena
-   Ukiona neno usitie neno ukitia neno utapatwa na neno.
MUHADHARA WA TANO
2.  DUA
Haya ni maombi ya kawaida kwa mizimu mahususi kwa ajili ya kupata mafanikio yanayotegemewa na muombaji.

         Mfano:
-   Dua fulani au kuomba mtu fulani apate rehema
(i)         TABANO
Ni manuizo ya maneno kama ya kiganga yasemwayo wakati wa shughuli ya kuzindika au kwa ajili ya kutaka mizimu au miungu ibariki uganga huo.
Mfano:
-   Wazee wetu...mwanenu kaja leo na hiki kidogo kuwataka radhi zenu....nawaomba mumpokee na kumkubalia maombi yake.
(ii)       MASIMULIZI
Ni fasihi yenye kusimulia habari fulani. Masimulizi huwa na sifa zifuatazo:
-   Mpangilio mahususi
-   Wahusika
-   Mandhari
-   Lugha ya kimaelezo
-   Utambaji
-   Maudhui ya kweli au ya kubuni yenye funzo fulani
Masimulizi yanaundwa na tanzu mbalimbali kama vile:
v Hadithi za kubuni; Hadithi hizi huweza kuwa:
(i)         Ngano au vigano
Hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama,mazimwi na watu katika kuonya na kuadibu kuhusu maisha.
(ii)       Ishara
Ni hadithi ambazo maana yake ya wazi huwakilisha maana ingine iliyofichika.
Mfano:
-   Kusadikika ni ishara kuhusu utawala wa mabavu wa kikoloni.

(iii)     Mbazi
Hadithi itolewayo kama kielelezo cha kufafanulia hadithi inayosimuliwa.
Mfano:
-   Mafundisho ya Yesu katika Biblia aliyafafanua
           kwa kutumia hadithi ndani ya masimulizi.
Ipo mbazi kuhusu kisa cha mtego wa panya, mbazi hii inasimuliwa hivi; .... siku moja katika nyumba fulani panya aligundua kuwa ametegewa mtego na kwa kuwa hakuweza kuutegua alienda kuomba msaada kwa ng’ombe lakini ng’ombe alikataa akidai kuwa huo ni mtengo wa panya yeye haumuhusu. Panya hakuchoka akapiga hodi kwa mbuzi na kumlilia shida yake, mbuzi naye akamjibu kama alivyojibu ng’ombe kuwa huo ni mtego wa panya wala haunihusu. Hatimaye panya akamwendea jogoo na kueleza yote lakini jogoo naye alimkataa panya na kumkejeli kuwa huo mtego hamhusu yeye jogoo. Baada ya kugonga mwamba panya akakosa amani akihofia mtego ulioitwa.. “ ...wa panya..” kwa kweli siku nzima ile panya hakuweza kujipatia riziki akihofia mtego. Usiku ulipofika baba mwenye nyumba alishituliwa na mkewe akiambiwa kuwa mtego umefyatuka na bila shaka panya atakuwa amenaswa. Baba yule akakurupuka na kuuendea mtego huku akipuuza hadhari ya mkewe kuwa asiende giza giza, alienda huku akijifariji kuwa panya hawezi kumdhuru chochote......alipoufikia mtego ule akapeleka mkono ili auchukue na kumsulubu panya aliyewasumbua kitambo. La haula! Kumbe hakuwa panya, mzee yule akarudi nyuma haraka huku akiagiza mkewe amletee taa haraka. Baada ya taa kuletwa ikabainika mtego ulinasa nyoka na hivyo mzee yule aliumwa na nyoka yule.....ghafla hamkani ikaingia ndani ya nyumba kutafuta dawa ya kumponya mzee mwenye nyumba. Muda si muda mzee yule alikata roho kwa kuzidiwa na sumu ya nyoka na nyumba ikawa na msiba. Siku ya kwanza wageni wachache ikabidi achinjwe jogoo kupata kitoweo. Siku ya pili wageni ni wengi kiasi ikabidi achinjwe mbuzi ili kukidhi mahitaji. Baada ya maziko siku ya tatu na kumaliza tanga akachinjwa ng’ombe.

Funzo:
Hivi ule mtego ulikuwa wa panya,ng’ombe,mbuzi,kuku au baba mwenye nyumba? Mbazi hii inasadifu umuhimu wa kushirikiana kuokoa mambo ambayo yakiharibika yataathiri wengi.
(iv)       Mchapo
Ni hadithi fupi aghalabu husimuliwa kwa watu wanaofahamu historia ya jambo linalotolewa mchapo huo.
Mfano:
-   Kawawa alipoambiwa afunike kikombe ughaibuni ili asiendelee kutiliwa chai hali ametosheka.
-   Mchapo wa kuchapwa viboko kwa Samwel Sitta baada ya kuongoza wanafunzi wenzake kudai siagi akiwa chuo kikuu.
(v)         Hekaya
Ni hadithi ndefu na yenye kuzingatia matukio machache ya kusisimua na ya kustaajabisha. Msuko wake hauchangamani na wahusika huwa ni wachache na bapa.

Mfano:
-   Hekaya za Abunuwasi, Alfu-lela Ulela
   Moja wapo ya hekaya za Abunuwasi ni hii:
Abunuwasi baada ya kutofurahishwa na utawala wa mfalme wake aliamua kupanga njama za kumpa adhabu mfalme wake huyo, basi siku moja Abunuwasi akapika wali wake na ulipoiva akaufunua ili upoe naye akaendelea na shughuli zingine,baada ya muda akarudi na kukuta nzi wamejaa kwenye chakula chake. Hapo abunuwasi akazua kisa kuwa nzi wamekula harufu yote ya wali wake hivyo akamwendea mfamle ampe waraka utakaomruhusu (Abunuwasi) kuwaua nzi popote atakapowaona. Mfalme bila kujua akampa Abunuwasi waraka huo. Abunuwasi kisha kupata waraka huo akachonga rungu kubwa maalumu kwa kazi ya kuwasaka na kuwaua nzi. Siku moja mfalme akawa na karamu nyumbani kwake iliyohusisha wananchi wake wote akiwemo Abunuwasi. Katika karamu hiyo Abunuwasi alihudhuria na akaketi karibu kabisa na mfalme huku akiwa na rungu lake. Muda si muda huku sherehe ikiendelea ghafla Abunuwasi akainua lile rungu lake na kulishusha kwa nguvu kichwani kwa mfalme, mfalme alianguka palepale na kupoteza maisha. Walinzi wa mfalme walipomshika Abunuwasi akawatolea waraka wenye saini ya mfalme ukisomeka kuwa Abunuwasi ameruhusiwa kuua nzi popote atakapowaona. Basi hapo Abunuwasi akawaambia kuwa lengo lake halikuwa kumdhuru mfalme bali kumsulubu nzi aliyetua kichwani kwa mfalme huyo.”
(vi)       Salua
Ni kipengele cha kimasimulizi kinachojumuisha tanzu za kihistoria zenye kusimulia habari za zamani. Baadhi ya tanzu zake ni:
v Visakale
Ni masimulizi yanayohusu matukio yaliyopita ya kale/zamani kuhusu mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na historia.
Mfano:
-   Hadithi za Liyongo,Mkwawa,n.k
v Mapisi
Ni maelezo ya historia bila kutia maneno ya kubuni. Ni historia halisi ya mtu au kitu au jambo pasipokutiwa chuku.

Mfano:
-   Mapisi ya Tanganyika- mapisi ya historia ya kweli.
v Tarihi
Ni maelezo au jedwali la matukio muhimu na tarehe zake. Hutokea zaidi katika maandishi na huhusu matukio ya kihistoria.

v Nasaba/shajara/potifolio
Ni orodha ya wazee au wahenga wa mtu kuanzia baba,babu na wengine waliotangulia. katika baadhi ya makabila kila mtu hupaswa kufahamu majina ya wahenga wake hadi kizazi fulani.
Mfano:
-   Prof. Sengo anaweza kutaja orodha ndefu ya wahenga wake tangu kizazi cha kwanza hadi cha sasa alichopo yeye. (Tigiti-Yusuf-kibwana-Semindu-Mnyagatwa-Sengo)
-   Watu wengi wenye kuendeleza historia za makabila yao hupenda kutumia majina zaidi ya mawili (mf; John-Joseph-pombe-magufuli)

v Kumbukumbu
Ni maelezo ya matukio muhimu yanayohusu mtu binafsi au jamii ya watu. Fani za wasifu ni aina ya kumbukumbu.
Mfano:
-   Wasifu wa Siti Binti Saad
-   Dereva wa kwanza Tanganyika
-   Uhuru wa watumwa.



(vii)     Visasili
Ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii unaohusiana na asili ya ulimwengu na mwenendo wake.

   AINA ZA VISASILI
v Visasili vya usuli
Hivi ni visasili vinavyojaribu kuelezea asili ya chimbuko la taifa fulani au wanadamu kwa ujumla.
Mfano:
-   Hadithi ya wayahudi ya kuumbwa kwa ulimwengu na kutokea kwa mwanadamu (Adam na Hawa) ni mfano mzuri wa kisasili cha usuli. Baadhi ya visasili vya usuli hasa Afrika huelezea asili ya mila na desturi fulani ya jamii.
v Visasili vya ibada na dini
Visasili hivi huhusu matendo ya ibada na imani mbalimbali za dunia na mara nyingi hutungwa kisanaa (kuigizwa) katika ibada hizo.
Mfano:
-   Katika ibada za kikristo Ekaristi (kula pamoja chakula cha bwana) ni maigizo ya chakula cha mwisho alichokula Yesu Kristo na wanafunzi wake kabla ya kusulubiwa.
NB:
        - Madhehebu ni makundi ya watu wanaoongozwa 
   na imani fulani.
-     Dini-ni kikundi cha waamini wenye
             kufuata utaratibu fulani katika
             kumuabudu mungu wao.


v Visasili vya miungu na mizimu
Hivi hupatikana zaidi katika mataifa yenye miungu wengi kama vile Asia, Ulaya ya kale na Misri ya kale.
Hapa Afrika visasili hivi hupatikana kwa wingi katika lugha ya Wayoruba (Nigeria) na katika falme zinazozunguka ziwa victoria (Nyanza).

3. Maigizo (Drama)
Ni utendaji unaohusisha uigaji wa tabia na matendo ya watu au viumbe uli kuburudisha na kutoa ujumbe kwa njia ya sanaa. Drama za ki-Afrika huambatana na ngoma, utambaji, hadithi, nyimbo na matendo ya kimila kama jando na unyago. Drama nyingi hutumia maleba maalumu (mavazi maalumu) yanayovaliwa na waigizaji ili kuficha uhalisia wao.

       AINA ZA MAIGIZO
(i)         Maigizo ya watoto
Watoto wanapocheza mara nyingi huigiza matendo ya kimaisha wanayoyaona katika jamii zao kama vile kulima,kupika,harusi,vita, n.k
Maigizo ya aina hiyo ni sanaa za maonesho zenye kuburudisha na kuwaelimisha watoto pamoja na kukuza vipaji vyao vya ubunifu.

(ii)       Maigizo ya misibani
Maigizo haya hufanywa na watani au wajukuu wa marehemu na huhusiana na maisha, matendo na tabia za marehemu. Maigizo haya hufanywa ili kuwapunguzia wafiwa huzuni na kutoa mafundisho kwa watu waliopo msibani kuhusiana na tabia za marehemu.

Mfano:
-   Kama marehemu alikuwa na tabia mbaya waigizaji/ watani wanaweza kuigiza kwa njia ya kejeli au dhihaka juu ya tabia hiyo.
(iii)     Maigizo ya kwenye sherehe/kidini
Sherehe nyingi za kijadi na kidini huambatana na maigizo mfano; kusimika viongozi huweza kuambatanishwa na kuvishwa aina fulani ya mavazi na kukalishwa katika viti vya asili,kusemewa baadhi ya maneno,kutemewa mate ya Baraka pamoja na kupewa vinywaji fulani kama ishara ya jambo husika.

MUHADHARA WA SITA
1.NYIMBO
Zinaelezwa na baadhi ya wataalamu kuwa ni chochote kinachoimbika. Katika nyimbo tunapata ushairi simulizi na ngomezi.
(a)    Ushairi simulizi
Ni tungo za kinudhumu zinazotungwa kwa kufuata kanuni au kutofuata kanuni za urari wa sauti, mapigo ya sauti na mpangilio wa vipashio vya lugha. Lugha ya kishairi katika fasihi simulizi hupambanuliwa na lugha ya kawaida kwa namna inavyopagiliwa na jinsi inavyoingiliana na muktadha wa utendaji. Kanuni za kishairi hupambanuliwa kwa kufuata wizani (rithimu) maalumu na mawimbi ya sauti,mara nyingi lugha huwa ya mkato, tamathali na mafumbo hutumika.
Ushairi simulizi una tanzu nyingi lakini tunaweza kuzigawa zote katika makundi mawili ambayo ni nyimbo na maghani.
Mgawanyo huu ni kwa ajili ya uchambuzi tu kwani nyimbo nyingi pia ni maghani na maghani mengi ni nyimbo.

Nyimbo – ni kila kinachoimbika; dhanna hii inajumuisha tanzu nyingi baadhi zikiwa za kinathari pia huingia kwenye kundi hili pale zinapoimbwa.

Mambo muhimu yanayotambulisha nyimbo
-   Muziki wa sauti ya mwimbaji au waimbaji
-   Muziki wa ala
-   Matini au maneno yanayoimbwa
-   Hadhira inayoimbiwa
-   Muktadha (mazingira) yanayofungamana na wimbo mf: sherehe, Ibada,tanzia,kazi,n.k
Nui au tanzu kuu za nyimbo za Afrika Mashariki
Mashairi
Kundi hili linaundwa na vipengele mbalimbali kama vile:
(i)         Tumbuizo ; hizi ni nyimbo za kuliwaza au kufurahisha watu kwenye matukio mbalimbali kama msiba, ngoma au haruzi.
Tanzu za tumbuizo
(a)    Bembea/pembejezi; ni nyimbo za kubembeleza watoto na hupatikana katika kila kabila.
(b)    Mbolezi; ni nyimbo za kilio au maombolezo na hutumika kuliwaza wafiwa na kuwaondolea machungu.
(c)    Nyiso; ni nyimbo za jando au unyago na huimbwa na makabila yenye mila na desturi ya kupeleka watoto unyagoni au jandoni, nyimbo hizi hukusudiwa kuwaasa wari kuhusu majukumu ya kiutu uzima pindi watakapohitimu jando au unyago.

(ii)       Nyimbo za siasa
Hizi ni nyimbo ambazo huimbwa kwenye shughuli za kisiasa kwa lengo la kuelewesha,kuhamasisha,kubeza na kutumbuiza kwenye tukio husika. Mf: ccm... nambari wani, Tumejipanga.......mwaka huu wataisoma, Sasa kumekucha......jogoo limekwishawika Dodomaaa......n.k

(iii)     Tukuzo
Ni nyimbo zinazoimbwa kutukuza au kudhihirisha utukufu na ufahari wa taifa,mtawala,mtu au kitu fulani. Mf: Tazama ramani utaona nchi nzuri.......
Yenye mito na mabonde mengi ya nafakaa...nanenaa kwa kinywa halafu kwa kufikiri nchi iliyo mashuhuri huitwa Tanzaniaaaa.......majira yetu hayaaaa... yangekuwaje sasa...

Tanzu za tukuzo ni:
(a)    Kongozi; Ni nyimbo za kuaga mwaka au kuadhimisha mwandamo wa mwezi. Nyimbo hizi ni maarufu sana unguja na huchezwa kipindi cha sherehe za kuaga mwaka na huambatana na ngoma ijulikanayo kama Shindwe. Wachezaji huzunguka nyumba hadi nyumba na kupewa chochote wakati wakiimba.
(b)    Nyimbo za dini; Ni nyimbo za kidini ambazo huimbwa na kumtukuza Mungu.
Mfano:
-   Kaswida za kumsifu Mungu
-   Nyimbo za Kikristo kama Tenzi za rohoni, Tumwimbie Mungu na kwaya. Nyimbo za aina hii huwa na maudhui yanayooana na mafunzo ya dini zinazohusika hasa kuhusu Mungu,ibada,dhambi na mapatilizo ya jehanamu na akhera. Nyimbo hizi zinabeba maudhui yanayohusiana na dini zaidi.
(c)    Nyimbo za taifa; Ni nyimbo za kusifia taifa na huimbwa katika matukio maalumu. Kwa mfano mataifa mengi ya Afrika wimbo wa taifa ni mmoja na asili yake ni wimbo wa Afrika Kusini. (Nkosisikeleeeeliiii Afrikaaa ....... Mumgu ibariki Afrikaaaaa .......Almight God bless Afrikaaaa .......)
(iv)       Chapuzo
Ni nyimbo za kuchekesha na kuhamasisha shughuli au kuwahamasisha watendaji wasichoke wala wasikate tamaa.
Tanzu za chapuzo ni:
Tanzu za chapuzo hugawanywa katika makundi mbalimbali kama vile:
(a)    Kimai; Ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli za uvuvi. Huimbwa ili kuwaondolea wavuvi hofu hasa iwapo ni usiku na vilevile kuwatia ari ya kuvuta makasia.
(b)    Wawe; Ni nyimbo zinazoimbwa wakati wa kazi ya kulima na huimbwa kwa kufuata mapigo ya kupanda na kushuka kwa jembe kadiri walimaji wanavyoinua na kushusha majembe yao kuisakama ardhi.
(c)    Wimbo wa kutwanga; Wimbo huu huimbwa na wasichana au wanawake wanapopura (kupwaga) ulezi au nafaka yoyote na huimbwa kwa kupokezana wakishindana kupura nafaka. Wimbo huu huleta hamasa na kuwafanya wasichoke mpaka kazi imalizike.
(d)    Nyimbo za vita; nyimbo hizi huimbwa vitani na askari ili kuwahamasisha na kuwaondolea uwoga kwa kuwapandikiza hisia za kizalendo. Mf: ..... Iddi Amini akifa ...... mimi siwezi kuliaaa ... nitamtupa Kageraaa ...... awe chakula cha mambaaa ...piga magoti Amini ... Amini ... piga magoti Aminiiii ..... aaakija toboa ... toboa ... toboa ..... toboa ...  Nyimbo hizi huwasahaulisha kama kuna kufa na hujikuta wakisonga mbele na kumkabili adui.
(e)    Nyimbo za watoto; Nyimbo hizi huimbwa na watoto wakati wa michezo yao,hukusudiwa kunogesha michezo yao. Nyimbo hizi kwa kiasi kikubwa zinasetiri itikadi na falsafa ya jamii kuhusu mahusiano, ndoa na tabia mbalimbali za kibinadamu.
Tenzi au Tendi
Haya ni masimulizi ya kishairi yanayohusu matukio ya kihistoria au kishujaa. Hizi ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au kimawaidha ambazo zinahusiana na matukio ya kihistoria, nyimbo hizi zinaitwa tenzi na zinapohusu visa vya mashujaa huitwa tendi.
Mfano: Nyimbo za Issa Matona ni Tenzi, nyimbo za ngoma ya chakacha halikadhalika. Mfano wa tendi ni utendi wa Fumo Liyongo.

MUHADHARA WA SABA

MAGHANI NA NGOMEZI
Maghani ni ushairi unaoghaniwa au kutambwa hadharani. Sauti ya mghani aghalabu huwa kati ya mazungumzo na kuimba (hazungumzi wala haimbi).
Maghani hutambwa hadharani pamoja na ala za muziki au bila ala na huzungumzia masuala mazito ya kijamii au ya kibinafsi.

        Tanzu za maghani
(i)         Ghani nafsi; Ni ushairi simulizi wa kinafsi unaoelezea hisiya, matatizo na fikra za mtunzi mwenyewe. Mashairi ya mapenzi yanaingia katika kundi hili.
(ii)       Ghani tumbuizi; Ni ushairi wa kuliwaza, kufurahisha na kuburudisha na hughanwa badala ya kuimbwa.
(iii)     Ghani sifo; hili ni kundi mahususi la maghani ambalo hubeba tungo za kusifu hasa watu,wayama,mimea au vitu.
                   Tanzu za ghani sifo
(a)    Vivugo/kivugo; ni ghani la kujisifu ambalo hutungwa na kughaniwa na mhusika mwenyewe. Muundo wake hutegemea sababu za mtunzi na jadi ya utunzi. Mathalan jamii ya wahaya kivugo huwa na mambo yafuatayo:
-   Jina halisi au jina la sifa ya mtunzi
-   Sifa za nasaba yake ya kuumeni
-   Sifa za nasaba ya kikeni
-   Maelezo ya matendo makuu aliyoyatenda au matendo matukufu yanayozidi wengine wote
-   Ahadi ya kutenda makubwa zaidi kwa ajili ya mkubwa wako
-   Tamati- kujikabidhi rasmi kwa mkubwa.
(b)    Tondozi; Ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu vya kawaida. Pembezi ni aina moja wapo ya tondozi ambayo husifu watu wakubwa au watawala. Tondozi zinazohusu wanadamu moja kwa moja ndio nyingi zaidi. Watu husifia wapenzi wao,adui zao au wake zao.
Ghani simulizi; Ni ghani za kihadithi zenye mtiririko wenye msuko wa matukio uliojengwa ili kuleta taharuki na ujumbe fulani.
Tanzu za ghani masimulizi ni:
(a)    Rara; Ni ghani zinazotambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani na mara nyingi huambatana na muziki wa ala. Mtambaji huitwa Yeli/Manju na huwa ni mtaalamu wa kupiga ala fulani za muziki. Ala mashuhuri ni zeze, marimba, ngoma na njuga.
                      Sifa za rara
-   Huweza kuwa tenzi au tendi
-   Lazima ziwe ni tungo za kishairi
-   Isirudie hadithi au tukio kwa kirefu
-   Matini yake hutungwa papo kwa papo
(b)    Tendi; huu ndio utanzu mashuhuri zaidi katika kundi la ghani simulizi, utendi ni utungo mrefu unaosimulia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii au matukio ya kitaifa. Huweza kuwa ya kihistoria au yaliyochanganya historia na visakale au visasili.
Sifa za tendi
-   Muundo wa kinudhumu (kishairi)
-   Huwa na beti nyingi kati ya 700/800
-   Upatanifu au muunganiko
-   Maudhui kuhusu maisha na matendo ya kishujaa.

Ngomezi/ngoma;Ni fasihi ya ngoma ambapo baadhi ya makabila hupeleka habari kwa njia ya ngoma kupitia midundo fulani ambayo huwakilisha kauli fulani katika lugha ya kabila hilo. Utunzi wa ngoma hutumia kanuni na kaida za kimapokeo zinazofahamika kwa watu wengi katika jamii husika.
Umbo la ujumbe wa ngoma huwa ni la kishairi. Matukio ya dharura kama vita, hutangazwa kwa njia ya ngoma.
Sanaa ya ngoma haijachunguzwa kiasi cha kutosha na huenda ugunduzi huu ukapotea bila kuacha kumbukumbu za kuridhisha kama hazitachunguzwa kwa kina.

MUHADHARA WA NANE
1. USHAIRI
Ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari wa mawazo, maono na falsafa za ndani zenye kuvuta moyo kwa namna ya ajabu.
       Sifa za ushairi
-   Wimbo sharti uimbike,ughaniwe na kutongoleka
-   Maneno ya hekima yenye kufunza, kuonya na kuadibu
-   Lugha ya mkato, vina na mizani mf: mfanowe, mefumbata, nk
-   Lugha nzito au lugha ya kunata
Hisiya (lugha inayovuta moyo
Vijenzi vya ushairi wa Kiswahili
Fani na Maudhui
Muwala ni uwiano mzuri kati ya mtiririko wa fikra na umbo la shairi. Mawazo ya shairi yakifuatana kimantiki ubeti hadi ubeti na mstari hadi mstari hufikisha bara bara maudhui yaliyokusudiwa na hapo husemwa kuwa shairi lina muwala.
Muundo ni msuko,mwingiliano na uwiano wa vipengele vyote vinavyojenga shairi au kazi ya sanaa. Vipengele vya kimuundo hudhihirika katika umbo la shairi.
-   Idadi ya beti kwa shairi zima
-   Idadi ya mistari kwa kila ubeti
-   Vipande (ukwapi-utao-mwandamizi)
-   Kituo kila ubeti
-   Mizani
-   Vina
Maudhui ni wazo au mawazo yaliyomsukuma mtunzi wa kazi ya fasihi kutunga kazi ya sanaa. Maudhui huhusisha mtazamo, shabaha na ujumbe.
Umbo hutumika kwa maana ya sanaa ya nje ya shairi au kazi ya sanaa.
Mtindo unakuwa na uteuzi wa maneno; lugha ya Kiswahili huteua maneno maalumu yenye kuleta athari au matokeo yaliyokusudiwa.
-   Takriri- ni mbinu ya kurudiarudia neno au sehemu ya neno kwa lengo la kutia msisitizo.
-   Wizani- ni kiimbo yaani kupanda na kushuka kwa sauti kunakoleta mapigo ya kimuziki.
-   Mchezo wa maneno – ni mbinu ya kutumia maneno ya kiufundi ili kutanua maana ya kile kinachosemwa na kuongeza utamu wa usemaji mfano: wale wali wale wali wao (Mulokozi)
Wale wale ndio wao
Bado wapo palepale
Wao wale wenye vyao
  Na vya kwao vile vile
Wala kale wala leo
Kula huko kura kule
Mwendo huu ndio huo
Bado tupo palepale
-   Lugha ya mkato – shairi huzungumza mambo kwa ufupi kuliko ilivyo katika maongezi ya kawaida. Mfano: shairi la Hila zina maulaya (Amri Abeid)

Nijapotendwa ubaya na wabaya kuwajua
Mwenzi huona haya ubaya kuwatendea
Japo moyo una waya hufanya kuuzuia
Nacheka hali najua hila zinamaulaya
Hila zinamaulaya na wananishambulia
Nyama iliyooza mbaya mbesi hufurahia
-   Taswira – ni mbnu ya kuumba picha ya jambo katika mawazo ya msomaji au msikilizaji kwa kutumia maneno. Mfano: Amina (Shaaban Robert)
Amina umejitenga,kufa umetangulia
Kama ua umefunga,baada ya kuchanua
Nakuombea mwanga,peponi ukubaliwe
Mapenzi tuliyofunga,hapana wa kufungua

          Tamathali za semi
v Sitiari- ni mbinu ya kulinganisha vitu bila kutumia viunganishi linganishi.
Mfano:
-   Elimu ni bahari
-   Misitu ni uhai
-   Kilimo ni uti wa mgongo
v Tashibiha – ni mbinu ya kulinganisha vitu kwa kutumia maneno kama: mfano wa,mithili ya,kama,nk
Mfano:
-   Mrefu kama twiga
-   Mweusi mithili ya kiatu cha jeshi
-   Ananata mfano wa nta
v Tashihisi – ni mbinu ya kuvipa uhai na uwezo wa kutenda kama binadamu vitu au viumbe visivyo na uwezo huo.
Mfano:
-   Misitu ikatabasamu
-   Mawimbi yakapiga makofi
-   Kaburi likamkumbatia
v Tafsida – ni maneno yatumiwayo kwa lengo la kupunguza au kuficha utusi na ukali wa maneno.
Mfano:
-   Ametutoka (kufariki dunia)
-   Kupiga simu ( kwenda haja)
-   Kujifungua (kuzaa)
Ø Mdokezoni mbinu ya kumshirikisha msomaji kwa kumuachia akamilishe wazo fulani.
     Mfano:
-   Alipomtazama akamwambia ............ lakini nakupenda.
Ø Ishara – ni matumizi ya maneno yanayoashiria mambo au matukio katika jamii.
Mfano:
-   Mwezi – Baada ya kuona mwezi alirudi nyumbani akiwa na furaha.
Ø Balagha/mubalagha – ni mbinu ya kutia chumvi kwenye habari kwa lengo maalumu.
Mfano:
-   Alikuwa mweusi kama buti la jeshi.
-   Alikuwa mrefu mithili ya twiga
 Mbinu ya kikufu- Ni mbinu ya kukifanya kipande cha mwisho cha ubeti kiwe kipande cha mwanzo cha ubeti au mstari unaofuata.
   Mfano:
         Kutafuta hali njema, maana ya mapinduzi
         Unyonge kuusukuma, uonevu wa majizi
         Na kuonewa lazima, tung'owe yote mizizi
         Maana ya mapinduzi, Kutafuta hali njema.
 Mbinu ya pindu- Neno pindu katika ushairi lina maana mbili.
(i)         Kufanya neno au sehemu ya neno la kipande au mstari lianze katika kipande cha mstari unaofuata.
Mfano: (Zuko)
Tika kitupu hutika,TIKA upya unafuka
UKA huko ukaleni,LENI mapya kulaFUKA
FUKAra wa mzaMANI, MANI MAPYA hutaKA
TUKATAKA mawazoni,ZONI huna kukuSHIKA
SHIKAmimi sishiKANI,KANIzo zapukutika

(ii)       Mbinu ya kugeuza silabi za neno mwanzo kuwa za mwisho.
Mfano:
Saadan chambilecho, chambilecho humenyeka
Kinyume ni kiambacho,chomba akini hakina
Hila tatu chekecho,chokeche huzipinduka
Kwa wenye chongo kufika,mwe fumba lako jicho
Mbinu ya kidato – Ni mbinu ya kufupisha mshororo mmoja au zaidi kila ubeti kwa lengo maalumu. Malengo maalumu ni pamoja na kupata vina na mizani, kuuliza swali, n.k
Mfano: Nimeamka la S. A. Mohamed
       Sidanganywi kwa hotuba na mahubiri matupu
       Hata wanakula riba,wanaongoza vikapu
                 Nimeamka
        Nawaambia wahubiri,wanaodanganya watu
        Moyo umejaa ari,sizugiki tena katu
                  Nimeamka
Mbinu ya tungo mchoro – mbinu hii hutumika katika shairi la mchoro ambapo shairi hupangwa katika umbo lenye kufanana na kile kinachozungumziwa hivyo mada ya shairi hilo huonekana machoni licha ya kusikia masikioni.


       Mfano: Tafakari tesi
                 Masikini
               Haya ambayo
            Mawe yalifinyangwa
      na                      maumbile
    mawe                          ambayo
   yalisongwa                          na
   matambara                        maskani
  haya                                ambayo
 yalimiminishwa                           kwa
 saruji                              itokanayo

      HISIYA YA KISHAIRI
Hisiya za kishairi hutokana na msukumo wa ndani ya moyo alionao mshairi wakati anatunga shairi lake.
Aina za hisiya za kishairi
(i)         Hisiya ya furaha
Mfano wa shairi la Cheka kwa furaha

Dhiki ni kama mzaha,asiyecheka nani?
Haya cheka kha kha kha,ndio ada duniani
Basi cheka kwa!kwa!kwa!,usafike moyo wako



 
(ii)       Hisiya za chuki
Mfano shairi la Manzese mpaka Ostabei,  
Unaishi ostabei unapata mchumba/mpenzi Manzese, je atakula nini ilhali hali ya maisha ya manzese yajulikana?

(iii)     Hisiya za kimapinduzi
Mfano shairi la Tohara.
Linahamasisha jamii ya kinamama kuachana na mila za tohara kwa wanawake au wasichana.
(iv)       Hisiya za kichochezi
Mfano: shairi la “Hatumwoni” katika diwani ya Karibu Ndani mwandishi katika shairi lake anasema:
Miungu waliosimama kama vichaka
Waambieni wakae chini warefu
Kaeni chini! Wengi nyuma hatuoni!
Hatutaki vyenu visogo kuona.
Kaeni chini miungu, kaeni chini ndiyo amri!
Mlipewa uongozi ukawapaka rangi
Na madaraka madaraka yakawalevya
Sasa vueni wapisheni wenye nia!
Kokeni mioto mashujaa wa uonevu tuwabanike
Kamwe hapatakuwa na kilio wala matanga
Bali hoihoi za ushindi na madaraka kwa umma
(v)         Hisiya za huzuni
Mfano: Utenzi wa Hayati Sokoine katika diwani ya Mloka.
          Ilikuwa redioni
          Saa kumi za jioni
          Mwenyekiti kwa uchungu
          Umma kautangazia

MUHADHARA WA TISA
HISTORIA FUPI YA USHAIRI WA KISWAHILI
Wataalamu wengi wanakubaliana  kwamba asili ya ushairi wa Kiswahili ni tungo simulizi hasa ngoma na nyimbo. Kabla ya karne ya 10BK ushairi wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa na kughaniwa kwa ghibu (sanaa za asili) bila kuandikwa.
Ø Baadhi ya tanzu za ushairi zilihusu masuala ya dini hasa ya Kiislamu na taaluma ya uandishi kwa hati ya kiarabu.
Ø Miongoni mwa watunzi mashuhuri wa ushairi wa mwanzo wa Kiswahili ni Fumo Liyongo.
Ø Uandishi wa ushairi uliendelea kuwa wa ghibu hata baada ya karne ya 15 na kusawiri mabadiliko ya mifumo mbalimbali ya kimaendeleo katika maisha mfano: kipindi cha waarabu kiliambatana na migogoro mingi ya vita,upinzani,mizozo kati ya madola ya miji ya Pwani na kati ya watwana na mabwana.
Ø Vilevile wasomi wa kidini waliibua fasihi ya ushairi uliotafakari theolojia na falsafa ya maisha mfano: Utenzi wa Al-Inkishafi.
Ø Tendi za Kiislamu zilizungumzia pia matukio ya uarabuni enzi za Mtume Muhammad.
    Mfano:
-   Utenzi wa Shufaka (kuomba rehema)
-   Utenzi wa Ngamia na Paa (dua kutegemea aendako muombaji)
-   Utenzi wa Mikidadi na Mayasa (namna ya kuwaasa watoto wa kike na kiume)
-   Utenzi wa Ras L’ Ghuli



TUNGO ZA KITAMADUNI, MAWAIDHA NA TUMBUIZO
(a)    Tungo za kitamaduni (mawaidha na tumbuizo)
Mfano: utenzi wa Mwanakupona ulitungwa na Bi. Mwanakupona akimuasa binti yake juu ya nidhamu, heshima na utii kwa mumwe wake.

MASHAIRI YA SIASA
Watunzi mashuhuri wa kundi hili ni Muyaka bin Haji, Suud bin Said na Kibabina. Hawa ni baadhi ya watunzi wa mashairi ya kisiasa na walifungwa jela na kuuawa. Pia kulikuwa na mashairi ya kukataa kutawaliwa na wakoloni.
     Mfano:
-   Potugezi Afala
Mzungu Migheli
KARNE YA ISHIRINI
Ushairi karne ya 20 hadi sasa.
Maendeleo ya ushairi wa Kiswahili yaliathiriwa na mambo matatu ambayo ni:
-   Elimu ya kizungu
-   Hati ya maandishi ya kirumi
-   Taaluma ya uchapaji
Haya yote yaliletwa na wazungu.
ATHARI ZA UJIO WA WAARABU KATIKA USHAIRI WA KISWAHILI
(a)    Hati za kiarabu
(b)    Maudhui yalilenga elimu akhera zaidi ya siasa na mawaidha
(c)    Fani; kanuni zilianza kutumika kwa kuzingatia vina na mizani. Mwanzilishi wa kanuni za utunzi wa mashairi ni Plato kutoka Ugiriki.
(d)    Elimu;mashairi yalieneza elimu ya Kiswahili maeneo ya bara kupitia shule. Maarifa ya kusoma na kuandika,maarifa ya arudhi (kanuni ) za utunzi zilipewa kipaumbele katika kutunga mashairi.
(e)    Hati za kirumi; zilienea kupitia elimu ya shule,makanisani kwa kutumiwa na watunzi wengi badala ya hati za kiarabu.
-   Kipindi hiki ushairi ulianza kusomwa na watu wengi zaidi na hata wasio waislamu na baadhi yao wakaanza kutunga mashairi mfano: Mathias Mnyampala.
-   Utunzi huu uliingia magazetini na kuhamasisha watu wengi kusoma magazeti mfano: gazeti la Mambo Leo (1923).
-   Kuanzishwa kwa shirika la uchapaji nako kulichochea utunzi wa mashairi ya Kiswahili kwa sababu watunzi wengi walipata mahali pa kuchapa kazi zao (shirika la uchapaji la Afrika Mashariki : The East African Literature Bureau, 1948) lilichapa kazi mbalimbali za watunzi mashuhuri.
Mfano:
-   Mathias Mnyampala
-   Akilimali Snow-White
-   Amri Abeid.
         SHUGHULI ZA KISIASA ZA KUDAI UHURU (1950-1960)
1.Ushairi ulipamba moto ukihamasisha wanajamii kudai uhuru mfano: Mashairi ya Saadan Kandoro
2.Baada ya uhuru ushairi ulisambaa zaidi kutokana na msukumo wa kisiasa na fani mpya mfano; Ngonjera na Mavue ni mashairi yasiyo na kanuni. Mashairi huru yaliyoanzishwa ili kuzingatia mahitaji mapya ya kisiasa na kisanii.


             HISTORIA YA USHAIRI KIFASIHI
Historia ya ushairi kifasihi inaweza kubainishwa katika mihula mbalimbali kama alivyofanya Kezilahabi. Mihula minne aliyoianzisha Kezilahabi ni:
(i)         Muhula wa urasimi mkongwe; hiki ni kipindi ambacho ushairi ulitawaliwa na kanuni na mitazamo ya kidini na kimwingi.
(ii)       Muhula wa utasa (kipindi cha mpito); ni kipindi cha mabadiliko ya kiutamaduni na kielimu kulikoleta mabadiliko ya hati za maandishi. Kipindi hiki mashairi machache yalitungwa kwa lugha ya kiarabu na kanuni kubadilika.
(iii)     Muhula wa urasimi mpya; huu ulikuja wakati wa kufufua kanuni za utunzi ambapo palitungwa kitabu cha sheria na kanuni na kusambaza kwa watunzi. Kitabu hicho kilitungwa na Amri Abeid na kuchapishwa 1954.
(iv)       Muhula wa sasa (ulimbwende,1967); ni muhula wa mtazamo mpya kimawazo na kisanaa. Muhula huu umeibua mgogoro mkubwa kati ya uwanja wa ushairi baina ya wanamapokeo na wanausasa.
MUHADHARA WA KUMI
Kumbo za ushairi wa Kiswahili
Ushairi wa Kiswahili unaweza kuwekwa katika kumbo za aina tatu za kimtindo ambazo ni; Ushairi wa kijadi (kimapokeo), Ushairi wa Kisasa/mlegezo/masivina/mauve/mapingiti na Ushairi wa maigizo.
1. Ushairi wa kimapokeo; Haya ni mashairi yenye kuzingatia urari wa vina na mizani.
2. Ushairi wa mlegezo; Ni mashairi yasiyofungwa na kanuni za kimapokeo.
3. Ushairi wa maigizo; Ni ushairi unaotumia vitendo na hugawanyika katika aina mbili ambazo ni ngonjera na ushairi wa kidrama.
(i)         Ngonjera; Ni ushairi wa majibizano ulioanzishwa na Mathias Mnyampala 1960 na ulitumika sana katika kueneza siasa ya ujamaa. Katika ngonjera huwa kuna pande mbili, kuna upande uliopotoka na upande uliosahihi. Kila upande hujenga hoja za kushawishi upande mwingine kishairi.
Mwisho wa majibizano ya kingonjera huwa ni suluhisho ambalo kwa kiasi kikubwa upande uliopotoka huthibitisha kuzidiwa kwa hoja.
Mfano: ngonjera za UKUTA.
(ii)       Ushairii wa kidrama; Ni ushairi unaotumiwa katika baadhi ya tamthiliya kama sehemu ya mchezo wa kuigiza na ni moja wapo ya mitindo itumiwayo katika tamthiliya. Mfano; Tamthiliya ya Mfalme Edipode na Mabepari wa Venisi (mfarisi: J.K. Nyerere)
-   Ngonjera hupaswa kuwa na Mwanzo wa kingonjera.
            Bahari za ushairi kijadi
Bahari ya ushairi ni aina mahususi ya ushairi yenye sifa     fulani kiumbo zinazojipambanua na aina nyingine za ushairi.
(i)         Shairi; wanajadi walisema shairi ni utungo wenye mishororo minne kila ubeti na vipande viwili vya mizani nane kila kipande. Maudhui yanaweza kuhusu suala lolote linalomkuna mtunzi.
(ii)       Wimbo; Ni utungo wenye mishororo mitano kila ubeti na una vipande viwili na maudhui yanaweza kuwa ya mapenzi yaliyochepuka.
(iii)     Bahari ya utenzi; Ni shairi la masimulizi,mawaidha au maelezo marefu. Tenzi nyingi zina mizani nane kila mstari na vina hubadilika kila ubeti isipokuwa mstari wa mwisho. Maudhui ni ya kawaida, masimulizi, mawaidha ambayo huelezea wasifu au tawasifu, ushujaa, utendi, nk.
-   Wasifu ni historia inayomhusu mtu fulani na ambayo huandikwa na mtu mwingine.
-   Tawasifu ni historia ya mtu ambayo huandikwa na mtu mwenyewe.
Inkishafi/Dura Mandhuma; Ni aina ya ushairi ambayo imepata jina lake kutokana na utenzi wa Al-Inkishafi na Dura Mandhuma. Utenzi huu ulikuwa pamoja kwa sababu ya nafanana na pia zina maudhui ya kidini ingawa zinaweza kutumika kwa maudhui ya kidunia. Mpangilio wake ni mishororo minne na mizani kumi na moja kwa mgawanyo wa sita na tano jumla yake ni kumi na moja yaani 6 + 5 = 11.
NADHARIYA ZA UHAKIKI WA FASIHI YA KISWAHILI (PROF. T.S.Y. SENGO)
               (SENGO NA FASIHI ZA KINCHI 2009)
Nadhariya za fasihi
Nadhariya ya Nadhariya
Kwa mujibu wa Sengo, nadhariya ni….Wazo kuu,fikira kuu,mwongozo mkuu....wa mtu au watu (jamii), wa pahala fulani,wakati fulani, kwa sababu fulani.
Tunamtaka MWAAFRIKA ajisimamishe, ajiamini, ajiendeshe, aache mchezo, asikubali kuwa mume haramu, mke haramu, mtumwa, kijakazi.....wa mtu fulani kwa jina la uhisani, ufadhili, uwekezaji mgeni, tajiri, mume wa waume, jike la wake, n.k. Hayo maoni hatuyataki. Hii inaweza kusemwa ni NADHARIYA au ni FALSAFA.
1. Nadhariya ya Mtu - Utu
Kwa Afrika na mwaafrika, utu ndicho kitambulishi cha uungwana, ustaarabu,hekima,busara,fikra,mawazo na hadhari za mtu. Ujenzi wa wahusika katika kazi za ubunifu, maudhuwi ya kazi hizo hupewa kipaumbele na umuhimu hasa katika ujumbe na falsafa nzima ya kazi hiyo. Mtu – kwao. Tukisema Afrika, ndilo bara letu. Mengine yapo na watu wa huko, wana yao. Kimsingi utu unatakiwa uwe mmoja. Tafauti ni za kihulka, kitabiya na kimazingira. Kwa nadhariya hii Sengo anasisitiza kujali utu katika utunzi na uhakiki wa kazi za fasihi. Mtunzi hana budi kuwajali waAfrika na kuzijali jadi za muAfrika katika utunzi na kinyume chake ni kutojali utu wa muAfrika.
2. Mtu – Kwao, Ukwao wa Mtu, Asokwao.....
Ni nadhariya inayompima mtu kwa asili ya kizazi chake, kuzaliwa na kulelewa kwake,mbeko zake kwa watu wengine – wakubwa kwa wadogo. Mtu – kwao; mtu na wazazi wake,mtu na asili yake,mtu na ukoo wake,mtu na kabila lake,mtu na mazingira yake,mtu na taifa lake. Mtu na hisiya ya kuzaliwa na kulelewa kwake,kufanyiwa na kushukura kwake. Aso – kwao ni yule asiye kisogo,aso macho na uwezo wa kukisoma kisogo na kuyaona mengi alokwishafanyiwa kabla na watu mbalimbali. Mtovu wa utu na shukurani. Kila mtu ana asili yake na hiyo sharti iwe chimbuko hasa la fasihi yake, mtunzi anayeshabikiya ya nje na kuacha ya ndani ni sawa na msaliti wa jamii yake.
3. Taalimu ina kwao,Utamaduni una kwao,fasihi ina kwao;
Taalimu ina kwao; Taalimu ni kweli. Kweli ni dhanna. Kweli ni sifa. Kweli ya kitaalimu hupatikana kwa utafiti. Utafiti hufanywa na watu. Kila kweli ina asili na wakati wake na mazingira yake kwa kila jamii. Taalimu ya kiungwana kwao ni kwa waungwana,hawezi kuja mgeni na kumfunza mwenyeji kweli batili isiyoendana na wenyeji na hata hao wenyeji wakijifunza hayo ya wageni iwe ni kwa kuwajuwa tu hao wageni lakini sio kujifunza na kuyaona bora kuliko yao.
Utamaduni una kwao; mwanataalimu akutanapo na nadhariya yoyote, hasi, chanya, chapwa, sharti aitafutiye KWAO. Utamaduni wa jamii ya watu ni utambulishi wa jamii hiyo. Jamii ina eneo la kijiografiya katika ardhi. Watu wake wana mapisi marefu katika eneo hilo. Na kila jamii ni jamii ya mchanganyiko, tangu hapo hadi leo. Si jambo la Kihore atokaye Maragori tena ya Kenya au Okenyo wa Kisumu au Kakaibagarura wa Kiziba kuamuwa kuwa watoto wake sasa wamekuwa Wachina, Wajapani, Wangoni ati kwa kuwa wamezaliwa na kusema Kichina,Kijapani au Kingoni. Utamaduni wa watu na utambuzi wao si lugha tu kama sivyo mmbwa wote wa Waingereza wangekuwa Waingereza. Mchaga hawezi kuwa Mhaya kwa kuweza tu kusema Kihaya. Hivyo, jiografiya, mapisi(historiya), damu (biolojia), jadi, utamaduni, mila, desturi, ada, lugha, kawaida, mazoweya, mavazi na sanaa kwa ujumla ndio humpa mtu u UKWAO.
Fasihi ina kwao
Ili mtu aielewe fasihi simulizi ya jamii yoyote sharti akujuwe jamii hiyo inakoishi, utamaduni wao, mila na ada zao, lugha yao, n.k. fasihi ya Kiswahili kwao ni Uswahilini, Pwani ya Afrika Mashariki. Jiografiya ya Jumuiya ya Waswahili inaanziya Kismayu hadi Pemba asili ya Msumbiji kaskazini na visiwa vya Kilwa, Mafia, Unguja, Tumbatu, Pemba ya leo, Mombasa au Mvita, Lamu na Pate hadi visiwa vya Ngazija/Comoro.
Waswahili wana jadi zao katika viambo vyao, makaazi yao, vijiji vyao, miji yao, n.k. Wapare kama Wachaga wapo hawapo, pale uendapo kwao ukimtafuta Mchaga huambiwa huyu Mrombo, yule Mmachame, yule Mkibosho, Mmarangu, Muhimo, Msanyajuu, n.k. Kadhalika Mmakanya, Msangi na Nathaeli Mmbaga mwenye kikabila chake ndani ya Upare. Hivyo, jadi, Sanaa, kazi, mila, desturi, lugha na kawaida zina kwao, kila jamii ina zao na hakuna moja iliyo bora dhidi ya yenziye.  


       Vielezeya vya fasihi ya jamii yoyote ile ni:
(i)         Jamii; kwao fasihi ni jamiini
(ii)       Taalimu maalumu; fasihi ni taalimu kama zilizvyo taalimu nyingine kama uhandisi na udaktari
(iii)     Taalimu ya maneno mateule; maneno ya ishara za jamii, maneno kama pombe, nguruwe, kanisa, kimada, hawara...... hayatajwi kwa fakhari Uswahilini, hasa katika maeneo ya kina Sheikh.
(iv)       Ujumi wa jamii ambamo ndimo baharini mchotwamo ubunifu na upambifu wa hali na majambo.
(v)         Ubunifu
(vi)       Sanaa – usanii
(vii)     Umbuji na umahiri wa lugha na wa uwezo wa kuyatumiya maneno kisawasawa.
(viii)   Mvuto wa kusomeka
(ix)       Mafumbo tata au tatanishi
(x)         Semi za ndani na semi za barabarani
(xi)       Maneno mateule (kwa mukhtasari, fasihi ina mambo matatu muhimu na yasemwayo, na tamu/ladha ya ujumi wa baina ya hayo mawili. Fasihi ilizayo Ujerumani yaweza kuchekesha sana Afrika. Ukwao wa jamii ndiyo bahari ya fasihi na fasihi ya jamii ndiyo mvuwa za mchomo, vuli, za mbaazi, na za masika za kuineemesha jamii kiutamaduni na kimaisha. Mtu kwao. Watu na yao. Na haya yote huanza na wale waliomzaa, pale alipozaliwa kwa asili ya uzazi wa damu yake.
4. Nadhariya ya Ndani – Nnje
Mtafiti, mwalimu au mhakiki wa fasihi ya jamii fulani, ili aweze kuitafiti, kuifundisha au kuihakiki ni shuruti aimanye vizuri. Kuijuwa fasihi ya watu ni muhimu kwanza kuwajuwa wenyewe, utamaduni wao, mila zao, ada na desturi zao, bahari yao ambayo ndiyo chemchem ya ishara na dhanna zao. Ndani ni ndani. Mambo ya jamii sharti yazingatiye kweli za ndani za jambo. Mvaa suti ya kung’aa na ndani ana gagulo, hajavaa, sawa na mtu alofunga kilemba cha mita kumi na tano lakini ndani mwa uvaaji, maboga na muhogo vyaonekana ndani ya mawingu na kitumbuwa cha wavaaji viyoo viko ndani ya barafu ya sharubati, vyengine viko juu ya paji la uso au utosini mwa mtembezaji.
Utamaduni wa vyakula, mavazi, uwadilifu, imani ya dini, ucha – mungu, ujenzi, n.k. ni moja kati ya vitu vya ndani vya fasihi ya jamii ya watu fulani. Si kwa fasihi tu bali kwa mambo mengi yanayofahamika, vizuri zaidi kwa nadhariya ya ndani nnje.
5. Nadhariya ya Ukhalisiya
Penye ukame, huzungumzwa njaa, kutopatikana kwa maji na taabu za kukosa vitu fulani fulani.Hayazungumzwi mafuriko ya kawaida. Penye kiliyo, ni nadra sana kuchezwa ngoma ila kwa Jaluwo ndiyo jadi yao kuliya kwa ulevi na dansa la rumba au samba, bampingi au shekisheki. Penye ndowa na harusi, hapachurwi kwa wanga kuanguwa kiliyo. Mradi hali halisi ya pahala au ya jambo huwa ndiyo msingi wa matukiyo au hali fulani. Halipo la kupitwa na wakati, hakuna fikira au mawazo potofu (kuna fikira au mawazo tafauti).
Ukhalisiya wa kiuchumi, hali, wingi wa kina mama dhidi ya kina baba, ukhalisiya binafsi wa utu, wa hulka na tabiya, wa kuzaliwa huo ndio humuongoza mtu katika utunzi wa kazi yake ya fasihi.
Ukhalisiya wa miktadha na mandhari ya kazi ya fasihi umejikita katika kweli zote ziihusuzo kazi hiyo.
Ukhalisiya wa kutumia lugha ya watu kufundishiya yao – leo CIVICS – URAIYA kufundishwa kwa lugha ya kigeni hali wafundishwao hawaijuwi lugha hiyo ya kigeni, hapo hapana ukhalisiya bali kuua uzalendo wa watoto hao kwa kuwalazimishiya lugha isiyo kujifunza yao. Ukhalisiya ni NADHARIYA pana na kubwa. Isipelekwe Ulaya wala Marikani, isomwe viamboni, vijijini, mitaani na itumike kwa upana wake.

6. Nadhariya ya Kiislamu
Nadhariya hii inajikita katika kuelekeza watunzi na wahakiki wa kazi za fasihi kutunga na kuhakiki kwa kuzingatiya mafundisho na makatazo ya dini ya Kiislamu. Prof. Sengo katika nadhariya hii anasema; ..... Msanii, mbunifu, mwandishi, mtunzi, mhakiki mtumiyaji wa nadhariya hii ya Kiislamu, anatakiwa ashike adabu zake, afyate mkiya wake, akiri miya fil-miya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumba na mwendeshaji mmoja tu wa yote na vyote. Akibuni hubuni kutokana na uumbizi wa Allah. Kama ni riwaya, isiwe na ufuska wala mashizi katika starehe za muktadhani wala katika dhanna ya maendeleo kuwamo makasino, mabaa, madansa, madawa yoyote ya kulevya n.k. Kulewa, kuiba, kuzini, kufanya ujasusi, ufisidi, dhuluma n.k. yakiwemo iwe ni katika sababu za mtu kuadhibiwa kwa kufanya mambo hayo na isiwe kuyashabikia. Hii si nadhariya ya kubabaishia maisha bali ni ya uhakika wa maisha ya kivuli, ya duniani nay a ukweli wa maisha ya kudumu Peponi au Motoni.
7. Nadhariya ya Utambulishi
Fasihi inatambulisha sanaa za jadi za utamaduni wa jamii. Kila fasihi ina kwao. Hivyo utambulishi wa utamaduni – bahari ya fasihi – na fasihi-mvuwa imwagayo maji baharini, hutambulikana kama mzingiro mzima wa mila na desturi, ada na kawaida, ujenzi na ukaazi, utoto na usheza, nyago na nyagizi, jando, ngoma, starehe na pumbazi, ndowa na harusi, mavazi na hisiya, mapambo na pambizi, kupika, kupakuwa, kuandika chakula na kukila, kazi na ndima za kigosi, safari za anga, maji, ardhini, usiku, mchana na za kuruka kwa nyungo na mitungi. Nadhariya hii inatufundisha juu ya dhanna ya watu kwa yao. Kila watu ni watu kwao. Jamii zikishatambuu haya, sharti na zenyewe zibakiye hai kama jamii.
8. Nadhariya ya kimaudhuwi/kidhamira
Hii ni nadhariya kongwe sana na imetumiwa pia na wahakiki wakongwe kama Sengo na Kiango.

Sengo, anasema...Dhamira si dhamiri. Kwa hiyo msomaji asisome maneno ya mtunzi au mwandishi yanayoazimiya kadhaa nay eye akayachukuliya kuwa yaliyomo ni kadha wa kadha kutokana na hiyo kadhaa. Dhamira ni sehemu ya maudhuwi na maudhuwi ni yale yasemwayo na maandishi ya kazi ya fasihi. Dhamira ya mtunzi ya asili yaweza kuwa ni mgogoro wa wanandowa; maandishi yakatowa dhamira kadhaa juu ya kugongana wenyewe kwa wenyewe. Baada ya neno na neno, katikati, ndani na nnje ya maneno, mishororo, huwa mwapatikana visa na mikasa ya ajabu!

Aghalabu,mhusika mkuu, hubeba dhamira kuu na tajribu imetupa walimu fursa ya kumpima mtunzi au mwandishi kwa hayo yenye uzito kuwa ni yake yeye na huyo msemaji mkuu ni mwakilishi wake. Kuna kazi ambazo humpa nafasi huyo mtu aitwaye, “mpumbavu” kusemasema ya kipumbavu, kumbe hayo ndiyo kweli aliyoikusudiya mbunifu ama yale yanayodhihirika na ubunifu wenyewe.

Nadhariya hii ni kuu, nzito na muhimu sana. Kazi ya fasihi isipokuwa na yale mazito yasemwayo, huwa si kazi ya kuzingatiwa. Ama yawayo yawe kama maji ya mawaga au manyunyu yasiyojaza hata kikombe, hayo si maji ya mvuwa ya kifasihi inayoweza kukabidhiwa kokwa ardhini ikainywesha, ikaishibisha, ikaifungisha hadi kuifungulisha, ikaota, ikameya, ikachipuwa na kukuwa. Kwa wafanyao mitihani, ni swali la lazima kwa kila kitabu, kwa kila mtihani; wimbo unasema nini, riwaya yambaje, natiki inaeleza nini n.k.

9. Nadhariya ya fani
Kazi ya fasihi inasema nini, lipi, yepi, mwenziwe ni kazi hiyo ya fasihi yambaje, yasema vipi, kwa namna, mbinu, mtindo, lugha .... ipi? Duniya kusemwa ni ni jifa, mti mkavu, duniya, hadaa, nazi ama yai, na maisha ya mja kusemwa si lolote, si chochote, moto mkali, mtihani, hidaya, tunu, balaa..... Ni katika kupambika kwa fani ya usemaji. Uhodari wa kuitumiya lugha katika maandishi kunategemeya umahiri na umbuji wa hiyo lugha inayotumika. Fani ya lugha humudiwa na wenye lugha yao, ukitaka kukijuwa Kiswahili sharti uwajiye wenyewe Wapwani, ama kwa usuhuba ama kwa utafiti.

Tamathali za usemi kama zilivyoainishwa, sitiari, tashbiha, tashihisi, kejeli, vijembe...... n.k zinatokana na mtu kukuliya katika utamaduni wa viambo/mitaa ya lugha. Kiswahili kipana. Pemba kuna utajiri mwingi wa lugha ya Kiswahili ambao unauhitaji watafiti wa lugha kwenda kuufanyiziya kazi. Lugha ya sawasawa ikimkaa mtu, hasiti kuzimudu beti za kila bahari za arudhi ya Kiswahili asiliya, insha kabila zote, baruwa za kuliwaza na kupoza, posa pamoja na tungo aina aina za kila utanzu na vijitanzu – hakuna la kipera wala kapera. Kiswahili hakijashindwa wala hakishindwi ila kwa wanaotaka kukifisidi.
10. Nadhariya ya Dhima (Role) na kazi (Function)
Dhima ni wajibu. Kinyume chake ni jukumu, dhima ni kufanya lile litakiwalo. Dhima yamdai mtu kutimiza wajibu kwa jamii yake. suala la dhima si suala la orodha. Kuwa fasihi inafundisha, inaleya, inaonya, inaadibu, inaelekeza .... suala ni kwa vipi haya yanafanyika na kazi za fasihi zenyewe tafauti na kuonywa mtoto kwa kofi au fimbo? Utanzu wa ushairi kama vile wimbo au nyimbo, unaposemwa unafundisha, basi hufanya kazi zake hivi;
Wimbo Unaofundisha
Mwanangu kuwa usome,upende ujitahidi
Upate kazi uchume,ulipe na hizo kodi
Uzae wana utume,haya usiyakaidi
(TSYMS – ZNZ 18/04/08)

Unaleya
Mume wangu nakuomba,unisamehe ya jana
Mimi kwako ni mtamba,fahali ni lako jina
Kuleya ndowa ni kwamba,huba kusikilizana

Shairi linaloadibu
Unajiita katibu,Mtendaji wa Baraza
Kazi yako kuratibu,si mambo kujazajaza
Yafaa ujitanibu,acha watu kubamiza
U mtu wa bezabeza,wizara yakuadhibu

Utenzi unaoelekeza
Bi Fulani wanipenda
Kama kokwa kuipenda
Ama kisamvu kufunda
Kwanza kaa ufikiri

Nami piya nakuwaza
Moyoni wanikwaruza
Machoni wanipendeza
Hili jambo nalikiri






Tazama umri wangu
Mashavu na mvi zangu
Si mbali usoni kwangu
Kukuowa si vizuri

Ni huruma kukutoka
Edani nije kuweka
Mpweke utapwekeka
Hilo nahisi khattari

Likiwa ni la Qahari
Mwenyewe Akikhiyari
Nafsi inasubiri
Kwa ndowa iso fakhari

(TSYMS – SUZA 18/04/08)

Kama ni hadithi fupi, insha au riwaya, natiki ama utungo wowote basi kudondowa maneno, aya moja au mbili, huyafupisha yasemwayo lakini kwa ushahidi wa kazi zenyewe za fasihi kuthibitisha la Mussa la Mussa, la Issa la Issa na la Firauni la Firauni. Tukisema tu, fasihi inafundisha, kila somo lafanya hivyo, mapisi yanafundisha, elimunafsi au ushunuzi unafundisha, sayansi ama ulimbe unafundisha na asofunzwa na mamiye, hufundishwa na ulimwengu. Kinafundishwa nini? Kinafundishwa vipi?

Kazi ni kazi. Si kazi ya fasihi kuubadili Ulimwengu. Kazi ya fasihi kama dhima ni kuyaweka mambo uwanjani, Wachina wataelezeka uchina wao kwa kichina chao kwa ile fasihi yao hasa, na kwa lugha nyengine yoyote kwa manufaa ya hao wenye lugha hiyo kuwasoma na kupata fununu ya Wachina walivyo.

Kazi ya fasihi kilugha ni kumshawishi atakae kupata umahiri na umbuji wa lugha. Kamwe, fasihi haimfundishi mtu asiyetaka, lugha yoyote. Kama dhanna ya kazi ina nguvu, Afrika ndipo pahala pake. Hivyo ni juu ya walimu wa fasihi kutumiya mbinu mpya kushadidiya kwamba kila kifaacho katika fasihi, kwa manufaa ya jamii kitumiwe ili jamii nzima ijifunze kukitumiya. Kazi mojawapo ya fasihi, kwa kupitiya ubunifu ni kuwahamasisha na kuwahimiza wanafunzi watokezee kuwa watunzi na waandishi bora zaidi kuliko wa huko nyuma kwa vile wana wana vigezo, vyanzo na nyenzo zifaazo zaidi kuliko za zama za utangulizi.

11. Nadhariya ya Ushunuzi, Kero la Moyo, Hisiya za
    Nafsi
 Ili mtu apate ahuweni wa lile limkeralo, hapati pumbao wala pumuo, ila atowe pumzi zake kwa kutunga kitu-kiwe “kishada”, cha lulu na marijani, nudhumu, beti mbili tatu n.k. Mwalimu naye asomeshaye fasihi, na mwalimu wake mhakiki wa kazi za fasihi, raha yao ni kuyapa maneno fasili zao zinazotokana na ushunuzi nafsiya, kero za nyoyo au mioyo yao na vile wanavyojihisi. Mbinu hii ya hisiya, ndiyo iliyowatia kortini kina Sengo au Kiango (1973), kwa kudaiwa kutokana na HISI ZETU ati walisema FASIHI NI HISI. Hisiya za kila mtu ni maumbile ya kila mja. Mhakiki hamalizi kila kitu anapohakiki kazi ya fasihi. Pale anapoishiya yeye ndipo mwisho wa tamu na chungu yake, mwisho wa hisiya zake, hana tena. Hali hiyo isiwe sababu ya kumkwaza mhakiki wa pili na wa tatu, kufanya yao kwa uwezo wao. Waliokuja “kulima” wenzao, “kuwaponda”, karibu wote walikuwa wasungo wa lugha na fasihi, kisha ni mabega, hayakufika yakavikiuka vichwa; ni nazi, zilizojipiga mabweni, zilijipasuwa zenyewe.

Hisiya ni mbinu ya kiungwana, wasomi, wahakiki, waachiwe kazi, kwa kutaka ama bila ya kutaka, kwa kuweza ama bila ya kuweza; kila mmoja afanye anachotaka, anachoweza, kulingana na vionjo vyake na vile vilivyomzaa na kumleya.
12. Nadhariya ya Kiujumi
Kwa miyaka mingi, wanafasihi wa Uswahilini na wale wa fasihi kwa lugha ya Kiswahili, wamezowezwa kuzisoma kazi za fasihi kwa (i) kutazama maudhuwi-dhamira kuu na dhamira ndogo ndogo (ii) kutazama fani-lugha, mitindo mbalimbali, tamathali mbalimbali,miundo n.k. Nadhariya hii inatuelekeza tuanze kuzamiya mbizi ujumi-kwa maana ya ladha-tamu au chungu-ya kazi ya fasihi. Kuitazama kazi nzima na jinsi inavyomvutia msomaji kuisoma si mara moja wala mbili bali kila akimaliza, hupenda aisome tena na tena. Uhodari wa kubuni kitu au jambo hadi kikaonekana kwa macho au kikatamanika na ulimi, puwa na kuchekewa au kuliliwa na moyo, macho na kuhisika kwa hisiya zote hadi mkono au mguu ukatamani kugusa, huu ndiyo ubunifu wa kiujumi.


Mfano wa swali:
Bila kanuni fasihi isingekuwa na tanzu zinazofahamika. Ijadili kauli hii huku ukitoa mifano toka riwaya au tamthiliya zozote ulizosoma.
JIBU:
Ni kweli kwamba kazi yoyote ya fasihi isingeweza kutambulika tanzu zake na wala kuainishika kirahisi. Katika fasihi kanuni zinazotawala ni zile za kinadharia ambazo humuwezesha mtunzi au msomaji kubaini na kubainisha kazi ya fasihi iliyo mbele yake. Kwa minajili ya swali hili nitatalii mojawapo ya fasihi andishi kama ifuatavyo.
   Kanuni ya maudhui, kwa kuzingatia maudhui yanayojitokeza katika riwaya tunaweza kuzigawa riwaya katika tanzu mbili ambazo ni riwaya dhati na riwaya pendwa.
    Riwaya dhati ni zile zote ambazo maudhui yake huegemea kwenye kuifanya jamii iwe bora zaidi kimaudhui, kimaadili, kisiasa, kiuchumi na kifikra. Mifano ya riwaya dhati ni kama vile “ Wasifu wa Siti Binti Saad,” “ Vuta N’kuvute,” “ Kufikirika,” na “ Zawadi ya Ushindi”
        Riwaya pendwa ni zile ambazo maudhui yake huegemea kwenye masuala ya mapenzi,ujasusi,upelelezi na ujambazi. Ni riwaya ambazo hazina mchango katika kulinda na kutetea maadili ya jamii zaidi sana zinalenga kupata pesa, mifano ya riwaya pendwa ni kama vile, Mzimu wa Watu wa Kale, Simu ya Kifo, Tutarudi na Roho Zetu, Machozi Jasho na Damu, Mkimbizi, n.k
      Kanuni ya ukweli ni kanuni inayododosa ukweli kuhusu maisha ya wanadamu na jinsi anavyoyakabili mazingira yanayomzunguka kwa kigezo hicho tunapata riwaya za Ksaikolojia ambazo huwa zinasawiri maisha ya jamii. Riwaya hizi hutumia wahusika kuonesha jinsi mwanadamu anavyokabiliana na mazingira yake na kuyashinda au kushindwa na anaposhindwa huacha maswali mengi nyuma yake ambayo kila mmoja wa wasomaji atapata majibu yatakayompa ukweli. Mfano ni riwaya ya Rosa Mistika ambapo “Rosa” anapitia mazingira magumu yanayodhihirisha ubinadamu wake na mwisho anajiua na kuacha maswali juu ya kwanini amefanya hivi au vile. Kwa upande wa riwaya za kifalsafa hizi ni zile zinazolenga kutoa majibu ya maswali magumu katika jamii kwa kuonesha jinsi wahusika wanavyopambana hadi kupata suluhisho mfano riwaya ya Kiu ya Haki mhusika mkuu Mzee Toboa pamoja na kupatwa na shuruba nyingi alisimamia kweli na kila mtu akapata aki yake (Sikujua ambaye ndiye muuaji wa Pondamali akatiwa hatiani na kufungwa). Riwaya hizi kwa ujumla zinatoa majibu ya kisaikolojia na kifalsafa kuhusu maisha na ukweli wake.
        Kanuni ya mabadiliko; hii inaelekeza utunzi wa riwaya kwa kuzingatia uhalisia wa maisha ya historia ya jamii. Nchini Tanzania kanuni hii inazigawa riwaya katika vipindi mbalimbali kama vile kipindi cha uhuru ambacho kinachukua riwaya zilizotungwa kufurahia mafanikio hewa katika jamii mfano riwaya ya Ndoto ya Ndalia na Nyota ya Rehema hizi ni riwaya ambazo zilianza kuyaona mafanikio makubwa na yenye neema hata kabla inayotokea.
      Kipindi kilichofuata ni kile cha mfumo wa siasa ya ujamaa na kujitegemea na kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa, hapa watu walihubiriwa kuwa mafanikio yako vijijini kwenye kilimo kuliko mjini. Riwaya ya Shidani kielelezo cha mahubiri hayo na kipindi hiki pia kilikuwa na riwaya za kihakiki na zilizokosoa mfumo wa siasa uliopo kwa mfano riwaya ya Njozi za Usiku na Njozi Iliyopotea ni baadhi ya riwaya zilizokosoa utunzi wa kikasuku.
       Kipindi cha vita vya Kagera kiliibua riwaya za ujenzi wa jamii mpya zilizolenga kuhamasisha uzalendo kwa jamii. Mfano riwaya ya Zawadi ya Ushindi ambayo inaonesha jinsi vijana kama Sikamona wakijitoa muhanga kwenda vitani kupigana kwa ajili ya ukombozi wa nchi yao dhidi ya uvamizi wa nduli Iddi Amin wa Uganda.

         Kipindi cha mwisho ni kile cha kulegezwa kwa masharti na ujio wa uhuru wa soko huria na mwingiliano mkubwa wa kijamii. Kipindi hiki kina riwaya kama Makuwadi wa Soko Huria, Almasi za Bandia, Babu Alipofufuka, Kufikirika na Kusadikika. Kwa ujumla riwaya ni utanzu wenye kanuni zake ambazo kwazo wasomaji huweza kuziainisha na kuzibainisha katika makundi mbalimbali.
 
Powered by Blogger.