MAENDELEO YA KISWAHILI CHIMBUKO NA ASILI YA KISWAHILI
SURA YA TATU
MAENDELEO YA KISWAHILI
CHIMBUKO NA ASILI YA KISWAHILI
Neno chimbuko linarejelea
mahali kitu kilipoanzia. Hivyo basi tunapozungumzia chimbuko la
kiswahili ni dhahiri kuwa tunataka kujua ni wapi hasa kiswahili
kilianzia? Kuhusu chimbuko la kiswahili mpaka leo hakuna majibu sahihi
na yenye ushahidi wa kutosha kuthibitisha jambo hili na hii ni kusema
kuwa chimbuko la kiswahili halijulikani ni wapi hasa(Maelezo zaidi yapo
mbele). Neno asili lina
maana ya jinsi kitu au jambo lilivyotokea au lilivyoanza. Kwa hiyo
tunapoangalia asili ya kiswahili tunaangalia jinsi kiswahili
kilivyotokea au kilivyoanza
Kila lugha ina asili yake.Lugha huwapo ili kukidhi haja ya mahitaji ya
kimawasiliano ya jamii inayohusika . Lugha ya asili ya jamii yoyote
ndiyo inayotupa picha halisi ya shughuli za maisha ya jamii hiyo kwa
mfano shughuli ya kazi ,sanaa,ufundi,mila na desturi.
Historia ya Kiswahili inakabiliwa na matatizo ya ithibati (ushahidi) kuhusu chimbuko lake kutokana na:
i) kukosekana kwa ushahidi wa kutosha
ii) walioiandika historia hii ni wageni ambao waliandika kadiri walivyodhani baada ya kupata ushahidi mdogo sana
iii) kutofautiana kwa wataalamu kuhusu nadharia mbalimbali zinazohusu chimbuko la kiswahili.
Nadharia mbalimbali kuhusu asili ya Kiswahili.
1. Kiswahili asili yake ni Kongo.
Baadhi ya wataalamu hudai kuwa asili ya lugha ya kiswahili ni huko
Kongo ambayobaadaye iliitwa Zaire na sasa inaitwa Jamuhuri ya watu wa
Kongo.
Dai
hili linaimarishwa na wazo jingine linalodai kwamba katika vipindi
vilivyopita kuwa,sehemu za pwani ya Afrika mashariki hazikuwa zimekaliwa
na watu. Kutokana na hali ya vita sehemu za Kongo wabantu walisambaa
na kuja pwani ya Afrika mashariki kupitia Kigoma. Baadhi ya wabantu
hawa walipitia sehemu za Uganda wakati wa kusambaa kwao,walieneza pia
lugha zao ikiwemo hii ya kiswahili.
Udhaifu wa nadharia hii ni kwamba madai ya kuwa asili ya kiswahili ni
Kongo hayana msingi kwani mpaka sasa wataalamu wanaodai hivi hawajaweza
kueleza na kuthibitisha kisayansi ama kihistoria juu ya lini hasa watu
walianza kuishi pwani ya Afrika mashariki.
2. Kiswahili ni Pijini
Pijini
ni lugha mseto ya muda inayozuka pindi makundi mawili yenye lugha mbili
tofauti yakutanapo. Wenye kushikilia nadharia hii hudai kuwa Kiswahili
kimezuka kutokana na kuingiliana kwa wenyeji wa pwani na wageni wa
Kiarabu ambao kila mmoja alikuwa na lugha yake. Ili kufanikisha
mawasiliano katika shughuli za biashara ndipokulipozuka lugha hii ya
kati na kuwa lugha ya Kiswahili haikuwepo kabla ya ujio huu.
Kigezo
wanachokitumia ni msamiati mwingi wa Kiarabu katika Kiswahili kama vile
wakati , habari, salam.ahera, asante, shikamoo na mengineyo mengi.
Udhaifu
wa nadharia hii ni kuwa haiangalii vipengele vingine vya lugha kama
vile matamshi ya maneno, maumbo ya maneno na miundo ya tungo.
3. Kiswahili ni Krioli / lugha ya vizalia.
Kikrioli
ni pijini iliyokomaa na kutumiwa kama lugha ya awali ya wazungumzaji
wake . Wenye kuunga mkono nadharia hii husema kuwa Kiswahili kimetokana
na mwingiliano kati ya wanawake wenyeji wa pwani na waarabu ambapo
mwingiliano huo ulizaa uhusiano wa kimapenzi. Watoto waliozaliwa
(vizalia) ambao walikuwa ni chotara (suriyama) walijifunza maneno ya
kibantu toka kwa mama zao na ya kiarabu toka kwa baba zao. Katika
harakati za kujirekebisha wakajikuta wanaongea upotoshi wa lugha ya
Kiarabu. Hivyo Kiswahili ni upotoshi wa matamshi ya lugha ya kiarabu.
Kigezo wanachokitumia ni msamiati na matamshi
Mfano:
Wakt - wakati
Khabar – habari
Udhaifu
wa nadharia hii ni kuwa haiangalii lahaja zingine za Kiswahili ambazo
zinasikilizana katika msamiati, matamshi, maana za maneno na miuundo ya
tungo.
Lahaja
maana yake ni tofauti ya usemaji unaojitokeza kati ya wasema lugha
moja. Utofauti huu waweza kuwa wa kimatamshi ama maumbo ya maneno lakini
msingi wa maana na miundo hubaki kuwa ileile. Baadhi ya lahaja za
Kiswahili ni Kiunguja, Kimakunduchi Kimafia, Kilamu, Kimvita,
Kinzuwani,Kingazija , Kimtang’ata, nk.
ZOEZI:
1. Unadhani ni kwa sababu gani nadharia za pijini na krioli hazijitoshelezi kuthibitisha madai yao?
2. Eleza uarabu uliomo katika lugha ya Kiswahili.
4. Kiswahili ni Kiarabu
Kuna hoja kuu tatu ambazo baadhi ya wananadharia hii huzitumia kutetea nadharia hii kuwa Kiswahili asili yake ni Kiarabu.
(i)Inahusu
neno lenyewe Kiswahili ambalo asili yake ni Kiarabu. Neno Kiswahili
linatokana na neno “sahel”(umoja) na “sawahil”(wingi) kwa maana ya
pwani.
(ii) Inadaiwa kuwa maneno mengi yenye asili ya kiarabu yaliyomo
katika kiswahili ni ishara kuwa kiswahili kilianza kama pijini ya
kiarabu
(iii)
Inadaiwa kwamba kwa kuwa Kiswahili kilianzia pwani, na kwa kuwa idadi
kubwa sana ya wenyeji wa pwani ni waislamu na kwa kuwa uislamu uliletwa
na Waarabu, basi Kiswahili nacho kililetwa na Waarabu.
UDHAIFU
(i) Lugha ya Kiswahili imetokea kuwa na maneno ya kigeni yenye
asili ya Kiarabu, lakini si Kiarabu tu bali hata lugha nyingine kama
Kiajemi, Kireno,Kihispania nk. Wasemaji wa lugha mbili tofauti
wanapokutana hawaachi kuathiriana kilugha. Lugha kuwa na maneno mengi ya
kigeni toka lugha nyingine hakuifanyi iwe imetokana na hiyo lugha
nyingine.
.
(ii)
Kigezo cha dini nacho hakikubaliki, lugha haiwi lugha kwa sababu ya
imani. Hata hivyo lugha ya Kiarabu yenyewe ilikuwepo karne nyingi kabla
ya majilio ya uislam, kama ambavyo lugha nyingine za
kimagharibi zilivyokuwepo karne
nyingi kabla ya majilio ya ukristo. Kiingereza au Kijerumani si
ukristo, wala Kiarabu si uislamu ila tunaweza kutumia lugha kufasili
dini lakini hatuwezi kutumia dini kufasili lugha.
5. Kiswahili ni kibantu
Kswahili kimetambulishwa kuwa ni lugha mojawapo ya lugha za kibantu. Neno Bantu lina
maana ya mtu (wingi:Abantu) katika lugha nyingi za waafrika wanaoishi
kusini mwa jangwa la sahara . Lugha za watu wanaoishi katika eneo hili
huitwa lugha za kibantu. Lugha za kibantu zina ufanano katika msamiati
na
Muundo wa sentensi.
Mfano:
Neno ‘wana’ (watoto) – Kiswahili
Vana - kingoni
B’ana - kihaya
Pia muundo wa sentensi ya Kiswahili
“wana ( watoto) wawili wanaoga” unafanana na miundo ya :
i) Kingoni (vana bavili visamba)
N V T
ii)Kichaga( wana wawi wakesamba)
N V T
iii) Kizigua (Wana waidi wahaka)
N V T
iv) Kihaya ( Abana babili mb’oga)
N V T
Nadharia hii huiangalia lugha ya Kiswahili kuwa ni Kibantu.
Wanaounga mkono mtazamo huu hutumia zaidi ushahidi wa kiisimu.
Huichunguza lugha ya Kiswahili katika mfumo mzima wa historia ya
mgawanyiko na kusambaa kwa lugha za Kibantu na huhitimisha kuwa
Kiswahili ni mojawapo ya lugha katika jamii kubwa ya lugha za Kibantu.
Ubantu wa Kiswahili
Ushahidi wa kiisimu unathibitisha ubantu wa Kiswahili. Ushahidi wa
kiisimu ni ushahidi unaothibitishwa kwa misingi inayohusu sayansi ya
lugha. Isimu ni taaluma inayoangalia lugha kwa undani (kisayansi)
kuzungukia tanzu kama vile isimu historia, isimu linganishi ,isimu
jamii, isimu nafsi,isimu matumizi na isimu fafanuzi.
Lugha
ya Kiswahili ilifanyiwa utafiti na uchambuzi na wanataaluma kadhaa kwa
madhumuni ya kuiainisha kama ilikuwa yenye misingi ya Kibantu au
la.Vipengele vifuatavyo vinathibitisha ubantu wa Kiswahili.
1. MSAMIATI
Msamiati
wa msingi wa lugha ya Kiswahili na lugha za Kibantu unafanana
kabisa. Msamiati wa msingi ni ule unaohusu mambo ambayo hayabadiliki
badiliki kutokana na shughuli za utamaduni. Tofauti zinaweza kujitokeza
katika matamshi au mabadiliko kidogo ya viambishi vyake, lakini si
mzizi.
Mfano:
Kswahili: Mtu mtoto (Mwana) maji
Kizigua Umunu Umwana manzi Kihehe Muntu Umwana amanji
Kikurya Omonto Omona amanche
1. Tungo (sentensi) za Kiswahili
Miundo
ya tungo (sentensi) za Kiswahili inafanana sana na miundo ya tungo za
Kibantu. Sentensi za kiswahili na lugha za Kibantu zina kiima na
kiarifu.
K A
Kiswahili: watoto wawili / wanaoga
Kingoni: vana bavili / visamba
Kizigua: wana waidi / wahaka
Kichaga: wana wawi / wakesamba
3. Ngeli za majina
Hapa kuna makubaliano kufuatana na ngeli katika maumbo ya nomino (umoja na wingi wa majina) pamoja na upatanisho wa kisarufi.
(i)Maumbo ya majina
Kigezo
hiki hufuata maumbo ya umoja na uwingi katika kuyaainisha majina.
Majina mengi katika lugha ya Kiswahili na lugha za Kibantu hufuata
mkondo wa umoja na wingi. Majina ya lugha ya Kiswahili na lugha za
Kibantu mengi yana maumbo dhahiri ya umoja na uwing
Mfano:
Umoja Wingi
Kiswahili mtu Watu
Mtoto Watoto
Kibena Umwana Vana umunu Vanu
Kikuyu Omonto banto(abanto) Omona Bana(abana)
Kizigua Mwana bhana
(ii) Upatanisho wa kisarufi
Katika
kigezo hiki tunaangalia uhusiano uliopo kati ya nomino/ vivumishi na
viambishi awali vya nafsi katika vitenzi vya Kiswahili na
Kibantu. Vivumishi, majina pamoja na vitenzi hivyo hubadilika kutokana
na maumbo ya umoja na wingi.
Mfano:
Umoja wingi
Kiswahili baba analima Baba wanalima
Kindali tata akulima/ Abhatata chakulima
KikuryaTata ararema/Batata (tata) bararema
Kijita tata kalima /Batata kabalima
4.Vitenzi vya Kiswahili na Kibantu
Kuna
uhusiano mkubwa sana kati ya vitenzi vya Kiswahili na vile vya
Kibantu. Vipengele vinavyothibitisha uhusiano huu ni:viambishi,
mnyumbuliko, pamoja na mwanzo / mwisho wa vitenzi.
(i) viambishi
Lugha ya kiswahili na lugha za kibantu vitenzi vyake hujengwa na mzizi (kiini) pamoja na viambishi vyake (awali na tamati)
Mfano:
Kiswahili: -analima – A – na – lim- a
Kikuvya – ararema –A- ra_ rem –a
1 2 3 4
1. kiambishi awali kipatanishi cha nafsi
2. kiambishi awali cha njeo (wakati uliopo)
3. mzizi / kiini
4. kiambishi tamati
(ii)Mnyambuliko wa vitenzi
Mnyambuliko wa vitenzi vya lugha ya Kibantu hufafanana na ule wa vitenzi vya lugha ya Kiswahili
.
Mfano:
Kiswahili – kucheka – kuchekesha kuchekelea
Kibena – kuheka – kuhekesha – kuhekelela
Kinyamwezi – kuseka – kusekesha – kusekelela
(iii)mwanzo wa vitenzi
Vitenzi vingi vya Kiswahili na vitenzi vya lugha za Kibantu huanza na viambishi amabavyo ni viwakilishi vya nafsi:
mfano:
Kiswahili Ninakwenda
Kihaya Ningenda
Kiyao Ngwenda
(iv) Mwishilizo wa vitenzi
Vitenzi vya lugha za Kibantu na Kiswahili huishia na irabu – a
mfano:
Kiswahili - kukimbia
Kisukuma – kupela
Kiswahili - kula
Kizigua – kudya
Zoezi
1.Kwa kutumia mifano jadili asili ya kiswahili.
2.Kwa kutumia lugha yako (kibantu) jadili ubantu wa kiswahili.
3.“Uarabu wa kiswahili una hoja zake”, zitaje na zielezee.
4.“Kiswahili ni Kiarabu kwa jina lake, lakini ni Kibantu toka nitoke kwa asili yake” Thibitisha kauli hii kwa hoja madhubuti.
CHIMBUKO LA KISWAHILI
Neno chimbuko lina maana ya mahali kitu au jambo lilipoanzia. Ama kuhusu suala
la mahali hasa ambapo ndiyo chimbuko la lugha ya Kiswahili wataalamu
wanahitilafiana. Wengine wanadai kuwa lugha ya Kiswahili inatokana na
Kingozi lugha ya kaskazini mashariki mwa Kenya, na wengine wamesema kuwa
Kiswahili chimbuko lake ni Kishomvi kilichozungumzwa na watu wa
Bagamoyo na Mzizima eneo linalojulikana kwa jina la Dar –es Salaam hadi
Kilwa.
Wengine
wanadai kuwa baadhi ya wabantu walifanya maskani yao ya kudumu katika
mabonde ya kaskazini mwa mto Tana. Kikundi hiki cha wabantu ndicho
kinasadikiwa kuwa chimbuko la Kiswahili katika mabonde hayo, wabantu
walianzisha makazi yao Shupate na Shungwaya.
Mnamo
miaka 500 AD, makazi ya mto Tana yalivamiwa na kushambuliwa na kabila
la Wagala. Uvamizi huu uliwafanya wenyeji wake kukimbia na kusambaa
katika sehemu mbali mbali za pwani ya bahari ya Hindi.
Lakini
ikumbukwe kwamba kuna wakazi ambao walikuwa wakiishi maeneo mbali mbali
katika upwa wa Africa mashariki waliokuwa wakizungumza lugha zao mbali
mbali. Lakini kwa kuwa lugha hizo zote zilikuwa za Kibantu zilikuwa
hazitofautiani sana. Sasa basi, katika kuwasiliana wao kwa wao katika
masuala ya kibiashara wasemaji wa lugha hizo mbali mbali walilazimika
kurahisisha lugha zao kwa kiasi fulani ili waweze kuelewana na wenzao
katika kurahisisha lugha zao hizo katika maeneo mbali mbali kukazuka
lugha moja iliyoeleweka kwa watu wote wa eneo hilo.
Hali
hii ilitokea katika sehemu yote ya upwa wa Afrika mashariki kuanzia
kaskazini hadi kusini. Matokeo yake yakawa ni lugha ambazo baadaye
zilikuja julikana kama lahaja za kiswahili. Hivi ndivyo ilivyotokea
lahaja ya Kibajuni Kitikuu katika sehemu za kusini mwa Somalia hadi
kaskazini mwa Kenya. Kisiu sehemu za Pate, Kiamu katika Lamu,
Chichifundi, Kimvita .
Katika
sehemu za Mombasa, Kivumba, Kimtang’ata katika sehemu za pwani ya
kaskazini mwa Tanzania, Kimakunduchi, Kihadimu, Kitumbatu katika sehemu
za Unguja na Pemba n.k. Hilo ndilo lilikuwa Chimbuko la lugha ya
Kiswahili kama tuijuavyo leo.
Ukizichunguza
kwa makini lahaja hizo za Kiswahili ni dhahiri kuwa ni lugha kamili
zinazojitegemea. Vile vile lahaja hizo zinafanana zaidi na lugha
nyingine za Kibantu kuliko zinavyofanana na lahaja ya Kiswahili sanifu
ambayo ina maneno mengi ya kigeni.
ZOEZI
1. Eleza maana ya lahaja, kisha taja lahaja zisizopungua tano na utaje mahali zinakozungumzwa.
2. Kwanini lahaja za pwani ziliitwa Kiswahili?
3. Kiswahili ni matokeo ya lahaja mbali mbali, je ni mushkeli gani unazikumba lahaja hizo baada ya tokeo hilo?
KUKUA NA KUENEA KWA KISWAHILI WAKATI WA WAARABU
Waarabu
walifika pwani ya Afrika ya Mashariki karne ya 8, Walipofika waliwakuta
wenyeji wakizungumza lugha zao za Kibantu kikiwemo Kiswahili. Waarabu
walipofika na dini ya kiislamu walijikuta wakishirikiana na wenyeji wa
upwa huu katika mambo makuu matatu: Dini, biashara na kuoana (ndoa). Ili
waweze kueneza dini yao vyema, Waarabu walijifunza kwa dhati lugha ya
Kiswahili kwa vile walijishughulisha pia na biashara, waarabu waliweza
kujumuisha mambo mengi kwa mara moja.
BIASHARA
Ikumbukwe
kwamba wenyeji wa pwani na wenyeji wa bara walikuwa na mawasiliano ya
karne nyingi. Kulikuwa na safari za kibiashara baina ya pwani na bara
zilizokuwa zikifanywa na waafrika wenyewe.
Wageni walipofika katika upwa huu waliongozwa kwenda bara na
wafanyabiashara wenyeji wa pwani na bara. Wafanyabiashara hao ndio
walioanza kuieneza lugha ya kiswahili.
Watu waliofuatia katika kuineza lugha hii walikuwa wale wafanya
biashara wa kiarabu waliofuata pembe za ndovu na watumwa. Na hapa
inabidi ikumbukwe kwamba ingawa biashara ya pembe za ndovu na watumwa
iliendeshwa na waarabu wao sio walioineza lugha hii. Wao wenyewe
hawakuijua, walikuwa wakifundishwa na wenyeji wao. Walioieneza lugha hii
katika misafara hiyo ya kwenda bara walikuwa wenyeji wa pwani na bara
ambao walikuwa wapagazi wa waarabu.
(Ramani kuonyesha misafara ya biashara ichorwe hapa)
DINI
Mbali na shughuli za biashara uenezaji wa dini za kigeni pia ulichukua
nafasi muhimu sana katika kueneza lugha ya Kiswahili. Waarabu walipoleta
dini ya kiislamu walitumia sana lugha ya Kiswahili katika kuwashawishi
wenyeji wa pwani kuslimu. Kwa kuwa mafundisho ya dini ya kiislamu
yalikuwa katika Kiarabu, na kwa kuwa wenyeji wengi wa pwani hawakujua
kiarabu wahubiri wa dini walilazimika kujifunza Kiswahili ili waweze
kutoa mafundishop na fasili za Kurani katika lugha iliyoeleweka kwa
wengi. Baada ya hapo Waarabu waliojua
Kiswahili
pamoja na ndugu zao wenyeji wa pwani wakapeleka uislamu bara kwa
kutumia Kiswahili. Mashehe na Maulama wakaanzisha matumizi ya maandishi
ya Kiswahili kwa kutumia alfabeti ya kiarabu. Kwa kufanya hivyo, wakawa
wamesaidia sana katika kukineza Kiswahili.
Zoezi
1 Ni jinsi gani shughuli za waarabu zilichangia kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania?
KUKUA NA KUENEA KWA KISWAHILI WAKATI WA UTAWALA WA WAJERUMANI
Lugha
hukua inapojiongezea msamiati wa kutosha . Wajerumani walikuza lugha ya
Kiswahili kwa kuiongezea msamiati kama vile shule , mashine ,hela nk.
Kuenea kwa lugha maana yake ni lugha kuwa na eneo pana kimatumizi pamja na watumiaji wengi.
Wajerumani walipoingia Tanganyika walikuta tayari kuna misingi mizuri
ya lugha ya Kiswahili, hivyo utawala wa kijerumani ulipoanzishawa nchini
Kiswahili kilikuwa tayari kimeimarika.
Kwa misingi hiyo wajerumani waliona bora watumie lugha ya Kiswahili
katika shughuli zao, licha ya jambo hili kupingwa sana huko ujerumani
ambako waliona kuwa katika makoloni ilikuwa ni lazima lugha ya
Kijerumanii ienezwe ili hatimaye kujengwa dola ya Kijerumani iliyo imara
katika misingi yote ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Aidha baadhi
ya wajerumani waliona lugha ya Kiswahili ilihusiana sana na dini ya
kiislamu; kwa hiyo hawakuipenda kabisa. Jambo hili halikufanikiwa kwani
wajerumani wenyewe walitumia lugha ya Kiswahili katika shughuli zao,
ikiwa ni pamoja na mahubiri ya dini ya kikristo.
Katika
shughuli za utawala walilazimisha kila Akida afahamu Kiswahili barabara
ili aweze kutumwa na kufanya kazi mahali popote, siyo tu katika sehemu
aliyozaliwa na kukulia. Hivyo wajerumani waliweka Kiswahili kama chombo
cha kuwasiliana na watawaliwa wao na walilazimisha wafanyakazi wote wa
serikali kujua Kiswahili. Wajerumani wenyewe walijifunza kiswahili huko
kwao kabla ya kuja Tanganyika.
Shuleni
Kiswahili kilitumika kama lugha ya kufundishia na Wajerumani walijenga
shule Tabora, ujiji, Kilimatinde, Usangu mwaka 1905 na hatimaye Bukoba ,
Mpwapwa, Iringa, Mwanza, Kilosa, Tukuyu, na Moshi. Vyuo vya kufundishia
walimu vilianzishwa huko Tabora na Bukoba.
Vile
vile wajerumani walianzisha mashamba makubwa ya mazao ya biashara na
wakalazimisha watanganyika kutoka bara na pwani kufanya kazi ya kulima
katika mashamba hayo. Kwa kuwa walikuwa watu wa makabila mbali mbali
Kiswahili kilitumika sana katika mawasiliano na wale waliobahatika
kurejea nyumbani walisaidia kukieneza Kiswahili huko kwao.
Kutokana
na wajerumani kusisitiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli za
utawala, shule, mahakama na hata katika kuwasiliana na wananchi
walisaidia sana kukieneza sehemu mbali mbali za Tanganyika.
ZOEZI
1. Eleza kwa vipi wajerumani walikuza na kueneza lugha ya kiswahili nchini Tanzania.