Zitto Kabwe: ACT Tutasimama wenyewe
Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT – Wazalendo,
Zitto Kabwe (pichani) amesema kuwa chama chake hakitashirikiana na
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), badala yake
kitasimama chenyewe kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Kauli
hiyo inazima minong’ono iliyotawala miongoni mwa wanachama wa
ACT-Wazalendo waliokuwa wakimuuliza Zitto kuhusu chama hicho kujiunga na
Ukawa.
Zitto alimaliza uvumi huo jana jijini hapa
katika mkutano na viongozi wa chama, wanachama na watiania wa nafasi
mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu.
Alisema ACT-Wazalendo
haiwezi kuungana na Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD kwa vile sera ya chama hicho tofauti na vyama hivyo.
“Nawaomba
niwatoe hofu, Chama cha ACT-Wazalendo kitasimama chenyewe kama kilivyo,
hatutaki ushirikiano,” alisema Kabwe na kuongeza:
“Najua
chama chetu bado ni kichanga, kina miezi mitano tangu kuanzishwa kwake,
lakini si mnajua Timu ya Soka ya Mbeya City?” aliwauliza wajumbe
waliojibu: “ndiyo.”
“Ile timu ilianza kama masihara,
lakini mwisho wa siku ikawa tishio kwa timu za Ligi Kuu, basi chama hiki
kitakuwa hivyo,” alisema Zitto na kushangiliwa na wajumbe waliohudhuria
mkutano huo.”
Alibainisha kuwa chama chake kimedhamiria kuwatumikia Watanzania na kushika dola kwa njia halali.
Alisema ACT – Wazalendo kina azimio la Tabora, ambalo
ndani yake kuna kipengele namba nne, kinachozungumzia miiko na mali za
viongozi kabla ya kujiunga na chama hicho na kwamba chama chochote
kitakachotaka kujiunga ACT, lazima kikubaliane na kipengele hicho ili
kuzuia mianya ya rushwa na uroho wa madaraka ndani ya chama.
Aliwataka wanachama kutotishika na mtikisiko wa kisiasa utakaotokea muda wowote kuanzia wiki hii, kwani ni mambo ya kawaida.
“Mtikisiko
huu usiwatie presha, mtulie tena mnyooshe miguu juu, huu ni upepo wa
kisiasa na wala haututoi kwenye mstari. Narudia tena viongozi wangu ACT,
mkoa msiyumbishwe na hali itakayojitokeza,” alisema.
“Hatuna presha kufanya vikao vya mara kwa mara, chama kwa masilahi ya watu fulani, tutafuata ratiba yetu vizuri,” alisema Zitto.
Alisema ACT-Wazalendo kinaendeshwa na wanachama na siyo viongozi, hivyo kila uamuzi hufuata kanuni na taratibu za chama.
“Ndiyo
maana kuna chama kimoja (hakukitaja), hadi leo (jana) kinapiga danadana
kumtangaza mgombea wake wa urais sijui wanamsubiri atoke kwenye Sayari
ya Mars,” alihoji Zitto.
Zitto alisema kuwa
atashirikiana na wagombea wote watakaopitishwa na chama hicho kugombea
nafasi mbalimbali ili majimbo 10 ya Mkoa wa Dar es Salaam yaende
ACT-Wazalendo.
“Juzi nilikuwa Jimbo la Kigoma Mjini,
kuna chama kimoja kilikuwa kinatafuta mgombea atakayewakilisha jimbo
hilo maana kila anayeambiwa anakataa, kwa sababu wanasema ni ngome ya
ACT-Wazalendo,” alisema.