Wajawazito feki washtukiwa BVR Dar
Mkazi
wa Mtoni Mtongani jjijini Dar es Salaam, Gathi Kibacho (kushoto)
akibonyeza sehemu maalumu katika mashine ya BVR kuchukua alama za vidole
alipokuwa akijiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura. Kulia
ni Msimamizi wa uandikishaji, Frank Ernest. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapigakura kwa Mkoa wa Dar es Salaam, unaendelea pamoja na
kujitokeza kasoro kadhaa, ikiwa na pamoja na baadhi ya watu kutumia
mbinu mbalimbali ili kukwepa foleni.
Katika Kituo cha
Bwawani Shule, Mtoni Kijichi, wanawake wawili waliojifanya wajawazito,
walibainika kufanya udanganyifu huo huku mmoja akiwa tayari
amejiandikisha.
Gazeti hili lilishuhudia mzozo huo baada ya wasichana wawili kupitishwa kutokana na hali zao.
Hata hivyo, mmoja wa majirani ambaye anawafahamu, alidokeza kuwa anawafahamu wasichana hao na hawakuwa na wajawazito.
Mmoja alikuwa amekwishajiandikisha na aliwahi kuondoka mapema kabla ya mwenzake aliyekuja kwa staili hiyo na kushtukiwa.
Baada
ya mzozo huo, aliondoka taratibu eneo la tukio ndipo baadhi ya watu
walipoanza kumkimbiza kubaini iwapo ni mjauzito au la.
Kuona
hivyo, msichana huyo, aliyatoa makaratasi aliyokuwa ameyafunga tumboni
mithili ya ujauzito na kuyatupa, huku akikimbia na kutokomea katika
vichochoro vya Mitaa ya Mtoni Kijichi.
Mmoja wa
wasimamizi wa kituo hicho, alisema kuwa hawana kawaida ya kuwakagua
isipokuwa wanachoangalia ni hali za watu wakiwamo wajawazito, walemavu,
wazee na wenye watoto wachanga.
Mbali na kasoro hiyo,
baadhi ya vituo vya kuandikisha wapigakura vimeongezewa mashine za BVR
ili kukabiliana na ongezeko la watu katika vituo hivyo kabla ya kazi
hiyo kufungwa Julai 31.
Hata hivyo, bado kuna
msongamano mkubwa wa watu katika vituo vingi na kusababisha baadhi yao
kupigana kwa waliochukua namba na wale ambao ni wapya.
Vituo kadhaa Jimbo la Temeke vimeonekana kuwa na msongamano mkubwa wa wananchi licha ya kuongezewa mashine.
Mwenyekiti
wa Mtaa wa Mtoni, Kata ya Mtoni, Omary Mateso alisema kadiri siku
zinavyokwenda ndivyo kasi ya uandikishaji inavyoongezeka. Alisema siku
ya kwanza waliandikisha watu 495 na siku ya pili watu 587.
Mwandishi
msaidizi katika Kituo cha Shule ya Msingi Mtoni, Abdallah Luambano
alisema kutokana na mwitikio wa wananchi, waliamua kuomba mashine
nyingine ili kuongeza ufanisi.
“Changamoto
tunayokabiliana nayo ni kuharibika kwa mashine au wakati mwingine
kushindwa kusoma alama za vidole vya baadhi ya watu hasa wanawake
kutokana na kupaka mafuta mikononi,” alisema.
Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa wa Mbuyuni, Selemani Mpoyo alisema tatizo kubwa
lililopo kwenye vituo ni utaratibu unaotumika kuandikisha watu. Alisema
jana walikuwa wanaandikisha majina, lakini siku inayofuata watu
waliowahi kituoni hawakubali kuanza na majina ya jana.
Katika Kituo cha Shule ya Msingi Kibondemaji, Mbagala, uandikishaji ulikwenda vizuri.
Mwenyekiti
wa Mtaa za Zakhem Mbagala, Rajab Masunga alisema walianza na mashine
tatu za kuandikisha, lakini kutokana na wingiwa watu wameongezewa
nyingine tatu.
Katika kituo cha uandikishaji cha Shule
ya Msingi Mbagala, pia mashine ziliongezwa na kuthibitishwa na
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbagala, Said Makacha.
Kituo cha
Shule ya Msingi Makamba, Temeke mashine pia ziliongezwa sanjari na Kituo
cha Shule ya Msingi Makamba, lakini kilielezwa kuwa hakikuwa na
utaratibu mzuri wa kuandikisha.
Taharuki kwenye vituo
Baadhi ya wananchi walilazimika kuzipiga kavukavu kutokana na wengine kutaka kuwapita wenzao waliofika vituoni mapema.
Shuhuda
wa tukio hilo, Mohamed Hamad alisema watu waliopigana walikuwa
wakigombania nafasi ya kuwahi kujiandikisha na polisi walipopata taarifa
walifika na kumkamata mmoja.
Akizungumza kwa sharti
la kutotajwa jina lake, msimamizi wa kata hiyo amekiri kutokea kwa tukio
hilo na kueleza kuwa mtu huyo alishikiliwa na kuwekwa mahabusu kwa muda
na baadaye alichukuliwa kwenda kuandikishwa, kisha akaachiwa huru.
Msimamizi
wa mawakala wa Chama cha CUF, Kombo Mhina ameeleza kuwa kuna baadhi ya
watu 10 waliokuwa wamebaki jana na wakaandikana majina, lakini leo
wamejikuta wako 90, jambo ambalo limesababisha ngumi katika Kituo cha
Shule ya Msingi Makumbusho.
Naye Juma Yusufu alieleza kuwa uandikishaji unafanyika kwa kujuana.
Alisema
mtu akitoka anamwita mwingine aingie wakati amechelewa na kuna wakati
mtu unakwenda kujiandikisha kitambulisho kinatoka na jina la mtaa wa
mbali na unapojiandikishia.
Baadhi ya vituo hali ni shwari licha ya kulalamikiwa kwenda kwa kusuasua katika maeneo ya Tandale, Sinza na Manzese.
Katika
Kituo cha Sinza D, idadi ya watu waliojitokeza kujiandikisha ilikuwa si
kubwa kama maeneo ya Tandale, lakini malalamiko makubwa yalikuwa katika
ufanisi wa mashine za BVR.
Mara kwa mara mashine hizo
zimekuwa zikisumbua, hivyo kusababisha watendaji kusimamisha kazi kwa
muda ili kufanya matengenezo. Jambo hili limechangia kutuweka kituoni
kwa muda mrefu, alifafanua Rajab Hassan (34), mmoja kati ya watu
waliokuwa kwenye foleni hadi saa saba mchana.
Hata
hivyo, baada ya kufika saa moja na nusu asubuhi, mwandikishaji alikana
kumtambua na hivyo kulazimika kukaa tena kwenye foleni. Hadi gazeti
lilipokuwa likipita kwenye kituo hicho saa saba mchana kijana huyo
alikuwa bado hajajiandikisha.
Mkuu wa Kituo cha Sinza
D, ‘A’ Abdallah Amour, akizungumzia tatizo la kusuasua kwa uandishi
kunakosababishwa na matatizo ya mashine, alisema kuwa ni kweli kuwa
mashine hizo zimekuwa zikipata matatizo, lakini mafundi wao wamekuwa
wakizishughulikia.
Mwananchi lilishuhudia misururu
mirefu katika maeneo ya Shule ya Tandale Magharibi na Shule ya Mpakani,
Manzese karibu na eneo la Mabibo. Licha ya kutawaliwa na amani,
kulikuwa na malalamiko hayohayo ya kwenda taratibu kazi ya uandikishaji
kulikosababishwa na kususua kwa mashine.
Mnyika alonga
Mbunge
wa Ubungo, John Mnyika ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
iongeze mashine za uandikishaji katika maeneo mbalimbali ili kuendana
na wingi wa wananchi waliopo katika mkoa wa Dar es Salaam.
Kauli ya Nec
Mkurugenzi
wa NEC, Julius Malaba alisema jana kuwa suala la mashine kufanya kazi
usiku ni kawaida ila lazima watu katika eneo husika wakubaliane.
Kuhusu
kuharibika kwa mashine, Malaba alisema timu ya wataalamu wa IT inapita
kila kituo ambacho kimebainika mashine zake kutofanya kazi vzuri na
kuzirekebisha.“Hii iliwahi kutokea Arusha, kuna sehemu wadau
walikubaliana na wakaendesha uandikishaji hadi usiku, kuhusu mashine
tulishasema tutaziongeza ili kukidhi mahitaji kadiri siku zinavyokwenda
na kila mmoja mwenye sifa, ataandikishwa,” alisema.
“Suala la mashine kukutwa na majina kabla haijaanza kufanya kazi nitalifuatilia nijue ukweli wake.,” alisema Malaba.
Imeandikwa na Peter Elias, Suzan Mwillo, Emma Kalalu, Maimuna Kubegeya na Colnely Joseph.