Rais Kikwete apewa Tuzo ya Utawala Bora
Jakaya Kikwete
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete
ametunikiwa Tuzo ya Utawala Bora Afrika kwa mwaka 2015 kutokana na
jitihada zake za kudumisha na kuimarisha utawala bora nchini.
Taarifa
iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kuwa Rais
Kikwete ametunikiwa tuzo hiyo na Taasisi ya African Archievers Awards
yenye makao makuu nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa
taarifa hiyo, Rais Kikwete anaungana na Askofu Desmond Tutu wa Afrika
Kusini aliyekuwa wa kwanza kupewa tuzo hiyo mwaka 2011 kutokana na
mchango wake wa kutetea haki za binadamu, usawa na amani.
“Rais
Kikwete ameteuliwa kutoka miongoni mwa watu 1,202 ambao majina yao
yaliwasilishwa kwenye jopo la kimataifa, linalojitegemea na lenye
wajumbe kutoka Uingereza na Afrika Kusini kwa ajili ya uteuzi,” ilisema
taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, kutokana na
tuzo hiyo, Rais Kikwete amealikwa kwenda kuipokea nchini Afrika Kusini
kesho mjini Johannesburg.
Hata hivyo, Rais Kikwete
hataweza kwenda kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi, hivyo badala
yake atakwenda Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro.
Katika
barua ya kumjulisha Rais Kikwete kuhusu uteuzi wake, Mtendaji wa
African Achievers Awards, Rex Indaminabo alisema: “Uongozi wa African
Achievers Awards unayo furaha kukujulisha juu ya uteuzi wako wa kupokea
Tuzo katika kundi la Utawala Bora Afrika.”
Mtendaji
huyo aliongeza: “Ni kwa furaha na heshima kubwa kuwa wajumbe wa Bodi ya
Ushauri na Taasisi ya Uongozi na Menejimenti wanakupongeza kwa mafanikio
haya.”