Kishindo cha Obama Kenya

Nairobi, Kenya. Shangwe na shamrashamra zimeendelea kutawala mjini Nairobi kufuatia kuwasili kwa Rais wa Marekani Barack Obama aliyewasili jana akiwa ameambatana na ujumbe mzito.
Rais Obama ambaye alipokewa na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta na baadaye kuwa na mazungumzo mafupi hii ni ziara yake ya kihistoria na inafanyika katika wakati taifa la Kenya likijitahidi kujitambulisha upya baada ya kuandamwa na matukio ya kigaidi na mvutano wa siasa za ndani.
Leo kufungua mkutano wa kibiashara
Rais Obama leo atajitokeza hadharani kwa mara ya kwanza akifungua mkutano wa kimataifa unawajumuisha wajasiriamali, wachumi  pamoja na wawekezaji mkutano ambao unatajwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa uchumi wa Kenya.
Mkutano huo ambao pia unahudhuria na zaidi ya wajumbe 3,000 unachukuliwa kama daraja muhimu la kuanzisha majadiliano ya uwekezaji baina ya Marekani na Kenya hasa kupitia mpango unaojulikana kama Agoa.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kwa ziara yake hiyo mjini Washington, Rais Obama aliitaja Afrika kama bara linalochipua kwa kasi na linapaswa kuungwa mkono kwa kila hatua.
Hii ni ziara yake ya kwanza tangu aingia madarakani na kwamba inachukuliwa kama fursa ya pekee kwa Kenya kukuza utalii na kuwavutia wawekezaji wa kigeni.
Obama kuzungumza na wanafunzi, kuhutubia taifa
ADVERTISEMENT
Kesho inatarajiwa kuwa moja ya siku yenye shughuli nyingi kwa Rais Obama ikiwamo kukutana kwa faragha na ndugu na jamaa zake walisafiri kutoka kijiji alichozaliwa cha Kogelo hadi mjini Nairobi kukutana na kiongozi huyo.
Pia, Rais Obama atatembelea Chuo Kikuu cha Kenyatta na baadaye kuzungumza na viongozi vijana akielezea mambo mbalimbali yanayohusu utawala na kuwapa moyo  namna wanavyoweza kutimiza ndoto zao. Baadaye  ataelekea katika Uwanja wa Karasani ambako anatarajia kutoa hutuba yake inayosubiriwa na wengi.
Jumla ya watu 5,000 ikiwamo wabunge, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, wafanyabiashara na maofisa wa serikali watahudhuria mkutano huo. Haikuweza kufahamika mara moja yale yatakayojitokeza kwenye hotuba yake hiyo lakini kuna uwezekano mkubwa akagusia masuala yanayohusu utawala bora, mapambano dhidi ya ugaidi na vipaumbele vya maendeleo kwa Afrika.
Waziri Kenya aishukia CNN
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Nkaissery ameitaka a televisheni ya CNN ya Marekani kuwaomba radhi Wakenya kwa kuitaja nchi hiyo kuwa ni uwanja wa ugaidi.
Waziri Nkaissery amesema: Kama televisheni ya CNN imestaarabika vya kutosha basi ilipaswa kuwaomba radhi Wakenya. Waziri huyo alisema nchi hiyo inakabiliwa na mashambulizi ya kigaidi kama zilivyo nchi nyingine dunia lakini suala hilo haliifanyi kuwa eneo salama kwa ugaidi.
Waziri Mkaisserry amewataka Wakenya kuidharau ripoti ya televisheni ya CNN kama inavyostahiki. Msimamo huo mkali wa Kenya umekuja baada ya kituo cha televisheni ya CNN cha Marekani kupeperusha habari iliyodai kuwa Kenya ni ‘uwanja wa ugaidi’, siku moja kabla ya Rais wa Marekani kuwasili nchini humo.
 CNN ilipeperusha habari iliyodai, “Rais Barack Obama siyo tu anaenda nyumbani kwa babake, pia anazuru ‘uwanja wa ugaidi.”
Powered by Blogger.