Siri nzito Ukawa, vikao vyaendelea mfululizo
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe (kulia) akifurahia jambo na wajumbe wa Kamati
Kuu ya chama hicho walipohudhuria kikao cha dharura katika Hoteli ya
Bahari Beach, jijini Dar es Salaam jana. kuanzia kushoto ni Ezekia
Wenje, Mchungaji Peter Msigwa na Naibu Katibu wa chama hicho (Zanzibar),
Salum Mwalimu. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dar/Arusha. Licha ya Baraza Kuu la Uongozi
la Chama cha Wananchi (CUF) kupokea taarifa ya Ukawa na kuamua chama
hicho kiendelee kushiriki katika umoja huo, bado suala la mgombea urais
wa vyama vinavyounda umoja huo limeendelea kuwa siri nzito.
Taarifa
zilizopatikana kutoka ndani ya CUF jana, zilisema kuwa katika kikao
chake kilichoketi juzi na jana mjini Zanzibar, baraza hilo lilipokea
taarifa ya Ukawa, kuithibitisha na kuamua chama hicho kiendelee na
ushirikiano huo.
Mkutano wa waandishi wafutwa
Pamoja
na hayo, jana kutwa nzima viongozi wa Ukawa walikuwa kwenye vikao
mfululizo na hakukuwa na taarifa rasmi zilizopatikana na hata mkutano na
waandishi wa habari ulioitishwa jana jioni uliahirishwa bila kueleza
utaitishwa tena lini.
Ingawa taarifa ya mkutano wa
Ukawa na wanahabari haikutaja ajenda, habari zilizoenea katika mitandao
ya kijamii zilibainisha kuwa walikuwa wanakusudia ama kutangaza chama
kilichopitishwa na Ukawa kusimamisha mgombea urais au kutangaza jina la
mgombea mwenyewe pamoja na mgombea mwenza.
Vyanzo
mbalimbali ndani ya Ukawa, vilieleza kuwa ufunguo wa hatua hiyo ulikuwa
unashikiliwa na CUF, ambayo hivi karibuni ilijitenga na umoja huo ili
masuala yake yajadiliwe kwanza na vikao vyake vya maamuzi kabla ya
kurejea kwenye meza ya majadiliano.
Taarifa za uhakika
kutoka katika kikao hicho kilichoketi Zanzibar kwa siku mbili,
zilibainisha kuwa wajumbe waliafikiana kinyume na ilivyotarajiwa kuwa
wangevurugana.
Miongoni mwa mambo ambayo inadaiwa wameafikiana ni kuwa mgombea urais atoke Chadema na chama hicho kitoe mgombea mwenza.
Jussa: Watanzania mtafurahi
Hata
hivyo, mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Jussa Ismail Ladhu alipoulizwa
alisema ikiwa itaamuliwa mgombea mwenza wa Ukawa atoke CUF, hakutakuwa
na shida kwa kuwa chama hicho kina wanasiasa wazuri, safi na makini na
kwamba kitatoa mtu ambaye Watanzania wote watafurahi.
“Ikiamuliwa
kuwa mgombea mwenza atoke CUF, wananchi msiwe na wasiwasi, CUF ina
hazina nyingi, itatoa mtu bora, itawapa chaguo ambalo Watanzania wote
wataridhika nalo,” alisema Jussa.
Pamoja na
kuthibitisha kuwa Baraza hilo limeamua CUF iendelee kushiriki katika
umoja huo, Jussa alisema kwenye mjadala matatizo kidogo yalikuwapo
katika mgawanyo wa majimbo.
Hata hivyo alisema baada ya
kuweka vigezo vya kuwa na mgombea wa Ukawa, sasa hakuna shida kwa kuwa
majimbo machache yaliyosalia utaratibu wake utatangazwa hivi karibuni.
Kuhusu
mgombea mwenza, Jussa alisema CUF ina nafasi kubwa ya kutoa mgombea
huyo kwa sababu ndicho chama chenye nguvu Zanzibar na kina wanasiasa
mahiri na makini.
Wagombea wetu tunataka wawe ni wale
watakaohakikisha kuwa Katiba Mpya inapatikana mara baada ya uchaguzi ili
kuyaweka sawa mambo yanayohitaji kuwekwa sawa.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa Katiba, mgombea urais na mgombea mwenza wanapaswa
kutoka chama kimoja, hivyo kama Chadema itamtoa mgombea urais inabidi
pia mgombea mwenza atoke chama hicho.
Habari ambazo bado si rasmi zinasema kuwa mmoja wa viongozi wa CUF anaweza kuhamia Chadema ili kukidhi matakwa hayo ya Katiba.
Mkurugenzi
wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF,
Salim Bimani alisema kuwa mambo katika Ukawa ni mazuri, wapo waliofikiri
kuwa watavurugana, lakini wamekubaliana na sasa Watanzania wasubiri
kupata wagombea safi katika ngazi zote.
Bimani alisema CUF kitaendelea kushirikiana na vyama vingine vya upinzani nchini ili kuhakikisha demokrasia inazidi kukua.
Vikao mfululizo Chadema
Habari
zaidi zilizolifikia gazeti hili zilisema mshirika mwingine wa Ukawa,
Chadema jana viongozi wake walikuwa katika kikao cha dharura cha Kamati
Kuu kilichoshirikisha wajumbe wachache, hasa wale wanaopatikana kwa
kupigiwa kura ili kuweka mambo sawa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alikiri kuwapo kwa kikao hicho.
“Kamati
Kuu ya Chadema inaendelea kukutana jijini Dar es Salaam kwa kikao
maalumu cha dharura kujadili mambo mbalimbali,” alisema Makene katika
taarifa yake fupi aliyotuma jana usiku.
“Mambo hayo ni
pamoja na maandalizi ya chama kuelekea uchaguzi mkuu, kupokea taarifa za
mwenendo wa kura za maoni na uteuzi wa awali wa nafasi za ubunge wa
majimbo na viti maalumu zinazoendelea nchini nzima,” alisema Makene.
Habari
za ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika Hoteli ya Bahari Beach
jijini Dar es Salaam, zilisema kuwa kilikuwa na jukumu la kupokea
taarifa ya utafiti iliyofanywa nchini kote kuhusu mgombea anayekubalika
zaidi.
Ingawa hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu utafiti
huo, lakini taarifa zinazoendelea kusambaa zinalitaja jina la waziri
mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa yuko mbioni kuhama chama chake cha
CCM na kwenda Chadema, huku mgombea mwenza akitajwa kuwa atatoka upande
wa Zanzibar CUF.
Mgombea mwenza kuhamia Chadema
Habari
za ndani ya Ukawa zinasema chini ya makubaliano ya Ukawa ikiwa mgombea
urais atatoka Chadema, mgombea mwenza akitoka chama kingine itabidi
ahame chama chake ili aingie chama alicho mgombea urais ili kukidhi
matakwa ya kikatiba.
“Tutakaposhinda uchaguzi, kama
makamu wa rais atatoka CUF itabidi kila akitoka katika ofisi ya makamu
wa rais, kituo cha kwanza atasimama Makao Makuu ya CUF kwa ajili ya
kupeleka taarifa na kupata baraka za chama katika masuala muhimu.”
Chanzo
chetu cha habari kinasema: “Ikiwa Ukawa tutashinda Uchaguzi Mkuu
Oktoba 25 na kupata nafasi ya urais, jambo la kwanza litakuwa ni kufanya
Mabadiliko ya Katiba na kuruhusu demokrasia pana ya watu kuungana.”
Alisema hakuna ajabu yoyote kwa rais kutoka chama kimoja na makamu wa rais kutoka chama kingine.
“Hilo
hata sasa linatendeka Zanzibar ambako Rais na Makamu wa Kwanza wa Rais
wanatoka vyama tofauti na hakuna matatizo yoyote katika utendaji wa
Serikali, kila mmoja anasimamia kwanza maslahi ya Taifa pili kuhakikisha
sera za chama chake zinatekelezwa,” kilieleza chanzo cha habari.
Lowassa atajwa
Hii
ndiyo ajenda ambayo imetawala mijadala kuhusu fununu za Lowassa kuhama
CCM kwenda Chadema ili kukamilisha safari yake ya matumaini.
Gazeti
hili linafahamu kuwa mazungumzo na Lowassa yamekwishafikia hatua nzuri
ingawa kulikuwa na viongozi wachache ndani ya Chadema waliokuwa
wameshikilia msimamo wa kumkataa lakini kutokana na presha iliyopo ndani
na nje ya chama wasingefua dafu.
Mtei amkaribisha
Huku
mjadala kuhusu Lowassa ukizidi kukolea, mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei
amemkaribisha mwanasiasa huyo na makada wengine wa CCM kujiunga na chama
hicho kikuu cha upinzani.
Akizungumza na Mwananchi
jana, Mtei alisema kwa sasa Chadema na Ukawa wanahitaji kura za kutosha
kuing’oa CCM, hivyo hata kura ya mtu mmoja ni muhimu.
“Nimesikia
Lowassa anatajwa kutaka kujiunga na Chadema, mimi namkaribisha aje, si
yeye tu, aje na makada wengine wa CCM kwa kuwa tunapaswa kuimarisha
nguvu za kuiondoa CCM madarakani,” alisema.
Alisema
Chadema ni chama cha Watanzania wote hivyo hakiwezi kumfungia milango
Mtanzania mwenye sifa za kujiunga na chama hicho asijiunge.
Hata
hivyo, Mtei alisema makada hao wa CCM ambao wanataka kujiunga na
Chadema endapo watakuwa na nia ya kupata uongozi, wajue kuna vikao vya
kuwapitisha.
“Tunawakaribisha Chadema makada wote wa
CCM bila masharti na kama wana nia ya uongozi Chadema ina vikao vya
kupitia kulingana na sifa zao na vikao vitakuwa na maamuzi ya mwisho,”
alisema.
Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, alisema ana uhakika muungano wa upinzani ndio silaha kubwa ya kuing’oa CCM madarakani.
“Uchaguzi
uliopita Chadema tulishinda lakini tulichakachukuliwa lakini safari hii
kupitia Ukawa tumejipanga kuhakikisha upinzani tunashinda kwa kiasi
kikubwa,” alisema.
Alisema hadi sasa Chadema na ukawa kwa ujumla wake kuna viongozi wenye sifa ya kushinda urais na wanakubalika nchi nzima.