Kumekucha Yanga, Azam
Mshambuliaji
wa Yanga, Amissi Tambwe (chini) akishindwa kufunga bao huku beki wa Al
Khartoum, Hamza Daoud akimtazama wakati wa mchezo wa mwisho wa Kundi C
wa mashindano ya Kombe la Kagame uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam jana. Yanga ilishinda 1-0. Picha na Anthony Siame
Dar es Salaam. Fainali ya Kombe la Kagame
imekuja mapema, hicho ndicho unachoweza kusema baada ya wawakilishi wa
Tanzania Bara, Yanga na Azam kukutana katika mchezo wa robo fainali
itakayopigwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga
imekata tiketi ya kuivaa Azam baada ya kuifunga Al Khartoum 1-0
shurkani kwa bao pekee la Amissi Tambwe ambaye katika mchezo alipoteza
nafasi nyingi za kufunga.
Ushindi huo unawafanya
mabingwa hao wa Tanzania Bara kufikisha pointi tisa, na kushika nafasi
ya pili katika Kundi A akiwa nyuma kwa pointi moja kwa vinara Gor Mahia
(10),
Al Khartoum imeshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba.
Mchezo
kati ya Yanga na Azam utakuwa ni marudio ya fainali ya Kombe la Kagame
2013 iliyochezwa kwenye uwanja huo, ambao Yanga ilibuka na ushindi wa
mabao 2-0.
Pia mchezo huo utakuwa ni utangulizi wa mchezo wa Ngao ya Jamii itakayochezwa Agosti 22 baina ya timu hizo.
Katika
mchezo wa jana, Yanga ilianza mchezo huo taratibu na dakika ya 3, kipa
wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ alifanya makosa kwa kurudisha mpira
vibaya uliomkuta mshambuliaji wa Al Khartoum, Amin Ibrahimu, lakini
kabla ya kupiga shuti Mbuyu Twite aliwahi na kutoa mpira huo nje.
Yanga
ilitumia dakika 14 kabla ya kufika kwa mara ya kwanza langoni mwa Al
Khartoum kwa kutumia shambulizi la kushtukiza kupitia Joseph Zutah
aliyepia pasi ndefu kwa Busungu, lakini beki wa Wasudan hao walikuwa
makini kukoa hatari hiyo.
Wasudan hao walitawala mchezo
kwa kufanya mashambulizi mengi, lakini safu ya ulinzi ya Yanga ilikuwa
makini kuwadhibiti wasilete madhara golini kwao.
Tambwe
alifunga bao lake la kwanza katika mashindano hayo akiunganisha kwa
kichwa kona iliyopigwa na Haruna Niyonzima katika dakika 29, na kuamsha
shangwe kwa mashabiki wa Yanga.
Kuingia kwa bao hilo
kulifanya Yanga kujiamini na kuanza kushambulia kwa kutumia mipira
mirefu na krosi na dakika 34, Tambwe nusura afunge bao la pili baada ya
kuunganisha krosi ya Zutah kwa kubinuka tikitaka, lakini mpira wake
haukulenga lango.
Al Khartoum ilifanya mashabulizi yake kupitia Atif
Khalifa, Domenic Abui na Amin Ibrahim, lakini mashuti yao yote yaliishia
mikononi mwa Barthez na mengi yalitoka nje na kuifanya Yanga kwenda
mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kocha wa Yanga,
mwanzoni mwa kipindi cha pili alimtoa Oscar Joshua na kumwingiza Haji
Mwinyi katika jitihada zake za kupunguza mashambulizi ya Wasudani.
Niyonzima
alipiga shuti lililogonga mwamba na kumkuta Coutinho akiwa yeye na
lango, lakini shuti la Mbrazili huyo lilishindwa kulenga lango na kutoka
nje katika dakika ya 56, wakati mashabiki wa Yanga wakiwa hawaamini
kilichoteka, Tambwe naye akiwa yeye na kipa alishindwa
kuunganisha krosi ya Msuva kwa kupiga shuti juu katika dakika 58.
Licha
ya mchezo huo kuwa wa kukamilisha ratiba na kutafuta nafasi ya pili,
ulikuwa wa bahati mbaya kwa Al Khaetoum, kwani walipoteza nafasi nyingi
za wazi kama ilivyokuwa kwa Yanga.
Kasi ya mchezo
ilikuwa juu kwa kila timu kushambulia kwa zamu kadri inavyopata nafasi
ya kufanya hivyo na kuufanya mchezo kushindwa kutabirika mshindi hadi
kipenga cha mwisho, ingawa Yanga ilikuwa ikiongoza kwa bao hilo tangu
dakika ya 30.
Awali, mashabiki wa Gor Mahia baada ya
timu yao kushinda 3-1 dhidi ya Djibout Telecom, walikuwa wakiimba kwa
kusema ‘tunaitaka Yanga, tunaitaka Yanga’.
Mabingwa hao
wa Kenya, Gor Mahia imemaliza kwa kishindo hatua ya makundi kwa ushindi
huo mnono, shukrani kwa mabao ya Geogre Odhiambo katika dakika ya 13,
Michael Olunga alipachika bao la pili dakika ya 28 na Enock Agwanda
alipachika bao la tatu dakika 79, huku Said
Hassan
akifunga bao la kufutia machozi wa Telecom.Akizungumzia mchezo huo,
Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm alisema wapo tayari kuvaana na Azam
kwani kuingia katika mashindano ni kuwa tayari kukutana na mpinzani
yoyote.
Yanga: Ally Mustapha, Joseph
Zutah, Oscar Joshua/ Haji Mwinyi, Pato Ngonyani, Kelvin Yondani/Nadir
Haroub, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe,
Malimi Busungu na Andrey Coutinho/ Godfrey Mwashiuya.
Al Khartoum:
Mohamed Ibrahim. Amin Ibrahim, Hamza Daoud, Saleheldim Mahamoud,
Samawal Merghani, Wagdi Awad, Anthony Agay, Domenic Abui, Atif Khalif,
Badreldin Eldoon na Ahamed Adam.