Fomu za urais Chadema kaa la moto
Viongozi wa Chadema kutoka kulia ni Freeman Mbowe akifuatiwa na Tundu Lissu na Katibu Mkuu wa Chadema Dk.Wilbroad Slaa
Dar es Salaam. Wakati leo saa 10 jioni
ndiyo muda wa mwisho uliopangwa kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa
kuwania urais ndani ya Chadema, hadi sasa hakuna mwanachama hata mmoja
aliyejitokeza kuzichukua.
Badala yake zimetolewa kauli
tofauti kuhusu kusuasua kwa mchakato wa kumpata mgombea urais hadi chama
hicho kulazimika kusogeza mbele tarehe ya mwisho ya kuchukua na
kurejesha fomu.
Hali hiyo inazidisha sintofahamu
iliyougubika mchakato wa urais ndani ya chama hicho na ndani ya Ukawa,
kuwa huenda kuna ‘mtu wa nne’ anayesubiriwa kutoka nje ya chama hicho,
kama ilivyoripotiwa na gazeti hili, wiki iliyopita.
Likikariri
chanzo cha kuaminika ndani ya Ukawa, gazeti liliandika kuwa huenda
umoja huo na hasa Chadema, wanasubiri mgombea kutoka nje ya chama kwa
kuwa hata baada ya wajumbe wa vikao vya mashauriano kukubaliana kuwa
mgombea wa Ukawa awe Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, baadhi
ya wajumbe kutoka katika chama hicho wanadaiwa kukataa kutangazwa kwake.
Hata
baadaye walipoulizwa nini msimamo wao kuhusu tetesi za mpango wa
kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutoka CCM, viongozi
na wabunge wa chama hicho walisema anakaribishwa mradi tu afuate kanuni
na taratibu.
Suala la mgombea urais wa Chadema na Ukawa
limeendelea kuteka mjadala wa kisiasa nchini huku Watanzania wakisubiri
kufahamu nani atateuliwa kupambana na yule wa CCM, Dk John Magufuli,
hali inayosababisha baadhi ya watu kudai mchakato huo una mizengwe.
Hata
hivyo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa, Gaudence Mpangala
alisema anadhani hakuna mizengwe inayowazuia baadhi ya wanachama
wasiwanie nafasi hiyo kwa kuwa kanuni na taratibu za vyama ziko wazi.
Alisema anachokiona ni kwamba wanachama hawajajipanga kuwania nafasi
hiyo ya juu.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo alisema wako watu ambao
hawawezi kugombea nafasi ya urais kuwakilisha vyama vyao kwa sababu
wanawaogopa viongozi wa juu wa vyama hivyo.
“Jambo la
msingi la kuangalia ni haki kutendeka katika kila mchakato katika uteuzi
lakini watu wanawania nafasi kulingana na walivyojipanga,” alisema.
Alisema
wingi wa wagombea urais katika vyama si kigezo pekee cha kukua kwa
demokrasia bali mchakato wa kuwapata wagombea hao ukiendeshwa kwa haki
ndiyo demokrasia.
Alisema kuwa hakuna ubaya hata kama kuna mgombea mmoja anayewania urais bali kinachotakiwa kuangaliwa ni ubora wa mchakato.
Hakijaeleweka
Katika
mkutano wake uliofanyika mjini Mwanza Jumatano ambao ulipangwa kutumika
kumtangaza mgombea urais wa chama hicho, Mwenyekiti wa chama hicho,
Freeman Mbowe aliwaomba Watanzania wavumilie wakati wanakamilisha
taratibu za kumpata mgombea huyo.
Pia, ilielezwa kuwa
chama hicho kilikuwa kinasubiri mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF
unaofanyika leo, huku taarifa nyingine zikisema chama hicho kilikuwa
hakijampata mgombea mwenza kutoka Zanzibar.
Wakati hayo
yakiendelea, bado ratiba ya kuchukua fomu za urais na kurudisha ilikuwa
inaonyesha ni leo na hakukuwa na dalili zinazoonyesha watu kujitokeza
kuwania nafasi hiyo ya juu, ambayo mara kadhaa viongozi wa chama hicho
wametamka kuwa tayari wamempata mgombea anayefahamika ndani na nje ya
nchi.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Slaa aliliambia
Mwananchi jana kuwa asingeweza kusema lolote kuhusiana na suala hilo kwa
sababu alikuwa nje ya ofisi.
“Wasiliana na watu walioko ofisini, wao wataweza kujibu vizuri swali lako,” alisema Dk Slaa.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Dk Slaa aligombea urais na kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Gazeti
hili lilipotaka kufahamu iwapo safari hii Dk Slaa amechukua fomu,
alikataa kusema lolote akidai taarifa hizo zitapatikana kwa walioko
ofisini.
Wabadili ratiba
Akizungumzia
hali hiyo jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu
alisema kuna marekebisho yamefanyika katika tarehe hiyo ya mwisho
kurejesha fomu ambayo yatatangazwa ndani ya simu mbili au tatu ambayo
yalilenga kupisha mchakato wa kura za maoni.
“Unajua
viongozi wanatakiwa kusimamia kura za maoni majimboni, kwa hiyo tuliona
kwanza tumalize hili, suala la mgombea urais lisubiri kwanza.
Tunatarajia kutangaza tarehe mpya ya kurejesha fomu ndani ya siku
mbili,” alisema Mwalimu na kuthibitisha kuwa hadi wanasimamisha shughuli
hiyo hakukuwa na mwanachama yeyote aliyechukua fomu za kuomba kuteuliwa
kugombea urais.
Baadaye jioni jana, chama hicho kilitoa taarifa ya kusogeza mbele tarehe ya kurudisha fomu hadi Julai 31, 2015 saa 10 jioni.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, watiania wote watapaswa kurejesha fomu hizo
katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni, Dar es
Salaam.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa ratiba ya awali
iliathiriwa na kitendo cha kusogeza mbele tarehe za uchukuaji na
urejeshaji wa fomu za ubunge baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi
kutangaza majimbo mapya 26.
“Hatua hiyo iliathiri
ratiba ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania uteuzi wa kugombea
urais kupitia Chadema ambapo awali wanachama wenye sifa walipaswa kuanza
kuchukua fomu 20-25 Julai, mwaka huu,” ilisema taarifa hiyo.
Mkutano Mbeya waahirishwa
Katika
hatua nyingine, ziara ya Dk Slaa aliyetarajiwa kuwasili na kuhutubia
mkutano jijini Mbeya leo imefutwa hadi itakapotangazwa tena.
Mratibu
wa chama hicho Kanda ya Nyasa (Chadema), Frank Mwaisumbe alisema sababu
ya kufutwa ni viongozi wa kitaifa kuendelea na vikao vya ngazi ya juu
jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chadema mkoani
hapa, Joseph China alisema ziara hiyo imefutwa kutokana na viongozi
wakuu wa kitaifa kutingwa na vikao vya Ukawa.
Viongozi wa kitaifa wa Chadema wakiwa Mwanza walitangaza kwamba wangefanya mikutano mingine, Mbeya, Arusha na Dar es Salaam.