Obama awagusa Wakenya, awataka kuacha ukabila
Rais wa Marekani, Barack Obama (kulia), akiwasalimia wananchi wa Kenya kwenye Ukumbi wa Safaricom Arena baada ya kuwahutubia mjini Nairobi jana. Picha na AFP
Nairobi, Kenya. Rais wa Marekani, Barack
Obama amezungumzia safari yake ya kwanza aliyoifanya Kenya, mwaka 1988
na kupoteza begi lake baada ya kushuka katika Uwanja wa Ndege wa Jomo
Kenyatta (JKIA).
Akizungumza na Wakenya katika Uwanja
wa Kasarani, jijini Nairobi, Obama alisema anamshukuru dada yake, Auma
Obama kwa kumpokea katika safari hiyo miaka kadhaa iliyopita.
Obama alisema anafurahia kufika nchini humo akiwa rais wa kwanza wa Marekani.
Obama
alipokwenda Kenya wakati huo, begi lake lilipotea na baada ya
kufuatilia aliambiwa kwamba lilisafirishwa hadi Afrika Kusini na ndege
aliyokuwa amepanda.
Katika hotuba yake, Obama alimshukuru pia Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa ukarimu wake na mapokezi makubwa aliyoyapata.
Pia aliwaomba radhi ndugu zake wa Kijiji cha Kogello kwa kutofika huko kwa ajili ya kuwasalimia.
Rais
huyo alisema anatambua juhudi zilizofanywa na wazee wakati wa kupigania
uhuru akiwamo babu yake ambaye alikuwa ni mmoja wa wapiganaji katika
Jeshi la Kings African Riffles (KAR).
“Babu yangu alikuwa Burma akitumikia Waingereza. Baada ya vita alifungwa kwa muda kwa kupinga ukoloni,” alisema Obama.
Rais Obama alisema ameona mabadiliko makubwa nchini humo, ikiwamo kukua kwa uchumi wa Kenya.
Alisema zamani Afrika Kusini ndiyo iliyokuwa na uchumi mkubwa, lakini sasa Kenya inakaribia kuifikia Afrika Kusini kiuchumi.
Rushwa inazuia uchumi Kenya
Rais
Obama alisema rushwa imekuwa changamoto kubwa kwa nchi nyingi za Afrika
na tatizo hilo limekuwa likisababisha ukiukwaji wa haki za binadamu na
kuathiri shughuli za Serikali.
“Urasimu ni kikwazo cha
utawala bora na mfumo wa utoaji haki, Serikali haina budi kujenga
mazingira mazuri kwa watu wake na kupambana na rushwa,” alisema Rais
Obama, huku akishangiliwa na watu waliohudhuria mkutano huo.
Alisema
rushwa inarudisha nyuma maendeleo ya uchumi na aliwataka Wakenya
kubadilisha mtazamo wao juu ya rushwa ili waweze kukabiliana na tatizo
hilo.
Rais Obama alisema licha ya kuahidi kuwapatia
kinamama na vijana mabilioni ya fedha, wasi wasi wake mkubwa ni rushwa
ambayo imekuwa ikikwamisha ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.
Pia, alizungumzia ugaidi na kuwataka Wakenya kuongeza juhudi za kupambana nao.
Obama ameahidi kushirikiana na Kenya katika kupambana
na magaidi likiwamo kundi la Al-Shabaab ambalo limekuwa likiishambulia
Kenya na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha.
Kenya, Marekani kudhibiti ugaidi
Katika
uwanja huo ambako maelfu ya watu walikusanyika kumsikiliza Rais Obama,
alisema amezungumza na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu nchi hizo mbili
zitakavyopambana na ugaidi.
“Kwa kiasi kikubwa
tumepunguza nguvu ya Al Shabaab, lakini haimaanishi kwamba tumefanikiwa
kutatua tatizo la ugaidi,” alisema Rais Obama.
Alisema
Serikali ya Marekani inafurahia juhudi za Kenya katika kukabiliana na
mashambulizi ya kigaidi na kwamba atashirikiana na nchi hiyo katika
kudhibiti makundi ya kigaidi nchini humo.
“Ugaidi ni
mbaya, sasa tunaomboleza waliouawa Westgate na Garissa na katika maeneo
mengine. Kenya ipo njia panda katika kufikia malengo yake,” alisema Rais
Obama.
Rais Obama alilazimika kutoa kauli hiyo
kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea katika jengo la Westgate
na kusababisha watu 67 kupoteza maisha na wengine 148 kufariki dunia
Aprili mwaka huu kwenye Chuo Kikuu Cha Garissa baada ya Al-Shabaab
kushambulia chuo hicho.
Mbali na hayo, Obama aliwataka
Wakenya kuheshimu haki za binadamu na kuacha vitendo vya udhalilishaji
kwa wanawake, huku akionya raia wa nchi hiyo kuacha kuwaozesha wasichana
wadogo.
“Mimi ni Mwafrika ninayeishi Marekani, naumia
sana ninapoona watu wananyimwa haki zao kutokana na sheria kupindishwa,
hili halikubaliki,” alisema.
Katika hatua nyingine;
Rais Obama aligusia suala la mapenzi ya jinsia moja, lakini Rais
Kenyatta alisema kwamba suala la haki za binadamu katika upande wa
mapenzi ya jinsia moja halikubaliki na kwamba, hoja hiyo haina mashiko
kwa raia wa nchi hiyo.
Demokrasia na ukabila
Pia, aliwataka Wakenya kuimarisha demokrasia na kutumia fursa mbalimbali kuwawezesha vijana kuinuka kiuchumi.
Pia,
aliwaonya Wakenya kuacha tabia ya kubaguana kwa majina yao ya mwisho na
kutupilia mbali siasa za ukabila kwa sababu zinaharibu maendeleo ya
Taifa hilo.
“Watu hawafai kuhukumiwa kwa sababu ya
majina yao ya mwisho au dini. Tukianza kubaguana kwa misingi ya
kikabila na ukiutazama uchumi wa Kenya, mwisho tutaumia,” alisema.
Lakini
wakati watu wengi wakifurahia ziara ya Rais Obama, wafanyabiashara wa
44 walikuwa wakilalamika jana kwa kushindwa kufungua biashara zao baada
ya kufungwa kwa Barabara ya Thika kutokana ziara hiyo. Obama aliondoka
jana kwenda Ethiopia.
Imeandikwa na Peter Elias kwa msaada wa mashirika ya habari.