Ikulu yakanusha Rais kulipwa Dola 16,000 kwa mwezi


Dar es Salaam. Siku moja baada ya tovuti ya Mwananchi kunukuu habari zilizoripotiwa na Mtandao wa African Review, kuhusu mishahara ya marais wa Afrika na kwingineko duniani, Ikulu imekanusha habari hizo ikisema si za kweli.
Bila kutaja mshahara wa rais ni kiasi gani, taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu juzi, ilisema habari hizi siyo za kweli. Ni uongo na uzandiki. Ni uzushi mtupu na ni uzushi wa hatari.
Taarifa ya Ikulu imeikariri ripoti hiyo ya Mtandao wa African Review ikisema: “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete anashikilia nafasi ya tano miongoni mwa viongozi 38 wa Afrika wanaolipwa mshahara mnono zaidi.
“... Kuwa Rais Kikwete analipwa Dola za Marekani 192,000 kwa mwaka, ikiwa ni malipo ya Dola za Marekani 16,000 kwa mwezi… Mshahara wa Rais kwa mwezi ama kwa mwaka haufikii na hata wala kukaribia kabisa kiwango kinachotajwa na Gazeti la Mwananchi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo bila kutaja kiwango anacholipwa.
Taarifa hiyo iliendelea kusema: “Tangu Uhuru, mwaka 1961, Rais wa Tanganyika na baadaye tangu mwaka 1964 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa miongoni mwa viongozi wanaolipwa mishahara ya chini kabisa duniani. Mshahara wa Rais wa Tanzania kwa mwezi ni wa chini kiasi cha kwamba mshahara wake unazidiwa, tena kwa mbali na mishahara wanayolipwa baadhi ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma nchini.
“Ni jambo la kushangaza kwamba Gazeti la Mwananchi, linalochapishwa hapa nchini, linaweza kupata kiasi cha uongo anacholipwa Rais wa Tanzania katika mitandao ya nje badala ya kuuliza rasmi na kupewa majibu sahihi kwa kujiingiza katika uzushi wa kupindua kiasi hiki.
“Gazeti la Mwananchi haliwezi kuwa na nia nyingine yoyote isipokuwa nia ya kuwachochea wananchi na kuwajengea chuki dhidi ya Serikali yao na kiongozi wao mkuu,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Ilimaliza taarifa hiyo kwa kusema: “Ni matarajio yetu, kuwa Gazeti la Mwananchi litafanya jitihada za makusudi, kama taaluma ya uandishi wa habari inavyoelekeza, kutafuta usahihi wa jambo hili na kuwaambia Watanzania ukweli.”
Powered by Blogger.