Wastara: Ulemavu Unanikosesha Hamu ya Kuolewa

Leo kwenye safu hii mwanadada Wastara Juma yupo hapa kujibu maswali 10 aliyoulizwa na Mwandishi Wetu Imelda Mtema. Unataka kujua kaulizwa nini na akajibu nini? Fuatilia hapa chini…
Ijumaa: Hivi ulipopata kilema cha kukosa mguu mmoja wakati ulishazoea kutembea na miguu miwili ulijisikiaje?
Wastara: Nakumbuka nilipoteza matumaini kabisa na kuona ndoto zangu zimefutika.
Ijumaa: Changamoto gani ulikutana nazo tangu ulipopata ulemavu?
Wastara: Ni nyingi sana, kwanza kubadili aina ya mwendo wakati watu walizoea kukuona ukidunda. Kifupi wengi walinishangaa kwa jinsi nilivyoanza kutembea, pilika za kimaisha kama utafutaji pia vilinifanya nipate changamoto kubwa kwani sikuwa nikisaidiwa.
Ijumaa: Uliwezaje kukabiliana na badiliko kubwa kama hilo katika mwili wako?
Wastara: Ilikuwa kazi kubwa sana kuzoea hali hii maana nilikuwa naanguka kila siku kwa kujisahau na kuona bado nina miguu yote. Kutokana na hali hiyo nilichelewa sana kupona mpaka daktari aliyekuwa ananitibu akaamua kunipa dawa ambazo zilinifanya nilale saa 24.
Ijumaa: Ulemavu wako haukupi mawazo hasa unapofikiria ishu ya kuolewa tena?
Wastara: Hili suala la kuolewa ndiyo gumu kabisa na naweza kusema ulemavu huu unanikosesha hamu ya kuolewa kwani kila mwanaume anayekuja naona hana mapenzi ya kweli na mimi, naamua kughairi.
Ijumaa: Uliwaza nini kuamua kugombea ubunge na hiyo hali yako?
Wastara:  Nimefikiria vitu vingi sana na lengo ni kuwasaidia walemavu kwa kila hali.
Ijumaa: Wewe ulishawahi kunyanyapaliwa kutokana na hivyo ulivyo?
Wastara: Nilishawahi kwani nakumbuka siku moja nilitembelea nchi fulani nikapewa chumba nilale na mwenyeji wangu lakini alipoona ni mlemavu alihama.
Ijumaa: Ni maumivu gani uliyoyapitia kwa kipindi chote hiki?
Wastara: Kubwa zaidi ni maumivu ya mwili kwani kuvaa mguu wa plastiki ni mateso makubwa asikwambie mtu.
Ijumaa: Ni yapi umepanga kuyafanya kwenye siasa?
Wastara: Kwanza nitahakikisha serikali inaweka huduma nzuri hospitalini, benki na kwenye mabasi kwa walemavu.
Ijumaa: Je, umejipangaje katika kuikabili mizengwe kwenye siasa?
Wastara: Siasa siiogopi, nimejipanga kwa kila kitu na watu wasubiri waone.
Ijumaa: Huogopi mchezo mchafu unaofanywa na wanasiasa?
Wastara: Hakika nimejipanga na niko tayari kukabiliana na changamoto zote.


Powered by Blogger.