CUF wajifungia kutegua kitendawili cha Ukawa
Viongozi wa CUF
Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF)
kinafanya kikao chake cha Baraza Kuu la Uongozi leo mjini Zanzibar huku
wafuasi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
wakisubiri kwa hamu kitakachoamuliwa kuhusu mgombea urais wa umoja huo.
Vyama
vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi
vilisaini makubaliano ya kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
Oktoba 25, mwaka huu kwamba vitamsimamisha mgombea mmoja katika nafasi
ya rais, ubunge na udiwani.
Hata hivyo, wakati viongozi
wa vyama hivyo wakiwa katika vikao vya uteuzi wa nafasi ya rais
atayepeperusha bendera ya Ukawa, CUF walikaa kando wakisema wanasubiri
uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu la uongozi linaloketi leo ili kuendelea
na mchakato huo.
Hatua hiyo ilisababisha sintofahamu na
zilienea habari kwamba CUF wamejitoa. Lakini Naibu Katibu Mkuu wa CUF
(Bara), Magdalena Sakaya aliwaambia waandishi wa habari kwamba wao bado
wamo ndani ya Ukawa isipokuwa wanasubiri kupewa Baraka na Baraza Kuu la
Uongozi.
Sakaya alifafanua kwamba Baraza hilo litajadili na kutoa uamuzi ili wanaposhiriki vikao vya Ukawa wawe kitu kimoja.
Juzi,
katika mkutano wa Chadema uliofanyika jijini Mwanza, Naibu Katibu Mkuu
wa Chadema (Bara), John Mnyika na yule wa Zanzibar, Salim Mwalimu
walisema chama hicho kinasubiri hatima ya kikao cha wenzao wa CUF
kinachofanyika ili waweze kumtangaza mgombea urais wa Ukawa.
Akizungumza
na gazeti hili jana, Sakaya alisema kikao hicho cha siku moja
kitafanyika leo kama kilivyopangwa mjini Zanzibar na ajenda zitakuwa
masuala ya Ukawa na hasa nafasi ya mgombea wa nafasi ya urais.
Alisema ajenda nyingine ni kujadili na kuwapitisha wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani.
“Kikao kitajadili masuala ya ndani ya chama na tutawapa taarifa kuhusu yatakayoamuliwa baada ya kikao,” alisema.
Aidha,
habari za ndani zinasema kikao hicho kitajadili shughuli inayoendelea
ya uandikishaji wapigakura kupitia mfumo wa Biometric Voters
Registration (BVR). Hatua hiyo inatokana na matatizo mbalimbali
yaliyojitokeza wakati uandikishaji hali iliyosababisha baadhi ya watu
kushindwa kujiandikisha na hivyo kukosa haki yao ya kupiga kura.
Wafuasi
wa vyama hivyo na Watanzania kwa ujumla wanasubiri kusikia jina la
mgombea wa Ukawa hasa baada ya CCM kumtangaza Waziri wa Ujenzi, Dk John
Magufuli kuwa mgombea wake wa urais.