Wafanyabiashara walia na Tanesco
Dodoma. Kukosekana kwa umeme kwa wakazi wa
mjini hapa kwa muda wa wiki mbili sasa, kumezua maswali hali
inayosababisha baadhi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao.
Kutokana
na tatizo hilo, wakazi hao wametafsiri kuwapo kwa mgawo wa umeme wa saa
12 huku kukiwa hakuna taarifa zozote kutoka ofisi za Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Dodoma.
Mfanyabiashara
Emmanuel John anayeuza duka la vifaa vya ofisini katika Mtaa wa Uhindini
alisema kuwa, kwa muda wa wiki mbili sasa analazimika kufunga duka
kutokana na kukosekana kwa umeme mchana kutwa.
Kibaya
alilalamikia tatizo la kukatika kwa umeme bila kupewa taarifa zozote na
kusema: “Kama ni bili tumelipa, tunafanya kubahatisha tu kuja kazini
kama tutapata umeme au hapana.”
Fransis Nkya
mfanyabiashara wa bucha la nyama alisema, wakati mwingine nyama huwa
inaharibika kutokana na kukosekana kwa umeme mfululizo hali inayo
wasababishia hasara.
Mji wa Dodoma umekuwa ukisikika
milio ya majenereta ambayo yanatumika kama mbadala wa Tanesco hali
inayodaiwa kuwaumiza wafanyabiashara wengi wanaotegemea umeme huo.
Ofisa
Habari wa Tanesco, Innocent Lupenza alipoulizwa kuhusiana na suala hilo
alisema kuwa yupo kwenye kikao na kumtaka mwandishi amtumie ujumbe
mfupi wa maandishi.
Alipotumiwa ujumbe huo alisema kuwa
yupo nje ya mkoa na kumtaka mwandishi amweleze kinachoendelea,
alipoelezwa alijibu kuwa siyo kweli.
“Nchi nzima ilikuwa hapo, si ungesikia au ulikuwa unamaanisha vipi?” alihoji Lupenza kwenye ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.