Shinikizo la Lowassa Kuhamia CHADEMA Lazidi Kupamba Moto......Mkewe Ampigia Magoti Akimsihi Asihame!!
Shinikizo dhidi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
la kumtaka akihame Chama Cha Mapinduzi (CCM) linazidi kuongezeka na
katika timu yake ya ndani ni watu wawili tu wanaonekana kumtaka abakie
ndani ya chama hicho.
Habari za ndani ya vikao vya kujadili hatua za kuchukuliwa
na Lowassa baada ya jina lake kukatwa kwenye mchakato wa kugombea urais
kupitia CCM, zinasema kuwa wandani wake wanaamini kuwa hana atakachopata
kama ataendelea kubaki kwenye chama hicho tawala.
"Kaka sikiliza, inavyoelekea shinikizo dhidi ya Lowassa
ni kubwa sana. Watu wake wa ndani wanataka aondoke CCM. Wanaona kama
amedhalilishwa mno,"kilisema chanzo chetu ndani ya vikao hivyo.
Chanzo hicho kilichoomba kutokutajwa jina kwa sasa,
kilisema kuwa watu wake wa ndani wanaamini Lowassa akiendelea kubaki CCM
atakuwa amewavunja moyo wale wote waliompigania, hasa vijana waliojaa
matumaini ya kumuona akiongoza taifa hili.
Wandani wa Lowassa wanaamini kuwa kama akiamua kujiunga na
chama chenye nguvu cha upinzani anaweza kutimiza ndoto yake ya
kuwatumikia Watanzania kama rais wa awamu ya tano.
Chanzo chetu kinasema kuwa Lowassa mwenyewe amekwisha
kuamua kufanya uamuzi mgumu, ila kuna msuguano juu ya namna ya kuondoka
CCM.
Taarifa zaidi zinasema kuwa watu wawili katika timu ya
ndani ya Lowassa ndio wanaelekea kuwa na mawazo tofauti. Hawa ni Rostam
Aziz, mwanasiasa na mfanyabiashara mashuhuri nchini na mtu mwingine
anayetofautiana na mkakati huu mpya wa kung'oka CCM ni mkewe, Mama
Regina Lowassa.
Chanzo chetu kinasema kuwa wawili hao wanaamini mapigo
ambayo Lowassa amekumbana nayo ni mengi na yanatosha, kwa maana hiyo
ingefaa tu apumzike.
"Sijui ni kwa nini RA (Rostam Aziz) anakuwa skeptical
(shaka). Si unakumbuka ndiye aliyesema amechoshwa na siasa uchwara...
sasa sijui kwa nini anapunguza makali,"chanzo kilisema.
Hata hivyo, vyanzo vyetu vinaongeza kuwa pamoja na upinzani
huo Lowassa anadaiwa kuwa amekwisha kuamua na kinachosubiriwa sasa ni
muda tu wa kutamka anakokwenda.
Wakati hali ikiwa hivyo ndani ya kambi ya Lowassa, kuna
taarifa za kuaminika kuwa kumekuwa na mashauriano baina ya watu wake na
viongozi waandamizi wa kambi ya upinzani juu ya mwelekeo wake wa
kisiasa.
Mwandani mwingine katika kambi ya Lowassa alisema kimsingi
yeye (Lowassa) amekwisha kuamua, anachofanya ni kuona kwamba watu wake
wa karibu hawadhuriki na uamuzi wake huo.
Chanzo hicho kilisema kuwa wenye msimamo mkali katika kambi
ya Lowassa wanaamini utabiri wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuwa
upinzani utatoka ndani ya CCM utatimia mwaka huu.
"Mnakumbuka ya Mrema (Augustino) alipoondoka CCM siasa za Tanzania zilibadilika mpaka leo? Sasa safari hii ni zaidi," alisema.
Takriban wiki mbili sasa, Lowassa amekuwa na jambo kubwa moyoni analitaka kuwaambia Watanzania.
Mara ya kwanza alikuwa afanye mkutano na waandishi wa
habari Julai 13 mwaka huu mjini Dodoma majira ya asubuhi, lakini mkutano
huo ukahamishiwa Dar es Salaam ambako pia ukaahirishwa kwa muda
usiojulikana.
Tangu wakati huo kumekuwa na tetesi kuwa alikuwa atangaze kujiondoa CCM.
Lowassa ni miongoni mwa makada 38 waliojitosa kuwania
kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi ya urais wa CCM katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Hata hivyo, jina lake halikuwamo katika orodha ya makada
watano waliopitishwa kwenye vikao vya juu vya chama hicho ambavyo
mwishowe vilimteua John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais
atakayekabiliana na wagombea wa upinzani katika uchaguzi mkuu huo.