‘Wanawake wajasiriamali litumieni soko la EAC’
Mmoja wa wajasiriamali akionyesha bidhaa zake katika moja ya maonyesho ya biashara. PICHA|MTANDAO
Tanga. Diwani wa Kata ya Mabawa katika
Halmashauri ya Jiji la Tanga, Muzzamillu Shamdoe amewataka wajasiriamali
wanawake kulitumia soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
kutangaza bidhaa zao.
Akizungumza baada ya kufungua
Kituo cha ushonaji nguo cha Raha Gani kwa watoto wanaoishi katika
mazingira magumu jana, Shemdoe alisema wajasiriamali hawalitumii soko
hilo ndiyo maana kazi zao hazijulikani.
Alisema wajasiriamli kutoka nchi wanachama wamekuwa wakilitumia kikamilifu soko hilo na bidhaa zao kutangazika.
Shamdoe aliwakumbusha wajasiriamali nchini, kulifikia soko hilo ili kufikia malengo waliyojiwekea.
“Wajasiriamali
wa hapa kwetu hawana uelewa wa soko la pamoja, angalia wenzetu bidhaa
zao zilivyoenea nchini kila kona ni bidhaa za nje,” alisema Shemdoe na
kuongeza:
“Nawashauri pelekeni kazi zenu kwa wenzenu huenda ni bora zaidi, msing’ang’anie hapa tu, hamtaweza kufikia malengo yenu.”
Wakati huohuo; Mkuu
wa Kituo cha Raha Gani, Hafifa Kijazi alisema kituo hicho kina watoto
yatima 18 wanaoishi katika mazingira magumu kutokana na kukabiliwa na
upungufu wa vitendea kazi.
Alisema kituo hicho kina
cherehani saba jambo ambalo amedai ni gumu kuwafundisha watoto wote kwa
wakati mmoja, hivyo kuchukua muda mrefu kumfikia kila mmoja.
Kijazi aliyataka mashirika na taasisi za watu binafsi kukisaidia kituo hicho ili kuwapa elimu watoto hao.
Alisema
endapo watapatiwa msaada wa vitendea kazi watoto hao wakipata elimu
wataweza kujitegemea pamoja na kujiepusha na vishawishi vya mitaani.
Alisema
watoto hao ambao wote ni wa kike wakiachwa wanaweza kujitumbukiza
katika vitendo viovu, hivyo ni wajibu kwa jamii kukiangalia ili kufikia
malengo.