Easta Bulaya ni Moto wa Kuoteka Mbali........Apata mapokezi ya kishindo Bunda, Amchamba na Kumlipua Wassira
ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Mara kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi.Esta Bulaya ambaye juzi alitangaza
kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amepata
mapokezi makubwa Mjini Bunda jana akitokea jijini Mwanza akiwa na
viongozi wa CHADEMA mkoani humo na Kanda ya Ziwa.
Akiwahutubia wananchi katika Viwanja vya Stendi ya Zamani,
Bi.Bulaya aliwapongeza wananchi kwa mapokezi makubwa waliyompa na
kumlipua mbunge wa jimbo hilo aliyemaliza muda wake, Bw. Stephen Wassira
akisema muda wake wa kukaa serikalini unatosha.
Alisema katika Serikali ya Awamu ya Tano, viongozi kama Bw.
Wassira hawafai kwani amekuwa Waziri muda mrefu lakini jimbo hilo bado
halina maendeleo yaliyotarajiwa na wananchi.
"Wazazi wangu mimi ni mwanachama wa CCM na mimi
nimekulia ndani ya chama hicho hivyo mkiona nimekimbia, mjue mambo
yamenifika shingoni, katika mkoa huu kuna rasilimali nyingi ambazo
hazijatumika vizuri ili ziwaondolee wananchi umaskini," alisema.
Akizungumzia uwazi na uwajibikaji, alisema viongozi wengi
wa CCM hawataki kuwatetea wananchi na kushindwa kuwasimamia watendaji wa
Serikali akitolea mfano mradi mkubwa wa maji mjini humo ambao umechukua
miaka tisa bila Bw.Wassira kuukamilisha.
"Leo hii Wassira atakuja na sera gani kwa wananchi
wakati ameshindwa kutekeleza wajibu wake kama mbunge na kiongozi wa
Serikali, tuwakatae viongozi wa ngazi zote wanaotokana na CCM," alisema.
Aliongeza kuwa, umefika wakati wa majimbo yote mkoani humo
kuchukuliwa na wagombea wa CHADEMA ambao watatimiza ahadi zao kwa
wananchi na kutatua kero walizonazo.
Bi.Bulaya aliweka wazi dhamira yake ya kuwania ubunge wa
Bunda Mjini kwa tiketi ya CHADEMA ambapo leo atashiriki kura ya maoni ya
kumpata mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA.
Naye mbunge wa Kahama, Bw. James Lembeli, alidai kuchoshwa
na ufisadi uliopo ndani ya CCM na kuwataka wananchi wakubali kuiunga
mkono CHADEMA kwa kuwaweka madarakani na kushika dola katika Uchaguzi
Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Mbunge wa Musoma Mjini, Bw. Vicent Nyerere, alilitaka Jeshi
la Polisi kutoa ushirikiano katika Uchaguzi Mkuu na kuacha kuitetea CCM
huku akidai jeshi hilo ni sehemu ya Watanzania ambao wote wamepigika.