FORM 3-KISWAHILI-MADA 1-MJENGO WA TUNGO

MJENGO WA TUNGO
Tungo
Maana ya Tungo
Tungo ni kipashio cha kisarufi kilichoundwa kwa kuunganisha pamoja vipashio vidogovidogo vilivyo chini yake. Au tungo ni neno au kikundi cha maneno ambacho hudokeza taarifa fulani ambayo huweza kuwa kamili au isiyo kamili.
Kwa maana hii, tungo hujengwa na vipashio vidogovidogo kama vile mofimu kuunda neno, neno kuunda kirai, kirai kunda kishazi na kishazi kuunda sentensi. Kama tulivyokwisha kuona hapo juu tungo huanzia neno; rejea aina za tungo.
Aina za tungo
Bainisha aina mbalimbali za tungo
Tungo neno: Tungo neno ni tungo ambayo huundwa na vipashio vidogo zaidi ya neno ambayo ni mofimu au fonimu. Mfano; anacheza, kakimbia.
Tungo Kirai: ni kipashio cha kimuundo chenye neno moja au zaidi lakini ambacho hakina muundo wa kiima kiarifu. Mfano; mtoto mzuri, kiyama chake, bondeni
Tungo kishazi:Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe.
Kirai na Uainishaji wake
Maana ya Kirai na Uainishaji wake
Dhana ya kirai itaeleweka vizuri kwa kuzingatia sifa zake zifuatazo:
  • Kirai huwa ni kipashio cha kimuundo kisichokamilika; yaani ni kipashio kisichokuwa na muundo wa kiima – kiarifu kama zilivyo sentensi ambazo zinahusisha mtendaji wa tendo na tendo linalotendwa.
  • Kirai huainishwa kimuundo kulingana na neno kuu la kirai husika.
  • Kirai ni tungo, yaani ni aina moja wapo ya tungo, aina nyingine za tungo ni neno,kishazi na sentensi.
  • Kirai hudokeza maana, lakini maana hiyo si kamili.
  • Maneno katika kirai lazima yapangwe kimantiki kwa mpangilio unaokubalika katika sarufi ya lugha husika. Japo virai huainishwa kimuundo, huweza kutumika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kisarufi. Kirai huweza kutokea upande wowote, wa kiima au kiarifu katika sentensi. Kirai ni kikubwa kuliko neno
Kama tulivyobainisha hapo juu aina ya virai hukitwa katika aina za maneno ambazo ndizo chimbuko la mahusiano maalumu ndani ya vipashio hivyo.
  1. Kirai nomino (KN);Ni kirai ambapo neno lake kuu ni nomino. Ni kirai ambacho muundo wake umekitwa kwenye nomino au mahusiano ya nomino na neno au mafungu ya maneno.
  2. Kirai kitenzi (KT); Kirai-kitenzi ni kirai ambacho kimekitwa katika kitenzi au katika mahusiano ya Kitenzi na neno au mafungu mengine ya maneno. Hii ina maana kuwa neno kuu katika aina hii ya virai huwa ni kitenzi.
  3. Kirai kivumishi (KV); Kirai-kivumishi ni kirai ambacho muundo wake umekitwa katika kivumishi. Kwa kawaida muundo huu huwa ni wa kivumishi na neno au fungu la maneno linaloandamana nacho.
  4. Kirai Kielezi (KE); Tofauti na aina nyingine ya virai miundo ya virai vielezi haielekei kukitwa kwenye mahusiano ya lazima baina ya neno kuu (yaani kielezi) na neno au fungu la maneno linaloandamana nalo. Badala yake miuundo inayohusika hapa ni ya maneno ambayo hufanya kazi pamoja katika Lugha kama misemo, neno au maneno yanayofuata neno lililotangulia yakifafanua zaidi neno hilo.
  5. Virai viunganishi (KV); Ni kirai ambacho muundo wake umekitwa katika mahusiano baina ya kwa na katika, au kwenye na fungu la maneno linaloandamana nacho. Kwa maneno mengine kirai hicho ni kile ambacho neno kuu ni kiunganishi.
Tungo kishazi
Maana ya Kishazi na Uainishaji wake
Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe.
Sifa za kishazi
  • Kishazi hupatikana katika/ ndani ya sentensi.
  • Lazima kishazi kiwe na kitenzi, sehemu yoyote ya sentensi isiyo na kitenzi, haiwezi kuwa kishazi. Kishazi huru hutawaliwa na kishazi kikuu na kishazi tegemezi hutawaliwa na kishazi tegemezi.
  • Baadhi ya vishazi huweza kujitegemea kama sentensi hata vikiondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu. Kishazi kinachoweza kujisimamia kama sentensi huitwa kishazi huru kikiwa ndani ya sentensi kuu na huitwa “sentensi sahili” kikiwa sentensi inayojitegemea.
  • Baadhi ya vishazi haviwezi kujitegemea kama sentensi ikiwa vitaondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu.
  • Vishazi vingi, hata vishazi huru huwa na kiima dhahiri.
  • Kishazi kwa kawaida, hasa kishazi huru huwa na kitenzi kimoja kikuu.
  • Kitenzi hicho huweza kuandamana na kitenzi kisaidizi. Pia, kitenzi katika kishazi huweza kuwa kitenzi kishirikishi.
  • Kishazi hutekeleza majukumu mbalimbali ya kisarufi.
  • Tofauti ya kishazi na sentensi ni kwamba kishazi hupatikana ndani ya sentensi lakini sentensi hujisimamia kimuundo na kimaana.Kishazi huwa na kiarifu kimoja na kiima kimoja, Lakini sentensi huweza kuwa na kiima kimoja.
Aina za vishazi
  1. Vishazi huru: Kishazi huru ni kishazi kinachotaewaliwa ka kitenzi kikuu, ambacho kwa kawaida hutoa ujumbe kamili usiohitaji maelezo zaidi ya kukamilisha maana. Ni kishazi ambacho hata kikiondolewa katika muktadha wa sentensi ambamo vimejikita huweza kujitegemea kama sentensi.
  2. Vishazi tegemezi: Kishazi huru ni kishazi kinachotawaliwa ka kitenzi kisaidizi, ambacho muundo wake hukifanya kutegemea kitenzi cha kishazi huru ili kuweza kutoa ujumbe uliokusudiwa. Kishazi tegemezi peke yake hakitoi ujumbe unaojitosheleza
Sifa za Kishazi tegemezi
  • Kishazi tegegemezi hutoa maana kamili kinapoandamana na kishazi huru.
  • Kishazi tegemezi kinaweza kufutwa katika sentensi bila kuharibu maana ya sentensi nzima.
  • Kishazi tegemezi hutambulishwa na viambishi vya utegemezi
  • Vinavyoambatanishwa kwenye kitenzi.
  • Kishazi tegemezi vile vile kinaweza kutambuliwa kwa kuwepo vishazi kama vile ingawa, kwamba, ili, kwa sababu, mzizi wa amba, mofu ya masharti n.k
Aina ya vishazi tegemezi
Vishazi tegemezi vivumishi
  • Vishazi tegemezi vinavyotokea pamoja na nomino inayovumishwa.
  • Vishazi tegemezi visivyoambatana na nomino inayovumishwa
Vishazi tegemezi vielezi
  • Vishazi tegemezi vya mahali
  • Vishazi tegemezi vya wakati
  • Vishazi tegemezi vya namna au jinsi
  • Vishazi tegemezi vya masharti
  • Vishazi tegemezi vya hali, hitilafu au kasoro iliyoko katika tendo.
  • Vishazi tegemezi vya sababu/chanzo
Dhima na hadhi ya vishazi
Kishazi chaweza kuwa huru kikajitegemea chenyewe kwa kuwa na maana kamili inayojitosheleza. Lakini kuna vishazi ambavyo havijitoshelezi vyenyewe, bali hutegemea vishazi vingine. Kishazi huru kina hadhi ya sentensi (sahili). Kishazi tegemezi hakina hadhi hii, vishazi tegemezi ambavyo hutegemea vishazi vingine hushuka daraja na kuchukua dhima ya kikundi. Baadhi ya vishazi tegemezi huchukua dhima (hufanya kazi) ya kivumishi katika tungo ambayo kwa kawaida ni dhima ya kikundi au neno. Vishazi hivi huvumisha nomino katika tungo hiyo
Powered by Blogger.