FORM 3-KISWAHILI-UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI

UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Fani katika Tamthiliya ya Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe
JINA LA KITABU: NGOSWE PENZI KITOVU CHA UZEMBE
MWANDISHI: EDWIN SEMZABA
WACHAPISHAJI: NYAMBARI NYANGWINE PUBLISHERS
MWAKA:2006
UTANGULIZI WA KITABU
Ngoswe penzi kitovu cha uzembe ni tamthiliya maarufu sana ambayo imewahi kuigizwa katika redio Tanzania na katika majukwaa mbalimbali hapa nchini. Ni tamthiliya ambayo imeundwa vyema katika vipengele vya fani na maudhui. Ameteua lugha nzuri na yenye mvuto kwa wasomaji yenye mbinu za kifasihi zilizosheheni, muundo wenye mtiririko mzuri, unaoakisi kuanza kuchipuka kwa matukio mpaka kilele cha matukio. Wahusika wamebeba vyema uhusika wao mfano Ngoswe.
Ameibua dhamira kuhusu mambo yanayoigusa jamii ya leo kama vile uzembe, madhara ya ulevi, uzembe kazini, suala la matabaka kati ya mjini na vijijini. Mtazamo, falsafa na msimamo wake ni kulenga kuibadilisha jamii na kuleta maendeleo.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu “Ngoswe penzi kitovu cha uzembe” ni jina ambalo limesawiri vyema yaliyomo ndani ya kitabu hicho, kwani Ngoswe ndio jina la mhusika mkuu anayebeba dhamira kuu ya tamthiliya. Pia penzi limeonekana kuwa ni kitovu cha uzembe kwani ndio yaliyopelekea kuteketezwa kwa karatasi za takwimu za sensa. Hivyo jina la kitabu si tu kwamba limesawiri yaliyomo katika kitabu bali pia katika jamii.
MTINDO
Mtindo alioutumia mwandishi ni dayalojia au majibizano. Mwandishi amepanga visa na masimulizi kwa kutumia majibizano ya wahusika.
  • Matumizi ya nafsi ya kwanza.Mwandishi ndiye ameyafafanua na kuelezea baadhi ya matukio. Katika karibu kurasa zote mwandishi ameonekana kuwa ndiye msimuliaji wa matukio.
  • Matumizi ya nafsi ya pili.Hapa watu wawili na zaidi wanajibizana. Tamthilya hii wahusika wanaojibizana kuibua dhamira na migogoro. Kuna majibizano baina ya mzee Mitomingi, Ngoswe na Mazoea nk.unaweza kupata mfano uk. wowote kwani ndio mtindo uliotawala.
MUUNDO
Muundo uliotumika ni muundo wa mojakwamoja au sahili. Kwani ameonesha tangu mwanzo wa mambo mpaka mwisho, anajenga visa vidogo mpaka visa vikuu au kileleni.Amepanga visa na matukio yake katika maonesho matano. Kila kichwa kina maelezo yaliyojadiliwa katika onesho hilo.
  • KIJITO:Hapa yanaeleza jinsi mambo yanavyoanza. Jinsi Ngoswe anavyoingia kijijini anavyopokelewa na kuanza kufahamiana na wenyeji wake.
  • VIJITO:Hapa Ngoswe anaanza kufanya kazi iliyompeleka kijijini na tunaanza kuoneshwa changamoto anazokumbana nazo.
  • MTO:Ni mwendelezo wa matukio ya mwanzo hapa visa vinazidi kukua.
  • JITO:Hapa Ngoswe anakumbana na changamoto nyingi zaidi katika kazi yake. Na hapa anazidi kuanguka kwani anajiingiza katika mapenzi na msichana Mazoea, anaendekeza ulevi na kuharibu kazi kabisa.
  • BAHARINI:Hapa inaoneshwa mwisho wa mambo jinsi yalivyokuwa. Yanaonekana mahojiano baina ya Serikali na Ngoswe na Mitomingi juu ya uzembe uliofanyika wa kupoteza takwimu na hapa ndipo suluhisho linapotolewa juu ya matatizo hayo.
WAHUSIKA
NGOSWE
  • Kijana wa kiume umri kati yamiaka 20-25
  • Ameelimika na amestaarabika
  • Anatumwa na serikali kufanya sensa kijijini
  • Anajihusisha na mapenzi na msichana mazoea
  • Ni mlevi
  • Hana umakini katika kazi
  • Aliharibu kazi ya serikali
  • Hafai kuigwa na jamii
MAZOEA
  • Ni msichana mwenye umri kati ya miaka 18-20
  • Ni binti wa Mzee Ngengemkeni Mitomingi
  • Hana elimu na hajastaarabika
  • Ana nidhamu ya woga
  • Ana tama
  • Hana msimamo alikubali kuchukuliwa na Ngoswe hali akijua alishatolewa mahari
  • Hafai kuigwa na jamii.
NGENGEMKENI MITOMINGI
  • Ni balozi katika kijiji chake
  • Ni baba mzazi wa Mazoea
  • Ameoa ndoa ya mitara, ana wake wawili
  • Hajaelimika
  • Anashikilia mila na desturi za kale
  • Mlevi
  • Mkali sana
  • Anateketeza karatasi za takwimu
MZEE JIMBI
  • Mwanakijiji
  • Hajaelimika kwani hajui hata umri wake
  • Ni mlevi
  • Ana wake wawili
  • Anashikilia ukale
MAMA MAZOEA
  • Mke mkubwa wa Mitomingi
  • Mama yake Mazoea
  • Mlezi wa familia
  • Hapewi nafasi ya kutoa maamuzi katika familia
MAMA INDA
  • Mke wa pili Mzee Mitomingi
  • Mama yake Huzuni
  • Hapewi nafasi ya kutoa maamuzi
  • Ni mlezi wa familia.
MANDHARI
Mandhari ya tamthiliya hii imechorwa katika mazingira ya kijijini. Mambo yanayoelezwa ni ya kijijini mfano kilimo, hali ya watu kimaisha, huduma duni sana za kijamii kama vile shule, umbali wa makazi toka nyumba moja hadi nyingine. Haya yanatudhihirishia vyema mandhari hiyo ambayo kwayo imeibua dhamira mbalimbali kama vile umaskini, ukosefu wa elimu, huduma duni za afya vijijini, masuala ya imani potofu nk.
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na rahisi kueleweka kwa wasomaji. Pia kuna matumizi ya lugha nyingine mfanouk. 1 “bell bottom”
Matumizi ya semi
  • Methali:Uk.22 “Penye nia pana njia”.Uk.27 “Waona vyaelea vyaundwa.”
  • Misemo:Uk.14 “Akuwaniae ujovu haji kweupe”
  • Nahau:Uk.11 “hebu keti tutupe mawe pangoni” –tule chakulaUk.7 “mbongo zimelala”-ana maarifaUk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda”- anapenda pombe sana.
Matumizi ya tamathali za semi
  • Tafsida:Uk.21 “Wala hajarudi, kama ingekuwa ni kujisaidia si angekuwa amekwishamaliza?”
  • Tashbiha:Uk.1 “vumbi jekundu kama ugoro wa subiana”Uk.8 “sarawili yake miguuni kama kengele ya bomani”Uk.17 “wanaondoka huku wakitazamwa kama vile mizuka”
  • Sitiari:Uk.7 Mama Mazoea : “kiziwi mkubwa wee!”Uk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda!”Uk.26. “karatasi? za takwimu? Ndio wanyama gani hao?”
  • Mubaalagha:Uk.11 Mama Mazoea : “kupeleka chakula ndio umefanya makao!”Mama mazoea : “Kujibu swali ndio ukachukua mwaka mzima!”
Mbinu nyingine za kisanaa
  • Mdokezo:Uk.22 Mazoea : “sijui….. siwezi….. namuogopa baba”Uk.16 Ngoswe : “huyo mtoto wenu wa kwanza anaishi hapa au…..”
  • Takriri:Uk.9 “Mama Masikio! We Mama Masikio!”Uk.13. “Hodi! Hodi!”Uk.2 “karibu karibu”
  • Tashtiti:Uk.5 Ngoswe: “hivyo waitwa nani?”Mazoea: “mie?”Uk.22 Ngoswe: “mchumba? Kwani mchumba ni kitu gani?”Uk.26 Mitomingi: “karatasi? Za takwimu? Ndio wanyama gani hao?Hapa wahusika waliuliza maswali ambayo majibu yake waliyaelewa ila kutokana na kutaka kudhihirisha hasira, msisitizo nk. Ndio maana wametumia tashtiti.
  • Onomatopea/tanakali sauti:Uk.7 Kifaruhande anacheka “Ha! ha! ha!
Ujenzi wa taswira
Mwandishi ametumia taswira ya mto kuelezea visa vyake. Sehemu ya kwanza ni sehemu ya kijito, kijito ni kimto kidigo mwandishi hapa anaanza kueleza mambo yakiwa machanga kabisa ndio yanaanza.
Sehemu ya pili ni vijito. Huu ni muunganiko wa vijito vidogovidogo hapa mwandishi anaanza kueleza visa vidogovidogo. Sehemu inayofuata ni sehemu ya Mto. Hii inaashiria mambo yameanza kuwa mazito, visa vinakua zaidi na Ngoswe anazidi kuingia katika changamoto kubwa zaidi.
Pia Jito ni taswira ambayo mwandishi ameitumia kuashiria hatari zaidi mambo makubwa zaidi na hapa ndipo tunaona Ngoswe anaanguka kabisa katika kazi yake kwani Jito ni lenye maji mengi na yanayoenda kwa kasi hivyo huhitaji umakini mkubwa zaidi.
Mwisho sehemu ya Bahari ambapo hapa ndipo hatima ya mambo inaelezwa Ngoswe anazama na kupotea kabisa! Hafanikiwi kutoa takwimu kwani karatasi zilichomwa moto.
Fani katika Tamthiliya ya Kilio Chetu
Hakiki fani katika tamthiliya ya Kilio Chetu
MWANDISHI: MEDICAL AID FOUNDATION
WACHAPISHAJI: TANZANIA PUBLISHING HOUSE (TPH)
MWAKA: 1996
JINA LA KITABU
KILIO CHETU ni jina ambalo linaasadifu yaliyomo katika kitabu. Masuala yanayotajwa mule kama vile upotofu wa maadili kwa vijana wadogo kama Suzi na Joti, suala la mimba za utotoni, madhara ya gonjwa hatari la UKIMWI kwa jamii kweli ni kilio chetu ni kilio cha Taifa zima. Kwani katika mambo yanayoiyumbisha jamii kimaendeleo ni upotovu wa maaadili.
Jina hili ni sadifu katika jamii. Mwandishi amelitumia wakati muafaka kabisa kwani mambo anayoyaeleza ndio changamoto katika jamii ya leo. Hivyo kupitia hili jamii si budi kubadilika.
UTANGULIZI WA KITABU
Kilio chetu ni tamthiliya ambayo imejieleza vyema katika fani na maudhui. Tamthiliya hii inamuhusu mhusika Suzi na Joti ambao ni watoto wadogo sana. Wanajiingiza katika mapenzi katika umri mdogo kutokana na ukosefu wa elimu ya kijinsia. Inatueleza kuhusu athari za ugonjwa huu usiobagua. Pia tunafahamishwa kuhusu mtazamo wa wazazi na walezi kuhusu utoaji wa elimu ya jinsia kwa vijana wao. Wapo wanaolipokea kwa mtazamo chanya na wengine hasi.
Kwa ujumla ni tamthiliya nzuri kwani ina mtazamo wa kimabadiliko unaolenga kuwakomboa vijana wetu kutoka katika janga la ugonjwa hatari wa UKIMWI.
MUUNDO
  • Sehemu ya kwanza:Inaonesha jinsi gonjwa la UKIMWI linavyoikumba jamii. Mwandishi anaeleza kuhusu Dubwana linaloikumba jamii.
  • Sehemu ya pili:Mwandishi anaeleza kuhusu athari za UKIMWI, jambo ambalo lilipelekea kifo cha Fausta. Pia Suzi agundulika kujihusisha na mapenzi baada ya kukutwa na vidonge vya kuzuia mimba.
  • Sehemu ya tatu:Inaeleza juu ya watoto ambao wameshajiingiza katika suala la mapenzi licha ya kuwa na umri mdogo mfano ni Joti na Suzi. Pia madhara ya utandawazi yanaelezwa hapa mfano kuoneshwa kwa picha za ngono.
  • Sehemu ya nne:Tunaelezwa juu ya tabia hatarishi za Joti za kuwa na mahusiano na wasichana wengi mfano Chausiku, Yoranda, Gelda na Suzi. Hapa Joti anafanikiwa kumrubuni tena Suzi. Pia tunaoneshwa jinsi Ana anavopingana na vishawishi kutokana na kupata elimu ya jinsia.
  • Sehemu ya tano:Suzi anagundulika kuwa na mimba ya Joti, anajutia kosa hilo anajilaumu sana.
  • Sehemu ya sita:Inatuonesha jinsi Joti alivyokuwa magonjwa tayari kutokana na UKIMWI. Hapa ushauri mzuri unatolewa kuhusu namna ya kumtunza mgonjwa wa UKIMWI na kumfanya aishi kwa matumaini. Hapa mwandishi anapinga mila potofu kuhusu UKIMWI kuwa si kurogwa bali ni ugonjwa unaoambukizwa.
MTINDO
Tamthiliya hii imesheheni katika mitindo kadha wa kadha inayopamba kazi hii. Mtindo uliotumika ni dayalojia au majibizano.
Mwandishi ametumia mtindo wa mianzo na miisho ya kifomula ya usimulizi ambao ni mtindo wa usimulizi wa fasihi ya kiafrika. Mfanouk.1 mwandishi anasema “paukwa….. pakawaa…. Niendelee…. nisiendelee? ….. au mmechoka? Uk.113,piauk.36 mwandishi anasema “na hadithi yangu imeishia hapo”.Pia mwandishi ametumia mtindo wa utambaji kwani ndiye anayesimulia na kuelezea matukio.
Matumizi ya nafsi
Nafsi ya pili ndiyo iliyotawala, mwandishi ametumia majibizano ya watu wawili mfano Suzi na Joti, pia watu watatu n.k.Pia mwandishi ametumia tanzu nyingine za fasihi mfano wimbo uk.27
Wahusika
SUZI
  • Ni binti mdogo wa darasa la sita
  • Anajihusisha na mapenzi na Joti
  • Hana msimamo
  • Anapata mimba katika umri mdogo
  • Ana hatari ya kuwa na UKIMWI
  • Hakupewa elimu ya jinsia
  • Ana tamaa kwani alitamani vitu alivyohongwa na Joti.
  • Hafai kuigwa na jamii tutokana na tabia zake au sifa zake
JOTI
  • Ni kijana mdogo wa kiume
  • Ana mahusianao ya mapenzi na wasichana wengi Suzi, Gelda, Yoranda na Chausiku
  • Hana elimu ya jinsia
  • Ana makundi mabaya ya marafiki
  • Anaathirika na kufa kwa gonjwa la UKIMWI
  • Amechangia kuharibu maisha ya Suzi kwa kumrubuni
  • Ni mlaghai
  • Hafai kuigwa na jamii
MAMA SUZI
  • Ni mzazi wa Suzi
  • Anashikilia ukale hataki mabadiliko
  • Hampi mwanae elimu ya jinsia
  • Alichangia kuharibu maisha ya Suzi
  • Ni mkali sana katika malezi hatumii busara bali hasira
  • Hafai kuigwa na jamii
BABA JOTI
  • Ni mzazi wa Joti
  • Hayupo tayari kutoa elimua ya jinsia
  • Anashikilia ukale
  • Ni mkali anatumia viboko kuelimisha jambo ambalo si sahihi
  • Amechangia kuharibu maisha ya Joti
  • Ni muhuni, si muaminifu katika ndoa yake
  • Hafai kuigwa na jamii
ANNA
  • Ni binti mdogo wa shule
  • Ana elimu ya jinsia
  • Ana msimamo mzuri anashinda vishawishi
  • Anatoa elimu kwa vijana wenzake kuhusu athari za kujiingiza katika mapenzi katika umri mdogo
  • Ana tabia njema
  • Hana tama
  • Anafaa kuigwa na jamii.
BABA ANNA
  • Ni mzazi wa Anna
  • Anatoa elimu ya jinsia kwa wazazi na watoto
  • Ni mlezi bora
  • Alichangia maisha ya Anna kuwa ya mafanikio
  • Anafaa kuigwa na jamii
MJOMBA
  • Ni kaka yake Mama Suzi
  • Anaendana na wakati wa sasa
  • Anatoa elimu ya jinsia kwa vijana na wazazi
  • Ni mlezi bora ni mshauri bora
  • Anatoa elimu ya UKIMWI kwa Baba Joti anapinga mila potofu
  • Anafaa kuigwa na jamii
MAMA JOTI
  • Mzazi wa Joti
  • Ndoa yake ipo matatani kuingiliwa na mke mwingine
  • Anaelewa kuwa jamii imebadilika na wazazi wanapaswa kuwaelimisha watoto
JIRANI
  • Ni jirani wa Baba Joti
  • Ana imani potofu za kishirikina, anaamini Joti alilogwa
  • Haamini kuwa UKIMWI upo
CHAUSIKU
  • Ni msichana wa mtaani
  • Mfanyabiashara wa vitumbua
  • Ni jirani wa Suzi
  • Ana tabia mbaya ni muhuni
  • Alichangia kuharibu maisha ya Joti
  • Ana mahusiano ya kimpenzi na vijana wadogo mfano Joti na watu wazima pia, mfano Mpemba.
CHOGO, MWARAMI NA JUMBE
  • Ni marafiki wa Joti
  • Ni wanafunzi wadogo
  • Si marafiki wazuri
  • Wana tabia mbaya wanashauriana kuhusu mambo mabaya
  • Hawafai kuigwa na jamii
MANDHARI
Mandhari ni sehemu / mahali / mazingira ambayo ni matukio ya hadithi au masimulizi juteneka /hufanyika /hutokea.
Mandhari huweza kuwa halisi ikijumuisha mazingira yanayoweza kudhihirika katika ukawaida na pia mandhari yaweza kuweza kuwa halisi ikijumuisha mazingira yanayoweza kudhihirika katika ukawaida na pia mandhari yaweza kuwa ya kubuni ikiwa haina uhalisia, katika tamthiria hii tunaweza kusema mwandishi ametumia mazingira ya uhalisia kutokanana mandhari zifatazo;
  • Mandhari ya shule,kwa upande wa joti na suzi kwanzia sehemu ya kwanza,
  • Mandari ya nyumbani na mtaani uk 12
Mandhari aliyoitumia mwandishi ni ya mjini, hii ni kutokana na maelezo ya mhusika jirani anaposemauk.32 “……mie toka siku ile nimwone hospitali sijakaa mjini. Nilikwenda zangu shamba kupambana na Nyani wala nafaka.”Pia lugha ya mtaani iliyotumiwa na vijana Joti, Mwarami na wenzake, masuala ya picha ya “X” yaani viashiria vya mambo ya mjini kwani yamekithiri sana mijini. Maeneo yanayotajwa kama vile uwanja wa Sabasaba ni uwanja uliopo mjini, masuala ya lifti kwa wasichana hasa wanafunzi yapo mijini. Mfano.uk.27 pia kuna mandhari ya nyumbani na mtaani.
Mandhari aliyotumia mwandishi inasawiri maudhui yake katika jamii. Kwani anaibua mambo yaliyo katika jamii.
MATUMZI YA LUGHA
Lugha iliyotumika ni lugha iliyo na ubunifu wa kipekee wenye mvuto wa kisanaa. Lugha ni rahisi na inayoeleweka vyema kwa hadhira lengwa. Pia kuna matumizi ya lugha nyingine mfano kiingereza na lugha za kikabila. Kiingereza mfanouk.21 “tuition” uk.16 “come”.Lugha za kikabila mfano wimbo uk.35“Joti afitwe sanda salauya; Ena ena salauya …………………….”
Matumizi ya lugha ya mtaani
Mfanouk.16 “mshefa” “mshikaji”-rafiki.Uk.17 “kamba” –kudanganya jambo;Uk.22 “vidosho” –wasichana;Uk.16 “kanitolea nje”– kukataa jambo fulani.
Matumizi ya tamathali za semi
  • Tashibiha:Uk.1 “wakapukutika kama majani”Uk.5 “mgumu kama mpingo”Uk.6 “miti inaungua kama mabua”Uk.13 “Dubwana limetanda kama utando wa Buibui”
  • Tashihisi:Uk.2 “vifo vikawazoa”kifo huua tu lakini kimepewa uwezo wa kuzoa
  • Sitiari:Uk.8 “We Mbwa mweusi”Uk.9 “Nyoka wee”Uk.21 “huyo kinyago wako anakimbia nini?”
  • Tafsida:Uk.4 “kafa kwa kukanyaga nyaya”– kafa kwa UKIMWI
  • Mubaalagha:Uk.4 “Mtu si mtu, kizuka si kizuka”
Matumizi ya mbinu nyingine za kisanaa
  • Tanakali sauti/ Onomatopea:Uk. Joti akasema“….acha moyo unipwite “Pwi! Pwi! Pwi!”Uk.25 “….hebu nitolee uchafu wako mie ptuu!”
  • Tashtiti:Uk.15 “….huyu ni Suzi kweli au nani?”Uk.36 “kwanini Joti……… kwanini Joti afe?”
  • Takriri:Uk.1 “watu wakapukutika, wakapukutika…..” “tunakwisha, tunakwisha”Uk.2 “vifo vikawzoa, vikawazoa .…. vikawazoa”Uk.16 “piga domo, piga domo”
Matumizi ya semi
  • Methali:Uk.6 “wembamba wa Reli Treni inapita”Uk.11 “mzazi usipomfunza walimwengu watamfundisha”Uk.19 “shukrani ya Punda ni mateke”Uk.24 ‘Ndege mjanja ananaswa na tundu bovu
  • Nahau:Uk.6 “nimekuvulia kofia”-nakuheshimuUk.21 “anajigongagonga” –anajipendekeza
  • Misemo:Uk.4 “kuwa nyumanyuma kama koti”Uk.6 “kifua simkingii maana siwi naye”Uk.7 “makapera kibao Mume wangu wa nini?”Uk.22 “mapenzi ni tiba”Uk.26 “…..unakimbilia suti na nepi hujavaa”
Matumizi ya taswira
UK.1 “dubwana” –ugonjwa wa UKIMWI;Uk.7 “Nguru” –aina ya Samaki wabayaamefananishwa na mtu mbaya;Uk.21 “kinyago”- Suzi.
Fani katika Tamthiliya ya Orodha
Hakiki fani katika tamthiliya ya Orodha
JINA LA KITABU
Jina la kitabu ORODHA ni sadifu kwa yaliyomo. Katika kitabu inatajwa orodha ya mambo ambayo yanaweza kusaidia kuepusha UKIMWI. Orodha hii inatolewa na mhusika Furaha ambaye aliomba isomwe katika mazishi yake. Mambo hayo au orodha hiyo ni pamoja na uwazi, ukweli, uadilifu, matumizi ya kondom, uelewa, upendo, elimu, uwajibikaji na msamaha. Mwandishi anaona kuwa endapo mambo haya yatazingatiwa hakika tutapunguza maambukizi zaidi ya virusi vya UKIMWI.
UTANGULIZI
Tamthiliya ya Orodha ni tamthiliya inayohusu suala zima la ugonjwa wa UKIMWI na madhara yake katika jamii. Mwandishi anaweka wazi kuhusu gonjwa hili. Mhusika mkuu Furaha anaathirika na gonjwa hili na kufariki dunia. Kimaudhui tamthiliya hii imesawiri maisha ya sasa ya jamii ya Watanzania kwani ugonjwa huu bado ni tishio. Kwa upande wa fani, mwandishi amewaumba vyema wahusika wake, muundo wake ni unaomvutia msomaji kujua ni nini kingeendelea mbeleni, ameteua lugha nzuri ya kisanaa. Haya yote yanajielekeza katika uchambuzi tutaoenda kuufanya.
MUUNDO
Mwandishi ametumia muundo changamano kwani katika sehemu ya 1 na 2 anatuonesha mazishini ambapo yanafanyika mazishi ya Furaha. Sehemu ya 3-20 anaanza kutuelezea juu ya maisha ya Furaha mpaka kifo chake ambao huu ni msago au muundo sahili. Halafu sehemu ya 17-19 na ishirini 20 anatuonesha juu ya mzozo wa orodha na hatma ya mazishi ya Furaha.
Mwandishi ameweka kazi yake katika onyesho moja. Na katika onyesho hilo ameweka sehemu ndogondogo ishirini zinazojengana kukamilisha tamthiliya nzima.
  • Sehemu ya kwanza:Inaanza kwa kuonesha vifani vinne vimeganda kifani cha kwanza, wahusika wameganda katika mikao inayotambulisha wasifu wa wahusika. Kifani cha pili kinaonesha wagonjwa wakiwa katika mateso. Kifani cha tatu kinaonesha wagonjwa wakiwa katika maumivu makali sana.
  • Sehemu ya pili:Hapa inaelezwa juu ya siku ya msiba wa Furaha. Mama yake Furaha anaeleza watu kuwa Furaha aliacha orodha ambayo alitaka isomwe hadharani katika mazishi yake. Suala hili linazua mgogoro na hofu kuu kwa watu. Padre James anaweka juhudi kuzuia barua isisomwe.
  • Sehemu ya tatu:Sehemu hii tunaoneshwa juu ya maisha ya Furaha nyumbani kwao, baba na mama yake na wadogo zake. Baba yake anaonekana kutofurahishwa na mwenendo wa Furaha kwani anamkanya kwa maneno makali ya laana. Kama vile hatopata mtu wa kumuoa. Anamuasa Furaha kuonesha mfano mzuri kwa wadogo zake.
  • Sehemu ya nne:Hapa Furaha kwa mara ya kwanza anatoroka nyumbani kwao usiku wa manane pamoja na Mery kwenda baa. Mdogo wake anabaini kitendo hicho na kutishia kushitaki kwa wazazi lakini Furaha anamtishia kumchinja.
  • Sehemu ya tano:Wanaonekana Mery na Furaha wako baa wakinywa pombe na kucheza na wanaume. Hapa Furaha anajifunza mambo mapya mabaya kama vile ulevi kupitia rafiki yake Mery. Pia anaanza mahusiano ya mapenzi na wanaume mfano Bw. Ecko.
  • Sehemu ya sita:Hapa Furaha anamwendea Padre James kwa ajili ya maungamo kwani alikunywa pombe na kulala na wanaume, lakini Padre James anamwambia Furaha aende kesho yake katika chumba chake cha kujisomea nyuma ya kanisa na taa zitakuwa zimezimwa kuficha utambulisho. Na hapa ndipo Furaha anapozini na Padre kwani Padre alishikwa na tamaa.
  • Sehemu ya saba:Baba na Mama Furaha wanamkanya Furaha kuhusu tabia yake ya umalaya na ulevi. Furaha anaomba msamaha.
  • Sehemu ya nane:Furaha anakutana na Kitunda aendapo sokoni, katumwa na mama yake. Lakini anamkuta Kitunda akisikiliza mziki Furaha anashawishika, Kitunda anamshawishi zaidi na hata avute bangi ila hakubali. Pia wanazungumzia juu ya jiji la Dar es Salaam. Habari hizo zinampagawisha Furaha na kutamani sana aende.
  • Sehemu ya tisa:Salim anarudi toka masomoni Dar es Salaam. Anaonana na mpenzi wake wa zamani Furaha. Wanasalimiana kwa hamu na furaha tele.
  • Sehemu ya kumi:Salim na Furaha wanakutana na kuelezana habari za kitambo kwani walitengana kwa muda mrefu, wanapanga mipango juu ya mahusiano yao.
  • Sehemu ya kumi na moja:Wanakijiji wanazungumzia juu ya tabia ya umalaya ya Furaha, pia wanazungumzia juu ya mahusiano ya Furaha na Salim. Hawapendezwi na tabia ya Furaha na kuamua kumtaarifu mama yake.
  • Sehemu ya kumi na mbili:Mama Furaha anachukua jukumu la kumhoji mwanae juu ya tabia yake. Furaha hakubaliani na lolote. Hali ya Furaha inaanza kudhoofu na mama yake anaaingiwa hofu.
  • Sehemu ya kumi na tatu:Furaha yupo sebuleni akisali. Baba yake anamuonya zaidi na kumshauri aolewe na Salim kwani ni kijana mzuri anayefaa.
  • Sehemu ya kumi na nne:Hapa hali ya Furaha inazidi kutetereka, anachukuliwa vipimo vya damu na kugundulika kuwa ana virusi vya UKIMWI. Hali hii inamshitua sana mama yake. Anamuhoji kama aliwahi kutembea na mwanaume yeyote, anamueleza njia za upataji wa UKIMWI na Furaha naanza kulia kwa kutambua kosa lake.
  • Sehemu ya kumi na tano:Wanakijiji wanapata habari juu ya kuumwa kwa Furaha na wanazieneza. Juma, Kitunda, Padre James, Salim, Bw. Ecko wanapata pia habari hizi. Wanaingiwa na hofu kubwa endapo watakuwa wameambukizwa UKIMWI au majina yao yamo kwenye orodha?
  • Sehemu ya kumi na sita:Salim anaamua kumtembelea Furaha nyumbani. Akiwa katika hali mbaya sana ya ugonjwa Furaha anamuweka wazi Salim juu ya kuathirika kwake kwa UKIMWI. Salim anaingiwa hofu anamuomba Furaha barua yenye orodha kwa shauku lakini hampatii. Hali hii inamuudhi Salim. Na hapa ndipo Furaha anapokata roho!
  • Sehemu ya kumi na saba:Hapa tunaelezwa juu ya juhudi za Bw. Ecko, na Juma za kutaka kuiba barua yenye orodha katika chumba alicholazwa maiti ya Furaha. Lakini hawafanikiwi. Familia ya Furaha wanaamini kuwa kuna mizimu katika chumba cha maiti kutokana na kelele za Juma na Bw. Ecko, na Kitunda.
  • Sehemu ya kumi na nane:Padre James anaomba kusomewa barua hiyo kabla ya mazishi lakini mama furaha anakataa. Anaamua kuitafuta mwenyewe sebuleni bila mafanikio.
  • Sehemu ya kumi na tisa:Asubuhi siku ya mazishi. Ecko, Juma na Salim wanaonekana wakitafuta suluhu ya namna ya kuzuia orodha isisomwe ila hawafanikiwi.
  • Sehemu ya ishirini:Ni siku ya mazishi ambapo Mama Furaha anaisoma barua ya orodha. Padre James anajitahidi kumpinga mama Furaha asiisome orodha lakini hafanikiwi. Salim anapora barua na kuchana baadhi ya sehemu lakini hiyo haiharibu kitu kwani anaunga vipande na kusoma mbele ya wanakijiji wote. Ndani ya orodha hakuna jina la mtu yeyote lililotajwa bali mambo yatakayosaidia kuuepuka UKIMWI.
MTINDO
Mtindo aliotumia mwandishi ni wa dayalojia au majibizano. Mwandishi ameunda visa na masimulizi yake kupitia majibizano ya wahusika. Pia kwa kiasi kidogo ametumia mtindo wa monolojia, mfano uk. 27 padre James anasema:
“Bwana natazamiwa kuiendesha sala hiyo! Ni kitu ambacho hakikubaliki! Shetani yu kazini kjijini hapa! Furaha anavuna mbegu ya kifo aliyoipanda! Oh! Njia ya mtumishi wa bwana ni ngumu. Imejaa majaribu! Mtu lazima awe na nguvu na kuileta kazi ya bwana kwa watu hawa wa kawaida. Nimepewa kazi iliyo rahisi lakini ni ngumu sana! ni kazi ya upweke!!! Mwili ni mdhoofu! Oh Bwana utulinde.”
Hapa padre James aliongea mwenyewe akifikiri kuwaza na kujutia kazi anayofanya. Pia uk. Huohuo tunaona maneno ya Salim anaongea mwenyewe, pia uk.10, 23,37 na 40.
Pia mwandishi ametumia mtindo wa barua katika kazi yake lengo ikiwa ni kuweka mkazo katika mambo muhimu ya kuzingatia ili kuiepuka UKIMWI. Barua yenyewe ilisema hivi, uk.44“Kwa Kijiji changu kipendwa,
Nawasukuru kwa kufika kwenu na kuyasikiliza maneno yangu ya mwisho. Msiogope kwani nadhani maneno haya yanaweza kuwasaidia. Katika hii miezi ya mwisho nimelala kitandani nikifa, nikizidi kuugua. Nilipata muda mwingi wa kufikiri, kubadilika kukua kama mtu; hata ninapokuwa nakufa. Katika ukurasa unaofuata kuna Orodha ya vitu amabvyo vilisaidia kuyafupisha maisha yangu, orodha ambayo inaonesha kwenu nyote ukweli juu ya kifo changu. Mama, tafadhali wasomee watu wote orodha hii.
  • Uepukaji
  • Kondomu,
  • uaminifu ,
  • elimu,
  • welewa,
  • uwazi,
  • uadilifu,
  • uwajibikaji,
  • ukweli,
  • upendo,
  • msamaha.
Ukosefu wa mambo yote haya ndio ulioniua. Ufuatiliaji wa mambo yote haya unaweza kuwaokoa ninyi nyote. Chukueni orodha yangu na muinakili. Ipelekeni kwenye vijiji vingine, miji mingine na majiji mengine katika nchi yetu hii nzuri. Wanusuruni watu wetu ili waweze kuyafaidia maisha kikamilifu .Wanusuruni watoto wetu ili wasiwe yatima. Muinusuru Afrika…. Afrika yetu nzuri
Kwa kijiji changu kiishi maisha marefu na kiwe na furaha! Msihukukumu mapema mno. Kwa Mama, baba dada zangu, nawapenda. Jaribuni kuwa wenye furaha wakati mnaweza kufanya hivyo.Wenu awapendae Furaha.”
Matumizi ya nafsi
Mwandishi ametumia nafsi mbalimbali na hii ni mifano:
  • Nafsi ya kwanza umoja na wingi:Uk.28 Salim: “nilidhani sitakuona tena sijakuona muda mrefu”Uk.42 “oh huwezi kuamini jinsi tulivyojaribu”.
  • Nafsi ya pili:Salim : usifurahi kupita kiasiSalim: hufai kuhukumu unalala kama…..Mama Furaha: usiwe hivyo wewe u mtoto mzuri.
  • Nafsi ya tatu:Mama Furaha: kabla Furaha hajafa alitaka niahidi kumfanyia kitu fulani hapa kwenye mazishi ingawaje alikuwa na maumivu na mateso aliandika barua hii hapa na kunipa.
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na inayoleweka kwa wasomaji wake.
Matumizi ya tamathali za semi
  • Sitiari:Uk.2 “Waridi changa” “Ua kavu” –Mama anamfananisha Furaha na waridi au ua.Uk.4 “Nyie Mbu mlolaaniwa” –Baba Furaha anawaita wadogo zake Furaha;Uk.6 “Ua” –Furaha.Uk.25 “Slim”- UKIMWI. Wanakijiji wanaufananisha ugonjwa huu na jina hili kutokana na sifa yake ya kukondesha mwili.
  • Tashibiha:Uk.18 “yeye ni kama Punda wa kijiji”.Mwanakijiji wa 1 anamfananisha Furaha na Punda kutokana na tabia yake ya kuwa na wanume wengi. Malaya.Uk.13. “kisura ni kama jiji la New York…”Uk.43 “…vipande vinaanguka kama theluji”.
  • Mubaalagha:Uk.13 “kisura ni kama Jiji la New York ya Afrika Mashariki. Kule kuna majengoMajengo makubwa kiasi kwamba unaweza kuona mlima Kilimanjaro kwaJuu” pia anasema“Ndiyo mpenzi na Maduka… wana moja linaloitwaShoppers Plaza…! Pengine ndilo eneo kubwa lenye maduka makubwaKuliko yote katika Afrika”Uk.20 Furaha: nani aliyesema mambo hayo?Mama Furaha: Nusu ya kijiji kizima badala ya watu wengi. Mama Furahaanazidisha chumvi Kuonesha ukubwa wa hilo jambo.
  • Tafsida:Uk.7 maongezi kati ya wahusika;Mary: hiyo ni bia yake ya mwanzo.Furaha: ni chunguMary: ladha yake utaizoea tuBw. Juma: kama ulivyizoea wewe mayai yangu madogo!Bw. Ecko: Unaona! Inashangaza jinsi ambavyo mtu unaizoea haraka ladha hiyo!Bw. Juma:(kwa mary) kama ulivyofaanya wewe, mishikaki yangu midogo….Mazungumzo haya yamepunguza ukali wa maneno, maneno kama vile “Mishikaki” na “Mayai” ni sehemu za siri.
Mbinu nyingine za kisanaa
  • Mdokezo:Uk.8 “ndiyo padre….. ni …..”Uk.9 “Furaha…..fur….tuta…..”Uk.20 “ame…..tuseme…..”Uk.36 “misamaha padre mi…”Uk.44 “uepukaji….”
  • Nidaa:Uk.15 “Ooo!”Uk.34 “Oh!”Uk.41 “Eee”
  • Takriri:Uk.28 “Hapana hapana hapana nitauona!” “mpumbavu mpumbavu mimi”Uk.9 “hili ni jambo zito sana… sanasana…..sana hasa…”Uk 44 na 45 maneno haya yamerudiwa kuonesha msisitizo.Mwanakijiji wa 2: kondomMwanakijiji wa 3: elimuMwanakijiji wa 4: elimuMwanakijiji wa 1: uwaziKitunda: uadilifuPadre James: ukweliMary: upendoSalim: msamaha.
  • Tashtiti:Uk.20 mama Furaha: wewe na marafiki zako wa kiumeFuraha: marafiki gani wa kiume?Furaha anauliza swali ambalo majibu yake anayo ila tu anataka kuupindisha ukweli.Uk.38 baba: msalaba wako, padri. Uko shingoni mwako!Padre James: kweli?Baba: padre!Padre James: hakika?Padre James alijua wazi kuwa msalaba ulikuwa shingoni lakini kutokana na kutaka kuuficha ukweli alipokutwa katika pilika za kutafuta barua na kusingizia amedondosha msalaba. Alijifanya kuuliza kama vile hajui.
  • Onomatopea au tanakali sauti:Uk.33-34 “Myaau!” Uk.35 “Oooowww!”
Matumizi ya semi
  • Misemo:Uk.27 “Furaha anavuna mbegu ya kifo aliyopanda”
WAHUSIKA
FURAHA
  • Ni binti mdogo wa miaka kati ya 13-19
  • Ni Malaya
  • Anaathirika kwa ugonjwa wa UKIMWI
  • Alikuwa na bidii na mwenye kujituma
  • Ana tama
  • Ni mlevi
  • Ni mkweli na muwazi
  • Ni jasiri
BABA
  • Ni baba yake Furaha
  • Ni mkali
  • Ana upendo
MAMA FURAHA
  • Ni mama yake Furaha
  • Ni mkweli na muwazi
  • Ana upendo
  • Ni jasiri
  • Ni mchapakazi
  • Ni mpole
  • Ana msimamo
  • Anafaa kuigwa na jami
MARY
  • Ni binti mdogo
  • Ni Malaya
  • Si rafiki mwema
  • Anachangia kuharibu maisha ya Furaha
  • Ni mlevi
  • Anapenda anasa
  • Ana tama
  • Hafai kuigwa na jamii
BW. ECKO
  • Ni mwanaume mtu mzima
  • Ni Malaya
  • Si muaminifu katika ndoa yake
  • Ni mrubinifu kwa mabinti wadogo
  • Ni mlevi
  • Ni mfanyabiashara
  • Ni muathirika wa UKIMWI
JUMA
  • Ni mwanaume mtu mzima
  • Ni Malaya
  • Ni laghai kwa mabinti wadogo
  • Ni mlevi
  • Anapenda anasa
  • Ana tama
  • Ni rafiki wa Bw. Ecko
PADRI JAMES
  • Ni mtumishi wa Mungu katika kanisa katoliki
  • Si muadilifu
  • Anaogopa ukweli na uwazi
  • Ni dhaifu kwa wanawake
  • Anaweza kuwa ni muathirika wa UKIMWI
KITUNDA
  • Ni kijana wa mtaani
  • Anapenda anasa
  • Ana tama
  • Ni mlaghai kwa wasichana
  • Ni muhuni
  • Ni mlevi na mvuta bangi
  • Ana lugha ya kihuni
SALIM
  • Ni kijana wa kiume
  • Ni msomi
  • Ni mchumba wa Furaha
  • Anaweza kuwa ni muathirika wa UKIMWI
  • Si mkweli na muwazi
  • Si muadilifu
  • Wanakijiji 1,2 na 3
  • Ni wanakijiji katika kijiji cha Furaha
  • Hawana elimu juu ya UKIMWI
  • Ni wambea
  • Wana imani potofu
DADA MDOGO
  • Ni mdogo wake Furaha
  • Ana tabia njema
  • Ni mkweli lakini muoga
  • Hapendezwi na tabia ya dada yake
MANDHARI
Mandhari aliyotumia mwandishi ni ya vijiji vya Afrika Mashariki kwa ujumla wake. Mwandishi ametumia mandhari hii makusudi kwani imeendana na yale anayoyazungumza katika kitabu. Suala la ujinga na upotofu wa dhana kuhusu UKIMWI lipo zaidi vijijini. Wanakijiji hawaelewi juu ya UKIMWI. Mambo anayoyaibua mwandishi yanaendana na jamii ya watu wa vijiji hivyo mandhari ni sadifu.
Fani katika Tamthiliya ya Watoto wa Mama N’tiliye
Hakaiki fani katika tamthiliya ya Watoto wa Mama N’tiliye
MWANDISHI: EMMANUEL MBOGO
WACHAPISHAJI: HEKO PUBLISHERS
MWAKA: 2002
JINA LA KITABU
Jina la kitabu WATOTO WA MAMA NTILIE limesadifu yaliyomo ndani ya kitabu, kinaeleza kuhusu maisha ya watoto wa mama ntilie. Maisha ya dhiki, umaskini uliokithiri, maisha yasiyo ya faraja yaliyokosa malezi bora, chakula bora, elimu, huduma ya afya nk. Jina la kitabu linaakisi yaliyomo ndani ya kitabu na katika jamii yetu ya leo kwani akina mama wengi hawana kazi nzuri za kuwaingizia kipato kikubwa na bado wanategemewa katika malezi. Mwandishi ametumia jina hili ili kibua kero na matatizo yaliyoko katika jamii.
UTANGULIZI WA KITABU
Riwaya ya Watoto wa Mama N’tilie ni riwaya ambayo inasadifu maisha ya Mtanzania wa leo. Inaangazia suala la umaskini na hali ngumu ya maisha, wimbi la watoto wa mitaani, masuala ya uhalifu wizi na ujambazi, malezi nk. Mwandishi Mbogo amejitahidi sana. Pia katika fani ametumia muundo na mtindo wenye kuwavutia wasomaji pia kawaumba wahusika wake kwa usadifu wa hali ya juu huku mandhari yake ikiwa ni halisi inayosawiri maisha ya Tanzania.
MUUNDO
Muundo uliotawala katika riwaya hii ni muundo wa rukia au rejea. Mfano sura ya tatu mwandishi anatuelezea juu ya safari ya Mama ntilie kwenda matombo uk.34. Lakini anaacha kisa hicho ndani ya sura hiyohiyo anaanza kutuelezea juu ya kuzaliwa kwa watoto Kurwa na Doto na asili yao. Pia uk.80 mwandishi anatudokeza juu ya safari ya kwenda kwa Musa na hatuoneshi hatma ya safari yake bali anarukia kisa kingine na kuanza kutuelezea juu ya Zita kupandwa na kichaa uk.81. Vilevile uk.85-86 anatusimulia juu ya safari ya Mama Zita na Zenabu kuelekea hospitali kumwona Zita lakini hatuoneshi hatma ya safari yao bali anarukia kisa kingine na kuturudisha nyumbani kwa Mzee Lomolomo na jinsi anavyofakamia pombe alafu anaturudisha tena kutuambia juu ya kifo cha Zita hospitalini Muhimbili.
Mwandishi amegawa visa na matukio katika sura tano. Sura hizi zimejengwa katika muundo unaotegemeana ili kukamilisha kilele cha masimulizi.
MTINDO
Mtindo aliotumia mwandishi ni wa masimulizi ya mjazo au lugha ya nathari ameeleza visa mwenyewe na vingine wahusika wamevielezea. Pia ametumia mitindo kadha wa kadha. Mfano;Matumizi ya nafsi.
  • Nafsi ya tatu wingi na umoja:Uk.15 “Peter aliokota kipande cha muhogo” “alisafisha kipande cha muhogo”Uk.27 “walisaidiana wakaubeba” uk.26 “watu walisongamana walisukumana…..”.Kwa kiasi kikubwa matumizi ya nafsi ya tatu ndiyo yaliyotawala.
  • Nafsi ya kwanza umoja na wingi:Uk.58 “nitasema nitasema!”Uk.58 “njoo tuongee”Uk.56 “twende tule”.
  • Matumizi ya nafsi ya pili au dayalojia:Uk.89 pale Mama ntilie alipokumbuka majibizano yake na Zita.MAMA NTILIE: na hiyo nguo namna gani? Mbona chafu hivyo na leo ndio kwanza.Jumanne.PETER: mbwa Mama……ZITA: amenikwaruza kidogo na makucha yake.
  • Matumizi ya tanzu nyingine za kifasihi, mfano wimbo;Uk.78 “Jua ni moto,Tena ni mwangazaWa Dunia,Nadina yooNadina mama,Tumwombe Mungu Baba”Uk.10 wimbo alouimba mzee Lomolomo. “Kuleni nae,Hata bangi vuteni nae,Lakini ni kazi bure,Mwenzenu nimezaa naye,Pepepe kijani cha mbaazi,Kijaluba na msondoKiboko yao”.
Hivyo mwandishi ametumia mitindo hiyo ili kutomchosha msomaji mfano wimbo unamburudisha msomaji, majibizano yanavuta umakini zaidi na matumizi ya nafsi mbalimbali.
MATUMIZI YA LUGHA
Riwaya ya Watoto wa Mama Ntilie imetumia lugha rahisi, fasaha na inayoeleweka kwa wasomaji. Kuna matumizi ya lugha ya kiingereza mfano.Uk.36 “chloroquine”, “RosewinenaQueenElizabeth”,Uk.83 “faster faster mama” uk.1 “landrover”. Pia kuna matumizi ya lugha ya miitaaniuk.41 “kudeku…..”
Matumizi ya tamathali za semi
  • Tashibiha:uk.10 “mdomo wake ulio kaa kama bakuli la pombe”Uk.12 “mama ntilie alikaa kama kapigwa na radi”Uk.15 “miguu kama ya mamba”Uk.46 “aliinamisha shingo nayo ikapinda kama mforosadi” “kichwa kama stafeli”Uk.40. “kitovu chake kama jicho chongo”Uk.23 “Kurwa aliruka nyuma kama Chui”Uk.45 “akaruka kama Paa”
  • Tashihisi:Uk. 10 “mabega yenyewe tayari yalikuwa yamechongwa kwa pombe ya gongo.Yameangalia juu karibu yakutane na masikio”Uk.17 “aliziona nywele za kipilipili za Musa ngumu kama katani hazijaonja maji walasabuni”Uk.19 “ moshi wenye harufu ya kuudhi ulilelea hewani na kumlaki mtoto Peter.”Uk.35 “…… visogo vitatu vilikata kona na kupotea”Uk.46 “koo lilimsaliti”Uk.40 “miguuni raba zinazocheka kwa huzuni”Uk.46 “mlango ule wa kuungwa na gundi ulitika labeka”
  • Sitiari:Uk.10 “Nyama nyie”Uk.86 “…… wakatembea mwendo wa Farasi”
  • Ritifaa:Uk.38 “Mama? Mama yuko wapi, Baba yuko wapi? Mapenzi yao yako wapi?”Uk.92 “Zita! Zita! Zita! Zita umekwenda! Umenitoroka, Zita mwanangu”Uk.93 “Baba! Baba watoto? Mwenzangu! Ee! Amka, simama! Usiniachie tanzia hii peke Yangu”
  • Tafsida:Uk.91 “haja kubwa”
Matumizi ya mbinu nyingine za kisanaa
  • Onomatopea /tanakali sauti:Uk.5 “….. aliupinda mgongo kwa mbele akausikia unalia ka-ka-ka-ka, alitema mate tena Phuuuu”Uk.11 “alikohoa ukho! okho!”Uk.19 “…. Kwa kupiga chafya mbili au tatu Tcha! Tcha! Tcha!”Uk.50 “Bwee! Bwee! Bwee! Mbwa ….”Uk.50 “Hali … vicheko Woo! Woo! Weee! Weee! Heheheee! Leooo!”
  • Takriri:Uk.12 “twende! Twende! Nakuwacha nakauwacha!”Uk.58 “ Nivione! Nivione! Nivione vya kazi gani!”Uk.60 “ Nipishe! Nipishe! Nipishe!Uk.61 “kukurukakara, kukurukakara,kukurkakara”Uk.91 “ Baba! Baba! amka Baba”
  • Mjalizo:Uk. 40 “… akapata pesa, akala, akashiba”
  • Mdokezo:Uk.58 “usiseme hivyo! Unasikia ee! Usi……”Uk.71mara akaanza kuimba tena uleule wimbo wake wa “siwezi kuuwa mtu mama”Uk.73 “lakini…….”Uk.79 “ alikumbuka jaa laa jiji na ………”
  • Nidaa:Uk.44 “ Oh! Mungu wangu!”Uk.91 “ Mama wee!”Uk.90 “Hamadi! Mtume!”
Matumizi ya semi
  • Nahau:Uk.43 “…. Kupiga usingizi”
  • Methali:Uk.34 “ kamba hukatikia pembamba”Uk. 69 “fadhila za Punda”
  • Misemo:Uk.35 “ mtu wa maji” – mlevi.Uk.13 “kwake pombe ya mataputapu na gongo alivifanya dini”.
Matumizi ya taswira
  • Taswira mwonekano mfano:Uk.1 “ Mbwa huyu mweusi mwenye mkia mweupe, alionekana akitembea mwendo wa polepole. Ulimi wake mrefu ulionekana ukidondoka mate ya utelezi” hii inatufanya tupate picha halisi ya jinsi Mbwa huyo alivyo kupitia maneno ya msanii”.Uk.5 “….. hatua tatu mbele yake Sufuria, Vikombe na Sahani chafu zilizagaa pale nje zikimtazama. Akawaona nzi wakitembea na kurukaruka juu ya vyombo vichafu.Uk.10 “ mabega yenyewe tayari yalikuwa yamechonngoka kwa pombe ya gongo yameangalia juu karibu yakutane na masikio.”Uk.69 “Zenabu alibaki pale mlangoni kavaa gauni aina ya shifti, kitambaa cha Hariri”
  • Taswira hisi:Uk.91 “ Mzee Lomolomo alilala mdomo wazi Nzi wakubwa wa kijani kibichi wamejaa tele mdomoni mwake”.Hii inamfanya msomaji ajisikie kinyaa kutokana na hali hiyo ya Mzee Lomolomo anaposema nzi wa kijani kibichi, kwani hao ni nzi wanaokaa sana chooni na kwenye uchafu.
WAHUSIKA
Mama Ntilie
  • Ni mama mzazi wa Peter na Zita
  • Ni mke wa Mzee Lomolomo
  • Mlezi mzuri wa familia
  • Ni mvumilivu sana
  • Ana huruma
  • Ni mchapakazi na anayejituma
  • Ana hali ngumu kimaisha
Mzee Lomolomo
  • Ni mme wa mama ntilie
  • Baba wa Peter na Zita
  • Mlevi
  • Mvivu
  • Si mlezi bora hajali familia
  • Anakufa kwa sababu ya kunywa sana pombe
Peter
  • Mtoto wa mama ntilie
  • Anakosa elimu kwa sababu ya umaskini
  • Ana bidii na mchapakazi
  • Ana huruma
  • Anafungwa jela sababu ya kufanya biashara haramu ya madawa ya kulevya
Zita
  • Mtoto wa kike wa mama ntilie
  • Anakosa elimu sababu ya umaskini
  • Ni mchapakazi
  • Anagombana na Kurwa hakupenda aje kwao, roho mbaya
  • Anakufa kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa
Doto
  • Ni mtoto yatima
  • Mtoto wa mtaani
  • Doto anauawa baada ya kujiingiza katika uhalifu wa wizi
  • Ni mgomvi na katili
Kurwa
  • Ni ndugu yake Doto
  • Anaishi mtaani
  • Ni yatima
  • Ana huruma
  • Ana nguvu na jasiri
  • Ni mchapakazi
  • Anaishia jela kwa sababu ya makosa ya Musa na Peter
Musa
  • Ni mtoto aliyekosa elimu baada ya kukosa sare na ada
  • Alikosa malezi mazuri ya wazazi
  • Mhalifu, anafanya biashara haramu za madawa ya kulevya
  • Ana tamaa ya pesa
  • Ni rafiki mbaya kwani alimshauri Peter kuuza madawa ya kulevya
Mwalimu Chikoya
  • Ni mwalimu wa akina Peter na Zita
  • Aliwafukuza Peter na Zita shule sababu ya kukosa ada
  • Si mwalimu mzuri
MANDHARI
Mandhari iliyotumika katika riwaya hii ni mandhari ya jiji la Dar es Salaam. Hii ni kutokana na kutajwa kwa maeneo ya jiji mfano, Manzese, Tabata, Kiwanda cha Urafiki, Kisutu, Muhimbili nk. Pia ametumia mandhari ya nyumbani mfano nyumbani kwa Mama Ntilie uk.5, mandhari ya hospitali ya Muhimbili uk.89, mandhari ya jaani-jaa la Tabata uk.20.
Kwa hiyo mwandishi ametumia mandhari inayosadifu aliyoyaeleza anaibua dhamira halisi zinazosawiri maisha ya Mtanzania wa leo kwa mandhari hiyo mfano suala la umaskini na wimbi la watoto wa mitaani.
Powered by Blogger.