UCHAMBUZI -TAMTHILIYA YA NGUZO MAMA



KITABU: NGUZO MAMA

MWANDISHI: PENINA MUHANDO

WACHAPISHAJI: DUP

MWAKA: 1982

UTANGULIZI
Tamthiliya ya Nguzo Mama aliyoandikwa na Penina Muhando inayasawiri na kuyaelezea matatizo mbalimbali yanayowakabili na kuwaelemea wanawake wengi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Wanawake wengi wamekuwa wakinyanyasika kwa kunyanyaswa na kuteswa na waume zao.Mwandishi  anathibitisha hayo kwa kutueleza maisha waliyokuwa wakiishi wanawake wa Patata.
MAUDHUI
DHAMIRA KUU: UKOMBOZI WA MWANAMKE
Mwandishi wa  kitabu hiki cha Nguzo Mama anaelezea na kuonesha juhudi mbali mbali zifanywazo na wanawake katika kujikomboa kutoka minyororo ya utumwa wa mwanaume na manyanyaso mazito anayoyapata kutoka kwa mwanaume na jamii nzima inayomzunguka. Mwandishi, baada ya kusawiri maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika na manyanyaso anayoyapata kama vile kupigwa, kufanyishwa kazi kuliko uwezo wake, mfano :- kulima peke yake, kufua, kuosha  vyombo, kukusanya kuni n.k., anaamua kutumia kipaji chakekuelezea jinsi gani mwanamke anaweza kujikomboa.
Katika kitabu cha Nguzo  Mama,mwandishi anawaonesha wanawake wa Patata wahangaikavyo katika kujikomboa.Ukombozi huo umegusa nyanja zote za maisha yaani kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kiuchumi,katika kujikomboa wanawake wa Patata wanaamua kuanzisha miradi mbalimbali ambayo itawawezesha kujipatia fedha kwa ajili ya maendeleo. Miradi ikashamiri sehemu zote za Patata.
‘’..........Miradi tutatilia mikazo, miradi ya kila aina vilabu vya pombe, maduka ya khanga, ushirika wa kushona, kupika, hoteli na mengi........’’(uk 52).
Bi Pili yeye akaamua kuanzisha kilabu cha pombe ili aweze kujikomboa kwenye maisha magumu yanayomkabili.
’Kaamua Bi Pili, Pombe kujipikia, na kilabuni kuiuza
Pesa akipata, Pesa msema kweli
Na nguzo mama itasimama’’ (uk 14).
Mwandishi anaonesha umuhimu wa pesa katika kujikomboa kwa wanawake,kwani pesa ndio hasa iletayo maendeleo stahiki.Hali kadhalika Bi Moja na wenzake nao wakajiunga na kuanzisha viwanda vyao vya kufuma mapambo ya nyumbani.
Kutokea Bi Moja,Na lake jipya kiwa nda kuanzisha
Mapambo ya nyumbani kufuma
Mapambo akiyauza na pesa kujipatia
Itakuwaje nguzo mama isisimame’’ (uk 17).
Kijamii, wanawake wa Patata wamehamasika kwa kuanzisha vikundi vya akina mama, ambavyo vitasimama imara kutetea maslahi yao na kusaidiana wao kwa wao katika kujikomboa.Mfano mzuri ni kikundi lcha kina Bi Nne, yeye alikuwa kiongozi wa umoja huo akiwahamasisha wanawake wenzake ili waweze kuinua ‘’nguzo Mama’’
‘’Bi Nne anapiga makofi nao
Anasimama na kutoa hotuba
Nguzo mama hoyee’’ (uk 11).
Bi Nne naye hakuwa nyuma katika kazi yake ya ualimu.Akaanzisha Umoja wa Walimu, nia ikiwa kuwasaidia kutatua matatizo yao mbalimbali yanayowakabili katika ufundishaji, Bi Nne anawashauri walimu wenzake kuanzisha umoja huo ili kwanza waanze na matatizo yao yanayowakabili katika hatua ya kujikomboa kama wanawake.
’Kutokea Bi Nne, wenzake wengi
Makubwa hawakujitakia, vizuri walishauri
Tuanze na yetu matatizo, Ndani yah ii yetu kazi
Kazi yetu ya kufunza vyema kuichapa
 Vigingi vikitokomea, vyema vijana watafunzika
Wakifunzika wote Patata
‘’Nguzo Mama itasimama’’ (uk 20).
Hapa mwandishi anaonesha elimu kama njia moja wapo itakayoweza kuwakomboa wanawake pale aliposema;
’Vigingi vikitokomea, vyema vijana watafunzika, wakifunzika wote Patata nguzo mama itasimama’’
Mwandishi pia anaonesha ushirikianao wa jamii nzima, wanawake kwa wanaume kutasaidia sana katika kuleta ukombozi wa mwanamke na mwanamke peke yake, abadani hatoweza kusimamisha ‘’Nguzo Mama’’
’Bi Nane ‘’Tushirikishe wanaume pia. Nguzo mama ina faida kwa wote
Tuite na watoto wote faida kwa wote – wao taifa la kesho’’
Kwa hiyo, mwandishi licha ya kuonesha utakiwaji wa jamii nzima katika ukombozi wa mwanamke, pia anaonesha faida za ukombozi huo hazitamlenga mwanamke tu bali na jamii nzima inayomzunguka mwanamke.
Pia umoja nao unaoneshwa kama njia itakayowezesha wanawake waweze kujikomboa.
’Bora tufanye mikutano
Labda na maandamano
Maazimio tuyatangaze
Tukupambeje maua’’ (uk 7).
Mikutano kama ilivyo kawaida yake ingewezesha kuwapasha watu wengi zaidi juu ya ukombozi wa mwanamke na manyanyaso wapatayo. Hivyo watu wengi wangehabalishwa katika uwanja wa siasa. Nafasi za uongozi kwa wanawake ni moja kati ya njia ambazo zingemwezesha mwanamke kujikomboa.
Katika tamthiliya hii, mwandishi anaonesha juhudi mbalimbali zifanywazo na wanawake wa Patata katika kuchukua  uongozi wa Serikali.
‘’.........Akina mama watapewa vyeo, orodha tumeshapanga. Tutapata mawaziri, mameneja, mabalozi na kadhalika. Wengine tayari wameshapata kama mnavyofahamu’’ (uk 52).
Baadhi ya wanawake ambao walipata uongozi ni Bi Nne ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya vyeo.
‘’He! Kweli nimekumbuka looo!
Nimechelewa mkutano wa kamati ya vyeo
Na mimi ndiye mwenyekiti, si mnajua tunavyokazana kuwaombea mabibi vyeo maana wanasahauliwa. Lazima tufanye huo mkutano’’ (uk 42).
Bi Tatu yeye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya malezi bora
’My God ! Mmeona! Tena Shangazi mwenyewe ndiye mwenyekiti wa malezi bora’’ (uk 50).
Ukombozi wa fikra pia umeoneshwa kama tatizo linalowasumbua wanawake wa Patata. Mfano anamuonesha Bi Nane dhidi ya madai aliyoambiwa. Bi Nane hasa alipokubaliana na kila kitu alichoelezwa na Bi Nne.
DHAMIRA NDOGONDOGO
1.   UONGOZI MBAYA
 Mwandishi wa tamthiliya hii, anaanza kwa kuonesha umuhimu wa kiongozi katika jamii yoyote ile. Pia anaonesha kiongozi kama mtu aliyeshikilia jamii anayeweza kuipeleka jamii anayeweza kuipeleka jamii yake kwenye neema au mdomo wa samba kutegemeana na uongozi wake atakavyokuwa anaupeleka.
‘’........Tena kwetu sie kiongozi huongoza njia
Aweza kuwapeleka kwenye neema
Au mdomoni kwa samba........’’ (uk 22).
Lakini viongozi hao, wengi wao wamekuwa wakizipeleka jamii zao kwenye mdomo wa samba,kwani viongozi hao hutumia uongozi kama dhana ya kuonesha wao ni watu watukufu na walio kwenye daraja la juu katika jamii.Wakiamuawatakavyo bila kufuata miongozo iliyopo katika uongozi huo.
‘’ Bi Nane akawaza
Kumbe kazi hii ya uongozi au uwenyekiti
Inampa mtu uwezo wa kufanya
Mambo kinyume cha kawaida......’’ (uk 24).
Mwandishi  anaonesha uongozi mbovu kama ndio chanzo cha matatizo yanayoikabili jamii ya Wanapatata. Viongozi kama akina Bi Nne na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashauri,wanaoneshwa kama viongozi wabovu wanaosababisha kuwa na matatizo katika jamii ya Patata.
‘’ Lahaula! Kumbe ndio maanawatu wengi wanaulilia uwenyekiti,kwani ni rahisi kazi yake,kiholela mambo kujifanyia,masikini Patata si ajabu kumbe vurugu kutapakaa’’ (uk 25).
Mwandishi anaonesha vurugu zinazoisonga Patata kuwa zimechangiwa na uongozi mbovu.Udikteta pia unaoneshwa kuwa ni zao la uongozi mbovu uliopo kwenye jamii ya wana Patata.Viongozi kama mwenyekiti wa kamati ya mashauri wamechorwa kama madikteta,wanaotumia uongozi wao watakavyo,wajisikiavyo kutoka mioyoni mwao au vile waambiwavyo na watu wao wa karibu bila kufuata misingi  na miongozo waliyowekewa na katiba ya jamii zao. Mwenyekiti wa kamati ya mashauri anatumia vitisho kumlazimisha Bi Nane kusemaasichokijua ili mradi tu yeye ni kiongozi.
Pia mwenyekiti anaonesha udikteta wake pale alipotaka kuamua kesi aliyosikiliza upande mmoja tu wa mashtaka,tena maelezo hayo kapewa wakati mshtakiwa hayupo.
‘’........Vipi mtu atakubali kutoa ushauri kutumia vitisho!
Kufuatilia maelezo ya mshtaki peke yake
Tena yaliyoelezwa wakati mshtakiwa hakuwepo
Vipi mtu atamshauri mshtakiwa
Bila kujua mawazo yake’’  (uk 24).
Pia mwandishi anaonesha udikteta uliokithiri unavyoitawala jamii ya Patata, yaani mtu mmoja anaweza kuamua maamuzi yanayotakiwa kufanywa na kamati nzima. Tena ajifanyiaye mambo  bila kushirikisha kamati hiyo.Mfano ni pale mwenyekiti wa kamati ya mashauri walipokaa na kuunda kamati ya watu wawiliili wamshitaki Bi Nane.
‘’ ....Vipi  watu hawa, wawili, moja, mbili kujifanya wao kikao.
Katiba gani inasema mwenyekiti peke yake
Awe na kikaocha kuamua mashauri
Au asaidiane na mtu si mwanakamati
Mwenyekiti na mshtaki  kuwa kikao?!
Sijapata kusikia, hiki ni kikao cha hila.
Kusema sitajisumbua, kimya akijikalia’’ (uk 24).
Mwandishi anaendelea kutuonesha maajabu ya uongozi mbaya wa   wanaPatata ulivyokithiri,kwani wale viongozi walikuwa wanategemewa ndio haohao wanaofanya mambo ya ajabu.
’Na ajabu kupita yote
Vipi mwenyekiti bila kamati
Akatoa ushauri katika mashtaka?’’ (uk 25).
Hapa msimulizi alikuwa anaendelea kutuonesha jinsi mambo yalivyo mabaya hapo Patata.
Kwa wema na huruma
‘’Mwanangu mie sijui labda kamuulize Bi Nne’’ (uk 54).
Chizi anamshangaa Bi Saba, kwani licha ya kuwa kiongozi  hajui hata ninimaana ya Nguzo Mama. Chizi anaendelea kusema;
‘’Lakini juzi kachaguliwa katibu
Sijui wa kamati gani ile. Nimesahau’’ (uk 55).
                       
2.   DHULUMA
Mwandishi  amejadili  tatizo la dhuluma lilivyoigubika jamii yetu ya leo.Katika tamthiliya yake ya Nguzo Mama anajaribu kutuonesha jinsi jamii ya Patata, kama zilivyo jamii nyingine, ilivyooza kwa dhuluma,hasa kwa wanawake wajane pindi tu wanapofiwa na waume zao.
Katika tamthiliya ya Nguzo Mama,mwandishi anatumia mhusika wake Bi Saba kuonesha jinsi ganiwanawake wengi wa Kiafrika wanavyodhulumiwa mali na ndugu za waume zao pindi tu wanapofariki. Bi Saba baada ya tu ya kufiwa, shemeji yake walikuja na kugawana vitu vya Bi Saba pasipo kumuachia hata kitu. Watoto nao walichukuliwa, wakimwacha Bi Saba masikini akihangaika huku na kule bila mafanikio.
‘’ Haa! Shemeji mmerudi kuchukua hata kitanda!
Hata sufuria! Nitalala wapi na nitapika wapi jamani?’’ (uk 43).
Mwandishi anaendelea kueleza uozo wa dhuluma ndani ya Patata ilivyoletamatatizo na huzuni kwa wanaodhulumiwa huku wakikosekana watu wa kuwasaidia, hakuna mtu wa kumsaidia mwenzak, dhuluma imetapakaa kila mahali Patata.
’Akalia Bi Saba tena akalia, hana wa kumsaidia
Mumewe kafa nduguze wamekuja juu,
Pesa wamechukua senti tano haikubaki
Vyombo na nguo zote wakagawana
Roho ikampasuka Bi Saba kuwaona hao ndugu
Walivyogombania  mali wasiyochuma
’Kiti hiki changu’’ Mie lile jembe’’
‘’Mie suruali hizi’’ ili mradi ilikuwa zogo’’ (uk 43-44).
Mwandishi pia anaelezea juu ya dhuluma, kwa kitu au mali uliyoichuma kwa jasho lako mwenyewe,ukahangaika huku na kule kutafuta mali hiyo lakini mwisho wanakuja wachache kukudhuluma mali hiyo. Mfano Bi Saba.
Uongozi mbaya pia umesababisha kuondoka kwa demokrasia kwa watu wa Patata, kwani  wachache wenye madaraka ndio wanaoonekana kupewa kipaumbele kuzidi wenzao, wanaowaongoza.Mfano ni pale Chizi alipokuwa anamuuliza Bi Nne akimwonesha kuwa yeye ni mtu mkubwa na anapewa kipaumbele zaidi. Anasema;
‘’.......Lakini bibi yangu aliniambia
Binadamu wote sawa, lakini wengine  ni sawa zaidi.
Na huyu ni mmoja wa hao’’ (uk 58)
Pia mwenyekiti wa kamati ya mashauri hafuati  demokrasia inayotakiwa kwa kumlazimisha na kumpa masharti yaliyo kinyume kabisa na katiba,yenye kuonesha udikteta uliokithiri usiofuata na unaoepuka kabisa demokrasia .
’ Jambo la pili nakueleza kuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kufanya mkutano bila kibali cha ofisi hii. Na ofisi hii lazima iletwe kumbukumbu za mikutano yote iliyofanyika hapa Patata. Sheria hii ipo na inajulikana kwa hiyo urudi ufuate mashauri yangu’’ (uk 25).
Viongozi wa Patata wanaoneshwa pia viongozi  wasiopenda kuwajibika katika kufanya kazi za kuliletea taifa lao maendeleo yao, wawapo tu! Kazi kuongea maneno yasiyotekelezwa. Mfano ni Bi Tatu, yeye ni kiongozi wa malezi bora lakini ameshindwa hata kulea watoto wa kaka yake anayehangaika mtaani (chizi). Pia anashindwa hata kujishughulisha kufanya vijibiashara.
‘’My God! Mmeona! Tena Shangazi mwenyewe ndiye mwenyekiti wa kamati ya malezi bora yeye mwenyewe hafanyikazi…..’’(uk 50).
Licha ya kuwa viongozi wa Patata hawapendi kuwajibika, lakini pia wanaoneshwa kama wasiokuwa na elimu, na wasiojua nini kinaendelea hata kwenye uongozi wao.Chizi anasema;
‘’…..Siku  moja nikamwendea, labda niwe kweli chizi
‘’Shikamoo’’ ‘’Marhaba’’ Bi Saba nieleze.
Nini kitu Nguzo Mama, naona hapa Patata mambo yamevurugika, kila ninakogeuka nasikia nguzo mama, Nguzo Mama kitu gani? Vizuri, alijibu.
Yeye alihangaika huku na kule ili ajiletee maendeleo yake naya watoto wake, lakini bado mumewe alipofariki nduguze wakaja na kumdhulumu jasho halali.
’Atawaambiaje watu hawa,
Kuwa vyote walivyochukua Zaidi ni jasho lake
Watoto wake wapenzi mwenyewe aliwalea
Wakati wao baba mnatindi akiyachapa
Na pesa kwa pombe kuangamiza
Pesa ya ndugu yao iliishia chooni’’ (Uk 44)
Hivyo mwandishi anaitaka jamii kupinga dhuluma ili kuleta maendeleo.
3.   ELIMU
Katika tamthiliya hii elimu inaoneshwa kama jambo la muhimu sana kwenye maendeleo ya jamii yoyote ile.Mwandishiameonesha kuwa kila nyumba ya mafanikio au maendeleo yoyote yale kuna elimu. Bi Nne anakubaliana na ukweli huu pale alipokuwa anasisitiza somo la ushonaji liingizwe kwenye mitaala ya wanafunzi mashuleni ili waweze kujifunza kushona vitu mbalimbali kama mapambo na nguo. Kisha wauze wapate maendeleo.
’……….Pia somo la ushonaji litatiliwa mkazo mashuleni. Kila shule italifundisha ili watoto wetu wajue kushona, wavae vizuri na kupamba nyumba zao vizuri’’ (uk 18).
Bi Nane naye anaonesha na kuthibitisha ukweli juu ya umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya jamii ya Patata. Yeye anaonesha kuwa kama watu hawatapata elimu, basi hata maendeleo hawatayasimamisha yakasimama.
‘’…….Tuvitoe vigingi vile vituzuiavyo
Kazi yetu ya kufunza vyema kuichapa vigingi vikitokomea, vyema vijana watafunzika
Wakifunzika wote Patata.
Nguzo Mama itasimama’’ (uk 20).
Ukosefu wa elimu nao unaoneshwa kama tatizo kubwa kwa jamii ya Patata linalosababisha kukosekana kwa maendeleo na kuwakomboa wanawake. Viongozi wanaoneshwa kama watu wasiokuwa na elimu, wasiojua hata kinachoendelea kwenye uongozi wao. Mfano ni pale Chizi alipomuuliza Bi Saba ambaye ni kiongozi kuhusu maana ya Nguzo Mama. Lakini Bi Saba anaonekana hajui chochote kuhusu Nguzo Mama. Baada ya Chizi kumuuliza Bi Saba anajibu;
’Mwanangu mie sijui labda kamuulize Bi Nne’’.
Yaani Bi Saba anaonekana mtu asiye na elimu kabisa, kwani hajui hata jambo alifanyalo, Chizi anaendelea kutuhabarisha kuhusu Bi Saba,
’Lakini sijui kachaguliwa katibu sijui wa kamati gani ile. Nimesahau’’ (uk 55)
Elimu pia inaoneshwa ilivyopana na katika hayo mapana yake ya kila sehemu ina umuhimu wake. Elimu ya malezi, kama zilivyo elimu nyingine, inaonekana kuwa na umuhimu mkubwa sana katika jamii hasa ikizingatia kwenye kipindi hiki ambacho magonjwa ya ajabu yanayoizunguka jamii kama vile Kisonono, Kaswende na Ukimwi. Hivyo mwandishi anasisitiza kuwepo na elimu ya malezi itakayowasaidia vijana na wanawake hasa wale wanaotupa watoto kwenye mapipa na vyooni. ‘’……….Pia wasichana kutupa watoto kwenye mapipa, kuna semina wiki ijayo kuzungumzia swala hili, ni aibu kubwa sana kwetu’’ (uk 52).Sharti wapate elimu ya malezi waache tabia hiyo.
4.   USALITI
Ni tendo la kuchonganisha watu kwa kuchukua maneno ya huku na kuyapeleka huku ili wapate kugombana .Kama tafsiri ya usaliti ilivyo, Mwandishi amefanikiwa kuonesha suala la usaliti kwa ustadi mkubwa,pale alipowachora wahusika wake kama wasaliti. mfano ni pale walimu walipomsaliti mwenzao Bi Nane kwa kutoa siri za vikao wanavyovifanya na kumpelekea Bi Nne,ambaye anaonekana kama adui wa Bi Nane.
‘’……..Tena Mwenyekiti mimi nilikwambia hao walimu wengine hawampendi huyu Bi Nane, yeye tu ndiye anayejiweka kimbelembele kama wanampenda mbona walimu hao hao wanatoka wanakuja kunieleza mipango yao? Sema basi tukusikie’’ (uk 22-23).
Matokeo ya usaliti huu yalimuweka pabaya Bi Nane, kwani alisongwasongwa na kuhangaishwa na uongozi wakimtuhumu kama msaliti na mvuruga Amani anayetaka kusimamisha maendeleo ya Patata.
’Lahaula!
Sawa hawajakaa makubwa yakawakuta!
Barazani wakaitwa mashtaka kuyajibu’’ (uk 20).
Mwandishi anaendelea kutuonesha usaliti ulivyosababisha Bi Nane kuingia kwenyematatizo pale mwenyekiti alipokuwa anamuhoji.
’Kwa kifupi ni kwamba, tumepata habari kwamba wewe umeanzisha kikundi cha kupinga juhudi za wenzetu hapa Patata za kusimamisha Nguzo Mama. Tena kikundi hicho cha walimu watupu kinabagua wasio walimu. Tena kikundi hicho kimekuwa kikifanya mikutano kupanga njama za kuchafua juhudi za wenzenu’’ (uk 21).
Mwandishi pia ameonesha dhamira yenye kufanana na usaliti japokuwa kitafsiri sio usaliti.
5.   UMASIKINI NA MAGONJWA
Umasikini ni hali ya kukosa mali, yaani mtu kutoweza kukidhi haja ya mahitaji yake ya kila siku. Kuishi chini ya kiwango kinachotakiwa.Umasikini ni  tatizo kubwa linalozisumbua nchi za dunia ya tatu,limejadiliwa kwa kina na mwandishi.Patata ni moja ya jamii za watu masikini wasioweza kujimudu kimaisha wahangaikao huku na kule kusaka riziki bila mafanikio. Jamii ya Patata inaonekana ikisumbuliwa na shida chungu nzima.Bi Tano shida zimemwandama, watoto wake wanapata tabu, hata hela ya kuwanunulia nguo hana sembuse chakula. Watoto wake siku nyingine wanashinda na njaa wakiangalia siku inavyopita, jua likitokea mashariki kuelekea magharibi.
‘’Taabu, taabu! Taabu!
Watoto wangu hawana chakula
Hawana nguo, hawana chakula
Watoto wanashinda na njaa.
Wanalala na njaa’’ (uk 40).
Hali kadhalika Chizi naye anaonesha hali hii ya umasikini pale anapolalamika kuumwa na njaa na njaa yenyewe inaonekana si ya siku moja tu bali ni muda mrefu, kwani anaelezea kuwa njaa hiyo huwa haijimuisha.
’Labda tuite njaa
Kama hii inayomuuma
Njaa kamwe haimuishi’’ (uk 31).
Mwandishi pia anaelezea umasikini ulivyotawala Patata kiasi ambacho watu wanashindwa hata kubadili nguo,yaani wao wamekuwa na nguo za ‘’kauka nikuvae’’.
’Bi Pili : Nimeifua mchana huu, asubuhi si nilidamkia shambani…..’’(uk 36).
Mumewe bwana Sudi anajibu,
‘’Kelele! Sasa mimi nitavaa nini
Utaikausha kwa moto hiyo nakwambia
Mimi nataka kurudi, nilikotoka nimeacha pombe kafiri unATAKA WENZANGU WAIMALIZE!
Kausha hiyo nguo haraka kabla sijakupiga’’ (uk 36).
Mwandishi katika kuonesha umasikini ulivyoibuka Patata anazichunguza na kuzifichua sababu zinazoleta umasikini huo.Moja kati ya sababu hizo ni uvivu na kutojituma katika kufanya kazi.Wananchi wa Patata ni wavivu na hawajitumi.Wanawake wapo tu wanapiga soga huku miguu waitandaza kwenye mikeka.Mfano Bi Moja yeye asilani yumo ndani tu anashinda utadhani mwali anayefundwa.Kutwa domo akilipiga tena huku miguu kainyosha , na kamwe hutamwona jasho likimtoka akifanya kazi.
‘’Mwenzenu miye nashangazwa na maneno ya Bi Moja
Hiyo dhahabu na fedha, na huu wake uturi
Wapi atavipata, kumbe ndani anashinda
Miguu kainyosha na domo kujipigia
Kamwe sijamuona, akilitoa jasho kazi kujifanyia
Wapi niambie inapatikana fedha na dhahabu
Bila kazi kufanyia, niende na mie Chizi
Nyingi nikajitolee’’ (uk 47-48).
Kama ilivyo kwa wanawake wa Patata, wanaume ikiwa ni mara mbili yao kutwa nzima kiguu na njia, wanaume hawajui hata jembe linashikwa vipi.Wao ni pombe tu,pombe na wao, kutwa nzima wanashinda vilabuni, wakinywa na kupiga zogo tu mara hiki mara kile. Uvivu umewajaa hawataki kabisa kujishughulisha.Kazi zote wamewaachia wake zao hata zile za kuihudumia familia.Hata kile kidogo kinachozalishwa na wake zao basi huwapokonya.
‘’Huyu Bi Pili rohoni anasikitisha, Atakufa masikini hohehahe kama mie, Lakini ninashangaa kala nini bibi huyu, Walahi sijaona mwingine hodari kumpita lakini yule wake mume, nini kamlisha kazi zote afanya yeye bi Pili, matunda yote ale Bwana Sudi.
Jasho lake Bi Pili laishia kilabuni,huyu wake bwana Sudi Matindi anayatandika usiku na mchana siku moja nitamuuliza Bwana Sudi, Dawa gani aliyompa Bi Pili na mie nikabahatika mke kujipatia awe kama Bi Pili ambaye taabu yote atakubali, watoto anizalie na pia anilelee, chakula anilimie na pia anipikie.Nguo anifulie na pombe anipatie.Nikipata yote haya!
Kama ilivyo shilingi yenye pande mbili,ndivyo kila mwenye umasikini maradhi nayo hayaeshi.Jamii ya Patata inaoneshwa kama jamii yenye kusumbuliwa na maradhi mbalimbali hasa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
‘’……Nimeishi siku nyingi, Na mengi nimeyaona, ugonjwa wa kaputula na ule wa magunia
Pia kipindupindu vile vita vya mdachi.
Na yule Nduli Amini Lkini ya Patata.
Sijui niite vita au ugonjwa’’ (uk 31).
Umasikini pia umeoneshwa wakati Bi Moja alipokuwa anamdai mume wake fedha za kununulia khanga (Shabani).
’Nimekwambia mie hela sina sasa unataka nikaibe?’’ (uk 35).

6.   UVIVU NA UZEMBE
Uwajibikaji ni hali ya kufanya jambo pasipo hiari,yaani unalazimika kulifanya.Tofauti na ilivyo kawaida kwa watu wa jamii ya Patata wenyewe wamekuwa si wawajibikaji,yaani hawawajibiki ipasavyo katika kufanya kazi.Wananchi wa Patata wanaoneshwa kama watu wavivu wasiopenda kujituma katika kufanya kazi.Dhamira hii,mwandishi anaonesha uvivu na uzembe  kama chanzo kilichosababisha kufifia na kushindwa kuinua Nguzo Mama.Mfano mzuri ni pale wanawake wa Patata waliposhindwa kuinua ‘’Nguzo Mama’’. Mfano Bi Moja yeye anaacha kuinua na kuvuta Kamba na kuanza kuongea na Bi Tano kuhusu khanga. Kwa muktadha waliokuwepo wasingepaswa kuzungumzia mambo hayo.Bi Tano anamuelekeza kuwa zinapatikana kwa Mwarabu na pia anamtahadharisha kuwa anapaswa kuziwahi la sivyo zitakwisha.Mara Bi Moja anaondoka na hapo Bi Nane anashituka na kuuliza,
‘’ Sasa jamani Bi Moja anakwenda wapi tena!!
Bi Moja akiwa mbali anajibu,
‘’Aaa jamani nitarudi lakini khanga hizi sizikosi’’ (uk 34).
Bi Sita naye anaoneshwa kama mwanamke asiye muwajibikaji na asiyejali umuhimu wa kazi za maendeleo, kwani naye baadaye anaacha kuvuta kamba na kumfuata mwanaume eti kwasababu alimkonyeza ili amfuate licha ya umuhimu uliopo kwenye kuinua ‘’Nguzo Mama’’.
‘’……Mara anatokea Maganga, Bi Sita anamfuata wanachekeana. Maganga anamfanyia ishara amfuate’’
Bi Tano anaona yanayofanyika upesi anaacha kamba na kuwafuata’’ (uk 38).
Bi Tatu naye kwake Nguzo Mama si mali kitu  Zaidi ya mume na sherehe,hivyo anawasusia wewnzake kamba na  kutimkia kwenye Volvo lililomfuata na kuelekea kwenye pati ambayo kwake yeye ni muhimu Zaidi kuliko Nguzo Mama.
‘’Jamani mie naondoka mnaiona Volvo hiyo imenifuata mie’’. Anaendelea kusisitiza ‘’Siyo utani ndugu nyangu,Tunakwenda kwenye pati na mume wangu leo saa moja lazima nipalilie unga kwa baba watoto wangu ati. Nitakula nini’’ (uk 41).
Hata viongozi nao wanaonekana wababaishaji waliojaa maneno matamu mdomoni lakini pasipo uwajibikaji kwa vitendo.Bi Nne kama kiongozi naye anaondoka kwenye kazi muhimu, kazi ya vitendo itakayowezesha maendeleo ya mwanamke kupatikana na kwenda kwenye vikao,kazi ya kupiga soga bila utekelezaji.
’Hee! Kweli nimekumbuka. Loo!
Nimechelewa mkutano wa kamati ya vyeo na mimi ndiye mwenyekiti……’’ (uk 42).
Kwa kutowajibika huko wanawake hao wa Patata wakasababisha kushindikana kuinua kwa ‘’NguzoMama’’, nguzo ambayo ni egemeo lao la maendeleo.Na ndiyo ufunguo ambao ungeweza kuwaondoa kwenye minyororo ya utumwa na ukandamizwaji wa siku nyingi. Lakini kutowajibika kukawakosesha.Mwandishi  pia anaonesha ugumu wa maisha wa watu wa Patata unavyotokana na kutowajibika kwao.Bi Moja anaonekana kama mwanamke asiyejishughulisha na kazi yoyote ile kutwa yumo ndani tu katulia,kwa hali kama hii ya kutowajibika ndiyo hasa chanzo cha umasikini.
‘’Mwenzenu mie nashangazwa na maneno ya Bi Moja
Hivyo dhahabu na fedha na huo wote uturi
Wapi ataupata, kumbe ndani anashinda
Miguu kuinyosha na domo kujipigia.
Kamwe sijamuona akilitoa jasho kazi kujifanyia…….’’ (uk 42).
7.   MAPENZI NA NDOA
Katika tamthiliya ya   ‘’Nguzo Mama’’ mwandishi anaelezea mapenzi yasiyokuwa ya kweli, yanayojali pesa na usaliti kati ya wanandoa.Mfano ni Maganga (mume wa Bi Tano) na mkewe Bi Tano,Maganga anaonekana kutokuwa na mapenzi ya kweli kwa kumsaliti mkewe na kumchukua Bi Sita.
’Wee Bi Sita mshenzi, unanichukulia mume wangu hivihivi kimachomacho’’ (uk 39).
Usaliti huu wa mapenzi unaleta sononeko la moyo kwa Bi Tano. Pia unaleta hali ngumu kwa familia ya Bi Tano, kwani watoto wanalala njaa kwa kukosa chakula na mahitaji muhimu kwa kuwa Maganga (baba yao) anamaliza pesa zote kwa wanawake.
Mwandishi pia anaonesha mapenzi yanayoendeshwa na pesa kuliko utashi wa mtu na mtu, mfano ni pale Bi Tatu alipowaambia wenzake alipofuatwa na mumewe.
’Sio utani ndugu yangu, Tunakwenda kwenye pati na mume wangu leo saa moja usiku, lazima nipalilie unga kwa baba watoto wangu ati, nitakula nini’’ (uk 44).
Pia anaonesha suala la mwanaume kuwa na mke zaidi ya mmoja lisivyokubaliwa na wanawake na jinsi gani wanavyohangaika kulibadilisha suala hili.
8.   NAFASI YA MWANAMKE KATIKA JAMII
Katika tamthiliya ya Nguzo Mama mwanamke amechorwa katika nafasi tofauti kama ifuatavyo;
Kwanza amechorwa kama chombo cha starehe kilichopo kwa ajili ya kustarehesha wanaume.Mwandishi ameonesha kuwa mwanamke anatumia mwili wake kama bidhaa iuzwayo sokoni na kumpatia faida.Mfano ni Bi Sita ambaye ni changuidoa.
“Mwenzio nautafuta huo muda siupati.
Laiti ningeupata wengi zaidi kunasa.
Kwani mmoja, wawili wanafaa kitu gani?” (uk 29).
Pili,Mwanamke pia amechorwa kama jasiri  anayejitoa mhanga kuusema ukweli.Mwandishi anamuonesha Bi Nne anayeamua kumwambia ukweli mwenyekiti juu ya kutokubaliana kwake na maamuzi aliyoyatoa.
“Sikubali Mwenyekiti kama nashtakiwa haki ninayo ya kutoa maelezo vile ninavyotaka.
Nitaeleza kwa maandishi nakala wanaohusika wote nitawapa.Kesho nitakuletea ahadi ninaweka,ukishasoma maelezo yangu ukae ukihukumu.Lakini kabla ya hapo sipokei hukumu wala ushauri” (uk 29).
Tatu,Mwanamke amechorwa kama kiumbe duni kisicho na thamani wala uwezo wakufanya jambo lolote katika jamii. Katika kijiji cha Patata wanaume waliwadharau na kuwabeza wanawake wakiwaona kama watu wasiokuwa wakamilifu (uk 46).
Nne,Mwanamke amechorwa kama uvumilivu nao umeoneshwa kama sifa ya mwanamke kwenye tamthiliya hii.Mwanamke anaonekana kutokata tamaa katika juhudi zake za kuinua  Nguzo Mama licha ya ugumu unaowakabili (uk 11).
Tano,Mwanamke amechorwa kama mtu anayekandamizwa na asiyepewa haki zake za msingi.Mfano ni Bi Saba alipodhulumiwa vitu vyake na nduguze mumewe na kuambiwa hana haki ya kurithi vitu vya marehemu mumewe (uk 43).
Sita,Mwanamke amechorwa kama mtumwa wa mumewe.Hii inaonekana pale Bwana Sudi alipokuwa anamtumikisha mkewe Bi Pili kufanya shughuli zote za nyumbani na shambani yeye akiwa anakunywa pombe tu (uk 49).
Saba,Mwanamke anachorwa kama kiongozi wa familia ndiye aikuzaye jamii, kama hapatokuwepo na mwanamke katika jamii, hakuna jamii itakayoweza kuwepo. (uk 44-45)
UJUMBE
·       Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu
·       Kwa kila jambo la maendeleo jamii nzima (yaani wanawake, wanaume,wazee,vijana na watoto) lazima washirikiane.
·       Ulevi ni adui wa maendeleo.
·       Uongozi bora ni muhimu katika kufikiamalengo.
·       Malezi bora ni muhimu katika familia
·       Wanawake wanafanikiwa kujikomboa siku watakayoamua kuungana na kushirikiana
·       Wanawake nao wapewe nafasi za uon gozi.

MIGOGORO
v Mgogoro kati ya Bi Pili na mumewe (Bwana Sudi),Chanzo cha mgogoro wao ni pesa.Bwana Sudi anataka kuchukua pesa za mkewe alizouzia pombe.Suluhisho ni Sudi kumpiga mkewe baada ya kukataa kumpatia pesa hizo.
v Mgogoro kati ya Bwana Sudi,Shaba na Totolo,Chanzo ni baada ya Shaba na Totolo kumtetea Bi Pili mke wa Sudi asipigwe na mumewe.Suluhisho ni Shaba na Totolo kumwacha Bwana Sudi aendelee na matusi juu yao,kwani waligundua kuwa alikuwa amelewa.
v Mgogoro kati ya Bi Tano na Wanakikundi,Chanzo ni kutonunuliwa kwa vitambaa.Suluhisho ni kugawana vitambaa hivyo kwa kila mwanakikundi akauze kivyake.
MSIMAMO
Msanii ana msimamo wa kimapinduzi kwa kuyatolea macho matatizo yanayowakabili wanawake katika kujikomboa na vipi wafanye ili waweze kujikomboa.
FALSAFA
Msanii anaamini kwamba ili wanawake wajikomboe  lazima wawe na msimamo,maelewano,pamoja na umoja na ushirikiano pasipo wivu wala kubaguana.
FANI
MUUNDO
Msanii ametumia muundo wa moja kwa moja.Tamthiliya hii imeanza kwa kuonesha jinsi nguzo mama ilivyolala na harakati za kina mama kashika na kunyanyua nguzo mama. Mchezo umegawanyika katika sehemu nne.
MTINDO
Msanii ametumia mtindo wa dayolojia na masimulizi.Vilevile ametumia lugha ya kishairi ili kuleta mvuto katika mchezo wake.Pia msanii ametumia nyimbo na mianzo ya hadithi za fasihi simulizi. (uk 3).
MATUMIZI YA LUGHA
MISEMO/ NAHAU
v Utakiona cha mtema kuni (uk 42).
v Watoto ni taifa kesho (uk 55).
v Utakufa kibudu (uk 22).
v Akachanganya ulimi {uk 57).
v Dume Malaya si dume roho yako kusumbua (uk 40).
METHALI
v La mgambo likilia lina jambo (uk 45).
v Aso mwana aeleke jiwe (uk 45).
v Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu (uk 33).


TAMATHALI ZA SEMI
TASHIBIHA
v Anatembea kama kapigwa bumbuazi (uk 9).
v Sikilizeni na sauti kama ndege nyikani (uk 30).
v Wanaswagwa kama mbuzi (uk 44).
v Amevaa kama mkulima wa bara (uk 24).
TASHIHISI
Ø Hasira zikampanda Bi Nane (uk 8).
SITIARI
v Mbwa mume wako  anayefuata wanawakeovyo.
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
TAKRIRI
v Wakajaribu ,wakajaribu (uk 5).
v Mwachie! Mwachie! Mwachie! (uk 8).
v Toka! Toka! Toka usirudi tena (uk 8).
v Akaenda, akaenda, akaenda (uk 40).

MDOKEZO
v Wakavuta…….wakavuta……….(uk 35).
v Siku moja ………ngojeni niwaoneshe (uk 49).
v Ee ndiyo malezi ya watoto wetu………(uk 52).
v Hebu tutazame kwanza kwanini hawasogei….(uk 58).
TANAKALI SAUTI
v Lu lu lu lu lu lu lu lu lu! (uk 2 na 18).
v Ai ai ai ai ai ai ai ai ai ai! (uk 2).

MATUMIZI YA KIINGEREZA
v My God  (uk 32, 49, 50).
LUGHA ZA MATUSI
*  Shika adabu yako  (uk 39).
*  Malaya mkubwa wewe (uk 39).
*  Mbwa wee! (uk 39).
*  Mbwa mume wako anayefuata wanawake ovyo (uk 39).
WAHUSIKA
Bi Moja
v Mke wa Shabani
v Hakuwa na msimamo katika kusimamisha Nguzo Mama.
v Alikuwa na tama.
v Hafai kuigwa na jamii.
 Bi Pili
v Mke wa Sudi
v Alinyanyaswa na mume wake.
v Ni mvumilivu katika matatizo.
v Ni mlezi bora wa familia.
v Anafaa kuigwa na jamii.
Bi Tatu
v Ni mpenda starehe.
v Hapendi kazi ambazo hazina mshahara.
v Anambembeleza mume wake kwa kuogopa kuachwa.
v Hafai kuigwa na jamii.
Bi Nne
v Ni mtu asiyependa maendeleo ya wenzake.
v Ana wivu, mbinafsi, mfitini na ana chuki binafsi.
v Hafai kuigwa na jamii.
Bi Tano
v Ni mke wa Maganga.
v Ana hasira sana.
v Hakumpenda Bi Sita.
Bi Sita
v Alikuwa kahaba na alikuwa anatembea na waume za watu.
v Ni mkorofi na hakupenda ushirikiano.
v Hafai kuigwa.
Bi Saba
v Alifiwa na mume wake.
v Ni mlezi swa watoto.
v Ni kiumbe duni kwani shemeji zake walimnyang’anya mali zake zote na hata watoto baada ya mume wake kufa.
 Bi Nane
v Alipenda ushirikiano na swenzake.
v Alikuwa na elimuya kutosha.
v Alipenda kuelimisha wenzakekatika shughuli za maendeleo.
v Hakuwa na chuki na mtu.
v Anafaa kuigwa.
 Chizi
v Ni mpenda demokrasia.
v Alipiga vita uoga.
v Ni mfichua maovu yaliyoko katika jamii
v Anaonesha wazi matatizo yanayosababisha wanawakekushindwa kujikomboa.
v Anafaa kuigwa na jamii.
 Mwenyekiti
v Ni mtu mwenye uongozi mbaya
v Anapenda kusiliza majungu na fitina.
v Anawachukia wanawake wasomi.
v Hafai kuigwa na jamii.
MANDHARI
Mandhari ya tamthiliya hii ni ya kubuni lakini yanasawiri maisha ya vijijini na kiasi maisha ya mjini,kwani mwandishi ameonesha mandhari ya vilabuni,uwanjani na nyumbani.Mandhari yaliyooneshwa yanaoana sana na nchi za Kiafrika vile Tanzania,kwani unyanyasaji na ugandamizwaji wa wanawake wa Kitanzania ni sawa kabisa na wale wa Patata.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu Nguzo Mamalinasadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu hiki.Kitaswira “Nguzo Mama” ni umoja wa wanawake Tanzania (U.W.T) ambao uliundwa kwa lengo la kuwatetea, kuwalinda na kuwapa haki na maendeleo wanawake sawa na wanaume.Tamthiliya hii inaonesha harakati za wanawake wa Patata wakiwemo wakulima,wasomi,waalimu,makahaba na wanaungana kuimarisha umoja na maendeleo yao.Wanafungua miradi mbalimbali kama vile kushona,kupika pombe,pamoja na tofauti zilizopo kati yao kama vile uzembe,majungu,fitina na kutoelewana.
KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
KUFAULU
Kimaudhuimwandishi amefaulu kwa kiwango cha juu katika maudhui yaliyomo ndani ya mchezo huu,kwani amefaulu kutueleza matatizo yaliyowapata wanawake wengi wa Kiafrika hususani  Tanzania.
Kifani,mwandishi ametumia lugha rahisi inayoeleweka,lugha ya kishairi inayofurahisha pia na nyimbo zinazoburudisha. Hivyo kufanya mchezo usichoshe.
KUTOFAULU
Kimaudhui,mwandishi ameshindwa kutueleza hatma ya wanawake wa Patata na jamii nzima baada ya kushindwa kuinua nguzo mama.
Kifani,matumizi ya lugha ya matusi ni udhaifu wa mwandishi,kwani matusi ni lugha isiyotakiwa katika jamii.



Powered by Blogger.